Friday, December 13, 2013

Saa 8 mbinguni - Sehemu ya 2




Mchungaji Ricardo Cid


Ndugu msomaji wa blog hii, katika sehemu ya kwanza ya ushuhuda huu tuliona jinsi ambavyo Ricardo amechukuliwa na malaika wa Bwana kupelekwa mbinguni kukutana na Bwana Yesu. Walikuwa wamepita mbingu ya kwanza na wako kwenye mbingu ya pili. Wakati akiwa anaangalia shughuli mbalimbali za mapepo kwenye mbingu hiyo, kwa mbali aliona nyota yenye mwanga mkali ikiwajia pale. Je, hiyo ilikuwa ni nyota ya namna gani? Na je, nini kiliendelea baada ya hapo? Tafadhali karibu kwenye sehemu ya 2 na ya mwisho ya ushuhuda huu wenye ujumbe muhimu kwa Kanisa.

………………………………..

Kadiri nyota ile ilivyokaribia, ilikuwa ikileta sifa kubwa na kumwabudu Bwana. Lakini kumbe hii haikuwa nyota. Walikuwa ni mamilioni ya malaika wakiwa wamepanda farasi weupe huku wakimsifu Bwana wa Majeshi!! Walikuwa wakipaza sauti wakisema, “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu. Ni Yeye aliye hai toka enzi hata enzi! Bwana ndiye Alfa na Omega; Mwanzo na Mwisho; na kila mwenye pumzi na amsifu Bwana.” Hatimaye niliona vita vikuu na wale mapepo hawakuonekana tena. “Usiogope tena maana wako malaika wengi zaidi upande wetu kuliko wale walio upande wa adui!”

Malaika hawa walifungua njia kuelekea kwenye mbingu ya tatu. Walijigawa katika makundi mawili; moja kulia na jingine kushoto. Njia ya kuelekea kwenye mbingu ya tatu ilikuwa sasa wazi! Njia hii ilifika hadi mbinguni na ungewea kuona mji wa Mungu. (Kuna satelaiti duniani ambayo imewahi kupiga picha ya mji huu. Mji huu wa kiroho upo! Hili lilitajwa kwenye redio na TV). Niliweza kuiona njia hii ya malaika wenye utukufu na wanaovutia. Walisafisha eneo lote na kukawa hakuna tena mapepo; na hawakuacha kumsifu Mungu na kulibariki Jina lake! Malaika wale waliniweka mbele yao na kuniambia, “Ni lazima usubiri hapa!”

Kisha kwa mbali, nilitazama kwenye ule mji, nilimwona mmoja akiwa amevaa mavazi meupe, akiwa juu ya farasi mweupe. Kadiri alivyonikaribia mimi, malaika hawakuacha kumsifu na kumwinua Mungu. Alikuja hadi takriban meta 4 kutoka kwangu. Alikuwa ni mzuri sana kuliko wale malaika wote. Nilitarajia angezungumza nami. Lakini alichofanya ni ni kunitazama kwa muda kidogo kisha akapaza sauti akisema, “Ni mimi! Mimi ni Mikaeli, malaika mkuu ambaye anasimamia ulinzi juu yako na juu ya Kanisa duniani!” Nilikutana na malaika mkuu uso kwa uso, na alikuwa ni kiumbe wa thamani sana! Aligeukia upande na kuonyesha njia ili niweze kuingia ule mji wa mbinguni. Alisema, “Ingia! Bwana Yesu anakusubiri!”

Nilikuwa natembea kwenye barabara kuingia kwenye mji. Malaika walikuwa wakipaza sauti zao na kumsifu Bwana. Nililia na kulia wakati nikiwa wautazama mji ule.



Mji ulikuwa umejengwa kwa dhahabu safi iliyo kama kioo na milango ya kuingilia mji ilitengenezwa kwa lulu. Sakafu ilikuwa ni kama fuwele (crystal) kwa mwonekano. Sikuwa

nimewahi kuona kitu kama hiki duniani; na wala hakuna mwanadamu anayeweza kukitengeneza. Mjenzi wake alikuwa ni Bwana na Mungu wa ulimwengu wote. Nilikuwa nje ya mji na milango ilikuwa wazi. Na milango ile bado iko wazi. Niliweza kuona ndani ya mji; na kwenye kuta kulikuwa na rubi na yakuti samawi na lulu ambazo zilikuwa zinang’aa sana. Na ndani ya mji kulikuwa na mamilioni kwa mamilioni ya sauti zikimsifu Mungu! Nilitetemeka kutokea nje ya mji niliposikia hivyo. Nilisikia sauti moja ambayo ilitetemesha mbingu na nyuma ya sauti hii mamilioni kwa mamilioni ya sifa kwa Mungu yakisema, “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu ni Mwana Kondoo wa Mungu na Baba ambaye utukufu na heshima ni zake milele na milele, Amen!”


Sauti hii kuu ilisema, “IWENI WATAKATIFU, MAANA MIMI NI MTAKATIFU! NI WALIO WATAKATIFU TU NDIO WATAKAOINGIA HUMU! MAANA PASIPO UTAKATIFU HAIWEZEKANI KUMWONA BWANA!” Bila ya utakatifu, haiwezekani kumwona Yeye.

Sauti moja ilisema, “Ingia,” nami nikaingia kwenye mji ule. Na niliona kiti cha enzi cha ajabu kikiwaka moto. Na moto ulipokuwa ukitoka kwenye kiti kile, nikawa makini na nikamwona Yesu, Mfalme wa wafalme na Bwana wa mabwana! Nilianguka chini mbele zake sina nguvu. Mkono wake ulitokea kwenye ule moto na kunielekea mimi; na akasema, “Simama kwa miguu yako!”

Nilipata nguvu na nikasimama. Mara moja nilianza kugusa miguu yake na mikono na mwili wake. Nilipoona uso wake, mwonekano wake haufanani hata kidogo na kile ambacho wasanii huchora duniani! Watu wengi hutengeneza miungu ya miti na sanamu zingine mbalimbali! Lakini napenda niwaambie ndugu zangu, kwamba Yesu hakuwa na sura hizo. Alikuwa ni Mungu aliyejaa misuli! Si Mungu wa lelemama na dhaifu. Ni Mwenye Nguvu!! Alisema, “Mimi si Mungu aliyeundwa kwa chaki au mti. Mimi ni Mungu aliye hai na aliyepo!” Aliendelea kusema, “Kawaambie Kanisa langu duniani kwamba Mimi ni halisi!! Mimi kweli naishi na nipo! Waambie watu wangu kuwa mbingu ni halisi na Mimi ninawangojea.”

Aliniambia, “Njoo. Tembea pamoja nami ili nikuonyeshe jambo moja kubwa.” Tulitazama chini na kuona dunia na vyote vilivyomo humo. Yesu akasema, “Ninao uwezo wa kuona kila kitu ambacho Kanisa langu linafanya!”

Anajua kila kitu tufanyacho na niliweza kuwaona wengi wenu kutokea mbinguni. Yesu aliniambia, “Liangalie Kanisa langu!” Nami niliwaona ndugu wakiwa kinyume na ndugu; kanisa kinyume na kanisa. Yesu aliniambia, “Kanisa langu limeshapoteza imani yake. Hawataki kuniamini Mimi. Uovu umeongezeka duniani na watu hawataki kuamini kuwa Mimi nipo. Waambie watu wangu kuwa naenda kufanya jambo kubwa duniani! Kanisa langu linarudi nyuma badala ya kukua.”

Bwana alianza kulia kwa ajili ya Kanisa lake, na akasema, “Kanisa hili si Kanisa langu!” Nikasema, “Bwana, usiseme hivyo! Sisi ni Kanisa lako.” Kisha Bwana akajibu, “Hapana, kanisa langu linatembea katika nguvu za miujiza na ishara na maajabu! Kanisa langu limepungua! Hata hivyo, waambie, nitarudi kuja kuwainua tena!”

Aliniambia niendelee kutembea na Yeye na tukapita kwenye mlango mmoja; na chini kulikuwa ni dhahabu tupu. Nilianza kukimbia kwenye mtaa wa dhahabu na kuchukua mavumbi ya dhahabu na kujimwagia kwenye mwili wangu. Kisha Bwana aliniambia nirudi na kukuambia wewe kwamba kuna mitaa ya dhahabu mbinguni.

“Yote haya ni kwa ajili ya watu wangu,” Bwana alisema. “Lakini, ndani ya Kanisa langu wapo wezi ambao wanaiba zaka zangu na matoleo yangu! Waambie watu wangu kuwa hakuna mwizi atakayeingia kwenye ufalme wangu wa mbinguni.”

Tunatakiwa kuyanyosha maisha yetu kwa ajili ya Bwana. Kisha tuliona meza ndefu sana kwa ajili ya mamilioni ya watu, ikiwa imejaa vyakula na viburudisho tele. Kulikuwako pia mataji  mengi na vikombe vya vito kama kioo kwa jili ya watu kunywea humo. Bwana akasema, “Ricardo, yote haya yameshaandaliwa kwa ajili ya watu wangu!” Hii ilikuwa ni meza iliyoandaliwa kwa ajili ya harusi ya Mwana-Kondoo.

Yupo dada mwingine katika Kristo ambaye naye alipelekwa mbinguni na kuonyeshwa malaika wakipita huku na  kule wakiandaa hiyo meza. Nikamwambia Bwana, “Mbona dada yule aliona malaika wakiandaa vitu hapa, lakini sioni maandalizi yoyote yakiendelea?” Bwana akanijibu, “Hiyo ni kwa sababu maandalizi yote yameshakamilika!”

Kuna mataji kwa wale wote ambao wanatenda kazi na ni watii kwa Bwana. Kisha nikasema, “Bwana, sasa utarudi lini kama maandalizi yote yamekamilika? Bado muda gani umebakia hadi urudi? Hebu nionyeshe saa. Ni muda gani umebakia kwenye saa ya mbinguni?” Watu wengine wengi walishaota juu ya saa, ambayo inaonyesha usiku wa kati Bwana anapotakiwa kurudi. Nikauliza, “Bwana, ni lini saa itagonga kwenye muda? Je, bado dakika moja? Bado dakika tano?” Bwana aliniangalia usoni kwa sekunde chache kisha akasema, “Ricardo, mbinguni hakuna tena saa!” Nami nikasema, “Sasa Bwana, kama hakuna tena muda, mbona sasa haujarudi?” Yesu aliinua mkono wake na kwa kutumia kidole gumba na kidole cha shahada akafanya ishara kuonyesha kwamba bado kamuda kidogo sana; na akasema, “Muda wote uliosalia kimsingi ni rehema tu za Baba kwa ajili ya wale waliorudi nyuma ili kuwapa nafasi ya kutubu na kuyafanya matendo yao ya kwanza.” Na Bwana wa majeshi hajarudi kwa sababu ametupa hako kamuda kadogo kwa ajili ya kutubu; na muda huo unaitwa ‘Muda wa neema ya Baba.’ Yesu anakuja muda wowote. Ni lazima tuanze kumtafuta kwa mioyo yetu yote na kufunga na kuomba na kuyafanya matendo yetu ya kwanza. Karibu namaliza. Yesu alirudia kusema, “Tuko kwenye kipindi cha neema ya Mungu.”

Kisha malaika alitokea kulia kwetu na kupaza sauti akisema, “Muda umefika!! Muda umekwisha. Maandalizi yote yako tayari! Yesu anampokea bibi harusi wake!”

Bwana anakuja na dalili zote katika maandiko zimeshatimizwa! Sinema zinaonyesha kwamba kuna jambo la uangamivu mkubwa linakuja. Wanasayansi wanajua kuwa kuna jambo kubwa linaenda kutokea; hawaelewi tu jambo lenyewe ni nini! Hata hivyo, sisi Kanisa tunajua kwamba Yesu anarudi hivi karibuni! Yule malaika alipomaliza kusema vile kwa sauti, mamilioni ya malaika wote walianza kurukaruka na kushangilia kwamba bibi harusi hatimaye anarudi mbinguni. Nikawa nasema, “Kuna nini kinachoendelea?” Lakini hakuna aliyenizingatia. Wote walikuwa wanashangilia zile habari njema. Hivyo, nami nilihngana na malaika wale na kuanza kuliinua jina la Yesu! Wakati huo, nilipoinua mikono yangu, nilihisi mtu ameninyanyua kutoka mbinguni na kunipeleka chini kwa kasi ya ajabu.

Hivi sasa malaika wote wanashangilia kwamba bibi harusi anarudi. Nilirudi duniani na nilidondoshwa kwenye madhabahu ambako nitaomba kila siku. Muda umebaki kidogo sana!! Kama hutaki kuniamini mimi, basi usoamini. Lakini anakuja na itakuwa ni jambo la milele. Watu wa Mungu hawataki kuamini juu ya unyakuo. Tafadhali amkeni. Amkeni katika ukweli!! (hapa Ricardo Analia).



Bwana alikuwa hapa pembeni yangu na ameniambia, “Ricardo,

hivi ndivyo unyakuo ungekuwa kama ungetokea sasa hivi!” Niliweza kuona dunia yote pamoja na Roho Mtakatifu wa thamani na mzuri, Yeye atupaye Amani na furaha, akiondoka duniani. Kisha niliona mvuke unaingia kwenye Kanisa na kunizunguka; nami nikamwuliza Bwana, “Hii ni nini?” Akasema, “Hiki ndicho ninachokiita Unyakuo.” Niliona watu wakivunja milango ya kanisa wakitaka kuingia ndani, huku wakipaza sauti, “Watoto wangu wako wapi? Wote wametoweka!”


Watoto wote duniani walikuwa wameshatoweka kwa sababu Mungu hatamwacha hata mmoja nyuma. Wa kwanza kuingia kanisani alikuwa ni kiongozi wa kwaya. Alipiga kelele, “Kanisa limeenda wapi! Nimeachwa! Nimeachwa!” Baada ya kiongozi wa kwaya, niliona wachungaji wengine na ndugu wa kiume na kike na waangalizi wa Kanisa, wote wakiangua vilio, “Nimeachwa!”

Wazazi wengi na wenza wengi walikuwa wakiwatafuta wenzi wao na watu Kanisani walijibu, “Wapendwa wako hawako hapa! Bwana ameshawachukua.” Kisha watu wanaanza kulia, “Kumbe ilikuwa kweli. Yesu amekuja na kuchukua bibi harusi wake!”

Watu walikuwa wakilia na kutamani kama wangemwamini Yesu Kristo. Kila ambaye hamwamini Yesu kama Masihi amepotea! Niliona watu wengi na wachungaji wakilia; na watu wakaanza kuwadai wachungaji, “Kwa nini hamkufundisha kweli? Kwa nini hamkufundisha utakatifu na kunionya juu ya haya? Nimeachwa kwa sababu yenu!” Wengi wataachwa kwa sababu hawaishi maisha matakatifu. Tunatakiwa kufundisha utakatifu wa kweli na kuwafundisha watu kufanya toba ya kweli! Niliona watu wakiwapiga wachungaji na kuwachanachana na kung’oa nywele zao. Wachungaji wakalia na kuwaomba watu wasiwadhuru. Watu hawakuwaacha maana sasa walishaingiwa na mapepo.

Yapo makanisa mazimamazima ambayo yataachwa. Nilimwona kaka mmoja ambaye alikuwa anajaribu kung’oa macho yake kutokana na huzuni. Watu wote walijigonga vichwa vyao sakafuni na kwenye kuta kwa sababu hawakuelewa kuwa Yesu alikuwa ndiye jibu pekee. Kwa kuwa watu walitaka kuendelea kwenye dhambi na uovu, na kuishi kama walivyopebda. Watu walijikata na kubamiza vichwa vyao hadi unaona vichwa vinapasuka, kisha wanaanguka ardhini. Damu ilikuwa ikitiririka kanisani kwa sababu ya watu waliokuwa wakijiumiza. Kisha nikamwona kijana akimlilia Mungu, “Tafadhali Bwana, nichukue na mimi!” Alikuwa ameshachelewa. Tayari Yesu alishakuja na kulichukua Kanisa lake. Nilianguka chini kwa sababu niliona mambo mengine zaidi ya kutisha.

Yesu akaniambia, “Wakati wa dhiki kuu, kutakuwa na mateso kuliko ilivyowahi kutokea.” Kisha nikauliza, “Kwa nini watu wanaruka na kujiumiza vibaya namna hiyo?” Bwana Yesu akajibu, “Kwa sababu katika wakati huu, watu watatamani kufa, lakini hawatakufa. Kifo kitakuwa kilishakimbia duniani.” Nikamwuliza Bwana, “Kwa nini wachungaji na watu hawa wote wameachwa?” Na Bwana akasema, “Ni kwa sababu ninawajua. Najua mioyo yao.”

Mungu anatujua. Anajua mioyo yetu yote. Nilianguka ardhini, karibu ya kupoteza fahamu. Yesu akasema, “Nilitaka kukuonyesha haya ili kwamba ukalionye Kanisa na kulipatia matumaini. Waambie kuwa, kama watu wakitubu sasa, nitawasamehe maadamu kungali na muda. Nitatenda jambo kubwa sana duniani.”

Tafadhali, fungueni macho yenu. Kanisa la kiinjili Chile linazidi kukua. “Waambie watu wangu kwamba, kama wakiomba msamaha, nitasamehe.”

Kisha nikaona maono mengine ya moto ambao ulifunika anga lote. Yesu akauliza, “Je, umeona? Huo moto uliouona juu ya dunia, ni moto juu ya nchi ya Chile; maana Chile itakuwa kwa ajili ya Kristo! Mungu ataibadili Chile!” Kisha nikaona moto ule unasogea na kutaka kuja juu ya Chile; na Yesu akasema, “Macho ya Baba yangu yako juu ya Chile.” Moto utakapoangukia Chile, nchi nyingine zitaona na kutambua kuwa Mungu anatembea humo. Kanisa duniani kote lilifurahia kwa sababu ya Mungu kutembea Chile. Mungu alinichukua katika maono hadi kwenye sehemu inayoitwa ‘Paseo Hamada’ na kunionyesha watu ambao walikuwa wametiwa ulemavu na uwete. Kisha nikaona waamini wa kweli wakiwaombea viwete wasio na miguu na kuamuru miguu iote. Miguu ilitii na kuota mbele ya macho yao. Watu wasio na mikono walipata mikono mara moja!

Katika wakati huu, Bwana ataonyesha miujiza inayoumba. Katika makanisa, watu wataponywa. Katika siku hii, wafu watafufuliwa na Mungu atawatumia Chile kufanya miujiza kama hiyo ambayo mitume wa zamani waliifanya kwenye Biblia.

Huo ndio ufunuo mzima ambao Mungu alinipatia mimi (Ricardo Cid). Anakuja hivi karibuni. Maranatha! Amen!

………………………………….

Kama ungependa kusoma ushuhuda huu kwa Kiingereza, bofya HAPA. Bwana Yesu azidi kukubariki mpendwa msomaji wa blog hii.

Kama ungependa kupata ushuhuda huu kama E-book, niandikie kwenye ijuekweli77@yahoo.co.uk ukisema tu: nitumie e-book ya Ricardo, nami nitakutumia mara moja.

12 comments:

  1. Mungu akubariki kwa kutuletea ushuhuda huu

    ReplyDelete
  2. Bwana atugeuze mioyo yetu na tamaa za dunia hii

    ReplyDelete
  3. wenye maskio na waskie.....ubarikiwe sana james

    ReplyDelete
  4. Kweli Mungu akubariki. Tuombeane kwa bidii jamani tusiikose mbingu.

    ReplyDelete
  5. Ubarikiwe sana,ndugu kwa kazi hii kubwa utalipwa usipozimiya moyo,napenda hizi shuhuda sana,Mu gu nijalie neema nishinde diniya na mambo yake

    ReplyDelete