Maandiko yanasema
kwamba: Kwa kuwa nia ya mwili ni mauti; bali nia ya
roho ni uzima na amani. Kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu, kwa
maana haitii sheria ya Mungu, wala haiwezi kuitii. (Warumi 8:6-7).
Ndugu, yapo mashindano
makali sana ndani mwetu ambayo yanaendelea kila dakika ya maisha yetu. Mwili unataka
hivi na roho inataka vile. Wewe na mimi tuko hapo katikati. Uamuzi unatoka
kwetu – ama kufuata mwili au kufuata roho!
·
Ukipanda
daladala, halafu kondakta akawa hajakudai nauli kabisa hadi ukafika wakati na
kushuka, iko sauti inayokwambia, “Lipa.” Sauti nyingine inasema, “Nenda tu.”
·
Ukivaa
vazi lisilo sawa, sauti moja inakwambia, “Badili uvae nguo nyingine.” Sauti nyingine
inasema, “Mbona wanaovaa hivi wengi tu.”
·
Mtu akikukosea,
sauti moja inasema, “Msamehe.” Ya pili inasema, “Asikuchezee huyo!”
Kwa kifupi, sauti ya
kwanza ni hiyo inayoitwa “nia ya roho” katika andiko la Warumi hapo juu. Na ile
ya pili ndiyo “nia ya mwili.”
Na tunaambiwa wazi
kwamba nia ya roho mwisho wake ni uzima na amani, lakini nia ya mwili inamfanya
mtu awe na uadui na Mungu!
Sauti hizi zipo kwenye
karibu kila eneo la maisha yetu; tangu asubuhi hadi asubuhi inayofuata; kila
siku; kila dakika!
Lakini mara nyingi
tunajikuta tunaishi kwa kuitii ile nia ya mwili (japo wengi wetu hatujitambui
kama tuko namna hiyo). Paulo anasema: Kwa maana lile jema nilipendalo silitendi; bali lile
baya nisilolipenda ndilo nilitendalo. (Warumi 7:19).
Ndiyo! Hivyo ndivyo
tulivyo mara nyingi. Tunaishi kwa kuifuata nia ya mwili.
Yesu anasema wazi,
Makwazo hayana budi kuja. (Luka 17:1). Lakini sasa, yakija unatii nini? Unatii roho
au mwili? Na matokeo ya huo
uchaguzi ni nini? Imeandikwa: Hamjui ya kuwa kwake yeye ambaye mnajitoa nafsi zenu kuwa
watumwa wake yule mnayemtii, kwamba ni utumishi wa dhambi uletao mauti au
kwamba ni utumishi wa utii uletao haki. (Warumi 6:16).
Wengi tunasema, “Nataka
kuisikia sauti ya Mungu.” Sikatai kwamba Mungu huzungumza wakati mwingine kwa
sauti ya kusikika kabisa, lakini sauti ya Mungu ipo ndani yetu KILA DAKIKA! Na
hapa ndipo pa kuanzia.
Jifunze na ujizoeze
kusikiliza moyo wako katika kila jambo. Utaanza kuyaona kwa uwazi mambo yaliyo
kinyume na Neno la Mungu (Hapa ieleweke kwamba lazima usome Biblia ili Neno hilo
liwe ndani yako ndipo utaweza kujua lipi ni kinyume na Neno na lipi ni sawa na
Neno).
Pia utaweza kuitambua
ile sauti ya Roho Mtakatifu inayokushauri katika kila jambo na kukupitisha
kwenye njia ya haki. Atakushauri kupitia hilo Neno uliloweka moyoni mwako. Ndiyo
maana ya neno lisemalo: Moyoni mwangu nimeliweka neno lako nisije nikakutenda
dhambi. (Zaburi 119:11).
Kisha anza kuifuata
sauti hiyo. Bwana anasema: Basi nasema, Enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe
tamaa za mwili. Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho
kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya
mnayotaka. (Wagalatia 5:16).
·
Kondakta
akikusahau, mkumbushe na umlipe.
·
Roho akikuambia
samehe, tii kwa kusamehe hata kama una kila haki ya kumkasirikia aliyekukosea;
n.k.
Biblia pia inasema
kuhusu wana wa Israeli: BWANA naye akawatangulia mchana ndani ya wingu mfano wa
nguzo, ili awaongoze njia; na usiku, ndani ya moto, mfano wa nguzo, ili kuwapa
nuru, wapate kusafiri mchana na usiku; ile nguzo ya wingu haikuondoka mchana,
wala ile nguzo ya moto haiukuondoka usiku, mbele ya hao watu. (Kutoka
13:21-22).
Hiyo sauti iliyo ndani
yako na ndani yangu, ndiyo nguzo ya wingu na nguzo ya moto inayotuongoza mchana
na usiku katika maisha haya.
Bwana anasema na kila
mwanadamu wakati wote. Ni uchaguzi wetu kutii au kukataa kutii. Lakini ni heri
kutii kuliko kuasi.
Imeandikwa: Kondoo wangu
waisikia sauti yangu; nami nawajua, nao wanifuata. Nami nawapa uzima wa milele;
wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu.
(Yohana 10:27-28). Mtii BWANA!
Bwana akubariki
unapoenda kumtii katika kila jambo maishani mwako; na hakika, utafika salama
kwenye Kanaani iliyo mbele yako!
asante kaka
ReplyDelete