Maandiko yanasema: Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya
mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani. (1
Wakorintho 10:11).
Yale waliyopitia ndiyo tunayopitia sisi leo. Kilichowaagusha
ndicho kitakachotuangusha na sisi kama hatutatenda kinachotakiwa. Kilichowapa
ushindi ndicho kitakachotupa nasi ushindi tukitenda sawasawa.
Wengi wetu tunafahamu kuhusu habari ya Daudi na Goliati.
Ilitokea kwamba kulikuwa na vita kati ya Wafilisti na Waisraeli.
Kabla ya makabiliano, Wafilisti walikuwa upande mmoja kwenye mlima, na
Waisraeli nao kwenye mlima upande mwingine.
Katika nyakati hizo hakukuwa na bunduki wala mabomu kama leo. Vita vilikuwa vikipiganwa kwa makabiliano ya uso kwa uso;
mtu kwa mtu. Askari walitumia mikuki, mapanga, mashoka, mawe na silaha zingine
ambazo zilihitaji nguvu za kimwili za binadamu.
Goliati alikuwa ni
askari shujaa wa Wafilisti. Alikuwa akitoka kila siku asubuhi na jioni na
kusimama juu ya mlima. Kisha, kwa sauti ya juu, akawatukana Israeli na kutamba
kwa majigambo na dharau nyingi akisema: Je! Mimi si Mfilisti, na ninyi si
watumishi wa Sauli? Jichagulieni mtu, akanishukie mimi. Kama mkiweza kupigana
nami na kuniua, sisi tutakuwa watumwa wenu; nami nikimshinda yeye na kumwua,
ninyi mtakuwa watumwa wetu, na kututumikia. (1 Samweli 17:8-9).
Ndivyo anavyofanya
ibilisi kwako leo. Unapita katika majaribu mazito ambayo umepambana nayo lakini
inaonekana kama umefika mwisho. Kila wakati shetani anasema moyoni mwako, “Hii
shida mpaka ikuue! Huna cha kufanya! Hutapona kamwe ugonjwa huu! Hata ufanyeje
hutoki humu!” n.k.
Lakini je, huyu
Goliati alikuwa ni mtu wa namna gani?
Kulingana na maandiko,
zamani kulikuwako na uzao wa wanadamu waliokuwa wakijulikana kama majitu.
Biblia inasema: Nchi hiyo nayo yadhaniwa kuwa ni nchi ya Warefai; hapo kale
Warefai walikaa humo; lakini Waamoni wakawaita Wazamzumi, nao ni watu wengi,
wakubwa, warefu, kama Waanaki. (Kumbukumbu
la Torati 2:20-21).
Katika Biblia ya
Kiingereza, neno Warefai ni giants. Hili ni neno lenye maana ya majitu,
mapandikizi, au makubwa sana. Goliati alikuwa ni uzao wa hao
Warefai.
Sasa katika vita hivi
kati ya Wafilisti na Waisraeli, maandiko yanasema: Ndipo akatoka Goliathi, wa
Gathi, ambaye urefu wake ulikuwa mikono sita na shubiri moja. Alikuwa na chapeo
ya shaba kichwani, tena amevaa darii ya shaba; na uzani wake ile darii ya shaba
ulikuwa shekeli elfu tano za shaba. Tena amevaa mabamba ya shaba miguuni mwake,
naye alikuwa na mkuki wa shaba kati ya mabega yake; na mti wa fumo lake ulikuwa
kama mti wa mfumaji; na kichwa cha mkuki wake kilikuwa shekeli mia sita za
chuma uzito wake; na mtu aliyemchukulia ngao yake akamtangulia. (1 Samweli
17:4-7). Huyu hakika alikuwa ni pandikizi la mtu kweli kweli!
UREFU WA GOLIATI
Mikono sita na shubiri moja.
Mkono 1 = inchi 18
Mikono sita = 18 X 6 = inchi 108.
Shubiri moja = inchi 9
Ichi 108 + inchi 9 = inchi 117
Hizi ni sawa na sm 274.32
Watu wengi tunaowaona
kuwa ni warefu, wana urefu wa futi kama 6 hivi. Hizi ni sawa na meta 1.8.
Lakini Goliati alikuwa na urefu wa futi 9. Hizi ni meta 2.7. Yaani ni meta 3
kasoro sentimeta chache tu!
DARII YA GOLIATI
Darii au dirii ni koti
la chuma. Lile la Goliati lilitengenezwa kwa shaba. Hili lilikuwa na uzito wa
shekeli elfu tano.
Shekeli 1 = kilo 0.011
Shekeli elfu tano = 5000 X 0.011 = kg 55
Huu ni uzito sawa na
mfuko mmoja wa simenti, kisha uongeze kilo tano zaidi. Ina maana kuwa kama
angekutupia tu hilo koti lake, unakufa palepale; achilia mbali mkuki na silaha
zingine alizokuwa nazo; au yeye mwenyewe akukamate!
KICHWA CHA MKUKI WA
GOLIATI
Kilikuwa na uzito wa shekeli 600
Shekeli 600 X 0.011 = kg 6.6.
Hapa hatuhesabii mpini wake ambao tunaambiwa ulikuwa ni
kama mti wa mfumaji. Kimsingi huu si mpini bali ni mlingoti!
Kumbuka kuwa, hapa
hatuelezwi chochote kuhusu uzito wa mabamba ya miguuni, mpini wa mkuki, chapeo
(yaani kofia) ya shaba aliyovaa, pamoja na upanga wake. Ina maana kuwa vitu
alivyokuwa amebeba na kuvaa, vilikuwa na uzito wa karibu kilo mia moja; sawa na
gunia moja la mahindi!
Kutokana na jinsi
alivyokuwa anatisha, katika kule kutoka kwake kila asubuhi na jioni mbele ya
Waisraeli, maandiko yanasema: Yule Mfilisti akasema, Nayatukana leo majeshi ya
Israeli; nipeni mtu tupigane. Basi Sauli
na Israeli wote waliposikia maneno hayo ya Mfilisti, wakafadhaika na kuogopa
sana. (1 Samweli 17:10-11). Goliati aliendeleza tambo hizi kwa siku arobaini!
Je, Goliati wako
anayekutisha maishani ni nani? Je, ni
ukosefu wa kazi? Ni ugonjwa usiopona? Ni masimango? Ni uchumi
mbaya? Ni dawa za kulevya zinakutesa? Ni hofu au mashaka juu ya kesho? Ni
uchungu au chuki dhidi ya mtu au watu fulani waliokusaliti?
Hayo yote ndio akina
Goliati wa maisha yetu. Huo ndio uhalisia wa maisha. Dunia si mbingu. Shida
zikiondoka, dunia itakuwa ni mbingu si dunia tena. Maisha ya dunia ni pamoja na
shida na majaribu.
Ni kweli uko baharini
na dhoruba ni kali. Lakini akina Goliati wakikukabili wewe unafanya nini?
Unalalamika au kuogopa kama Waisraeli walivyonywea mbele ya Goliati? Au unawaza
hata kujiua? Ni kweli kuna nyakati maisha yanatisha mno.
Sasa sikia jibu la
Mungu wako aliyekuumba ili uwe mshindi; si uwe wa kushindwa.
Katikati ya fedheha na
matukano ya Goliati, alitokea Daudi; kijana mdogo tu. Daudi japo alikuwa
hata hajafikia umri wa watu waendao vitani, aliamua kumkabili yule pandikizi.
Alisema: Wewe unanijia mimi kwa mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la
BWANA wa majeshi ya Israeli uliowatukana. Siku hii ya leo atakuua mkononi mwangu,
.... Nao jamii ya watu wote pia wajue ya kwamba BWANA haokoi kwa upanga wala
kwa mkuki; maana vita ni vya BWANA, naye atawatia ninyi mikononi mwetu. (1
Samweli 17:45-47).
Daudi alizungusha
kombeo lililokuwa na kijiwe kidogo kisha akakiachia. Kijiwe kidogo kilimpata
jitu wa kutisha na silaha zake hazikumwokoa. Alianguka chini na kufa palepale!
Elimu, fedha,
umaarufu, cheo, ujanja au uwezo wowote wa kibinadamu ni sawa na upanga na
mkuki. Kuna shida na majaribu mengi ambayo hayatatuliki kwa upanga au mkuki.
Kila mwanadamu ana mahali pake pa kukwamia; lazima! Hapo ni mahali ambapo
Goliati anakunanga kila siku na wewe unabakia umeinamisha kichwa tu.
Labda umefika mahali
hapo na ukasema, “Hapa sasa basi. Sina tena cha kufanya.” Ni kweli huna cha kufanya
lakini, kama alivyofanya Daudi, liko JINA lipitalo majina yote. Hilo ni jina la
YESU! Mkabili Goliati wako kwa jina hilo.
Goliati ni uzao wa
majitu. Atakuja na kwako pia kwa sura mbalimbali! Anatisha! Ana nguvu! Sijui
unakabiliana na Goliati gani hivi sasa. LAKINI tunaweza kumkabili, si kwa
upanga wala mkuki, bali kwa JINA LA BWANA!
Bwana anaagiza kwamba, Uwe hodari na moyo wa ushujaa; usiogope wala usifadhaike; kwa kuwa BWANA,
Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako. (Yoshua 1:9).
Tena anasema kwamba, Utokapo kwenda vitani kupigana na adui zako, na kuona farasi, na magari, na
watu wengi kuliko wewe, usiwaogope; kwa kuwa BWANA, Mungu wako yu pamoja nawe,
aliyekukweza kutoka nchi ya Misri. (Kumb. 20:1).
Simama na ahadi ya
Bwana. Usiangalie ukubwa wa tatizo au adui yako. Mtazame Yeye aliye Mkuu na
Mwaminifu, Yesu Kristo. Ni lazima utashinda!
somo zur sana be blessed
ReplyDeleteAmen. Be blessed too
DeleteAsante kwa kutembelea blog hii. Mungu akubariki rafiki.
ReplyDeleteKaka james John hii ni kazi njema na kubwa sana unayoifanya mbele za Mungu, hakika Bwana atakulipa usipozimia roho.
ReplyDeleteSambamba na hilo nilitamani pia mafundisho haya kuwafikia wengi zaidi ili kama mimi ninavyobarikiwa basi wengine pia wabarikiwe vilevile.Kwa sababu hio nilikuwa naomba kibali kuwa nashare kwa wengine kwa njia mbalimbali kwa lengo hilo, nimeona si vyema kufanya hivo bila kibali chako.
Shalom. Asante kwa maoni yako na ni kweli Mungu atusaidie tusizimie moyo hadi mwisho wa safari. Ndugu, unaweza kushare kadiri uwezavyo.
DeleteThanks
ReplyDelete