Sunday, October 14, 2012

Nilihisi kama Mungu Amenisaliti!
Utangulizi kutoka kwa blogger

Je, unahisi kuwa una huzuni kubwa isiyoweza kuondoka, umekata tama, unajiona huna maana, unahisi kama vile Mungu amekudanganya au amekuacha; unahisi kama vile  Mungu si wa kuaminiwa au Neno lake si la kuaminiwa, unahisi kuwa Mungu hasikii maombi yako, hakupendi; unahisi kwamba umeshapoteza wokovu wako, au unahisi kuwa umetenda sana dhambi kiasi kwamba Mungu hawezi kukusamehe tena?

Napenda nikuletee habari njema kwamba, bado liko tumaini, tena kubwa sana kwa ajili yako. Karibu usome ushuhuda huu ambao, si tu ni ushuhuda wa mpendwa aliyepita kwenye mapito kama hayo, lakini pia ni somo zuri mno kiasi kwamba, kama kawaida, Mungu anayo mengi ya kutufundisha kupitia mambo ambayo wengine walipitia kama sisi na wakashinda kwa neema ya Mungu ambayo iko kwa ajili ya kila mwanadamu, ukiwamo na wewe. Pendo la Mungu ni zaidi ya maji ya bahari, hivyo hakika kabisa unayo sehemu yako humo ambayo inakungoja uingie na kupokea.


Tatizo la wengi wetu ni ukosefu tu wa maarifa; tumempa shetani nafasi kubwa mioyoni mwetu – bila ya sisi kujua – kiasi kwamba amevuruga kabisa akilini na mawazo yetu; ametujaza giza lake la kuzimu na kutufanya tuhisi wakati wote kuwa wokovu ni mgumu sana na kwamba sheria ya Mungu ni ngumu mno.

Usikubali tena kudanganywa na ibilisi. Simama kwenye nafasi yako. Roho Mtakatifu yuko tayari saa 24 kutuchukua taratibu ila kwa uhakika hadi kwenye mwisho wenye ushindi USIO NA SHAKA HATA KIDOGO! Inua uso wako sasa uanze kusonga mbele kwa nguvu za Baba yetu wa mbinguni ambazo zimewekwa tayari kutuvusha kila bonde la uovu na mauti!

***********************

Ujumbe wa mhariri wa makala haya kwa Kiingereza: 
Tumeona ni vema kutotaja jina la mwandishi wa ushuhuda huu kwa sababu za usalama wake.  

Kama umewahi kuhisi kana kwamba Mungu amekusaliti, au tu ungependa kufahamu zaidi kuhusu ulimwengu wa giza na jinsi unavyoathiri Wakristo, tunapendekeza sana usome ushuhuda huu. Mwandishi wa ushuhuda huu si tu kwamba amepitia kile ambacho alikiona kama ni kusalitiwa na Mungu, bali pia alijifunza mambo machungu ... ambayo tunaamini yatawanufaisha wengi ambao nao wanahisi wako kwenye hali ambayo wanafikiri kuwa ni bora kuachana na Mungu.

*****************

Ushuhuda wenyewe
Niliingia kwenye Ukristo nilipofikisha miaka 18. Nilizaliwa kusini mwa Urusi. Nilimpenda sana Yesu, na nikawa na bidii sana Kanisani, nikabatizwa kwa Roho Mtakatifu na nikawa nawashuhudia watu Injili. Mungu amenibariki sana.

Mungu aliponibatiza kwa Roho Mtakatifu nilipata shauku kubwa sana ya kuwashuhudia watu habari za Yesu. Nilikuwa nikiongea Habari Njema za Yesu karibu kila siku. Nilijihisi niko karibu sana na Mungu. Nilitumia saa nyingi kuomba na kusoma Biblia.

Wakati fulani nilipatwa na jinamizi. Niliota kuwa ibilisi ananifukuza. Aliapa kuwa ni lazima atanipata. Nilipozinduka usiku ule, hofu haikuondoka. Badala yake ilizidi kuongezeka. Hofu iliongezeka sana kiasi kwamba nikawa nimechanganyikiwa kabisa. Nilijua kuwa niko katikati ya uovu. Nilikuwa chumbani kwangu, lakini ilionekana kana kwamba niko mahali pengine kabisa. Nilianza kuhangaika kuomba na kumsifu Mungu. Hili lilikuwa ni jambo pekee lililonifanya nibakie na akili zangu timamu. Niliomba karibia usiku kucha. Ile hali ya uovu ilikuja kuondoka asubuhi.

Nilipomsimulia jambo lile mmoja wa wamisionari wa Kimarekani kanisani kwangu, aliniambia kuwa ibilisi amefungwa na kuwa hana uwezo wa kumdhuru Mkristo yeyote. Nilikuwa sijawahi kufundishwa chochote kuhusiana na vita vya kiroho na sikujua kuwa nilitakiwa kufanya kitu ili kumpinga adui. Nimekuja kujifunza ukweli huo kwa njia ngumu kabisa. Ni miaka mitatu baadaye ndipo nilipofahamu kuwa ibilisi yu hai na yuko duniani; na anachukia sana na kushindana na kila mmoja anayeamua kuyatoa maisha yake kwa Yesu Kristo.

Muda mfupi baada ya kupata ubatizo wa Roho Mtakatifu, kwa ndani moyoni, nilianza kujiona kuwa mimi nilikuwa mtu  maalum sana kwa Mungu kuliko Mkristo mwingine yeyote au watu wengine. Nilianza kuhisi hivyo kwa sababu ya baraka zote za kimwili na kiroho alizonipa Mungu.  Kazi yangu ya ukufunzi ilikuwa inakua kule Urusi; nilipokea fedha kwa ajili ya kusafiri ng’ambo, na zaidi ya hapo, nilipewa skolashipu kamili ya kwenda kusoma Chuo Kikuu cha  Columbia kule New York.

Siku moja wakati nikiomba, Mungu aliniambia kuwa ninatakiwa kutubu. Mungu alinionya kuhusiana na majivuno yangu na kuniambia nitubu, vinginevyo NINGEANGUKA. Alisema kuwa mimi sikuwa mtu maalum kuliko mtu mwingine yeyote. Pia aliniambia niache kuwahukumu wengine. Kwa bahati mbaya, mimi nilikuwa nimesisimka zaidi kutokana na ukweli kwamba Mungu anasema nami badala ya ukweli kwamba nilitakiwa kumtii na kufanya kile anachoniambia. 

Kuishi katika jiji la New York...

Miaka minne iliyopita, toka tarehe ya kuandikwa kwa ushuhuda huu, nilienda New York ili kusomea shahada ya pili kwenye Chuo Kikuu cha Columbia. Nikiwa New York, mambo hayakwenda kama nilivyokuwa nimetarajia. Nilikuwa na vita vikubwa na sikuelewa kwa nini Mungu aliruhusu nipitie mateso kiasi hicho. Japokuwa Mungu alinibariki sana kwa skolashipu kamili kwenda kusomea Columbia, sikumwamini na wala sikumshukuru wakati wa mapito yangu magumu. Badala yake, nilipachukia New York na Columbia na nikaanza kunung’unika na kulalamika sana.   

Huu ulikuwa ndio mwanzo wa kuanguka kwangu. Niliingiwa na huzuni kubwa sana na nikawa katika maumivu na hofu kubwa. Nilifunga, nikaomba mara kwa mara, nikasoma Biblia, nikaenda kanisani, lakini maumivu na hofu ile havikuondoka! Hali ile ilikuwa  inatia uchungu moyo wangu kiasi kwamba ikawa ni vigumu kwangu kutembea au kuzungumza. Kila dakika ilihitaji nguvu sana. Ilikuwa ni kama vile mtu ananivuta chini na kunizuia kupiga hatua. Muda wote nilikuwa nanyanyaswa na ibilisi ambaye alikuwa akiniambia kuwa mimi nimeshashindwa kabisa.

Baada ya mwaka mzima wa mateso yangu, Mungu alinivuta tena kwake kwa muda mfupi. Alizungumza nami na nikaandika maneno yake kwenye kitabu changu cha kumbukumbu. Ni kwa miaka miwili tu ndio nilielewa kile alichokuwa ameniambia. Mungu aliniambia kuwa nitapitia majaribu makali sana na kwamba ningeteseka sana, lakini aliahidi kunivusha katika yote hayo na kuleta mabadiliko yenye matunda mema ndani yangu.

Wakati nilipokuwa naisikia sauti ya Mungu, nilikuwa naweza pia kusikia sauti za mapepo. Nilikuwa sijui kabisa kwamba mapepo yanaweza kuiga sauti ya Mungu ili kuwadanganya Wakristo. Sikujua kuwa natakiwa kulijaribu kila neno kwa njia ya Biblia. Ndiyo maana, niliposikia kuwa ningeenda kufanya mafunzo ya vitendo kwenye Benki ya Dunia na kwamba ningekutana na mume wangu wa baadaye kule D.C, niliamini kuwa hayo yanatoka kwa Mungu. Kumbe pepo alikuwa anasema na tamaa zangu za kimwili. Niliyapenda maneno hayo na nikayaamini. Nilikuwa na mashaka, lakini pia nilidhani kwamba Mungu hawezi kuruhusu pepo anidanganye. 

Muda mfupi baada ya hapo, rafiki yangu pekee Mkristo wa New York aliondoka kwenda kwenye mapumziko ya majira ya joto. Nilibakia peke yangu. Japokuwa nilikuwa nimeshakaa kwenye jiji hilo kwa mwaka mzima, bado sikuwa na marafiki wa Kikristo. Nilihudhuria kanisani, lakini sikuwa namfahamu yeyote pale.

Nilijawa na huzuni zaidi. Nilikuwa peke yangu kabisa na sikuwa na mtu wa kumshirikisha mashindano yangu. Nilidhani kuwa Mungu alikuwa hajali na hakunipenda tena kwa kuwa hakujibu maombi yangu ya kupata kanisa na kuwa na marafiki wa Kikristo. Niliishiwa na nguvu kabisa pale niliposhindwa kwenye usaili kwenye Benki ya Dunia na kukosa kazi. Sikuelewa kwa nini Mungu aliruhusu pepo anidanganye. Sikuwa na hamu ya kuishi tena na nikaanza kuwaza juu ya kujiua! Sikuweza kabisa kustahimili maumivu yangu yasiyokoma. 

Kisha nilitambua kuwa nisingeweza kufa kwa sababu nikijiua ningeenda jehanamu na kutumbukia kwenye mateso makubwa zaidi, tena ya milele! Nikajiona kama mtu aliyenaswa. Kuishi sitaki lakini wakati huohuo kujiua nako siwezi. Nilijihisi kama vile niko jehanamu. Maumivu yalikuwa makali sana kiasi kwamba nilianza kujikata kwa kisu, maana maumivu ya kimwili yalionekana kwangu kuwa ni mepesi kuliko mateso ya moyoni mwangu. Uovu ulikuwa wakati wote umenizunguka, ukipenya ubongo wangu, ukinitesa moyo wangu, wakati wote ukiwa tayari kusema nami na kuniburuta chini! Kadiri nilivyozidi kuomba na kusoma Biblia, ndivyo nilivyozidi kuteswa na hizo sauti, na ndivyo maumivu yalivyozidi. Sikujua cha kufanya na sikuwa na jinsi ya kuzuia!

Ndipo nilifanya jambo ambalo si la kawaida. Sikuwa na uwezo wa kustahimili maumivu zaidi ya hapo, hivyo nikawa nimeanguka kabisa. Nilijawa na hasira sana dhidi ya Mungu kiasi kwamba nikamwambia aondoke kwangu na aachane nami! Nilimwambia kuwa simpendi na sikuwa tayari kuzungumza naye tena wala kuwa naye. Kwa kuwa nilikuwa ni mtu wa kuzungumza naye kila wakati, ilibidi nijilazimishe sana kuacha kumfikiria. Niliacha kuomba na kusoma Biblia. Nikaamua kufuata njia zangu mwenyewe. Sikuwa najua sawasawa madhara ya hatua yangu hiyo. Sikujua kuwa nilimwacha Mungu na kumfuata ibilisi. Sikutambua kuwa mtu huwa ama yuko anamtumikia Mungu au anamtumikia shetani – hakuna namna ya kusema ‘mimi siko kwa Mungu wala kwa shetani.’ Ukiwa kwa Mungu unakuwa hauko kwa shetani. Ukiwa nje ya Mungu, moja kwa moja unakuwa uko kwa shetani. Hakuna sehemu ya kati!

Hivi sasa ninatambua kwamba Mungu alikuwa muda wote ananiangalia licha ya maamuzi yangu yote mabaya.

Katikati ya majira ya joto, nilipata kanisa na kuwa na marafiki kadhaa. Hatimaye sasa nilikuwa na mtu wa kuzungumza naye na angalau kutoka naye. New York ni sehemu ngumu sana kwa Wakristo. Pia, hivi sasa ninatambua kuwa kumbe hata marafiki zangu pale kanisani nao walikuwa wanapitia magumu mengi vilevile kama mimi! Hata hivyo, kuwa wewe na kuombeana na kumtazama Yesu yalikuwa ni mambo ambayo tulikuwa hatufanyi. Kutafuta mafanikio ya kazi lilikuwa ndilo jambo tulilolipa umuhimu zaidi.

Jumapili moja nilikutana na mwanamume mmoja kanisani. Mara moja nilivutiwa naye. Ninapotafakari sasa ... natambua kuwa mara nilipoondoa macho yangu kwa Yesu, nilifanyika mtu rahisi sana kushambuliwa na shetani. Hilo lilimpa nguvu juu yangu na kudhibiti hisia zangu na mawazo yangu. Na kwa kuwa sikuwa na upendo kwa Mungu moyoni mwangu, nilihitaji kitu mbadala. Nikawa nimevutika kabisa kwa huyu mwanamume.

Pale nilipokuja kutambua kuwa uhusiano wangu naye hauwezi kufika mbali, nilianza kumwomba Mungu na kusoma Biblia. Hata hivyo, bado nikawa sikumwomba Mungu awe Bwana wa maisha yangu tena. Nilitaka tu anisaidie kwenye matatizo yangu niliyojisababishia mwenyewe. Kwa kule kutoyatoa maisha yangu yote kwa Mungu, sikuwa na uwezo kabisa wa kuvunja ule uhusiano. Sikujua wakati ule kwa nini sikuweza kumkatalia yule bwana kunitumia mimi, na kumwambia ‘hapana’. Nilikuwa nimenaswa kwenye hisia zangu mwenyewe na sikuwa na uwezo wa kutoka humo. Nilijua kwa moyo wangu wote kuwa nilikuwa namtenda Mungu dhambi.  

Nilibakia nikiwa nimenaswa kwenye uhusiano huu kwa mwaka mzima. Kwa kuwa huyu bwana hakuwa msomaji wa Biblia na hakupenda kuzungumza kuhusu Mungu, mimi nami pia niliamua kuacha kuyafanya hayo. Kwa hiyo, nikawa nimeenda mbali zaidi na Mungu na hatimaye nikawa nimekuwa mwenyewe tu.

Baada ya mahafali yangu ya chuo, nilifanya kazi New York katika kipindi cha majira ya joto. Nilipata kazi kwenye benki yenye hadhi na nilikuwa na uwezo sana kwenye kazi yangu. Bosi wangu aliniambia jinsi ambavyo alipenda kazi yangu na jinsi nilivyokuwa bora na mwenye akili. Nilijawa na majivuno na kiburi hata zaidi.

Baada ya uhusiano wangu na yule bwana kuvunjika, nilijihisi kuwa ninataka kugeukia kwenye kitu kingine ili kujaza uwazi uliotokea. Bado nilikuwa najiona kuwa simhitaji Mungu. Nilikuwa bado nina hasira naye kutokana na kutonipatia kile nilichohitaji. Ndipo kazi yangu ikawa ndiyo mungu wangu. Nilimuabudu huyu mungu wangu kwa bidii zote.

Kuishi Moscow…

Nilipoenda Moscow,  nilipanga kufanya usaili na mabenki kumi makubwa ya nje. Cha kushangaza, mambo yaligoma kabisa! Sikuweza popote kupata kazi niliyoitaka! Najua sasa kuwa, sababu mojawapo ya mimi kushindwa kwenye kila usaili ilikuwa ni tabia yangu ya majivuno ambayo ilionekana kunisaidia sana wakati nikiwa New York, lakini hakuna mtu aliyehitaji kiburi hiki kule Moscow.

Niliishia kupata kazi ambayo niliichukia kabisa. Hata hivyo, ilibidi niiache baada tu ya miezi mitatu. Niliweza kupata kazi nyingine Moscow. Nilipoambiwa niache kazi yangu ya pili, kwa vile sikuwa nafaa kabisa kwenye kazi hiyo, na pale nilipokataliwa kwenye kila usaili niliofanya kule London, nilitambua kuwa Mungu alikuwa anajaribu kila njia kunifanya nishtuke.

Nilipoteza kazi yangu Aprili (2004). Nilifanya usaili mara kadhaa, lakini kazi sikupata. Kila jitihada ilikuwa haizai matunda kwangu! Hatimaye Mungu alifanikiwa kuvuta umakini wangu. Nikaanza kumwomba. Hata hivyo, nilijihisi kuwa hata nikitubu vipi, siwezi kusamehewa. Nilipakua Biblia kutoka kwenye intaneti maana nilishatupilia mbali Biblia zangu zote pale nilipoondoka New York.  Nikaanza kusoma Agano Jipya tena.

Siku moja, nilipojua kuwa usaili wangu wote umekwama, nilimlilia Mungu ili anisaidie. Nilijiona sina tena matumaini kabisa.

Ndipo nilianza tena kusikia sauti ya ibilisi ikiniambia kuwa Mungu hanipendi na hatanisamehe; na kwamba inabidi nijitupe kupitia dirishani. Sauti ile ilikuwa ina ushawishi mkubwa na nguvu sana kiasi kwamba nilidhani kuwa nitakuwa kichaa. Huku nikilia, nilifungua Biblia na kuanza kusoma kwa sauti japokuwa nilikuwa sielewi hata neno moja. Lakini sauti ile ikawa imetoweka!   

Nilitambua kuwa nilikuwa nimemtenda dhambi Mungu sana na nilihitaji kujua iwapo angenisamehe. Nikakumbuka hadithi za kwenye Agano la Kale kuhusu Israeli – wafalme waliomtenda dhambi Mungu, lakini wakatubu. Nikaanza kusoma hadithi zile. Nikatambua kuwa majivuno yangu na kutotii zilikuwa ndizo dhambi zangu kubwa mbili.  

Katika kipindi cha kurudi kwangu kwa Mungu nilikutana na tovuti yenye Shuhuda za Thamani. (www.precious-testimonies.com). Nilisoma shuhuda karibu zote humo! Niliguswa sana na upendo wa Mungu kwenye maisha ya watu mbalimbali. Niliguswa sana na mateso na maumivu ambayo kila mmoja aliyapitia hadi kuja kumpata Yesu Kristo. Lengo langu, nilikuwa nataka sana kujua kama Mungu angeweza kunisamehe dhambi zangu.  

Kupitia kwenye Biblia, na shuhuda zile, nilitambua kuwa sikuwa nimempa Yesu maisha yangu yote na kwamba nilikuwa bado nimeshikilia mambo yale niliyoyapenda na nilikuwa naogopa kuyaachia na kumpatia Yesu. Pia nilitambua jinsi ambavyo dhambi zangu zilimpatia shetani nguvu kubwa ya kuharibu maisha yangu. Nilijifunza jinsi ilivyo kutembea kwenye njia ya ibilisi. Sitaki ubinafsi tena! Nilitaka kumtumikia Yesu japokuwa isingekuwa rahisi na wakati mwingine ingekuwa vigumu sana. Lakini Yesu hutoa uzima wa kweli na anajua kile kinachofaa kwa ajili yetu.  

Mungu alikuwa na rehema na neema sana kwangu na Roho Mtakatifu wake aliniongoza kwenye toba. Alihukumu majivuno yangu na kukosa kwangu utii na uzinzi wangu. Tarehe  12 Juni, 2004, nilimpokea Yesu kama Bwana na Mwokozi wa maisha yangu yote – si kwa sehemu yake tu!  Nilimwambia achukue ndoto na mapenzi yangu yote ya ubinafsi na aweke ndani yangu  ndoto na mapenzi yake. Nilimkabidhi hofu zangu zote. Nilimwambia kuwa sikutaka tena kumtumikia shetani bali nataka kumtumikia Yeye – Yesu. Maamuzi yangu yote ya nyuma yalinipeleka kwenye kushindwa kabisa. Nilitaka sasa Yesu atawale maisha yangu na kuyabadili apendavyo, na si vile ninavyotaka mimi. 

Baada ya kufanya hivyo, nilijisikia faraja kubwa sana! Kwa mara ya kwanza katika miaka mitatu, nilikuwa natembea barabarani huku nikitabasamu na kupumua kwa uhuru tena. Nilijisikia mwepesi na huru kabisa.

Nilikuwa nimeishi Moscow kwa karibu mwaka mzima, lakini nilikuwa sina rafiki Mkristo hata mmoja. Kabla ya toba yangu, nilihudhuria kanisa jingine lakini bado nilikuwa simfahamu hata mtu mmoja. Kutokana na tabia yangu ya New York ya kutojiweka wazi, nilikuta ni vigumu sana kuweka wazi mambo yangu ya moyoni kwa watu wengine. Hii ndiyo sababu hakuna aliyejua kile nilichokuwa napitia; na pia ndiyo sababu sikuwa na mtu wa kumweleza kuhusu mapito yangu.

Baada ya uamuzi wangu huo, nilidhani kuwa ningeweza kurudi kwa Mungu kwa nguvu za maombi yangu, toba na kusoma Biblia  mwenyewe. Lakini siku chache baada ya kuamua kumrudia Mungu, nilihisi kama kuzimu yote imesimama kinyume nami! Nilianza kuona kiumbe mwenye manywele mengi. Taswira hii ilikuwa mbele za macho yangu muda wote kwa wiki kadhaa. Nilikuwa ninaomba na kuomba na kusoma Biblia. Nilifunga pia. Nilikiri damu ya Yesu juu yangu. Taswira hii mbaya wala haikuondoka! Nilihisi kuwa ninachanganyikiwa. Usiku haikuwa rahisi kulala. Sauti ilianza kuniambia tena kuwa Mungu hatanisamehe kwa kuwa nimemkufuru Roho Mtakatifu na kutenda dhambi ambayo Yesu hawezi kusamehe.  

Siku moja niliamka nikiwa na uchungu na hasira. Nilihisi ule mzigo na uzito tena. Nikaanza kumwomba Mungu anisamehe na kumshukuru Yesu kwa kunifia. Lakini mashindano yangu yakaendelea kuwa magumu zaidi na zaidi. Siku ile nilitambua kuwa siwezi kushindana na ibilisi peke yangu. Nilihitaji msaada. Nilihitaji sana mtu wa kuniombea.  

Kweli imeshafunuliwa

Pale nilipotambua kuwa nahitaji mtu wa kuniombea, niliamua kupeleka mahitaji yangu ya maombi kwa watumishi wa tovuti ya Precious Testimonies. Watumishi hao si tu kwamba waliniombea, bali pia walinipatia mwongozo muhimu sana kwa njia ya baruapepe. Ilikuwa ni wao ndio walionifungua macho kuhusiana na ukweli kwamba ibilisi yu hai na yuko duniani huku akifanya vita dhidi ya Wakristo. Nilitambua kuwa yalikuwa ni mapepo ndiyo yaliyokuwa yananiletea maumivu na mateso makubwa namna hiyo. Nimejifunza pia kuwa ibilisi anawapepeta Wakristo wote kama ngano. Adui aliwashambulia na kuwatesa Petro na Paulo na mitume wengine. Anafanya hivyo hata leo kwa nguvu na ukali uleule!

Ulimwengu wa roho…

Nilipokuwa ninakandamizwa na adui mara baada ya kutubu kwangu, Mungu alinifungua macho ili niweze kuona ulimwengu wa roho. Kama nilivyosema, nilidhani kuwa ninachanganyikiwa pale nilipoona kiumbe mwenye manywele mengi. Baada ya kutuma mahitaji yangu ya maombi, nilijisikia amani kubwa. Nilijua kuwa kuna mtu ameanza kuniombea.

Hata hivyo, niliendelea kuyaona mapepo yakinizunguka. Nilipoamka siku iliyofuata, si tu kwamba niliweza kuyaona mapepo, bali pia nilimwona malaika wangu. Taswira zilikuwa kama kioo. Nilikuwa sina hofu hata kidogo. Niliweza kuona kwenye ulimwengu wa roho kwa wiki kadhaa. Mungu alinifundisha masomo muhimu sana katika kipindi hicho.

Somo la 1:  Mapepo hayawezi kustahimili kusikia Neno la Mungu.

Wakati fulani nilirudi nyumbani kutokea kanisani na nikawa nasoma Maandiko. Niliinua macho na kuyaona mapepo kadhaa. Nikaanza kumwomba Mungu anisaidie. Sikuwa nina hofu lakini nilikuwa tu sijisikii amani kuyaona. Wakati nikiwa namwomba Mungu anisaidie, nilisikia sauti moyoni mwangu ikisema, “Soma Maandiko.”

Nikauliza: “Nini?” Sauti ile ikarudia tena: “Soma Maandiko.”  Nilitii na nikaanza kusoma Maandiko. Lakini baada ya muda kidogo, Mungu akaniambia: “Soma kwa sauti.” Nikawa kama nimechanganyikiwa kidogo, lakini Mungu akarudia tena: “Soma Maandiko kwa sauti.” Nilipoanza kusoma Maandiko kwa sauti niliona kuwa mapepo yale yanafunika masikio yao kwa mikono yao yenye makucha na kuanza kuhangaika kwa mateso makubwa. Hivi ndivyo nilivyojifunza kuwa mapepo hayawezi kustahimili kusikia Neno la Mungu. Neno la Mungu likitumika kwa imani na kweli, ni silaha kubwa dhidi ya nguvu za giza.

Tangu hapo, nimejenga tabia ya kusoma Neno la Mungu kwa sauti. Pia nimepakua kutoka kwenye intaneti Agano Jipya la sauti (lililo katika fomati ya MP3). Nikiwa nyumbani, karibu muda wote huwa nimefungulia Biblia hiyo. Huwa naisikiliza nikiwa nakula, napika, najipamba, nk. Mara kadhaa Mungu amekuwa akielekeza umakini wangu kwenye mistari ya muhimu sana na kunieleza maana yake wakati nikiwa nakula au najiandaa kwenda kazini. Mwenzangu mmoja aliniuliza ni rekodi ya aina gani hii ambayo huwa naisikiliza karibu saa 24 kila siku. Nilimweleza na kumshirikisha sababu zangu za kufanya hivyo, lakini najua kuwa hakunielewa kikamilifu.

Vilevile nilipakua Agano Jipya kwa ajili ya kompyuta yangu ya mfukoni. Kila ninapopata nafasi, huwa najaribu kusikiliza Maandiko niwapo kazini. Mara nyingi ninapopatwa na mashambulizi ya adui nikiwa kazini, huwa naamua kusikiliza Biblia hiyo kama njia yangu mojawapo ya kunisaidi kushinda vita.

Pia nilijifuza kwamba mapepo huteswa sana hasa na Kitabu cha Ufunuo, na hususani sura ya 17, 18, 19, pale ambapo Maandiko yanazungumzia kuhusu hatima yao ya mwisho. Hayawezi kabisa kusikiliza mistari kuhusu Babeli ulioanguka na mistari kuhusu ibilisi na manabii wake wa uongo kutupwa kwenye ziwa la moto.  

Kuna mara kadhaa ambapo niliyatishia mapepo kuyasomea Kitabu cha Ufunuo kama hayakuacha kunisumbua au kuondoka. Ni wazi kuwa sikuyatishia tu, bali nilisoma sehemu hizo. Mbinu hii hata hivyo si kwamba ndiyo jibu la kila kitu. Haikuhakikishii ushindi kwenye kila shambulizi, lakini ni mbinu nzuri ya msaada upande wetu. Mungu mara zote hunisaidia kupata mstari ambao unaweza kunyamazisha kabisa sauti ya adui. Nimeshajifunza kuwa si kila mstari utanyamazisha manyanyaso ya adui bali ni ile mistari ambayo inahusiana moja kwa moja na tatizo lililopo. Ni kama ilivyo kuinua upanga hewani na kupiga kushoto wakati adui yuko kulia. Hiyo haisaidii kumshinda adui. Ni pale tu unapoelekeza mapigo yako kwenye lengo ndipo utashinda mapambano. Hali ni ileile hata kwenye mistari ya Biblia na uongo na unyanyasaji wa adui. Ndiyo maana NI LAZIMA  kujifunza Maandiko kwa bidii na kuweka mistari kwenye kumbukumbu kichwani. 

Katika majaribu ya Yesu ya siku 40 kule jangwani – pale shetani alipomjaribu – je, Yesu alifanya nini? Alimjibu shetani kwa kutumia mistari sahihi kutoka kwenye Neno la Mungu. Alishindana na shetani kwa kutumia upanga wa Roho Mtakatifu, ambao ni Neno la Mungu. Shetani anamnukulia Yesu Neno lakini si kikamilifu; anataja nusu ukweli. Ukweli nusu mara zote huwa ni uongo uliokusudiwa kudanganya wanadamu na kupoteza makusudi ya Mungu kwa ajili ya wanadamu. Yesu alimnukulia shetani Kweli yote kwa  100%  ... na shetani hakuwa na kitu chochote cha kushindana na mbinu ya mapambano ya Yesu. Shetani alishindwa kwa 100% kwenye vita hivyo. Mungu hakuruhusu jambo hili liandikwe kwenye Biblia kwa bahati tu ili kujaza nafasi. Shindana na mashambulizi ya mapepo kwa kutumia kwa usahihi Neno la Mungu.

Lijue Neno ... Liamini Neno ... Fahamu lini pa kulitumia kwa usahihi (usinukuu tu Neno nje ya uhalisia wa hali yako; mapepo watakucheka!); kisha tamka Neno la Mungu kwa sauti, imba nyimbo zinazotokana na Maandiko; omba Neno wakati wa maombi yako na kuyaambia mapepo yanayokuzunguka, (japo huenda hutakaa uyaone) – sikiliza Neno la Mungu linapoongelewa dhidi ya matatizo yanayokukabili, lakini kwa mwongozo wa Roho Mtakatifu.

Mambo yote yanaweza kushindwa lakini haiwezekani kwa Neno la Mungu kushindwa maana Roho Mtakatifu ndiye anayelifanya litende kazi. Mungu hawezi kusema uongo; hivyo Neno la Mungu nalo haliwezi kuongopa. Wanadamu hapa duniani wanaweza wasilielewe Neno la Mungu, hivyo wakalitumia kimakosa katika hali zao, lakini hilo haliwezi kutokea kwa msaada wa Roho Mtakatifu. Hilo kila mara hutokea kwa sababu ya nguvu za kipepo na mawazo ya kimwili ya wanadamu ambao hawana ufunuo kamili wa Neno la Mungu, au huenda wamelipindisha bila wao kujua, na kulifanya liseme kitu ambacho Mungu hajasema. Kama Mungu alivyoandika:   "Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe.” (Tazama: Mt. 24:35; Mk 13:31; Lk 21:33).  Mtu anapopokea ufunuo kamili kwamba Yesu Kristo ndiye Neno, haishangazi basi kwamba halitapita kamwe.

Somo la 2: Mapepo hujaribu muda wote kuingiza mawazo maovu/ya udanganyifu kwenye akili yako. 

Mara nyingi mapepo wanaficha sana udanganyifu wao kiasi kwamba ni vigumu kutofautisha kati ya sauti na mawazo yao na yako. Hivyo, kulisha ufahamu wako kwa Neno la Mungu kila wakati, kuomba na kuwa mwangalifu ni mambo ya muhimu ili kuweza kutofautisha kati ya mawazo yako na uongo wa adui.

Nilipojua ukweli juu ya hasira kali ya ibilisi na mapepo, nilianza kutambua mengi ya mashambulizi yao yaliyofichika, hususani mashambulizi ya kutaka kunishawishi nikubali uongo wao. Nimegundua kuwa mambo mengi yanayokuja kwenye ufahamu wangu hayatoki kwangu au kwa Roho Mtakatifu, bali ni kutoka kwa mapepo.  

Ukweli kwamba niliweza kuona jinsi ambavyo mapepo yanafanya kazi kunizunguka mimi, kumenisaidia sana kutambua mashambulizi yao na kupambana nao. Ni muhimu kabisa kutambua mashambulizi yao mara tu yanapoanza na kutoyaruhusu kukamata akili yako. Jambo la kwanza yanachofanya ni kupenyeza uongo kwenye akili zetu. Kama uongo wowote ukikubaliwa na akili zetu, ni vigumu sana kuja kuutambua baadaye na kupambana na mapepo. Si ajabu basi Maandiko yanatuonya mara , yakitutaka kuwa macho kila wakati, kuzifunga nia zetu, kukesha, kutofuatisha namna ya dunia hii bali kufanywa upya nia zetu (kufanywa upya kwa Neno la Mungu). 

Nimejifunza kuwa kudhibiti akili zangu ni jambo la lazima. Maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome; tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo [Neno lake] (Tazama 2 Kor. 10:4-5). Ni mashindano yasiyokoma kwangu kufanya kila wazo limtii Kristo na kuharibu kila kitu ambacho mapepo yanajaribu kukiinua akilini mwangu kinyume na elimu ya Kristo.

Ninakumbuka shambulizi moja ambapo akili yangu ilishambuliwa kwa nguvu sana na adui na ilinibidi nisome Maandiko kwa sauti mfululizo kwa saa kadhaa.


Mapepo yanaposhambulia akili, nimekuta pia kuwa kuna nguvu sana ninapoyajulisha kuwa nimeshajua kwamba yananishambulia. Kwa kuwa menyewe hupenda kutenda kazi zao kwa kificho na hayapendi kuwekwa wazi, njia mojawapo yenye nguvu ya kupambana nayo ni kuyafanya yajue kuwa umeyatambua.

Nakumbuka pia mapambano fulani ambapo nilijihisi kuwa siwezi kabisa kuzuia manyanyaso ya adui. Mapepo yaliendelea kunikumbusha jinsi ambavyo niliudhiwa na kuaibishwa kazini. Yalikuwa yakiingiza akilini mwangu kila aina ya uongo yakitaka kunifanya niwachukie wafanyakazi wenzangu na kumwasi Mungu. Nilijaribu kila njia iliyokuwa ikiwashinda hapo kabla kwenye mashambulizi mengine, lakini haikuwezekana. Yalikuwa ni mashambulizi mfululizo ambayo sikuweza kupata namna ya kushinda. Kisha asubuhi moja, mapepo yalipofanya mashambulizi yao kama kawaida, Mungu alinifundisha mbinu yenye nguvu. Niliyaambia mapepo kwamba, kila mara yatakaponikumbusha jambo linalohusu kunyanyaswa kwangu na wafanyakazi wenzangu, basi mimi nitawaombea, nitayafunga mapepo yanayowadhibiti na nitamwomba Mungu awaimarishe malaika wa vita ambao wanapigana kinyume na mapepo yale. Kweli kabisa baada ya kuhakikisha kuwa nilikuwa sitanii juu ya kuwaombea wafanyakazi wenzangu, mara moja mapepo yaliondoka na nikawa nimeshinda vita ile. Ni wazi kuwa hata sasa bado naendelea kuwaombea wafanyakazi wenzangu kila ninapokuwa kwenye maombi.

Somo la 3: Mapepo yanaathiri hisia zako ili kukudanganya.

(Angalizo muhimu:  Kabla ya kuendelea na Somo la 3, napenda nikutahadharishe kabla kuwa somo ambalo Mungu amenifundisha juu ya hisia ni gumu kuelewa kinadharia bila mtu kupitia mwenyewe kile nitakachosema. Napenda kusisitiza pia kwamba sisemi kuwa mawazo yote mabaya yanatoka kwa mapepo. Pia, sisemi kuwa ni lazima wakati wote tujisikie vizuri na tujisikie kuinuliwa. Sisi binadamu ni viumbe wa hisia sana na tunaathiriwa na hali ngumu na matokeo yake tunapata hisia za aina mbalimbali.

Hata hivyo, kuna nyakati ambapo hisia zetu hasi zinakuja kutoka kwa mapepo moja kwa moja. Ni lazima wakati wote tutafute mwongozo wa Mungu na kumwomba atufundishe jinsi ya kutofautisha kati ya hisia zinazotoka kwetu na ambazo ni mashambulizi ya mapepo na tumwombe atufundishe jinsi ya kupambana na mapepo yanayotuletea hisia mbaya).

Nimejifunza kuwa mapepo yana uwezo wa kuathiri hisia zetu kwa kutumia huzuni, kukata tamaa, kujiona hatuna maana, kuhisi kama vile Mungu ametudanganya au ametuacha (na kwa upande wangu, nilihisi kabisa kuwa Mungu amenisaliti) kuhisi kama vile Mungu si wa kuaminiwa au Neno lake si la kuaminiwa, kuhisi Mungu hasikii maombi yetu, achilia mbali kujibu; kuhisi kuwa Mungu hatupendi; kwamba tumeshapoteza wokovu wetu, au kama tumemkasirikia sana Mungu, kuhisi kuwa Mungu hatatusamehe, nk. Lengo la mapepo ni kukuibia wewe na mimi furaha ya wokovu wetu ambayo imo ndani ya mioyo yetu. Nimejifunza kupambana na uongo na kusimama kwenye kweli ya Injili (furaha na amani nilizopewa na Yesu katika roho yangu) badala ya kukubaliana na nguvu ya udanganyifu ya mapepo inayotaka mimi niamini hisia zangu badala ya kuamini Kweli na Neno la Mungu ... na kufanya Neno la Mungu liwe ndiyo lenye mamlaka ya mwisho kwenye kila jambo.

Nakumbuka wakati fulani wa majira ya joto ambapo nilirudi kazini nikiwa nimekata tamaa kabisa na nikayaona mapepo yamenizunguka yakirukaruka kwa furaha kwa sababu hiyo. Jambo hilo lilinighadhibisha mno Kama kuna kitu ambacho sikuwa tayari nacho ni kuyapa mapepo nafasi ya kushinda na kufurahia kwenye maisha yangu. Kwa hiyo, nilichofanya ni kuyatazama, nikavuta pumzi kwa nguvu, nikala chakula cha jioni, kisha nikakusanya nguvu zangu zote nilizokuwa nimezipoteza na nikasema kwa sauti: “Mungu, asante kwa kazi na asante kwa furaha na amani niliyonayo kwenye moyo wangu.” Nilienda chumbani kwangu na kuanza kusoma Maandiko kwa sauti. Baada ya hapo sikuyaona tena yakiwa yanarukaruka kwa furaha.

Nakumbuka pia wakati mwingine mapepo yalikuwa yananishambulia kwa hisia za kukata tamaa pamoja na huzuni kubwa. Nilishindana nayo sana. Huwa hayatumii sana mbinu hiyo kwangu. Haina nguvu sana kwa sababu huwa najitahidi kutofuata KAMWE hisia zangu. Huwa sisomi Biblia kwa vile tu eti NAJISIKIA kufanya hivyo au kuomba kwa vile najisikia kufanya hivyo. Ninasoma Neno na kuomba kwa sababu nimeamuriwa kufanya hivyo na kwa sababu ninataka kuonyesha uaminifu wangu kwa Mungu. Ninapotambua kuwa mapepo yananishambulia kwa hisia hasi, mara moja ninamshukuru Mungu kwa ajili ya furaha na amani niliyonayo katika roho yangu, nayakemea, kisha naendelea na kile ambacho nilikuwa nimepanga kufanya.

Lengo kuu la mapepo katika kushambulia hisia zangu ni kutaka kunidhibiti kupitia hisia. Sasa kama sitazifuata hisia zangu, lakini nikafuata Neno la Mungu, mashambulizi yao yanakuwa ni kazi bure.

Ninajua kuwa mapepo huathiri si tu hisia zetu kwa kutujaza hisia hasi, bali pia kwa kutumia hisia chanya za bandia ambazo ni rahisi kwa mtu kuzitafsiri kuwa ni uwepo wa Mungu. Nimejifunza kuwa Mungu hatendi kazi kupitia hisia zetu. Mungu hutenda kazi kupitia Neno lake na imani yetu tu. Mapepo mara zote hutenda kazi kupitia hisia za mtu kiasi kwamba mtu huyo atasoma Biblia na kuomba pale anapojisikia kufanya hivyo na si kwa vile Mungu ameamuru afanye hivyo. Ni vibaya sana kwamba Wakristo wengi hawatambui kuwa kujisikia vizuri wakati wa kuomba au kuabudu, haimaanishi kuwa hisia hizo ni lazima ziwe zinatoka kwa Mungu. Ni nadra kwa Mungu kufanya jambo ili tu kutufanya tujisikie vizuri kihisia. Yeye ana malengo mengine tofauti kabisa kwa ajili yetu. Anataka kutufundisha kujilisha mioyo yetu kwa kutumia Kweli (Neno la Mungu). Kweli mara zote hukubaliana na roho inayotafuta kumpendeza Roho Mtakatifu. Kwa roho zetu na Roho Mtakatifu kutenda kazi kwa pamoja na kwa kukubaliana kabisa, hisia zetu zitaanza kufuata mstari, na ndipo itakuwa rahisi kutambua ni nani anayeendesha hisia zetu. 

Wakati fulani nilihudhuria ibada kwenye kanisa fulani. Nilihisi hali fulani ambayo mwanzoni nilikuwa nikiita ni “uwepo wa Roho Mtakatifu.” Baada ya ibada nilimwendea binti mmoja. Aliniambia kuwa alifurahia sana “uwepo wa Bwana.” Mara moja nilijiuliza swali, “Ni kweli ni uwepo wa Bwana? Je, Mungu wangu ninayemtumikia anawaita watoto wake ili wawe wakimya tu? Au Mungu wangu anawaagiza watoto wake wawe macho na wawe waombaji muda wote?”

Hivi karibuni Mungu amenifundisha nisikubali kabisa hisia za “uwepo bandia wa Bwana” unaokuja kutoka kwa mapepo. Kwenye sehemu ya jumuiya ambako watu wanatafuta kuwa kwenye uwepo wa Mungu, muziki wa sauti kubwa, kupaza sauti kwa watu pamoja na spika kunaweza kusiwe chochote bali ni uchocheaji wa hisia zetu hadi kiwango cha juu kiasi kwamba kunaweza kudhaniwa kuwa ndio “uwepo wa Mungu” wakati siyo. Na inapotokea hivyo, shetani anaweza kuleta udanganyifu kwa kila namna unaoweza kuonekana kama ni utendaji kazi wa Roho Mtakatifu kumbe Roho Mtakatifu anaweza kuwa yuko uani anatapika (yaani anaweza kuwa anajisikia kinyaa kwa hali kama hiyo). Uwepo wa kweli wa Mungu huwa unatambulika kwa mtu mmojammoja peke yake – kwenye utulivu – katika ushirika binafsi na Mungu. Yesu hakuwa na haja ya kuchochea watu kihisia kwenye sehemu ya watu wengi ili kusikia kile ambacho Baba yake alitaka afanye. Mara zote ilikuwa ni kwenye utulivu, mahali ambako hakuna vurugu. Hapo ndipo aliona “uwepo wa Mungu.”  

Lakini imekuwa ni kinyume chake ambapo kundi la Wakristo “husubiri kwa kimya uwepo wa Roho” uwatembelee. “Watetemekaji” na "wachekaji" na "waliaji" wamekuja na kupita; na watakuja na kupita ... na kama udhihirisho wa nguvu unaotokea wakati huo, hauzai matunda yaliyo wazi kwa dhambi kuwekwa wazi na kutubiwa – roho haziokolewi – hakuna huduma inayoburudisha ya Neno la Mungu – hakuna uponyaji wa hakika ambao umethibitishwa na wataalamu wa afya – watu wanaanguka kwa kile kinachodhaniwa kuwa ni nguvu za Mungu, kitu ambacho hakifanyi lolote zaidi tu ya kuvutia machoni mwa watazamaji. Mapepo yanapewa uwanja wa kudhihirika kwa “wakristo” kwenye ibada bila ya Wakristo hao kufuatiliwa kibinafsi. Wakristo ni lazima wawe makini sana kukubali kwamba “miujiza hiyo inatoka kwa Mungu.” Japokuwa Mungu amefanya na ataendelea kufanya yote hayo niliyotaja hapo juu, shetani naye anaweza, na ataendelea kuigiza mambo hayahaya.

Nimegundua kuwa mara mashambulizi ya adui yanapotambulika na mtu akapambana nayo kwa bidii zote kwa kutumia upanga (Neno) na ngao (Imani), adui huondoka mara moja. Ashukuriwe Mungu atupaye kushinda kupitia Bwana wetu Yesu Kristo (1 Kor. 15:57) na ambaye hutufanya kushinda (2 Kor. 2:14).

Kutambulishwa kwenye vitabu vya Rebecca Brown

Baada ya kutambua jinsi adui yangu alivyo na nguvu na ukatili, niliamua kujifunza zaidi kuhusu vita vya kiroho kutoka kwenye vitabu vya Kikristo mbali na kujifunza Biblia na kutoka kwenye uzoefu wangu binafsi. Nilitambulishwa kwenye vitabu vya Rebecca Brown na Mkristo mmoja kwenye kanisa nililoanza kuhudhuria mara baada ya kuokoka. Nilitiwa moyo sana kuona kuwa kumbe mambo mengi niliyojifunza katika vita vyangu vya kiroho yanathibitishwa na  Rebecca katika kitabu chake. Kupokea uthibitisho wa uzoefu wangu limekuwa ni jambo muhimu sana kwangu kwa kuwa sikuwa na mtu yeyote ambaye ningeweza kumshirikisha uzoefu wangu.

Zaidi ya hapo, ilikuwa ni muhimu pia kwangu kutambua kuwa sikuwa peke yangu niliyeshambuliwa na adui. Wapo watoto wengi wa Mungu wanaopitia mashindano makali kama yaleyale. Kujua hili kumenisaidia kunyamazisha sauti ya adui aliyekuwa akininyanyasa kutokana na ukweli kwamba “niko mpweke na peke yangu na sina marafiki.”  Kwa neema ya Mungu, hathubutu kufanya hivi tena, maana ninajua kuwa siko mpweke (Yesu yuko nami daima) wala siko peke yangu (watoto wengi wa Mungu nao pia wanashindana na adui). Japokuwa sina marafiki wa Kikristo waliokomaa hapa Moscow muda huu ninapoandika, najua kuwa hili limepangwa na Mungu kama sehemu ya mafunzo yangu ili nijifunze kumtegemea Yeye kunifundisha jinsi ya kufanya vita vya kiroho vyenye ushindi dhidi ya nguvu za kipepo. Nisingependa watu wapate picha kwamba "ni mimi naYesu tu"; kwamba siwahitaji Wakristo wengine kutoa mchango kwenye maisha yangu, na kuniombea mimi pamoja na mwito wa Mungu maishani mwangu - hapana. Isipokuwa kwamba kwa sasa niko kwenye kipindi ambacho Mungu ananifundisha mambo mengi moja kwa moja kutoka kwa Roho wake. Ni Mungu tu ajuaye kile kitakachotokea kwenye maisha yangu yajayo.

 Udanganyifu wa shetani makanisani

Baada ya kusoma vitabu vya Rebecca nilifanya utafiti kwenye mtandao wa Google na kuiona tovuti yake. Kwenye tovuti hiyo nilikutana na unabii/maono mawili kuhusiana na uchaguzi mbalimbali wa Marekani yaliyoandikwa na mume wa Rebecca, Daniel. Nilishtuka sana baada ya kufahamu kuhusu mbinu za adui.

Nimeshahuhudia uthibitisho mwingi kote kwenye habari za dunia na kanisani kwamba unabii wa Daniel ulikuwa kweli kwa 100% na unatoka kwa Mungu. Macho yangu yamefunguka na kuona kazi ya adui iliyo ya kificho sana dhidi ya kanisa ikiwa ni pamoja na:

-        Maombi yaliyojaa ubinafsi na kujitazama mwenyewe tu.
-        Mahubiri yanayolenga upendo wa Mungu kama njia ya kunufaika sisi na kile ambacho Mungu anaweza kututendea na si kile tunachoweza kutenda katika kumtumikia na kuenenda kwa utii mbele zake.
-        Unabii kuhusina na upendo wa Mungu usiokoma na si kuhusu haja ya kuacha dhambi na kuwajali waliopotea.
-        Mara chache sana nimesikia makanisani kwamba Wakristo watateseka kwa ajili ya Yesu (na kiukweli, kadiri wanavyojitoa kwa bidii kwa Mungu ndivyo huenda watateseka zaidi isivyo haki); kwamba wanatakiwa kutambua na kujifunza kuukana ubinafsi wao; kwamba mateso ni jambo linalotokea kila siku kwa namna moja au nyingine na kwamba wanatakiwa kubeba misalaba yao ya mateso yasiyo ya haki yatokanayo na kuonewa na kumfuata Kristo bila kujali kuna maumivu kiasi gani – bila kujali gharama inayotakiwa.
-        Kile ambacho nimeona kuwa kinasikika zaidi ni ujumbe wa kificho wa kile ambacho Mungu atanitendea kama nikifuata kwa usahihi  “kanuni” fulani fulani na si kile ambacho ninatakiwa kufanya kwa ajili yake ili kuenenda katika utakatifu na kuachana na ubinafsi wangu ili kuwasaidia wengine kuja kwa Mungu na kukua ndani ya Mungu.

    Gharama ya kuwa Mwanafunzi wa Yesu
Septemba iliyopita, nilijitolea kufundisha masomo ya Biblia ili kutoa picha ya gharama ya kuwa mwanafunzi wa Yesu pamoja na vita vya shetani dhidi ya Wakristo. Nilichagua mistari inayojibu maswali yafuatayo: 
·            Je, Yesu anaahidi utajiri kwa wanafunzi wake?
·            Je, Yesu anaahidi afya kamili ya kimwili kwa wanafunzi wake?
·             Je, ahadi ya kuteswa na kuteseka ilitimia kwenye maisha ya Wakristo wa Agano Jipya?
·            Je, Mungu anavumilia dhambi kwenye maisha ya Mkristo? Kwa nini Wakristo waliteswa?
·            Kwa nini Neno la Mungu linasema kuwa kila anayetaka kuishi maisha ya uchaji Mungu atateswa?
·            Je, Mungu anamruhusu shetani kuwashambulia Wakristo moja kwa moja?

Niligundua kuwa wakati nikisoma Maandiko haya baadhi ya watu walikosa utulivu. Nilipofika kwenye kusoma Maandiko yanayoongelea kuhusu shetani kumpepeta Petro kama ngano, kijana mmoja alipayuka kwa hasira. Alipinga kabisa mimi kusoma mstari huo. Alisema kuwa mstari haukuwa unahusiana kwa namna yoyote na Petro kumkana Yesu, na hakuniruhusu kuendelea kusoma Maandiko zaidi ili kufafanua mstari huo. Nilikuwa sijawahi kukutana na upinzani mkali namna hiyo kwa Neno la Mungu kutoka kwenye kundi la waamini, na sikutaja chochote kinachonihusu mimi binafsi. Nilikuwa nasoma tu kutoka kwenye Neno la Mungu!

Nilipomwomba kijana yule aniache angalau niendelee kusoma Maandiko, alisema kuwa hataruhusu mafundisho yoyote ya uongo kwenye kundi letu dogo. Wanakikundi wengine nao walinikabili na kunitaka niwaeleze sababu hasa ya mimi kuwasomea mistari ile. Karibu wakimbie kabisa kutoka kwenye nyumba yangu ungedhani mimi ni mchawi. Niliumia na kulia.

Baada ya siku chache, Mungu alisema nami. Aliniambia: “Watalikataa jina lako kama uovu. Thawabu yako ni kubwa mbinguni. Niamini Mimi tu, Neno langu tu. Nitakuja na kumlipa kila mmoja kwa kazi yake. Waombee. Vifungo nilazima viharibiwe kwanza. Vifungo ni:
·      Mwili
·      Kupenda mali
·      Kujipenda mwenyewe
·      Starehe
Utateseka, usijipende mwenyewe, jikane mwenyewe, jifunze kujikana katika kila kitu kinachopingana na Mimi. Soma Neno langu na kuomba kila wakati. Nitajitukuza kupitia wewe. Hii itakuja kupitia maumivu na mateso utakayopitia. Jifunze kuridhika na ulicho nacho. Nataka kuwa chanzo pekee cha furaha yako na ridhiko. Asiwepo mwingine. Omba kwa ajili ya kuenea kwa Neno langu na kuharibiwa kwa kazi za adui. Jifunze kuniamini Mimi. Jifunze kufurahi kwenye mateso yako. Omba kwa ajili ya kuharibiwa kwa uongo na udanganyifu unaoharibu akili za wanangu. Nawapenda wote sawasawa. Jiachie kwenye mapenzi yangu. Utukufu ni wa kwangu peke yangu. Omba kila wakati, omba. Uharibifu unakuja kwenye dunia hii. Wale wanaonitumikia ndio watakaopona; wale wasionitumikia hawatapona. Omba.”
Baadaye nilipata uthibitisho ufuatao kwenye Neno la Mungu.  
2 Timotheo 3:1-5:  
Lakini ufahamu neno hili, ya kuwa siku za mwisho kutakuwako nyakati za hatari.

Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu,

wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi, wasiowapenda wa kwao, wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji, wasiojizuia, wakali, wasiopenda mema,

wasaliti, wakaidi, wenye kujivuna, wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu;
wenye mfano wa utauwa, lakini wakikana nguvu zake; hao nao ujiepushe nao.

Nguvu ya Mungu inatolewa si tu kuokoa, bali pia kuponya na kukomboa na kuua asili yetu ya ubinafsi, anguko na kukosa utii ... sio tiketi ya kusamehewa tena na tena huku mtu anaendelea kutenda dhambi ileile tena na tena na kuyapuuza kana kwamba toba ndogo tu inatakiwa kufanya kila kitu kiwe sawa kati yetu na Mungu, halafu mtu anarudi tena kuyafanya matendo hayo hayo  ya uasi hadi atakapoenda tena kutubu. Unakuwa ni mduara unaojirudia tena na tena kama kwamba Ukristo si zaidi ya kusema: "Unajua nini? Naweza kutenda dhambi na ilimradi ninatubu, naweza kufanya dhambi ileile tena na tena na kila kitu kinakuwa sawa tu kati yangu na Mungu! Napenda kweli aina hii ya Ukristo!”

Hapana! Haitakiwi kuwa hivyo!

Tangu niokoke, nimekumbana na mashambulizi kadhaa kutoka kwa adui ambayo yanakuja kupitia kwa mtu tunayekaa naye chumba kimoja, wafanyakazi wenzangu, na hata washirika wa kundi langu dogo la wapendwa, japo ndiyo yanakuja kutoka kwenye tamaa za mwili wangu. Adui anatumia kila kitu na kila mtu kunijaribu na kujaribu kuniharibu. Nimejifunza kuwa Yesu kweli alimaanisha pale aliposema: Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate. (Luka 9:23). Wakati mapambano yangu yanapokuwa makali kabisa, wakati mwingine nahiksi kama vile msalaba wangu ni mzito kupita kiasi. Ni vigumu sana kushinda mashambulizi ya mara kwa mara ya adui, lakini Mungu amekuwa kila wakati mwaminifu na hunipatia mstari unaofaa wa kumnyamazisha adui na amenipa hekima ya kujishusha mbele zake na kutofunua kinywa changu mbele za wale wanaonizushia mambo ya uongo.

Hivi karibuni nimegundua kwamba hata kwenye mapambano makali, pale ambapo kila kitu na kila mtu anakuwa kinyume nami INAWEZEKANA kubakia na furaha na amani ambayo Yesu anatuahidi kwenye roho zetu, hata kama sijisikii furaha na amani kihisia. Mapepo yanaweza tu kunidhuru kimwili na kihisia, lakini kama nikisimama kwenye Neno la Mungu, hawawezi kunidhuru moyo wangu ambako ndiko anakokaa Mungu. Neno la Mungu, maombi na imani NI SILAHA ZENYE NGUVU SANA dhidi ya adui.

Kuingilia himaya ya shetani

Novemba 2004, nilikutana na jambo ambalo lilinipa msukumo wa kujifunza zaidi kuhusiana na ibilisi na imani za siri. Nilisoma makala kwenye gazeti kuhusiana na tovuti fulani ya Kirusi ambayo ilikuwa inahamasisha watu kujiua. makala hayo yalikuwa yanahusiana na vijana waliokuwa na majonzi na mawazo ya kujiua ambao hatimaye walijiua kutokana na ushawishi wa tovuti hiyo. Makala yalisema kuwa tovuti hiyo ilikuwa na taarifa nyingi za namna ambavyo mtu anaweza kujiua kwa mafanikio. Vijana kadhaa waliosaidia kuitengeneza tovuti hiyo, baadaye walikutwa wakiwa wamekufa. Wazazi wao walimshitaki kiongozi/mwanzilishi wa tovuti hiyo.

Baada ya kusoma makala niliamua kuitazama tovuti hiyo. Nilikuwa sijui kabisa kwamba tovuti hiyo ilikuwa ina uvuvio wa shetani na kuendeshwa na waabudu shetani. Tovuti hiyo ni ya uovu kamili ikiwa na picha za watu waliokufa na mandhari yenye giza ambayo yanamfanya mtu asiyekuwa na huzuni au mfadhaiko aupate. Mbali na mwonekano wa ajabu wa nje, tovuti hiyo unatoa giza la kiroho ambalo linawaathiri moja kwa moja watu wanaoitembelea.

Nilisoma maelezo kuwahusu watu kadhaa humo ndani. Wote walikuwa na historia zinazofanana. Walikuwa ni watu walionyanyaswa sana wangali watoto; walitoka kwenye ndoa zilizovunjika; walikataliwa na wazazi wao wakiwa wadogo; hawajawahi kupata upendo au matunzo ya wazazi. Niliamua kwenda kwenye sehemu ya kutoa maoni ili angalau niweze kusema nao kwamba kuna mmoja anayeweza kuponya maumivu yao na kuwaweka huru mbali na huzuni na fadhaa zao. kwa kutojua kwangu, nilidhani kuwa huenda naweza kuwafikia watu wale.

Mtu mmoja akawa amevutiwa na kile nilichosema na akataka kufahamu zaidi kuhusiana na kuwekwa huru. Hata hivyo, nilipoanza kumweleza kuhusu kweli za Biblia, kila mara nilipoandika jina la Yesu Kristo lilifutika. Kwa siku nzima nilizuiwa kabisa kuchangia chochote kwenye ukurasa huo.

Usiku wa kwanza baada ya kuchangia kwenye tovuti ile, nilipatwa na jinamizi baya sana! Mungu aliniamsha katikati ya usiku na akaniambia niombe. Nilijawa na hofu kubwa kutokana na uwepo wa uovu chumbani kwangu.

Siku iliyofuata nilijisikia kichefuchefu. Nilienda kwenye tovuti ile asubuhi. Msichana mmoja aliandika swali, akiuliza ni dawa gani atumie na ni kwa kiasi gani ili aweze kujiua. Nilijaribu kumtumia ujumbe ili kumwambia amwite Yesu. Ujumbe wangu ulizuiwa kwenda. Msichana yule alipata ujumbe kutoka kwa mtu mwingine ukimshauri atembelee sehemu nyingine kwenye tovuti ile inayoeleza kwa undani namna mbalimbali za kujiua. Nilitambua kuwa, kwa makusudi, nilikuwa nimezuiwa kabisa kuandika ujumbe wowote kwenye tovuti ile.

Niliamua kuwaeleza kundi lile letu dogo la maombi ili tuombe dhidi ya ile tovuti na kwa ajili ya watu na kwa ajili yangu (maana nilianza kupata majinamizi). Hata hivyo, hadithi yangu iliamsha chuki na hasira nyingi!  Wanakikundi walinizuia kwa ukali kuzungumzia tena kuhusiana na tovuti ile na wakaanza kuhoji kama na mimi nilikuwa na mawazo ya kutaka kujiua, na kama kweli nilikuwa nimekombolewa kutoka kwenye mfadhaiko. Sikuamini kile nilichokuwa nakisikia kutoka kwao!

Kisha kwa ukali waliniambia niondoke kwenye kikundi kile cha Biblia kama nilikuwa sipendi vile walivyokuwa wakiomba sana kwa ajili yao kibinafsi na kwa ajili ya wanakikundi wenyewe. Nilikuwa sijawahi kutamka chochote juu ya kuondoka kwenye kikundi. Ni wazi kwamba niliumia sana, nikalia na nikajaribiwa kuinuka na kuondoka zangu. Hata hivyo, Mungu aliweka ndani yangu moyo wa kubakia, kwa hiyo nilibakia pale.

Nilifurahi kwamba nilibakia kwa sababu mama mmoja mtu mzima aliomba kwa ajili yangu. Aliniambia kuwa niliingia kwenye himaya ya shetani bila ya kuambiwa na Mungu. Alinishauri kuwa niombe tu kwa ajili ya watu wale wa kwenye tovuti, lakini akashauri kwa nguvu sana kwamba niache kutembelea tovuti ile. Nilielewa kuwa alikuwa sahihi. Nilijua kuwa siwezi kushindana na uovu niliokutana nao. Haikuwa ni mashambulizi tu ya kawaida. Hapana. Ilikuwa ni zaidi ya hapo – uovu mkubwa ambao usingekaa kimya kwa sababu nimeingilia himaya yake. Nilizingatia ushauri wake. Hata hivyo, majinamizi, hofu kubwa na uwepo wa uovu usiku viliendelea kuniandama kwa muda.

Miezi miwili baadaye nilikuja kufahamu kuwa baadhi ya watu wanaoendesha tovuti ile ni waabudu shetani. Kama ningejua hilo kabla, nisingejaribu hata kuifungua tovuti ile. Namshukuru Mungu kwa kuniweka salama wakati wa kukosa kwangu umakini. Mungu aliniambia niendelee kuwaombea wale walio na mfadhaiko na kwa ajili ya kuharibiwa kwa tovuti ile.

Baada ya tukio lile, niliamua kuijifunza mengi kadiri iwezekanavyo kuhusiana na vita vya kiroho na adui na wale wanaojihusisha na imani za siri. Najua kuwa kuingilia himaya ya adui bila mwongozo wa moja kwa moja wa Mungu kunaweza kuwa ni jambo la hatari sana. Katika kutafuta kwangu kufahamu juu ya ulimwengu wa kipepo, nilinunua maandiko ya Howard Pittman, Jessie-Penny Lewis na Rebecca Brown.   Ninapendekeza kila Mkristo asome kitabu kilichoandikwa na Jessie-Penn Lewis.  Ni moja ya vitabu vilivyoandikwa kwa uzuri na kwa undani kuhusiana na mambo ya ulimwengu wa roho, kama ambavyo wengine wengi nao wanakubaliana na hili. Nadhani Wakristo wote wanaweza kupokea mafunuo mengi kupitia kitabu hiki, nacho kinaweza kupatikana kwa kubofya: Hapa

Ufupisho wa masomo niliyojifunza kutoka kwa Mungu 

Kwa kifupi, Mungu alinifundisha mambo yafuatayo:
1.   Kila Mkristo amepangiwa mapepo na shetani yanayomfuatilia ili yamharibu. Hakuna asiyekuwa nayo. Mungu kwa upande wake ametupangia malaika mmoja au zaidi wa kutusaidia. Kama tungeruhusiwa kuona ulimwengu wa roho unaotuzunguka, tutaona malaika na mapepo wametuzunguka.
 
2.   Mapepo hutufuata kila wakati. Wanafahamu udhaifu wetu, hivyo wanapanga kutushambulia katika muda ulio mwafaka kwao. Ni muhimu kwangu kufahamu udhaifu wangu na kumwomba Bwana augeuze kuwa nguvu kwangu. Kujikana mwenyewe na kuachana na kila kitu ninachokipenda sana ambacho hakimtukuzi Mungu ni jambo la lazima. Ni njia pekee ya kupunguza uwezekano wa kushambuliwa na adui.
 
3.   Lengo la mapepo ni kunifanya nimuasi Mungu, kunifanya niwe mtu wa kumnung’unikia, kumlalamikia, na kumkasirikia Bwana wangu Yesu, na kuwadharau watu wa Mungu wasio na sifa mbalimbali. Nilipogundua kuwa mateso na matatizo yangu yanatoka kwa adui na si kwa Mungu, nilijifunza kuelekeza hasira zangu zote kwa mapepo.
 
4.   Mbinu ninayotumia kumaliza hasira zangu kwa mapepo pale yanaponishambulia ni kwa kujitahidi kufanya kile ambacho Mungu ananiagiza kufanya na kutompa kabisa adui nafasi. Ninajua kile ambacho adui anataka kwangu na mimi siko tayari kumpatia kwa hiyari yangu mwenyewe. Ni wazi kuwa haya ni mapambano makali na magumu. Namjua yule ninayekabiliana naye; ni kiumbe mwenye nguvu zaidi baada ya Mungu. Ni adui mwovu kabisa ambaye mwanadamu anaweza kuwa naye hapa duniani. Sitarajii haki yoyote kutoka kwa adui. Sitarajii kuwa ataniruhusu tu nisababishe madhara kwenye ufalme wake kisha niendelee kuishi kwa furaha tu hapa kwenye ufalme wake duniani. Nimeshahesabu gharama zangu. Kila kitu maishani mwangu kiko hatarini. Najua kuwa adui daima anadai, ama moja kwa moja au si moja kwa moja, ili Baba amruhusu, yeye ibilisi anijaribu. Na pale ruhusa inapotolewa, najua kuwa ibilisi atanivuta kuliko uwezo wangu. Lakini pia najua kuwa Mungu ameahidi kuwa atanisaidia kushinda na kustahimili. Yesu hakuwahi kuahidi kuwa ataniepusha na mateso, lakini aliahidi kuwa atanifundisha kushinda na kustahimili. Niko tayari kubeba msalaba wangu kila siku hadi mwisho, kushinda na kustahimili. Pia niko tayari kupokea thawabu nzuri kwenye ufalme wa Mungu. Katika vita vyangu siko tayari kurudi nyuma – sina mahali popote pa kurudia nyumba – nina kusonga mbele tu!
 
5.   Hakuna kitu kinachotetemesha ufalme wa shetani na jeshi lake la mapepo kama pale watoto wa Mungu wanapoendelea kushikilia utii wao kwa Bwana Yesu kupitia kumshukuru kila wanapoteswa na kufedheheshwa na adui. Mungu amewapa mitume wake , maandiko mengi "kuhesabu kuwa furaha" tunapoteswa isivyo haki na shetani na kustahimili, maana thawabu yetu itakuwa kubwa mbinguni. (Ibilisi muda wote anataka tuhisi kuwa Mungu ni katili kwa sababu hatupatii thawabu zile tunazotaka kwenye maisha haya; na ni lazima tuwe waangalifu ili tusiingiwe na hisia za kujionea huruma kama kila kitu kinaonekana kiko kinyume nasi; vinginevyo ibilisi anaweza kutumia hali hiyo kufanya shauku yetu ya kumtumikia Mungu ishuke chini). 
 
6.   Kumbuka ... maisha haya ni mafupi mno kulinganisha na milele. Mateso yoyote ambayo Mungu anaruhusu tuyapitie kwa miaka michache hii tuliyo nayo hapa duniani, hata kama ni makali kiasi gani, hayawezi kulinganishwa na uzito wa milele wa utukufu yatakayotuletea. Hilo ni Neno la Mungu! (Tazama: 2 Kor. 4:17-18). 

Kwa wale wanaojiona wamesalitiwa na Mungu

Kama kuna kipindi ulikuwa na moto na Mungu, ukiomba kwa bidii na kusoma Biblia kwa bidii, lakini kidogo kidogo umeingiwa na uchungu dhidi ya Mungu kwa sababu ya matatizo au mateso na dhiki, mambo yafuatayo ni kwa ajili yako kibinafsi.

Kwa kuwa na mimi nimepita mahali uliko hivi sasa, na ninafahamu uchungu wa kihisia na mfadhaiko unaokutesa, ningependa kukupatia hatua kadhaa ambazo zilinisaidia mimi kupata uhuru kutoka kwenye nguvu za shetani. 

Njia yangu kuelekea kwenye kukombolewa:

1. Mungu alinisaidia kutambua kuwa Yesu hanichukii wala hanilaani.
Nilienda kutazama sinema ya “Mateso ya Kristo”. Kwa kutazama mateso ya Kristo nilitambua kuwa Kristo hakunichukia hata kidogo. Mapepo yalinishawishi kwamba Mungu alinichukia na kunilaani na kwamba Yesu hakupata mateso makubwa ya kihisia. Uongo wao uliota mizizi kwenye akili yangu. Niliteswa na uongo huu kwa miaka miwili. Kupitia sinema ile, Mungu alivunja nguvu ya giza lile kwenye akili yangu. Nilitambua kuwa Yesu, si tu kwamba hakunichukia, bali pia aliteseka sana kwa ajili yangu. Hii ilikuwa ni hatua yangu ya kwanza na ya muhimu sana kuelekea kwenye uhuru wangu.

2. Kwa kusoma shuhuda za waliookoka, nilielewa kuwa kumbe sikuwa peke yangu kwenye mateso na dhiki. Kabla ya kuja kwa Kristo, watu wengi walipitia mateso makali zaidi kuliko ya kwangu.

Mwanzoni mwa mchakato wa ukombozi wangu, mapepo yalishikilia kwa nguvu sana akili yangu kiasi kwamba sikuelewa Biblia na sikuweza kustahimili kusikiliza au kusoma Neno la Mungu. Hata hivyo, nilikuwa na shauku ya kutaka kujua kama kulikuwa na Wakristo wengine waliokuwa na mapito kama yangu. Wakati nikitafiti kwenye  mtandao wa Google, Mungu aliniongoza kwenye tovuti ya Shuhuda za Thamani (www.precious-testimonies.com). Wakati ninasoma shuhuda, Mungu alivunja uongo mwingine uliokuwa umejikita kwenye akili yangu: nilitambua kuwa sikuwa kamwe peke yangu kwenye mateso, kama ambavyo nilikuwa nikiamini hapo kabla. Wapo wengi walioteswa zaidi yangu na shetani. Kwenye shuhuda hizo, niliweza pia kuona namna shetani alivyoharibu maisha ya wengine na jinsi Yesu Kristo alivyowaweka huru na kuwapa maisha mapya.

Kweli kabisa “wao (Wakristo) walimshinda  yeye (shetani) kwa damu ya Mwana-Kondoo, na KWA NENO LA USHUHUDA WAO; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa. (Ufunuo 12:11).

Baada ya kutubu, niliamua kuyatoa maisha yangu yote kwa Kristo. Nilitia saini agano langu la kwanza na Mungu ambapo niliachana na ndoto zangu zote za duniani; shauku zangu na matumaini yangu. Nilimpa Mungu haki zangu zote ili aamue iwapo niwe na kazi au la; kama nitaolewa au la. Katika agano langu nilijitoa kumtumikia Mungu bila kujali niko mwenyewe au nimeolewa; niwe na kazi au sina.

Wakati nikisoma Maandiko baada ya kuokoka kwangu, nimegundua kuwa sababu kuu ya mimi kuharibu imani yangu ni kuwa sikuwa nimefundishwa kwa usahihi mafundisho ya Yesu Kristo. Katika karne ya kwanza, Wakristo waliteswa na kufa kwa ajili ya Kristo na HAWAKUMKANA Kristo. Mimi sikuwa nimepokea shauku za tamaa zangu za kimwili ndiyo maana nikamkana Kristo!!! Unadhani hilo liliwafanya shetani na mapepo wafurahi?

Katika karne ya kwanza Wakristo walifundishwa mafundisho ya Kristo kuhusu kuvumilia mateso kwa ajili ya Kristo. Nilikuwa sikufundishwa au kusikia juu ya kuhesabu gharama ya kumfuata Kristo. Sikuwa nimesikia juu ya kustahimili mateso kwa ajili ya Kristo au  kwamba inanibidi nijikane mwenyewe, nibebe msalaba wangu na kumfuata Kristo. Sikuwa nimesikia au kufundishwa kwamba inabidi nikane ubinafsi wangu ili kumfuata Yesu (achilia mbali kujifunza namna ya kubaini ubinafsi hasa ni nini!)

Badala yake, katika vitabu vya Kikristo nilijifunza mafundisho ya mashetani kuhusiana na Mungu kutaka kunipatia kila kitu ambacho moyo wangu unakitamani. Kwa namna fulani labda sikuona sura kwenye vitabu hivyo ambayo inanionya kuwa Mungu hatanipatia kila shauku ya moyo wangu kama shauku hizo ni za ubinafsi na si sehemu ya mpango wa Mungu kwa maisha yangu. Ilikuwa ni makosa yangu mwenyewe kuamini mafundisho ya mashetani. Sikufanya kile ambacho Mungu ameniamuru kwenye Neno lake. Sikuijaribu kila roho kwa Neno la Mungu na sikuwa makini na manabii wa uongo na walimu wa uongo. Matokeo yake, niliamini mafundisho mengi ya mashetani.

Ilikuwa ni makosa yangu kuamini kila kitu nilichosoma kwenye vitabu vya Kikristo. Na pale Yesu alipoacha kutimiza shauku za moyo wangu za kidunia, na pale matizo yalipokuja maishani mwangu kama Yesu alivyoahidi katika Yohana 16:13, sikujua namna ya kustahimili. Kwa hiyo mwishowe nilianguka.

Hatima ya mafundisho ya mashetani ni kuwadanganya wateule na kusababisha imani yao kuharibika.

Yafuatayo ni mafundisho ya mashetani ambayo niliyaamini. Mafundisho haya ya mashetani yako kwenye makanisa mengi, vitabu, kanda na CD na kwenye intaneti:

1.   Kwamba Mungu anataka kukufanikisha kwa mali za kidunia na kwamba ‘kuridhika na ulichonacho’ (Tazama: 1 Tim 6:8 na Ebr. 13:5) maana yake ni kuridhika na si chini ya dola milioni moja.”

2.   Kwamba Mungu anataka kukupa kila haja ya moyo wako, na mapenzi yake kamili ni kujibu kila ombi utakaloomba – huku akijibu kama wewe unavyotarajia ajibu.” (Kwa maneno mengine, hakuna haja ya kutilia maanani ubinafsi).

3.   Kwamba shetani aliharibiwa kabisa msalabani, na kwamba shetani hana nguvu juu ya maisha ya Wakristo. Hivyo, usipoteze muda wako, hata wa dakika moja, kumfikiria. Vinginevyo, utakuwa unampa utukufu ambao unamstahili Yesu.”

4.   Shetani amefungwa na hawezi kuwagusa au kuwadhuru Wakristo – kwamba anachoweza yeye ni kudanganya tu. Wakati wa Ayubu ulishapita kwa sababu Yesu alishamshinda shetani msalabani. Hivyo, shetani hawezi tena kuwashitaki Wakristo mbele za Mungu. Kwamba shetani hawezi kuchukua chochote tena kutoka kwa Wakristo.

5.   Hauna haja ya kuteseka kwa ajili ya Kristo. Mateso si sehemu ya Wakristo tena.  

6.   Kila wakati Mungu anataka uwe mzima kimwili bila kutilia maanani mambo mengine. Vipi kama Mungu anataka kumpeleka mtu huyo mgonjwa nyumbani mbinguni? Vipi kama Mungu anataka kumfundisha jambo ambalo kwa njia nyingine hawezi kujifunza; kwa mfano kujifunza kumtukuza Mungu katika madhaifu yake? Vipi kuhusu watu wanaoshiriki meza ya Bwana bila kujihukumu na kujikagua wenyewe sawasawa? Maandiko yanasema kuwa watu wanaweza kuugua na kufa wangali na umri mdogo kutokana na kutojihukumu wenyewe sawasawa. (Tazama: 1 Wakorintho 11:29-31).  Inaonekana kwangu kwamba hekima inatutaka tuangalie uponyaji wa kimwili kama tunavyoangalia dhambi. Tunajua kuwa Mungu anataka dhambi yote iondolewe kwenye dunia, lakini hilo halitatokea hadi baadaye huko mbeleni. Japokuwa tuko salama kuamini kwamba uponyaji wa kila aina hakika umo ndani ya upatanisho kwa ajili ya watu wa Mungu, ni lazima tuwe na hekima ya kutomwacha shetani aharibu imani yetu pale tunapomtafuta Mungu kwa ajili ya uponyaji ... hasa pale uponyaji huo unapogoma kutokea licha ya kuomba kwetu kwa bidii.

7.   Kamwe usiseme, "Hata hivyo, si mapenzi yangu bali mapenzi ya Mungu yafanyike maishani mwangu," kama hukupata kutoka kwa Mungu kitu ambacho ulikiomba kwa Mungu. "Haujui mapenzi ya Mungu kwa maisha yako, hivyo unatakiwa kuendelea kuomba zaidi na zaidi ili Mungu akutendee kile unachokitaka.”

Yapo na mengine mengi zaidi – mafundisho ya kificho ya mashetani yanayoendelea kufundishwa. KAMWE usiamini kila kitu unachofundishwa kanisani au unachosoma kwenye vitabu vya Kikristo kabla ya kukijaribu kama kinaendana na ushauri wa Neno la Mungu katika Agano Jipya lote (pamoja na kanuni, miongozo na amri za Agano la Kale ambazo hazipingani na kweli iliyofunuliwa katika Agano Jipya, bali zinaiunga mkono). Unafanyaje hivyo?  Ibilisi anapenda kuchukua neno moja au mawili kutoka kwenye Maandiko ambayo yanazua maswali katika utekelezaji wake na kuyafanya yaseme kitu ambacho Mungu hata hakukikusudia. Kila inapowezekana, acha Maandiko yatafsiri Maandiko mengine. Acha hali ya kujirudia kwa mawazo yaliyo kwenye Maandiko kujithibitishe kwenyewe ili kuumba imani thabiti. Kutafsiri neno moja au mawili (au labda matatu au manne) katika tafsiri zetu za Biblia za kileo kusichukuliwe kuwa ni lazima kwamba kunaeleza kikamilifu maana iliyokusudiwa iliyokuwa kwenye lugha za asili za Kiebrania na Kigiriki. Maneno, na namna yanavyowasilishwa, yanaweza kubadilika kutoka utamaduni mmoja hadi mwingine kadiri muda unavyopita. Roho Mtakatifu atathibitisha kile kilicho cha muhimu kuamini na kipi sicho cha muhimu kutoka kwenye Maandiko ili kumpendeza Mungu Baba kama tutanyenyekea kiasi cha kutosha kukiri kuwa tunaweza kuwa tumekosea kutokana na kile tunachoamini juu ya maeneo kadha wa kadha ya Biblia ambayo hayaeleweki kirahisi. 

Wakati huohuo, katika jitihada zetu za kuelewa na kutumia sawasawa Neno la Mungu, tusisahau kamwe ukweli kwamba, ndicho chanzo pekee cha kuaminika ambacho Mungu amewapa wanadamu ili waweze kujua mapenzi ya Mungu. Neno la Mungu ndilo mapenzi ya Mungu. Mapenzi ya Mungu yamewekwa wazi kwenye Neno lake. Hatuna cha kujitetea kwamba hatuwezi kujua mapenzi ya Mungu yaliyowekwa wazi kwetu, (au miongozo ya namna ya kutafuta mapenzi ya Mungu kwa ajili ya maisha yetu kibinafsi), kama hatujui Neno la Mungu.

Huenda chapisho bora kabisa ambalo linaweza kumnufaisha sana mtu katika kujifunza jinsi ya kujua kwa njia salama na ya hekima kitu cha kuamini kuhusiana na Neno la Mungu linaweza kupatikana kwa kubofya: Hapa.

Kumbuka, katika jamii tajiri, mafundisho ya mashetani ni nadra sana kuwaambia watu kuwa ni lazima kuteseka kwa ajili ya Kristo, ni lazima kumpinga shetani na ni lazima kujikana mwenyewe, ubebe msalaba wako na kumfuata Kristo. Pale ambapo kuna utajiri mwingi wa kimwili, mafundisho mengi ya mashetani yana mvuto mkubwa kwa kimwili – karibu mara zote huwa ni kwa ajili ya kile ambacho Mungu anaweza kututendea na si kile ambacho tunatakiwa kutenda ili kumpendeza Yeye.   

Mafundisho ya mashetani karibu kila wakati huwa ni kwa ajili ya kulisha tamaa zetu za kimwili, zenye ubinafsi; yanalenga kupotosha maana na matumizi halisi ya Neno la Mungu; yanalenga kushushia hadhi usahihi na uhalisi wa Neno la Mungu; yanalenga kumpokonya Mungu utukufu anaostahili; yanalenga kuwadanganya na kuwajaribu watu ili wamchukie Mungu wakati kumbe ni shetani ndiye wanayetakiwa kumchukia.  

Shetani anataka watu waamini kuwa jehanamu si halisi ili kusiwepo na hofu yoyote ya Mungu na nia kuacha dhambi; kwamba mapepo hawapo au kwamba hayana nguvu kabisa juu ya watu waliookoka kwelikweli, maana kwa njia hiyo, Wakristo hawatamtafuta Mungu kwa ajili ya kupewa uwezo wa kufanya kile wanachotakiwa kufanya katika kusaidia kupambana na kazi za kipepo duniani na kwenye maisha ya wapendwa wao. Orodha ya udanganyifu wa shetani inaendelea na kuendelea ...

Shetani amejaribu, na hataacha kamwe kuendelea kujaribu, kuwafanya watu wa Mungu wasitambue kuwa Neno la Mungu lililoandikwa ndilo pekee lenye mamlaka ambalo Mungu analiafiki na kulitia nguvu.

Hii ndiyo amri ya Mungu: Kwamba uyajaribu mafundisho yote unayoyasikia kanisani au unayoyasoma vitabuni au kwenye intaneti na kuwa makini na manabii wa uongo na walimu wa uongo. Kama hujasoma sawasawa Agano Jipya bado, basi waendee waelewa kadhaa tofauti wa Biblia wa kiprotestanti kabla ya kuumba imani yako thabiti juu ya jambo lolote. Duka lolote la vitabu vya Kikristo linaloheshimika linaweza kukutajia waelewa hao. Kama hakuna duka karibu, bofya tovuti hii na kuwauliza. Wanaaminika na wanaweza kukuelekeza kwenye mwelekeo sahihi: www.gospelcom.net 

1 John 4:1  Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani.

Philippians 3:2  Jihadharini na mbwa, jihadharini na watendao mabaya, jihadharini na wajikatao.

Kumbuka: mafundisho ya mashetani yana uwezo mkubwa sana ya kumharibu Mkristo kama ukiyaamini na kuyafuata. Mafundisho ya mashetani yatakufanya usiwe na nguvu kwenye ufalme wa Yesu na badala yake ukawa ni mtu wa kufuata tu ubinafsi wako au yatafanya imani yako ife kabisa. 

Shetani amejitoa kwa nguvu zote kufanya vita dhidi ya wafuasi wa Kristo. Ni wale TU wanaofuata mafundisho sahihi ya Kristo ndio wataweza kupona mashambulizi makali ya adui na kupokea “taji ya uzima” kutoka kwa Mungu.

Ni lazima umwombe Mungu akufundishe jinsi ya kupambanua kati ya uongo na kweli. Kumbuka kuwa kamwe hutaweza kushinda uongo wa shetani kwa nguvu zako pekee. Ni kwa nguvu za Yesu TU ndipo utaweza kuutambua uongo wa adui.

Nakutia moyo usome Biblia kwa bidii, kila siku. Mungu ndiye Mwalimu BORA kabisa. Hakuna kitabu au mahubiri yoyote yanayoweza kuchukua nafasi yote ya ushauri na mafundisho kutoka kwa Mungu mwenyewe moja kwa moja.  Shauku ya Mungu kwa ajili ya watoto wake ni waijue kweli na kuweza kupambanua kati ya jema na baya kama inavyosemwa kwenye Waebrania 5:14.

Mimi si pekee niliyeangukia kwenye uongo wa shetani; wako wengi wanaopita kwenye matatizo kama niliyopitia mimi. Ni kwa sababu tu ya rehema na neema kuu za Mungu ndiyo maana alinivuta nirudi kwake na akanikomboa kutoka kwenye nguvu za shetani. 

Ninamwomba Mungu atumie ushuhuda huu wangu kwa ajili ya kueneza Ufalme wa Yesu na kuharibu ufalme wa shetani.

Endapo unanyanyaswa na nguvu za giza, au uko tayari kuachana na Ukristo kwa vile unahisi kuwa Mungu amekusaliti, kama ambavyo nami nilidanganywa na kuamini hivyo, unaweza kuniandikia baruapepe. Nitafurahi kumtumikia Bwana wangu Yesu katika kujibu maswali yako.

Anwani yangu ya baruapepe ni:  ok2004@columbia.edu 

***************
[Angalizo za blogger: Kwa kuwa ushuhuda huu nimeutafsiri kutoka kwenye Kiingereza, mwandishi wake si Mswahili. Hivyo, kama utamwandikia, ni muhimu iwe ni kwa lugha ya Kiingereza.]
***************

Kama ushuhuda huu umekubariki, tafadhali tumia muda mfupi kutushirikisha JINSI ulivyobarikiwa. Kusikia kutoka kwako ni muhimu sana. Tafadhali taja mwandishi wa ushuhuda huu na kichwa cha ushuhuda wenyewe unapotuandikia baruapepe yako. Asante sana! Baruapepe yetu ni: ptoffice@precious-testimonies.com

***************
[Angalizo za blogger: Kama utapenda kuwaandikia jinsi ulivyobarikiwa, tafadhali hapa pia tumia lugha ya Kiingereza. Jina la mwandishi wa ushuhuda, kama ulivyoona mwanzoni, halikutajwa. Lakini kichwa cha ushuhuda ni “I Felt Betrayed by God”]13 comments:

 1. I will immediately snatch your rss feed as I can not to find your email subscription hyperlink or e-newsletter service. Do you’ve any? Please permit me understand in order that I could subscribe. Thanks.

  ReplyDelete
 2. Can I just say what a relief to find someone who actually knows what theyre talking about on the internet. You definitely know how to bring an issue to light and make it important. More people need to read this and understand this side of the story. I cant believe youre not more popular because you definitely have the gift.

  ReplyDelete
 3. Hello.

  I am glad to see your comments. Sorry for my missing my rss feed.

  May I say that I really am not yet very competent in blogging, so there are many things that i still don't understand how to manipulate them - even though they may be very easy for others.

  One of the things is this RSS. Another is comments. I have been trying to set this blog in a way that allows Threaded Comments. I havent been able to do it so far.

  So, please, bear with me as I go on learning how to do these things. By the grace of God, I will find someone who will help me to sort them out.

  May the Lord bless you.

  ReplyDelete
 4. I don't even know how I ended up here, but I thought this post was good. I don't know who you are but certainly you are going to a famous blogger if you aren't already ;) Cheers!

  my blog creative group

  ReplyDelete
 5. Hi there to every body, it's my first go to see of this webpage; this blog contains remarkable and actually excellent information for visitors.

  my blog post - email newsletters templates

  ReplyDelete
 6. Thank you for the good writeup. It in fact was a amusement
  account it. Look advanced to far added agreeable from you!
  However, how can we communicate?

  Also visit my webpage: simply click the up coming website page

  ReplyDelete
  Replies
  1. Hi. You seem to have written so many comments. But you hardly say anything specifically referring to the topic in question. You are very vague.

   Delete
 7. Mmh mtumishi James. Ushuhuda huu ni mzito sana na bila roho mtakatifu kukupa mafunuo huwezi elewa kitu. Nimeona alivyo identify siri za kipepo katika kucontrol maisha ya kikistro kwa njia ya uwongo.naomba clarification zifuatazo
  1. Inamaana kupiga mziki katika maombezi au vyombo vya mziki,au kusifu na kuabudu wakati wa kufanya maombezi au kabla ya maombezi according ulivyotafisiri ni kuamsha hisia wala hakuna uwepo wa Mungu?
  2. Mwandishi anasema kuna wakati aliingia katika mtego wa kishetani kuingia katika website ya kishetani sasa je kusudi tusije kurudia makosa wewe binafsi ulishafanyia kazi hii mitandao ya precioustestmonies.com,gospel.com.net ya mwisho hiyo ni kucheki kama neno hilo ulilolipata ni la kweli au laah.Na je njia nzuri ni kutegemea iyo website ya kuclarify kama neno ilo la ukweli au kushirikisha wachungaji wetu.
  3. Anachofundisha uyu bwana kutokana na alichopitia haya mafunzo hata mimi yaani. Precaution! Lakini jee tunajaribu vip kila neno linalotoka kila kwa nabii.au mafunzo au kitu chochote. Je how do u test? Biblia imetoa precaution kuwa tutest according to maandiko. Lkn tuna test vip? yes nisaidie hayo kwanza.

  ReplyDelete
  Replies
  1. Ndugu James. Bwana Yesu asifiwe. Pole na majukumu. Najua upo bize. Lakin pia hujui jinsi hii blog ilivyoongeza nguvu ya Mungu ndani yangu. Yan kuna siku nitatoa shuhuda. Pia naomba unijibu hayo maswali hapo juu. Barikiwa na bwana

   Delete
  2. Shalom Joseph,


   UMEULIZA KUHUSU KUPIGA MUZIKI:
   Biblia inaongelea sehemu nyingi kuhusu kumwimbia Bwana na pia kumpigia muziki tena kwa vyombo mbalimbali. Kwa mfano:
   MWIMBIENI Bwana zaburi, Enyi watauwa wake. Na kufanya shukrani. Kwa kumbukumbu la utakatifu wake. (Zaburi 30:4)


   MWIMBIENI BWANA WIMBO MPYA, Na sifa zake tokea mwisho wa dunia; Ninyi mshukao baharini, na vyote vilivyomo, Na visiwa, nao wakaao humo. (Isaya 42:10)


   Haleluya. MWIMBIENI Bwana wimbo mpya, Sifa zake katika kusanyiko la watauwa. Israeli na amfurahie Yeye aliyemfanya, Wana wa Sayuni na WAMSHANGILIE mfalme wao. Na WALISIFU jina lake kwa KUCHEZA, KWA MATARI NA KINUBI WAMWIMBIE. Kwa kuwa Bwana awaridhia watu wake, Huwapamba wenye upole kwa wokovu. (Zaburi 149:1-4)


   Anachoongelea huyu dada mwenye ushuhuda huu sio KATAZO la kumwimbia Bwana na kumpigia. Hebu tuanze kwa kuangalia mfano huu:
   “Msilete tena matoleo ya ubatili; uvumba ni chukizo kwangu; mwezi mpya na sabato, kuita makutano; siyawezi maovu hayo na makutano ya ibada. Sikukuu zenu za mwezi mpya na karamu zenu zilizoamriwa, nafsi yangu yazichukia; mambo hayo yanilemea; nimechoka kuyachukua.” (Isaya 1:13-14).


   Mungu ndiye aliyeagiza kwenye agano la kale watu washerehekee sikukuu kadhaa na kutunza sabato. Iweje basi aongee hapa kwa kuyachukia kiasi hiki mambo yaleyale ambayo aliyaagiza mwenyewe?


   Kumbe tunaona tatizo haliko kwenye maagizo menyewe, bali ni hapa:
   “Msilete tena matoleo ya UBATILI.”


   SIKU ZOTE, iwe ni sadaka, msaada, sala, n.k., hukubalika mbele za Mungu kutokana na hali ya moyo ya mwanadamu (attitude towards God). Yaani, unachofanya, unafanya kwa sababu gani?


   Je, unaenda Kanisani kumwabudu Mungu au unaenda tu kuburudishwa na magitaa na muziki mtamu kwa sababu ya shida zako na mawazo na huzuni ulizo nazo. Ni wazi kuwa muziki ni kitu kinachoamsha hisia za watu. Lakini NJE YA HAPO, uhusiano wako na Mungu ukoje?


   Uhusiano na Mungu unatakiwa kuwa ni jambo la kudumu – kila saa kila sekunde. KILA unalosema, unalowaza na unalotenda ni lazima ujiulize kama Bwana analiridhia.


   “Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye.” (Kol 3:17)


   Mtu mwenye mtazamo huu, hawezi kutenda jambo ovu kwa sababu eti hakuna mtu anayemwona; maana hofu yake haiku kwa wanadamu bali kwa Bwana. Wakati wote anakuwa aware kwamba jicho la Bwana linamwangalia. Na siku zote anatafuta kumpendeza Bwana.


   Kwa hiyo, mtu wa hivi, hata muziki wa Kanisani ukipigwa, yeye anapoimba, anapocheza, anakuwa anafanya hivyo kwa ajili ya Bwana – SIO KWA AJILI YA KUTAFUTA FARAJA KWA SABABU ALIGOMBANA NA MUME AU MKE WAKE NYUMBANI.


   NJE YA HAPA, kuimba au kucheza kwetu muziki ni UBATILI na machukizo mbele za Bwana. Na ndicho anachokikataa kwa hasira Bwana hapo juu kwenye Isaya 1 – yaani: “MSILETE MATOLEO YA UBATILI.


   Kwa maana nyingine: LETENI MATOLEO LAKINI SITAKI MATOLEO YA UBATILI.

   Delete
  3. UMEULIZA KUHUSU MTEGO WA KUINGIA KWENYE WEBSITE ZA KISHETANI

   Unaposoma ushuhuda huu, unatambua jambo moja kwamba – alipita kwenye kipindi fulani cha uchanga wa kiroho. Alikuwa ni mtu anayemtafuta Mungu, lakini alikuwa katika ile hatua ambayo MTU HUWA ANAWAZA KUWA NI LAZIMA MUNGU ANIPE KILA NIOMBACHO KWA WAKATI NITAKAO KWA KUWA NIMEOMBA.

   Kisha akicheleweshwa kidogo; au akitikiswa kidogo na jaribu, anatetereka na kumwacha Bwana. Huu ni uchanga wa kiroho.

   Mtu anayemjua Bwana na amesimama sawasawa na amekua kiroho ana msimamo wa Shadraki, Meshaki na Abednego:
   Ee Nebukadreza, hamna haja kukujibu katika neno hili. Kama ni hivyo, Mungu wetu tunayemtumikia aweza kutuokoa na tanuru ile iwakayo moto; naye atatuokoa na mkono wako, Ee mfalme. BALI KAMA SI HIVYO, UJUE, EE MFALME, YA KUWA SISI HATUKUBALI KUITUMIKIA MIUNGU YAKO, wala kuisujudia hiyo sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha. (Danieli 3:17-18).

   Anajua kuwa Mungu ni MWAMINIFU TU, hata kama mambo yanaonekana hayaendi sawa kama alivyoomba au kutarajia. Mtu wa aina hii anakuwa amesimama kwenye Mwamba usiotikisika.

   Na Yesu anasema wazi:
   “Tazama nimewapa amri (authority) ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, WALA HAKUNA KITU CHOCHOTE KITAKACHOWADHURU.” (Lk 10:19).

   Ukiwa umesimama sawasawa na Yesu hakuna kazi YOYOTE YA KUZIMU itakayokushinda – iwe ni website ya wachawi au ya ibilisi mwenyewe. Lakini bila hivyo, ni rahisi na inawezekana kabisa kuathiriwa au kudhuriwa kama ilivyokuwa kwa huyu dada.

   Delete
  4. UMEULIZA KUHUSU KUZIJARIBU ROHO

   Kuzijaribu roho, kunahitaji mambo makuu mawili.

   Kwanza ni lazima ujenge uhusiano wako na Yesu (Roho Mtakatifu) SIKU HADI SIKU – kuomba, kusoma Neno lake na kumtii kadiri anavyokuongoza. Na katika utendaji (real practice) tu ndipo unaweza kujifunza KIBINAFSI kutambua sauti ya Roho Mtakatifu – wengine husikia sauti wazi kama ilivyo kwa huyu dada, na wengine inakuwa tu kama wazo linakujia. With time unakuwa unaweza kutofautisha kati ya Roho Mtakatifu na mawazo binafsi – si kitu unachoweza kukijua sawasawa kutokana na maelezo ya mtu mwingine.

   Kondoo wangu WAISIKIA SAUTI YANGU; nami nawajua, nao wanifuata. (Yoh 10:27).


   Ukiwa mtii kwa Bwana, kweli kabisa hatakuacha upotee. Si kwamba hautaingia kwenye matatizo – NI LAZIMA ATAKUPITISHA HUKO. LAZIMA! Lakini kwa kuwa una tunda la Roho, UVUMILIVU utakutunza hadi wakati wa kujibiwa kwako kwa kuwa UNAMWAMINI Bwana; na Bwana ni mwaminifu.

   Pili, ukishakuwa na Neno la kutosha ndani yako – ndipo kila jambo unalosikia, wazo linalokujia, n.k., unaweza kujua kuwa ni la kweli au si la kweli kwa sababu ama linakubaliana na Neno la Mungu au linapingana nalo. Kama linapingana na Neno la Mungu, hiyo ni roho ya uongo hata kama anayesema jambo hilo ni askofu au mchungaji wako.

   Delete