MPANGO WA MUNGU KUHUSU
MAWAZO YETU
Bila mimi hamuwezi
Mawazo yetu ni muhimu sana kwa maisha yetu ya sasa na yale
yajayo. Kwa hiyo, Mungu anayo mengi ya kusema kuyahusu. Ametuwekea utaratibu na
mwongozo wa kuweza kuvuna baraka zake kwa kupitia kwenye mawazo yetu. Hata
hivyo ni muhimu kukumbuka wakati wote kuwa msaada wetu unatoka kwa Bwana. (Zaburi 124:8).
Pia Yeye anasema: “Mimi ni mzabibu ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami
ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamuwezi kufanya neno
lolote.” (Yohana 15:5).
3
Kwa hiyo, hata katika suala la kuwaza au kutafakari, bila
msaada wake, hatuwezi kitu. Kama kuwaza tu kwa namna inayofaa hatuwezi, sembuse
kuyafanya hayo mawazo yetu yatupatie shauku za mioyo yetu? Agizo la muhimu
analotupa Bwana, tunalopaswa kulizingatia ni kuwa, “Mtumaini Bwana kwa moyo
wako wote, wala usizitegemee akili zako mwenyewe.” (Mithali 3:5).
Bwana anasema nisizitumainie akili zangu! Hili ni jambo la
kushangaza kabisa. Kuzitumainia akili maana yake ni kufanya mambo yangu bila
kumpa Mungu nafasi. Yaani, nikishawaza jambo tu, ninalitenda. Tena ninakuwa ninajua
tu kuwa yale yote ninayoyafanya ni ujanja, uwezo na juhudi zangu mwenyewe.
Mungu anatuonya kuhusu kuzitumainia akili, si kuhusu
kuzitumia. Tunatumia akili zetu kuchagua wapi pa kutumainia. Biblia
inasema, “Tumieni akili kama ipasavyo, wala msitende dhambi.” (1Wakorintho 15:34)
JINSI YA KUWA NA MAWAZO YENYE NGUVU
Hivi itakuwaje kama nitaweza, kila siku, kuwa na mawazo ya
kushinda, kuweza, kufanikiwa, kupona na mengine ya namna hii hata kama kwa
namna ya kibinadamu mambo yanaonekana kuwa ni mabaya? Bila shaka maisha yangu
yatabadilika kwa haraka sana kuelekea kwenye ubora. Tunaweza kabisa kuzifunza
akili zetu kuwaza mawazo chanya na si mawazo hasi, yaani tunaweza kuwa na imani. Na uzuri ni kwamba yupo Bwana upande wetu
ambaye anatusaidia katika kila hatua.
Kutofautisha nia
Ili tuweze kujenga tabia ya kutafakari kwa mafanikio, ni
lazima tuwe na uwezo wa kuchunguza na kutambua nia iliyomo ndani mwetu kila wakati.
Ndani mwetu kuna nia za aina mbili. Biblia inasema, “Kwa
kuwa nia ya mwili ni mauti; bali nia ya roho ni uzima na
amani.” (Warumi 8:6). Kwa hiyo, kuna nia ya mwili na nia ya roho. Nia ya
mwili ni nia ambayo hujificha sana kiasi kwamba wakati mwingine ni vigumu kuigundua.
Bila shaka umeshawahi kukutana na hali zifuatazo:
• Unapotaka kulala unaomba ulinzi wa Mungu uzingire nyumba
yako. Lakini, baadaye ukisikia kishindo chochote nje, unaingiwa na hofu kubwa. Kilichokufanya
uombe ni nia ya roho, lakini kilicholeta hofu ni nia ya mwili. Hii imekufanya
usimwamini Mungu ambaye hapo tu kabla uliomba ulinzi wake.
• Unaposafiri, unalifunika gari kwa damu ya Yesu. Lakini,
gari likiyumba kidogo tu njiani, hukumbuki tena maombi uliyofanya. Hofu
inaletwa na nia ya mwili.
• Unaweza kuomba Bwana akufungulie milango ya mafanikio,
kisha baada ya muda mfupi unaanza kusema hali ni ngumu, maisha ni magumu. Nia
ya roho ilikusukuma kuomba lakini nia ya mwili ikakufanya ukiri kutowezekana.
• Watumishi wa Mungu wanaposema kuwa Bwana ametupa mamlaka
ya kutoa pepo na kuponya wagonjwa, unashangilia na kupiga makofi. Lakini ukiangalia, hujawahi kumwombea
mgonjwa yoyote wala kukemea pepo. Nia ya roho ilikufanya upige makofi ya furaha
lakini nia ya mwili inakuzuia kuyatendea kazi mambo hayo.
Mifano hii michache inatuonyesha kuwa, kumbe kwa nje
unaweza kuonyesha kuwa uko upande wa Mungu, lakini ndani yako ukawa uko kinyume
kabisa. Shida ni kwamba, ile nia ya ndani ambayo iko kinyume na Mungu ndiyo inakuwa
na nguvu, na ndiyo inayoshinda. Kibaya zaidi ni kuwa, unakuwa hujitambui kwamba
una hali hiyo.
Kuchagua nia sahihi
Ili upate mazao mengi na bora shambani ni lazima ufanye
kazi. Lakini, ili upate magugu mengi na mazao yako yaharibiwe, unatakiwa ukae
tu bila kufanya chochote. Magugu yatakuja yenyewe tu. Hayahitaji juhudi yoyote.
Akili ya mwanadamu ni kama shamba. Mawazo safi ni mazao bora. Mawazo mabaya ni magugu.
Usipojibidisha kwa lolote kuhusu mawazo yako, ni lazima utavamiwa na lundo la magugu,
yaani mawazo yasiyofaa! Wakati mwingine unaweza usilitambue hilo.
Dalili zinazoonyesha kuwa akili yako ina magugu hayo ni
hizi zifuatazo: kusonya kila mara, kunung’unika, kulaumu watu wengine, kukosa
raha, kujiinamia, kutikisa kichwa, kushika tama, kukosa usingizi, n.k.
Ili uwe na mawazo bora yatakayozaa matunda mema maishani,
ni lazima ufanye kazi ya kung’oa magugu wewe mwenyewe, kwa maana, “Maandalio ya moyo ni ya mwanadamu.” (Mithali 16:1).
Ni lazima kufanya uchaguzi wa makusudi (conscious selection) wa mawazo mema kutoka katika Neno la Mungu, na kuyatafakari
hayo muda wote. Kufanya uchaguzi wa makusudi maana yake ni kuwa, usiache tu mawazo yoyote yaingie na kutoka akilini
kama yapendavyo. Simama katika mlango wa akili yako kukagua kila wazo linalojitokeza,
kisha ruhusu yaingie yaliyo safi na zuia yaliyo magugu.
Ni lazima kuitambua nia ya mwili kila wakati na kuishinda
kabisa na kubaki na nia moja tu – ya roho. Unaishinda kwa kukiri neno la Mungu.
Kwa mfano, unapoingiwa na hofu, unasema, “Imeandikwa kuwa Mungu hajanipa roho
ya woga bali ya nguvu.”
Kitendo cha wewe kusema hivyo kinadhihirisha kuwa
umetambua kwamba kuna magugu, yaani nia isiyo sahihi. Kwa njia hiyo tu ndipo utaona
nguvu za Mungu zikifanya kazi maishani mwako. Hili ni jambo la muhimu sana!
Endapo hufanyi hivyo, uwezekano mkubwa
ni kuwa uko katika kundi la wale ambao hawajui kuwa
wamevamiwa na wanaendeshwa na hiyo nia ya mwili.
Kumbuka kuwa, mwanzoni hii itakuwa ni vita kubwa. Utapata
upinzani mkubwa. Hili ni jambo la kawaida kabisa. Maana kuhusu adui zetu, Bwana
anasema, “Sitawafukuza mbele yako katika mwaka mmoja nchi isiwe ukiwa na
wanyama wa bara wakaongezeka kukusumbua. Nitawafukuza kidogo kidogo mbele yako,
hata utakapoongezeka wewe, na kuirithi hiyo nchi.” (Kutoka 23:29-30).
Kasi ya kushinda kwako inategemea kuongezeka kwako - katika
ufahamu, maarifa na nguvu. Kwa hiyo, Bwana anatutia moyo akisema, “Je, si mimi
niliyekuamuru? Uwe hodari na moyo wa ushujaa; usiogope wala usifadhaike; kwa
kuwa BWANA, Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako.” (Yoshua 1:9).
Ukidumu katika kuyazuia mawazo mabaya kuingia akilini
mwako kwa kutafakari mawazo mema kutoka katika neno la Mungu, hakika yake,
baada ya muda mfupi utaona unabadilika kabisa! Hakika! Kwa maana, neno hilo ni
roho na roho ndiyo itiayo uzima! (Yohana 6:63).
Kwa mfano, unapoumwa, badala ya kutafakari jinsi mwili
unavyouma na udhaifu ulio nao, tafakari kwamba, “Kwa kupigwa kwake mimi nimepona;
yeye ameyachukua magonjwa yangu. Mimi ni mzima katika Jina la Yesu.” Unapoishiwa
fedha, badala ya kutafakari jinsi ambavyo shida uliyonayo ni kubwa kuliko fedha
unayopata, tafakari, kwa mfano, “Yote yawezekana kwa imani. Kwa Jina la Yesu naamuru
fedha zije kwa ajili ya hitaji hili nililonalo.”
Kwa kufanya hivi, utakuwa unatimiza andiko linalosema,
“Linda sana moyo wako maana ndiko zitokako chemchemi za uzima.” (Mithali 4:23).
Uzima haushii kwenye kupona tu magonjwa. Hata kupata fedha, chakula na nguo ni
sehemu ya uzima. Ndani ya moyo kuna chemchemi itakayotoa huo uponyaji na hizo fedha
ambayo ni mahitaji yako.
Ukiyawaza yale yaliyo kinyume na neno la Mungu, unakuwa
katika kundi hili: “Asiyetawala roho yake ni mfano wa mji uliobomolewa, usio na
kuta.” (Mithali 25:25). Utaanza tu kukiri udhaifu na kushindwa. Hatimaye,
utavamiwa na roho za kuzimu za kila namna, maana hauna ulinzi. Na hizo ndizo zitakazokudidimiza
chini zaidi na zaidi ili litimie andiko lisemalo, “Mauti …. huwa katika uwezo wa
ulimi.” (Mithali 18:21).
Chagua mawazo ya kutafakari! Usikubali hata kidogo kuwa
mtumwa wa mawazo. Usitawaliwe na mawazo, bali uwe mtawala wa mawazo. Yaani, wewe
ndiyo uchague nini cha kuwaza na nini cha kutupa nje. Kasha utaona ahadi za
Mungu zikitimia maishani mwako
I am real blessed with this study, real i was looking for this teachings, May LORD GOD bless the publisher, may HIM bless all readers.This is good work in the eyes of the LORD.amen
ReplyDeleteits Assenga Yudathade- Tanzania
Shalom Assenga. I thank the Lord if you have been able to benefit from this lesson. Be blessed.
DeleteThanks, it has helps a lot. Be blessed.
ReplyDeletePraise the lord.
ReplyDeleteUbarikiwe MTUMISHI NIMEJIFUNZA KITU KIKUBWA SANA.
ReplyDelete