Bwana alizungumza waziwazi.
“Wakati huu, shughuli za kiroho za makanisa
zinapingana na kile ambazo niliwakusudia. Viongozi na waumini wananiabudu
kimazoea tu na wananijua kwa nadharia tu za vitabuni. Iweni na shauku kubwa
kisha mnijie Mimi.”
Bwana wetu ana shauku ya
kutuonyesha uhalisia wa kuingia kwenye mapambano ya kiroho dhidi ya mapepo
wabaya na kufungua macho yetu ya kiroho ili kwamba tuweze kuona moja kwa moja
Mbinguni, kuzimu, malaika na shetani.
==== SIKU YA 16 ====
Lee, Yoo-Kyung:
* Mabishano
husababisha nyumba yako ya mbinguni ianguke.
Huko Mbinguni niliuliza, “Yesu, niliambiwa kuwa tuna nyumba Mbinguni.
Ningependa kuona nyumba yangu.” Alinipeleka hadi kwenye nyumba
yangu. Tulitembea kwa kitambo, ndipo nilipoona nyumba ya dhahabu inayong’aa.
Yesu alisema, “Hii ndiyo nyumba yako.” Nilishangazwa
sana na uzuri wake. Malaika walikuwa wakipita huku na kule katika harakati za
kuijenga nyumba yangu.
Nilipouliza ni nyumba ya
ghorofa ngapi, alisema kuwa ghorofa ya tano ilikuwa karibu kukamilika na nguzo
zaidi zilikuwa zikijengwa ili kuongeza ghorofa zingine zaidi. Pia niliona
nyumba ya ndugu Haak-Sung na ghorofa ya saba ilikuwa ndio imekamilika.
Nilipoomba kuonyeshwa
nyumba ya Joseph na ya Joo-Eun, Yesu alionekana mwenye wasiwasi, akasema, “Nifanye nini? Nini kinaweza kufanyika?” Nikamwuliza Yesu
kama kulikuwa na tatizo. Alisema kuwa ghrofa ya tatu na ya nne zilikuwa karibu
kumalizika, lakini walipoingia kwenye mabishano, nyumba zilianguka. Yesu
alinifundisha kuwa mtu akiwa mchoyo, mbishani au mtukanaji, nyumba yake
Mbinguni huanguka. Hii inawahusu watoto na watu wazima. Yesu aliniambia
nikawaambie Joseph na Joo-Eun waache kabisa kugombana na kubishana kunapotokea
kutoelewana.
Yesu alionekana mwenye uso
wa huzuni sana alipoangalia nyumba iliyoanguka. Hakuficha huzuni yake. “Oh, tufanye nini? Kwa nini Joseph na Joo-Eun hubishana
kiasi hicho? Tafadhali, Yoo-Kyung, waambie Joseph na Joo-Eun waache kugombana.
Wote huanza kutaniana na kuishia kupigana, na wakati wanapocheza mpira, huishia
kwenye mabishano. Nyumba hii ilijengwa kwa ugumu sana na malaika kwa maagizo
yangu. Tutaijengaje tena sasa?”
Mara nyingi huwa nagombana
na kaka yangu, Haak-Sung, na sasa natambua kuwa natakiwa kuwa makini sana
katika mabishano yetu.
Yesu alinivisha joho la
dhahabu lenye mabawa akisema, “Mpendwa
wangu Yoo-Kyung, wewe unawashuhudia watu wengi sana nami nakupenda sana
kutokana na hilo.” Mara moja
nilisema, “Bwana, hata kesho nitaenda kushuhudia pia.” Yesu akasema, “Kweli? Endelea na moto huohuo. Nitaijenga
nyumba yako kwa haraka.”
Lee, Haak-Sung:
*Kadiri tunavyokutana na
ulimwengu wa roho kiundani zaidi, ndivyo unavyozidi kuwa wa kushangaza.
Takribani dakika 10 baada
ya kuanza kuomba, mashetani watatu walitokea. Moja lilikuwa la kiume na halina
kichwa. Pepo la kike limevaa gauni, huku kukiwa na mvumo wa upepo, lilijaribu
kuniparua kwa makucha yake makali. Joka kubwa likiwa na vichwa pande zote lilitokea,
huku kila kichwa kikitaka kutangulia. Nilipiga kelele, “Yesu, niokoe! Tafadhali nisaidie!”
Alikuja mara moja na kuyafukuza mashetani yale.
Yesu alituzunguka wakati
tukiomba na alimgusa kila mmoja wetu. Yesu alimgusa Mchungaji Kim kichwani na
mgongo uliokuwa ukiuma; aligusa mguu wa Joseph na mgongo wa Joo-Eun. Yesu
akasema, “Joseph, niambie shauku
yako mojawapo.” Akajibu, “Yesu, tafadhali msaidie kaka Oh, Jong-Suk asipoteze kazi yake na aendelee
kuhudhuria kanisani kwa bidii.” Yesu alikubali na akanipongeza akisema, “Haak-Sung, kuna baridi sana leo, lakini bado
ulitoka kwenda kushuhudia na kuwahubiria watu Injili. Umenifurahisha sana.”
Baada ya Yesu kuondoka,
pepo la kike lililovaa gauni lilinisogelea. Lilionekana kama msichana
mwanafunzi wa shule. Sikulitilia maanani nikaendelea tu kuomba kwa kunena kwa
lugha. Alilazimisha uso wake uwe mbele yangu na kutekenya pua zangu kwa unyoya
wakati nikiomba. Nikamwamuru aondoke.
Kumeshakuwa na mapepo mengi
tofautitofauti na mambo ya ajabu yameshatoa tangu nianze kuomba kwa bidii.
Kadiri ninavyozama ndani, ndivyo ninavyozidi kukutana na vitu visivyokuwapo
kwenye ulimwengu wa mwili.
Kim, Yong-Doo:
*Adhabu ya kutoa siri
Jana mchungaji wa kanisa
lililo karibu yetu pamoja na mke wake walikuja kwa ajili ya mazungumzo.
Waliuliza kama wanaweza kujiunga na kikundi cha maombi. Nilijaribu kukwepa hayo
mazungumzo kwa njia isiyo ya wazi sana. Lakini mke aliendelea kuuliza nami
sikutaka nionekane nisiyekuwa na adabu. Hatimaye nilijikuta nimesema, sawa.
Nilijua moyoni mwangu kuwa SIKUTAKIWA kufanya hivyo. Huzuni kubwa ilijaa moyoni
mwangu, maana nilikumbuka jinsi ambavyo Yesu alituambia tusimweleze mtu yeyote
nje ya kundi letu juu ya mkutano wetu wa maombi hadi kitabu kitakapotoka. Watu hawajui
nini kinachoendelea na wakati wa maombi tunakuwa kwenye vita vya kufa na kupona
dhidi ya mapepo.
Yesu alinitaka niwe thabiti
na nikatae shauku ya yule mke wa mchungaji ya kujiunga na kikundi cha maombi. Nilishindwa
na ndani kabisa ya moyo wangu nilikuwa naogopa kile ambacho kingeenda kutokea
kutokana na kukosa kwangu utii. Ibada ya Jumapili usiku iliisha kiajabu kwa
sababu ya kuhudhuria kwa huyo mke wa mchungaji ambako hakukutakiwa. Mapema
alfajiri, kwenye saa 8, nilimaliza sehemu ya kwanza ya maombi na nilitaka
kumwambia aende nyumbani, lakini alikaa kana kwamba alitaka kusema jambo.
Nilihakikisha kuwa hakuna mtu kwenye kundi lile ambaye angesema chochote,
lakini kwa namna fulani mimi na mke wangu ndio tulioishia kutoa siri.
Nilifichua siri kwamba
tumekuwa tukitembelea Mbinguni na kuzimu tunapoomba iwe hivyo na wengi
wamepokea vipawa vya macho ya kiroho, unabii, kupambanua kati ya roho za
Mbinguni na za kuzimu, kunena kwa lugha, imani, hekima na maarifa. Nilifichua
kuwa, nilikuwa kwenye harakati za kuandika matukio hayo kwenye kitabu ambacho
kingechapishwa. Kwa hiyo, nilimtia moyo arudi kwenye kanisa lake na waombe kwa
bidii.
Mungu alishapanga kufunua
macho yangu ya rohoni Jumapili ile usiku wakati wa maombi na alithibitisha hilo
kwa kupitia washirika ambayo tayari macho yao yalishafunguka. Lakini Mungu
alikasirishwa na tabia yangu ya kushindwa kuficha siri zake. Akili yangu ndogo
ilidhani kuwa ilikuwa sawa tu kufichwa baadhi ya mambo, kumbe nilifanya kosa
kubwa sana. Kwa sababu hiyo, mpango wa kufunguliwa macho yangu uliondolewa.
Yesu alihuzunika sana.
Wakati wa maombi, Dada Baek, Bong-Nyo alilia, “Iweje kile tulichokisema kiwe ni jambo kubwa kiasi hicho?” Alilia sana. Kwa vile
nilishindwa kutunza siri, nilijiona sifai na sikuweza kustahimili ile hatia.
Je, Samsoni alijisikiaje alipotoa siri yake? Alisaliti uhusiano wake na
Mungu.
Sister Baek, Bong-Nyo:
*Makemeo ya Bwana kwa Mchungaji Kim
“Mpendwa
wangu Bong-Nyo, kwa nini unalia kiasi hicho? Mchungaji wa kanisa lako, Kim,
Yong-Doo amefanya kosa kubwa. Lakini kwa nini unalia? Yesu aliuliza kwa sauti ya ukali. “Mchungaji
Kim anatakiwa atubu. Matukio yanayoendelea kwenye kanisa lenu ni lazima
yaandikwe kwenye kitabu na kufunuliwa kwa ulimwengu. Lakini kabla ya hapo, ni
lazima iwe siri. Lakini kwa nini alifunua siri na kunitenda dhambi?”
Bwana alisikitishwa sana na hilo.
“Siri
hii inafunua uhalisia wa ibilisi. Kwa hiyo, kutakuwapo majaribu mengi njiani.
Huna haja ya kulia. Kamweleze Mchungaji Kim haya niliyokwambia.” Hasira ya kutisha ya Yesu iliendelea. “Mchungaji Kim amefunua siri kwa mke wa
mchungaji wa kanisa la karibu na sijui ni kwa nini amefanya dhambi hii. Kosa la Mchungaji Kim ni kubwa, lakini usilie.”
Yesu
alitoa maelezo. “Namna
ambavyo kusanyiko linaomba kwa umoja na matukio yote yaliyotokea, yatapeleka
mtikisiko mkubwa duniani kote. Ibilisi hataki uhalisia wake ujulikane kwa
ulimwengu na anajaribu kwa nguvu kuuficha. Anaogopa kuwa mambo mliyoyaona
yatamweka wazi yeye na malaika zake. Kama ukweli huu juu ya uwepo wake na namna
alivyo utawekwa wazi kabla ya kitabu kutoka, mashambulizi ya shetani
yataongezeka. Kwa hiyo, itabidi mvumilie matatizo zaidi. Hadi mambo yote kuhusu
mikesha hii yawe yamerekodiwa ipasavyo, hii ni siri kabisa. nitawapa nafasi
nyingine. Mchungaji Kim itabidi awe kwenye kuomba na kuandika kitabu. Pia, kila
mmoja mwenye kipawa cha unabii ni lazima aache kwanza kuwaombea wengine.”
Yesu
aliwakemea wachungaji na wake zao kwa ukali kutokana na kukosa kwao mwelekeo
(focus). Kwa uthabiti, Yesu alisema, kuwa makanisa yote yaliyojengwa kwa Jina
lake ni lazima yaweze kupata majibu ya tatizo lolote, hata kama ni kubwa kiasi
gani, ndani yao wenyewe. “Kunapokuwa na tatizo, mchungaji na mke
wake ni lazima waombe kwa kukubaliana na hakika jibu litatokea kutoka kwa
Mungu. Wengi hawana uwezo wa kustahimili, wanaenda huku na kule, wakitafuta watu
wenye vipawa vya unabii ili wawaombee. Kuwa
wengi sana mlio namna hii na hilo linanisikitisha sana. Wake wa wachungaji
wanaposaidia na kuomba pamoja na wachungaji wao, wakiwa wamepiga magoti
madhabahuni mwa makanisa yao, Mungu atajibu maombi yao. Pia, kama umeomba na
kumwachia Mungu mambo yako yako yote, basi ngoja, maana hiyo ndiyo imani ya
kweli.”
Wakati wa ibada ya mchana,
hata kama Mchungaji Kim angeendesha sifa kwa kumaanisha kiasi gani, au
angehubiri kwa nguvu kiasi gani, Yesu alisimama pembeni ya madhabahu kimya huku
akiwa amechukia. Mchungaji Kim aliendesha ibada huku jasho likimtoka usoni,
lakini hasira ya Yesu haikuonekana kupungua. Mchungaji alionekana kama mtu
aliyetelekezwa. Nilifanya maombi toka moyoni kabisa kwa Yesu, lakini alijibu
kwa uthabiti kabisa kwamba, “Njia
pekee ni kwa Mchungaji Kim kuomba msamaha kwa moyo wa toba, na Baba yetu wa
Mbinguni ataangalia na kuamua.”
Yesu alisema kwa mamlaka, “Kama
mkifunua siri hii kwa watu, karama zote za rohoni mlizopewa zitaondolewa!”
Mchungaji Kim atatakiwa ajitenge na ndugu zake na marafiki zake na kujifungia
kwa ajili ya maombi. Yesu aliomba kwamba Mchungaji ajihusishe zaidi na maombi
na kurekodi kila kitu ambacho Bwana amemwonyesha, ili aweze kuchapisha kitabu
hicho mapema.
Niliuliza, “Yesu,
vipi kama mke wa mchungaji toka kwenye lile kanisa jirani aliyekuja kwa
Mchungaji Kim akirudi tena kwa Mchungaji Kim Jumapili mchana kwenye ibada na
kwa ajili ya kuongea na kuomba? Mchungaji wetu ni mpole na hawezi kusema,
hapana.” Bwana akasema kwa mamlaka, “Mimi
ni mganga wa kienyeji? Kwa nini unaniulizauliza kila mara kana kwamba mimi ni
mbashiri?” Kwa wachungaji na wake zao akasema, “Ni lazima mjibidishe kuomba, kunitafuta na
kunililia. Ndipo nitawajibu. Sijui kwa nini mnarukaruka toka sehemu moja kwenda
nyingine mkitafuta majibu!” Alikuwa hana furaha kabisa juu ya
hili.
No comments:
Post a Comment