Tuesday, June 24, 2014

Niliokolewa Toka Kwenye Nguvu za Giza - Sehemu ya 10




Sura ya 8: Silaha za Mwamini


- Jina la Yesu
- Damu ya Yesu
- Neno la Mungu
- Sifa za Mkristo


Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.” (Efe 6:10-11). 

“Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa.” (Ufu 12:11).


Nimeshasema mengi huko nyuma juu ya jambo hili, lakini ningependa kuwapa tu matukio machache. Tafadhali, tambua kuwa kuna nguvu katika Jina la Yesu! Kuna nguvu katika Damu ya Yesu! Maandiko yanasema: tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba.” (Wafilipi. 2: 8-11).

Tena Maandiko yanasema: “Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa.” (Ufu 12:11).

Hebu Jina Yesu na liwe midomoni mwako kila wakati! Haya mawili, Jina na Damu ya Yesu, husambaratisha kabisa mipango ya shetani, na ukweli ni kwamba, huharibu mbinu za shetani na maajenti wake. Pili, ni lazima ujifunze kuimba sifa kwa Mungu kila wakati. Iko nguvu ndani ya sifa.

Alikuwapo mchungaji mmoja – Mchungaji I.K. (sitataja jina lake). Alikuwa akichunga Kanisa kule Ebute Metta. Nilikuwa ninamuwinda na makosa yake yalikuwa ni kuwa:
1. alivuruga amani yetu kwa kuendesha ibada kila asubuhi.
2. alikuwa akizunguka na kipaza sauti hadi anapofika kituo Na. 2 cha mabasi kwenye barabara ya Akintola, Ebute Metta. Akifika pale anaanza kuhubiri. Anakuwa haishii hapo bali anaendelea kuyafunga mapepo, n.k.
3. akiwa Kanisani kwake anahubiri, anaweka wazi kazi za giza, kisha anaanza kuyafunga mapepo.
4. alikuwa mwombaji sana.
5. kila wakati alikuwa akiimba na kumsifu Mungu.


Nilituma mjumbe kwake lakini hakuweza kumuua, kwa hiyo nikaamua kuifanya kazi hiyo mimi mwenyewe.  Kwenye siku iliyopangwa, nilimwona akitembea mahali fulani. Jambo muhimu la kutaja hapa ni kuwa, mchungaji huyu, kila mara tulipomwendea, tuliona nguzo za mawingu kulia na kushoto kwake, zikiwa zinatembea pamoja naye, hivyo zilituzuia. Lakini kwenye siku hii, sikuona chochote. Kwa hiyo, nilipata uhakika kabisa kuwa mpango wangu ungefanikiwa. Niliamuru mvua inyeshe ili niweze kumpiga kwa radi. Mvua ilianza na radi pia. Miti yote kwenye eneo lile ikaanza kupoteza matawi yake, lakini huyu mchungaji alikuwa akiimba tu kwa furaha!  Bado naukumbuka wimbo aliokuwa akiimba: “In Jesus Name every knee shall bow,” yaani katika Jina la Yesu kila goti litapigwa.

Kadiri alivyoendelea na wimbo huu, mvua ilikoma, na radi nazo zikakoma. Kisha mara moja walitokea malaika wawili, mmoja kila upande, wakiwa na panga za moto. Macho na panga zao vilikuwa kama ndimi za moto. Halafu ulikuja upepo mkali ukanibeba na nikajikuta niko kwenye mji mwingine kabisa! Kiukweli, nilipatwa na mshangao sana. Lakini kwa kuwa mioyo yetu ilishafanywa kuwa migumu sana, nilichosema tu ni kuwa, “Huyu bwana ameponyoka tena!” Mchungaji mwenyewe wala hakujua vita vya kiroho ambavyo vilipiganwa kwa ajili yake. Kwa hiyo, unaweza kuona jinsi ambavyo mwana wa Mungu analindwa kikamilifu. Biblia inaposema, “hakuna kitakachowadhuru,” inamaanisha hivyohivyo!

Ushuhuda wa pili unamhusu Mkristo mmoja ambaye tulipanda naye teksi moja. Alikuwa na bidii sana na akaanza kugawa vipeperushi vya Injili ndani ya teksi. Aliponipatia na mimi, nilikataa. Akaanza kuhubiri. Kwa hiyo, nikaghadhibika na nikamgonga kwa pete iliyokuwa kwenye kidole changu. Hiyo ilikuwa ni kwa lengo la kumuua. Kijana huyu alipaza sauti: “Damu ya Yesu!” Mara moja radi na moto na malaika walitokea. Hapo tena upepo mkali ulinisomba, nikatolewa kwa nguvu nje ya teksi na kujikuta niko porini! Kama nisingekuwa ni mtu ninayesaidiwa na nguvu za giza, ningepotelea kwenye lile pori. Yule Mkristo naye wala hakujua vita iliyokuwa imepiganwa kwa niaba yake. Alichojua tu, yeye pamoja na abiria wengine ni kwamba, nilitoweka ndani ya teksi!

Jina la Yesu au Damu ya Yesu kwenye kinywa cha mwamini hutoa moto, n.k. Maandiko yanasema: Jina la Bwana ni ngome imara; Mwenye haki huikimbilia, akawa salama.(Mith 18:10).

Mpendwa msomaji, kama wewe ni mwana wa Mungu, kumbuka kuwa Mungu amelikuza sana Neno lake juu hata ya Jina lake (Zab. 138:2). Kwa hiyo, kiri Neno (Neno la Mungu) huku ukiamini kuwa kile ulichokiri kinaenda kutokea, na itakuwa hivyo. Hiyo ni ahadi ya Mungu!

Niseme tena hapa kuwa unaweza kukiri kile tu unachokijua. Maandiko yanatuita tujifurahishe katika Neno la Mungu, huku tukilitafakati usiku na mchana (Zab 1:2). Ili uweze kuligawa Neno la Kweli sawasawa, ni lazima ulijue – Kol 3:16. Maandiko yanasema: Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote.”  Vilevile, Zaburi 1:1-3 inasema:Heri mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha. Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo, Na sheria yake huitafakari mchana na usiku. Naye atakuwa kama mti uliopandwa Kandokando ya vijito vya maji, Uzaao matunda yake kwa majira yake, Wala jani lake halinyauki; Na kila alitendalo litafanikiwa.”

Kaa karibu na Biblia yako; omba bila kukoma; uwe na moyo wa kuimba; na usimame na kutendea kazi mamlaka uliyopewa na Bwana Yesu Kristo!


Sura ya 9: Sasa nini kinafuata?


“Na Roho na Bibi-arusi wasema, Njoo! Naye asikiaye na aseme, Njoo! Naye mwenye kiu na aje; na yeye atakaye, na ayatwae maji ya uzima bure.” (Ufu 22:17). 

Baada ya kusoma ushuhuda huu, huhitaji mahubiri zaidi ili kumpa Yesu Kristo maisha yako. Maandiko yanasema: Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele.” (Yoh 10:10).

Shetani anakuchukia na ameandaa mbinu mbalimbali za kukupeleka jehanamu pamoja naye. Hilo unaweza kulithibitisha kutokana na ushuhuda huu. Kama shetani akitoa ahadi kwako au hata akikupa zawadi, fahamu tu kuwa kuwa ni kwa lengo baya juu yako. Shetani ni mwongo na baba wa uongo (Yoh 8:44). Mungu alimwita kuwa ni adui yako. Kwa nini usimwamini Mungu na Neno lake?

Hujakutana na ushuhuda huu kwa bahati tu. Jichunguze na uhakikishe kuwa umo ndani ya Kristo. Utafanikiwa tu kujidanganya mwenyewe kama ukichagua kubakia  'mwendaji tu wa Kanisani'; na kibaya zaidi, kama ukiamua kupuuza uamuzi huu muhimu kabisa kwa maisha yako.

Tunakusihi kwa niaba ya Kristo: Upatanishwe na Mungu. Kama bado hujaokoka, yaani kama, kulingana na Maandiko, bado hujampokea Bwana Yesu Kristo kama Bwana na Mwokozi wako binafsi, na kubatizwa kwa kuzamishwa majini, tunakuhimiza ufanye hivyo bila kuchelewa. 
Kesho inaweza isiwe yako.

(Waebrania 3:15)
MWISHO

…………………………………………….

Kama ungependa kuusoma ushuhuda huu kwa lugha ya Kiingereza, tafadhali, bofya HAPA.



Kama ungependa nikutumie ushuhuda huu kama PDF E-BOOK, niandikie kwenye ijuekweli77@yahoo.co.uk na kusema tu: Nitumie e-book ya Emmanuel Eni.

Bwana akubariki

Sambaza upendo

Pokea wokovu wa Yesu sasa na kudumu ndani yake.
 

6 comments:

  1. mungu akubarik james

    ReplyDelete
  2. james mbona story haiendelei.......?

    ReplyDelete
    Replies
    1. Mbona imeshafika mwisho? Sasa hivi ni wakati wa ushuhuda mwingine. Nitauleta si muda mrefu.

      Delete
  3. ndugu james mbona kimya tunasubir ushuhuda......au mambo yamekutinga sana.

    ReplyDelete