Saturday, May 11, 2013

Siri Inayohusu Moyo wa Mwanadamu - Sehemu ya 2




Mwanadamu alivyoumbwa

Tukisoma Biblia kuhusiana na uumbaji wa mwanadamu, imeandikwa hivi:

Bwana Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai. (Mwanzo 2:7).

Kulingana na andiko hili, tunajifunza yafuatayo:
(a) Mwanadamu ana sehemu kuu mbili.
(b) Sehemu ya kwanza ni mavumbi, yaani mwili unaoonekana 
     kwa  nje na tunaweza kuugusa.
(c) Sehemu ya pili ni pumzi ya uhai ambayo iko ndani na hatuwezi
     kuiona wala kuigusa.
(d) Mavumbi pamoja na pumzi ya uhai yanaunda nafsi hai.


Tunafamu kuwa mwanadamu aliye hai ana hisia, mawazo, akili, utashi na kumbukumbu. Lakini haya yote ni mambo yasiyoonekana kwa macho ya nyama – ila tuna uhakika kabisa kuwa yapo.

Vilevile, tunafahamu kuwa mtu akifa, mwili unaobakia hauna hata moja kati ya mambo hayo hapo juu, yaani:
- Hauwezi kuhisi
- Hauwezi kuwaza
- Hauna akili
- Hauna utashi
- Hauna kumbukumbu.

Hili linatupa ishara kuwa, mambo haya ni sehemu ya ile pumzi ya uhai. Tunasema hivi kwa sababu, tunaposoma habari ya tajiri na Lazaro kwenye Luka 16:19-31, tunaona kwamba:
(a) Ana hisia ndiyo maana anateseka kwa joto
(b) Ana mawazo na akili, kumbukumbu na utashi ndiyo maana
     anawafikiria ndugu zake waliokuwa duniani na anaamua
     kuomba msaada kwa Ibrahimu ili yamkini Lazaro aende 
     kuwapelekea maonyo kule duniani.

Lakini, ni wazi kuwa mambo hayo yote, mwili wake uliobakia duniani hauna kamwe uwezo wa kuyafanya.Kumbe basi, pumzi ya uhai ndiyo inayobeba mambo haya yote ambayo hayaonekani wala kugusika. Haya ni sehemu ya yule mtu wa ndani, ambaye adumu milele.

Pumzi ya uhai
Tukiachana na mwili sasa, hebu tuangalie huyu mtu wa ndani kwa ukaribu zaidi.

Biblia inasema kuwa: Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu (Yohana 6:63). Pia inasema: Maana kama vile mwili pasipo roho umekufa … (Yakobo 2:26).

Kumbe basi, mtu halisi ni roho. Roho ni mtu mwenye umbile kama ulivyo mwili wetu wa nyama (mavumbi). Na roho ikitoka inaondoka na yale yote yasiyooneka huku mwili ukibakia bila ufahamu hata chembe.

Hii roho ndiyo yule mtu wa ndani kwa ujumla wake; ndiyo ile pumzi ya uhai aliyopulizia Mungu ndani ya mavumbi. Na ndani ya hii roho ndimo ulimo moyo na akili na utashi, n.k.

Kielelezo kifuatacho kinaweza kutusaidia kuelewa kirahisi haya ambayo tumeyasema hadi hapa. Sina uhakika kabisa iwapo moyo unakaa kichwani tu na kwenye mwili wote kama roho. Ila hiki ni kielelezo tu kuonyesha uhusiano ulivyo. Huenda moyo umejaa kila sehemu. Ila ninachojua tu ni kwamba, upo.


Tafadhali, nakukaribisha uungane nami tena kwenye Sehemu ya 3 ya somo hili kuhusu moyo ili tuweze kupiga hatua zaidi.

Kama kuna swali lolote au hata ushauri au ufafanuzi kama kuna mahali nimeeleza isivyo sawa, tafadhali usisite kuandika maoni kwenye sehemu ya comments au kwenye baruapepe yangu: ijuekweli77@yahoo.co.uk.

Mungu akubariki.

2 comments:

  1. Tumsifu Yesu Kristu kaka James, Nazidi kumshukuru Mungu kwa mema mengi anayozidi kunitendea. namshukuru Mungu pia kwa zawadi ya karama aliyokujalia na unaitumia vema katika kusaidia walio wengi kuokoka roho zao. Mungu azidi kukuneemesha katika kazi yake.

    Kaka James, nina ombi moja kwako naomba tafadhali unisaidie kama itakuwa ndani ya uwezo wako. huwa nazichukuwa hizi tafakari zako na kuwatumia rafiki zangu wengi nilionao katika kurasa za face book nk. sasa baadhi yao au wengi wao lugha ya kiswahili inawapiga chenga hivyo wameona nilichopost kwao ni kizuri baada ya wao kusoma mistari ya biblia ulizoziainisha ktk tafakari hizo. sasa wameniomba nitafsiri ujumbe uliopo katika tafsiri hizo ili nao waonje kile nilichokipata katika tafakari hizo.

    Kristu ndiye tumaini letu daima.

    Nakutakia kazi njema kaka James.

    Ni mimi Henry

    ReplyDelete
    Replies
    1. Amina Br. Henry. Nimekuwa siko kwenye blog kwa muda kidogo sasa. Kuna mahali niliko; namalizia majukumu yangu kisha nitarudi na kuona cha kufanya kuhusu ombi hili.

      Delete