Friday, April 5, 2013

Kuna Nguvu Katika Mawazo Yetu – Sehemu ya 2Mawazo ni kama sumaku

Sumaku ina nguvu za aina mbili - nguvu ya kuvuta vitu vije kwake na nguvu ya kusukuma vitu viende mbali nayo. Sumaku huvuta au kusukuma vitu vinavyofanana nayo, kwa mfano vipande vya chuma. Haiwezi kuvuta au kusukuma kipande cha mti, maana hakifanani nayo. Mawazo, hali kadhalika, huvuta au kusukuma mambo yanayofanana nayo. Hili ni jambo la kweli kabisa! Kwa mfano, kuna watu wengi ambao utawasikia wakisema, “Najisikia kama nataka kuumwa. Nadhani nitakuwa na malaria.”


Ukiwa na mawazo ya kuumwaumwa, mawazo hayo yatavuta magonjwa na udhaifu vije kwako. Iwapo una mawazo ya kuweza na kufanikiwa, vivyo hivyo, mawazo hayo ni lazima yatavuta mafanikio yaje kwako.Kiroho inakuwa hivi: Maandiko yanasema kuwa Mungu huliangalia neno lake ili kulitimiza (Yeremia 1:12). Pia, imeandikwa: Mhimidini BWANA, enyi malaika zake, ninyi mlio hodari, mtendao neno lake, mkisikiliza sauti ya neno lake. (Zab. 103:20).


Malaika husikiliza neno la Bwana na kulitekeleza kwa amri ya Bwana. Neno hili hulisikiliza kutoka wapi? Ni kutoka kwa Bwana mwenyewe na kutoka kwa watakatifu wake.


Kama malaika watakatifu wanasikiliza neno la Bwana, uwe na uhakika kuwa na malaika wachafu nao wanasikiliza vilevile.


Kwa hiyo, ukisema, kwa mfano, “Imeandikwa ‘kwa kupigwa kwake sisi tumepona,’ basi hata kama ulikuwa unajisikia kuumwa, basi malaika watakatifu watasikia na kuanza kutendea kazi neno ulilosema, maana ni neno la Bwana. Wakati huohuo, malaika wachafu nao watasikia na kuanza kukimbia, maana hawawezi kustahimili kusimama mbele ya neno la Bwana – neno la Bwana ni upanga mkali kwao (Waefeso 6:17).


Lakini kama tukisema maneno yaliyo kinyume na neno la Mungu, hali inakuwa kinyume chake. Malaika watakatifu wanaanza kurudi nyuma na malaika wachafu wanasonga mbele ili kulitimiza lile tunalosema, lililo kinyume na neno la Mungu.


Kile anachowaza mtu muda mwingi ndicho atakachokipata. Kama huwa ninawaza, ‘Lazima nitapona,’ mawazo hayo ndiyo sumaku itakayovuta uponyaji uje kwangu. Endapo ninawaza kinyume, mawazo hayo ndiyo sumaku itakayosukuma uponyaji mbali na mimi.


Kumbuka Biblia inasema, “Mtu mwema katika hazina ya moyo wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya moyo wake hutoa yaliyo maovu; kwa kuwa mtu, kinywa chake hunena yale yaujazayo moyo wake.” (Luka 6:45).


Tunapokuwa tumejawa na mawazo ya aina fulani moyoni, huwa hatubaki kimya. Lakini, tutaanza kuyatoa kwa vinywa vyetu. Kisha linatimia neno lisemalo: “Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi.” (Mithali 18:21).


Nia mbili

Mungu anapenda watu wenye msimamo mmoja ulio thabiti. Ndiyo maana anasema, “Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri ungekuwa baridi au moto. Basi kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.” (Ufunuo 3:15-16).


Kuwa na nia mbili ni kuwa katikati ya mawazo mawili yanayopingana. Kwa mfano, mtu anakuwa ana hitaji la fedha. Wazo moja ndani yake linasema, ‘Nitapata tu.’ Wazo jingine linasema, ‘Haiwezekani. Mambo ni magumu mno!’ Mtu wa aina hii hayuko kulia wala kushoto. Amegawanyika ndani yake.


Kwa mtu kujiwa na mawazo mazuri (mawazo chanya) na mawazo yasiyo mazuri (mawazo hasi) si jambo la ajabu. Kinachojalisha ni je, yanapokuja unachagua kusimamia upande upi kati ya pande hizo mbili zinazopingana?


Asilimia kubwa ya watu wana mgawanyiko wa mawazo bila ya wao kujitambua. Tena mawazo yao mazuri na mabaya huja akilini mwao bila mpangilio wala kizuizi chochote. Kwa hiyo, akili
inakuwa na namna fulani ya mvurugiko au mchafuko ambao hawaelewi unaletwa na kitu gani.


Ukimwambia mtu, “Utamiliki gari kwa Jina la Yesu,” hawezi kutuliza akili yake na kulitafakari wazo hilo hadi moyo wake ulikubali. Kila anapojaribu kulitafakari, akili yake inavamiwa
na mafuriko ya mawazo mengine mia. Hatimaye, anaanza kuyumbayumba kutoka wazo moja hadi lingine. Mathalani anaanza kuwaza, “Ni kweli naweza kumiliki gari. Kwani wenye magari si watu kama mimi? Lakini, mh! Na uchumi wenyewe huu! Fedha yenyewe nitapata wapi? Kwanza baiskeli yenyewe tu sina. Fedha yangu kwa mwezi haizidi laki moja, gari ni shilingi milioni nne. Ah! Hili jambo ni gumu kweli!”


Je, huyu mtu utasema anataka gari au hataki? Katika hali halisi, wala huwezi kusema anataka au hataki, kwani hayuko upande wowote. Si moto, si baridi! Ndivyo Mungu anavyotuona
tunapokuwa hatuna msimamo.


Mtu huyu tayari amezalisha nguvu kubwa ndani yake ambayo imelisukuma mbali kabisa gari lake. Kwa habari ya mtu kama huyu, Biblia inasema, “Mwenye shaka ni kama wimbi la bahari lililochukuliwa na upepo, na kupeperushwa huku na huku. Maana mtu kama yule asidhani kuwa atapokea kitu kwa Bwana. Mtu wa nia mbili husitasita katika njia zake zote.” (Yakobo 1:6-8).


Lakini hebu mwangalie huyu mwingine. Yeye anawaza: “Ni kweli naweza kumiliki gari. Kwani wenye magari si ni watu tu kama mimi? Japo hali ya uchumi kila mtu anasema ni mbaya, lakini Mungu amesema, ukiamini, yote yanawezekana! Pia, anasema, Si kwa uwezo wala si kwa nguvu, bali ni kwa roho yake. Naelewa kuwa fedha yangu kwa mwezi ni ndogo, lakini Bwana anasema kuwa fedha na dhahabu zote ni mali yake. Yeye ndiye atakayenipatia gari japokuwa sielewi ni kwa njia gani. Kwa Mungu yote yanawezekana. Yeye anasema, Mkiniomba lolote kwa jina langu, hilo nitalifanya. Bwana, naomba unipatie gari kwa Jina la Yesu. Asante kwa gari ulilonipa.”


Mtu huyu anaweza kuwa ni maskini kabisa kwa mwonekano wa nje. Lakini, mawazo yake haya yamezalisha nguvu kubwa inayolivuta gari lake lije kwake, maana yana msingi wake katika neno la Mungu. Anachotakiwa kufanya ni kudumu katika mawazo haya hadi mwisho.


Biblia inasema, “Mkabidhi Bwana kazi zako na mawazo yako yatathibitika.” (Mithali 16:3). Mtu huyu hajiulizi, ‘Je, gari lenyewe litakuja kwa namna gani? Fedha nitapata kwa njia gani?’ Kwa habari ya kazi ya kuyafanya hayo yatokee, amemkabidhi Bwana Yesu. Na kwa sababu anatambua kuwa kwa Bwana Yesu kila kitu kinawezekana, ni lazima mawazo yake ya kuwa ameshapata gari, yatakuwa thabiti – yaani, yatathibitika!


Mawazo yakithibitika, ndiyo imani yenyewe. Na iliko imani, yote yanawezekana! “Yesu akajibu akamwambia, Mwamini Mungu. Amin, nawaambia, Yeyote atakayeuambia milima huu, ng’oka ukatupwe baharini, wala asione shaka moyoni mwake, ila aamini kwamba hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake. Kwa sababu hiyo nawaambia, yoyote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu.” (Marko 11:22 – 24). Thibitika katika nia yako!

3 comments: