Thursday, May 9, 2013

Siri Inayohusu Moyo wa Mwanadamu – Sehemu ya 1
Mungu anasema mengi sana kuhusiana na moyo. Lakini moyo ni nini? Na umuhimu wa moyo ni nini katika maisha yetu ya kiroho na ya kimwili?

Hebu angalia maandiko machache yafuatayo na uone kile ambacho Bwana anasema kuhusiana na moyo.

Naye akanifundisha, akaniambia, moyo wako uyahifadhi maneno yangu; shika amri zangu ukaishi. (Mith 4:4). 

Mwanangu, usiisahau sheria yangu, bali moyo wako uzishike amri zangu. (Mith 3:1).

Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi. (Zab 119:11). 

Yafunge hayo katika moyo wako daima; jivike hayo shingoni mwako. (Mith 6:21). 

Maandiko haya yanaonyesha kuwa sheria ya Mungu inatakiwa kushikwa au kuwekwa kwenye moyo. Je, maana yake ni nini?  Pia inaashiria kuwa huwa hatuweki sheria yake mioyoni mwetu. Je, huwa tunaiweka wapi badala yake?

Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, wala usizitegemee akili zako mwenyewe (Mith 3:5). 

Ninatakiwa kumtumaini Bwana kwa moyo; sio kwa akili. Hii maana yake ni nini? Kuna tofauti gani kati ya moyo na akili hapa?

Na maneno haya ninayokuamuru leo, yatakuwa katika moyo wako (Kumb 6:6).

Mungu anaposema kuwa maneno yake yawe kwenye moyo wangu, anaamanisha yasiwe wapi? 

Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; maana ndiko zitokako chemchemi za uzima. (Mith 4:23).

Hii inaonyesha kuwa moyo ni wa muhimu sana. Kumbe uzima unatokea moyoni! Lakini je, moyo unalindwaje? 

Ee Yerusalemu, jioshe moyo wako usiwe na uovu, upate kuokoka. Mawazo yako mabaya yatakaa ndani yako hata lini? (Yer 4:14). 

Heri wenye moyo safi; Maana hao watamwona Mungu. (Mt 5:8). 

Je, moyo unaoshwaje? Kuna uhusiano gani kati ya uchafu wa moyo na mawazo?

Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani mkiwa na shina na msingi katika upendo. (Efe 3:17). 

Kristo anakaaje moyoni kwa imani? Nitajuaje kuwa Kristo sasa yuko moyoni mwangu? Nifanye nini ili Kristo akae moyoni mwangu?

Rafiki mpendwa, mambo ya Mungu wetu ni rahisi mno! Tatizo letu ni ukosefu wa maarifa tu! Bwana anasema:

Kwa maana maagizo haya nikuagizayo leo, si mazito mno kwako, wala si mbali.

Si mbinguni, hata useme, Ni nani atakayetupandia mbinguni akatuletee, aje atuambie tusikie, tupate kuyafanya?

Wala si ng'ambo ya pili ya bahari, hata useme, Ni nani atakayetuvukia bahari, akatuletee, aje atuambie, tusikie, tupate kuyafanya?

Lakini neno li karibu nawe sana, li katika kinywa chako na moyo wako, upate kulifanya. (Kumbukumbu 30:11-14).

Mpendwa, iko siri ya ajabu sana kuhusiana na mioyo yetu. Humo ndimo kuna kila kitu tunachohitaji ili kuwa washindi katika maisha haya na yale yajayo.

Fuatana nami katika sehemu ya 2 ya somo hili muhimu sana. Mwisho wa yote utafurahia hakika kile ambacho Bwana ametuandalia. Tena utaelewa nini maana ya andiko hili:

Yote yawezekana kwake aaminiye. (Marko 9:23).

Bwana Yesu akubariki na kuufungua moyo wako.

9 comments:

 1. Ndugu yangu James Bwana Yesu asifiwe. Uzidi kubarikiwa kwa kazi nzuri ya Mungu unayoendelea kuifanya. bado nazidi kukiri kuvutiwa sana na tafakari zako. kwa leo nimeipenda sana hii kwani inazidi kunipa mwanga wa kujitambua mimi ni nani ktk dunia hii na natakiwa kufanya nini. Ubarikiwa sana. kama hutajali kaka; nina maswali machache naomba nikuulize kwa ajili ya kupata uelewa zaidi ila sitauliza kwa sasa mpaka nitakapopata idhini yako.

  Mungu azidi kukubariki.

  Kwa jina naitwa Henry Philip.

  ReplyDelete
  Replies
  1. Shalom Henry.
   Asante kwa kutembelea blog hii. Nasukuru pia kwa kuendelea kunitia moyo kwa kazi hii. Kuhusu kuuliza maswali, tafadhali uliza tu wakati wowote na maswali yoyote.
   Ubarikiwe.

   Delete
 2. Asante sana Kaka James. Ninaomba unisaidie kuhusu maswala ya vyakula. Kwa ninavyofahamu ktk vyakula Mungu aliumba vitu vyote kwa uzuri na hakuna kilicho najisi mbele zake naye alitupa uhuru wa kuvitumia kwa kutumia utashi na akili alizotupa maadamu tu tutagundua kama vinafaa kwa afya na mwili wa mwanadamu. Sasa huwa natatizika pale baadhi ya madhehebu wanapobatilisha baadhi ya vyakula kuwa Mungu alivikataza tusivile; mfano nguruwe, sungura na wanyama wengine ambao kwato zao hazijagawanyika katikati, hata kwa upande wa samaki wasio na magamba pia Mungu alikataza- Imani hii iko kwa wasabato zaidi. Je Mungu anatuambia nini kuhusu suala la vyakula? Nitashukuru sana endapo utanisaidia katika hili ili niondoe utata ulio ndani yangu na pia niweze kuwasaidia wengine walio katika utata huu.

  Ubarikiwe sana kaka James.

  ReplyDelete
  Replies
  1. Asante sana kwa swali lako. Ninaposoma Biblia naona mtiririko ufuatao kuhusiana na Yehova kuenenda na wanadamu tangu mwanzo.

   Lengo kuu kabisa la Mungu wetu ni sisi tukaishi naye milele makaoni mwake mbinguni ili tukamwabudu, tukamjue, tukamfurahie, na ajabu zaidi, anasema TUKATAWALE naye milele. Lakini baada ya anguko la mwanadamu na dhambi kuingia ulimwenguni, amekuwa akiendelea na kusudi hilo hilo hatua kwa hatua. Kwa vile mwanadamu alishajichafua kwa dhambi, Mungu aliandaa utaratibu wa kumsafisha na kumtakasa kabisa kiasi cha kuweza kuingia mbinguni.

   Aliandaa Mwanakondoo wa sadaka ambaye ni Yesu Kristo, ambaye angemwaga damu yake itakasayo dhambi kabisa. Kwa hiyo, alianza kumwandaa na kumfundisha mwanadamu hatua moja baada ya nyingine.

   Kwanza, alianza kumfundisha kuhusu dhambi kupitia maisha ya kimwili (kwa mfano kulikuwa na amri zinazozuia kugusa mzoga au maiti na kutokula vyakula mbalimbali kama ulivyotaja). Lakini baada ya Yesu kufa, Bwana anasema kupitia Paulo: Basi ikiwa mlikufa pamoja na Kristo mkayaacha yale mafundisho ya awali ya ulimwengu, kwa nini kujitia chini ya amri, kama wenye kuishi duniani, Msishike, msionje, msiguse (Kol 2:20-21. Na hata Yesu mwnyewe alipokuja: Akawaita makutano akawaambia, Sikilizeni, mfahamu; Sicho kiingiacho kinywani kimtiacho mtu unajisi; bali kitokacho kinywani ndicho kimtiacho mtu unajisi. (Mt 15:10-11).

   Kulikuwa pia na adhabu za kimwili. Kwa mfano, aliyekamatwa kwenye uzinzi, alipigwa mawe hadi kufa. Vilevile, aliyetaka kusamehewa, alitoa mnyama kabisa ambaye alichinjwa na damu yake ilihesabiwa kuwa ni badala ya yule mdhambi.

   Lakini hayo yote yalikuwa ni ishara ya kile ambacho kilikuwa kinangojewa, yaani Yesu. Torati kwa ujumla wake ilikuwa na lengo la kutuonyesha jinsi ambavyo hatuwezi kuishi sawasawa na amri za Mungu ili tuone ulazima wa kumtegemea Bwana Yesu ambaye ndiye atutakasaye.

   Sasa, hebu naomba angalia upande wa kulia wa blog hii kuna Blog Archive. Bonyeza mwaka 2012. Kisha bonyeza mwezi mei. Humo kuna somo ambalo lina kichwa: JE, SABATO NI SIKU KATIKA JUMA? Humo utapata mwanga fulani juu ya lengo la agano la kale na mambo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na vyakula. Japo lengo kuu kabisa la somo hilo si vyakula, lakini hebu lisome halafu tuendelee kujadiliana juu ya jambo hili. Asante.

   Delete
 3. Hallo kaka James, Tumsifu Yesu kristu daima. natumai tena leo uko mzima ukiendelea na utume wa kazi ya Mungu. Nashukuru kwa kunijibu kwa ufasaha swali langu na nimepata mwanga zaidi kwa kupitia somo ulilonielekeza. kusema kweli nimepata uelewa mkubwa sana hata wa mambo mengine ambayo kwangu ilinitatiza.

  Tuombe uzima, nitaendelea kuwasiliana nawe endapo kuna maswali mengine nitakayokutana nayo.

  Mungu akubariki sana katika kazi yake.

  ReplyDelete
  Replies
  1. Milele amina. Tumsifu Yesu Kristu. Namshukuru Mungu kama umepata jambo la kukufaa katika makala hayo. Karibu tena na tena na tuzidi kujifunza. Bwana Yesu azidi kukubariki.

   Delete
 4. Amen mtumishi wa Mungu,yaani somo hili limeniweka mahala pa zuri na kujua kumbe mimi ni shujaa.

  ReplyDelete
  Replies
  1. Amen brother Yusufu. Natumaini umesoma pia sehemu ya 2 na ya 3. Bwana Yesu akubariki.

   Delete
 5. Ubarikiwe sana kwa mafundisho haya yamenifungua kwakweli nilikuwa najiuliza mbona huwa sijisikii ishara yeyote moyoni mwangu kumbe moyo umegubikwa na matatizo. sasa nataka nianze maombi ya nguvu ya kuufungua moyo nimeokoka muda mrefu lakini sijawahi kuihisi nguvu ya Mungu ikipita ndani yangu au kuusikia moyo wangu amani au kukosa amani, nimeombewa na kuombewa lakini sijawahi kuhisi chochote ndani ya moyo wangu, na mimi ni mwanamaombi haswa lakini moyo wangu hujawahi kuhisi chochote kile na huwa namwambia Yesu aingie moyoni mwangu basi anibadilishe hata utu wangu wa ndani lakini sijahisi chochote namwambia na Roho Mtakatifu afanye hivyo lakini wapi sa najiuliza mimi na shida gani, na sinaga tabia ya kutokusamehe au kumfungia mtu kinyongo lakini nashindwa kuelewa mbona chemchem na maji ya uzima haitoki moyoni mwangu nawakati Yesu alisema yeyote atakae niamini mimi mito ya maji ya uzima itabubujika kutoka moyoni mwake mbona mi haitoki. nilikuwa katika hali ya vifungo kwa muda mrefu lakini namshukuru Yesu kanifungua lakini shida mbona huyu Yesu namwita kila wakati na hajifunui moyoni mwangu

  Hebu mtumishi nielekeze hata maombi ya kuomba ili moyo wangu upate kufunguka na mito ya maji ya uzima ianze kutiririka.

  ReplyDelete