Thursday, April 4, 2013

Kuna Nguvu Katika Mawazo Yetu – Sehemu ya 1



Je, mawazo yana athari au mchango katika uhusiano wetu na Mungu? Je, yanaweza kutumika kuboresha uhusiano huo?

Kila mmoja wetu huwa anawaza mambo mbalimbali kila wakati, maadamu tuko macho. Wakati mwingine huwa tunawaza kwa kuamua na wakati mwingine huonekana kana kwamba mawazo fulani yanavamia tu akili zetu; na kila tukijitahidi kuyaondoa inakuwa ni vigumu.


Kuwaza ni kipawa cha muhimu sana alichotupatia Mungu kwa ajili ya kutuwezesha kukua katika kumjua Yeye na kuimarisha wokovu wetu na pia kuishi kwa mafanikio katika ulimwengu huu.  

Akili ya mwanadamu imeumbwa kwa namna ambayo haiwezi kutulia bila kuwaza. Maadamu uko macho, akili huwaza muda wote – mara jambo hili, mara jambo lile.


Aina za mawazo
Kuna aina kuu mbili za mawazo, yaani mawazo yanayokuja yenyewe akilini (unconscious thoughts) na mawazo tunayoamua wenyewe kuyawaza (conscious thoughts), yaani kwa utashi wetu.

Mawazo yanayokuja yenyewe
Mawazo ya aina hii ndiyo mengi zaidi kwa watu walio wengi. Tena, mengi ya mawazo haya ni yale yanayohusu matatizo, mapungufu au vikwazo mbalimbali. Hivyo, haya husababisha mtu akose amani na furaha.

Mawazo ya kuamua
Mawazo ambayo mtu huwa unayawaza kwa kukusudia ni mawazo ambayo unayachagua. Kwa mfano, unapokutana na jambo gumu ambalo unatakiwa ulitolee uamuzi, mara nyingi utasema, “Hebu nipe muda nifikirie.” Hapa, unaenda kukaa mahali penye utulivu na unaanza kulichambua wazo hilo hadi unafikia uamuzi fulani.


Kutafakari
Kutafakari ni kitendo cha kutumia akili zetu kuwaza kwa undani kuhusu jambo au wazo moja tu bila kuchanganya na mawazo mengine.

Ni kitendo cha kuchokoachokoa wazo au jambo hilo hadi unatambua mambo yaliyojificha ndani yake. Kutafakari ni jambo linalofanyikia moyoni wakati kunapokuwa na hali ya utulivu kabisa.

Kutafakari jambo ni kama kutafuna kipande cha nyama taratibu. Kwanza unaweka mdomoni kipande kikubwa. Kisha unatafuna, na kutafuna, na kutafuna hadi kinasagika na kuwa vipande vidogo vidogo.

Unapotafakari, hali kadhalika unaanza na wazo moja kubwa. Kwa mfano, “Kwa kupigwa kwake sisi tumepona.” (1Petro 2:24).
Ukishaingiza akilini wazo hili, unatulia na kufunga mambo mengine yasiyohusiana nalo. Kisha, unaelekeza akili yako yote kwenye wazo hilo. Hatimaye unaanza kulivunjavunja. Kwa mfano:
  • Anaposema ‘sisi tumepona’ ina maana na mimi ni mmojawapo. 
  • Anaposema ‘tumepona’ na wala si ‘tutapona’ ina maana tumepona sasa.
  • ‘Tumepona’ pia ina maana ni kila ugonjwa na kila tatizo – maana hajataja ugonjwa au tatizo fulani maalum.
  • Kwa hiyo, ugonjwa huu unaonisumbua au tatizo hili nililo nalo si langu.
  • Ni Mungu kasema nimepona!
  • Kile ambacho macho yangu yanaona, yaani ugonjwa au tatizo, ni uongo tu wa shetani.
  • Kile anachosema Mungu, kuwa nimepona, ndiyo kweli halisi! Kwa vile shetani ni mwongo na Yesu ni mkweli, basi ninashikilia kweli ya Yesu.
Uhusiano wa mawazo na maisha yetu

Maisha ni picha ya mawazo
Ukiyaangalia maisha ya mtu na yeye mwenyewe alivyo, unaweza kwa kiasi fulani kufahamu aina ya mawazo - si mawazo yenyewe - ambayo huwa anawaza.

Biblia inasema, “Moyo uliochangamka ni dawa nzuri; bali moyo uliopondeka huikausha mifupa.” (Mithali 17:22). Moyo ukiwa umechangamka, changamko lake hilo hudhihirika kwa nje.

Vivyo hivyo, moyo ukiwa umenyong’onyea, nao hudhihirishwa na dalili zinazoonekana kwa nje. Mawazo unayowaza ni nguvu halisi kabisa!

Vile ulivyo sasa, ndivyo na mawazo yako yalivyo. Huwezi kuwa na maisha yanayovuka kiwango cha mawazo yako. Aina ya mawazo uliyo nayo, ndiyo iliyokufikisha hapo ulipo. Je, ni mawazo ya kuweza au kushindwa? Ni mawazo ya ujasiri au hofu? Ni mawazo ya kupona au kuendelea kuumwa? Ni mawazo ya kupata au kukosa?

Si kwamba hali uliyonayo ndiyo iliyosababisha mawazo uliyo nayo. Hapana! Bali, mawazo ambayo umekuwa nayo, hata kama ni bila kujua, ndiyo yaliyozaa hali uliyo nayo sasa. Ni mambo ambayo umetoka nayo mbali.

Uliyonayo sasa ni matunda ya mapando uliyopanda kule nyuma mawazoni mwako. “Maana aonavyo nafsini mwake ndivyo alivyo.” (Mithali 23:7).

Vivyo hivyo, yale unayopanda sasa, utavuna matunda yake muda ujao. Kwa maana imeandikwa, “Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa chochote apandacho mtu, ndicho atakachovuna.” (Wagalatia 6:7).

Mtu anaweza akasema, “Akili yangu haijatulia kabisa. Sina amani moyoni. Nadhani ni kwa sababu ya tatizo A au B.” Ili maisha yetu yabadilike, wajibu wetu hasa si kuomba hali inayokuzunguka ibadilike ili mioyo yetu itulie, bali ni kubadili mawazo yetu ili yaendane na Neno la Mungu. Mabadiliko hayo ndani yetu ndiyo
yatasababisha hali iliyo nje isalimu amri na kubadilika.

Kwa mfano, hali inayokukabili yaweza kuwa ni mtoto mtukutu anayekusumbua hadi moyo wako unakosa raha. Ukishakosa raha moyoni, utaanza kusema, “Jamani, mimi mtoto huyu amenichosha. Mungu naomba mfanye abadilike ili moyo wangu utulie.” Kwa jinsi hiyo huwezi kufanikisha lolote maana, katika hali halisi, ndani yako bado una mtizamo wa kwamba, jambo hili ni gumu sana. Ulichofanya hapo ni kunung’unika tu.

Lakini ukiamua kubadili mawazo yako ukasema, “Naamini mwanangu atabadilika. Ni lazima abadilike kwa Jina la Yesu! Asante Yesu.” Unasema hivi huku mwanao bado ni msumbufu vilevile. Hapa umeelekeza mawazo yako kwenye mtizamo wa ‘inawezekana’ kwa kumwamini Mungu. Kwa kubadilika ndani yako
namna hii, ni lazima utasababisha mabadiliko nje yako, yaani kwa mwanao. Lazima!

Je, wewe unajionaje mwenyewe? Unaweza kujiweka katika kundi la watu wanaojiona wanaweza au wanaojiona hawawezi? Je, unajiona umebarikiwa au unajiona una bahati mbaya?

Kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya maisha ya mtu yalivyo na vile anavyojiona mwenyewe, yaani anavyowaza moyoni mwake.

3 comments: