Monday, March 10, 2014

Mwanafunzi wa Mchawi - Sehemu ya 4


Kuhubiri Injili kwa kila kiumbe na kila mahali


Matibabu ya kisaikolojia (psychotherapy) ni aina nyingine ya mazoezi ambayo yanaonekana ni ya kisayansi kabisa, kama njia ya kuwasaidia watu. Watalamu wengi wa  ‘psychotherapy’ hutumia taaluma hii kuwasaidia watu sababu hasa ya majonzi yao (depression) au kubadili namna ya tabia au mazoea mabaya waliyo nayo. Lakini ni nini hasa kinachoendelea humo? Wanafungua milango ya ndani na kwa kufanya hivyo, wanafungua njia kwa kazi za mapepo. Hii ni pamoja na aina zote za mapumziko ya kisaikolojia (psychological relaxations).


Leo nchini kwenu kuna mambo ya uaguzi (fortunetelling). Ziko namna nyingi za kufanya haya. Haya ni mambo kutoka kwa shetani moja kwa moja. Watu wakikubaliana na uaguzi wanakuwa wamefungulia mlango kwa mapepo.  Haya ni mapepo ambayo hutabiri mambo yajayo. Yanaweza kuigiza kama ndugu waliokufa zamani, maana yaliishi nao na yanafahamu historia nzima ya familia husika.

Neno la Mungu liko wazi kabisa hata katika eneo hili na linatutaka kuzijaribu roho kama zimetoka kwa Mungu au la.  Kwa mfano, hakuna pepo linaloweza kusema kuwa Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu aliye hai, ambaye alikuja katika mwili. (Law. 19:31, 20:27, Kumb. 18:9-19, 1Yoh 4:1-3). Nilipokuwa ndani ya kundi la New Age na nikitaka kuharibu mafundisho ya Kikristo katika muda fulani maalum, nilikuwa nikituma kundi la watu kwenye jumuiya za hayo makanisa ya uamsho. Nilikuwa nikilenga hasa yale makanisa ambayo yana bidii sana katika kuhubiri. Kwa nini tulikuwa tukienda kwenye makanisa kama hayo? Ni kwa sababu Kanisa ambalo halifanyi bidii kuhubiria watu Injili kwenye mitaa yao na kwingineko halina nguvu wala halisababishi hatari yoyote. Katika ulimwengu wa kiroho, Kanisa kama hilo si hatari na halina maana yoyote – halihatarishi nguvu za kipepo.

Hii ndiyo sababu nilichagua yale makanisa kwa ajili ya timu zetu ambazo zilikuwa zikihubiri injili kuliko hata makanisa yote mengine. Nilituma kule wale watu ambao walijua namna ya kujifanya kuwa wameokoka kwelikweli. Hawa walikuwa ni wapelelezi wa kiroho. Jambo la kwanza walilofanya lilikuwa ni kujua hayo makanisa yana nguvu kiasi gani katika maombi na kama wanaamini katika nguvu ya Roho Mtakatifu. Baada ya hapo tunapeleleza iwapo wanaamini katika miujiza ya huyo Roho Mtakatifu ambayo ilifanywa na Yesu Kristo. Swali jingine lilikuwa: Je, wana matatizo ya msengenyo, ugomvi, mashindano? Je, ni nini kinachowagawanya?

Tunapoyapata mambo hayo kwenye makanisa haya, tunayatumia. Watu wetu hatimaye huwachukua watu walio na ushawishi na kuwatumia kueneza matatizo hayo kwa watu wengine hadi tunaposababisha ghasia na kuyaharibu makanisa hayo. Msaada mkubwa kwetu ulikuwa ni pale tunapokuta wana kikundi cha vijana chenye nguvu. Tuliwatafuta wale wenye ushawishi mkubwa na kuwalenga hao. Humo tuliingiza mafundisho ya uasi dhidi ya wazee. Huu wote ni udhaifu ulio kwenye makanisa. Kwa njia hii tuliyaharibu makanisa mengi sana. Chini ya uongozi wangu, tuliharibu makanisa 300. Baadhi yake yalikuwa ni makanisa yenye nguvu sana mwanzoni.

Kwa hiyo, nimekuja kwenu kuwaletea mambo haya waziwazi; kuwaambia kuwa kundi hili litakuja kwenu na litasimama kinyume na yale makanisa yaliyo hai nchini mwenu. Wakati umefika kwa dunia yote. Bwana Yesu anarudi; ama unaamini au la! Miujiza mingi inaanza kutokea kwa nguvu ambayo haijawahi kushuhudiwa kabla. Kulingana na Biblia, mfumo mmoja wa kilimwengu uko tayari kuondoka ili kupisha mfumo mpya uanze. Zaidi ya yote, haya yanatokea kwa sababu wakati u tayari.

Kabla sijarudi kwa Yesu Kristo, nilifanya kazi kwenye Baraza la Kilimwengu la Mataifa (World Council for Nations) kwenye kundi la New Age. Nilikuwa ninapigania kuleta mfumo mmoja wa kidini duniani kote. Si kwamba ni aina moja ya mafundisho. Kwa mwanzoni, utajidhihirisha kwa njia na kwa sura nyingi.  Hata hivyo, manabii wa uongo wataitwa, nao wataanza kutaka kuwapo kwa dini moja tu. Huu ndio mpango wa New Age.

Nimeshakuwa kwenye makundi mengi ya New Age lakini nataka kuwaambia kuwa hakuna mafundisho wala dini yoyote inayoweza kulinganishwa na mafundisho na maisha ya Bwana Yesu Kristo. Watu wengi wataanguka hata baada ya kumpokea Yesu Kristo kwa sababu hawakumfanya kuwa Mwokozi na Bwana wao kibinafsi. Walipokea wokovu lakini hawakuingia kwenye njia ya kumtii Bwana wetu Yesu. Kwa watu kama hao, tulifanikiwa sana. Tuliweza kuwatoa kwenye makanisa. Kwa yale makanisa ambayo hayafanyi uinjilisti, ilikuwa ni rahisi sana kuwapata watu kama hao. Tuliwaondoa kanisani taratibu na polepole tunawaingiza kwenye mambo ya New Age. Ni kwa vipi inawezekana? Kanisa ambalo haliishi katika nguvu za Roho Mtakatifu na halifanya uinjilisti kwa bidii ni dhaifu sana. Hivyo, watu wao wapya wanakuwa na shauku ya kujua mambo mapya na kulishwa kiroho; maana kumpokea Bwana Yesu bila tena kuwa na uongozi wa Roho Mtakatifu haitoshi. Ndiyo maana inatakiwa kuwalisha watu hawa kwa Neno la Mungu katika nguvu za Roho Mtakatifu, vinginevyo watakwenda mahali pengine. Kanisa lilijionyesha kuwa halina nguvu, ndiyo maana ilikuwa ni rahisi sana kwao kutoka humo.

Tuliwaonyesha aina mbalimbali za uaguzi, majedwali na matufe  (crystal balls). Baada ya hapo, tulikuwa tukianza na mafundisho kuhusiana na taamuli (meditation), na kuwafanyisha aina mbalimbali za taamuli (au tafakari). Aina hii ya taamuli inayofanywa na New Age ni kinyume na Mungu aliye hai. Maandiko yanatutaka tufanye taamuli (tutafakari) kuhusu Neno la Mungu tu (Zab. 1:2, Fil. 4:8, 1Tim. 4:15, Zab. 119:11, 15 167 nk.)


Kutafakari kulingana na New Age ni kuungana na ulimwengu au kuifanya akili iwe tupu, n.k. Kwa njia hii, unafungua moyo wako kwa mapepo na roho chafu. Bwana Mungu anasema tutafakari kuhusu Neno lake; kujaza fahamu zetu kwa Neno la Mungu. Maana ukifanya akili yako kuwa tupu kwa njia inayotumiwa na New Age, basi ni lazima kije kitu kingine kujaza huo utupu – haiwezekani kamwe akili kubakia tupu tu. Ndiyo maana tunatakiwa kujilisha kwa Neno la Mungu na kulitafakari. Hii hasa ni muhimu wa wale wanaoanza tu kumjua Mungu. Vinginevyo, watarudi nyuma na kumwacha Mungu (1Pt 2:2).

Njia nyingine tuliyokuwa tukitumia kuwaonyesha Wakristo walio dhaifu na ambao hawajaamua kusimama kwelikweli, ilikuwa ni aina mbalimbali za kuangama (levitation), yaani mtu kuelea juujuu bila kugusa chini. Hii ni pamoja kufanya vitu mbalimbali kuangama. Kwa mfano, viti au watu wanaweza kunyanyuliwa juu bila nguvu ya kibinadamu. Kinachofanyika ni kuwa vitu hivi hunyanyuliwa na nguvu ya roho ambayo huwezi kuiona. Roho hizohizo zinaweza kukunja vijiko, kuhamisha vitu, n.k. Ni mbinu inayoweza kuwatoa watu kwa Mungu, hasa kama Kanisa linafundisha bila mafundisho hayo kufuatiwa na ishara na maajabu ya Mungu. Kwa njia hii, watu wa New Age wanawanasa watu wengi makanisani.

Nilipokuwa kwenye ngazi ya mwisho, ambayo ilikuwa ya juu sana kwenye New Age, nilikuwa nina roho ambayo iliweza kunipeleka sehemu mbalimbali.  Huyu “kiongozi wa kiroho” niliyekuwa naye, aliweza kunifanya nisionekane, na wakati huo ananiingiza kwenye ulimwengu wa kipepo na kunionyesha jinsi mambo haya yanavyofanyika huko kwenye ulimwengu wa kipepo na jinsi sasa yanavyodhihirika kwenye ulimwengu wetu wa kawaida.

Mtu anapogusa fahamu za wengine, au anapoingiza matakwa yake kwenye akili ya mtu mwingine na huyo mwingine akatenda jambo hilo; au kama mtu anasoma mawazo ya wengine, au kujua yanayofanyika ndani ya chumba kilichofungwa; yote hii ni kazi ya mapepo. Hilo pepo huenda tu kwenye hicho chumba na kusikiliza kila kitu na kuja kwambia huyu mwenye hilo pepo. Hii pi ndiyo njia ya kusafirisha mawazo na ishara katika umbali mkubwa, n.k. Ni kazi ya roho zisizoonekana, kitu ambacho shetani atakitumia kuwadanganya wengi. Yote haya asili yake ni kuzimu.

Bwana Mungu anata tutembee katika ulimwengu wa roho kupitia kwa Mwanawe, Bwana Yesu Kristo peke yake. Shetani tangu mwanzo amekuwa anafanya bidii kuondoa macho ya mwanadamu kwa Yesu Kristo kama Mwokozi wetu na kuyapeleka kwenye kazi zake zilizoko duniani. Kupitia kuangama pamoja na miujiza mingine isiyo ya kimungu, anataka tuelekeze macho yetu kwake, na kumshangaa yeye kuwa anaweza kufanya mambo kama hayo. Hii ndiyo sababu ni muhimu sana kwa Wakristo wanaookoka walishwe Neno la Mungu na Wakristo waliokomaa ili kujua namna ya kukabiliana na kila hali; yaani kujua Biblia inasema nini kuhusiana na hali mbalimbali za maisha.

Nilipokuwa kwenye hizo kazi za upinga Kristo katika New Age, washirika wangu wakubwa walikuwa ni yale makanisa yasiyo na Roho Mtakatifu – ni makanisa mafu yasiyoruhusu ishara na maajabu ya Agano Jipya na udhihirisho wa Roho Mtakatifu; yanazuia nguvu zake kuu, na kufungua milango kwa ajili ya falsafa mpya na roho mbalimbali chafu.

Makanisa ambayo hayakuruhusu timu zangu kuingia yalikuwa ni yale yenye nguvu za Roho Mtakatifu katikati yao. Haya ndiyo pekee yaliyokuwa na nguvu za kukabiliana na mbinu zetu. Kabla ya kuanza chochote kwenye kanisa la aina hiyo, tunagunduliwa na kufukuzwa.

Mbinu nyingine ya kuchanganya Neno la Mungu na falsafa zingine ni kuanza, kwa mfano, na ubudha, uhindu au dini zingine zozote za mashariki kwa namna ya kisasa. Marekani, katika miaka ya sitini wakati wa mgogoro wa Vietinamu, ilifungua mlango kwa dini za mashariki. Kwa njia hii, watu wa New Age walikuwa wakipenya kwenye taasisi za kiserikali, bunge, mfumo wa elimu na utamaduni. Makanisa yalishangazwa na jambo hilo, na kwa ujumla hayakusimama kulipinga. Watu hawa walianza kubadili sheria zilizopo na kuleta sheria mpya. Kwa makusudi kabisa, walilenga kuharibu Ukristo na utamaduni wa Kikristo.

Leo tuko mahali ambapo ni marufuku kuhubiri Injili mashuleni waziwazi; ni jambo ambalo limekuwa ni kinyume cha sheria! Katika baadhi ya majimbo Marekani, ni kinyume cha sheria hata kuhubiri Injili mitaani. Lakini kwa upande mwingine, mashuleni na kwenye vyombo vya habari, yanaendelea mafundisho ya imani za kishetani, New Age, n.k. Hili linatokeaje? Kulikuwa na wakati ambapo Marekani ilikuwa imebarikiwa sana. Wale walioitwa ‘pilgrim fathers”, yaani waanzilishi wa taifa la Marekani – walijenga sheria zao kulingana na Biblia, ambazo ziliheshimiwa hata na wasioamini.

Katika wakati ule uliobarikiwa tulimtumikia Mungu mmoja tu – Yesu Kristo. Lakini tuligeuka na kuanza kusikiliza mafundisho ya New Age. Watu walianza kuwatembelea wasoma nyota na wabashiri (astrologers and fortunetellers). Maamuzi yao yaliongozwa na kile ambacho wasoma nyota hawa waliwaambia. Baadhi yao hata walikiri waziwazi kuwa walikuwa wanachama wa  New Age. Bwana Mungu ameshageuza uso wake mbali na nchi hii. Leo makanisa yanapata shida sana kujenga ushirika uliokuwapo mwanzoni. Naomba kwamba jambo hilo lisitokee hapa jamhuri ya Cheki.

Bado mna safari ndefu ya kujenga jamii huru ya kidemokrasia. Kuhusiana na upande wa kiuchumi na kijamii, hamjapiga hatua sana. Lakini matatizo yote yaliyopo yanaweza kutatuliwa kama mtamshikilia kabisa Bwana Yesu Kristo. Tupilieni mbali mafundisho yote yale ya New Age kwenye nchi yenu yasijekuwa kansa kwa nchi yenu. Msije kufanya kosa kama ilivyo kwa Marekani kwamba, kulingana na sheria, dini zote ni sawa tu. Wameasi sheria ya kwanza na kutamka kuwa tunatakiwa kumwabudu Mungu mmoja tu; wameasi kwa maana ya kusema kwamba dini zote ni kweli. Jambo hili limefungua mlango kwa ibada ya sanamu na New Age.

Nimesafiri kwenye nchi yenu kwa wiki tatu sasa na nimeona shughuli nyingi zinazohusu New Age. Upande wa kaskazini wa Prague, nimeona maonyesho ya watu wa New Age. Kama mkiruhusu mambo haya kufundishwa kwenye nchi yenu, itaharibika kabisa. (Kumbuka: mambo haya tayari yamesharuhusiwa. Jamhuri ya Cheki imejaa imani za siri, uabudu shetani, dini za mashariki, n.k.).

Nilipokuwa mwanachama wa Baraza la Ushauri la Umoja wa Mataifa, nilisaidia kuandika program yenye mambo 13 na sheria ya New Age. Mambo hayo nayo ninayaongelea kwenye ushuhuda huu. Yasome uyaelewe. Program hii yenye mambo 13 imekuwa ndio msingi wa mafundisho duniani kote ya kanuni za New Age. Watu wote walio kwenye New Age wanafanya juhudi kuyatekeleza mambo haya 13 hadi kufikia mwaka 2000. Kwa sababu hiyo, wanafanya bidii kuwapata watu wote maarufu kwenye siasa na mashirika mbalimbali.

6 comments:

 1. Kwa ujumbe huu nimepata changamoto ya kuzidi kuhubiri injili ya Kweli ya Yesu Kristo.

  ReplyDelete
  Replies
  1. Amen. Bwana azidi kukushika mkono na kukuinua katika utumishi aliokupa.

   Delete
  2. Hizi shuhuda zimeniinuwa sana kiroho change,nataka utambuwe hilo kwani shuhuda ya kwanza kuisoma nilielekezwa na Roho mtakatifu kuhusu jinsi shetani anavyo zuia maombi .Roho mtakatifu ndiye aliye nielekeaza na kunifunulia kuhusu blog yako.Aliniambia andika kwenye google jinsi ibilisi anavyo zuia maombi yako.Kifipi nimekuwa hodari kwenye maombi imenipelekea pamoja na mafundisho mengine sasa nimekuwa nahubiri injiri.Mungu akubariki sana Kazi yako si bure kama kuna watu umewainuwa nafikiri mimi ni miongoni mwao kupitia shuhuda kwenye blog yako.

   Delete
  3. Amen mpendwa. Asante sana kwa ushuhuda huu - maana huu uliotoa hapa nao ni ushuhuda mkubwa sana. Bwana azidi kukubariki na kukuinua. Sifa zote kwa Bwana wetu, Yesu Kristo.

   Delete
 2. Hallo James, Hata mimi nabarikiwa sana na shuhuda hizi na zinazidi kunipa mafunuo mengi kuhusu ulimwengu tunayoishi na ule ulimwengu ambao wengi wetu hatujui kinachoendelea, yaaani ulimwengu wa kiroho; kimsingi mimi nilipata kujua blog yako baada ya kuwa nasearch ktk google kuwa "ROHO NI NINI" nilihitaji sana kujua roho ni kitu gani maana mara nyingi nimekuwa nikitafakari namna Mungu alivyoniumba na najiona nimeumbwa wa ajabu sana; nikitafakari hata namna ninapolala usingizi na kesho yake naamka na kuendelea na maisha, kwangu huu ni muujiza wa ajabu maana hata sielewi yale yote yanayotokea ninapokuwa usingizini na hapo ndipo natambua kuwa yuko Mkuu (Yesu) aliyetenda haya kwa ufundi wa hali ya juu. Namrudishia Mungu wangu utukufu kwa kuniumba nilivyo; namshukuru pia kwa kuwaumba watu kama ninyi wenye karama za kuwalisha wengine neno la uzima. Hakika kupitia blog hii, nilikuja tambua roho ni nini! kuwa kumbe katika mwili huu tulionao ni kama box tu ambalo ndani yake ndimo ninapoishi, yaani ndipo nafsi yangu ilipo. Mungu akubariki sana kaka James. Mimi Henry Philip

  ReplyDelete
  Replies
  1. Shalom brother Henry. Ashukuriwe Bwana Yesu kwa kuwa umepata kile ambacho moyo wako ulikionea shauku kwa muda mwingi. Zidi kubarikiwa katika Jina la Yesu.

   Delete