Wednesday, August 29, 2012

Ulinzi Kutoka kwa Waganga wa Kienyeji



Naamini umeshasikia mara kadhaa watu wakitaja kile kinachoitwa “sayansi ya kiafrika”. Kwa kifupi maneno haya yanaongelea kazi za waganga wa kienyeji. Ni wazi kuwa yanamaanisha upigaji ramli, uaguzi, usafishaji nyota, na hata ulozi na mengine kama hayo.

Siku hizi watu wengi wanakimbilia kwa waganga wa kienyeji kwa lengo la kupata “mafanikio”, wakiwamo wanasiasa, wafanyabiashara, wafanyakazi, wake, waume, wapenzi, wachumba, wanamuziki, na hata wale wanaotaka  kuwakomesha wabaya wao.

Ukipita sehemu nyingi, utakutana na matangazo ambayo, japo yanashangaza, lakini watu wanaenda kwa hao walioyaweka!

Kumfunga mpenzi mkorofi, kuzindika nyumba, kusafisha nyota, kupata kazi, n.k. ni baadhi ya maneno yaliyo kwenye mabango hayo. Kilichonishangaza mimi ni kuwa, kuna hata matangazo yanayosema wazi kabisa “Njoo tukusaidie kupata utajiri wa majini”!!

Sisemi kuwa hakuna dawa za kienyeji. La hasha! Zipo nyingi na nzuri kabisa. Lakini linapofikia suala la kuaguana na kuambiana kutumia dawa huku mtu yuko uchi, au aangalie mashariki, au akanywee makaburini, n.k., hapo liko jambo.

Kabla sijamjua Yesu, niliwahi kwenda kwa mganga mmoja. Alinipa dawa kwenye kichupa kidogo. Na akanipa sharti la kwenda kuinywa usiku wakati watu wote wamelala; na nihakikishe hanioni mtu yeyote.

Lakini kabla ya kuondoka kwake, alinichanja chale, ambapo aliniambia nifumbe macho na nisifungue kabisa wakati anaponichanja! Haya ni mambo ambayo yanafanyika kila siku sehemu mbalimbali.

Alikuwapo mfalme mmoja wa Israeli aliyeitwa Sauli, ambaye alimwasi BWANA. Baada ya kuona mambo hayamwendei vema, siku moja aliwaambia watumishi wake: Nitafutieni mwanamke mwenye pepo wa utambuzi, nipate kumwendea na kuuliza kwake. (1 Samweli 28:7).

Alipofika kwa huyo mwanamke, akamwambia: Tafadhali nibashirie kwa utambuzi, ukanipandishie yeye nitakayemtaja kwako.... Nipandishie Samweli. (1 Sam 28:8, 11).

Samweli alikuwa ni nabii mkubwa wa Mungu ambaye kwa wakati huo alishakufa. Kwa hiyo, kwa kutojua kwake, Sauli akataka eti apandishiwe huyo nabii kutoka huko aliko apate kuomba msaada kwake ili mambo yake ya kiutawala yamnyokee.

Hatimaye, huyo mwanamke mtabiri alipopiga manyanga yake na kuzama kwenye ulimwengu wa roho, akasema: Naona mungu anatoka katika nchi. Sauli akainama mpaka nchi, akasujudia. (1 Sam 28:13-14). Ukweli ni kuwa huyo aliyeonekana hakuwa Mungu wala Samweli.

Ndivyo ilivyo hata leo. Ukienda kwa mpiga ramli atafanya mambo yake, kisha ataondoka katika ufahamu wa kawaida wa kibinadamu ili aweze kuwasiliana na viumbe wa rohoni.

Sasa ni kitu gani hasa kinachoendelea hapa?

Ulimwengu huu unaongozwa na nguvu zisizoonekana. Zipo nguvu za aina mbili kuu – kuna nguvu za nuru na nguvu za giza.

Niseme tu kuwa hakuna kitu kama “sayansi ya kiafrika”, bali ni matumizi ya mapepo/majini/mashetani. Hawa ni viumbe halisi kabisa, lakini ni wenye akili na nguvu kuliko mwanadamu.

Yule aliyeonwa na mwanamke ambaye mfalme Sauli alimwendea alikuwa ni pepo wa kutoka kuzimu. Mungu hatoki katika nchi; anatoka mbinguni!

Ndivyo watu wanavyodanganywa hata leo hii. Wanasema wanaongea na babu au bibi zao waliokufa. Ukweli ni kuwa huyo anakuwa ni pepo kabisa. Anapokuja, anakutaka labda ufanye mambo ya uganga, n.k. Ni pepo; ni jini; ni shetani!

Au wale wanaoenda kutambika kwenye makaburi wakidhani wanaongea na wazee wao. Ndugu, hapo unafanya biashara na mashetani kabisa! Biblia inasema: Kwa kuwa liko tumaini kwa yule aliyeambatana na wote walio hai; (maana ni afadhali mbwa aliye hai kuliko simba aliyekufa); kwa sababu walio hai wanajua ya kwamba watakufa; lakini wafu hawajui lolote, wala hawana ijara tena; maana kumbukumbu lao limesahauliwa. (Mhubiri 9:4-5).

Tapeli anapokuja kwako kwa maneno matamu, laini, ya kuvutia, utafurahi na kudhani umepata rafiki. Lakini nia yake ni kukumaliza. Unaweza hata kunywa soda yake tamu, halafu kesho yake ukajikuta uko mtaroni, hujitambui, na umeibiwa kila kitu. Majini ni viumbe wenye hila. Hata kama wanachofanya kinaonekana kizuri, mwisho wake ni uangamivu. Maana kama ni “kufanikiwa”, utafanikiwa kabisa.

Maandiko yanasema: Wala si ajabu, maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru. (2 Wakorintho 11:14).

Lakini Bwana Yesu anatupa hali halisi ilivyo kuhusiana na Shetani na mapepo yake. Anasema: mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu. (Yohana 10:10). Shetani ni mwizi, mharibifu na mwuaji tu. Hana pungufu au zaidi ya hapo! Akikupa kitu , hata iwe ni utajiri wa mabilioni, ni kwa lengo moja tu; kukuangamiza! 
Mungu anasemaje kuhusu hii ‘sayansi ya kiafrika’?

Naamini umeshasikia mara nyingi watu wakisema, “Jisaidie na Mungu naye atakusaidia.” Siwezi kukataa lakini kama ni Mungu huyu ninayekuambia habari zake hapa, Yeye anasema kinyume kabisa cha hayo. Imeandikwa: Mtumaini BWANA kwa moyo wako wote, wala usizitegemee akili zako mwenyewe. Katika njia zako zote mkiri yeye, naye atayanyosha mapito yako. (Mithali 3:5-6).

Sasa watu wengi wanasema kuwa kwenda kwa waganga ni katika jitihada hizo za kujisaidia. Bwana wa majeshi anasema hivi: Msiwaendee wenye pepo, wala wachawi; msiwatafute, ili kutiwa unajisi na wao; Mimi ndimi BWANA, Mungu wenu. (Mambo ya Walawi 19:31)

Na anaonya kwa ukali kabisa kuwa: Na mtu yule atakayewaendea wenye pepo, na wachawi, ili kuzini pamoja nao, nitakaza uso wangu juu ya mtu yule, nitamtenga na watu wake.  (Mambo ya Walawi 20:6). Kuzini inaweza kumaanisha maana hii ya kawaida tunayoifahamu, lakini pia kibiblia, Mungu anaichukulia nchi kama mke. Nchi inapomwasi Bwana (yaani mume wake) na kwenda kwa miungu mingine, basi inakuwa inafanya uzinzi).

Pia Mungu anasema: Asionekane kwako mtu ampitishaye mwanawe au binti yake kati ya moto, wala asionekane mtu atazamaye bao, wala mtu atazamaye nyakati mbaya, wala mwenye kubashiri, wala msihiri, wala mtu alogaye kwa kupiga mafundo, wala mtu apandishaye pepo, wala mchawi, wala mtu awaombaye wafu. Kwa maana mtu atendaye hayo ni chukizo kwa BWANA. (Kumb 18:10-12). 

Cha kusikitisha ni kuwa kuna hata makanisa yanayowaomba wafu. [Bibilia inasema: Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa. (Hosea 4:6)]. Ndugu, usifanye tu mambo kwa kuwa tu kiongozi mkubwa wa dini amesema ufanye. Tambua kuwa andiko hapo juu halisemi "wanaangamia" kama wengi ambavyo husema; linasema "wanaangamizwa". Hakikisha kwanza mambo hayo kwenye Biblia ndipo uyafanye. Neno “sikujua” halitakuwa kamwe moja ya utetezi katika siku ya mwisho.

Mungu anatuasa kupitia nabii Isaya, akisema: Na wakati watakapokuambia, Tazama habari kwa watu wenye pepo na kwa wachawi; waliao kama ndege na kunong’ona; je! Haiwapasi watu kutafuta habari kwa Mungu wao? Je! Waende kwa watu waliokufa kwa ajili ya watu walio hai? (Isaya 8:19).

Alikuwapo mfalme wa Israeli ambaye aliitwa Manase. Mungu alikuwa na hasira naye kwa sababu ya mambo haya ya kuwaendea waganga. Imeandikwa: Tena akawapitisha wanawe motoni katika bonde la mwana wa Hinomu; akatazama bao, akabashiri, akafanya uganga, akajishughulisha na hao wenye pepo wa utambuzi, na wachawi; akafanya mabaya mengi machoni pa BWANA, hata kumkasirisha. (2 Mambo ya Nyakati 33:6). 

Unapoenda kwa mganga, anakuwa ananong’onanong’ona maneno usiyoweza hata kuyaelewa. Unadhani ni upuuzi tu? Hapana. Mwenzako anafanya mawasiliano kamili na mashetani walio katika ulimwengu wa roho.

Uhusiano kati ya ulimwengu wa mwili (yaani wa wanadamu) na ulimwengu wa kiroho ni uhusiano wa kimikataba na kimaagano. Yaani ili uwasiliane au upate kitu kutoka kwenye ulimwengu wa kiroho, ni lazima utimize sheria fulani. Sasa, mikataba hiyo hufungwa kwa njia ya sadaka/dhabihu. Na mara nyingi sadaka hizo huwa ni za damu.

Hatuwezi kuelewa kwa undani sana uzito wa damu katika ulimwengu wa roho, lakini ina nguvu sana. Kwa kifupi, damu ndiyo uhai. Maandiko yanasema: Kwa kuwa uhai wa mwili u katika hiyo damu. (Mambo ya Walawi 17:11). Unaweza kumpa mtu kila zawadi, lakini kama ukimpa uhai wako, nadhani hiyo itakuwa ni zawadi inayozidi zote.

Imeandikwa: Msile kitu chochote pamoja na damu yake. (Law 19:26). Sasa kama unapenda kisusio, ni bora ujitafakari upya.

Labda utasema, “Ah, haya si yalikuwa mambo ya agano la kale tu?” Baada ya Yesu kuondoka duniani, mitume wake waliwahi kukaa kikao mjini Yerusalemu kujadili mambo kadha wa kadha. Katika maamuzi waliyopitisha, wakasema tusiwabebeshe wale wasio Wayahudi sheria zitakazokuwa mzigo kwao, bali tuwaandikie kwamba wajiepushe na unajisi wa sanamu, na uasherati, na nyama zilizosongolewa, na damu. (Matendo ya Mitume 15:20). Kusongolewa ni kunyongwa, hivyo damu inagandia humohumo ndani ya mwili.

Zamani kabla Yesu hajaja na kufa, Wayahudi walilazimika kutoa sadaka kwa kuchinja wanyama ili kumwaga damu kwa ajili ya kusamehewa dhambi zao. Na sheria ya Mungu inasema hivi: Kisha mtu awaye yote wa nyumba ya Israeli; au miongoni mwa wageni wakaao kati yao, atakayekula damu, ya aina yoyote nitakunja uso wangu juu ya mtu huyo alaye damu, nami nitamkatilia mbali na watu wake. (Mambo ya Walawi 17:10).

Kwa nini anasema hivi? Ni kwa sababu: nami nimewapa ninyi hiyo damu juu ya madhabahu, ili kufanya upatanisho juu ya nafsi zenu; kwani ni hiyo damu ifanyayo upatanisho kwa sababu ya nafsi. (Mambo ya Walawi 17:11).

Kwa hiyo, unapopeleka damu kwa mganga wa kienyeji, iwe ni kupitia kuchanjwa chale, kutoa kuku, au mbuzi, au sadaka ya juu kabisa (mwanadamu), unaingizwa kwenye mikataba au maagano na mashetani, hata kama akilini mwako wewe hukusema hivyo na hujui. Unakuwa wa kwao! Kunakuwa na kupatana kati ya nafsi yako na shetani.
 
Simaanishi kuwa hutafanikiwa. La hasha! Utafanikiwa na utaona matokeo ambayo umeyatarajia.

Lakini Biblia inasema hivi: Na Shetani akimtoa Shetani, amefitinika juu ya nafsi yake; basi ufalme wake utasimamaje? (Mt 12:26). Waulize waganga wanaoweza kukuambia. Huwa hawatoi pepo. Anachofanya anakupa pepo kubwa zaidi ili kumtuliza yule mdogo. Lakini baada ya muda na hilo nalo linaanza kukuletea mateso; maana asili, wajibu na kazi yao ni uharibifu. Ulinzi si asili yao!

Kwa sasa hutajua maana au madhara yake. Lakini kama hukutangua mikataba uliyoingia na ufalme wa giza, mara tu utakapovuka ng’ambo ya maisha haya, yaani ukifa tu, palepale kila kitu kinakuwa wazi kabisa. Unadhani ni kwa nini baadhi ya watu huhangaika sana wakati wa kufa, ilihali wengine wanakufa kwa utulivu tu?

Wengi wao anakuwa ameshaona kule aendako, sasa anakuwa anajaribu kupambana ili asiende kule. Wale wa upande anakohusika wanakuwa tayari wameshafika pale kumchukua. Sasa kama ni wale wabaya, ndio mtu anaanza kujaribu kushindana. Kwenye ulimwengu wa roho kila kitu ni dhahiri kabisa.

Mungu hutuonya juu ya kila kitu cha hatari lakini kamwe huwa hatulazimishi kutii. Utii ni uamuzi wako binafsi. Anachofanya baada ya kuonya ni kukungoja mwisho wa safari. Huko ndipo kuna kutoa hesabu.

Kuhusiana na mtu aliyewatumainia waganga, pale mambo yatakapofika ukomo, BWANA  anamwambia: Simama sasa na uganga wako, na wingi wa uchawi wako, uliojitaabisha nao tangu ujana wako; labda utaweza kupata faida, labda utaweza kushinda. Umechoka kwa wingi wa mashauri yako; basi, na wasimame hao wajuao falaki, wazitazamao nyota, watabirio kila mwezi mambo ya mwezi huo, wakakuokoe na mambo yatakayokupata. Tazama, watakuwa kama mabua makavu; moto utawateketeza; hawatajiokoa na nguvu za mwali wa moto; hautakuwa kaa la kukota moto wa kukaa karibu nao. Ndivyo yatakavyokuwa mambo hayo uliyojitaabisha nayo; wale waliofanya biashara nawe tangu ujana wako watatanga-tanga mbali nawe, kila mtu akienda zake; hapatakuwa na mtu wa kukuokoa. (Isaya 47:12-15).

Watu wajuao falaki, wazitazamao nyota, watabirio kila mwezi mambo ya mwezi huo, kwa kifupi ni hawa tunaowaita wasoma nyota. Hao ni machukizo mbele za Mungu, na hataki kamwe tuwaendee. Je, nawe ni mmoja wa watu wanaosoma nyota kwenye magazeti kila mwezi au kila siku ili kuangalia “bahati” yako imekaaje? Huo ni mtego wa kutoka kuzimu. Jiepushe nao.

Sasa unafanyaje?

Yesu anaitwa Mwana-Kondoo wa Mungu kwa sababu alitolewa kafara kwa ajili ya dhambi za ulimwengu wote. Na kwa sababu torati inasema uhai umo kwenye hiyo damu; damu ya Yesu ndio uhai wake, yaani alitoa uhai wake.

Ukiingia ndani yake na kumwamini kama Mwokozi wako, unafunikwa na damu yake (uhai wake). Uhai huu ni moto mbele ya mashetani na wachawi.

Kwa hiyo, unakuwa ni mmojawapo wa wale wanaofaidi ulinzi wa kiungu ambao una nguvu dhidi ya ibilisi na majeshi yake, na wakala wake wa kibinadamu. Imeandikwa: Hakika hapana uchawi juu ya Yakobo, wala hapana uganga juu ya Israeli. (Hesabu 23:23).

Myahudi si tu yule wa Israeli, bali ni mtu yeyote ambaye Yesu ni Bwana na Mwokozi wake. Wanga wote waliowahi kucheza na watu wa aina hii, wanajua vizuri maana ya andiko hili.

Ndugu, Mungu si wa mchezo. Ni ngao kwelikweli. Hapa tena anasema: BWANA, mkombozi wako, yeye akliyekuumba tumboni, asema hivi; Mimi ni BWANA, nifanyaye vitu vyote; nizitandaye mbingu peke yangu; niienezaye nchi; ni nani aliye pamoja nami? Nizitanguaye ishara za waongo, na kuwatia waganga wazimu; niwarudishaye nyuma wenye hekima, na kuyageuza maarifa yao kuwa ujinga; nilithibitishaye neno la mtumishi wangu, na kuyafikiliza mashauri ya wajumbe wangu. (Isaya 44:24-26).

Karibu kwa Yesu. Acha kujifariji kwa dini. Je, unatambua kuwa Yesu hakuwa mkristo wala hakuleta ukristo? Yesu alikuja kuchukua dhambi za ulimwengu ili wanadamu wote wapone. Mambo ya dini yalianzishwa na wanadamu baadaye. Dini si mbaya, lakini si kitu cha msingi! Utakuwa na dini lakini bado wanga watakuwangia tu! Kuvaa hirizi na kuzindika kila kitu ni kumwekea shetani mteremko wa kushukia kwa ulaini maishani mwako!

Usalama uko kwa Yesu si kwenye dini; na zaidi sana, si kwenye hirizi na uongo wa waganga wa kienyeji!

6 comments:

  1. Uliosema ni ya kweli sana kiukweli nimejifunza vingi sana

    ReplyDelete
  2. Huwa nabarikiwa na kufarijika sana naamn mara nyingine nitakapoulizwa swali kama ilo "Nani kakwambia kwenda kwa mganga ni dhambi" nitakua na majibu na maandiko ya kutosha nitazima sauti za mawakala wa shetani kwakua na wenyewe wanaforce ukwel kuwa uongo

    Mungu akubariki mtumishi Wa Mungu

    ReplyDelete
  3. Huwa nabarikiwa na kufarijika sana naamn mara nyingine nitakapoulizwa swali kama ilo "Nani kakwambia kwenda kwa mganga ni dhambi" nitakua na majibu na maandiko ya kutosha nitazima sauti za mawakala wa shetani kwakua na wenyewe wanaforce ukwel kuwa uongo

    Mungu akubariki mtumishi Wa Mungu

    ReplyDelete
  4. Mungu akutie nguvu mtumishi wa mungu

    ReplyDelete