Emmanuel Eni alizaliwa nchini Naijeria. Alipitia mateso na dhiki nyingi chini ya vifungo vizito vya ibilisi. Katika ushuhuda huu, anatusimulia kile kilichotokea maishani mwake, mateso aliyopata na hatiamaye jinsi Bwana alivyompa ushindi.
……………………………………………………..
Sura ya 1: Kutorokea kwangu kwenye "Maisha Mapya"
“Mlee mtoto katika njia impasayo, naye
hataiacha, hata atakapokuwa mzee.” (Mithali
22:6)
Hii ni
hadithi inayohusu kazi za Mungu – kubwa, za ajabu na za kushangaza – kufuatia
kutii kwangu agizo la YESU KRISTO kwangu kwamba: “Nenda ukashuhudie
kile nilichokutendea.”
Mara nyingi
watu huchukulia matatizo kama ni mambo yaliyo nje ya uwezo wetu na kwamba
hatuna tunaloweza kufanya kubadili matukio maishani mwetu. Kwa kiasi fulani
hili ni kweli. Kuhusiana na mwana wa Mungu, maisha yake yako katika mpango
(Mith 16:9). Kama mpango huo utatimia au la, inategemea mambo kadhaa, yakiwamo ukaribu
wa mhusika na Mungu, mtazamo wake juu ya makusudi hasa ya maisha, pamoja na
aina ya mazingira ya kijamii na kiroho anakojikuta.
Mtiririko wa
maisha yako unatiwa changamoto na mambo yaliyo nje yako. Mgogoro mkuu unafikiwa
pale unapotupilia mbali UTASHI wako, kwa uzuri au kwa ubaya. Unaweza kupenda au
kuchukia. Unaweza kutaka kuelewa au kutoelewa. Utashi wa kutii ndio nguvu kubwa
kabisa ya Mkristo aliyezaliwa upya; huku utashi wa kutokutii ndio nguvu kubwa
kabisa inayomharibu mwenye dhambi.
Mtoto
akiachwa peke yake duniani, anatawaliwa na mojawapo kati ya nguvu mbili – uzuri
au ubaya; kuwa sawa au kuwa mkosaji; Mungu au ibilisi. Kila mtu anatiwa
changamoto na nguvu hizi mbili katika maisha; na kila mmoja wetu ni lazima
achague ni maisha gani atakayoishi. Na naamini hicho ndicho ambacho Biblia inachomaanisha
pale inaposema: “Mlee mtoto
katika njia impasayo, Naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee.” Utakubaliana na mimi kuwa mtu
aliye karibu kabisa na moyo wa mtoto yeyote ni mama yake. Yatima ana bahati
mbaya hivyo anaweza kushambuliwa na ibilisi kirahisi zaidi kuliko mtoto mwenye
wazazi. Mama ni mlinzi wa mwili na roho lakini inakuwa ni matatizo makubwa
wazazi wanapokuwa wamepotea, tena katika mazingira ya kutatanisha.
Hadithi
yangu ilianza miaka 22 iliyopita katika kijiji kidogo kiitwacho Amerie Iriegbu
Ozu Item katika Mamlaka ya Serikali ya Mtaa ya Bende, kwenye Jimbo la Imo.
Wazazi wangu hawakuwa kati ya watu matajiri lakini baba yangu alibahatika
kumiliki hekta 42 za ardhi kutoka kwa babu yangu, baraka ambayo leo imegeuka
laana kubwa katika historia ya familia yetu. Baba yangu alikuwa akionewa sana
wivu na ndugu zake wa karibu na wa mbali kwa sababu ambazo sizielewi. Labda ni
kwa sababu ya hicho kipande kikubwa cha ardhi alichorithi.
Tulikuwa ni
familia yenye furaha; tukiwa tumezaliwa ndugu wane: Love, Margaret, Emmanuel na
Chinyere. Baada ya kupata mabinti wawili, wazazi wetu walisubiri kwa miaka 14
ndipo nilipozaliwa mimi (mvulana pekee) na baadaye ndipo akazaliwa mdogo wangu
wa kike, Chinyere. Hii ilileta furaha kubwa sana kwenye familia japo haikuwa ya
muda mrefu kwani muda mfupi baadaye ndipo janga la kwanza lilipotokea. Mama
yangu mpendwa alifariki. Ilidaiwa kuwa alikufa kwa kulogwa; na miaka minne
baadaye, baba yangu naye alifariki. Naye ilidaiwa kuwa alilogwa.
Miaka miwili
baada ya hapo, dada yangu mkubwa, Love, alipotea kusikojulikana na Margaret,
anayemfuata, alipata ukichaa. Ulikuwa ni mlolongo wa majanga kwenye familia
ambayo ilikuwa haina makuu lakini yenye furaha.
Mimi na dada
yangu wa mwisho tulipelekwa kwa babu na bibi yetu. Huko nilimaliza shule ya
msingi na kujiunga baadaye na Item High School. Nilisoma hadi Darasa la III na
kuacha shule kwa kukosa ada, n.k. Muda mfupi baada ya hapo, babu na bibi nao
walikufa. Baada ya taratibu zote za mazishi kwisha, ndugu tusiyemjua alikuja
kumchukua mdogo wangu, Chinyere na hadi leo sijui yuko wapi. Kutokana na mateso
mengi, nililazimika kurudi kwenye nyumba ya baba yangu, na nikawa naishi peke
yangu toka nikiwa na miaka 13. Mtoto wa miaka 13 anawezaje kujitunza peke yake
katikati ya maadui wa baba yake ambao pia ni maadui zake? Nilikuwa ni mtu aliyejawa
na hofu sana! Matukio hayo yote yalikuwa ni kama yamenifikisha mahali ambako hata
kuishi kukawa hakuna maana. Je, kulikuwa na yeyote anayejali? Je, kulikuwa na
mtu aliyewaza juu ya majaliwa ya huyu mtoto mdogo?
Siku moja
nilikutana na rafiki niliyemjua shuleni, aliyeitwa Chinedum Onwukwe. Chinedum
alinipenda sana na baada ya kusikia yote yaliyonikuta, alinichukua hadi kwa
wazazi wake ambao nao walikuwa tayari kunipokea kama mtoto wao mwingine. Maisha
yalirudi kwenye hali ya kawaida tena. Nilikuwa mwenye furaha tena. Ndipo
nilipojua kuwa Mungu ambaye mama yangu alimwomba pale alipokuwa hai alikuwa ni
Mungu aliye hai mahali fulani na ndiye aliyenipatia wazazi wengine wapya. Hivyo
ndivyo nilivyowaza moyoni mwangu. Nilifurahia hali hii kwa miaka ipatayo
miwili, kisha ibilisi alivamia tena!
Chinedum na wazazi wake walikuwa wanasafiri hadi Umuahia na gari yao iligongana na lori lililobeba mchanga. Chinedum na wazazi wake walikufa papo hapo! Niliposikia habari hizi, nilipoteza fahamu. Majonzi yangu yalikuwa makubwa sana. Niliweza kustahimili hadi msiba ulipoisha, ambapo nilikuwa nikiwaletea kuni na vitu vingine wale waliokuwa wakipika. Mwisho wake nilirudi tena kwenye nyumba ya baba yangu na kuanza tena kufanya kazi za mikono ili niweze kuishi.
Niliendelea kufanya kazi mbalimbali kwenye mashamba, bustani, kuvua samaki, n.k. hadi siku moja, mtu mmoja alinichukua ili nikamlimie shamba lake kwa pesa kidogo (50k). Kule shambani alinihoji maswali mengi sana. Kwanza, aliniambia nimwonyeshe ardhi ya baba yangu. Pili, nimkabidhi hiyo ardhi. Nilimkatalia katakata matakwa yake, naye akawa amechukia. Akaapa kuwa angeniulia hukohuko porini. Niliogopa na nikaanza kukimbia huku nikipiga yowe kuomba msaada.
Kwa bahati
mbaya, kwa kuwa sehemu yenyewe ilikuwa ni mbali porini, hakuna aliyekuja kunisaidia,
bali Mungu mwenyewe. Mtu huyo alinifukuza huku ameshika kisu. Lakini kwa sababu
nilikuwa mdogo, niliweza kukimbia kwa wepesi kuliko yeye. Hatimaye nililitumbukia
kwenye shimo la kina cha meta kama 1.82 hivi na nikafunikwa na majani ndani
yake. Alinitafuta lakini baada ya muda alikata tamaa. Baadaye nilitoka shimoni
na kwa kutumia njia nyingine, nilirudi kijijini. Nilitoa taarifa kwa wazee
lakini hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa – hali ambayo huwakuta yatima wote.
Jambo hili lilijenga chuki kubwa sana kwenye moyo wangu wa kitoto – hakuna aliyenipenda;
hakuna aliyenijali! Niliwaza moyoni mwangu, kwa nini mtu atake kuniua huku
akijua kuwa sina wazazi? Maisha yalikuwa yamejaa mateso.
Sasa naelewa
kuwa Mungu katika upendo wake alimzuia ibilisi kuniingizia mawazo ya kujiua.
Niligeukia Kanisa na kuwa mshirika kamili wa Kanisa la Wokovu (Assemblies of
God) pale kijijini kwangu – na hadi sasa bado ni mshirika – lakini kwa bahati
mbaya, hata hapo hakuna aliyenijali japo baadhi ya washirika walifahamu hali
yangu. Ni muhimu kukumbuka kwamba, nilifanyika mshirika kamili wa Kanisa hata
kabla ya kumjua Yesu Kristo. Sikujua maana ya KUZALIWA UPYA. Kama uko kwenye
Kanisa la Yesu Kristo na ukajikuta kwenye hali niliyopitia, mpe Bwana Yesu
maisha yako. Maandiko yanasema: “…huku
mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo
yenu.” (1 Petro 5:7).
Katikati ya
magumu na mateso haya yote
ALICE alitokea! Alice alikuwa ni msichana niliyemfahamu tokea shuleni. Alikuwa mkubwa
kwangu kwa miaka mitano zaidi na tulitokea kijiji kimoja. Tulikuwa darasa moja;
tulikaa dawati moja; na tulikuwa marafiki wakubwa. Tukiwa katika ‘mapenzi’ haya
ya kitoto, tuliahidiana kuwa tutakuja kuoana tukiwa wakubwa. Mzaha mkubwa! Mtoto
wa miaka 11 wakati huo, asiye na wazazi, asiye na elimu, asiye na chakula, anaahidi
kumuoa msichana aliyemzidi kwa miaka mitano! Baadaye Alice aliondoka na kwenda
Akure kwa ajili ya masomo yake ya sekondari na akawa ananitumia barua nyingi
sana za ‘mapenzi’.
Kwa mara
nyingine nilipokutana na Alice, nilikuwa nina miaka 15 na yeye 20. Alishamaliza
elimu ya sekondari na alikuwa akifanya kazi Standard Bank Lagos (inayoitwa sasa
First Bank), huko ambako waliishi wazazi wake.
Kwa vile Alice
alifahamu historia yangu na shida nilizopitia, aliamua kuitumia hali hiyo kwa
faida yake. Aliniambia nisafiri hadi Lagos kwenda kuungana naye na akanitumia
Naira 50 (Naira ni fedha ya Naijeria)! Hizo zilikuwa ni fedha nyingi sana kwa
mtoto wa miaka 15 ambaye hajawahi kupata hata N2 kwa siku! Hii ilikuwa ni mana
kutoka mbinguni; nah ii ilinipa picha kuwa Lagos ni lazima kutakuwa ni mahali
pazuri sana, penye fedha nyingi na vitu vizurivizuri kwa ajili ya kula raha. Kwa
hiyo niliwaza kuwa ni lazima niende Lagos ili na mimi nikatafute fedha zangu na
kuwa tajiri kama wengine. Akilini mwangu, kwenda Lagos ilikuwa ndiyo njia pekee ya kutoroka kutoka kwenye
mateso yangu; kutoroka mbali na maadui wa baba yangu; mbali na maadui zangu;
mbali na njaa na matatizo yangu yote! Kutoroka!
Kutoroka! Ndiyo, kutoroka mbali na kila
kilicho kilicho kiovu!!!
………………………………………….
Je, nini
kilitokea kwa Emmanuel baada ya hapa? Fuatana nami kwenye Sehemu ya 2 ya
ushuhuda huu.
Asante kwa shuhuda hii nasubiri sehemu ya 2 Naitwa Wane Msukwa-Sehemu ya pili unaiweka lini?
ReplyDeleteAsante Wane. Sehemu ya 2 iko tayari kwenye page.
DeleteNinawiwa kumshukuru Mungu Kwa Ajili yako kazi yako njema Mtu wa Mungu Ninasubiri sehemu ya pili Asante = Apostle Peter Minja JPP-MINISTRY
ReplyDeleteBarikiwa Mtumishi wa Mungu aliye hai, Apostle Peter. Naendelea kuweka sehemu moja baada ya nyingine.
Deletemungu akubariki mtumishi wa mungu James, nimejifunza jambo kubwa sana kuwa mpango wa kuokolewa kwa mtu unnaanza mbali sana. Anyango
ReplyDeleteShalom Anyango
ReplyDeleteubarikiwe na Bwana. Tuendelee kujifunza.