Wednesday, December 10, 2014

Kubatizwa kwa Moto Uwakao - 5


====  SIKU YA 11  ====

Kim, Joo-Eun

Kadiri nilivyoomba kwa bidii, nuru kali ilitokea mbele yangu, na mbele ya hiyo nuru alisimama Yesu. "Joo-Eun, nakupenda. Omba bila kukoma; omba kwa bidii; omba kwa moyo wako wote. Usiache kuomba." Nilihisi ujotojoto na niliweza kumwona Yesu kwa wazi zaidi. Ndipo nikatambua ni kwa nini Yesu aliniambia niinue mikono yangu juu zaidi. Niliweza kumwona wazi zaidi nilipofanya hivyo. Nikamwambia, "Haa! Nakuona waziwazi, Bwana. Ni vizuri sana, Yesu. Nakushukuru." Kutokana na kule kujisikia vizuri sana, nilijikuta ninaacha kuomba kwa muda kidogo. Mara lilitokea pepo chafu. Lilikuwa jeusi tii kuliko giza. Nikalifukuza kwa Jina la Yesu, na nikaendelea kuomba kwa kunena kwa lugha. Lee, Yoo-Kyung 

Nikiwa naomba kwa kunena, lilitokea pepo moja lenye kope ndefu. Lilikuwa likilia, na likaniomba nilisikilize juu ya kile lilichokuwa likisema. "Kuna baridi sana. Najisikia baridi sana. Je, unaweza kunisaidia nipate joto? Tafadhali sana?" Nikalijibu, "Ewe pepo mchafu. Kwa Jina la Yesu ondoka kwangu!"


Dada Baek, Bong-Nyo

Leo Yesu alinipeleka Mbinguni. Si rahisi mtu kuelezea kwa maneno ya kibinadamu jinsi mwonekano wa Mbingu ulivyo. Tulikuwa mbele ya kiti cha Baba. Utukufu wa Baba ulikuwa mkubwa sana! Sikuweza kuinua kichwa changu. Niliinama mbele zake. Jinsi Baba alivyo hata haiwezekani kuelezea. Ukuu wake ni zaidi ya maelezo. Nilijaribu kunyanyua kichwa changu ili angalau nimtazame Baba kidogo, lakini ukali wa nuru yake ukanifanya nishindwe. Baba Mungu ni Nuru. Akili ya mwanadamu haiwezi kupata picha halisi ya utukufu wake. Ukubwa wa Baba Mungu ulionekana kuwa amejaza kimo na kina cha Mbingu toka mashariki hadi magharibi. Kulionekana kama kuna mawingu juu ya kiti chake cha enzi. Mwanga mkali kuliko wa jua ulikuwa uko juu yake. Nilijiona kama punje ya mchanga mbele za Mungu.


Baadaye, nilipokuwa naondoka Mbinguni, malaika alinisindikiza hadi duniani. Lakini wakati tukirudi, kukawa na kundi la mashetani ambalo lilianza kutufukuza. Mapepo hayo yalikuwa na sura mbaya sana na za kutisha. Japokuwa malaika aliyenisindikiza alikuwa na kasi kubwa, lakini mapepo yale nayo yalikuwa na kasi sana. Mmoja alikuwa dragoni, mwingine joka, mwingine ana kichwa cha chura na wa nne ana kichwa cha binadamu. Yalikuwa yakicheka wakati yakitufukuza. Nikamwambia malaika, "Je, tunaweza kwenda kasi zaidi?" mashetani yale yalikuwa tayari yameshatupita na yanataka kuziba njia ya kurudi kanisani. Mengine yalikuwa nyuma na yanajiandaa kushambulia. Malaika alipaza sauti, akisema, "Bwana, tafadhali njoo sasa!" Mara aliposema hivyo, Bwana alitokea mbele yetu. Kwa sauti kubwa na yenye nguvu aliyakemea yale mashetani, "Mnawezaje kuthubutu kumvamia mwanangu! Ondokeni sasa!" Kufumba na kufumbua, yakawa yameshatoweka.====  SIKU YA 12  ====


Dada Baek, Bong-Nyo

Nilikuwa nikiomba kwa kunena kwa lugha, na baada ya dakika thelathini, niliona malaika watano wakiruka kunielekea mimi. Niliamua kuwajaribu wale malaika ili nijue kuwa hawakuwa mapepo. Niliendelea kunena kwa lugha. Niliona tabasamu kwenye nyuso zao nao wakajiweka kiurafiki wakati nikiendelea kunena kwa bidii. Niliamini kuwa kuomba kwangu kwa bidii kungedhihirisha iwapo wale ni malaika au la. Baada ya dakika chache, mavazi yao meupe yaligeuka kuwa meusi tii na mabawa yao yakatoweka! Kadiri walivyotembea, miili yao ikawa inajinyonganyonga. Niliongeza bidii kuomba kwa kunena, nao wakaanza kuanguka chini sakafuni. Kusema kweli, karama ya kunena kwa lugha ina nguvu sana. Mara wakawa kama majitu niliyoyaona kwenye sinema. Yalikuwa na sura mbaya sana; yakitia kinyaa! Niliyatoa yote moja baada ya jingine kwa Jina la Yesu Kristo. Yote yalikimbia. Wakati nikiendelea kuyafukuza, “Yesu” alikuja na kusema,   "Bong-Nyo, Mimi ni Bwana wako. Niamini Mimi!" Hata hivyo, sauti yake ilikuwa haiko sawasawa na tabia yake ilikuwa ya kutia mashaka. Kila mara Yesu alipokuja kwangu hapo kabla, kulikuwa na upole, utulivu na amani. Lakini sasa nilijisikia kukosa amani na nikawa na woga. Nilijisikia nywele zikinisimama. Kwa ujasiri, nilisema kwa sauti, "Kwa Jina la Yesu, ondoka kwangu!"  Mara aligeuka na kuwa kiumbe chenye sura mbaya kabisa. Na nilipoendelea kumkemea, akatoweka. 


Mara roho nyingine ilitokea. Ilikuwa na sura nzuri sana. Nikawaza, "Ha! Yaani mwanamke huyu ni mzuri!" Yule pepo alikuwa ni mzuri mno kuliko mwanamke yeyote humu duniani. Alikuwa mwembamba mwenye umbo zuri. Alikuwa amevaa suti ya kiofisi. Alitembea kama mwanamitindo na akanikaribia kwa taratibu. Aliinama na kunisalimia na kusema,  "Umekuwa ukihudhuria Kanisa hili tangu lini?" Nilipuuza lile swali na nikaendelea tu kunena kwa lugha. Alipiga magoti pembeni yangu; na japokuwa alionekana amependeza sana, mwili wangu ulianza kujisikia msisimko wa woga. Ghafla uso wake uligawanyika mara mbili, akageuka kiumbe cha kutisha sana. Akapaza sauti akisema,  "Haya endelea kuomba, lakini haitakuwa rahisi. Sitaondoka!" Pepo lile likawa haliondoki. Nikamsikia Bwana akisema, "Bong-Nyo, endelea tu kuomba. Omba kwa bidii. Nitamkemea na kumzuia huyo pepo mchafu.


Mara yule pepo aliruka juu na kujigeuza kuwa mwanamke mrembo tena. Safari hii alikuwa amevaa gauni zuri la harusi. Alionekana mrembo sana. Aliruka kuja kwangu, huku akifumba na kufumbua macho yake ya mviringo. Bwana akaninong’oneza sikioni akisema, "Endelea kuomba na utazame kwa makini jinsi huyo mwanamke mrembo atakavyogeuka tena kuwa pepo lenye sura mbaya." Niliendelea kuomba kwa bidii kama Bwana alivyoniamuru. Muda si mrefu, huyo mwanamke aligeuka na kuwa na sura mbaya sana. Nikamkemea naye akatoweka.


Baadaye, Yesu alinionyesha sehemu kule kuzimu inayojulikana kama wilaya ya mwanga mwekundu. Niliona mlima mkubwa sana ukiwa umefunikwa kwa miili. Miili ya watu ilikuwa imefunikwa na wadudu weupe na mikono yao ilikuwa imefungwa. Watu wale hawakuwa na namna yoyote ya kuwatoa wadudu wale. Wadudu hao walikuwa wanapenya miili yao kwenye ngozi, pua, midomo na masikio. Wanapoliwa na wadudu hao, wanageuka na kuwa na sura mbaya sana, kisha wanabakia mifupa tu. Walikuwa kwenye maumivu makali mno. Nikasema, "Bwana, kwa nini watu hawa wako kwenye mateso makali kiasi hiki?" Yesu akasema, "Wanawake walio hapa ni wale waliokuwa wakijiuza miili yao. Wanaume ni wale waliofanya uzinzi na hao wanawake."  Kulikuwa na joto kali sana, nami nilikuwa kwenye maumivu sana. Nilitamani tu kuondoka. 


Kim, Joo-Eun 

Leo kulikuwa na mashambulizi kadhaa toka kwa mapepo, roho chafu na madragoni, lakini kwa uweza wa Yesu, yote yalikimbia. Hatimaye, lilikuja kundi la mapepo ambayo hayakuwa na miili. Kimsingi, yalikuwa na mwonekano wa ajabu kama jicho. Yalikuwa yakipiga tu kelele, "Msiombe! Tutavuruga mawazo na umakini wenu." Yalikuwa yakirudia tena na tena kusema hivyo. Nikiwa nimeingiwa na hofu, nilisema kwa sauti, "Kwa Jina la Yesu, ondokeni hapa!" Lakini yakawa bado yapo tu, na yakaanza kupiga kelele za ajabuajabu. Mara Bwana alirudi na kusema, "Joo-Eun, usiangalie wala kusikiliza chochote isipokuwa kinachotoka kwangu tu." Alifunika masikio yangu kwa mikono yake na kusema, "Joe-Eun, unaweza kuongea na Mimi." Mapepo yale maovu yalitawanyika kutokana na uwepo wake. 

No comments:

Post a Comment