Tuesday, August 28, 2012

Jicho lako likiwa bovu



Bwana wetu Yesu alisema kwamba:
Taa ya mwili ni jicho; basi jicho lako likiwa safi, mwili wako wote unao mwanga; lakini likiwa bovu, mwili wako nao una giza. Angalia basi, mwanga ulio ndani yako usije ukawa giza.

Basi kama mwanga umeenea katika mwili wako wote, wala hauna sehemu iliyo na giza, mwili wako wote utakuwa na mwanga mtupu; kama vile taa ikumulikiapo kwa mwanga wake. (Luka 11:34-36).
Kati ya mambo ambayo adui yetu shetani anajaribu sana kuyafanya ni kuiba muda ambao tunatakiwa kuwa na Bwana – iwe ni katika kumwomba, kutafakari, kusoma Biblia, kusikiliza ibada, n.k. Adui anajua kuwa, kama akiweza kutufanya tutumie muda mwingi kwa ajili ya mambo mengine badala ya Bwana Yesu, basi mwisho wa safari atakuwa ametunasa, maana Biblia inasema wazi:

Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna. Maana yeye apandaye kwa mwili wake, katika mwili wake atavuna uharibifu; bali yeye apandaye kwa Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele. (Wagalatia 6:7-8).

Ili aweze kuiba muda huo, anajaza mambo mengi ndani ya fahamu zetu ili kwamba kila wakati tuwe tunayawaza hayo. Na njia muhimu kabisa ya kuyajaza ni kupitia kuona. Mambo mengi unayowaza muda wote ni kwa sababu uliona, ukahifadhi akilini, na sasa hata unapojitahidi kuyafuta, hayafutiki. Inakuwa ni vita kubwa inayoendelea ndani ya moyo.

Na kitu chochote ambacho kinatufanya tuwaze mambo mengine zaidi ya kumuwaza Kristo, ni ishara kuwa kuna giza tayari ndani yetu. Kama mimi ni mtu wa kumuwaza Kristo inapofika tu jumapili, hii ni ishara ya wazi kuwa kuna giza ndani yangu; na jicho langu limekuwa bovu. Hii ni kwa sababu, katika moyo wangu, simuoni kabisa Kristo bali ninachoona ni yale tu yaujazayo moyo wangu – kwa mfano fedha, starehe, n.k.

Kristo ni kila kitu! Tunatakiwa kumuwaza yeye kila dakika. Chochote tunachofanya, kinatakiwa kwanza tukipime kwa viwango na vigezo vya Mwokozi wetu. Ni lazima kujiuliza, “Jambo hili ninalowaza/ ninalotaka kusema/ninalotaka kutenda, je,  Bwana analikubali?”

Mara moja Roho Mtakatifu atasema nasi kupitia dhamiri zetu. Mtu atajua mara moja kama anatakiwa kulifanya au kuliacha. 

Lakini kama umeshamzimisha Roho kiasi kwamba hata dhamiri yako haiukusuti tena, hapo ndipo unaweza usimuwaze Kristo kabisa – maana ndani kunakuwa kuna hilo giza.

Katika Mathayo 15:11, Bwana anasema: Sicho kiingiacho kinywani kimtiacho mtu unajisi; bali kitokacho kinywani ndicho kimtiacho mtu unajisi. Lakini hapa alikuwa anazungumzia kuhusu vyakula; yaani mioyo yetu hainajisiki kutokana na vyakula tunavyokula, maana hivyo huenda tumboni na si moyoni.

Lakini kwa habari ya macho (au milango ya fahamu kwa ujumla), yako mambo mengi sana ambayo yamwingiapo mtu, humtia unajisi kabisa.

Bwana anaposema kuwa kile kimtokacho mtu ndicho kimtiacho unajisi, analenga kuzungumzia juu ya mawazo mabaya, kama vile uuaji, hasira, wivu, uchungu, tamaa mbaya, n.k.
Sasa haya mawazo mabaya, kabla ya kuanza kumtoka mtu ndani, yanakuwa yamefikaje humo ndani?

Jibu ni huo mstari katika Luka 11 ambao tumeanza nao hapo juu, yaani jicho linakuwa limefungua mlango nayo yakaingia.

Katika maisha yetu ya leo tumezungukwa na mambo mengi sana ya kunajisi. Kwa mfano filamu. Ziko filamu nyingi sana ambazo wengi tunadhani kuwa ni sehemu tu ya burudani. Lakini ukweli ni kuwa, ndani yake adui amewekeza mitego na mambo mengi sana ambayo anajua kuwa, bila hata wewe kujua, unapokuwa unayaangalia, kuna vitu vikubwa vinavyoingia na kufanya makao kwenye ufahamu wako. Baadaye akili yako inakuwa inawaza vitu hivyo ‘automatically’ hata kama wewe mwenyewe hukusudii kufanya hivyo. 

Naamini umeshajikuta katika hali ambayo ukitulia tu, akilini mwako unakuja labda wimbo fulani kutoka kwenye tangazo la biashara; au mawazo juu ya jambo fulani ambalo uliliona. Hata kama utajitahidi kuyafuta na kuyasukumia nyuma ya akili zako, utakuta yanatokeza tena na tena. Ni kwa sababu uliona (au ulisikia), na mambo hayo pamoja na ubaya wake yakaingia ndani ya moyo na kubaki humo.
Sasa hebu fikiria mtu ambaye hata kanisani huwa haendi, au anaenda kwa saa moja tu siku ya jumapili! Je, ndani yake kunakuwaje? Nani atakuwa na nguvu ya kiutawala ndani yake? Je, ni Mungu au ni adui?

Mambo mengine ambayo adui hutumia kuchafua jicho letu ni magazeti ya udaku. Haya huandika habari na kuonyesha picha ambazo, kimsingi ni mradi wake adui. Ukiuliza wachapishaji, watakwambia kuwa wao wanaandika ili kuelimisha jamii. Haya ni maneno mazuri yanayoonekana kama ya kweli – lakini hayana ukweli wowote! Kama ingekuwa ni kweli, mbona hawaandiki masomo ya Biblia wakati kila mtu anajua kuwa Biblia inaelimisha jamii?

Mambo mengine, kama vile picha za ngono, hayo hayana utata. Yanaeleweka wazi kuwa hayafai. Lakini watu hutazama na, matokeo yake, jicho pamoja na mwili wao unatiwa giza.
 
Nikakumbuka wakati fulani ambapo mimi pia nilikuwa nikisema, “Muziki wa kidunia una mashauri na maonyo mazuri tu. Hata unapoyachunguza utakuta mengi yanaendana na mafundisho ya Biblia.”

Huo ni uongo wa adui! Ukiwa na chakula safi kilichojaa kwenye chombo safi, halafu kikawa kimechanganywa na kijiko kimoja tu cha uchafu, huwezi kusema kuwa chakula hicho ni safi kwa vile uchafu ni asilimia moja tu. Hapana! Chakula hicho chote sasa ni kichafu! 

Ndivyo ilivyo kwa muziki wa kidunia. Hata kama una maneno fulani fulani mazuri, lakini roho iliyo nyuma yake ni mbaya. Ukishaingia ndani yako, unachafua mwili wote kama anavyosema Bwana kwenye Luka 11 hapo juu. Ukweli kabisa, kinachotusukuma kuusikiliza si kutafuta mafunzo, bali ni kutimiza tu tamaa za mwili. Mwili una tamaa za aina nyingi – za chakula, za burudani kama muziki, za uzinzi, n.k.

Tunatakiwa kufanya nini sasa?

Kazi kubwa tuliyo nayo ni kuchunga sana mawazo yetu tuyawazayo. Haya yatatuonyesha ni kitu gani tumekuwa tukiangalia au kusikiliza. Hivyo, tutaweza kuamua kujiepusha na mambo hayo kadiri iwezekanavyo.

Na kwa sababu mambo yenyewe yametuzunguka kila kona, kikubwa ni kuzidi sana kumwomba Roho Mtakatifu atupe uwezo wa kuyashinda; atupe uwezo wa kumtafakari Kristo zaidi kuliko kutafakari mambo maovu ambayo, si tu yanachafua roho zetu, bali pia na miili yetu.

Imeandikwa:
Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakarini hayo. (Wafilipi 4:8).
Na hatuwezi kuyapata mambo haya kokote kule isipokuwa kwenye Neno la Mungu, yaani Biblia.

Ndugu yangu, si jambo rahisi kushinda mambo yanayotupinga hata kidogo! Nguvu inayotuvuta kuyapenda ni kubwa mno kuliko uwezo wetu wa kibinadamu!

Tunashindana na mapandikizi ya mashetani ambayo yana uzoefu wa miaka mingi katika uovu na hila. Wao kazi yao ni hiyo hiyo tu usiku na mchana – kuhakikisha kuwa unabakia gizani hadi siku ya mwisho! 

Unapowaza kuyaacha mambo haya yanayotuvuta, utasema tu, “Sitaweza kukaa bila kusikiliza muziki wa kidunia; sitaweza kukaa bila kusoma magazeti ya udaku; sitaweza kukaa bila kutazama picha za ngono; sitaweza kukaa bila kutazama filamu za vita na mapigano, n.k.”

Ni kweli kabisa. Hatuwezi! Lakini suala si kuacha kwa sababu ya uwezo wetu. Suala ni kukubali kunyenyekea chini ya Bwana Yesu na kumwambia, “Bwana, nataka kukutii wewe. Kwa nguvu zangu siwezi kushinda giza hili lililomo ndani yangu. Naomba unisaidie.”
Bwana ni mwaminifu mno, mno! Utajikuta tu, bila unafiki wowote, yale mambo ya kidunia uliyokuwa unayapenda na yalikuwa yakiiba muda wako kila siku, yanapoteza ladha kabisa. Utaona kwamba kusikiliza muziki wa kidunia ambao ulikuwa unaupenda sana, sasa inakuwa ni kama kula uchafu. Ili kufikia hatua hiyo, hii si kazi ya mwanadamu hata kidogo. Ni Roho Mtakatifu mwenyewe ndiye anayeweza kutufikisha hapo. Lakini usiponyenyekea na kumwambia, utabakia gizani huku ukidhani kuwa ‘haiwezekani’
kushinda – kumbe mawazo hayo nayo ni uongo na giza la adui.

Nimalizie kwa kusema tena maneno ya Bwana wetu Yesu anayotushauri sisi katika Luka 11 hapo juu: Angalia basi, mwanga wako ulio ndani yako usije ukawa giza.

3 comments:

  1. Amena,nimebarikiwa na somo hili,nami ntajitaidi niwafunze wengine.

    ReplyDelete
  2. Aisee ndug yangu asante sana hili somo notalisambaza kadri niwezavyoo
    Kwa msaada wa mungu

    ReplyDelete