Mpendwa mmoja aliniuliza maswali
yafuatayo ambayo nimeona ni muhimu niyajibu kama Makala fupi kwa ajili hata ya
faida ya watu wengine wenye maswali kama haya:
Swali la 1: Hivi watu wakifa,
roho zao zinakuwa wapi hasa?
Swali la 2: Roho hizo zinakuwa
katika hali gani hasa?
WATU WAKIFA, ROHO
ZAO ZINAKUWA WAPI?
Biblia
inasema kuhusu Bwana Yesu kuwa:
Kwa
hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili
kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na
vya chini ya nchi; (Wafilipi 2:9-10).
Kulingana
na mstari huu, tunagundua kuwa kuna sehemu kuu tatu:
Mbinguni
Duniani
Chini ya nchi
Mbinguni
ni mahali aliko Mungu; duniani ni mahali tuliko sisi wanadamu tulio hai; na
chini ya nchi ni mahali aliko ibilisi.
Tangu
nyakati za Adamu kulikuwapo wanadamu wema na waovu. Wanadamu wema walikufa na
waovu nao walikufa. Swali ni kuwa, je, walipokufa walienda wapi?
Mwinjilisti
Luka anatupatia picha nzuri kutokana na kisa alichosimulia Bwana Yesu juu ya
tajiri na Lazaro. Tunasoma katika Luke 16:22-26:
22
Ikawa yule maskini alikufa, akachukuliwa na malaika mpaka kifuani kwa Ibrahimu. Yule
tajiri naye akafa, akazikwa.
23
Basi, kule kuzimu aliyainua macho yake, alipokuwa katika mateso,
akamwona Ibrahimu kwa mbali, na Lazaro kifuani mwake.
24
Akalia, akasema, Ee baba Ibrahimu, nihurumie, umtume Lazaro achovye ncha ya
kidole chake majini, auburudishe ulimi wangu; kwa sababu ninateswa katika moto
huu.
25
Ibrahimu akasema, Mwanangu, kumbuka ya kwamba wewe uliyapokea mambo mema yako
katika maisha yako, na Lazaro vivyo alipata mabaya; na sasa yeye yupo hapa
anafarijiwa, na wewe unaumizwa.
26
Na zaidi ya hayo, kati yetu sisi na ninyi kumewekwa shimo kubwa,
ili wale watakao kutoka huku kwenda kwenu wasiweze; wala watu wa kwenu wasivuke
kuja kwetu.
Tunachoona
hapani kuwa Lazaro alikuwa ni mwenye haki kama Ibrahimu na tajiri alikuwa ni
asiye na haki. Hawa walikaa sehemu mbili tofauti, maana zilitenganishwa na
bonde. Sehemu hizi zote mbili zilikuwa chini ya nchi.
Kabla
ya Yesu kufa, wanadamu wote walipokufa walienda chini ya nchi. Na huko kulikuwa
na sehemu mbili – kwa shetani na kifuani mwa Ibrahimu. Katika habari hii ya
tajiri na Lazaro – ambayo ilitokea zamani sana hata kabla ya Musa, Bwana Yesu
anatuonyesha kuwa tajiri alikuwa kwenye mateso; na Lazaro alikuwa penye raha.
Lakini
mtu anaweza kusema hivi, “Huoni kuwa tajiri aliinua macho yake? Je, hii si ishara kuwa Lazaro na Ibrahimu
walikuwa mbinguni?
Wakati
huo mbingu zilikuwa hazijafunguliwa kwa ajili ya wanadamu. Tuendelee kusoma na
hapo mbele tutapata jibu la maswali hayo.
Bwana
alipokuja duniani, akateswa na akauawa, tunaambiwa kuwa:
Kwa
maana Kristo naye aliteswa mara moja kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili
yao wasio haki, ili atulete kwa Mungu; mwili wake akauawa, bali roho yake
akahuishwa, ambayo kwa hiyo aliwaendea
roho waliokaa kifungoni, akawahubiri. (1Petro 3:18-19)
Mbinguni
hakuna vifungo; vifungo viko chini ya nchi. Kwa hiyo, Bwana alienda kuwahubiria
waliokuwa kifungoni.
Bila
shaka hii ndiyo sehemu ambayo Wakatoliki huita toharani. Sehemu hii ilikuwapo
zamani kama makao ya muda kwa wale waliokufa kabla ya Kristo. Humo waliwekwa
kungojea ukombozi wa mwanadamu ufanye na Kristo. Lakini sasa hivi haipo tena.
Maana
ya andiko hili katika Petro ni kuwa, wale waliokuwa kifuani mwa Ibrahimu (au
tuseme toharani), Bwana alienda akawahubiria katika zile siku tatu alipokuwa katika
tumbo la nchi.
Je,
baada ya kuwahubiria, nini kilifuata?
Imeandikwa:
Hivyo
husema, alipopaa juu aliteka mateka,
Akawapa wanadamu vipawa. Basi neno hilo,
Alipaa, maana yake nini kama siyo kusema kwamba yeye naye alishuka mpaka pande
zilizo chini za nchi? (Efe 4:8)
Shetani
alikuwa amewashikilia wanadamu wote kuzimu, lakini Bwana akaenda akawateka na
kuondoka ndao. Na ndiyo maana kabla Bwana hajafa, alisema:
Ama
awezaje mtu kuingia ndani ya nyumba ya mtu mwenye nguvu na kuviteka vyombo
vyake, asipomfunga kwanza yule mwenye nguvu? Ndipo atakapoiteka nyumba yake. (Mathayo
12:29)
Na
ushahidi wa jambo hili uko wazi kwa sababu Biblia inatuambia kwamba baada ya
Bwana kufa, watakatifu waliokuwa wamekufa zamani walionekana Yerusalemu.
Naye Yesu akiisha kupaza
sauti tena kwa nguvu, akaitoa roho yake. Na tazama, pazia la hekalu likapasuka
vipande viwili toka juu hata chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka; makaburi
yakafunuka; ikainuka miili mingi ya watakatifu waliolala; nao wakiisha kutoka
makaburini mwao, baada ya kufufuka kwake, wakauingia mji mtakatifu, wakawatokea
wengi. (Mat 27:50-53)
Je,
alipoteka mateka aliwapeleka wapi?
Imeandikwa
kuhusu yule mwizi aliyesulubiwa pamoja na Bwana:
Kisha
akasema, Ee Yesu, nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako. Yesu akamwambia,
Amin, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami peponi. (Luka 23:42-43)
Ukisoma
kwenye Kiingereza, imeandikwa hivi: And Jesus said unto him, Verily I say unto
thee, To day shalt thou be with me in paradise.
Peponi ndio paradiso.
Paradiso
si Yerusalemu Mpya. Paradiso ni makao ya muda kwa ajili ya watakatifu,
kusubiria mwisho wa mambo yote ambapo Yerusalemu mpya itafunguliwa na kuwa makao
ya milele pamoja na Bwana.
Kama
ambavyo watakatifu wako kwenye makao ya muda paradiso, ndivyo ambavyo na wenye
dhambi wako kwenye makao ya muda kuzimu aliko shetani sasa – maana shetani hayuko jehanamu bado. Yaani,
wako kule alikokuwa yule tajiri aliyezungumza na Ibrahimu kuhusiana na Lazaro
kutumwa duniani.
Pia
tunasoma kuwa:
Kwa
maana ikiwa Mungu hakuwaachilia malaika waliokosa, bali aliwatupa shimoni,
akawatia katika vifungo vya giza, walindwe
hata ije hukumu. (2Petro 2:4)
Hawa mashetani wako kifungoni
lakini kumbe wala hiyo si hukumu bado. Ndiyo maana anasema wako pale hata ije hukumu. Itakapofika sasa
mwisho wa mambo yote, ndipo kila mtu ataenda sasa kwenye makao ya milele.
Biblia
inasema kuhusu wakati huo:
Kisha
Mfalme atawaambia wale walioko mkono wake wa kuume, Njoni, mliobarikiwa na Baba
yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu; (Mat
25:34)
Kisha
atawaambia na wale walioko mkono wake wa kushoto, Ondokeni kwangu, mliolaaniwa,
mwende katika moto wa milele,
aliowekewa tayari Ibilisi na malaika zake; (Mat 25:41).
Kumbe
moto wa milele ndiyo hukumu ya mwisho iliyotajwa hapo juu.
Hata
tukisoma kwenye Ufunuo imeandikwa: Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na
wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu
yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na
kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili.
(Ufu 21:8)
Kwa
nini inaitwa mauti ya pili? Ni kwa sababu japo tajiri yuko kwenye mateso na
hayuko duniani tena (yaani alishakufa); japo wale malaika walio kifungoni wako
kwenye mateso sasa; lakini iko mauti nyingine tofauti nay a sasa. Kitendo cha
kutupwa kwenye ziwa la moto (jehanamu) na kubaki humo milele ndicho kinachoitwa
mauti ya pili.
Hata
roho hii ya mauti inayotutoa duniani
sasa pamoja na kuzimu aliko shetani
sasa navyo vitaingia jehanamu kwenye mauti ya pili:
Imeandikwa:
Mauti na Kuzimu zikatupwa katika lile ziwa la moto. Hii ndiyo mauti ya pili,
yaani, hilo ziwa la moto. (Ufu 20:14)
JE, ROHO ZILIZOONDOKA DUNIANI
ZINAKUWA KATIKA HALI GANI?
Hawa ni watu kamili kama tulivyo sisi. Sisi
kama roho tumo ndani ya mwili wa nyama, lakini ukivua mwili huu (yaani, ukifa)
unavikwa mwili wa kiroho; na unaendelea kuishi kama kawaida.
Biblia
inasema: Tena kuna miili ya mbinguni, na miili ya duniani; lakini fahari yake
ile ya mbinguni ni mbali, na fahari yake ile ya duniani ni mbali. (1Kor
15:40)
Tofauti ni majukumu tu. Huku tunafanya kazi,
tunasafiri, n.k. Lakini kule wenye dhambi wanateswa na watakatifu wanamfurahia
Yesu, kwa mfano kwa kusifu.
HITIMISHO
Kuzimu ni mahali aliko shetani sasa hivi pamoja
na wanadamu wote wanaokufa katika dhambi. Haya ndiyo makao makuu ya uovu wote
unaoendelea duniani leo. Baada ya mambo yote, yaani mwisho wa nyakati, kuzimu
na kila kilichomo ndani yake vitatupwa kwenye ziwa la moto wa milele.
Wanadamu wanaokufa ndani ya Yesu wako paradise
sasa hivi. Baada ya mwisho wa mambo yote, wataingia Yerusalemu mpya na kuishi pamoja
na Bwana milele na milele.
Usipange kukosa kuingia Yerusalemu Mpya!
Ubarikiwe sana Mtumishi
ReplyDelete