Friday, December 21, 2012

Nia ya Ndani ya Moyo
Tunapofanya jambo lolote, mara nyingi huwa tunasukumwa na nia fulani iliyomo ndani yetu. Kwa mfano, mtu anaweza kumpatia mtu mwingine fedha ili:
 •  Kumsaidia katika mahitaji yake,
 • Kujionyesha mbele za watu kwamba yeye ni mwema,
 • Aweze kuja kumwomba jambo fulani, n.k.

Kwa mfano, katika biashara nyingi utakuta makampuni yakitangaza kwamba: Mteja kwetu ni mfalme; Tuko hapa kwa ajili yako; Tunakuthamini na kukujali; Tumekuandalia bidhaa kabambe kwa ajili yako na familia yako, n.k.Je, ni kweli kwamba hicho kinachofanyika kinatokana na nia ya dhati kama maneno yao yanavyosema? Ni wazi kabisa kuwa jibu ni hapana! Wanachotaka wao ni fedha zako. Haya ni maneno ya kukulainisha moyo ili utoe fedha zako kuwapatia wao.


Nia ya ndani ya moyo au huo msukumo wa moyoni unaomfanya mtu atende jambo fulani ndicho kitu kinacholifanya tendo lililotendwa liwe na thamani au liwe halina thamani kabisa. Hii ni kwa sababu nia inaweza kuwa nzuri au mbaya. Ndiyo maana mtu akikufanyia wema halafu ukamshukuru sana, lakini baadaye ukagundua kuwa alikuwa hamaanishi toka moyoni kile alichofanya, ni lazima unakosa furaha kabisa. Pia, zile shukurani ulizotoa unahisi wazi kuwa mtu huyo hakustahili kuzipata hata kidogo.


Vivyo hivyo, sisi nasi huwa tunamwendea Mungu na kumwomba mambo mbalimbali au tukafanya mambo kama vile kutoa sadaka, kuwasaidia maskini, kuimba, n.k. kutokana na nia zilizo mioyoni mwetu. Nia hizi, nazo zinaweza kuwa nzuri au mbaya.


Yesu alimwambia yule mwanamke Msamaria pale kisimani: Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba anawatafuta watu kama hao wamwabudu. Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli. (Yohana 4:23-24).


Kimsingi hapa Bwana anaongelea kuhusu nia inayotakiwa kuwapo ndani ya moyo wa mwombaji. Yule anayeabudu katika kweli ni mtu anayeabudu kwa nia safi na inayokubalika mbele za Mungu.


Lakini pia, Bwana analenga kuonyesha kuwa kuna watu wa aina mbili: kuna wale wanaomwabudu Mungu katika mwili na uongo (yaani kwa nia mbaya) na wapo wanaomwabudu katika roho na kweli (yaani kwa nia nzuri).


Ile nia ya ndani inayomsukuma mtu kuomba na kulia na kulalama mbele za Mungu ndiyo inayoamua kama hicho anachokifanya kikubalike mbele za Mungu au kionekane ni kelele tu. Tofauti na sisi wanadamu ambao wakati mwingi hatuwezi kujua nia ya mtu anayetujia, Mungu anauona moyo wa mtu wazi kabisa pamoja na nia iliyomo ndani yake.


Biblia inasema kuhusu Bwana:
 • Maana ndiye azijuaye siri za moyo (Zaburi 44:21)
 •  Ee BWANA, umenichunguza na kunijua. Wewe wajua kuketi kwangu na kuondoka kwangu; umelifahamu wazo langu tokea mbali. Umepepeta kwenda kwangu na kulala kwangu, umeelewa na njia zangu zote. Maana hamna neno ulimini mwangu usilolijua kabisa, BWANA. (Zaburi 139:1-4).
 • Pumzi ya mwanadamu ni taa ya BWANA; hupeleleza yote yaliyomo ndani yake. (Mithali 20:27).
 • Mimi, BWANA, nauchunguza moyo, navijaribu viuno, hata kumpa kila mtu kiasi cha njia zake, kiasi cha matunda ya matendo yake. (Yeremia 17:10).

Bwana anajali sana sana nia yetu ya moyoni katika kila jambo tufanyalo kati yetu na yeye. Ni jambo la muhimu sana kukagua na kuitambua nia yangu ya ndani kabisa wakati ninapomwomba Mungu.


Ingawaje kwa kiasi kikubwa tunaweza kutambua nia zetu, lakini wakati mwingine mtu anaweza kweli asijue kama yumo ndani ya mapenzi ya Mungu au yuko nje kabisa, maana maandiko yako wazi kwamba: Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote. (Yer. 17:9).


Bwana, kupitia Yakobo, anasema kuwa: Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu. (Yakobo 4:3).


Mara nyingi sisi huwa tumejaa ubinafsi. Tunamwomba Mungu kwa kuwa tu tuna uhitaji wa mambo fulani fulani.
 • Bwana naomba uniponye
 • wana naomba unipatie mchumba
 • Bwana naomba unipatie pesa
 • Bwana naomba unipatie nyumba, n.k.

Wengi wetu tunaenda kanisani leo kwa sababu tu tunaenda kutafuta kupata. Na kibaya zaidi ni kuwa, hata Injili zinazohubiriwa kanisani leo zinachangia katika kuumba nia zisizofaa mbele za Mungu.


Leo utasikia makanisa yakialika na kufundisha watu juu ya kupata fedha, magari, majumba, safari za ng’ambo, waume, wake, na mengine kama hayo.


Mambo haya si mabaya. Lakini shida inapokuja ni kwamba, yanamwondoa mtu kwenye kujiuliza anatakiwa afanye nini kwa ajili ya Mungu na ufalme wake. Badala yake mambo haya yanampeleka mtu kwenye kuwaza muda wote anachotamani yeye binafsi. Ni aina hii ya maombi na mafundisho yanayohusu MIMI, MIMI, MIMI tu na si Mungu!


Ninatakiwa nijiulize kwamba, ni kwa kiasi gani niko hapa kwa ajili ya ufalme wa Baba KWANZA kabla ya mambo mengine. Je, ni kweli nimemkabidhi BWANA maisha yangu au bado nimeyang'ang'ania kiasi kwamba ninachotaka tu ni mimi kupata, kupata, kupata! Kupokea, kupokea, kupokea!


Ndiyo maana watu wengi leo wanapokea wokovu na baada ya siku chache wanaucha na kurudi tena duniani. Je, ni kwa nini? Ni kwa sababu hawakwenda kwa Bwana, bali walienda kusaka hayo mambo wanayoitiwa na makanisa ya leo. Pale wanapoona umepita mwezi au miezi miwili na hajapata kile ambacho alikiendea, anaachana na wokovu.


Makusudi makuu ya Bwana Yesu kuja duniani kimsingi hayakuwa kutuletea mali na utajiri wa kutuburudisha kwa maisha ya kimwili japo hayo ni SEHEMU ya malengo yake. Haya ni mambo ambayo Bwana anasema, “Ninajua kuwa mnayahitaji hayo; hayo nitawapa tu.” Uafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa. (Mathayo 6:33).

Bwana Yesu alikuja KUOKOA ulimwengu. Alikuja kututoa katika hali ya UMAUTI kutokana na dhambi ili kutupatia uzima na uzima tele, yaani uzima katika dunia hii, kisha uzima wa milele katika ulimwengu ujao. Alikuja kuturejesha tena kwenye Bustani ya Edeni.


Kutafuta kwanza ufalme wa Mungu na haki ya Mungu ni kutafuta UTAKATIFU. Ni kushughulika na mambo ya ufalme wa Mungu kwanza. Kwa mfano, kuhakikisha kuwa tunda la Roho (Gal. 5:22) linaumbika maishani mwetu.


Lakini sisi tumegeuza mambo kichwa chini miguu juu. Ni kama tunamwambia Bwana, “Nipe kwanza fedha, afya, watoto, gari, n.k. na mengine yote ya kuhubiri, kutoa sadaka, kusaidia maskini, kulipa zaka, nk nitakufanyia.” Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote. (Yer. 17:9).

 • Je, wewe ni mtakatifu?
 • Je, wewe ni mgonjwa au maskini kimwili?
 • Kama wewe si mtakatifu lakini unatumia muda mwingi sana kutafuta mambo ya mwili kuliko huo utakatifu, basi hapo ndipo penye tatizo.
 • Je, uko tayari kuhangaikia utakatifu zaidi hata kama kwa upande wa kimwili utabakia maskini, mgonjwa, na mhitaji?

Hapa ndipo penye kipimo. Kipaumbele changu ni nini? Natanguliza ufame wa Mungu au natanguliza fedha, afya, nyumba, gari, n.k. kwa ajili yangu tu? Hili naweza kulijua kwa kuangalia aina ya maombi yangu ambayo, kwa sehemu kubwa, ndiyo ninayoomba.


Je, ni kwa kiasi gani ninaombea Injili iende mbele? Ni kwa kiasi gani naomba kwa ajili ya wasiookoka waokolewe? Ni kwa kiasi gani naomba kwa ajili ya majirani na maadui zangu wanaoniudhi? Haya ndiyo mambo ya ufalme. Hivi ndivyo vipaumbele vya ufalme wa Mungu.


Bwana anasema: Kwa kuwa mtu atakaye kuikoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona. (Mathayo 16:25).


Mtu anayetaka kuikoa nafsi yake maana yake ni kwamba anahaha huku na kule kusaka mambo ya kimwili; ana wasiwasi juu ya mahitaji na maisha yake; kwa hiyo, hata maombi yake yote ni kuhusu kupata mahitaji hayo.


Mtu anayeipoteza nafsi yake ni yule anayesema, “Bwana ajua.” Hata kama anafanya biashara, lakini yeye anachojua ni kuwa mleta wateja na mleta faida ni Bwana. Kama wateja hawajapatikana au mtaji umekatika, anachosema yeye ni hichohicho: “Bwana ajua.” Anahaingaikia kwanza na kile anachohitaji Bwana. Na matokeo yake ni lazima Bwana atahangaika na mahitaji yake.


Mtu wa aina ya kwanza ataenda kanisani kutafuta gari na fedha; lakini mtu wa aina ya pili ataenda kanisa kumtafuta Bwana. Mtu wa aina ya kwanza atakapokosa fedha, ataondoka kanisani na kwenye wokovu. Mtu wa aina ya pili, hata akikosa fedha, hatetereki maana kwanza fedha si kipaumbele katika maisha yake. Ataendelea kubakia na Bwana maana huyo ndiye kipaumbele chake.


Simaanishi kuwa tuache kutafuta mahitaji ya kimwili. Lakini swali ni kuwa uwiano kati ya kile ninachofanya kwa ajili ya ufalme wa Mungu na kile ninachofanya kwa ajili ya maisha yangu binafsi ukoje? Ni upande upi ambao hasa umeteka moyo wangu zaidi?


Naomba ieleweke kuwa sisemi hata kidogo kuwa hili ni jambo rahisi. La hasha! Ndiyo maana hata Bwana mwenyewe anaita huku kuwa ni kubeba msalaba kila siku na kumfuata hadi mwisho. Msalaba si jambo rahisi. Ni mzigo. Lakini bila shaka ni maswali ya muhimu kujiuliza na kujipima kibinafsi. Na wala sisemi kuwa mimi ninayeandika haya nimepiga hatua sana kuelekea kwenye utimilifu. Ila najua neno moja - kama ndugu yetu Paulo anavyosema: Si kwamba nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu; la! Bali nakaza mwendo ili nipate kulishika lile ambalo kwa ajili yake nimeshikwa na Kristo Yesu. Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele; nakaza mwendo, niifikie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu. (Wafilipi 3:12-14).


Ndugu, njia ya ufalme wa Mungu hakika ni nyembamba na imesonga, nao waionao ni wachache. Uwe mmoja wa watu hao. Mfanye Bwana kuwa namba  moja maishani mwako. Fanya nia ya maombi yako yote iwe ni: BWANA KWANZA.  Ukifanikiwa katika hilo, ni lazima naye atatimiza upande wake, usemao: na hayo yote mtazidishiwa (Mt. 6:33), yaani hayo mahitaji ya chakula, mavazi, magari, na kadhalika.


Na hata kama Bwana  hatatimiza kama ulivyokuwa umetarajia hilo halitakuwa kwazo kwako la kukufanya uanguke na kumwacha Bwana na wokovu wake wa thamani. Utaendelea kusonga mbele kwa ushindi hadi mwisho – maana hata Paulo alipewa mwiba maishani mwake ambao alitamani sana Bwana amwondolee ambapo anasema: Kwa ajili ya kitu hicho nalimsihi Bwana mara tatu kwamba kinitoke. Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. (2 Wakorintho 12:8-9).


Bwana atusaide ili nia zetu ziwe safi na thabiti mbele zake SIKU ZOTE maisha yetu hadi mwisho wa safari hii ya wokovu; ziwe ni nia zilizo sawasawa na mapenzi yake na makusudi ya ufalme wa Mungu udumuo milele, katika Jina la Yesu. Amina.

No comments:

Post a Comment