Mchungaji Ricardo Cid
|
Mchungaji Ricardo alipata
mafunuo mbalimbali kutoka kwa Bwana Yesu kuhusiana na hali ya kanisa, haja ya
kuwa waombaji wenye bidii, haja ya kujiandaa kwa ujio wa Bwana, unyakuo na
kadhalika. Karibu kwenye Sehemu ya 1 ya ushuhuda huu wenye nguvu ambao, kupitia
humu, Bwana atasema na moyo wako na kukupatia msukumo mwingine wa kusonga mbele
zaidi katika safari hii ya kiroho katika maisha haya ya kimwili.
...........................
Bwana anasema, “Natuma ujumbe huu kwa watu wangu walioko duniani, maana
Mimi nakaa kwenye ulimwengu wa roho.”
Ufunuo 4:1
Baada ya hayo naliona, na tazama, mlango
ukafunguka mbinguni, na sauti ile ya kwanza niliyoisikia kama sauti ya baragumu
ikinena nami, ikisema, Panda hata huku, nami nitakuonyesha mambo ambayo hayana
budi kuwako baada ya hayo.
Ufunuo 5:11-12
Nikaona nikasikia sauti ya malaika wengi pande
zote za kile kiti cha enzi, na za wale wenye uhai, na za wale wazee, na hesabu
yao ilikuwa elfu kumi mara elfu kumi na elfu mara elfu, wakisema kwa sauti kuu,
Astahili Mwana-Kondoo aliyechinjwa, kuupokea uweza na utajiri na hekima na
nguvu na heshima na utukufu na baraka.
Tafadhali Kanisa
sikilizeni kile ambacho kilitokea maishani mwangu. Bwana alianza kushughulika
nami kupitia kwenye ndoto. Nakumbuka
katika ndoto ile, nilitoka kwenye nyumba yangu. Nilitembea kwenye mitaa yangu
ya jirani na nilihisi kama kuna mtu alininyanyua kwa mikono yangu hadi juu
mawinguni na nilikuwa nakimbia kwenye mawingu huku nikimtukuza Mungu. Nuru kali
sana ilinijia na sauti kutokea humo ilisema, “Ricardo,
Ricardo. Acha kazi yako maana kuna jambo nataka kufanya na maisha yako pamoja
na Kanisa langu lililoko duniani.” Baada ya kusikia maneno haya,
nilitetemeka sana na kuamka kutoka usingizini. Niliinuka na kuanza kumlilia
Mungu na kumwuliza, “Hii ni nini, Bwana?”
Sauti ile ilinijia kwa
nguvu sana. Ilinijia kwa siku nyingi. Kisha nililala tena na kuota ndoto ileile
na Bwana alirudia ujumbe uleule kwangu. Kila ilipokuja nikawa naamka napiga
kelele kwa sababu sauti ya Mungu inakuwa inakuja kwa nguvu zaidi. Na ninapoamka
ninatetemeka, ninapiga kelele na wazazi wangu wananiuliza, “Kuna nini?” Nikawa nawasimulia ile ndoto na mama yangu aliniombea
na kuniambia, “Kama ni Bwana anasema na
wewe, basi atakupatia ufahamu wa kuelewa.”
Tuliendelea kuomba usiku
kucha hadi ilipofika wakati wangu wa kwenda kazini asubuhi iliyofuata. Mama
yangu aliniambia nijiweke tayari kwenda kazini. Tulimwomba Bwana ishara ili
tujue iwapo alikuwa ni Yeye aliyezungumza nami au la. Nilioga, nikajiandaa,
kisha nikaenda kazini. Nilikuwa nikifanya kazi “Chile Laboratories.”
Kwa kweli niliipenda kazi
yangu. Nilikuwa nikichukuliwa na gari kutoka kituoni na kwenda kazini.
Niliposhuka tu kwenye gari, mtu mmoja alinimbia, “Unafanya nini hapa? Hautakiwi kuendelea kuwapo mahali hapa.”
Kwa mara kadhaa, watu
wengine nao waliniambia jambo hilohilo. Cha ajabu ni kuwa hata hawakuwa
wameokoka. Hii ndiyo ishara ambayo Bwana alinipa. Baada ya ishara ile, niliamua
kwenda kwa bosi wangu kuacha kazi. Nilimwambia, “Ni lazima niondoke kwenye kampuni hii kwa sababu Mungu ameniambia
nifanye hivyo.” Bwana akitoa amri ni LAZIMA tutii. Bosi wangu akawa na
wasiwasi na mimi, akaniuliza, “Utaenda
kufanya nini sasa? Utapata wapi kazi nyingine nzuri kama hii?” Nikamwambia
kuwa ni lazima nimtii Mungu. Kwa hiyo, waliandaa sherehe ya watu elfu mbili kwa
ajili ya kuniaga mimi. Baada ya hapo, nilikusanya kila kitu changu na kuelekea
nyumbani.
Nilipofika nyumbani huku
ningali nalia, mama yangu alikuwa tayari ananisubiri kwenye kibaraza cha mbele
ya nyumba. Nilimwambia kuwa nimeacha kazi kwa sababu Bwana amethibitisha ndoto
yangu kupitia watu wale. Akajibu, “Kama
Bwana amesema nawe, basi na ayatumie maisha yako kama apendavyo.” Tuliingia
ndani ya nyumba na kuongea hadi usiku ukaingia. Kisha nikamwambia kuwa nahitaji
kwenda kulala kwa sababu Mungu atasema nami ndotoni usiku ule.
Nilidhani Bwana
angezungumza nami ndotoni lakini hakufanya hivyo kama nilivyowaza. Lakini
alikuwa anaenda kushughulika nami kwa njia tofauti. Nilipoenda chumbani kwangu
na kuvua nguo zangu, chumba kilianza kutikisika. Nikaanza kupiga kelele, “Kuna tetemeko linalopiga hapa Santiago,
Chile.” Nilijaribu kutoka kwenye chumba changu; lakini mtu nisiyemwona
alikuwa akinizuia kutoka mlangoni. Niliweza kuwaona mama na ndugu zangu nje ya
chumba; na nikapiga kelele za kuomba msaada lakini hakuna aliyekuwa akinisikia.
Sasa najua kuwa yule aliyekuwa haonekani alikuwa ni malaika wa Bwana. Nilirudi
nyuma na kulala kitandani na kumlilia Mungu, huku nikimwomba anieleze kile
kilichokuwa kikiendelea pale.
Ndipo nikasikia sauti ya
waziwazi ikisema nami. Roho Mtakatifu alianza kusema na mimi kwa sauti nzuri
sana. Aliniambia, “Ricardo, kwa kuwa sasa
umeshaacha kazi yako, nataka uende Kanisani na ukaombe kwa saa saba kwa siku
kila siku kwa ajili ya maisha yako, na kwa ajili ya Kanisa langu duniani.”
Bwana alipomaliza
kuzungumza, chumba kiliacha kutikisika. Ndipo nikanyosha mkono wangu kupitia
mlangoni nikagundua kuwa kumbe sasa naweza tena kutoka. Nikakimbia hadi kwa
mama yangu na kusema, “Nimesikia sauti ya
Roho Mtakatifu!” Nikatoka nje ya nyumba na kuanza kusema hivyo kwa sauti ya
juu kule nje.
Baadhi ya watu hawaamini
kuwa Mungu bado anazungumza na wanadamu leo; lakini nakuambia anafanya hivyo
kabisa! Kama Bwana alizungumza na Ibrahimu, bado anaweza kuzungumza nasi,
Kanisa lake, leo! Nilienda Kanisani na kuzugumza na askofu na tukakubaliana
kufungua kanisa kila siku saa mbili asubuhi ili niweze kuomba na kutii agizo la
Mungu. Kila asubuhi nikawa nakwenda kuomba kwa saa moja, mbili na inapofika ya
tatu, nakuwa sina tena kitu cha kuomba. Nikawa namwuliza Mungu, “Bwana, niombee nini tena sasa? Bado nina
saa nne mbele!”
Kisha, nikasikia ngurumo
chini ya ardhi ikianzia mlango wa nyuma wa kanisa. Nilihisi kanisa likiyumba
toka kushoto hadi kulia kama mtu aliyelewa. Wakati huu, Bwana aliongea nami kwa
sauti ya wazi kabisa lakini si kwa sauti aliyotumia kwenye ndoto hapo kabla.
Sauti aliyosema nami kabla ilikuwa ya mamlaka. Safari hii aliongea kwa sauti ya
huzuni na masikitiko. Alisema, “Ricardo, Ricardo,
ombea Kanisa langu! Kanisa langu haliko tena kama lilivyokuwa!! Kanisa langu
limepoteza imani yake. Kanisa langu haliniamini Mimi wala kuamini juu ya uwepo
wangu! Liambie Kanisa langu kwamba Mimi nipo!! Liombee Kanisa langu, maana
Kanisa langu haliombi wala kufunga tena!” Hatimaye ule mtikisiko ukakoma
baada ya kuwa amemaliza kuongea nami.
Ndipo na mimi nikaanza
kuombea Kanisa huku nikitembea humo kanisani kwa saa zile nne zilizobakia;
nikiomba watu wa Mungu waamke.
Alhamisi ya wiki ya pili
ya maombezi, niliamka nilikuwa na maumivu makali sana ya mifupa na maungio
hivyo sikutaka kuamka. Mama yangu alikuwa ananiamsha ili niende kanisani
kuomba; lakini nililalamika kuwa mwili wangu na mifupa yangu ilikuwa na
maumivu. Kwa hiyo badala yake alipendekeza niombee nyumbani. Lakini
nikamkumbusha kwamba Mungu alisema kuwa natakiwa kuombea kanisani. Kwa hiyo,
aliniandalia nguo na akanipeleka kanisani. Asubuhi ile walikuwapo watu wengi
wakiomba kanisani na nikaomba waniombee kwa sababu ya yale maumivu ya mwili.
Niliwaambia kuwa nilikuwa najisikia mdhaifu sana kuomba. Kwa hiyo, walinipaka
mafuta na kuniombea, nami nikapokea nguvu isiyo ya kawaida kutoka kwa Mungu!!
Haleluya! Nilianza kuomba nikitembea, huku nikimwomba Mungu rehema kwa ajili ya
taifa la Chile na familia na watu wanaotumia dawa za kulevya na Kanisa.
Nilimaliza maombezi, kisha
nilirudi baadaye jioni kwa ajili ya ibada. Baada ya baraka za askofu, niliinua
mikono yangu na nikahisi kuna mtu amepita na kunigusa mgongoni. Hapo nilipotewa
na nguvu zote na kuanguka sakafuni. Askofu aliuliza kuna tatizo gani kwangu
nami nikamwambia kuwa sijui, sina tu nguvu na hata kuongea naongea kwa shida.
Kisha Kanisa lilinizunguka na kuanza kunena kwa lugha na kupaza sauti. Matokeo
yake, baadhi ya waumini waliweza kumwona malaika aliyekuja na kunitaka nitoke
kwenye mwili wangu. Askofu akasema, “Hautatoka
kwenye mwili wako!” Aliposema hivi, yule malaika akaacha kuniashiria nitoke
kwenye mwili wangu. Unajua, mtu yeyote mwenye mamlaka katika Yesu ataheshimiwa
na malaika wa Bwana.
Ndipo askofu aliniuliza
mimi, “Malaika anataka kukutoa kwenye
mwili wako kwa muda gani?” Nilimwuliza yule malaika, “Unataka kunichukua kwa saa moja? Mbili? Saa tatu?” Malaika
akajibu, “Hapana. Hautakuwapo kwa saa 8
ili ukamwone Yesu kwenye mbingu ya tatu, maana anataka kuzungumza na wewe.”
Halafu malaika akaniambia, “Si mimi
nitakayekusindikiza hadi mbinguni, maana mimi ni malaika wako mlinzi ambaye
nimekuwa ninakulinda kwa siku zako zote ambazo umeishi hapa duniani. Malaika
wawili watakuja kutoka mbinguni ili wakuchukue hadi mbingu ya tatu usiku wa
manane.” Nilimweleza haya askofu na akaamua kunipeleka kwa gari ya
ndugu mwingine hadi kwenye nyumba ya
mchungaji iliyo kwenye ghorofa ya pili. Nilipolala kwenye chumba, tulisikia
mbwa wakibweka na watu wakipiga mayowe.
Baada ya kurudi,
nilielezwa kuwa watu wawili wakiwa na mavazi meupe walionekana katikati ya mtaa
na kutembea hadi kwenye ghorofa ya kwanza ya jengo lile na kuja hadi kwenye
ghorofa ya pili nilikokuwa. Malaika hawa walikuwa wazuri sana. Walikuwa na
nywele nyeupe zinazomeremeta; nyeupe kuliko theluji, na macho yao yalikuwa na
maumbo ya lulu. Ngozi zao zilikuwa laini kama za watoto wachanga lakini miili
yao ilikuwa ina misuli kama ya watu wanaojenga misuli. Malaika hawa wana nguvu
sana!!!
Nilimweleza askofu kuwa
wale malaika wameshafika na kwamba wametumwa kunipeleka mbinguni. Malaika mmoja
alianza kutoa ishara ili niweze kutoka ndani ya mwili. Wakati hili linatendeka,
mifupa yangu ilianza kuhisi maumivu tena. Kwa hiyo, ndugu zangu katika Kristo
waliokuwa karibu yangu walianza kusugua mwili wangu na kuniambia kuwa ulikuwa
unapoa kama barafu. Kisha wakaenda kuchukua vipasha joto ili kuupasha moto
mwili wangu tena.
Malaika walipokuwa
wakiniita nitoke nje ya mwili wangu, nilianza kujisikia kukata tamaa na nikawa
najisogeza kutoka upande mmoja hadi mwingine. Nilianza kuhisi mauti inazidi
kufunika mwili wangu. Nikawapazia sauti wapendwa katika Kristo, “Msinizike!
Nitarudi!”
Nilitoka kwenye mwili
wangu na kuruka kitandani mwangu. Niliwaona ndugu zangu katika Kristo
wakigusagusa mwili wangu na kusema, “Ameshaondoka.
Ametoka kwenye mwili wake.” Lakini nilikuwa hapo tu pembeni yao huku
nikiwaambia, “Niko hapa!” Hata hivyo,
hawakuweza kuniona wala kunisikia maana nilikuwa na mwili wa kiroho
usioharibika. Walianza kuufunga mwili wangu kwa blangeti.
Mmoja wa wale malaika
akaniambia, “Ni wakati wa kuondoka, maana
Bwana anakusubiri!” Kila malaika alinishika mkono mmoja na wakaninyanyua
kuelekea mbinguni huku tukiwa tunakatisha kwenye anga kwa kasi kubwa mno.
Nakwambia hivi, hata kama huamini haya, Yesu Kristo wangu ni halisi na yu hai
milele!!
Baadaye Bwana alipokuja
kuniambia nirudi kwenye mwili wangu, nilimwambia, “Ni nani duniani ambaye ataniamini? Acha tu nibaki na Wewe hapa!!
Hakuna mtu atakayeamini ufunuo huu. Hakuna atakayeamini haya kwa kuwa hawana
imani! Ukosefu wa imani duniani ni mkubwa sana. Ni nani atakayeamini mambo
haya?” Bwana akaniambia, “Yupo mtu ataamini
hadithi yako. Wale tu walio kwenye Kanisa langu la kweli watakuamini.”
Nilipotoka kwenye mwili
wangu usiku ule na nikawa napaa kwa kasi ya ajabu kwenda kumtembelea Bwana,
niliweza kutazama chini kwenye dunia. Kisha nilipita karibu kabisa na mwezi;
mwezi huu unaoangazia dunia wakati wa usiku. Halafu niliweza kuliona jua na
ukubwa wake kwa macho yangu. Niliweza kuona ndimi za moto zikilipuka na kupasha
joto dunia. Tuliendelea kupaa na nikaona nyota nyingi kadiri tulivyopita. Mungu
aliniruhusu nione jua, mwezi na nyota kwa makusudi maalum. Makusudi hayo ni
kuwaambia ninyi nyote kuwa Mungu wetu ni Muumba Mkuu wa ulimwengu wote!!! Yeye
si mdogo hata kidogo!
Tuliendelea kusafiri kwa
kasi sana hadi tukafika mahali ambako hakuna nyota hata moja. Hakuna kitu, ni
giza tu. Nilitazama chini na kuziona nyota zote chini yangu. Nikaanza kuogopa
na kuwauliza malaika, “Mnanipeleka wapi? Tafadhalini mnirudishe duniani kwenye
mwili wangu!” Kisha waliniminya kwa nguvu na kuzungusha miguu yao
mmojammoja kwenye miguu yangu na kunishikilia. Nilianza kuinama katika mkao
ambao ni kama wa hatari kwa sababu ya hofu. Malaika wakasema, “Kaa kimya! Tunakupeleka kwenye mbingu ya
tatu ambako Yesu anakusubiri ili azungumze nawe!” Wale malaika walisimama,
na wakati huo nilikuwa naangalia kila upande lakini sikuona kitu chochote
kilichoumbwa. Sijui nilikuwa wapi lakini nadhani ilikuwa ni kwenye mbingu ya
pili.
Nilikuwa najikakamua
katika mkao wa hatari wakati malaika wamenishikilia na nilihisi na kusikia
sauti ya kutisha kama vishindo vya watu wakikimbia. Malaika walinishikilia kwa
nguvu na kusema, “Ricardo, usiogope. Yesu
yuko pamoja nasi!” Wakati wakiongea, pia walisema, “Geuza kichwa chako na utazame juu!”
Nilishangazwa na kile
nilichokiona maana kulikuwa kama na viumbe wanajongeajongea juu yetu. Mmoja wa
wale malaika akasema, “Tazama,
tutakuonyesha kile unachokitazama juu yetu!” Na mmoja wao akafanya ishara kwa
mkono kutokea upande mmoja hadi mwingine na anga lote juu yetu likajaa nuru.
Baada ya kutokea kwa ile nuru, hakukuwa na kingine zaidi ya mapepo na mashetani
wakiwa wamejaa kwenye anga lote. Bwana aliwakemea wote kwa Jina la Yesu!!
Biblia ni ya kweli!! Kila kinachoendelea kwenye dunia hii ni kile unachoona
kwenye Ufunuo. Yesu anakuja hivi karibuni!! Nawezaje kuwafanya muamini hili? Ni
hivi karibuni sana!!
Niliwauliza wale malaika, “Hapa ni wapi?” Mmoja wao akajibu, “Huu ni ulimwengu wa roho wa giza anakoishi
shetani na mapepo yake.” Nikaanza kusema, “Kumbe ndiyo maana kuna uovu mwingi sana duniani! Haya mapepo huja
duniani kutokea hapa na kusababisha uharibifu wa kila namna na uovu miongoni
mwa wanadamu. Dunia imejaa mapepo!!” Kuna mamilioni kwa mamilioni ya
mapepo. Idadi yao haihesabiki.
Kisha malaika walianza kuniashiria nitazame kwa makini zaidi na wakanionyesha nyuso za viumbe hawa; na kumbe
wengi
wao tayari tunaonyeshwa kwenye televisheni. Viumbe hawa walikuwa ni majitu ya
kutisha!! Niliwaona akina Thundercat na Power Rangers na viumbe vingine ambavyo
huonekana kwenye sinema za mambo ya kutisha (horror movies). Watengenezaji wote
wa sinema na vikatuni hivi wana mikataba na ibilisi ili kutengeneza vitu hivi
kwa
ajili
ya televisheni na sinema!! Michoro yote hiyo hutoka kwenye ulimwengu wa roho wa
giza niliouona. Kwa nini unadhania siku hizi watoto ni wakaidi kiasi hicho?? Ni
kwa sababu yale mapepo huwaingia watoto wako pale wanapotazama televisheni
zinazoonyesha picha hizo.
Ndiyo maana tunatakiwa
kujifunza namna ya kuwafundisha watoto wetu jinsi ya kupambanua kipi cha
kutazama na kipi si cha kutazama kwenye televisheni. Malaika aliniambia kuwa
yote hayo ni mambo halisi kabisa. Mapepo haya yapo na watu wanafanya mikataba
na ibilisi ili kuyaleta duniani.
Mapepo hayo yalianza
kunilaani mimi, kanisa, na Baba, na Bwana Yesu na dunia kwa sababu hayamheshimu
Mungu wala viumbe wake wowote. Kisha nililiona kabisa pepo linaloitwa Hugo,
ambaye ni katuni maarufu kule Chile. Alikuwa anatisha sana kumwangalia. Alikuja
karibu yangu na kuniambia, “Tutaenda
duniani kote na kuwaua watoto wote!”
Kwa nini unadhani watoto
wanaua watoto wenzao? Ni kwa sababu baadhi yao husema kuna kitu kilikuja kutoka
kwenye televisheni na kuniambia nifanye hivi au vile. Mapepo haya yanapandikiza
chuki duniani. Bwana na aiokoe na kuitakasa Chile!!
Mmoja wa wale malaika
akaniambia, “Endelea kutazama!” Na
yale mapepo yakasema, “Tumejaribu
kuliharibu Kanisa lakini hatuwezi kwa sababu kila tukiua mmoja, basi maelfu
wanaibuka kujazia kwenye kifo hicho!” Tangu mwanzo wa Kanisa, shetani
amejaribu kuliangamiza, yaani Kanisa linalohubiri Injili ya kweli na kutenda
kazi ya Mungu, lakini hawezi kwa sababu Bwana Yesu anatulinda! Utukufu kwa
Mungu!
Kisha mapepo yakasema, “Hebu tufanye jambo jipya. Hebu tukaingie
ndani ya makanisa, maana wapo wengi ndani humo ambao ni mali yetu! Tutaenda
kuwatumia watu hawa kueneza uzushi na migawanyiko miongoni mwa ndugu
makanisani. Tutasababisha makanisa kuanguka kupitia uzushi na Roho Mtakatifu
atahuzunishwa na kuliacha Kanisa.” Shetani anaenda kila mahali akitafuta
kuwaharibu wale wanaopenda haki ya Mungu, kama inavyosema kwenye andiko hili:
Mwe na kiasi
na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye,
huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze.
Sikutaka kuendelea
kuangalia mambo yale zaidi. Lakini malaika aliniambia niendelee kutazama
matukio yaliyokuwa yanatokea. Niliona mapepo yakiruka kila mahali wakati nyota
moja inayong’aa ilipokuwa inakuja.
...........................
Bwana akubariki msomaji wa
blog hii. Karibu kwenye sehemu ya 2 na ya mwisho ya ushuhuda huu katika makala
yatakayofuata.
No comments:
Post a Comment