Wednesday, August 22, 2012

Waislamu Wanamgeukia Yesu





Video hii inamwonyesha mtu ambaye ni mzaliwa wa ukoo wa Abu Bakr Saddiq, ambaye alikuwa ni rafiki mkubwa wa Mtume Mohammad. Abu Bakr Saddiq pia ndiye aliyekuwa Khalifa wa kwanza kwenye ulimwengu wote wa kiislamu baada ya kifo cha Mtume Mohammad.

Mzaliwa huyu anaitwa Dk. Nasir Siddiki. Yeye pia ametokea kwenye familia tajiri. Akiwa na umri wa miaka 35 alikuwa tayari ni milionea, huku akimiliki kila kitu cha kupendeza ambacho unaweza kukifikiria – iwe ni magari ya kifahari, majumba, nk.

Lakini ilitokea kwamba akapata ugonjwa mbaya sana, ambao ulianza kama lengelenge sehemu ya shingoni. Alipofikishwa hospitalini (alikuwa Kanada), walisema ana ugonjwa wa mbaya kabisa wa aina fulani ya upele (shingles). Ilikuwa ni upande mmoja wa uso hadi kwenye bega.

Nasir anasema kuwa, alipolazwa, asubuhi iliyofuata, sikio lake la upande ulioathirika, lilivimba kama puto hadi likagusa bega!
Madaktari walimhudumia, lakini walifika mahali wakasema, haiwezekani; kwamba Nasir alikuwa ni wa kufa tu. Walisema kuwa mfumo wake wa kinga umeshasimama, haufanyi kazi tena; na tatizo linasambaa kote mwilini. Kwa hiyo wakasema kuwa, hadi asubuhi itakayofuata, angekuwa amekufa!
Madaktari walimweleza hayo mkewe na kusema kuwa, kama Nasir angeishi, basi angekuwa kipofu, kiziwi na mwenye matatizo ya akili!
Kwa vile alikuwa mwislamu, Nasir anasema, “Allah si mponyaji; wala Muhammad si mponyaji. Kwa hiyo, hatuwageukii hao tunapojikuta katika hali ya kutaka uponyaji.”
Nasir anaendelea kusema, “Nilikuwa na hofu ya kifo.”

“Kwa nini?” mtangazaji anamwuliza.

“Kwa kuwa sikujua nini kitanikuta baada ya kufa. Watu pekee niliokuwa nimewatumainia, ni wale madaktari. Sasa, nao walikuwa wameshanikatia tamaa!”

Nasir anaendelea kusema, “Kutokana na hofu, nilijikuta nikisema, ‘Mungu, kama upo nisaidie nisife.’ Allah hakuja; wala Mohammad hakuja,” anamalizia kusema Nasir.

“Lakini usiku ule,” anaendelea kusema Nasir, “alitokea mtu upande mmoja wa kitanda. Alikuwa anang’aa sana kiasi kwamba huwezi kuona uso wake. Mara moja nilijua kuwa huyo ni Yesu.”

[Maelezo ya blogger: Ukisoma Ufunuo 1:16, Mtume Yohana alipotokewa na Bwana Yesu anaandika kwamba: Naye alikuwa na nyota saba katika mkono wake wa kuume; na upanga mkali, wenye  makali kuwili, ukitoka katika kinywa chake; na uso wake kama jua liking'aa kwa nguvu zake.]

Nasir anasema kuwa mtu huyo alimwambia mambo mawili. Kwanza alimwambia, ‘Mimi ni Mungu wa Wakristo.’ Pili, alimwambia, ‘Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo.’

Nasir anaendelea kusema, “Kilichonishangaza zaidi ni kuwa, asubuhi iliyofuata, madaktari walewale walipokuja, wakasema, ‘Hatuelewi kinachoendelea. Huu ni muujiza. Badala ya ugonjwa kusambaa, unaanza kupungua!’”

Anasema, “Niliwaambia, sijui niwaambieje. Kulikuwa na mtu hapa. Yesu ameniponya. Hawakuniamini.”

Nasir alibaki anajiuliza, labda kama na wewe unavyojiuliza, “Huyu Yesu aliyenitokea kwenye kile chumba ni nabii kama Uislamu ulivyonifundisha maishani mwangu mwote au ni Mwana wa Mungu? Nilibaki nikijiuliza swali hilo.”

Siku iliyofuata Nasir aliruhusiwa kwenda nyumbani. Alipofika nyumbani, siku iliyofuata tena alijikuta akiamka mapema sana, kwenye saa 12 asubuhi, jambo ambalo hata yeye linamshangaza.

Cha ajabu ni kuwa alipowasha tu TV, alikumbana uso kwa uso na watu wawili ambao walikuwa wanaendesha kipindi kilichohusu jambo lile lile lililokuwa linamtatiza – yaani mjadala juu ya kama Yesu ni Mwana wa Mungu au la! 

[Hakika Bwana Yesu ni Mungu wa ajabu. Yeye hawahi wala hachelewi!]

“Nikiwa mwislamu,” anasema Nasri, “nilikuwa nimefundishwa kuwa, ili kwenda mbinguni, matendo mema ya mtu ni lazima yawe mengi kuliko matendo mabaya. Ni matendo yako tu ndiyo yanaweza kukupeleka peponi. Tofauti pekee iliyopo ni kwenye jihad. Yaani kama ukifa kwa ajili ya Mungu wako.” 

[Yaani ukifa kwenye jihad ndipo haijalishi kama matendo yako mema ni mengi au machache. Hata mabaya yakiwa mengi zaidi, basi wewe utaenda tu peponi kwa kuwa umefia kwenye jihad.]

“Kilichonishangaza sana,” Nasir anasema, “Hapa watu hawa wanasema, si suala la wewe  kufa kwa ajili ya Mungu wako; bali Mungu ndiye alikufa kwa ajili yako! Sikuwahi kukutana na upendo wa aina hiyo maishani mwangu! Nikasema, hivi hii ni kweli? ... Walipomaliza mjadala wao nilipiga magoti. Waliniongoza kuomba sala. Nikamkaribisha Yesu kuwa Bwana wa maisha yangu.”

Baada ya hapo, Nasir anasema alitafuta picha inayoonyesha jinsi alivyokuwa kabla ya kuugua (maana makovu bado yalikuwapo). Akaanza kumwomba Bwana Yesu akisema, “Je, unaweza kunifanya niwe na sura kama hii niliyokuwa nayo mwanzo?”

“Siku tano baadaye,” anasema Nasir, “Niliamka na kukuta magamba kitandani kwangu. Madaktari waliniambia nisijikune na walinionya nisiguse sehemu iliyoathirika, maana ugonjwa huo unaambukiza. Baada ya hapo niliingia bafuni na kuoga kwa karibu saa moja na nusu. Magamba yote yalianguka chini na kwisha kabisa!! Madaktari waliniambia kuwa nikipona nitabakia na makovu. Lakini kama unavyoniona, sina hata kovu moja!”

Mtangazaji anamwuliza, “Je, hivi sasa kuna shaka yoyote akilini mwako kwamba Mungu ni Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo; na kwamba Yesu ni Mwana wake?”

“Hakuna hata kidogo!” anajibu Nasir.
---------------

Je, wewe ni Mwislamu na umefundishwa kwamba Yesu SI Mungu na kwamba SI Mwana wa Mungu – kwa kuwa Mungu hazai? 
Katika mambo mawili yanayopingana kabisa, haiwezekani kamwe kila upande ukawa sahihi!

Ukristo unasema kuwa Yesu NI Mwana wa Mungu kabisa! Uislamu unasema Yesu SI Mwana wa Mungu kamwe! 

HAIWEZEKANI KAMWE pande hizi mbili zikawa zote sahihi katika jambo hili. Ama Ukristo uko sahihi au Uislamu uko sahihi. Basi!
Tazama kazi za Bwana Yesu ambazo zinamshuhudia usiku na mchana, nawe utajua ukweli ni nini.

Yesu akawajibu, Naliwaambia, lakini ninyi hamsadiki. Kazi hizi ninazozifanya kwa jina la Baba yangu ndizo zinazonishuhudia. (Yohana 10:25).

Kama mtu akikwambia, “Ukitumia jina langu utapona” halafu wewe ukaja kulitumia jina lake na ukapona, je, utatilia shaka mambo mengine ambayo nayo alikuambia?

Na tena Bwana Yesu alipokuwa anajiandaa kuondoka duniani kurudi mbinguni alisema hivi: Amin, amin, nawaambieni, Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba.  (Yohana 14:12).
 
Bwana Yesu anajithibitisha mwenyewe usiku na mchana kila mahali watumishi wake wanapoliitia jina lake. 

Nasir anasema kuwa alikuwa anahofia kufa kwa sababu alikuwa ana wasiwasi na kule ambako angeenda baada ya hapo. Vipi kuhusu wewe msomaji?

Bwana Yesu alisema: Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi. Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali. Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi muwepo. Nami niendako mwaijua njia. (John 14:1-4).

Lakini kwa wewe ndugu yangu Mwislamu, naomba unisaidie katika hili, ili yamkini na mimi niweze kuwa Mwislamu kama wewe na kuirithi pepo.

Allah anamwambia Mohammad aseme hivi katika sura Al-Ahqaf 46:9:

....nor do I know what will be done with me or you. I follow only what is revealed to me.

Yaani,

.... na wala mimi sifahamu kile nitakachotendewa wala kile ninyi mtakachotendewa. Mimi nafuata tu kile ninachofunuliwa.

Sasa je, ni salama kweli kumfuata mtu ambaye hajui mbele yake kuna nini? Wewe ni mjuzi zaidi katika hayo, unaweza kunielewesha. Lakini mimi nakukaribisha kwa Yesu Kristo Mwokozi wa wanadamu wote. 

Bwana Yesu anasema wazi: Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.  (Yohana 14:6). Fanya uamuzi sasa!

Na kwa wewe ndugu yangu Mkristo ambaye unasema hakuna kuokoka duniani, sikia maneno ya Bwana wa Majeshi:

Amin nawaambia, watoza ushuru na makahaba wanatangulia mbele yenu kuingia katika ufalme wa Mungu. Kwa sababu Yohana alikuja kwenu kwa njia ya haki, ninyi msimwamini; lakini watoza ushuru na makahaba walimwamini, nanyi hata mlipoona, hamkutubu baadaye, ili kumwamini. (Mt. 21:31-32).

Anachomaanisha Bwana hapa ni kuwa, kuwa na dini yenye jina zuri si jambo la maana kama mtu hana Yesu mwenyewe ndani yake. Maana hapa alikuwa anaongewa na makuhani wakuu na wazee wa watu – kundi ambalo ndilo lilikuwa la washika dini hasa. Sisi kama Wakristo, tusiridhike tu na kuwa na dini ya Kikristo. Swali kuu ni lazima liwe, “Je, ninaye Kristo mwenyewe?”

Bila kuwa na Kristo kama Bwana na Mwokozi maishani mwetu, maneno hayo ya Bwana katika Mt. 21:31-32 hapo juu, yatatimia kwetu vilevile kama alivyosema.

Maneno ya Bwana yanatisha kama nini. Lakini ndio ukweli wenyewe. Anasema tena:

Nami nawaambieni, ya kwamba wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi pamoja na Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo katika ufalme wa mbinguni; bali wana wa ufalme watatupwa katika giza la nje, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. (Mt. 8:11-12).

Fanya uamuzi sasa kama alivyofanya Nasir – wa kumpokea Yesu Kristo awe Bwana na Mwokozi wa maisha yako. Usikubali kuachwa ilihali wewe hukuwa na tatizo na Yesu kuwa Mungu na kuwa Mwana wa Mungu!

Mimi sikuambii uachane na dhehebu lako. Ninachokuambia tu ni kwamba mwongezee Yesu ndani ya moyo wako, kisha mfanye kuwa namba moja na dhehebu lako liwe namba mbili; na si kinyume chake! Jenga uhusiano na Yesu kama mtu ambaye yuko na wewe saa ishirini na nne – maana hivyo ndivyo ilivyo.

Unapoona mtu anajiita Mkristo lakini ni mgomvi, mwizi, mwongo, mzinzi, nk, maana yake ni moja tu – Yesu hayumo moyoni mwake. Anaishi kana kwamba Yesu yuko maili milioni kadhaa kule mbinguni. Anaowaogopa ni wanadamu lakini si Yesu.

Lakini ukiwa kweli na Yesu moyoni, huyo ndiye utamwogopa, maana unajua kwamba kila sekunde yuko nawe; na anaangalia na kupima maneno, matendo na hata mawazo yako!! Naamini hapa sasa unaelewa tofauti kati ya kuwa na dini na kuwa na Yesu.

Bwana Yesu akubariki.






No comments:

Post a Comment