Sura ya 2: Kuingizwa Kundini
“Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu,
lakini mwisho wake ni njia za mauti.”
(Mithali 14:12).
“Bali wabaya wanafanana na bahari iliyochafuka; maana haiwezi kutulia, na maji yake hutoa tope na takataka. Hapana amani kwa wabaya; asema Mungu wangu.” (Isaya 57:20-21).
Maisha nje
ya Yesu ni vivyo hivyo kama yanavyosema maandiko hayo hapo juu. Niliondoka
kijijini kwangu nikiwa na Naira 50 pamoja na anwani niliyopewa na Alice, nikitaraji
kutorokea kwenye uhuru na raha
pamoja na yote yanayoandamana navyo. Lakini kama utakavyoona baadaye, hali
halisi ilikuwa tofauti kabisa na mawazo yangu ya kitoto yalivyokuwa. Nilipofika
Lagos, kulikuwa kuzuri sana machoni mwangu na nikailinganisha na mbinguni; japo
sijui mbingu zenyewe zikoje. Niliona majengo yote yale marefu na ya kuvutia na
kwenye kila uso wa mtu niliona furaha (ndivyo nilivyowaza). Watu walionekana
wako bize sana huku kila mmoja akiwa na shughuli zake. Nilifurahi na kusema
moyoni, “Sasa najua kuwa niko huru!”
Nilifika
Akintola Road, Victoria Island na kupokewa vizuri na Alice na wazazi wake.
Wazazi walinifahamu mimi pamoja na historia yangu maana tulitoka kijiji kimoja;
lakini hawakujua uhusiano kati yangu na binti yao. Alice alinitambulisha kwao
kama mwanamume ‘aliyemchagua’ kuolewa naye. Wazazi wake walishtuka sana lakini
baada ya majadiliano naye, walikubali kwa masharti kwamba wataniendeleza
kielimu. Alice alikataa mapendekezo yao na akaomba kwamba niruhusiwe kuishi
naye kwenye nyumba yake. Wazazi walikataa lakini akasisitiza. Walikuwa na
mabishano makali kwa muda wa siku nne na kwa namna nisiyoweza kuielewa,
walikubali nami nikahamia kwa Alice.
Alice, msichana mrembo sana,
aliniambia kuwa yeye ni mhasibu kwenye Standard Bank na kwamba atanifanya niwe
tajiri na kunipa kila nikitakacho maishani; na kasema, “Wewe tulia tu kwanza na
ufurahie maisha!”
Mtazamo wangu wa kwanza kuhusu
Lagos ulikuwa kweli hata hivyo. Miezi michache iliyotangulia nilikuwa kwenye
kijiji kidogo katika kibanda kidogo huku nikiwa nimezungukwa na chuki, njaa na
mateso; na sasa niko hapa – naishi kwenye jiji kubwa, kwenye nyumba yenye
samani nzuri, na ‘mke’ mrembo ambaye aliahidi kunipatia kila kitu kizuri
maishani! Alinipatia zawadi nyingi,
fedha, mavazi, ‘mapenzi’, n.k. Sikujua kuwa dunia imejaa ‘vitu vizuri’ namna
hii. Ibilisi hakika ni mdanganyifu! Maandiko yanasema vizuri: “Mwivi
haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha
wawe nao tele.” (Yohana 10: 10). Mpendwa msomaji, ibilisi
hana zawadi ya bure! Chochote akupacho ni lazima mbadilishane na roho yako.
Hali hii ya raha ilidumu kwa muda mfupi sana. Baada ya miezi mitatu, mambo ya
ajabu yalianza kutokea.
Mambo ya Ajabu
Siku moja
niliamka usiku wa manane na kukuta joka kubwa liko pembeni yangu. Nilitaka
kupiga kelele lakini sikuweza. Siku zingine usiku ningeamka na kukuta mwili wa
Alice uko kama kioo, yaani unaweza kuona hadi upande wa pili. Nyakati zingine
za usiku, aliweza kutoweka na kurudi tena. Wakati mwingine nilisikia sauti za
ajabuajabu za watu wakicheza sebuleni, n.k. Sikuweza kuvumilia zaidi mambo haya
ya kutisha, hivyo niliamua kumwuliza. Mwitikio wake wa kwanza ulikuwa ni vurugu
na kunionya kwa nguvu sana. Alisema, “Usiniulize swali hili tena vinginevyo
nitakushughulikia!”
Kuanzia hapo
nilijua kuwa maisha yangu yamo hatarini. Nikatamani mateso yangu ya kijijini
kuliko hiki nilichojiingiza kwacho. Nikawa namwogopa sana Alice. Zilipita siku
mbili na akaja kwangu na tabasamu, zawadi pamoja na kunikumbatia. Aliniambia
jinsi alivyonipenda na kunijali na akanitia moyo kuwa nisiogope; na akaniahidi
kuwa atanifanya niwe tajiri, n.k. Pia aliniambia, “Siku
moja utajua yote ninayoyajua!” Tulirudiana na maisha yakaendelea kama
mwanzo. Ndani yangu nilijua kuwa niko hatarini lakini nitatorokaje? Na nitaenda
wapi? Ni muhimu kujua hapa kuwa wazazi wa Alice hawakujua kuwa binti yao, japo
alikuwa mdogo, alikuwa amezama kabisa kwenye ibada za kishetani; na alinionya
sana kuwa, kama napenda maisha yangu, nisiwaambie kamwe wazazi wake ukweli huo.
Mpendwa msomaji, unaweza kupata picha ya msichana wa miaka 20 akifanya mambo
haya? Kule nje, dunia ilimwona kama msichana mrembo asiye na madhara,
anayefanya kazi kwenye benki kubwa. Lakini ukweli ni kuwa alikuwa ajenti wa
ibilisi. Wako kina Alice wengi duniani leo kama ambavyo utafahamu kwenye kitabu
hiki hapo baadaye.
Ugunduzi wa Kutisha
Siku moja,
alipoondoka kwenda kazini, niliamua kuikagua nyumba. Pamoja na udogo wa Alice,
nyumba ile ilikuwa imejaa samani nzuri sana. Alikuwa na mafriji manne na nilipofungua
mojawapo, niliona mafuvu ya watu, sehemu mbalimbali za miili ya watu – ambazo
ni mbichi na zilizokauka! Ndani ya dari kulikuwa na viunzi (skeletons). Kwenye
kona mojawapo ya chumba kingine, niliona (ambacho nilikuja kukijua baadaye kama ‘chamber’) mtungi ambao ulijazwa damu na mti
mdogo uko katikati ya mtungi huo, kibuyu pamoja na nguo nyekundu pembeni yake.
Sikuweza kuendelea zaidi. Sasa nilijua kuwa nimeshakufa mimi; na hasa kwa kuwa
sikuwa na mahali pa kukimbilia! Nilitoa maisha yangu kwa chochote
kitakachonikuta – iwe ni kuishi au kufa na nikafunga kinywa changu kabisa. Alice
alirudi kutoka kazini na kwa namna alivyoniangalia, nilijua kuwa tangu ofisini
kwake alishajua nilichofanya kwenye nyumba yake.
Kukutana na Ulimwengu
wa Ibada za Kishetani
Siku
iliyofuata, aliniomba nifuatane naye kwenye mkutano. Tayari nilikuwa mateka na
sikuwa na jinsi. Tulienda kwenye jengo moja kubwa sana nje ya Lagos.
Tulipofika, (jengo lile lilikuwa na ukumbi wa mikutano wa chini ya ardhi),
nilielekezwa na Alice niingie kinyumenyume. Naye pia alifanya vivyo hivyo.
Ukumbi ulikuwa mkubwa sana ukiwa na vijana wa kike na kiume takriban 500
waliokaa kwenye duara; na juu yao alikaa kiongozi wao, mwanamume ambaye alikuwa
na kichwa tu bila kiwiliwili! Baadhi ya
hawa vijana walikuwa ni wanafunzi, wanachuo, walimu, n.k. Alice alibonyeza
kitufe ukutani na kiti kikatokea toka ardhini, nami nikakaa. Alifanya
hivyohivyo na kingine kikatokea naye akakaa. Alinitambulisha kwenye kundi kama
mshiriki mpya nao wakapiga makofi na kunikaribisha. Alice alipandishwa cheo kwa
ajili ya hili. Katika vyote walivyojadili kwenye mkutano ule sikuelewa hata
kimoja. Mwishowe, wakati tunajiandaa kuondoka, niliambiwa na kiongozi, nirudi
peke yangu siku iliyofuata. Hii ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kukutana na
ulimwengu wa waabudu shetani.
Usiku uleule,
kwenye saa nane usiku (na huu ni muda wa kawaida wa mikutano na operesheni za
hatari za nguvu za giza na maajenti wao), Alice aliniamsha na kunionyesha mambo
fulanifulani. Alisema, “Mimi si binadamu wa kawaida. Mimi ni nusu binadamu na
nusu roho lakini zaidi ni roho. Unachoona kwenye ‘chamber’ yangu ndicho
ninachotumia wakati wa sala zangu kila asubuhi, ili kwamba zile roho ziniongoze
kwa siku nzima. Na kuhusu viunzi (skeletons), nitakuja kukueleza baadaye.”
Sikusema
neno lolote! Alitoa baadhi ya vitabu kuhusiana na mambo ya giza kwa ajili ya
mimi kusoma, na kwa sababu ya akili yangu ya kutaka kujua, niliamua kuvizoma.
Kwa muda mfupi, nikawa nimevutiwa; na yeye naye akagundua kuwa nimevutiwa
navyo. Bila ya mimi kujua, alipeleka jina langu kwenye chama cha waabudu
shetani kule India.
Kama
nilivyokuwa nimeelekezwa jana yake, siku iliyofuata nilienda kwenye lile jengo
peke yangu na nikakutana na watu nane wengine pamoja na baadhi ya mashahidi.
Tulikuwa tunaingizwa kwenye kundi. Tuliitwa hadi katikati ya ukumbi na
tukafanyiwa mambo yafuatayo:
- Tulipakwa mwilini utomvu fulani. Hii inakufanya ustahili kuwa mwanachama kamili.
- Tulipewa kimiminika kama mafuta kwenye glasi tukanywa. Hii inakufanya ustahili kuwa ajenti.
- Tulipakwa kichwani kitu kama unga. Hii inakufanya ustahili kujua siri zao.
Bila mimi kujua, sherehe hii ya kuingizwa kundini nayo ilikuwa inarekodiwa India na siku iliyofuata nilipokea barua kutoka kwao. Humo ndani nilielekezwa nipake barua ile damu yangu na kuituma kwao tena kwa njia ambayo waliielezea - si kwa njia ya posta. Nilifanya hivyo. Kuanzia hapa, kulikuwa hakuna kurudi nyuma. Kurudi nyuma ilimaanisha kifo kama ambavyo ulikumbushwa tena na tena; nami nilijua kuwa hakukuwa na tumaini tena kwangu!
No comments:
Post a Comment