Sunday, April 6, 2014

Niliokolewa Toka Kwenye Nguvu za Giza - Sehemu ay 3
Agano Langu na Alice
Mapema asubuhi moja, Alice aliniambia kuwa kulikuwa na sherehe ya muhimu iliyotakiwa kufanywa kwenye nyumba yake. Saa 8 usiku alileta mtoto mchanga wa kike anayetambaa, akiwa hai. Mbele ya macho yangu, Alice alitumia vidole vyake kunyofoa macho ya mtoto yule! Kilio cha mtoto huyo kiliniumiza sana! Kisha alimkatakata vipande na kumimina damu pamoja na nyama kwenye sinia na kuniambia nile. Nilikataa! Alinitazama moja kwa moja usoni na kile kilichotokea machoni mwake siwezi kukielezea kwa kuandika. Kabla sijajua nini kinaendela, nilijikuta si tu natafuna zile nyama, bali pia nilikuwa nalamba damu. Wakati haya yakiendelea alisema, “Hili ni agano kati yetu. Hautasema chochote kamwe utakachoona nikifanya au chochote kuhusiana na mimi kwa mwanadamu yeyote duniani. Siku utakayovunja agano hili, lako litatoweka.” Alimaanisha kuwa siku nitakayovunja agano hilo, nitauawa!


Baada ya tukio lile, nilianza kuwa na hisia za ajabu ndani yangu. Nilibadilishwa kabisa na sikuweza kujidhibiti mwenyewe. Neno la onyo kwa akina mama – Je, unamfahamu mtumishi wako wa ndani? Historia yake ikoje? Je, unajibidisha kujua yote yanayomhusu kabla ya kumkabidhi maisha  ya wanao, n.k. Unaweza kuuliza, je, Alice aliwezaje kupata kile kichanga alichokichinja? Kwa hiyo, wazazi muwajue wale wanaowasaidia nyumbani.

Alice alipoona kuwa tayari ameshaniingiza kikamilifu kwenye uabudu shetani na akawa anapanda ngazi kwa haraka ndani yake, aliridhika na kujua kuwa misheni yake imeshakamilika. Alinitafutia nyumba, akanisaidia kuweka fenicha, na baada ya hapo akavunja uhusiano kati yetu.

Agano kule India
Ile jumuiya kule Delhi, India ilinitumia barua ya pili, ikinitaka niende India. Ndani yake pia niliagizwa kufanya yafuatayo: Nile kinyesi, nile panya aliyekufa na kuoza akiwa na harufu mbaya, na kufanya mapenzi na mapepo makaburini usiku.

Baada ya kutimiza masharti hayo, nilifungwa ili nisiweze tena kamwe kuja kufanya mapenzi na mwanamke yeyote humu duniani. Niliwajibu barua yao nikiwaambia kuwa sikuwa na viza na wala sikujua namna ya kufika India. Kwa wakati huu nilishaanza kufanya ‘biashara’.  Nilikuwa mfanya magendo mkubwa, lakini kwa sababu ya nguvu zilizokuwa nyuma yangu, sikuwa na matatizo yoyote na watu wa forodha, n.k. Nilianza kuwa na fedha nyingi sana, chakula na vitu vingine.

Siku moja nilifunga nyumba yangu na kutoka nje. Niliporudi, nilifungua mlango na kukuta mwanamume mmoja amekaa sebuleni. Niliogopa sana. Aliniuliza, “Wewe ni Emmanuel Amos?”
Nikajibu, “Ndiyo.”
Akasema, “Nimetumwa nije kukuchukua na kukupeleka India, kwa hiyo jiandae.”
Nilifunga kila mahali, kisha nikaenda na kukaa kando yake kwenye kochi tayari kwa amri itakayofuata. Lakini alinigusa na, kama umeme, tulitoweka!  

Kilichofuata, nilijikuta niko kwenye ukumbi mkubwa wa mikutano kule Delhi, India, huku kukiwa na watu wengi ambao walikaa tayari wakisubiri kutukaribisha. Walileta mafaili ambamo jina langu lilishaandikwa tayari na wakaniambia niweke saini yangu. Nilifanya hivyo. Kisha lililetwa sinia lililojaa nyama za binadamu zilizokatwakatwa vipande, pamoja na beseni lililojaa damu. Kila mmoja wetu alipewa jagi tupu. Mtu mmoja ambaye hakuwa na kichwa alipita akimmiminia kila mmoja damu na nyama kwenye jagi. Kulikuwa na aina mbalimbali  za mishumaa na ubani vikichomwa. Yule mtu asiye na kichwa alitamka maneno na kila mtu alikunywa damu ile na kula zile nyama, na mkutano ukawa umeishia hapo. 

Kuingizwa Kundini India
Sasa muda wangu wa kujaribiwa ulikuwa umeshafika. Nilipelekwa kwenye bonde lenye kina cha kama meta 200 hivi. Ndani yake kulikuwa na viumbe mbalimbali wa hatari sana pamoja na wanyama wa mwituni. Hawa walitakiwa kunitesa. Sikuruhusiwa kupiga kelele; maana nikipiga kelele, basi nakuwa nimefeli mtihani wangu; na matokeo yake ni KIFO! Baada ya siku saba za mateso nilitolewa na kupelekwa mahali panapoitwa ‘MSITU WA INDIA.’

Katika msitu huu niliona aina mbalimbali za ndege wa kipepo. Ni wa kipepo kwa sababu wengine walikuwa na nyuso kama za mbwa, kama paka, n.k., lakini bado wana mabawa. Ndani ya msitu huu kulikuwa na pango. Pango hili hufunguliwa na hao ndege wa kipepo tu. Walifungua lile pango nami nikaingia. Mambo niliyoyaona humo ni vigumu kuelezea. Kulikuwa na viumbe wa kutisha; wengine kama binadamu lakini wakiwa na mikia ila hawana nyuso za kibinadamu, n.k.  Hapa palikuwa ni mahali pengine pa mateso. Mateso ya pale naweza kusema tu ni nusu jehanamu! Nilikuwa katika hali hiyo kwa muda wa siku 7 kisha nikatolewa.

Hatimaye nilipelekwa kwenye maktaba moja kubwa sana yenye vitabu vingi vikubwakubwa vya mambo ya siri ya giza. Nilichukua vitabu viwili: Abbysinia, kinachomaanisha uangamivu, na Assina, kinachomaanisha kutoa uzima au kuponya. Baadaye nilipewa vitabu zaidi. Nikaelekezwa nijenge chumba mara nitakaporudi Naijeria na kiwe na vitu vifuatavyo: mtungi uliojaa damu ya binadamu, mti ulio hai ndani yake, fuvu la binadamu, manyoya ya tai, ngozi za wanyama wa porini, ngozi ya  chatu, na jiwe linalong’aa pembeni mwa mtungi huo. Nilitakiwa niwe nakunywa damu iliyo kwenye mtungi kila asubuhi huku nikitamka maneno fulani. Vilevile, niliagizwa kuwa nisile kabisa chakula kilichopikwa na mwanadamu; badala yake nitakuwa nikilishwa kimiujiza. Baada ya hapo, nilirudi tena Naijeria kwa njia ileile niliyoijia; na nikaenda kutekeleza masharti hayo yote.  
Nikiwa Nyumbani Naijeria
Sasa nilishakuwa sehemu ya ulimwengu wa roho na niliweza kusafiri kwenda kokote duniani kadiri nipendavyo. Kulingana na vitabu nilivyorudi navyo, nilisoma kuwa mapepo yanaishi angani. Nikawaza kuwa labda yanaweza kuniongezea nguvu; hivyo, nikaamua kujaribu. Nilitoka nje ya nyumba yangu, nikatamka maneno fulani na kuita upepo wa kisulisuli na nikatoweka. Mara nikajikuta niko kwenye anga na nikayaona hayo mapepo.
“Unataka nini?” yaliniuliza.
“Nataka nguvu zaidi,” niliyajibu.

Nilirudi duniani baada ya wiki mbili huku nikiwa nimepata nguvu kutoka kwao.  Kama nilivyosema mwanzo, nilikuwa sina tena uwezo wa kujitawala au kujidhibiti. Licha ya nguvu zote hizo ambazo nilikuwa nimepata, bado nilijisikia kuhitaji nguvu hata zaidi! Hivyo, niliamua kwenda kwenye ulimwengu wa chini ili kuthibisha kile kilichoandikwa kwenye vitabu nilivyopewa.

Siku moja nilienda mahali palipojificha kichakani. Nilitamka maneno kama ilivyoelezwa kwenye kitabu na nikaamuru ardhi ifunguke. Kweli ardhi ilifunguka na mapepo yakatengeneza ngazi mara moja. Nilishuka moja kwa moja hadi chini ya ardhi. Kulikuwa na giza totoro ambalo linaweza kulinganishwa tu na lile lililotokea Misri kama ilivyoandikwa kwenye Biblia. Niliona mambo mengi sana ambayo ni vigumu kuyaelezea. Niliona watu wakiwa wamefungwa minyororo; watu wanaotumiwa kutengeneza fedha – wanafanya kazi usiku na mchana kutengeneza fedha kwa ajili ya wale waliowafunga.

Niliona badhi ya wanachama wa vikundi vya siri ambao walikuja huko kwa ajili ya kutoa kafara; kisha wanarudi duniani wakiwa na zawadi walizopewa na mapepo wanaotawala mahali hapo. Niliona baadhi ya viongozi wa Kanisa waliokuja kutafuta nguvu - yaani nguvu za kusema jambo Kanisani na likakubalika bila maswali. Nilikaa huko kwa wiki mbili na kurudi nikiwa nimepewa nguvu zaidi. Watu waliniona kama mtoto mdogo asiye na tatizo lolote lakini hawakujua kuwa nilikuwa ni mtu hatari sana. Kuna watu wengi wa aina hiyo kila mahali. Ni wale tu walio ndani ya Kristo ndio wenye usalama wa kweli.  

Agano na Malkia ya Pwani
Jioni moja, niliamua kutembeatembea. Nikiwa eneo la stendi ya mabasi ya Ebute Metta, nilimwona binti mmoja mrembo amesimama mahali. Sikumsemesha neno lolote. Siku iliyofuata wakati nikipita, nilimwona akiwa amesimama hapohapo. Siku ya tatu, nilimwona yuko palepale! Wakati napita, aliniita. Nilisimama na kujitambulisha kuwa naitwa  Emmanuel Amos lakini yeye alikataa kujitambulisha.

Nilimwuliza jina na anwani yake lakini alicheka tu. Aliniuliza anwani yangu nami nikamtajia mtaa TU. Nilipokuwa naondoka, alisema kuwa atakuja kunitembelea siku moja. Akilini mwangu niliwaza, ‘Hilo haliwezekani. Sikumtajia namba ya nyumba yangu; atawezaje kufika?” Lakini ajabu ni kuwa baada ya wiki moja alifika! Nilisikia mlango ukigongwa. Nilipofungua, alikuwa yuko pale mlangoni. Nilimkaribisha huku nikijiuliza, “Huyu msichana mrembo ni wa namna gani? Hivi hajui kuwa anaingia kwenye eneo la hatari?” Tuliongea na baadaye aliondoka. Kuanzia hapo akawa anakuja kunitembelea mara kwa mara lakini bila ya kuwa na mahusiano yoyote.  

Niligundua kuwa alikuwa akija muda uleule; hazidishi wala hapunguzi! Siku zingine nilikuwa nikimpeleka Lagos Barbeach, au Paramount Hotel au Ambassador Hotel, n.k. Kwa wakati huo wote, alikuwa hajaniambia jina lake. Nami niliamua kutojali kwa kuwa nilijua kuwa uhusiano wetu usingeenda zaidi ya ulivyokuwa sasa. Nilishapewa masharti kwamba nisije nikamgusa mwanamke.

Ghafla, alibadili muda na akaanza kuja usiku. Siku moja aliniambia, “Sasa ni wakati wa wewe kunitembelea na mimi.” Tulibaki pamoja usiku ule na ilipofika saa 2:00 asubuhi siku iliyofuata, tuliondoka. Tuliingia kwenye basi na akamwambia dereva atushushe Barbeach. Tuliposhuka nilimwuliza, “Tunaenda wapi?” Akasema, “Usijali. Utaijua nyumba yangu.” Alinipeleka kwenye kona mojawapo ya Barbeach, akatumia kitu kama mkanda kunifunga mimi na yeye. Mara moja ilikuja nguvu kutokea nyuma na kutusukumia baharini! Tulianza kupaa kwenye uso wa bahari kuelekea katikati ya bahari!

Mpendwa msomaji, haya yalinitokea kwenye ulimwengu wa mwili! Tulifika mahali tukazama hadi chini kabisa ya bahari na kwa mshangao wangu, nilijiona tunatembea kwenye barabara nzuri! Tuliingia kwenye jiji ambalo lilikuwa na watu wengi; kila mtu na harakati zake!

Ulimwengu wa Roho
Kule niliona maabara za kisayansi, za kuunda vitu, kumbi. Na nyuma ya jiji lile, niliona wasichana warembo wadogo na vijana wadogo wazuri.  Hakukuwa na wazee. Alinitambulisha kwao nami nikakaribishwa. Alinipeleka mahali ambako ni kama chumba cha giza, “darkroom”, chumba cha kukaushia, “drying room”, na chumba cha kufungashia, “packing room”. Kisha alinipeleka kwenye kiwanda kikuu na ghala, halafu tukaenda kwenye nyumba yake. Hapo ndipo aliniambia, “Mimi ni malkia ya pwani na ningependa sana kufanya kazi na wewe. Naahidi kuwa nitakupa utajiri na yote yanayoenda pamoja nao; ulinzi na vyote vinavyoenda nao; maisha pamoja na ‘malaika’ wa kukuongoza.”  

Alibonyeza kitufe na trei likatokea likiwa na nyama za binadamu, tukala pamoja. Aliamuru chatu atokee na kuniambia nimmeze! Nilishindwa. Alisisitiza lakini bado nilishindwa. Nawezaje kumeza chatu aliye hai? Kisha alitumia uwezo wake nami nikammeza. Haya yalikuwa ni maagano matatu: nyama ya binadamu na damu, chatu na malaika wa kipepo walikuwa pale kuhakikisha kuwa hakuna siri inayotoka.

Lakini yule ‘malaika’ alipewa uwezo wa kuniadhibu kama nikienda kinyume na pia kuniletea chakula kutoka baharini wakati wowote niwapo hapa duniani. Niliahidi kuwa nitamtii siku zote. Baada ya ahadi hii, alinipeleka sehemu nyingine ya bahari; safari hii kisiwani. Kulikuwa na miti na kila mti ulikuwa na kazi yake: 
- mti kwa ajili ya sumu,
- mti kwa ajili ya kuua,
- mti kwa ajili ya kuita (invoking), na
- mti kwa ajili ya kuponya.


Alinipa nguvu za kujibadili katika aina zote za wanyama wa baharini kama vile kiboko, chatu na mamba, halafu akatoweka. Nilikaa baharini kwa wiki nzima; na kwa njia mojawapo (yaani kama mamba) niliweza  kurudi duniani.


Maabara za Kuzimu
Nilikaa Lagos kwa wiki moja kisha nikarudi tena baharini; safari hii kwa miezi miwili. Nilienda kwenye maabara za kisayansi kuona nini kinachoendelea huko. Niliwaona wataalamu wa akili (psychiatrists) na wanasayansi wakifanya kazi kwa bidii sana. Kazi yao ni kuunda vitu vizuri kama vile magari ya kifahari, silaha, n.k.; na pia kujua siri za dunia hii. Kama ingewezekana kujua nguzo za dunia hii, wangefanya hivyo. Lakini ashukuriwe Mungu – NI MUNGU PEKE YAKE ANAYEZIJUA.
Nilihamia kwenye chumba cha kubuni na hapo niliona sampuli nyingi za vitambaa, manukato, na vipodozi mbalimbali. Vitu hivi vyote, kulingana na Lusifa, ni kwa ajili ya kuondoa macho na umakini wa watu kutoka kwa Mungu Mwenyezi. Pia niliona vifaa mbalimbali vya kielektroniki, kompyuta, na alamu.  Ilikuwapo pia TV iliyowawezesha kuwaona Wakristo waliookoka duniani. Hapo unaweza kutofautisha kati ya Wakristo wa kweli na wale wanaoenda tu Kanisani kutimiza wajibu.

Hatimaye, niliondoka kwenye maabara na kwenda kwenye chumba cha giza, ‘dark room’ na cha kukaushia, ‘drying room’. Chumba cha giza ni mahali pa kuwaulia wale wasio watii. Kwanza wananyonya damu ya mtu huyo kisha wanampeleka kwenye chumba chenye mashine ambako anasagwa kuwa unga. Huo unga unapelekwa kwenye chumba unakofungwa kwenye mifuko kwa ajili ya waganga wa kienyeji wanaokuja huko kuchukua dawa. Vilikuwapo vitu vingi sana ambavyo ni vigumu kuelezea kwa kuandika.

Lakini licha ya nguvu zote hizi ndani yangu, bado nilikuwa sijastahili kukutana na Lusifa ila nilikuwa nastahili tu kuwa ajenti wake. Hata hivyo, nilikuwa ninajisikia kuwa ninazo nguvu za kuweza kukabiliana na kitu chochote na kukiharibu kadiri nipendavyo. Nilikuwa najiuliza, “Kuna nguvu nyingine kweli zaidi ya hii niliyonayo inayoweza kunizidi?”

1 comment: