MAANA
YA DINI
Kamusi
ya Kiswahili Sanifu (Oxford: 2004) inaeleza neno ‘dini’ kama mfumo fulani wa
imani inayohusiana na mambo ya kiroho na njia ya kuabudu, kusali au
kuheshimu/kutii Muumba.
Kwa
hiyo tunaweza kusema kwa kifupi kwamba, dini ni utaratibu anaotumia mwanadamu
katika kumwabudu Mungu.
Zipo
dini mbalimbali duniani. Japokuwa zote zinaweza kusema zinamwabudu Mungu
aliyeumba vitu vyote, lakini kile kinachozitofautisha ni “utaratibu” zinazotumia
katika huko kumwabudu Mungu – ndiyo sababu zikawa ni dini au madhehebu mbalimbali.
Utaratibu
maana yake ni kanuni mahususi zinazotakiwa kufuatwa katika kufanya jambo
fulani. Mathalani, unapotaka kujiunga na chuo, utatakiwa kulipa gharama za
usajili, kujaza fomu, kufanya hivyo katika muda maalum, kuwasilisha maombi yako
kwenye ofisi maalum, nk. Hali kadhalika kwa upande wa dini, ili muumini
ahesabike kuwa ametekeleza ibada kwa Mungu, upo utaratibu au kanuni mbalimbali
zinazotakiwa kufuatwa. Kanuni hizo ni pamoja na:
- Kusema sala maalum;
- Kusema sala mara idadi maalum;
- Kusimama au kukaa kwa wakati maalum;
- Kuvaa mavazi maalum;
- Kutazama welekeo maalum; n.k.
YESU
ALIANZISHA DINI GANI?
Ukisoma
Biblia kwa makini, utagundua kwamba Yesu Kristo hakuanzisha Ukristo kama dini au
madhehebu. Wakati Bwana Yesu alipokuja, kulikuwa na dini ya Kiyahudi (Judaism).
Hii ni dini ambayo ilikuwa na utaratibu wake wa kumwabudu Mungu kama ilivyo
kawaida ya dini yoyote kuwa na utaratibu.
Lakini
ni wazi kwamba, Bwana Yesu hakukubalika kabisa ndani ya dini hii. Walikuwa ni wakuu
wa dini hiyohiyo ndio waliomshitaki Bwana na kuwachochoea watu wa kawaida
waanze kupiga kelele za kusema: asulubiwe, asulubiwe! Kati ya mashtaka yao,
walisema: Sisi tulimsikia akisema, Mimi nitalivunja hekalu hili lililofanyika
kwa mikono, na katika siku tatu nitajenga jingine lisilofanyika kwa mikono.
(Mk. 14:58).
Lakini
ni kwa nini walikuwa hawamtaki? Ni kwa sababu alikuwa anaonekana anavunja
utaratibu wa dini. Pia ni kwa sababu alionekana kujizolea umaarufu mwingi
kuliko wakuu wa dini. Kwa hiyo, waliona kwamba nafasi zao ziko hatarini. Kwa hiyo,
walimchukia na kumtungia hila nyingi ili waweze kupata sababu ya kumwua.
Tunaona
jambo hilohilo hata baadaye katika huduma ya mtume Paulo. Kabla ya kuokoka,
Paulo alikuwa ni mshika dini ya Kiyahudi. Yeye mwenyewe anasema kwamba: Nami
naliendelea katika dini ya Kiyahudi kuliko wengi walio hirimu zangu katika
kabila yangu, nikajitahidi sana katika kuyashika mapokeo ya baba zangu. (Gal.
1:14).
Lakini
pale alipoitwa na Bwana Yesu kwenye huduma, mambo yaligeuka kabisa. Wayahudi
walitafuta kumwua Paulo kwa sababu waliona kwamba tayari yuko kinyume na dini
yao. Mathalani, Paulo alipokuwa ameshikiliwa na utawala wa Kirumi, mjomba wa
Paulo alienda kumwambia jemadari wa Kirumi kwamba: ...Wayahudi wamepatana
kukuomba umlete Paulo chini kesho, ukamweke mbele ya baraza, kana kwamba
wanataka kupata habari zake kwa usahihi zaidi. Basi wewe usikubali; kwa maana
watu zaidi ya arobaini wanamwotea, wamejifunga kwa kiapo wasile wala wasinywe
hata watakapomwua; nao sasa wako tayari wakitazamia ahadi kwako. (Mdo.
23:20-21).
Na
ndiyo maana baadaye Paulo anasema: Maana, sasa je! Ni wanadamu ninaowashawishi,
au Mungu? Au nataka kuwapendeza wanadamu? Kama ningekuwa hata sasa nawapendeza
wanadamu, nisingekuwa mtumwa wa Kristo. (Gal. 1:10).
Hapa
Paulo anamaanisha kwamba, kabla ya kumjua Kristo alikuwa ni mshika dini tu
ambapo wakati huo uhusiano wake na washika dini ulikuwa wa amani kabisa. Lakini
baada ya kuachana na dini, ndio maana wakamchukia. Na anasema sasa, kama
angekuwa bado anawapendeza wanadamu wale washika dini, basi asingekuwa
anateseka hivyo kwa ajili ya Kristo.
Mtume
Paulo anaonyesha kwamba kutoka kwenye dini kwa ajili ya Kristo kuna neema
kubwa. Anasema: Lakini Mungu, aliyenitenga tangu tumboni mwa mama yangu,
akaniita kwa neema yake, alipoona vema kumdhihirisha Mwanawe ndani yangu, ili
niwahubiri mataifa habari zake. (Gal. 1:15-16).
Kumbe
Mungu anaita dini kuwa ni mapokeo ya mababa (Gal. 1:14). Na kumbe, alipomwita
Paulo katika huduma, hakutaka Paulo abakie tena humo ndani ya dini. Na kwa kuwa
sasa Paulo alitoka nje ya dini, alijikuta akizalisha maadui wengi sana.
Watu
waliokuwa wakimpinga Bwana Yesu na wale waliompinga Paulo hawakuwa wakitetea
maslahi ya kisiasa, bali walikuwa wakitetea dini yao.
Hata
hivyo, sote tunafahamu kwamba Mungu alikuwa anawaridhia kikamilifu Bwana Yesu
na Paulo. Swali la muhimu la kujiuliza ni kwamba, ndani ya dini kuna nini
ambacho hakimpendezi Mungu; na nje ya dini kuna nini ambacho ndicho anaonekana
kutaka sisi tukiendee?
WATAKATIFU
WOTE WALIKUWA NA DINI KAMA ZETU?
Ni
muhimu kukumbuka kwamba, wakati wote Bwana Yesu alipokuwa akiendesha huduma
yake hapa duniani, hakukuwako na Ukristo kama dini. Maana maandiko yanasema: Na
wanafunzi waliitwa Wakristo kwanza hapo Antiokia. (Mdo. 11:26).
Sasa
swali ni kwamba kama Yesu na mitume wake hawakukubalika katika dini ya Kiyahudi
na wakati huohuo Ukristo kama dini haukuwapo, je, Yesu pamoja na mitume wake
waliokufa kabla ya kuanza kwa Ukristo kama dini walikuwa watu wa dini gani?
Maana wangekuwa ni wa dini ya Kiyahudi kama Wayahudi wengine, wasingechukiwa
wala kuuawa. Lakini hapohapo hawakuwa na dini ya Kikristo, maana dini hiyo
haikuwapo!
Swali
jingine ni kwamba, mababa wa zamani kabla ya Musa, yaani akina Ibrahimu, Isaka
na Yakobo, ambao leo wako mbinguni, walikuwa wa dini gani; maana dini ya
Kiyahudi ilianza na Musa pale kwenye mlima wa Sinai? Je, watakatifu hao
walienda mbinguni kwa tiketi gani?
NINI KINACHOTAKIWA?
Ni
jambo gani ambalo Mungu anataka tufahamu kuhusiana na dini na madhehebu? Je,
vitu hivyo vina nafasi gani katika uhusiano wetu na Mungu?
Jibu
ni kwamba, Bwana Yesu hakuja kuleta dini. Mbele za Mungu dini ni aina ya maisha
ndani ya mtu yaliyotawaliwa na utii wa sheria za Mungu; na sio kuitwa mshirika
wa madhehebu fulani. Maandiko yanasema: Dini iliyo safi, isiyo na taka mbele za
Mungu Baba ni hii, Kwenda kuwatazama yatima na wajane katika dhiki yao, na
kujilinda na dunia pasipo mawaa. (Yak. 1:27).
Je,
ni lazima uwe mshirika wa madhehebu fulani ili ufanye mambo haya? Bila shaka
jibu ni hapana! Kinachotakiwa ni kuwa tu na Neno la Kristo moyoni, kisha
unalitii. Dini kwa maana ya madhehebu zilianzishwa na wanadamu.Lakini mbele za Mungu, dini ni aina ya maisha yanayompendeza Mungu na si kuwa mshirika wa kundi lenye jina na taratibu fulani.
Yesu anaita kwa nguvu akisema: Njoni kwangu ninyi
nyote wenye kulemewa na mizigo nami nitawapumzisha. (Mt. 11.28). kwa nini
anasema hivyo? Anasema: Mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele.
(Yoh. 10:10).
Tunatakiwa kukimbilia kwa Bwana Yesu mwenyewe; si
kwenye dini. Je, hakuna watu wa dini wanaoingia motoni? Jibu ni kwamba wapo. Kwa
nini waende motoni na huku wana dini? Ni kwa sababu unaweza kuwa na dini lakini
ukawa huna Yesu. Na hiki ndicho kinachotokea kwa watu wengi. Wengi wameridhika
na kuwa na dini wasijue kwamba hilo si hasa kusudi la kuishi kwetu hapa
duniani.
Lakini hakuna mtu aliye na Yesu ambaye anakwenda
motoni! Bwana mwenyewe anaahidi wazi kabisa: Kondoo wangu waisikia sauti yangu;
nami nawajua, nao wanifuata. Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea
kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu. (Yoh. 10:27). Haleluya!
Dini ni mzigo juu ya mabega ya watu. Ni taratibu
zilizoanzishwa na wanadamu na kuendelea kurithishwa kutoka kizazi hadi kizazi. Mojawapo
ya washika dini wazuri sana walikuwa ni mafarisayo. Kwa mfano, walikuwa
wakishika kwa uaminifu sana utaratibu wa kutokula bila kunawa mikono. Kwa hiyo,
siku moja walimkabili Bwana Yesu na kumwambia: Mbona wanafunzi wako huyahalifu
mapokeo ya wazee, kwa maana hawanawi mikono walapo chakula. (Mt. 15:1).
Kumbuka kwamba hapa hawaongei juu ya kanuni za afya
bora, la hasha! Wanaongelea utaratibu wa kidini. Bwana akasema: Mbona ninyi
nanyi huihalifu amri ya Mungu kwa ajili ya mapokeo yenu? (Mt. 15:3). Unsona? Haya
mapokeo ni yao; si ya kutoka kwa Mungu! Ukiendelea kusoma, utaona kwamba
hatimaye Bwana anawaambia hawa washika dini: Enyi wanafiki, ni vema
alivyotabiri Isaya kwa habari zenu, akisema, Watu hawa huniheshimu kwa midomo;
ila mioyo yao iko mbali nami. Nao waniabudu bure, wakifundisha mafundisho
yaliyo maagizo ya wanadamu. (Mt. 15:7-9).
Kumbe tunaweza tukawa tunaenda kwenye nyumba za
ibada, lakini tukawa tunafundishwa maagizo ya wanadamu!! Na kwa kuyafuata hayo
tunaweza kuwa tunamwabudu Mungu bure! Inatisha kama nini! Ukisikia kazi ya
hasara, basi ni pamoja na hii!
Rafiki, kwenye dini kumejaa maagizo ya wanadamu. Tena
msisitizo mwingi umo kwenye hayo maagizo badala ya kuwa kwenye maagizo ya
Mungu.
JE, TUACHE KUWA NA DINI?
Ninaomba
nieleweke kuwa, sisemi hata kidogo kwamba kuwa na dini au madhehebu ni vibaya.
Ni vizuri, tena ni muhimu kabisa. Dini zinatusaidia kukusanyika pamoja na
kupata mafundisho kutoka kwa walimu na wachungaji; kusaidia katika maisha;
kutiana moyo katika safari ya kiroho humu duniani, n.k.
Ninachomaanisha
ni kwamba, ni lazima tutambue kwamba dini inatakiwa
ifuate Neno la Mungu (Biblia) na si Neno lifuate dini au dhehebu!
Maana
yake ni kuwa kama dhehebu au dini inafundisha kitu kilicho nje ya Neno, kufuata
mafundisho hayo ni kujitia hatarini. Kumbuka kwamba Biblia inasema katika Hosea
4:6 kwamba, Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa. Sio wanaangamia,
hapana! Wanaangamizwa! Unadhani anayewaangamiza ni nani? Ni walimu wa uongo.
Yesu
Kristo ndiye anayetakiwa kuwa namba moja katika maisha yetu kabla ya vitu
vyote. Kama dini hainiwezeshi kufikia lengo hilo, basi kuna haja gani ya
kushikilia taratibu ambazo hazinisaidii; ambazo mwisho wa siku nitaingia upotevuni?
Kumbuka
siku zote kwamba, wito wa Bwana Yesu ni: Njoni kwangu
ninyi nyote wenye kulemewa na mizigo nami nitawapumzisha. (Mt. 11.28). Sio
nendeni kwenye dini!
Utajuaje kwamba
dini haikusaidii? Angalia matunda maishani mwako. Unazaa matunda gani katika
maisha yako.
Imeandikwa: Je!
Watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti? Vivyo hivyo kila mti
mwema huzaa matunda mazuri; na mti mwovu huzaa matunda mabaya. Mti mwema
hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri. (Mt.
7:16-18).
Matunda mabaya
ni yapi? Imeandikwa: Kwa maana, ndani ya mioyo ya watu hutoka mawazo mabaya,
uasherati, wivi, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya, ukorofi, hila, ufisadi, kijicho,
matukano, kiburi, upumbavu. Haya yote yaliyo maovu yatoka ndani, nayo yamtia
mtu unajisi. (Mt. 7:20-23).
Pia imeandikwa:
Basi matendo ya mwilini dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada
ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda,
ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo ... (Gal. 5:19-21).
Jichunguze maisha
yako na kujipima wewe binafsi. Je, dini uliyonayo imeweza kukutoa katika mambo hayo? Kama sivyo,
utaponaje? Kama sivyo, mwisho wake ni nini?
HITIMISHO
Kila mwanadamu
anamhitaji Yesu Kristo maishani mwake. Yeye anakupatia Roho wake Mtakatifu. Na Roho
Mtakatifu anapokuja ndani ya maisha ya mtu, maandiko yanasema: Lakini tunda la
Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole,
kiasi, ... (Gal. 5:22).
Ukiwa na Yesu
maishani mwako kibinafsi, ndipo dini yako itakuwa na maana. Bila Yesu, dini ni
mzigo usio na maana wala msaada wowote kwake yeye aliye nayo. Unakuwa unafanya
kazi tu ya kutekeleza maagizo ya wanadamu; na mwisho wa yote ni kuingia
upotevuni. Dini haiwezi kubadili maisha yako na kukufikisha kwenye utakatifu
anaotaka Mungu. Maana imeandikwa: Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu
wote, na huo utakatifu, ambao hakuna mtu atakayemwona Mungu asipokuwa nao. (Ebr.
12:14).
Kwa lugha
rahisi, utakatifu ni kitokuwa na dhambi. Dini haiwezi kukupa huo utakatifu. Kilichozaliwa
na mwili ni mwili na kilichozaliwa na Roho ni roho. (Yoh. 3:6). Mpokee Yesu
kama Bwana na Mwokozi wako ili uzaliwe katika Roho. Amin, amin, nakuambia, Mtu
asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu. (Yoh. 3:3). Kwa lugha
ya iliyozoeleka, kuzaliwa mara ya pili ni kuokoka. Pokea wokovu wa Kristo leo. Ukimkiri
Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu
alimfufua katika wafu, utaokoka. (Rum. 10:9).
Labda unasema, “Si
imeandikwa ‘utaokoka’, yaani baadaye?” Maandiko yanasema: ... wakati
uliokubalika nalikusikia, siku ya wokovu nalikusaidia; tazama, wakati
uliokubalika ndio sasa; tazama, siku ya wokovu ndiyo sasa. (2 Kor. 6:2).
Amka leo. Njoo kwa
Yesu upokee wokovu. Hatujaitwa kutumikia dini; tumeitwa kumtumikia Bwana Yesu!
very nice! because it only truth which will make people to be free, in this crazy world! may the sun of God Jesus Christ be with your work and you!
ReplyDeleteThank you emback for your comments. It's very true that we need the Truth in this life, which is Jesus Christ. Be so blessed.
ReplyDeleteGod is love
ReplyDelete