Tuesday, February 19, 2013

Bahasha za Zaka Makanisani Zinatoka Wapi?



Je, ni huduma kwanza au ni roho kwanza?
Wapendwa nawasalimu katika jina la Bwana wetu, Yesu Kristo.

Katika safari yetu ya kiroho tunakutana na mitihani na changamoto mbalimbali ambazo, ama zinatujenga au, kwa bahati mbaya, wakati mwingine zinatubomoa.

Lakini tunapokutana na changamoto kutoka kwa watu wasiomjua Mungu, hilo halitusumbui sana, maana tunajua kuwa kwa hao hilo ni jambo la kawaida. Mtihani mkubwa unakuja pale tunapopambana nazo kutokea kwa wale wanaomjua Mungu, na hasa kama ni vongozi wetu wa kiroho.

Nimekuwa nikijiuliza juu ya suala moja ambalo, nafikiri, limekuwa likifanyika kimazoea zaidi kuliko kimaandiko. Hili ni suala la ulipaji wa zaka.

Kutoa zaka ni agizo la Mungu kwetu. Imeandikwa: Leteni zaka kamili (Malaki 3:10.

Hata hivyo, kanuni ya utoaji kibiblia, naamini ni ileile. Biblia inasema kwamba: Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu. (2 Wakorintho 9:7).

Najua kuwa katika andiko hili, pale anaposema “Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake,” hapo anaongelea sadaka. Suala la zaka halina kukusudia moyoni mwako, maana siwezi kusema, nimepata laki moja, lakini safari hii ngoja nitoa 5000/= tu. Kwa upande wa zaka ni lazima iwe kamili.


Lakini sehemu inayosema: “si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu,” hiyo inahusu zote, yaani sadaka na zaka.


Ni muhimu sana kutoa sadaka na zaka kwa kupenda; kutoa kwa sababu ninampenda na kumtii Mungu wangu si kwa sababu nimelazimishwa au ninataka kuonekana kwa mchungaji wangu kwamba na mimi ni mtoaji.


Kutoa kwa kupenda na bila huzuni kunatokana na sababu moja tu, nayo ni kuelewa kile anachokisema Mungu, pamoja na umuhimu au faida zake.


Lakini liko jambo moja linaloendelea katikati ya waumini kwenye nyumba za ibada. Jambo lenyewe ni hali ya kunung’unika na kulalamika. Kwa upande fulani, eneo la utoaji limekuwa ni kikwazo katika ukuaji wa kiroho wa watu wengi. Kweli kabisa watu wengi wamerudi nyuma na kuacha kabisa wokovu kwa sababu ya masuala ya utoaji.


Nikirudi kwenye suala la msingi katika somo hili juu ya zaka, ninajiuliza maswali yafuatayo:

(a)       Ni wapi katika Biblia kunakosema kwamba waumini wanatakiwa kuwa na bahasha za zaka?
(b)      Hivi ni kweli kwamba bahasha au risiti za zaka (kama wafundishavyo baadhi ya watumishi) ni muhimu pale ninapopata tatizo, kwamba eti ninaweza kuziinua na kumwambia Bwana, “Tazama, nimekuwa mwaminifu kutoa zaka. Naomba unisaidie katika hili na hili”? Je, Mungu anahitajikuona risiti? Kwani Yeye mwanadamu anayesahau?
(c)       Je, si kweli kwamba inaelekea msisitizo uko kwenye kanisa (au mtumishi) kupata fedha kuliko muumini kupata kibali kwa Bwana?
(d)      Je, kuwapo kwa bahasha hakuwi kikwazo zaidi kwa waumini (hasa wachanga) kuliko kuwa baraka?
(e)       Kama watu wanarudi nyuma kwa sababu ya jambo ambalo hata Biblia hailiagizi, si bora kuliacha kwa ajili ya kuponya roho za watu hawa ambazo ni za thamani kuliko mapato ya kanisa?


Ni jambo linalotia uchungu sana kuona watu wakija kwenye wokovu kwa shauku kubwa ya kumjua Bwana Yesu na kupokea pumziko lakini baada ya siku chache wanavunjwa moyo na wanafukuzwa na hali zilizomo makanisani, ikiwa ni pamoja namna uendeshaji wa suala la utoaji zaka unavyofanyika.



Ninaweza nisiwe sahihi, lakini yafuatayo ndiyo ninayofikiri.

(a)       Suala la bahasha za zaka, japo si lazima liwe kosa, lakini haliko kokote kwenye Biblia na si jambo la lazima.
(b)      Suala la bahasha za zaka liko kwa ajili ya kutia utisho mioyoni mwa watu ili watoe hata kama mioyo yao haiko sawa mbele za Mungu na ndani yao kuna manung’uniko.
(c)       Mtu anayetoa zaka kwa uaminifu na kwa moyo mkunjufu kwa kila pato analopata bila hata ya kuwa na bahasha ya zaka anafanya vema zaidi kuliko mwenye bahasha anayetoa zaka huku ananung’unika.
(d)      Uaminifu wetu katika utoaji wa zaka unatakiwa kupata msukumo kutokana na sisi kumpenda na kumtii Bwana na si kwa sababu mchungaji ataangalia rekodi na kukuta mwezi huu sijatoa zaka.
(e)       Naamini kuwa suala la zaka halina tofauti na utoaji wa sadaka zingine. Katika sadaka za kawaida huwa hatuna bahasha wala majina, lakini watu wanatoa.
(f)            Nafikiri bahasha za zaka ni ishara ya kutomwamini Roho Mtakatifu kwamba atawagusa watu ili watoe sawasawa na mahitaji ya watumishi na kanisa.


Nimeshaona hata makanisa ambayo, muumini anatakiwa kubainisha mapema kipato chake anachotarajia kupata kwa mwezi. Baada ya kukibainisha, kila mwezi anatarajiwa kutoa kile kiasi. Asipokitoa, anaandikiwa deni.


Swali ni kuwa, je, zaka si inatokana na kile nilichopata? Kama sikupata nitatoa nini? Na kama nimepata pungufu, kwa nini nilazimike kutoa kiasi ambacho nilikibainisha?


Naamini kuwa roho za watu ni za thamani zaidi kuliko ongezeko la matoleo ya zaka. Tafadhali watumishi wa Mungu, msiwe sababu ya watu kuacha wokovu kwa sababu ya msisitizo wa zaka uliopita kiasi.


Kama mmeweza kuamini kwamba pale mnapowafundisha watu kuacha uongo, uzinzi, uchawi, n.k. watu hao wanabadilika bila ya ninyi kuwafuatilia mgongoni kila waendako, bila shaka hata suala la utoaji wa zaka linaweza kuenda sawasawa bila ya kulazimika kufuatilia jina la mtu mmojammoja kwamba ametoa au hajatoa.


Na hata pale mnapofundisha, ni vizuri sana kama mafundisho hayo yatakuwa kwa lengo la kumwonyesha mtu wajibu wake na sio kumsuta na kumlaumu na kumjaza ‘hofu mbaya’.


Ni wazi kuwa watu wasiotoa hawataisha. Wataendelea tu kuwapo. Lakini hapo ndipo ufundishaji na maombi vinapochukua nafasi yake, na bila shaka, Roho Mtakatifu atambadilisha kila mtu ‘kwa wakati wake.’

Hata dhambi zingine zote huwa hatuachi mara moja. Zingine zinaendelea kuwasumbua watu kwa muda mrefu, lakini kadiri mtu anavyodumu katika Neno, mafundisho na maombi, anafika wakati wa ushindi.


Inauma sana suala la zaka kuwa sababu ya watu kurudi nyuma; kurudi kwenye dini; kurudi duniani.


Je, bahasha za zaka zina faida kuliko hasara au zina hasara kuliko faida kiroho?





20 comments:

  1. Somo la wakati, Mungu akubariki sana.

    ReplyDelete
  2. ONGERA KWA NENO ZURI KWANI HATA MIMI BINAFSI NIKITOA ZAKA HUTOA KAMA SADAKA NA KAMWE SIKUBALI KUANDIKWA JINA KWANI HUAMINI SADAKA ZA KAWAIDA NA ZAKA NI MAHUSIANO YANGU NA MUNGU WANGU WALA HAKUNA YEYOTE APASWAE KUJUA . CHA AJABU MAKANISAA MENGINE HULAZIMISHA ZAKIA ITOLEWE KANISANI ILA MIMI HUTOA PALE NILIPO ONGOZWA NA ROHO MTKATIFU NASIO ROHO MTAKA VITU

    ReplyDelete
  3. MI NAONA NI VYEMA, UKATAFUTE MAELEZO MAANA, KUYELEWA MAONO AMBAYO MUNGU ANAMPA MTUMISHI WAKE NI VIGUMU SANA MPAKA TU UFAFANULIWE NA HUYO, LAKINI BILA HIVYO YAWEZEKANA KABISA UKAWA UNAMSHUTUMU MUNGU MWENYEWE (LUKA 24:15-18) AMBAPO ITAKUWA NI HATARI SANA, NJIA ZA MUNGU SI NJIA ZA MWANADAMU..

    ReplyDelete
    Replies
    1. Gido asante kwa maoni na ushauri wako. Hata hivyo, naamini mwongozo wetu mkuu ni Biblia. Je, kuna mahali kwenye makala haya kunakopingana na aya yoyote ya Biblia? Hata kama mtu amepewa maono na Mungu, je, hayatakiwi kuendana sawa na Biblia?

      Biblia inasema kuwa tusikubali kila roho bali tuzijaribu roho. Je, kama tukienda kwa kigezo cha kusema kwamba "haya ni maono ya mtumishi", tutawezaje kuzipima roho?

      Msingi wa hoja yangu ni kuwa, zaka ni lazima ilipwe na sisi. Lakini si lazima iwekwe kwenye bahasha kiasi cha kufikia kuanza kuitana majina ya waliotoa na wasiotoa; au kufikia mahali ambapo mtu akiwa na shida na akaenda kwa mchungaji kuombewa, mchungaji aanze kwa kuuliza, "Je, huyu analipa zaka?"

      Je, si Bwana wetu Yesu anayesema kuwa tufanye mambo kwa siri ili kumpendeza Yeye aonaye sirini na si kuwapendeza wanadamu?

      Ubarikiwe Gido.

      Delete
    2. Bwana Yesu asifiwe. Mimi naweza kusema hii blog imenitoa katika giza sababu ya kiwango cha Mungu kiasi hiki ndani yangu. Sijui na nazidi kumshangaa uyu Mungu. Mungu ananionyesha hata mambo yanayokuja na anayaprove baadae. Mungu karuusu kukuza imani yangu kupitia hii blog na kila napomwomba Mungu kwa niaba ya wengine Mungu anatenda. Kila napopiga magoti katika shida zao nikimwomba Mungu anatenda yan shuhuda ni nyingi mno. La ajabu nazidi kumueshimu uyu Mungu ni kwamba maombi yangu mimi Mungu anatenda kwa wakati wake. Na simlaumu bali nazidi kutetemeka na kumtukuza. Na wengine nikiwaombea Mungu hushuka na kutenda hapohapo. Simtafisiri ndo sheria yake bali natoa shuuda tuu. Biblia imeonya kuchunguza njia za Mungu.
      James naomba unieleweshe kuusu sadaka ya dhabihu. Na je inahusiano gani katika mtu kufanikiwa mambo yake kupitia sadaka hii ya dhabihu kama sehemu ya sala ya mtu binafsi? Na ni wakati gani na wapi ni sehemu nzuri kutoa sadaka ya dhabihu? Naomba unijibu ndugu usinisahau.

      Delete
    3. Amina, mtumishi Joseph.

      Nitalifanyia kazi swali lako.
      Bwana azidi kukubariki na kukuinua.

      Delete
    4. Barikiwa bado nakusubiri mtumishi... hapo juu

      Delete
  4. Kaka james naona umenisahau kaka?

    ReplyDelete
    Replies
    1. Shalom brother Joseph.

      Swali lako nalikumbuka kila siku wala sijalisahau.
      Nimekuwa tu kwenye ratiba ngumu inayoanza asubuhi hadi jioni kila siku
      lkn naamini ndani ya siku mbili au tatu hizi zijazo, nitaweka jibu lako.

      Bwana akubariki.

      Delete
  5. Shalom. Naomba mwenye uelewa wa swali nililoliuuliza hapo juu anisaidie. Inaonekana mtumishi wa Mungu hana mda kabisa. Au labla swali pengine ni gumu sana. Nimeuliza mda mrefu sana. Mpaka naanza kusahau. Na kuna vitu unataka kujua coz roho wa Mungu anataka kuongea nawe. Basi myu yoyote anayeweza kunisaidia anisaidie. Swala langu limekaa hapa sijui wiki ya nne hii. Asante kwa msaada.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Shalom mtumishi Joseph. Naona umengoja hadi umechoka. Lakini siku ya leo karibu yote nimekuwa naangalia swali lako. Hata hivyo, sijamaliza kabisa kulijibu, kwa hiyo nitapost kile ambacho nimepata, kisha kesho nitamalizia sehmu ya mwisho.

      Delete
    2. Shalom Joseph.
      Nimekuwa na mambo mengi kiasi kwamba sijaweza kujibu swali lako mapema inavyotakiwa.

      Lakini pia sasa baada ya kupata nafasi ya kuliangalia kwa undani, bado nikakuta ni swali kubwa, pana na lisilo na jibu la moja kwa moja. Kwenye swali lako umetaja SADAKA ZA DHABIHU. Kwa hiyo nitakachofanya mimi ni kuongelea sadaka kwa ujumla. Naamini kwamba, kwa kufanya hivyo, nitakuwa pia nimejibu swali kuhusiana na sadaka za dhabihu. Namwomba Bwana anisaidie kutoa jibu ambalo litakuwa la msaada si kwako tu bali na kwa mtu mwingine yeyote.

      Kuna maneno haya – sadaka, matoleo, dhabihu. Matoleo ni neno la jumla zaidi. Sadaka na dhabihu zina lengo la KUMPA MUNGU – hata kama kinachotolewa kinapokelewa na mtumishi wake. Lakini yapo matoleo ambayo hayamlengi Mungu moja kwa moja – kwa mfano kutoa msaada kwa mhitaji. Hiyo haiwezi kuitwa dhabihu.

      Utoaji sadaka ni agizo la Mungu toka zamani kabisa.

      (Mwa 4:4) Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. Bwana akamtakabali Habili na sadaka yake;

      (Mwa 8:20) Nuhu akamjengea Bwana madhabahu; akatwaa katika kila mnyama aliye safi, na katika kila ndege aliye safi, akavitoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu.

      KANUNI ya jumla ya utoaji wa sadaka ni KUTOA KWA MOYO pasipo kulazimishwa au kwa huzuni.

      (2Kor 9:7) Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu.

      Biblia inaongelea sadaka au matoleo ya aina mbalimbali. Tukiziangalia sadaka zote, tunaweza kuzigawa katika mafungu makuu mawili – sadaka za damu na sadaka zisizo za damu.

      Katika Agano la Kale, tunaona kuwa kulingana na torati kuna aina kuu zipatazo 5 za matoleo/sadaka/dhabihu. Sadaka au dhabihu hizi zote zilikuwa ni ishara ya ujio wa Mwokozi Yesu.

      SADAKA YA KUTEKETEZWA

      Hii ilikuwa ni sadaka ambayo iliteketezwa kabisa kwenye moto kisibaki kitu. Sadaka hii ilikuwa ni ya wanyama kama vile ng’ombe, mbuzi, kondoo na njiwa – kulingana na uwezo wa mtu.

      (Law 1:3) Matoleo yake kwamba ni sadaka ya kuteketezwa ya ng'ombe, atatoa ng'ombe mume mkamilifu; ataleta mlangoni pa hema ya kukutania, ili akubaliwe mbele ya Bwana.

      Mnyama wa sadaka hii ilikuwa ni lazima awe mkamilifu bila kilema, ugonjwa au upungufu wowote. Mletaji aliweka mikono kichwani mwa mnyama, ndipo huyo mnyama aliuawa KWA NIABA ya mtoa sadaka.

      (Law 1:4) Kisha ataweka mkono wake juu ya kichwa cha hiyo sadaka ya kuteketezwa; nayo itakubaliwa kwa ajili yake, ili kufanya upatanisho kwa ajili yake.


      Yesu kama sadaka ya kuteketezwa:


      (Ebr 10:12) Lakini huyu, alipokwisha kutoa kwa ajili ya dhambi dhabihu moja idumuyo hata milele, aliketi mkono wa kuume wa Mungu

      (1Yoh 2:2) naye ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu; wala si kwa dhambi zetu tu, bali na kwa dhambi za ulimwengu wote.

      (2Kor 5:21) Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye.

      Delete
    3. SADAKA YA AMANI
      Hii nayo ilihusisha wanyama ambao walitolewa sadaka lakini tofauti na sadaka ya kuteketezwa, hii iliteketezwa kiasi na kiasi kingine kilibakizwa, ambacho mtoaji pamoja na kuhani waliweza kula. Kwa kawaida hii ilitolewa kwa hiari ya mtu.

      Sadaka hii pia ilitolewa kwa ajili ya kuonyesha shukrani kwa Bwana kwa yale ambayo Bwana amemfanyia mtu huyo. Pia zilikuwa na lengo la kuonyesha ukaribu kati ya watu na Mungu wao.

      (Law 7:11-12) Na sheria ya matoleo ya sadaka za amani, atakazosongeza mtu kwa Bwana, ni hii. Kwamba aitoa kwa ajili ya shukrani, ndipo atakaposongeza pamoja na hiyo sadaka ya shukrani mikate isiyotiwa chachu, iliyoandaliwa na mafuta, na mikate ya kaki isiyochachwa iliyopakwa mafuta, na mikate ya unga mwembamba uliolowama mafuta.


      Yesu kama sadaka ya amani:
      (Efe 2:14) Kwa maana yeye ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi sote tuliokuwa wawili kuwa mmoja; akakibomoa kiambaza cha kati kilichotutenga.

      SADAKA YA DHAMBI
      Hii ilikuwa ni sadaka kwa ajili ya kulipia makosa yaliyotendwa bila kukusudia.

      (Law 4:1-4) Bwana akanena na Musa, na kumwambia, Haya, nena na wana wa Israeli, uwaambie, Kama mtu ye yote akifanya dhambi pasipo kukusudia, katika neno lo lote ambalo Bwana amelizuilia lisifanywe, na kutenda neno lo lote la maneno hayo; kama kuhani aliyetiwa mafuta akifanya dhambi, hata analeta hatia juu ya watu; ndipo na atoe kwa ajili ya dhambi yake aliyoifanya, na kumsongeza kwa Bwana ng'ombe mume mchanga mkamilifu, kuwa ni sadaka ya dhambi. Naye atamleta huyo ng'ombe na kumweka mlangoni pa hiyo hema ya kukutania, mbele za Bwana; naye ataweka mkono wake kichwani mwake ng'ombe, na kumchinja huyo ng'ombe mbele za Bwana.


      (2Kor 5:21) Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye.


      (Ebr 9:28) kadhalika Kristo naye, akiisha kutolewa sadaka mara moja azichukue dhambi za watu wengi; atatokea mara ya pili, pasipo dhambi, kwa hao wamtazamiao kwa wokovu.


      (1Yoh 2:2) naye ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu; wala si kwa dhambi zetu tu, bali na kwa dhambi za ulimwengu wote.


      (Isa 53:5) Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.

      SADAKA YA HATIA
      Hii ilikuwa ni sadaka kwa ajili ya dhambi ya kujipatia mapato kwa njia isiyo halali. Kwa mfano, kama mtu alimdanganya mwenzake kisha kwa udanganyifu huo akajipatia kipato, torati ilimtaka mtu huyo atoe sadaka hii.

      (Law 6:4-7) ndipo itakapokuwa, akiwa amefanya dhambi, na kupata hatia, atarudisha hicho alichokipata kwa kunyang'anya, au kitu kile alichokipata kwa kuonea, au ile amana aliyowekewa, au kitu kile kilichopotea alichokizumbua yeye, au kitu cho chote ambacho amekiapia uongo; atakirudisha hata kwa utimilifu wake, kisha ataongeza na sehemu ya tano zaidi juu yake; naye atampa huyo mwenyewe, siku hiyo ambayo atakapohukumiwa kuwa mwenye hatia. Kisha ataleta sadaka yake ya hatia kwa Bwana, ni kondoo mume wa katika kundi lake, mkamilifu, sawasawa na hesabu utakayomwandikia, kuwa sadaka ya hatia, na kumpa kuhani; na huyo kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake mbele za Bwana, naye atasamehewa; katika jambo lo lote alifanyalo hata akapata kuwa mwenye hatia kwalo.

      Hii ni sadaka iliyoonyesha malipo ya dhambi; kwamba Mungu hatamhesabia kuwa hana hatia mti mwenye hatia.

      SADAKA YA VYAKULA
      Hii ni sadaka ambayo haikuhusisha kumwaga damu. Ilikuwa ni ya vyakula mbalimbali kama vile unga. Hivi vilitakiwa kuchanganywa na mafuta na chumvi lakini havikutakiwa kuchanganywa na asali au chachu. Chumvi na mafuta ni vinazuia chakula kuharibika lakini chumvi na asali vinasababisha kuharibika.

      Delete
    4. JE, BADO TUNATOA SADAKA HIZI?
      Jibu ni NDIYO. Bwana anasema: (Mat 5:17) Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza.


      Na tena imeandikwa: Basi mambo hayo yaliwapata wao KWA JINSI YA MIFANO, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani. (1Wakorintho 10:11). Na tena: Kwa maana KRISTO NI MWISHO WA SHERIA, ili kila aaminiye ahesabiwe haki. (Rum 10:4)

      Sisi bado tunafanya kilekile isipokuwa katika utimilifu zaidi sio katika mfano. Kwa kuwa sadaka zile zilikuwa ni mfano wa sadaka kamili, ambayo ni Yesu, basi sisi leo ndio HASA tunaotimiza TORATI HALISI.

      Hiyo Warumi 10:4 inasema: ……ili kila AAMINIYE ahesabiwe haki.

      Tunapomwendea Baba tukiwa nan a dhambi au hitaji lolote KWA JINA LA YESU, tunakuwa tuko sawasawa na Myahudi wa mwilini aliyeenda na kondoo kwa kuhani; na huyo kondoo akachinjwa, kisha akatolewa kama dhabihu kwenye madhabahu ya Yehova – na tena sisi tunaye Mwanakondoo mkamilifu zaidi sana. Kila sadaka imekamilika ndani ya Kristo Yesu, Mwokozi wetu.

      Unapokuwa sasa na ile HAKI mbele za Mungu kwa njia ya Kristo, ndipo baraka za Mungu zinaweza kukufikia. Mungu hatunyimi Baraka bali ni dhambi zetu:

      (Yer 5:24-25) Wala hawasemi mioyoni mwao, Basi, na tumche Bwana, Mungu wetu, aletaye mvua, mvua ya mwaka, na mvua ya vuli, kwa wakati wake; na kutuwekea juma za mavuno zilizoamriwa. Maovu yenu yameyageuza haya, na dhambi zenu ZIMEWAZUILIA MEMA MSIYAPATE.

      Delete
    5. SADAKA ZINGINE KATIKA BIBLIA
      Zipo pia sadaka zingine kadhaa ndani ya maandiko ambazo nazo tunatakiwa kuzitoa katika kuenenda kwetu na Bwana.
      ZAKA

      (Mal 3:10) Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema Bwana wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la.


      (Law 27:30) Tena zaka yote ya nchi, kama ni mbegu ya nchi, au kama ni matunda ya nchi, ni ya Bwana; ni takatifu kwa Bwana.

      MALIMBUKO
      Hii ni sadaka kutokana na mapato YA KWANZA ya biashara, mshahara au ongezeko la mshahara, wanyama, mazao, n.k.

      (Eze 44:30) Na kitu cha kwanza cha malimbuko yote ya vitu vyote, na kila toleo la kila kitu cha matoleo yenu, litakuwa la makuhani. Tena mtampa kuhani sehemu ya kwanza ya unga mbichi, ili kukalisha baraka juu ya nyumba yako.

      MATOLEO MBALIMBALI
      Haya yanaweza kuwa ni kwa watu walio na uhitaji, wagonjwa, watumishi wa Mungu na kadhalika.

      (Luk 6:38) Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa.


      (Mith 19:17) Amhurumiaye maskini humkopesha Bwana; Naye atamlipa kwa tendo lake jema.

      NADHIRI
      Hii ni sadaka ambayo mtu anamwahidi Bwana kuwa atamtolea endapo atamtendea jambo fulani. Ni ahadi kwa Bwana kimsingi.

      (1Sam 1:11) Akaweka nadhiri, akasema, Ee Bwana wa majeshi, ikiwa wewe utaliangalia teso la mjakazi wako, na kunikumbuka, wala usinisahau mimi mjakazi wako, na kunipa mimi mjakazi wako mtoto mume, ndipo mimi nitakapompa Bwana huyo mtoto siku zote za maisha yake, wala wembe hautamfikilia kichwani kamwe.


      Hii ndiyo ambayo Bwana anaonya kwamba ni bora usiahidi kuliko kumwahidi halafu usitimize; tena akishakujibu, usiicheleweshe. Maana yake ni kuwa, haulazimiki kuahidi, lakini ukiahidi uwe makini kutimiza.


      (Mhu 5:4-5) Wewe ukimwekea Mungu nadhiri, usikawie kuiondoa; kwa kuwa yeye hawi radhi na wapumbavu; basi, uiondoe hiyo uliyoiweka nadhiri. Ni afadhali usiweke nadhiri, Kuliko kuiweka usiiondoe.

      Delete
    6. Kwa kweli nimejitahidi kutoa macho kwa umakini mkubwa but sijapata jibu nilililokuwa nimekuuliza. Infact kaka james sijaelewa. Yan safari hii nimetoka mweupe kabisa na kwa mara ya kwanza. Maana hii blog imekuwa msaada mkubwa sana kwangu sasa sijui kwa nn leo sielewi.

      Delete
  6. Somo hili ni zuri sana ila watumishi wengi yaani mapadre,wachungaji,waijilisti,mitume na manabii hawawezi kulipenda.Maana linafunua maoni binafsi ya mtumishi husika.Unaambiwa toa zaka kamili,toa sadaka inayogusa moyo wa Mungu,Pamba mbegu iliubarikiwe.Utakuaje maskini wakati wewe umeokolea?

    UNAKUA MASKINI SABABU SADAKA ZAKO HAZIGUSI MOYO WA MUNGU.
    Sasa uliza sadaka inayogusa moyo wa Mungu ni ipi...jibu utakalopewa utatamani hata utoke nje.Wakati neno linaendelea.Biblia iko mkononi mwake jibu unalopewa ni JANJA YA MANENO..yaani hakuna andiko lolote.

    Siajabu kiongozi wako wa DINI akasema TOA ZAKA KAMILI akakutajia kitabu cha Kutoka,Kumbukumbu la torati na Malaki.Lakini huyohuyo akakwambia''HAKUNA SABABU YOYOTE YA KUABUDU SIKU YA SABATO KWA KUA SABATO NI SHERIA ZA AGANO LA KALE.

    Uliza ni lini MUNGU ALITUTANGAZIA RASMI TUISHIKE JUMAPILI hakuna andiko lolote.Lakini kwakua zaka ni pesa na utajiri kwake.Hata leo hii wakuu wa DINI hawajui kama mitume waliabudu siku ya sabato baada ya Yesu.Hawajui kua JUMAPILI ilitukuzwa baadaye sana kipindi cha Upagani ulaya.

    Hawajui kwamba wakristo wa kweli milioni hamsini na zaidi walikufa kwa kuchinjwa na kuchomwa moto,nk.

    JE,WAJUA KUA MCHUNGAJI WAKO HUKAA NA MUHASIBU WA KANISA KUFANYA CHECKING WATU WANAOTOA ZAKA NYINGI? Kama ulikua haujui jua kuanzia leo.

    JE,WAJUA KUA WAUMINI WANAOTOA MICHANGO MIKUBWAMIKUBWA HATA WAKIFUMANIWA NA MICHEPUKO HAWAWAJIBISHWI?

    JE,WAJUA KUA KIJANA MASKINI ALIYEOKOKA AKIKUTWA NA MESEJI KAMA HII''Miss you dear...kiss me mwaaa,i love you''ANATENGWA NA KANISA KWA DHAMBI YA UZINZI?

    JE,WAJUA KUA VIONGOZI WA DINI NA MADHEHEBU WALIPATA LESENI ZA UDREVA KWA KUTOA RUSHWA ,HAKUHUDHURIA MAFUNZO KWENYE CHUO KINACHO HUSIKA,HAKUFANYIWA MAJARIBIO,KUKWEPA KODI ZA TRA?

    JE,UNAFAHAMU KUA MAKANISA MENGI NA MISIKITI HUIBA UMEME NA MAJI,NA WAUMINI WANAOHUSIKA KUFANIKISHA WIZI HUOKUPONGEZWA NA VIONGOZI WAO?

    Kupenda pesa ndio issue kuu.

    ReplyDelete
  7. Kila mtu na aitii mamlaka iliyo kuu, kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu, na ile iliyopo imeamliwa na Mungu,
    Hivyo amwasiye mwenye mamlaka hushindana na agizo la Mungu, nao washindanao watajipatia hukumu.

    Warumi 13:1-2

    ReplyDelete