Taa ya mwili ni jicho; basi jicho lako likiwa safi, mwili wako wote unao
mwanga; lakini likiwa bovu, mwili wako nao una giza. Angalia basi, mwanga ulio
ndani yako usije ukawa giza.
Basi kama mwanga umeenea katika mwili wako wote, wala hauna sehemu iliyo na
giza, mwili wako wote utakuwa na mwanga mtupu; kama vile taa ikumulikiapo kwa
mwanga wake. (Luka 11:34-36).
Kati ya mambo ambayo adui yetu shetani anajaribu
sana kuyafanya ni kuiba muda ambao tunatakiwa kuwa na Bwana – iwe ni katika
kumwomba, kutafakari, kusoma Biblia, kusikiliza ibada, n.k. Adui anajua kuwa,
kama akiweza kutufanya tutumie muda mwingi kwa ajili ya mambo mengine badala ya
Bwana Yesu, basi mwisho wa safari atakuwa ametunasa, maana Biblia inasema wazi:
Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho
atakachovuna. Maana yeye apandaye kwa mwili wake, katika mwili wake atavuna
uharibifu; bali yeye apandaye kwa Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele.
(Wagalatia 6:7-8).
Ili aweze kuiba muda huo, anajaza mambo mengi
ndani ya fahamu zetu ili kwamba kila wakati tuwe tunayawaza hayo. Na njia
muhimu kabisa ya kuyajaza ni kupitia kuona. Mambo mengi unayowaza muda wote ni
kwa sababu uliona, ukahifadhi akilini, na sasa hata unapojitahidi kuyafuta,
hayafutiki. Inakuwa ni vita kubwa inayoendelea ndani ya moyo.
Na kitu chochote ambacho kinatufanya tuwaze mambo
mengine zaidi ya kumuwaza Kristo, ni ishara kuwa kuna giza tayari ndani yetu. Kama
mimi ni mtu wa kumuwaza Kristo inapofika tu jumapili, hii ni ishara ya wazi
kuwa kuna giza ndani yangu; na jicho langu limekuwa bovu. Hii ni kwa sababu,
katika moyo wangu, simuoni kabisa Kristo bali ninachoona ni yale tu yaujazayo
moyo wangu – kwa mfano fedha, starehe, n.k.
Kristo ni kila kitu! Tunatakiwa kumuwaza yeye kila
dakika. Chochote tunachofanya, kinatakiwa kwanza tukipime kwa viwango na vigezo
vya Mwokozi wetu. Ni lazima kujiuliza, “Jambo hili ninalowaza/ ninalotaka kusema/ninalotaka
kutenda, je, Bwana analikubali?”
Mara moja Roho Mtakatifu atasema nasi kupitia
dhamiri zetu. Mtu atajua mara moja kama anatakiwa kulifanya au kuliacha.
Lakini kama umeshamzimisha Roho kiasi kwamba hata
dhamiri yako haiukusuti tena, hapo ndipo unaweza usimuwaze Kristo kabisa –
maana ndani kunakuwa kuna hilo giza.
Katika Mathayo 15:11, Bwana anasema: Sicho kiingiacho
kinywani kimtiacho mtu unajisi; bali kitokacho kinywani ndicho kimtiacho mtu
unajisi. Lakini hapa alikuwa anazungumzia kuhusu vyakula; yaani mioyo
yetu hainajisiki kutokana na vyakula tunavyokula, maana hivyo huenda tumboni na
si moyoni.
Lakini kwa habari ya macho (au milango ya fahamu
kwa ujumla), yako mambo mengi sana ambayo yamwingiapo
mtu, humtia unajisi kabisa.
Bwana anaposema kuwa kile kimtokacho mtu ndicho
kimtiacho unajisi, analenga kuzungumzia juu ya mawazo mabaya, kama vile uuaji,
hasira, wivu, uchungu, tamaa mbaya, n.k.
Sasa haya mawazo mabaya, kabla ya kuanza kumtoka
mtu ndani, yanakuwa yamefikaje humo ndani?
Jibu ni huo mstari katika Luka 11 ambao tumeanza
nao hapo juu, yaani jicho linakuwa limefungua mlango nayo yakaingia.
Katika maisha yetu ya leo tumezungukwa na mambo
mengi sana ya kunajisi. Kwa mfano filamu. Ziko filamu nyingi sana ambazo wengi
tunadhani kuwa ni sehemu tu ya burudani. Lakini ukweli ni kuwa, ndani yake adui
amewekeza mitego na mambo mengi sana ambayo anajua kuwa, bila hata wewe kujua,
unapokuwa unayaangalia, kuna vitu vikubwa vinavyoingia na kufanya makao kwenye
ufahamu wako. Baadaye akili yako inakuwa inawaza vitu hivyo ‘automatically’
hata kama wewe mwenyewe hukusudii kufanya hivyo.
Naamini umeshajikuta katika hali ambayo ukitulia
tu, akilini mwako unakuja labda wimbo fulani kutoka kwenye tangazo la biashara;
au mawazo juu ya jambo fulani ambalo uliliona. Hata kama utajitahidi kuyafuta
na kuyasukumia nyuma ya akili zako, utakuta yanatokeza tena na tena. Ni kwa
sababu uliona (au ulisikia), na mambo hayo pamoja na ubaya wake yakaingia ndani
ya moyo na kubaki humo.
Sasa hebu fikiria mtu ambaye hata kanisani huwa
haendi, au anaenda kwa saa moja tu siku ya jumapili! Je, ndani yake kunakuwaje?
Nani atakuwa na nguvu ya kiutawala ndani yake? Je, ni Mungu au ni adui?
Mambo mengine ambayo adui hutumia kuchafua jicho
letu ni magazeti ya udaku. Haya huandika habari na kuonyesha picha ambazo,
kimsingi ni mradi wake adui. Ukiuliza wachapishaji, watakwambia kuwa wao
wanaandika ili kuelimisha jamii. Haya ni maneno mazuri yanayoonekana kama ya
kweli – lakini hayana ukweli wowote! Kama ingekuwa ni kweli, mbona hawaandiki
masomo ya Biblia wakati kila mtu anajua kuwa Biblia inaelimisha jamii?
Mambo mengine, kama vile picha za ngono, hayo
hayana utata. Yanaeleweka wazi kuwa hayafai. Lakini watu hutazama na, matokeo
yake, jicho pamoja na mwili wao unatiwa giza.
Nikakumbuka wakati fulani ambapo mimi pia
nilikuwa nikisema, “Muziki wa kidunia una mashauri na maonyo mazuri tu. Hata unapoyachunguza
utakuta mengi yanaendana na mafundisho ya Biblia.”
Huo ni uongo wa adui! Ukiwa na chakula safi
kilichojaa kwenye chombo safi, halafu kikawa kimechanganywa na kijiko kimoja tu
cha uchafu, huwezi kusema kuwa chakula hicho ni safi kwa vile uchafu ni
asilimia moja tu. Hapana! Chakula hicho chote sasa ni kichafu!
Ndivyo ilivyo kwa muziki wa kidunia. Hata kama
una maneno fulani fulani mazuri, lakini roho iliyo nyuma yake ni mbaya. Ukishaingia
ndani yako, unachafua mwili wote kama anavyosema Bwana kwenye Luka 11 hapo juu.
Ukweli kabisa, kinachotusukuma kuusikiliza si kutafuta mafunzo, bali ni
kutimiza tu tamaa za mwili. Mwili una tamaa za aina nyingi – za chakula, za
burudani kama muziki, za uzinzi, n.k.
Tunatakiwa kufanya nini sasa?
Kazi kubwa tuliyo nayo ni kuchunga sana mawazo
yetu tuyawazayo. Haya yatatuonyesha ni kitu gani tumekuwa tukiangalia au
kusikiliza. Hivyo, tutaweza kuamua kujiepusha na mambo hayo kadiri
iwezekanavyo.
Na kwa sababu mambo yenyewe yametuzunguka kila
kona, kikubwa ni kuzidi sana kumwomba Roho Mtakatifu atupe uwezo wa kuyashinda;
atupe uwezo wa kumtafakari Kristo zaidi kuliko kutafakari mambo maovu ambayo,
si tu yanachafua roho zetu, bali pia na miili yetu.
Imeandikwa:
Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya
staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo
yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote,
yatafakarini hayo. (Wafilipi 4:8).
Na hatuwezi kuyapata mambo haya kokote kule
isipokuwa kwenye Neno la Mungu, yaani Biblia.
Ndugu yangu, si jambo rahisi kushinda mambo yanayotupinga
hata kidogo! Nguvu inayotuvuta kuyapenda ni kubwa mno kuliko uwezo wetu wa
kibinadamu!
Tunashindana na mapandikizi ya mashetani ambayo
yana uzoefu wa miaka mingi katika uovu na hila. Wao kazi yao ni hiyo hiyo tu
usiku na mchana – kuhakikisha kuwa unabakia gizani hadi siku ya mwisho!
Unapowaza kuyaacha mambo haya yanayotuvuta,
utasema tu, “Sitaweza kukaa bila kusikiliza muziki wa kidunia; sitaweza kukaa
bila kusoma magazeti ya udaku; sitaweza kukaa bila kutazama picha za ngono;
sitaweza kukaa bila kutazama filamu za vita na mapigano, n.k.”
Ni kweli kabisa. Hatuwezi! Lakini suala si kuacha
kwa sababu ya uwezo wetu. Suala ni kukubali kunyenyekea chini ya Bwana Yesu na
kumwambia, “Bwana, nataka kukutii wewe. Kwa nguvu zangu siwezi kushinda giza
hili lililomo ndani yangu. Naomba unisaidie.”
Bwana ni mwaminifu mno, mno! Utajikuta tu, bila
unafiki wowote, yale mambo ya kidunia uliyokuwa unayapenda na yalikuwa yakiiba
muda wako kila siku, yanapoteza ladha kabisa. Utaona kwamba kusikiliza muziki
wa kidunia ambao ulikuwa unaupenda sana, sasa inakuwa ni kama kula uchafu. Ili kufikia
hatua hiyo, hii si kazi ya mwanadamu hata kidogo. Ni Roho Mtakatifu mwenyewe
ndiye anayeweza kutufikisha hapo. Lakini usiponyenyekea na kumwambia, utabakia
gizani huku ukidhani kuwa ‘haiwezekani’
kushinda – kumbe mawazo hayo nayo ni
uongo na giza la adui.
Nimalizie kwa kusema tena maneno ya Bwana wetu Yesu anayotushauri sisi katika Luka 11 hapo juu: Angalia basi, mwanga wako ulio ndani yako usije ukawa giza.
Amena,nimebarikiwa na somo hili,nami ntajitaidi niwafunze wengine.
ReplyDeleteAmen Yusufu. Songa mbele na Bwana
DeleteAisee ndug yangu asante sana hili somo notalisambaza kadri niwezavyoo
ReplyDeleteKwa msaada wa mungu