Hadithi ya mwana mpotevu
inafahamika kwa wasomaji wa Biblia. Vilevile, inafahamika kwa habari ya uhusiano
wake na mtu yeyote asiyeokoka; yaani mwana mpotevu anawakilisha watu ambao hawajaamua
kumpokea Kristo awe Bwana na Mwokozi wao binafsi. Hadithi hii inaashiria jinsi
ambavyo Mungu amempa mtu wa aina hiyo uzima, afya na baraka nyinginezo, lakini
badala ya kukaa nyumbani mwa Baba, ameamua kwenda kule duniani na kuishi maisha
ya utapanyaji. Hata hivyo, pale anapotambua kuwa amepotea na kuamua kurudi kwa
Baba, muda wote Baba yuko tayari kumpokea kwa furaha na upendo mwingi. Sote
tuko hivyo. Hapo ndiko tunakoanzia.
Lakini huenda jambo ambalo
halizungumzwi sana ni kuwa, hadithi hiyo haina mwana mpotevu mmoja, bali
wawili. Pamoja na kwamba mwana mdogo alitenda makosa, pale aliporudi baba yake
hakusema, “We mtoto, yaani umeenda huko ukala kila kitu; sasa umeona kuwa
umeishiwa halafu unajidai eti ‘nimekosa, nimekosa’, ukome kabisa! Rudi huko
huko! Mjinga mkubwa we!”
Baba hakusema hata neno moja
la kumlaumu mwanawe au kuhusiana na makosa yake; hata moja! Kwa nini?
Maandiko yanasema: Tuikiziungama
dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na
kutusafisha na udhalimu wote. (1 Yohana 1:9).
Mara nyingi tunamkosea
Mungu na mawazo ya hatia yanatujaa mioyoni kiasi kwamba tunakosa amani, na
kushindwa tena hata kuomba. Hata mwana mpotevu naye alijawa na mawazo ya hatia
vivyo hivyo. Anapojadili moyoni mwake kwamba: Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu
na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako. (Luka 15:18).
Kimsingi, hii ilikuwa ni
hatia inayomtafuna moyoni mwake.
Tunapovamiwa na roho ya
hatia, kunakuwa na mambo mawili yanayokuwa mbele yetu, na mojawapo linaweza
kutokea.
1. Hatia ile inaweza kuwa
kubwa na mtu akakubaliana nayo, hivyo akakata tamaa, akanyong’onyea, akajiona
hafai na akaanza kumwogopa Baba. Matokeo yake ni kwenda mbali zaidi na zaidi.
Yuda Iskariote alikosa, lakini alilemewa sana na hatia ya kosa lake kiasi
kwamba, badala ya kwenda kwa Baba, alienda kujinyonga.
2. Jambo jingine linaloweza kutokea baada ya
kukosa na moyo kujawa na hatia ni kwenda kwa yule uliyemkosea, yaani kwa Baba.
Mwana mpotevu alisema, “Nitakwenda kwa baba…” Petro alipomkana Yesu, badala
ya kukimbia mbali kama Yuda, alipiga magoti na kumwomba Baba msamaha.
Mwana mpotevu alirudi kwa
baba yake na matokeo yake, badala ya kubaki akiwa amepotea, alipatikana; badala
ya kubaki akiwa mfu, alifufuka.
Ni muhimu kukumbuka jambo
hili: Pendo la Mungu kwetu halitegemei uzuri wetu. Baba hasemi kuwa, ‘Kwa vile
mwanangu huyu amekuwa na tabia nzuri, basi sasa ninampenda.’ Hapana! Mungu ni
pendo usiku na mchana! Uwe mtii au muuaji, Mungu anakupenda tu kwa pendo
kamilifu katika Kristo Yesu. Pendo hili halibadiliki kamwe.
Shetani asikudanganye
kwamba wewe ni mwovu mno kwa hiyo Mungu ana hasira sana na wewe. Mungu hapendi
dhambi; lakini wewe na mimi anatupenda kwa upendo wenye nguvu kuliko mauti.
Hii haina maana kuwa tuko
huru kutenda dhambi na kwenda kutubu tena na tena kisa eti Mungu anatupenda. La
hasha!!! Kati ya maandiko yanayoogopesha sana ni pamoja na hili: Maana, kama
tukifanya dhambi kusudi baada ya kuupokea ujuzi wa ile kweli, haibaki tena
dhabihu kwa ajili ya dhambi. (Waebrania 10:26).
Ni hakika kabisa kuwa
Mungu anatupenda SANA lakini pia Neno lake halitapita bure, lazima yote yatimie.
Atakapotoa hukumu siku ya mwisho, hatafanya hivyo kwa kuwa anawachukia wale
atakaowatupa motoni, bali ni kwa sababu hawezi kutenda nje ya Neno lake ambalo
ndilo sheria isiyobadilika ya maisha haya na yale yajayo. Neno linasema … mshahara wa
dhambi ni mauti. (Warumi 6:23). Sasa, kama mtu ameishi katika dhambi
maishani mwake; alikataa neema ya wokovu kwa hiari yake mwenyewe, Mungu hana
jinsi isipokuwa kutekeleza kile ambacho Neno linasema kuhusiana na mtu kama
huyo.
Hebu turudi sasa kwa mwana
mkubwa. Moyo wa toba wa mwana mdogo ulimwezesha kupokea pendo la Baba ambalo
lipo tu na halibadiliki wala kupungua na halikuwahi kubadilika au kupungua
tangu aondoke nyumbani.
Lakini kitendo cha
kumpokea tena mwana mpotevu huyu kiliamsha hisia za uchungu, wivu, masikitiko
na hata chuki ndani ya moyo wa mwana mkubwa. Alisema, Tazama, mimi nimekutumikia
miakamingapi hii,wala sijakosa amri yako wakati wowote, lakini hujanipa mimi
mwana-mbuzi, nifanye furaha na rafiki zangu; lakini, alipokuja huyu mwana wako
aliyekula vitu vyako pamoja na makahaba, umemchinjia yeye ndama aliyenona. (Luka
15:29-30).
Sijui ndugu msomaji
umekuwapo kanisani au ndani ya wokovu tangu lini. Huenda unasema, “Nimekuwa mwombaji,
nimekuwa mtii, ninatoa sadaka na zaka, ninawahi kanisani, ninashuhudia
wasiookoka, n.k., n.k., lakini Bwana uko wapi? Baba, hata kuniponya? Hata kunipa
mume/mke? Hata kunipa mtoto? Hebu ona hawa wengine; mbona wameokoka hivi
karibuni tu na umewajibu? Hii ni halali kweli?”
Siku moja Bwana Yesu
akaongelea juu ya maombi ya mtoza ushuru na farisayo. Wakati mtoza ushuru
anajuta kwa kujiona asivyo na haki na alivyo mpungufu mbele za Mungu, farisayo
yeye anaeleza jinsi alivyo na haki na namna
anavyostahili. Alisema: Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine,
wadhalimu, wanyang’anyi, wazinzi wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara
mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote. (Luka 1811-12).
Na Bwana anatueleza hukumu
ya Mungu juu ya hali hii. Anasema: Nawaambia, huyu (yaani mtoza ushuru) alishuka
kwenda nyumbani kwake akiwa amehesabiwa haki kuliko yule; (yaani farisayo)
kwa
maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa. (Luka
18:14).
Hii ni kusema kwamba, kati
ya wale watoto wawili wa yule baba, mtoto yule ambaye, kwa moyo wa unyenyekevu,
alijiona jinsi ambavyo hana kitu alipata; na yule aliyejiona ana kitu,
alipoteza vyote.
Maana yake ni kuwa, sisi binadamu
hatuna chochote cha kujisifia mbele za
Mungu isipokuwa katika kile ambacho tumepokea kutoka kwake. Maandiko yanasema: … matendo yetu
yote ya haki yamekuwa kama nguo iliyotiwa unajisi. (Isaya 64:6). Matendo
ya haki ni matendo yote mazuri kama kutoa sadaka, kusali, kusaidia wenye shida.
Lakini kinachoyatia unajisi ni ile hali
ya kudhani kuwa hayo ndiyo yanayonunua au kugharamia baraka na upendo wa Baba.
Kwanza tunatakiwa kutambua
kuwa baraka na upendo wa Baba tunaupokea kwa kuwa tu tumemwamini; si kwa vile
tumesali sana au tumetoa sadaka sana. Ndipo matendo ambayo Roho Mtakatifu
atayafanya kupitia sisi baada ya hapo ndiyo yanayokubalika mbele za Mungu. Hayo
ndiyo sadaka yenye harufu nzuri mbele za Baba.
Ninaponung’unika, hiyo ni
ishara kwamba nilikuwa ninatenda matendo mema kwa lengo la ‘kulipia’ au
‘kununua’ wema na baraka za Mungu.
Mwana mpotevu pamoja na
mtoza ushuru waliua kila kitu ndani yao ili kuvipata. Kwa kawaida nafsi huwa
inatuambia, “Hili jambo ni halali yako kabisa. Usikubali kunyang’anywa. Huyo mwingine
anayepewa hata hastahili.” Maandiko yanasema: Mwenye kuiona nafsi yake
ataipoteza; naye mwenye kuipoteza nafsi yake kwa ajili yangu ataiona. (Mathayo
10:39).
Mwana mkubwa alijihesabia
haki akifikiri kuwa pendo la Baba linapimwa kwa mizani – kwamba ukitenda zaidi,
unapendwa zaidi; ukitenda kidogo, unapendwa kidogo. Hakujua kuwa Baba
anawapenda watoto wake wote sawasawa – wawe wema au waovu.
Kwa hiyo, furaha ya mtoto
yeyote haitegemei pendo la Baba – haina maana kuwa, ukiwa na furaha kidogo ni
ishara kuwa umepokea pendo la Baba kidogo; au mwenye furaha kubwa amepokea
pendo zaidi la Baba. Hapana! Maana malango ya pendo la Baba yamefunguliwa hadi
mwisho. Baba ameshamwaga pendo lake lote kwetu sote.
Tofauti inatokana na
upande wetu. Inategemea kiasi ambacho kila mtoto amefungua mlango wa moyo wake
ili kuruhusu na kupokea mmwagiko wa pendo la Baba. Hatuna haja ya
kujilinganisha na wengine ili kwamba eti tuweze kujua kama tunapendwa au la.
Badala yake, tuna haja ya kujilinganisha na na ahadi ya Baba iliyo kwenye Neno
lake. Basi!
Baba anakupenda;
ananipenda kwa pendo kamilifu. Imeandikwa: … Mungu liupenda ulimwengu hata akamtoa mwanawe
… (Yohana 3:16). Lakini pale tunapojilinganisha na wengine, kisha
tukaona jinsi wao walivyo tofauti na sisi (yaani tunaona kuwa wamebarikiwa
zaidi), ndipo tunapofungulia milango ya uchungu, wivu, hasira, n.k.; na
kuufungia nje upendo wa Baba. Halafu tunageuka tena na kusema, “Baba hanipendi
kama anavyompenda fulani.”
Aina hii ya mawazo
ilimwingia pia Petro. Bwana aliwakuta Petro na wenzake wakiwa baharini wakivua
samaki. Baadaye Bwana akamwambia Petro: Nifuate.
(Yohana 21:19).
Maandiko yanasema kuna mtu
mwingine naye alisimama na kuanza kumfuata Bwana. Imeandikwa: Petro akageuka
akamwona Yule mwanafunzi aliyependwa na Yesu anafuata. (Yohana 21:20). Huyu
alikuwa ni Yohana. Bila shaka alifanya hivyo kwa kuwa alikuwa ana uhakika kuwa
Baba anampenda hata kama aliyekuwa ameitwa ni Petro.
Lakini Petro, badala ya
kutazama mwito alioitwa nao, na kusimama katika huo, alianza kumwangalia
mwanadamu (Yohana), kisha inasema: Basi Petro akamwona huyo, akamwambia Yesu, Bwana, na huyu
je? (Yohana 21:21).
Je, Baba alimjibu nini
Petro? Alimwambia: Ikiwa nataka huyu akae hata nijapo, imekupasaje wewe? Wewe unifuate
mimi. (Yohana 21:22).
Bwana anatuagiza kwamba: Msiwiwe na mtu
cho chote, isipokuwa kupendana. (Warumi
13:8). Jambo lolote lisilotokana na pendo halitokani na Baba. Wivu, hasira,
chuki, uchungu, manung’uniko …n.k., havitokani na Baba. Na kwa kiasi kikubwa, haya
yanatokana na sisi kujilinganisha na wengine na kujihesabia haki kutokana na
juhudi na bidii yetu katika Bwana.
Pamoja na uelekevu wake
mkubwa, Ayubu naye alifika mahali ambapo alilemewa na majaribu. Matokeo yake
alianza kuingiwa na hali ya kunung’unika. Ndipo Bwana akasema: Ni nani huyu
atiaye mashauri giza kwa maneno yasiyo na maarifa? Basi jifunge viuno kama
mwanamume, maana nitakuuliza neno nawe uniambie. (Ayubu 38:2-3).
Kisha Bwana alianza kumwuliza
Ayubu maswali ambayo, hatimaye, Ayubu alitambua jinsi ambavyo hana cha
kujisifia mbele za Bwana na wala hana cha kumdai Bwana hata kama angefanya
juhudi au wema kiasi gani.
Mambo yote tunayopitia ni
upendeleo tu kutoka kwa Bwana. Unapopitia shida kisha ukapata fursa ya
kumwamini licha ya ugumu wa hali inayohusika, ni upendeleo na baraka kubwa
kutoka kwake. Hatuwezi kuona kikamilifu maana yake sasa, lakini mwisho wa
safari, kila aliyesimama na Bwana atachekelea.
Kutokana na hayo
niliyoandika hapo juu, mtu anaweza kudhani kuona kama kwamba nataka kusema
kuwa, “Usihangaike na watu wengine. Wewe angalia mambo yako na Mungu tu.”
Ni kweli nimesema hivyo.
Lakini huo ni upande tu unaohusu kuchunga roho ya wivu, uchungu na
kujilinganisha na wengine isivyo sawa. Lakini maandiko yanasema kuwa tuwe na
nia ileile iliyokuwa ndani ya Bwana wetu Yesu Kristo (1 Petro 4:1). Ni lazima
tuwapende, tuwaombee, na kuwatakia mema wengine. Mwana mkubwa alitakiwa
kumwombea na kumtakia mema mdogo wake. Petro alitakiwa kufurahia pale Yohana
naye aliposimama kumfuata Bwana.
Lakini tunawezaje kufanya
haya? Hatuwezi! Ni Roho wa Baba ndiye anayetuwezesha. Bwana anasema wazi, Pasipo mimi hamwezi
kufanya neno lolote. (Yohana 15:5).
Jambo la kujiuliza kila
wakati ni je, nimechagua njia ya wivu, uchungu, manung’uniko na kujihesabia
haki au nimechagua kumwomba Bwana anisaidie?
Upotevu wa mwana mdogo si
hatari sana kama wa mwana mkubwa. Ule wa mwana mdogo unaonekana na kujulikana
wazi lakini ule wa mwana mkubwa umejificha na si rahisi kuutambua kama mtu
hayuko makini.
Baba alitoka kwenda
kumlaki mwana mdogo na mwana mdogo akafungua moyo wake wote, akapokea mmwagiko
wa pendo la Baba. Kwa kiwango kilekile cha pendo hakikumwacha mwana mkubwa. Imeandikwa,
Basi babaye
alitoka nje, akamsihi. (Luka 15:28).
Lakini huyo mkubwa alifunga
mlango wa moyo wake. Alifungia nje upendo wa Baba ambao ulikuwako kwa ajili
yake kama ilivyokuwa kwa ajili ya mdogo wake.
Matokeo yake, aliyekuwa
amekufa , alifufuka na kuingia kwenye furaha na pendo la Baba. Yule ambaye
alikuwa hai, alikufa na kukosa furaha na pendo la Baba!
Ndiyo maana Mungu anatuasa
kwa usahihi kabisa: Anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke. (1 Wakorintho
10:12). Pia anasema, … wengi watakuja kutoka
mashariki na magharibi ,nao wataketi pamoja na Ibrahimu, na Isaka, na
Yakobo katika ufalme wa mbinguni, bali
wana wa ufalme watatupwa katika giza la nje… (Mathayo 8:11-12).
Ni hatari sana kujiona
kuwa tunastahili sana baraka za Mungu kwa vile tu eti tunatoa sadaka, tunasali
sana, tunaimba, tunawahi kanisani, n.k., na hasa pale tunapotumia vigezo hivyo
kuwaona wengine kuwa hawafai.
Ni kweli unaweza kusema,
“Baba, umeniambia niombe, nami nimeomba lakini sijapata nilichokuwa naomba. Ninaomba
Roho Mtakatifu unisaidie kufanya kile ambacho kinapunguka hadi nifikie jibu
langu.” Lakini usiseme, “Baba, mimi nimeomba kama ulivyoagiza, mbona fulani
amepata jibu lake wakati yeye hata haombi kama mimi; hatoi kama mimi; hawahi
kanisani kama mimi?”
Huku ni kujihesabia haki
na kumdai Mungu. Hakuna mwanadamu anayeweza kumdai Mungu kitu chochote.
Ukristo na wokovu SI DINI!
Ni uhusiano binafsi na Mungu aliye hai kila saa, kila dakika, kila sekunde. Ni
maisha! Si mkusanyiko wa vitendo vya kusimama, kupiga magoti, kuimba, kufumba
macho, n.k., vinavyofanyika wakati fulani tu katikati ya kusanyiko liitwalo
“Kanisa” au “ibada.” Kanisa au ibada ni mwendelezo tu wa kile ambacho
kinatakiwa kuwa ndiyo maisha yetu muda wote.
Unyenyekevu mbele za Mungu
unaokiri kuwa “Siwezi bila wewe ee Bwana”; na uhakika kuwa pendo la Baba kwangu
halibadiliki kamwe ni mambo muhimu kuwa nayo moyoni kila wakati.
Pendo la Mungu Baba na
Mwana na ushirika wa Roho Mtakatifu viwe nawe siku zote. Amina.
Asante John, nimekupata vizuri sana kwenye ujumbe huu wa Mwana Mpotevu
ReplyDeleteAmen Stars. Barikiwa na Bwana Yesu.
DeleteAsante Yesu Kristo. Nimejifunza na kuelewa jambo muhimu sana kupitia mafundisho haya ya mtumishi wako. Amen...
ReplyDelete