Naamini umeshasikia
mara nyingi watu wakisema, “Usinihukumu bwana. Wewe si Mungu.”
Lakini swali ni kuwa, je,
dhana hii hutumiwa na watu kwa jinsi ilivyo sawa? Kabla hatujajibu swali hili,
hebu tuchunguze maandiko yafuatayo:
- Msihukumu msije mkahukumiwa. Kwa kuwa hukumu ile mhukumuyo, ndiyo mtakayohuku- miwa; na kipimo kile mpimiacho, ndicho mtakachopimiwa. (Mt. 7:1-2).
- Au hamjui ya kwamba watakatifu watauhukumu ulimwengu? Na ikiwa ulimwengu utahukumiwa na ninyi, je! Hamstahili kukata hukumu zilizo ndogo? Hamjui ya kuwa mtawahukumu malaika, basi si zaidi sana mambo ya maisha haya? (1 Wakor. 6:2).
Ukisoma maandiko haya
unaweza kusema, “Mbona maandiko haya yanapingana?” Au kuna makosa yalifanyika
hapa? Katika andiko la kwanza, Bwana Yesu anasema tusihukumu. Lakini katika andiko
la pili, Paulo anasema tunatakiwa kuhukumu.
Ajabu ni kuwa, Paulo
huyouhuyu ambaye hapa anayesema HUKUMUNI, ndiye anayesema kwenye sura iliyo
nyuma tu kidogo kwamba: Basi ninyi MSIHUKUMU neno kabla ya wakati wake, hata
ajapo Bwana; ambaye atayamulikisha yaliyositirika ya giza … (1 Wakor. 4:5).
Nini basi maana ya ‘kupingana’
huku?
Hebu tuanze na maneno
ya Bwana Yesu katika Mt. 7 hapo juu. Unapoendelea kusoma mistari inayofuata,
utaona kuwa Bwana anasema kwamba: Basi mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani
ya jicho la ndugu yako, na boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe
huiangalii? ... Mnafiki wewe,... (Mt. 7:3-5).
Lakini hata hivyo kuhukumu
maana yake ni nini hasa? Kuna maana mbili za neno hili. Kwanza, ni kubaini
kwamba jambo au hali fulani ni halali au si halali; ni sawa au si sawa;
inakubalika au haikubaliki. Mathalani, ukimsikia mtu anasema uongo, moyoni
mwako unatambua kuwa hilo ni kosa. Hapo umehukumu.
Maana ya pili ya neno ‘hukumu’
ni kutaja adhabu ya kosa. Kama utamwambia
huyo aliyesema uongo kwamba ‘usipotubu utaenda motoni’, hapo umehukumu.
Sasa je, ni kweli
kwamba maandiko hayaturuhusu kufanya hayo? Jibu ni hapana! Ukweli ni kwana,
Bwana Yesu hatuzuii hata kidogo kuhukumu. Tunatakiwa kuyafanya hayo. Maana kama
tungekuwa haturuhusiwi, utawezaje kumkanya mtu ambaye amekengeuka? Utawezaje kumhubiria
injili mtu asiyemjua Yesu? Utawezaje kusuluhisha ugomvi kati ya waliogombana?
Hata hivyo, ni kweli
kwamba maandiko yanapiga marufuku aina fulani ya watu kuhukumu; na yanatoa
ruhusa ya kufanya hivyo kwa watu maalumu.
Tumeona hapo juu Bwana
Yesu akisema kuwa mwenye boriti jichoni hawezi kuona kibanzi kwenye jicho la
mwenzake. Ni wazi kwamba hapa anaongelea uwezo wa kuona mambo kiroho. Ukiwa na
maisha ya dhambi hautakuwa na uhalali wa kumkemea au kumhukumu mwenye dhambi
mwingine. Dhambi hupofusha ufahamu wa mtu.
Kwa kawaida, mwenye
dhambi anapomhukumu mwenye dhambi mwingine, huwa anataka tu sifa na kujikosha
mbele za wanadamu ili uovu wake usimulikwe na kuonekana. Ndiyo maana Bwana
anamwita kuwa ni mnafiki.
Tunapokuwa wenye
dhambi halafu tunawahukumu wengine, tunakuwa wanafiki kwa sababu mioyoni mwetu
tunajua kuwa sisi wenyewe hatuna uwezo wa kuziacha zile dhambi za kwetu.
Hebu tuchukue mfano
halisi. Unakuwa uko kwenye daladala. Kisha unamwona msichana au mvulana amevaa
mavazi yasiyo ya heshima hata kidogo. Halafu unasema, “Watu wengine bwana,
hawana heshima kabisa. Hebu ona alivyo. Ovyo kweli kweli.”
Swali atakalokuuliza
Bwana ni kwamba: Ni kweli wewe huwa huvai mavazi ya heshima. Lakini, vipi
kuhusu uongo? Vipi kuhusu usengenyaji? Vipi kuhusu wivu?
Ndiyo maana Paulo
akasema kwamba: Lakini wewe, ukiwa unaitwa Myahudi na kuitegemea torati, na
kujisifu katika Mungu, na kuyajua mapenzi yake, na kuyakubali mambo yaliyo
bora, nawe umeelimishwa katika torati , na kujua hakika ya kuwa wewe mwenyewe u
kiongozi wa vipofu, mwanga wao walio gizani, mkufunzi wa wajinga, mwalimu wa
watoto wachanga, mwenye namna ya maarifa na ya kweli katika torati; basi wewe
umfundishaye mwingine, je! Hujifundishi mwenyewe? (Rum. 2:17-21).
Kwa kifupi anachosema
hapo ni kuwa, wewe ambaye unamwambia mwenzio kuwa ni hovyo kwa vile kavaa
vibaya unasema hivyo kwa kuwa moyoni mwako unayo namna fulani ya elimu njema
inayokufanya utambue jema na baya. Lakini, mbona unaitumia tu katika kushambua
wengine lakini huelekezi mishale hiyo kwako mwenyewe? Anza kwanza na dhambi
zako ndipo utakuwa na haki ya kuwahakimu juu ya wenye dhambi wengine.
Ni kweli kwamba sisi
kama binadamu hatuwezi kujua hali ya moyoni ya mwanadamu mwingine. Lakini Mungu
wa mbinguni anaona kila kitu. Ndiyo maana anasema kuwa, siku hiyo atamwambia
huyo mnafiki, “Wewe ulisema kuwa Hamisi ni mwongo/ni tapeli hadi watu
wakamchukia. Lakini mbona wewe ulikuwa mwizi wa mali ya umma japo wanadamu
wenzio hawakujua? Mbona wewe ulikuwa msengnenyaji? Kwa kuwa ulisababisha Hamisi
akachukiwa, na wewe ni lazima upate hukumu.”
Hicho ndicho
kitakachotokea. Lakini si Mungu wa mbinguni tu anayeona na kuyajua hayo; hata
mhusika mwenyewe anajijua alivyo japo anaweza kuwaficha wengine.
Ni kwamba, sote tu
wenye dhambi. Lakini yule mwenye dhambi ambazo hazikutubiwa, hana ruhusa ya
kumhukumu mwenye dhambi mwenzake. Msengenyaji hana ruhusa ya kumsema mlevi au
mwizi au mvaa ovyo kana kwamba yeye ni salama na bora kuliko wao; mwongo hana ruhusa
ya kumsema mchawi kwa kuwa wote wawili sehemu yao ni moja baada ya maisha haya.
Sasa, inakuwaje tena
Paulo anasema katika 1 Wakor. 6:2 kwamba tunatakiwa kuhukumu mambo ya maisha
haya?
Kimsingi, hata Bwana
Yesu anasema jambo lilelile. Wala hawa wawili hawapingani hata kidogo. Ukiendelea
kusoma katika Mathayo, Bwana anasema hivi: ... itoe kwanza ile boriti katika
jicho lako mwenyewe; ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi katika jicho la
ndugu yako. (Mt. 7:4-5).
Unaona sasa! Kumbe twaweza
kuhukumu. Lakini kwanza ondoa boriti jichoni. Kuondoa boriti maana yake kutubu
dhambi kwa maana ya kuziacha. Yaani, unatubu kwa nia na makusudi ya kutorudia
tena. Hata ikitokea umerudia, inakuwa ni kwa bahati mbaya kabisa, si kwa
makusudi huku ukiwaza kwamba, “Si nitatubu.”
Imeandikwa: Afichaye dhambi
zake hatafanikiwa; bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema. (Mith.
28:13).
Tunapotubu dhambi zetu
na kuishi maisha ya utakatifu na ukamilifu, hakika Bwana anatupa ruhusa na
wajibu wa kuhukumu na kuwa kinywa chake hapa duniani. Katika hali hiyo, hatuwi
mahakimu wadhalimu bali ni mahakimu tunaosukumwa na upendo wa Kristo ndani
yetu; ambao nia yetu ni watu wamjue Bwana na wafanikiwe maishani mwao.
Kwani ukimwambia mlevi
aache ulevi, wewe unapata faida gani kutoka kwake? Maana hata hizo fedha huwa
hakuletei wewe. Badala yake unamwambia hivyo ili iwe faida kwake na kwa familia
yake binafsi.
Mtakatifu anapomwona
msichana au mvulana amevaa mavazi yasiyo ya heshima hataanza kuongea
kichinichini juu ya namna alivyo ovyo. Huo ni usengenyaji ambao ni dhambi
(isipokuwa kama ni mhubiri anayehubiri waziwazi) bila kumlenga mtu mahususi. Badala
yake mtakatifu atahukumu kuwa jambo hili si sawa na ama atamwambia hivyo
mhusika au atamwombea.
Lakini kama wewe ni
mwizi, Bwana hakupi ruhusa ya kumhukumu huyo mlevi. Badala yake anakutaka utoe
kwanza boriti la wizi wako ndipo utaweza kuona kibanzi cha ulevi wa mwenzako.
Hukumu ya mwenye haki
si lawama, masimambo na usengenyaji. Hukumu ya mwenye haki huekea kwenye uponyaji
wa roho na mwili wa yule anayehukumiwa.
Kwa hiyo, si kweli hata
kidogo kwamba hatutakiwi kuhukumu!
Watakatifu tunatakiwa kuhukumu!
ahsante sana kwani nimejua nini maana ya hukum. Mungu wa Mbinguni akubariki!
ReplyDeleteMungu azidi kukubariki emback kwa kuendelea kujifunza na kuwa na shauku ya kumjua zaidi. ni jambo zuri kuendelea kujifunza zaidi na zaidi maana hekima yake kwa kweli haina mwisho, kwa hiyo tukikunja mikono na kubweteka, tunajikosesha mengi mno. Lakini tunapokuwa na shauku na kiu ya haki, Yeye yuko tayari siku zote kutufundisha. ubarikiwe sana.
ReplyDeleteJames kwa kuchangia tu mimi nadhani wakati mwingine unakuta unamuelewesha mtu kwa upendo tu yale anayoyafanya kuwa ni kinyume ni misingi ya ukrristo, unakuta mtu anaanza kuchachamaa usinihukumu hata wewe una dhambi, ni kweli mtu anaweza akawa na mapungufu yake pia lakini kukumbushana wajibu sio mbaya japo wakati mwingine watu hulichukulia hili neno vibaya matokeo yake wanaogopa kukemea dhambi wakihisi wataonekana wanahukumu
ReplyDeleteDhambi zisipokemewa kweli tutafika pabaya, na tunaona siku hizi hata makanisani dhambi zinachekewa, watu hawahubiri Kristo wanahubiri mafanikio, kuoa na kuolewa
Wasiwasi wangu ni kuwa na kundi kubwa lenye watu wenye mafanikio wanaolekea motoni
Sipo kumuhukumu mtu,ila huo ni mtazamo wangu wapendwa
Unachosema Star ni kweli. Mungu mwenyewe anataka yule anayeona kuwa mwenzake anakosea, amwonye. Lakini jambo msingi ni kuwa, siwezi kumwonya mtu katika jambo hata mimi ni mkosefu. Kama mimi ni mlevi halafu nikaanza kuwaambia wanangu, kwa mfano, acheni ulevi; hicho ndicho anachosema Bwana kuwa ni unafiki. Ni kushughulikia kibanzi cha mwingine wakati mimi nina boriti. Mungu akubariki.
ReplyDeleteAsante Bwana Yesu kwamba ukutuacha pasipo mwelekeo. Na mwelekeo huo ni Roho Mtakatifu ambaye kwa uhakika haachi kutuambia yaliyo katika Moyo wa Mungu. Naomba tuwe tayari kufundishwa kwani Yesu bado anayo mengi na wala hatutayamaliza.
ReplyDeleteKubwa ni kwamba tufuatilie majira haya tuliyomo ili tupate neema ya kuyapata yote ya majira haya na kuyaweka kwenye matendo kwa ajili ya utukufu wa Jina la Yesu.
Kuna hesabu katika yote aliyotuandalia:
-kwamba iko juu kwa kuwa tumekaa kwenye nafasi ya kuyaweka kwenye matendo na Bwana Yesu kuwa upande wetu.
-tumeshindwa kukaa kwenye nafasi na hivyo kushindwa kuyapata yale Roho Mtakatifu anayafunua kwetu. NI HATARI SANA KWANI HAKUNA MASHAKA YESU ATATUKATAA KWA KUWA FUNGU LETU NI PAMOJA NA ROHO WA UASI, roho wa shetani.
Kuwa na Yesu ni gharama ndugu zangu,watumishi mliopewa madhabahu waambieni ukweli watu wa Mungu ili Yesu upande wao na sio kuongelea ya dunia hii tu.
Mwenye sikio na asikie.
naomba ieleweke kuwa aliyeokoka/ambaye Bwana Yesu ni Bwana kwake KWAMBA NI MADHABAHU YA BWANA YESU.
ReplyDeleteNeno la Mungu linasema miili imenunuliwa kwa Damu ya thamani na kwahiyo Roho Mtakatifu anakaa, ni kwake, ni madhabahu ya Bwana.
Na ni Yeye Roho Mtakatifu anayetufundisha KWELI NA HIYO ITATUWEKA HURU. kwa nini nimesema hayo ili nionyeshe kuwa unapokuwa ndani ya wokovu kuna kuwajibika, ndiyo maana inakuwa gharama kwa kila mwana wa Mungu kuijua kweli naye aiseme kweli kwa wengine. Kwa machache haya nimalizie kusema kuwa ukweli hakutatoka kwenye makanisa tu ila kwa kila mwana wa Mungu NA HATIMAYE TUTAONYANA KWA NAMNA MUNGU ATAVUNA KWA INJILI YA KWELI KUSONGA MBELE. AMINA.
Shalom brother Revocatus. Asante sana kwa kututia moyo kwa mashauri yako ya kweli.
ReplyDeleteNi neno la kweli kabisa kwamba wokovu una gharama na kwamba sisi ni lazima tuitafute kweli ya Mungu wetu kwa bidii. Roho Mtakatifu aliye Mwalimu wetu mkuu yuko tayri kutufundisha kama sisi wenyewe tutataka kuyajua yale aliyotuandalia.
Mungu akubariki sana.
Thank u soo much may God bless u
ReplyDelete