Thursday, April 17, 2014

Niliokolewa Toka Kwenye Nguvu za Giza - Sehemu ya 4



Sura ya 3: Utawala mwovu


Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele. (Yohana 10:10) 


Baada ya kurudi Lagos, niliendelea na biashara; na baada ya wiki mbili nilirudi tena baharini. Malkia wa Pwani alinipatia kile aambacho alikiita ni “kazi ya kwanza”. Nilitakiwa kwenda kwenye kijiji changu na kumwua mjomba wangu, ambaye alikuwa ni mganga maarufu wa kienyeji, na ambaye huyu malkia  aliniambia kuwa ndiye aliyehusika kuwaua wazazi wangu.


Nilitii na kwenda lakini kwa kuwa nilikuwa sijawahi kuua kabla, sikupata ujasiri wa kumuua. Badala yake niliharibu dawa zake na kumfanya asiwe na nguvu kabisa. Matokeo yake, alipoteza wateja wake wote hadi hivi leo. Nilirudi kutoa ripoti ya kazi niliyopewa lakini yule malkia alinighadhibikia sana. Alisema kuwa adhabu ya kutotii maagizo yake ni kifo, lakini kwa kuwa alikuwa akinipenda, basi angenituma tena kwenye kijiji kilekile kuua wazee wawili ambao alisema kuwa walitoa msaada katika kuuawa kwa wazazi wangu. Sijui kama hii ilikuwa ni adhabu kwa kule kutotii maagizo yake au la.  

Hata hivyo, nilitii na kwenda kwenye kile kijiji na nikawaua wale wazee na kupeleka damu yao kwake. Kutokana na kifo cha kutatanisha cha wale wazee, wazee wengine pale kijijini walienda kuuliza kwa mganga mwingine mwenye nguvu ambaye kawaida yake huwa anatuma radi kwenda kupeleleza aliyefanya mauaji. Bahati mbaya kwa wazee hawa, nilikutana na yule mganga kwenye ulimwengu wa roho na nikamwonya asiseme kitu kama anayapenda maisha yake. Alirudi kwenye ulimwengu wa mwili na kuwaambia wale wazee warudi nyumbani na kumwomba msamaha mmoja wa watoto wao waliyekuwa wamemkosea, na hakutaja jina langu.

Radi aliyokuwa ameituma ilirudi na kuua mmoja wa wale wazee na kuwajeruhi wengine. Baada ya tukio hili la kwanza, nguvu zilizokuwa ndani yangu zilianza kujidhihirisha. Ningeweza hata kumtia ulemavu msichana ambaye alikataa kuwa na urafiki na mimi, n.k.

Mkutano wangu na shetani

Baadaye nilirudi tena Lagos. Siku moja msichana mmoja aliyeitwa NINA alikuja kwangu. NINA ambaye wazazi wake walitokea jimbo la Anambra alikuwa ni msichana mrembo sana lakini aliishi zaidi baharini, yaani kwenye ulimwengu wa chini ya maji wa mapepo. Alikuwa ni wakala mkubwa wa Malkia wa Pwani; na alikuwa mtu mwovu sana. Aliwachukia sana sana Wakristo na alifanya kila aliwezalo ili kupambana na Ukristo. Nilikutana naye nilipoenda kutembelea baharini mara ya kwanza. Alikuja akiwa ametumwa na Malkia wa Pwani.  

Tuliondoka mara moja na tulipofika kule ndipo nikajua kuwa ningekuwa na mkutano na Lusifa. Katika mkutano ule, shetani alitupa maelekezo yafuatayo: kupambana na wanaoamini na sio wale wasioamini, maana wasioamini tayari  ni wa kwake. Aliposema hivi, mmoja wetu akauliza, “Kwa nini?” Akasema ni kwa sababu Mungu alimfukuza kwenye ‘ile sehemu.’ (Hakutaka kutaja neno ‘Mbinguni’; na kwenye mkutano huo wetu wote pamoja naye, hakutaja kamwe neno ‘Mbinguni’. Badala yake alisema tu ‘sehemu ile’) kwa sababu ya kiburi na matokeo yake hataki Mkristo yeyote afike kule (Mbinguni).

Alituambia kuwa tusipambane na wanafiki. “Hao wako kama mimi,” alisema. Aliendelea kuzungumza na kusema, “Tunatakiwa kupambana na Wakristo wa kweli tu.” Pia akasema kuwa muda wake u karibu, hivyo, tupambane kuliko tulivyowahi kufanya na kuhakikisha kuwa hakuna anayeingia kwenye ‘sehemu ile’. Kwa hiyo, mmoja wetu akamwambia, “Tulisikia kuwa Mungu alituma mtu fulani kwenda kuwakomboa wanadamu warudi kwake.” Shetani akauliza, “Ni nani huyo?” Mmoja kati yetu akasema, “Yesu,” na kwa mshangao wetu mkubwa, Lusifa alianguka chini toka kwenye kiti chake!  Akapaza sauti kumwonya yule aliyesema hivyo asije akarudia tena kutaja jina hilo kwenye mikutano yetu kama anayapenda maisha yake.  Ni kweli kwamba kwenye Jina la Yesu lazima kila goti litapigwa (Fil 2: 10), hata la Shetani mwenyewe.

Baada ya tukio hili, alitutia moyo na kutuambia tusiwajali “hawa Wakristo”, maana yeye, Lusifa, atakuja duniani muda si mrefu kutawala na atatupa sisi maajenti wake nafasi nzuri ili kwamba tusije kuteseka pamoja na dunia iliyobakia; na atatufanya sisi kuwa watawala. Aliendelea kusema kuwa, kwa vile wanadamu wanapenda sana vitu vya kuvutia na kumetameta, ataendelea kutengeneza vitu hivyo na kuhakikisha kuwa mwanadamu hapati muda wa kuwa na Mungu wake; na kwamba atatumia mambo yafuatyo kuliharibu Kanisa:

                                  1. Fedha,
                                  2. Mali,
                                  3. Wanawake.


Baada ya hotuba yake, aliahirisha mkutano. Hii ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kukutana na shetani. Mikutano mingine mingi ilifuata baada ya huu. Tulipokuwa tunaondoka, Malkia wa Pwani, ambaye sasa anaonekana katika maumbo tofauti, alinikaribisha kwenye jumba lake. Aliingiza majivu ya wanadamu pamoja na vitu vingine ndani ya mifupa ya miguu yangu yote; jiwe kwenye kidole changu (si jiwe la kawaida); na kitu kingine ndani ya mfupa wa mkono wangu wa kulia.

Kila moja ya vitu hivi kilikuwa na kazi yake. Jiwe kwenye kidole changu lilikuwa na kazi ya kujua mawazo ya mtu yeyote yaliyo kinyume nami. Na kwenye mkono wangu wa kulia, ni kunipa nguvu ya kufanya uharibifu; na kwenye miguu ni kunifanya kuwa sugu na kuwa mtu wa hatari zaidi; na pia kuniwezesha kujigeuza kuwa mwanamke, mnyama, ndege, paka, n.k. Alinipeleka kwenye mojawapo ya maabara na kunionyesha teleskopu, TV na video. Hivi si vitu vya kawaida, bali vilikuwa ni kwa ajili ya kuwagundua Wakristo waliookoka na wale wanaoenda tu Kanisani.  

Mwishowe, alinipatia wasichana kumi na sita watakaofanya kazi nami kama maajenti. NINA likuwa mmoja wao. Nilirudi Lagos nikiwa nimesheheni ‘zawadi’ hizo nilizozitaja hapo juu.

No comments:

Post a Comment