Saturday, December 13, 2014

Kubatizwa kwa Moto Uwakao - 6====  SIKU YA 13  ==== 

Kim, Joo-Eun 

Leo yalikuwapo mashambulizi makubwa kutoka kwa mapepo. Wakati ninaomba, nilipelekwa hadi kwenye sehemu yenye giza, ambayo nilijua kuwa ni kuzimu. Niliona mapepo mengi ambayo yalikuwa yamezunguka kiumbe kikubwa kiovu. Kiumbe hiki kikubwa kilionekana kina hamaki pamoja na hofu. Kilipiga kelele na kuhaha huku na huku, na kuonekana kimechanganyikiwa na kisichokuwa na utulivu.Kiumbe hiki kikubwa kilionekana kuwa ndio kiongozi wa mapepo mengine ambayo yalikuwa mengi yasiyo na idadi. Mapepo yale yalikuwa yakingoja amri kutoka kwa hicho kiumbe kikubwa. Baada ya amri kutolewa, mapepo yale yasiyo na idadi yalipaa angani na yakaonekana kanisani kwetu. Kasi yao ilikuwa kubwa sana, hata haifiki sekunde. Mapepo yale yote yalishambulia kusanyiko, akiwamo Meena, yule mtoto wa miaka mitano. Lakini alipopaza sauti ya nguvu katika lugha yake ya maombi "Babaya," mapepo yaliyokuwa karibu yake yalianguka chini! Mashambulizi yalifanywa kwa mara moja juu ya wale wote tuliokuwa tunaomba kwa kunena. Mapepo yale yalianguka chini moja baada ya jingine. Pepo moja lilitoa amri likisema, "Sikilizeni ninyi nyote. Mshambulieni Mchungaji Kim. Kama kiongozi akianguka, wengine waliobaki wataanguka kirahisi. Enyi wajinga, mnangoja nini sasa? Mshambulieni Mchungaji Kim kwa nguvu zote!"


Ghafla, kundi kubwa la mapepo lilitokea na kumshambulia Mchungaji Kim. Lakini kilichotokea kilikuwa cha kushangaza sana – mengi ya mapepo haya yalianguka tu chini! Mapepo hayo yalijeruhiwa na kushindwa. Yote yaliogopa kutokana na kile kilichowatokea kwa ghafla kiasi kile. Kwa mara nyingine, lile jeshi ovu lilijaribu tena kushambulia, lakini yalishindwa kila upande. Mashambulizi yaliendelea, lakini kila mara yaliishia kushidwa vilevile! Hawakumgusa tena mchungaji. Yalipotambua kuwa juhudi zao zote zilikuwa bure, yalianza kumkwepa mchungaji. Yalieleaelea tu kumzunguka lakini hayakuthubutu kumkaribia. Nilipomtazama mchungaji, alikuwa hana hata habari ya kile kilichokuwa kinaendelea. Alikuwa tu anaomba kwa bidii kwa kunena kwa sauti kubwa. Kisha yale mapepo yalitupwa ukutani na kuvunjika vipandevipande. Yote yalilia kwa hofu. Nilipoona mapepo yakikimbia, nilijisikia ushindi na nikacheka kwa ushindi. Ndipo nikamwona ibilisi akisema kwa hasira, "Mchungaji Kim usiombe! Unadhani tutakuacha hivihivi kutokana na hili? Naapa nitakuua tu!" Alisaga meno na kuwaambia wale mapepo, "Wajinga nyie! Yaani kwa nguvu zenu zote mnashindwa hata na mchungaji mmoja tu? Haya, haraka; shambulieni!" Kisha ibilisi akasema kwa sauti, "Ah, huyu mchungaji anatuletea shida kweli! Ahh, nadhani nitachanganyikiwa. Achaneni na huyo mchungaji, tushambulie waumini. Haraka!"


Mapepo yalianza kushambulia waumini, lakini hata hivyo hayakuwashambulia kwa nguvu zote. Yalikuwa yakishambulia machachemachache kwa kila mtu. Yalisambaa kila upande na safari hii yaliamua kushambulia kila mtu kwenye kusanyiko. Kulikuwa na mapepo ya kila aina, yakiwa na maumbo mbalimbali. Haiwezekani kuyaelezea yote. Hata hivyo, vyovyote yalivyojaribu kushambulia, yalishindwa vibaya. Maombi ya kanisa kwa kunena kwa lugha yalitoa nguvu ya kuyashinda mapepo yale. Kadiri yalivyoshambulia, ndivyo yalivyozidi kuanguka. Mfalme wa mapepo akapaza sauti akisema, "Nyie watu wa kanisa hili acheni kuomba! Kwa nini mnaendelea kuomba?” Kisha akasema, “Nyie mapepo, mnafanya nini? Hakuna kati yenu anayeweza kuwafanya waache kuomba?" Mapepo yote yalikimbia kwa kuchanganyikiwa. Haikujalisha ni mapepo kiasi gani yalikuwa pale, maana maombi ya ujasiri ya waumini yaliyashinda yote!


Baadaye usiku, pepo jingine lilijaribu kunivamia. Likasema, "Acha kuomba. Nitakusumbua hadi ushindwe kuomba. Nitakulaani kwa magonjwa.  Ha ha ha ha," likacheka kicheko kiovu. Lakini pepo lile nalo lilishindwa kwa Jina la Yesu.


Hata baadaye usiku kadiri nilivyoendelea kunena kwa lugha, nilipelekwa kuzimu. Nilikuwa mahali ambapo kulikuwa na pepo lililokuwa likichoma mkuki mkali kwenye masanduku fulani. Kwa lugha chafu, lilisema, "Unadhani wewe ni mchungaji? Uliishi maisha ya namna gani? Nafurahi kwamba sasa uko na mimi hapa!" Pepo lile lilendelea kuchoma maboksi yale huku likitukana. Sauti kubwa za maumivu makali zilitoka kwenye maboksi yale, huku damu nayo ikitoka! Niliona kuwa maboksi yale yalifunikwa na kitambaa kwa juu, huku kukiwa na msalaba mkubwa uliochorwa pale. Masanduku yalipangwa vizuri na yalikuwa katika mstari mrefu usio na mwisho. Nilitambua kuwa yalikuwa ni majeneza. Mapepo yalikuwa yakichoma mikuki yao bila huruma. Nikamwuliza Bwana, "Yesu, kwa nini majeneza ya waliokuwa wachungaji yako hapa?" Yesu akajibu, "Wachungaji hawa hawakuhubiri Injili yangu. Walihubiri Injili nyingine, na wale waliowafuata wakapotoka. Huu ndio mwisho wao hapa kuzimu."  Yesu akasema, "Wachungaji waliopotoka watapata hukumu kubwa."


Katika sehemu nyingine ya kuzimu, niliona watu wengine wakiteswa. Walikuwa ndani ya kikaango kikubwa, wakipiga kelele, "Joto.  Ahh, nisaidieee!" Hicho kikaango kikubwa kilikuwa chekundu kwa moto, na mafuta yanapogusa ngozi zao, nyama yote inapukutika na kubaki mifupa tu. Walikuwa wakirukaruka tu kwa mahangaiko. Halafu nyama yao inarudi tena, na hali inakuwa ni ileile tena na tena bila mwisho, nikamwuliza Yesu ni nini walifanya. Yesu akasema,  "Walipokuwa duniani, hawakuwa waaminifu katika ndoa zao. Waliwasaliti wenzi wao. Walitenda mambo hayo kwa siri. Ndiyo maana wanateswa hapa."


Baadaye Yesu alinionyesha sehemu tofauti kuzimu ambako kulikuwa na shimo kubwa sana. Lilikuwa limejaa watu. Maelfu walikuwa wakiungua moto. Moto ule mwekundu ulionekana kama vile una uhai wake wenyewe. Watu walikuwa wakikimbia ndani ya shimo huku wakipiga kelele kutokana na joto kali. Yesu akaeleza, "Hawa ni watu walioamini dini za uongo au wale walioikataa Injili.


====  SIKU YA 14  ====

Kim, Joo-Eun 


Nilikuwa nikiomba kwa bidii, na baada ya muda mfupi, pepo lenye sura ya msichana mwenye gauni jeupe alitokea. Damu ilikuwa ikimtoka mdomoni. Akasema, "Usiombe. nitakushinda." Nikasema, "Ewe pepo mchafu; kwa Jina la Yesu, ondoka hapa!" Akatoweka. 


Kisha pepo jekundu lenye hasira sana likanijia, na mapepo mengine mengi yakaanza kutokea. Kadiri nilivyoomba kwa bidii, nilihisi mapepo yenye nguvu zaidi yanatokea. Cha ajabu, wakati huuhuu, nilihisi roho yangu nayo inakaribia Mbinguni. Mapepo yalikuwa yanajaribu kunizuia kuingia Mbinguni kwa kunitisha. Kwa hiyo nilizidisha bidii ya kuomba kwa lugha huku nimefumba macho. Nilijaribu kuyafukuza, lakini lile jekundu liligoma kukimbia. Ilibidi niendelee kukemea hadi likaondoka.


Bwana alikuja, na alionekana kuridhishwa na mimi, kwa umri wangu mdogo kufukuza mapepo! Yesu aliniita kwa jina langu la utani na kwa jina langu halisi, "Joo-Eun, Freckles (Mabaka), imani yako imeongezeka sana; kwa hiyo endelea kuomba kwa bidii huku umefumba macho yako."


Nikatia umakini kabisa wakati nikiomba na ghafla nikafunikwa na giza, upepo ukaanza kunipuliza. Nikaona mlango umefunguka kwa mbali. Ghafla, mwanga mkali ukatokea. Kidogo nifungue macho yangu maana ule mwanga ulizidi kuwa mkali, lakini nikagundua pia kuwa nilikuwa sina uwezo wa kufungua macho yangu. Woga ulianza kunijaa na mara Yesu akatokea. Akaanza kueleza, "Joo-Eun, ulipokuwa ukiomba kwa kunena, roho yako ilikuwa inakaribia Mbinguni huku ikisindikizwa na malaika. Hata hivyo, mapepo yalionekana kukutishia ili kwamba ufungue macho yako. Lakini niliingilia kati na kuyaamuru mapepo yale yaondoke. Ilikuwa ni Mimi ndio nilikuzuia kufungua macho yako. Joo-Eun, nadhani unahitaji kuomba tena zaidi kidogo. Sidhani kama utaenda Mbinguni leo." Nilivunjika moyo kweli! Lakini Yesu akanifariji kwa maneno ya kutia moyo, "Joo-Eun, usiogope. Naahidi kuwa nitakupeleka Mbinguni na kutembeza huko."


Lee, Haak-Sung


Yesu alinitembelea na kuanza kunionyesha kuzimu. Nilifika mahali ambako kulikuwa na kiumbe kikubwa kiovu kimekaa kwenye kiti. Mwonekano wake ulionyesha kuwa kilikuwa ndio mfalme wa eneo lile. Kulikuwa na mlango wa kufyatua mbele yake sakafuni. Watu walikuwa wamesimama juu ya mlango ule. Yule kiumbe anapokanyaga ule mlango, unafunguka na watu wale wanatumbukia kwenye lava inayotokota. Mara watu hao wanapotumbukia humo, wanawaka moto na wanaanza kulia kwa maumivu. Nilimwuliza Yesu kuhusu watu hawa naye akaniambia, "Hawa walikuwa ni wabashiri, au wateja wa wabashiri, wachawi na watu waliojiua wenyewe." Bwana alipozungumza kuhusu watu waliojiua, mjomba wangu, ambaye naye alijiua kwa kunywa vidonge vingi, alitokeza. Aliburutwa sakafuni na kusimamishwa kwenye ule mlango. Kisha kile kiumbe kilikanyaga ili mlango ufunguke. Nikamsihi Bwana amrehemu mjomba, "Tafadhali, Yesu, mjomba wangu yuko hatarini kuangukia kwenye lava. Tafadhali msaidie! Bwana, mjomba alikuwa siku zote mwema kwangu. Mjomba, njoo upande huu wangu haraka!” Akiwa na uso wa huzuni, Bwana akasema, "Haak-Sung, alishachelewa. Hakuna kinachoweza kufanyika sasa." Mara kile kiumbe kilikanyaga ule mlango nao ukafunguka. Mjomba wangu pamoja na watu wengine wakatumbukia kwenye lava. Wote walipiga kelele kubwa.


Miongoni mwa watu walio kwenye mateso – wale ambao hawakumjua Mungu – wengi walikuwa ni watawa wa kibudha, wengine ni Wakristo waliorudi nyuma, na kuna ambao walikuwa wakienda kanisani kwa sababu zao binafsi na wala sio kwa ajili ya Yesu.


Kwenye sehemu nyingine ya kuzimu, Yesu aliniambia, "Haak-Sung, angalia kwa makini." Walikuwapo watu wengi wakiwa wamezungukwa na nyoka wakubwa kwa wadogo. Wote walikuwa wamesongamana sana kwa pamoja. Nyoka wakubwa walijiviringisha kwenye vichwa vya watu huku wale wadogo wakijiviringisha kwenye miili. Nyoka hao walikuwa wakiwauma watu tena na tena. Watu walipiga kelele kwa maumivu. Nikamwuliza Bwana, "Bwana, watu hawa walitenda dhambi gani?" Yesu akajibu, "Hawakuwa na imani ya kweli kwangu. Hawakuniamini kwa moyo wa kweli. Hata pale walipodai kuwa wananiamini, matendo yao hayakuwa na msimamo thabiti. Walikuwa vigeugeu. Tabia yao ya kigeugeu iliathiri mahudhurio yao kanisani. Hawakuwa wameokoka kwelikweli. Wengi wao walikufa kwenye ajali, na hawakuweza kutubu kwelikweli. Haak-Sung, hata wewe una tabia ya kigeugeu. Hata hivyo, Ukristo wako ni imara."


Katika sehemu nyingine ya kuzimu, nilimwona mwanamke akilia kwa sauti sana, "Hii si sawa kabisa! sistahili adhabu ya namna hii. Maisha yangu duniani yalikuwa ya tabu. Sikuweza kustahimili zaidi. Ndio maana nilijiua. Lakini mateso ya kuzimu ni makubwa zaidi ya yale ya duniani. Kwa nini mlinileta kuzimu? Hii si sawa. Sikuwa nimesikia juu ya uhalisia wa kuzimu. Si sawa kabisa mimi kuwa hapa!” Alirudia tena na tena kusema hayo. Mmoja wa viumbe waovu akacheka na kusema, "Nilikudanganya kabisa hadi ukajiua. Haukuijua kweli. Ulihudhuria hata kanisani lakini hukuwahi kusikia kuhusu Mbingu na kuzimu.  Nilikuwa nina wasiwasi kuwa ungeweza kujua juu ya mahali hapa. Japokuwa ulikuwa ukienda kanisani, lakini bado ulijiua. Kwa hiyo, ni halali kwako kuwa hapa. Nilikuzidi akili na nikakudanganya. Niliishinda roho yako. Nitakuonyesha masomo mengi milele yote." Yule kiumbe alianza kumpiga yule mwanamke bila huruma. Vilio vyake na kusihi kwake kuhurumiwa ikawa ni kazi bure.


Yesu alinirudisha kanisani, na nikaendelea kuomba kwa kunena. Akaniambia, "Haak-Sung, maombi yako yanayoanzia usiku hadi asubuhi yana uwezo na nguvu zaidi kuliko maombi yako ya mchana. Kwa hiyo, jaribu kuomba zaidi usiku kuliko mchana."


Aliniambia nimtazame Yeye kwa karibu zaidi. Nikamwona Bwana amevaa taji ya miba kichwani; na nikaona matundu kwenye mikono na miguu yake. Kulikuwa na damu inayotoka kwenye kila kovu lake. Nikaendelea kutubu na kulia nikiwa namwangalia Bwana anavyoteseka.


Baada ya kumaliza kuomba, Bwana alinipeleka Mbinguni na kufuta machozi yangu. Niliweza kuona bahari ya Mbinguni ambayo ilikuwa angavu kama kioo.


Lee, Yoo-Kyung

Kwa kawaida, mapepo huninyanyasa mimi pale ninapoanza kuomba. Lakini leo, Bwana alikutana nami. Si tu kwamba alitokea, lakini pia alinipeleka Mbinguni. Yesu alisema, "Unajisikia vizuri leo, si ndiyo?" Nikasema, "Ndiyo, Bwana najisikia vizuri sana kwa sababu sijaona mapepo leo."


Kule Mbinguni, Bwana alinipeleka kwenye sehemu iliyo juu sana na akanionyesha dunia. Dunia ilionekana kadogo sana kutokea pale. Niliiona dunia ikizunguka. Nikamwambia Bwana, "Yesu, nataka kuishi Mbinguni. Sitaki kurudi tena duniani." Yesu akasema, "Muda wako haujafika bado.  Kwanza ni lazima unitumikie na kufanya kazi yangu kwa bidii. Katika muda uliopangwa, utakuja hapa." Tulikuwa na muda mzuri na Bwana kule Mbinguni. Tulifanya utani mwingi na kucheka sana. Nilifurahia sana. Baadaye, mimi na Bwana tulirudi kanisani.


Dada Baek, Bong-Nyo


Niliomba, "Bwana, kwa nini hukutimiza ahadi yako ya kutubariki kifedha? Umevunja ahadi yako. Hebu angalia tulivyo. Tunapoomba, tunaomba kwenye baridi kwa sababu hatuwezi kulipia gesi kwa ajili ya joto. Tunapoomba, tunakuwa tunatetemeka, na wakati wote tunakuwa tunasugua mikono yetu ili angalau tupate joto.  Sielewi ni kwa nini hujatubariki. Hatuna kitu cha kula zaidi ya mchele na kimchee... Familia ya mchungaji hawana fedha na familia yangu nayo hatuna fedha. Tunapata tabu … tunapoomba usiku kucha, tunaumia na kuvimba kwa sababu ya kuwa tumekaa mkao uleule. Miili yetu inauma kutokana na maumivu na kukakamaa. Hatuna miili yenye nguvu kwa sababu ya kukosa chakula kizuri. Kwa nini unaacha tuendelee kwa namna hii? Bwana, siwezi kuendelea zaidi." Nilikuwa naongea na kulalamika tu bila hata ya kutafakari kwanza. Lakini Bwana alikuwa akisikiliza kwa upole kila neno. Bwana kweli alikuwa mvumilivu kwangu. Kwa maneno mazuri, Bwana alianza kuongea kwa upole, "Mimi sina kinyongo na malalamiko yako. Hatuna haja ya kuwa na hofu juu ya kitu chochote."


Kisha akaanza kunionyesha kuzimu.  "Hebu twende. Sasa angalia hapa kulivyo," Yesu alisema. Niliona mnyama mkubwa sana; mkubwa kama mlima. Alifanana na mamba au dragoni, na mama yangu alikuwa pembeni yake. Alitumia ulimi wake kumviringa mtu, kisha anamtafuna na kummeza. Nililia na kulia.  "Bong-Nyo, unapolia, nayahisi maumivu yako. Moyo wako unapokuwa na masikitiko, moyo wangu unasikitika pia. Unapokuwa na huzuni, nami nakuwa na huzuni pia. Kama mama yako angekuwa bado hai, ningeweza kukusaidia. Lakini sasa haiwezekani tena. Kama ukitaka kulalamika na kuwa na hasira, unaweza kufanya hivyo. Nitakuwa hapa kusikiliza maumivu yako. Najua kuwa unateseka. Natamani utoe kila kilichomo moyoni mwako chote."


Baadaye, nilimwona baba wa mchungaji wetu kule kuzimu. Kiumbe mwovu alikuwa tayari kumtupa kwenye namna fulani ya chungu kikubwa ambacho kilikuwa na pombe nyeusi, iliyooza na inayochemka. Nikamwuliza Bwana kwa nini alikuwa pale. Yesu akajibu, "Alitenda dhambi sana na alikuwa akimtesa mke wake. Alipenda ulevi. Pombe ndiyo iliyokuwa mungu wake. Ulevi wake uliathiri kazi yake, na akawatelekeza watoto wake. Watoto wake walikuwa na maisha magumu. Matokeo yake, atakunywa na kuteswa kwenye  hii pombe milele."  Baba wa mchungaji akaanza kupaza sauti, "Ooh, nimefanya mambo mengi mabaya sana. Natamani mke wangu angekuwa amemkubali Yesu kama Mwokozi na Bwana. Angeweza kuingia mbinguni. Nilipokuwa duniani, nilicheza kamari na kulewa siku nzima. Sikujali kutunza familia yangu. Sikujali kuwapatia mahitaji yao ya msingi. Mke wangu alifanya kazi siku nzima ili kuwalisha watoto wetu. Mimi ndio nahusika na maisha yake magumu. Dhambi nilizotenda zinalipwa sasa. Nastahili kulaaniwa. Tafadhali, utakaporudi duniani, mwambie mwanangu mdogo aendelee kuhudhuria kanisani. Mwambie awe mwaminifu kwa Bwana na aamini." Pia aliniomba niwaambie wanawe wasihudhurie kanisani kiubatili tu. Watunze siku za jumapili kwa utakatifu, watubu kwa dhati, na waenende katika Bwana kwa uaminifu kama Wakristo.


Akaendelea kusema, "Niko kuzimu na ninateswa. Kuzimu ni mahali pa mwisho; mateso yasiyo na mwisho. Kunatisha sana. Tafadhali, wahubirie kaka, dada na ndugu zako ili wapate nafasi ya kuingia Mbinguni."


Yesu na mimi tuliendelea kutembea kule kuzimu. Tulifika mahali ambako niliona kundi kubwa la watu ambao wamejaza anga la kuzimu. Walikuwa wa kabila mbalimbali nao wamepigiliwa misumari kwenye misalaba. Misalaba ilikuwa ya miti, nao walikuwa wamesulubiwa kama ambavyo Yesu alisulubiwa. Nikamwuliza Yesu ni dhambi gani walitenda, naye akajibu kwa sauti iliyojaa ghadhabu, "Hawa ni watu waliohudhuria kanisani mara kwa mara. Hata walibeba Biblia zao wanapoenda kanisani. Lakini waliomba na kuabudu kiubatili tu. Walikuwa ni walaghai. Walikuwa wanafiki. Nje ya kanisa walikuwa ni walevi na wavuta sigara. Hawakutunza sabato. Baada ya ibada, walikuwa pia wakienda kwenye shughuli za burudani kama vile kupanda milima na kadhalika. Baadhi yao walikuwa ni wakopeshaji. Walikopesha na kudai riba kubwa. Walitajirika kutokana na hizo riba kubwa. Familia nyingi hazikuweza kulipa riba zao, kwa hiyo zikaishia kufilisika. Familia zilivunjika kutokana na matatizo ya kifedha. Mioyo na matendo yao vilikuwa vya kidunia, japokuwa maneno yao yalikiri imani. Kama wangeenenda kwa imani kwa mioyo na nguvu zao zote, wangeingia Mbinguni. Hawakuweza kuzaliwa upya kutokana na kukosa kwao uaminifu. Hawakuwa wamezaliwa upya kwa maji au kwa Roho Mtakatifu. Walifuata mapokeo badala ya Mungu.  Shughuli zao za kidunia walizipa kipaumbele zaidi kuliko Mungu. Matendo yao hayakuonyesha imani halisi. Walitumika kwa imani iliyo."


Mara watu wote wale waliokuwa kwenye misalaba walifunikwa na wadudu, wakubwa kwa wadogo, ambao walitafuna nyama za miili yao. Pia walivalishwa miiba kwenye shingo zao. Bwana aliniambia kuwa mambo hayo yatakuwa yanajirudia tena na tena milele. Bwana alikuwa madhubuti na muwazi kabisa katika onyo lake. Kisha aliniambia niwatazame watu waliokuwa wakiamini kwa ubatili tu.


Nilikuwa natetemeka kwa woga, na Bwana akaongea kwa upole nami akisema, "Bong-Nyo, unaogopa. Inatosha kwa leo, tuondoke sasa.  Bong-Nyo, umeshuhudia familia yako wakiwa kwenye mateso. Imekuwa ni jambo gumu sana kulistahimili. Umelia sana. Nataka kukufariji na kukuchangamsha sasa. Tutakapofika Mbinguni na kuingia kanisani, nataka ukaombe na kuangalia ibada." Kanisa la Mungu lililoko Mbinguni linang’aa kwa utukufu na nuru. Miali ya nuru ile ilifunika anga lote la Mbinguni. Ilipendeza sana, kukiwa na makundi kwa makundi ya malaika na watakatifu.

2 comments: