Saturday, December 8, 2012

Majibu ya Hamudi – Sehemu ya IVAdamu na Hawa walifukuzwa Edeni


Ndugu Hamudi, nilikuwa nimeahidi kuwa ningetoa jibu la jumla ili kuweza kuweka maisha ya mwanadamu katika picha yake sahihi; na ili tuweze kuona tulikotokea, tuliko na kwa nini tuko hapa; na ni wapi tunaelekea.


Tunaweza kujadiliana na kubishana sana kuhusu suala la Yesu kuwa Mungu au mwanadamu hadi mwisho wa dunia. Lakini jambo moja ni dhahiri – hatuwezi sote tukawa sahihi. Lakini hebu tuangalie uhusiano wa mwanadamu na Mungu kwa ujumla.Biblia na Quran zinataja mambo kadha wa kadha kwa namna inayofanana. Kwa mfano zote zinataja kuwa:
  •  Asili ya wanadamu ni wazazi wetu wa kwanza, yaani Adamu na Hawa. 
  •  Adamu na Hawa waliishi kwenye bustani ya Edeni. 
  •  Adamu na Hawa walikula matunda ya mti waliokatazwa baada ya kusikiliza ushauri wa shetani ambao ulikuwa kinyume na amri ya Mungu. 
  •  Wanadamu hawa walifukuzwa bustanini na Mungu.

Jambo tunaloliona hapa ni kuwa kabla ya kufukuzwa Edeni, wanadamu hawa walikuwa watakatifu (jambo ambalo halizungumzwi katika Uislamu). Hiyo ina maana kwamba, walikuwa ni watu wasiokuwa na dhambi hata kidogo. Kwa hiyo walikuwa watu wenye uhusiano mzuri na Mungu.


Kitendo cha wao kuasi amri ya Mungu ya kutokula matunda ya mti ule ndicho kilichowafanya wawe wenye dhambi. Dhambi hiyo ndiyo inayomkosanisha mwanadamu na Mungu. Dhambi ndilo jambo pekee linalovunja ushirika kati ya Mungu na mwanadamu na kuleta utengano baina yao.


Dhambi ndiyo iliyompa shetani mamlaka juu ya mwanadamu. Mwanadamu alifanyika mtumwa wa ibilisi na jeshi lake la mapepo, au mashetani au majini. Sasa walikuwa na uwezo wa kuathiri akili, hisia, mawazo na matendo yake. Waliweza kumletea magonjwa, umaskini, ugomvi, mafarakano, vita, n.k. Yote haya ndiyo mauti ambayo Mungu alimwambia mwanadamu: Siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika (Mwanzo 3:37), ambapo hatima kabisa ya mauti hii ni kutupwa kwenye ziwa la moto, yaani jehanamu ya milele.


Ni jambo lililo wazi kuwa sisi ni wenye dhambi, yaani wanadamu wote. Na Mungu kwa kuwa ni mtakatifu, hashirikiani kamwe na dhambi yoyote.


Kwa hiyo, historia nzima ya mwanadamu ni historia inayohusiana na harakati za Mungu za kusafisha dhambi za uzao wa Adamu ili baada ya maisha ya duniani, yule atakayekuwa tayari amesafika aweze kuishi milele katika ulimwengu ule ujao. Ni harakati za kurejesha uhusiano uliokuwapo mwanzo kabla ya anguko la mwanadamu wa kwanza. Tatizo la mwanadamu ni dhambi tu, yaani kuvunja sheria za Mungu.


Ni wazi kabisa kwamba tatizo si sheria za Mungu. Tatizo liko kwenye asili ya ndani ya mwanadamu. Kwa asili, sisi hatuwezi kuishi kwa utakatifu mkamilifu unaotakiwa kwa ajili ya kutufanya tustahili kuingia na kuishi kwenye mbingu za Mungu aliye mtakatifu na mkamilifu. Mbinguni HAKUNA waongo, wazinzi, watamanifu, wenye wivu, wagomvi, wavivu, wenye uchungu, wenye hasira, wezi, wauaji, n.k. Kumwambia mwanadamu aishi bila kutenda dhambi kabisa ni sawa na kumwambia fisi aache kula nyama maisha yake yote. Kwa asili yake hawezi hata kama atajitahidi kwa bidii zote. Lakini ili aweze, anahitaji nguvu iliyo nje ya asili hiyo yake; nguvu ambayo ni kubwa kuliko uwezo wake.


Adamu na Hawa walipokula tunda walilokatazwa, ndipo asili ile waliyokuwa nayo mwanzo ya utakatifu iliharibika. Matokeo yake wakawa na asili ya dhambi na uasi na mauti ndani yao. Vilevile, sisi tulio uzao wao, pia tukawa, kwa asili, ni wenye kutenda dhambi kama wao. Biblia inasema: ... kwa mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, na kwa dhambi hiyo mauti; na hivyo mauti ikawafikia watu wote kwa sababu wote wamefanya dhambi. (Warumi 5:12).


Hebu tujiulize maswali yafuatayo:

1.  Ni jambo gani zaidi ya dhambi linalomnyima mwanadamu tiketi ya kuingia mbinguni?

2.  Je, mimi ni mwenye dhambi au si mwenye dhambi?

3.  Mungu anasamehe wanadamu dhambi kwa kufuata kanuni gani? Je, anapima wingi wa makosa na wengi wa mema kisha mtu akiwa na mema mengi anamsamehe kama Uislamu unavyosema?

4.  Kama Adamu na Hawa walifukuzwa Edeni kwa kuvunja amri MOJA  sisi tunavunja amri ngapi kwa siku? Ni kitu gani ambacho kitatufanya sisi tusamehewe na kukubaliwa na Mungu wakati wao walikataliwa?

5.  Kama matendo mema yangekuwa ndicho kitu kinachohitajika ili mwanadamu ahesabike kuwa ni mwenye haki mbele za Mungu, kwa nini Mungu hakuwaambia Adamu na Hawa watende tu matendo mema kisha awarudishe kwenye bustani?


Mungu si kigeugeu hata kidogo. Akisema jambo, hivyo ndivyo linavyokuwa. Wanadamu wote ni wa kwake. Kwa hiyo, itakuwa ni ajabu kama atatoa amri za aina moja kwa kundi moja na amri za aina nyingine kwa kundi jingine; au akaadhibu watu fulani kwa kosa fulani, lakini akawasamehe wengine kwa kosa lilelile. Kama dhambi ndiyo iliyomtenga Adamu na Mungu, itakuwa ni vivyo hivyo kwa Waisraeli waliovunja amri za Torati, kwa Waarabu na kwa wanadamu wote wa leo, yaani sisi sote.


Baada ya kutokea dhambi kwenye bustani ya Edeni kupitia kwa wazazi wetu wa kwanza, ndipo Mungu alianza kuufunua mpango wake wa kumkomboa na kumrejesha mwanadamu kwenye hali ya kwanza ya uhusiano naye. Huu ni mpango wa WOKOVU.

Pale mwanadamu alipokosa, tunaona kuwa:

1.  Adamu na Hawa walisuka majani ili kuficha uchi wao. Lakini Biblia inasema: BWANA Mungu akawafanyia Adamu na mkewe mavazi ya ngozi, akawavika.  (Mwanzo 3:21). Hii inaonyesha kuwa alichinja mnyama .... Hiyo ilikuwa ni damu ya kwanza kumwagwa ili kushughulikia tatizo lililotokana na dhambi. Ilikuwa ni ishara au unabii kuwa gharama ya dhambi ni uhai na si suala la Mungu kusema kirahisi tu, “Nasamehe.”


2.  Kadiri wanadamu walivyoongezeka duniani, uovu nao ulizidi kuongezeka. Walizaliwa wanadamu wengi ambao hata hawakumfahamu Adamu wala Mungu. Lakini kama ilivyo kwa sisi leo, usipomfundisha mtoto kitu chochote, hatakuwa mwema bali atakuwa mwovu, maana mambo kama vile hasira, uchoyo, wivu, n.k. yamo tu ndani yetu kwa asili. Kwa hiyo, kupitia taifa la Israeli, Mungu alileta Torati ili mwanadamu aweze kufahamu nini anatakiwa kufanya na nini hatakiwi kufanya. Imeandikwa: maana kabla ya sheria dhambi ilikuwamo ulimwenguni, lakini dhambi haihesabiwi isipokuwapo sheria. (Warumi 5:13).3.  Mungu alipowatoa Israeli Misri alifanya nao AGANO pale Mlima Sinai. Hapo ndipo alipowapa hiyo sheria (Torati) kupitia Musa. Na kulingana na torati, suala la dhambi lilishughulikiwa kupitia kumwagika kwa damu za wanyama. Nafsi yoyote inayotenda dhambi inahesabika kuwa imekufa. Kwa hiyo, ili irudishiwe uhai, ni lazima ilipe uhai.


Imeandikwa: Kisha mtu awaye yote wa nyumba ya Israeli, au miongoni mwa hao wageni wakaao kati yao, atakayekula damu ya aina yoyote, nitakunja uso wangu juu ya mtu huyo alaye damu, nami nitamkatilia mbali na watu wake. Kwa kuwa uhai wa mwili u katika hiyo damu; nami nimewapa ninyi hiyo damu juu ya madhabahu, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu; kwani ni hiyo damu ifanyayo upatanisho kwa sababu ya nafsi. (Mambo ya Walawi 17:10-11).


4.  Taifa la Israeli ambalo Mungu alilichagua kati ya mataifa ya dunia lilikuwa na migogoro mingi kati yake na Mungu kutokana na sababu moja tu – KUASI KWAO SHERIA ZA MUNGU!


5.  Baada ya Musa walitumwa manabii wengi ambao kila mmoja alisisitiza jambo kuu moja – WATU WATII SHERIA ZA MUNGU. Na Mungu aliwaonya SANA kwamba wasipotaka kutii watapatwa na matatizo mengi ikiwa ni pamoja na taifa lao kuvamiwa na mataifa yenye nguvu na pia wao kutawanywa duniani kote na hata kuuawa. Na hicho ndicho kilichotokea.


6.  Lakini manabii wote, licha ya kusisitiza juu ya umuhimu wa kutii sheria za Mungu, kwa maelfu ya miaka, walikuwa na ujumbe MMOJA mkubwa. Kwamba atakuja MASIHI kwa ajili ya kuleta ukombozi wa mwanadamu dhidi ya dhambi ili kwamba mwanadamu huyu aweze kurudi kwenye uhusiano wa kwanza na Mungu, ikiwa ni pamoja na kupewa agano jingine ambalo ni kama lile la kwanza, isipokuwa tofauti ni kuwa la kwanza lilikuwa la kimwili, na la pili ni la kiroho.


Kwa mfano, tunaona Mungu akisema: Angalia, siku zinakuja, asema BWANA, nitakapofanya agano jipya na nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda. ... Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika; nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu ... maana nitausamehe uovu wao, wala dhambi yao sitaikumbuka tena. (Yeremia 31:31-34).


Manabii wote walitabiri kuhusiana na ujio wa Yesu Kristo. Hata Bwana Yesu mwenyewe alipokuja aliwakemea Wayahudi akiwaambia: Mwayachunguza maandiko, kwa sababu mnadhani ya kwamba ninyi mna uzima wa milele ndani yake; na hayo ndiyo yanayonishuhudia. Wala hamtaki kuja kwangu mpate kuwa na uzima. (Yohana 5:39-40).


Ifuatayo ni mifano michache ya unabii mbalimbali uliomhusu Yesu Kristo ambao ulitolewa kuanzia kitabu cha Mwanzo hadi kitabu cha mwisho cha Agano la Kale, yaani Malaki.

1.      Mwanzo 3:15 – uzao wa mwanamke – andiko hili linamhusu yule ambaye angezaliwa na mwanamke bila baba, yaani Yesu.

2.      Mwanzo 14:18 – Melkizedeki kuhani wa Mungu aliye juu. Katika torati ukuhani ulikabidhiwa kwa kabila la Lawi. Lakini Melkizedeki hakuwa wa kabila hilo. Huyu alikuwa hana baba wala mama. Yesu alipata ukuhani wake kulingana na Melkizedeki na si kulingana na Lawi (Waebrania 6:20). Kwa hiyo kuhani Melkizedeki alikuwa ni mtangulizi wa ukuhani mpya, yaani wa Yesu.

3.      Mwanzo 49:10 imeandikwa: Fimbo ya enzi haitaondoka katika Yuda, ... hata atakapokuja Yeye mwenye milki, ambaye mataifa watamtii. Huyu ni Yesu.

4.      Kutoka 12:5, imeandikwa kuhusu mwanakondoo wa dhabihu au kafara kulingana na torati ambaye waisraeli walitakiwa kumtoa, kwamba: Mwanakondoo wenu atakuwa hana ila, mume wa mwaka mmoja ... Huyu alikuwa ishara ya Yesu maana Yesu anaitwa Mwana-Kondoo wa Mungu. (Tazama Yohana 1:29).

5.      Kutoka 12:13 – Imeandikwa: Na ile damu itakuwa ishara kwenu … nami nitakapoiona … nitapita juu yenu, lisiwapate pigo lolote likawaharibu.

Ishara maana yake ni kiwakilishi cha jambo halisi. Israeli walikuwa Misri. Farao ni ishara ya shetani. Utumwa wao ni ishara ya utumwa wa dhambi za zetu. Damu inayotajwa hapa ni ishara ya damu ya Yesu ambayo tunapoiamini, halitupati pigo lolote, kwa maana ya kutupwa jehanamu.

6.      Kutoka 12:46 – Imeandikwa kuhusu namna ya kumuoka mwana-kondoo wa pasaka: wala msivunje mfupa wake uwao wote. Huu ulikuwa unabii juu ya Yesu, ambaye maelfu ya miaka baadaye alikuja kutolewa kafara kama Mwana-Kondoo wa Mungu na hakuna mfupa wowote wake uliovunjwa. (Tazama Yohana 19:31-36.)


7.            Hesabu 21:9 – Imeandikwa: Musa akafanya nyoka ya shaba, akaiweka juu ya mti, hata ikiwa nyoka amemwuma mtu, alipoitazama ile nyoka ya shaba, akaishi.

Waisraeli walipokuwa jangwani walitenda dhambi hivyo Mungu akaruhusu nyoka wengi wakawa wanawauma. Lakini yeyote aliyeumwa na akataka kupona alitakiwa kufanya kama andiko hili linavyosema. Tunapotenda dhambi tunafungulia mlango maishani mwetu unaoingiza matatizo mengi, ikiwamo mauti.


Nyoka ya shaba ilikuwa ni unabii juu ya Yesu. Maana ili na sisi tupone, tunatakiwa kumwangalia Yesu aliyeangikwa msalabani. Maana Yesu naye alikuja na kubeba matatizo yetu ya dhambi kisha akatundikwa msalabani. Imeandikwa: Na kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa; ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele katika yeye. (Yohana 3:14-15).

8.  Kumbukumbu 21:23 - Imeandikwa: aliyetundikwa amelaaniwa na Mungu ... Huu ulikuwa ni unabii kwamba Yesu angekuja kutundikwa msalabani hivyo kubeba laana YOTE ya dhambi za wanadamu ili wanadamu waweze kupokea wokovu kwa kumwamini Yeye. Ndiyo maana Wagalatia 3:13 inasema: Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu.


9. 2 Samuel 7:12 – Imeandikwa: Nawe siku zako zitakapotimia, … nitainua mzao wako nyuma yako ... yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa jina langu, nacho kiti cha enzi cha ufame wake nitakifanya imara milele.

Hapa Mungu alikuwa anamweleza Daudi mipango yake juu ya Daudi. Mzao anayetajwa ni Sulemani mwana wa Daudi. Lakini pia ni zaidi ya hapo. Sulemani alikushakufa; hayupo tena duniani. Kwa hiyo, neno milele halimhusu yeye. Neon hili linamhusu Yesu, maana Yesu anaitwa mwana wa Daudi. (Tazama Mathayo 1:1). Huyu ndiye anayetawala kwenye kiti cha Daudi milele.


10.        Zaburi 16:10 – Imeandikwa: Maana hutakuachia kuzimu nafsi yangu, wala hutamtoa mtakatifu wako aone uharibifu. Huu ulikuwa unabii juu ya kufa na kufufuka kwa Yesu.


11.        Zaburi 22:18 - Imeandikwa: wanagawana nguo zangu, na vazi langu wanalipigia kura. Huu ulikuwa unabii juu ya kile ambacho mavazi ya Yesu yangefanyiwa. Na hivyo ndivyo ilivyofanyika. (Tazama Mathayo 27:35).


12.        Mithali 30:4 - Imeandikwa: Ni nani aliyepanda mbinguni na kushuka chini? Ni nani aliyekamata upepo kwa makonzi yake? … Na ni nani jina la mwanawe, kama wajua? Huu ni unabii juu ya Yesu kuwa Mwana wa Mungu.

13. Isaya 7:14 - Imeandikwa: Tazama, bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli. Isaya alikuwa anatabiri juu ya bikira Mariamu ambaye alimzaa Yesu. Imanueli maana yake ni “Mungu pamoja nasi.” Yaani, Yesu ni Mungu pamoja na wanadamu au Mungu yumo katikati ya wanadamu au Mungu naye amekuwa mwanadamu.


14.        Isaya 11:1-2 Imeandikwa: Basi litatoka chipukizi katika shina la Yese, na tawi litatoka katika mizizi yake litazaa matunda. Na roho ya BWANA atakaa juu yake, na roho ya hekima na ufahamu, na roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha BWANA … Huyu ni Yesu ambaye anaitwa Mwana wa Daudi. Daudi ni mwana wa Yese.


15.        Isaya 50:6 - Imeandikwa: Naliwatolea wapigao mgongo wangu, na wang’oao ndevu mashavu yangu; sikuficha uso wangu usipate fedheha na kutemewa mate. Huu ulikuwa unabii juu ya yale ambayo anepitia Yesu. Na hivyo ndivyo ilivyofanyika. (Tazama Mathayo 27:26-30).


16.        Isaya 53:4-6 imeandikwa: Hakika ameyachukua masikitiko yetu, amejitwika huzuni zetu; lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, amepigwa na Mungu, na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, alichubuliwa kw amaovu yetu; adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, na kwa kupigwa kwake sisi tumepona. Sisi sote kama kondoo tumepotea; kila mmoja wetu amegeukia njia yetu mwenyewe; na BWANA ameweka juu yake maovu yetu sisi sote. Huu ulikuwa unabii juu ya Yesu na wala si mtu mwingine awaye yote.


17.        Isaya 53:8 - Imeandikwa: Kwa kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa; na maisha yake ni nani atakayeisimulia? Maana amekatiliwa mbali na nchi ya walio hai; alipigwa kwa sababu ya makosa ya watu wangu. Huu ulikuwa unabii juu ya kufa kwa Yesu.


18.   Yeremia 23:5-6 - Imeandikwa: Tazama siku zinakuja, asema BWANA, nitakapomchipushia Daudi Chipukizi la haki; naye atamiliki mfalme, atatenda kwa hekima, naye atafanya hukumu na haki katika nchi … na jina lake atakaloitwa, ni hili, BWANA ni haki yangu. Huyu ni Yesu. Jina hili, BWANA, ni jina la Mungu. Kwa hiyo Yesu ni Mungu.


19.     Danieli 7:13-14 - Imeandikwa: Nikaona katika njozi ya usiku, na tazama, mmoja aliye mfano wa mwanadamu akaja pamoja na mawingu ya mbingu akamkaribia huyo mzee wa siku, wakamleta karibu naye. Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na lugha zote, wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo hayatapita kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa. Aliye mfano wa mwanadamu hapa ni Yesu; na mzee wa siku ni Mungu Baba.


20.   Danieli 9:24 - Imeandikwa: Muda wa majuma sabini umeamriwa juu ya watu wako, na juu ya mji wako mtakatifu, ili kukomesha makosa, na kuishiliza dhambi, na kufanya upatanisho kwa ajili ya uovu, na kuleta haki ya milele …


Hapa Danieli alikuwa anaelezwa juu ya sadaka kuu ya damu ambayo ingemwagwa ili kumaliza KABISA tatizo la dhambi kwa mwanadamu na kuondoa kabisa ule utengano kati ya Mungu na mwanadamu uliotokea kule Edeni. Ndiyo maana anasema ‘kuleta haki ya milele.’ Hii yote ilihusu kifo cha Mwana-Kondoo wa Mungu, yaani Yesu ambaye alikuja kuuawa katika muda uleule ambao Danieli aliambiwa katika njozi hii. Maana tumeshaona kuwa dhambi ndilo kwazo pekee lililosimama kati ya Mungu na mwanadamu.


21.        Mika 5:2 - Imeandikwa: Bali wewe, Bethlehemu Efrata, uliye mdogo kuwa miongoni mwa elfu wa Yuda; kutoka kwako wewe atanitokea mmoja atakayekuwa mtawala katika Israeli; ambaye matokeo yake yamekuwa tangu zamani za kale, tangu milele.

Huu ulikuwa unabii kuhusu Yesu na kuzaliwa kwake. Tunatambua kutimia kwa unabii huu tunaposoma Mathayo 2:1-2. Unabii huu unabainisha kuwa huyu ambaye angezaliwa Bethlehemu na kuwa mtawala wa Israeli ni wa milele. Ni nani basi wa milele kama si Mungu pekee?


Kutokana na mambo yote hayo tuliyoyaona hapo juu, ni jambo lililo wazi kwamba:

  • wanadamu wote tuna dhambi; 
  •  damu (dhabihu) ndiyo imekuwa njia ya kuondoa dhambi kulingana na torati ya Musa; 
  • hakuna mwanadamu aliye na uwezo wa kujiondolea dhambi zake kiasi cha kumwezesha kuwa na utakatifu anaoutaka Mungu; 
  • hakuna mwanadamu mwenye uwezo wa kushinda asili ya dhambi isipokuwa kwa nguvu iliyo nje yake na ambayo si ya kibinadamu; 
  • Mungu ndiye pekee mwenye uwezo wa kuondoa dhambi; Mungu alikuja kama Yesu na akajitoa sadaka kwa ajili ya wale awapendao, yaani sisi wanadamu, ili sisi tuweze kuhesabiwa haki ya kuitwa wana wa Mungu lakini wakati huohuo sheria (torati) iwe imetimiziwa madai yake yanayotaka kila mwenye dhambi ahukumiwe mauiti. Kwa hiyo, Yesu alikubali kupokea mauti ile kwa niaba yetu.

Kumkataa Yesu ni kukataa uzima wa milele na kukumbatia mauti na hukumu ya jehanamu.

**********


Majibu kuhusiana na maswali mengine

Ndugu yangu Hamudi, najua kuwa uliniuliza pia maswali mengi sana kupitia ‘document’ inayoitwa ‘Project Reason’ yenye maswali zaidi ya mia nne yaliyowekwa humo na mtu asiyeamini kuwapo kwa Mungu (atheist),  aitwaye Sam Harris na mkewe Annaka Harris akijaribu kuonyesha kwamba Biblia inajikanganya yenyewe. Maswali hayo yanaweza kupatikana HAPA.


Kutokana na wingi wa maswali hayo, na kutokana na ukweli kwamba wapo watumishi wa Mungu wengi ambao tayari walishayajibu, nakuomba ufungue HAPA na HAPA nawe utaweza kukutana na majibu ya maswali hayo.

No comments:

Post a Comment