Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa
kufisha; nani awezaye kuujua?
(Yeremia 17:9).
Lakini kila mtu na aipime kazi yake mwenyewe, ndipo
atakapokuwa na sababu ya kujisifu ndani ya nafsi yake tu, wala si kwa mwenzake.
(Wagalatia 6:4).
Katika somo lililopita
nililoliita Nia ya Ndani ya Moyo niligusia kuhusu umuhimu wa kuwa makini na nia
zetu pale tunapomwendea Mungu, maana Mungu anajali sana hizo nia ambazo ndizo
zinazoamua endapo atayakubali maombi yetu au tutaishia kupata hasara.
Katika somo hili namwomba
Mungu anisaidie kufafanua kwa uwazi zaidi kile ambacho hasa kinaweza kuwa kinaendelea
ndani ya mioyo yetu, ambacho ndicho anachokiona Mungu wetu pale anapotutazama.
Katika nyakati za Biblia
kulikuwa na dhambi ambazo, labda niziite kuwa ni “za jumuiya.” Dhambi za namna
hii zingeweza kutendwa na mtu mmoja lakini athari zake zikaangukia familia au hata
taifa zima – ingawaje wengine wanakuwa hata hawakushiriki au hawakujua kwamba
mkosaji halisi alikuwa anatenda dhambi hiyo.
Kwa mfano, Mfalme Daudi alipofanya
kosa la kuwahesabu Israeli, alisababisha vifo kwa watu ambao hawakuhusika na
kosa lake. Imeandikwa: Basi Bwana akawaletea Israeli
tauni tangu asubuhi hata wakati ulioamriwa; nao wakafa watu toka Dani mpaka
Beer-sheba sabini elfu (2 Samweli 24:15).
Pia, tunasoma kuhusu wana wa Israeli kwa ujumla kuhesabika kuwa
wametenda dhambi kutokana na kosa la mtu mmoja, yaani Akani. Matokeo yake
walishindwa kwenye vita na kakabila kadogo sana ka Ai.
Imeandikwa: Lakini wana wa Israeli walifanya dhambi katika kitu
kilichowekwa wakfu; maana Akani, mwana wa Karmi, mwana wa Zabdi, mwana wa Zera,
wa kabila ya Yuda, alitwaa baadhi ya vitu vilivyowekwa wakfu; hasira ya Bwana
ikawaka juu ya wana wa Israeli. (Joshua 7:1).
Mbali na hivyo, kosa la Akani pia lilisababisha kuangamia
kwa familia yake yote. Imeandikwa: Kisha Yoshua, na Israeli wote pamoja naye,
wakamtwaa Akani, mwana wa Zera, na ile fedha, na lile joho, na ile kabari ya
dhahabu, na wanawe, na binti zake, na ng'ombe zake, na punda zake, na kondoo
zake, na hema yake, na vitu vyote alivyokuwa navyo, wakavileta juu hata bonde
la Akori. Yoshua akasema, Mbona
umetufadhaisha hivi? Bwana atakufadhaisha wewe leo. Ndipo Israeli wote
wakampiga kwa mawe, kisha wakawateketeza kwa moto, na kuwapiga kwa mawe.
(Yoshua 7:24-25).
Lakini ilifika mahali ambapo Bwana akasema: Tazama,
siku zinakuja, asema Bwana, nitakapoipanda nyumba ya Israeli, na nyumba ya
Yuda, mbegu ya mwanadamu na mbegu ya mnyama. … Siku zile, hawatasema tena, Baba
za watu wamekula zabibu kali, na meno ya watoto wao yametiwa ganzi. Bali kila mtu atakufa kwa sababu ya uovu wake
mwenyewe; kila mtu alaye zabibu kali, meno yake yatatiwa ganzi. (Yeremia
31:27, 29-30).
Na tena, ingawaje tunatakiwa kabisa kubebeana mizigo, kwa
maana ya kusaidiana kwa upendo ili kuleta furaha, amani, uponyaji, n.k., lakini
inapokuja kwenye hatima ya suala la dhambi na athari zake kwa yule azitendaye, imeandikwa:
…
kila mtu atalichukua furushi lake mwenyewe. (Wagalatia 6:5).
Ndugu zangu, ninachotaka kusema hapa ni kwamba, Mungu
anatupima kibinafsi katika kila
jambo tunalojihusisha nalo hapa duniani. Kama ambavyo unaona kwamba ukinunua
muda wa maongezi kwenye simu, hauwezi kamwe
kuidanganya mitambo ili kwamba eti uongee hata kwa nusu sekunde na usikatwe
pesa. Haiwezeani! Ukibonyeza tu, hata kama ingekuwa ni usiku wa manane, lazima
mtambo utatambua na pesa yako itakatwa mara moja kulingana na kiwango cha
upigaji simu wako!
Hiyo ni teknolojia ya kibinadamu. Mungu ni zaidi! Hakuna sekunde
yoyote katika maisha yetu inayompita. Hakuna!! Na kila kitu kinawekwa
kumbukumbu mbinguni – kiwe ni tendo linaloonekana kwa nje au ni wazo
lililojificha moyoni!! Ndiyo maana imeandikwa kwamba Mungu atazihukumu siri za
wanadamu (Warumi 2:16).
Je, ni kwa nini unafanya yale unayoyafanya?
Hakuna mwanadamu anayejua kile kinachoendelea moyoni mwako. Maana ni
nani katika binadamu ayajuaye mambo ya binadamu ila roho ya binadamu iliyo
ndani yake? (1 Wakorintho 2:11). Roho yako, au wewe mwenyewe (pamoja na
Bwana) ndio mnaojua kile kinachoendelea ndani ya moyo wako. Na kwangu vivyo
hivyo! Na kwa mwingine vilevile!
Sasa, kwa nini unafanya yale unayoyafanya? Nia yako ni nini?
Katika mambo ya kawaida kabisa ya kila siku maishani mwetu
ni lazima kujiuliza swali hili: Kwa nini ninafanya hivi? Makusudi yangu ni
nini?
- Kwa nini unataka nguo ya gharama kubwa wakati ziko za gharama ndogo za ubora uleule?
- Kwa nini unataka uwe na magari kumi?
- Kwa nini unataka kumiliki maduka matano?
- Kwa nini unachubua ngozi yako?
- Kwa nini umebadili rangi ya nywele zako?
- Kwa nini umechora ‘tattoo’ kwenye mwili wako?
- Kwa nini unavaa mavazi yanayoacha wazi sehemu za mwili wako ambazo hazitakiwi kuachwa wazi?
- Kwa nini umevaa mlegezo?
- Kwa nini ulitoa mchango mkubwa sana kwenye harusi ya yule ndugu?
- Kwa nini umevaa nyusi za bandia?
- Kwa nini ukiwa kanisani unaonyesha sura ya unyenyekevu lakini ukiwa nje haufanyi hivyo?
- Simu yako ni ya gharama. Kwa nini unapenda kuitoatoa mbele za watu hata kama haupigi au haujapigiwa?
- Kwa nini umevaa cheni na unafungua vifungo vya shati lako?
- Kwa nini umevaa nguo inayoacha maziwa nje?
- Kwa nini ulimsaidia yule mtu aliyeomba msaada?
Mengi ya mambo haya ni ya kawaida kabisa katika maisha yetu ya
kila siku na hayana ubaya hata kidogo!! Hakuna ubaya kuwa na magari kumi,
nyumba tano, simu ya shilingi milioni moja, n.k. Hakuna ubaya!
Swali hapa ni moja tu: Moyo wako au moyo wangu unakuwa
unanisukumaje mbele za watu? Kwa lugha rahisi, je, ninapenda kujionyesha? Ninaona
fahari fulani watu ‘wanaponitambua’? Ninakuwa na shauku kila mtu ajue kuwa mimi
ni wa kiwango cha juu? Je, kila wakati nakuwa naangalia kwa jicho la chati ili
kubaini kama kuna watu wananitupia angalau jicho sawasawa na ninavyotamani
wafanye?
Ni hakika kabisa hivi ndivyo maisha ya wengi wetu yalivyo. Ni
maisha ya maonyesho, maonyesho, maonyesho tu! Ni maisha ya kusaka sifa na
umaarufu! Ni maisha bandia! Hatumfikirii Bwana bali tunawafikiria wanadamu. Tunatamani
kusifiwa na wanadamu.
Kwa watu wa dunia hii ni sawa kabisa. Lakini je, kwa Mungu
nako ni sawa? Kwa wapendwa nako inatakiwa iwe hivyo?
Je, kanisa litatofautishwaje na dunia kama nalo linafanya
mambo haya? Je, ni kwa kiasi gani haujanaswa na mtego huu? Ni kwa kiasi gani
haujaingia kwenye kapu hili?
Kwa nini unafanya yale unayoyafanya?
Lakini
kila mtu na aipime kazi yake mwenyewe, ndipo atakapokuwa na sababu ya kujisifu
ndani ya nafsi yake tu, wala si kwa mwenzake.
(Wagalatia 6:4).
Labda binti au msichana unasema, “Sasa nisipojipodoa na
kujipamba nitapataje mume?” Dada yangu, kama Mungu ni Baba yako, basi lia na
Yeye. Kibinadamu unaonekana kuna mantiki kabisa. Inaonekana kana kwamba
usipojihangaisha kwa namna Fulani, basi utakosa mume. Lakini Bwana
anapotutazama anasikitika kwa sababu hayo si maagizo yake. Maagizo yake
yanasema: Maana twaenenda kwa imani, si kwa kuona. (2 Wakorintho 5:7). Kwa kuwa: Mwenye haki ataishi kwa imani.
(Warumi 1:17).
Jambo moja la msingi sana, si kwa akina dada tu, bali kwa
kila mwanadamu, ni kufika mahali pa KUAMUA kuwa, “Mimi nitasimama na Bwana peke
yake! Awe amenipa kile ninachokiomba au hakunipa. Basi!!”
Huku ndiko kuyatoa maisha YOTE kwa Bwana. Lakini hii
haitufanyi tuache kuomba kwa bidii zote yale ambayo mioyo yetu ina shauku nayo.
Ni hasara sana kuishi maisha ambayo yanataka tu kuwavutia
wanadamu na kutaka kusifiwa nao. Hayo ni maisha ya UBATILI mkubwa.
Bwana anatuagiza katika sura ya sita ya Kitabu cha Mathayo:
1 Angalieni
msifanye wema wenu machoni pa watu, kusudi mtazamwe na wao; kwa maana mkifanya
kama hayo, hampati thawabu kwa Baba yenu aliye mbinguni.
2
Basi wewe utoapo sadaka, usipige panda mbele yako, kama wanafiki
wafanyavyo katika masinagogi na njiani, ili watukuzwe na watu.
3 Amin, nawaambieni, Wamekwisha kupata
thawabu yao. Bali wewe utoapo sadaka, hata mkono wako wa kushoto usijue
ufanyalo mkono wako wa kuume;
4 sadaka yako iwe kwa siri; na Baba yako
aonaye sirini atakujazi.
5 Tena msalipo, msiwe kama wanafiki; kwa
maana wao wapenda kusali hali wamesimama katika masinagogi na katika pembe za
njia, ili waonekane na watu. Amin, nawaambia, Wamekwisha kupata thawabu yao.
6
Bali wewe usalipo, ingia katika chumba chako cha ndani, na ukiisha
kufunga mlango wako, usali mbele za Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye
sirini atakujazi.
7
Nanyi mkiwa katika kusali, msipayuke-payuke, kama watu wa mataifa; maana
wao hudhani ya kuwa watasikiwa kwa sababu ya maneno yao kuwa mengi.
8
Basi msifanane na hao; maana Baba yenu anajua mnayohitaji kabla ninyi
hamjamwomba. (Mathayo 6:1-8).
Japo hapa Bwana anaongelea zaidi suala la utoaji sadaka na
maombi, lakini, kimsingi, yuko kinyume na maisha ya maonyesho mbele za watu. Tukifanya
mambo kwa nia ya kuonekana mbele za watu ni kweli kabisa tutafanikiwa katika
hilo. Tutasifiwa na kupata umaarufu huu batili wa dunia. Lakini hiyo ndiyo
itakuwa thawabu yetu.
Simaanishi kuwa sasa basi uwe mchafumchafu kwa sababu tu eti
hauko hapa kuifurahisha dunia bali Bwana! La hasha! Uchafu pia ni dhambi. Ninachomaanisha
ni mtu kufanya mambo yake hasa kwa
ajili ya Bwana. Ni kufika mahali ambapo kila kitu ninachofanya ni kwa ajili ya
kumtukuza Bwana wangu, Yesu Kristo. Kama kwa jambo hilo dunia itanisifu, sawa. Kama
haitanisifu, nako sawa pia. Lakini kusifiwa na wanadamu kusiwe ndio sababu ya
msingi inayonisukuma kufanya jambo lolote.
Bwana anaagiza: Basi, mlapo, au mnywapo, au mtendapo neno lo
lote, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu. (1 Wakorintho 10:31).
Siamini kamwe kwamba mtu aliyeamua kwa dhati kuyafanya yote
kwa utukufu wa Mungu atahangaika na mambo haya. Tunahangaika nayo kwa kuwa tu
tumenaswa na ubatili wa dunia.
Ni nani yuko tayari kumwangalia Bwana pekee na kuachana na
ulimwengu huu? Ni nani ee Bwana aliye tayari kutafuta kwa bidii sifa kutoka
kwako badala ya sifa za wanadamu? Ni nani aliye tayari ee Bwana kujikagua katika
KILA wazo, neno na tendo, KILA sekunde ya maisha yake?
Hakika yake Bwana hatuwezi. Hatuwezi kabisa bila neema yako.
Tusaidie kuishi maisha matakatifu badala ya kushiriki na kuwa sehemu ya giza la
dunia hii. Maana umesema kuwa sisi ni nuru ya ulimwengu. Lakini badala yake
tumemezwa na giza; na sasa tunatafuta kila sababu [hata za kimaandiko] za
kuhalalisha mambo haya ya giza. Tupe ufunuo wa rohoni ee Roho Mtakatifu ili
tujue umuhimu na kuwa na utayari wa kubadilishwa na kupewa mioyo mipya
inayoweza kukutii. Ni katika jina la Yesu naomba. Amina.
Amina
ReplyDeleteAmina sana mtumishi Mungu azidi kukubariki na kukutumia kwa viwango vya tofauti. Nimebarikiwa sana na somo hil, hakika ni wakati wa kubadilisha mtizamo na kumtazama Yesu pekee katika Maisha yangu.
ReplyDelete