Sunday, October 21, 2012

Majibu ya Ndugu Hamudi – Sehemu ya I

Katika blog hii kuna makala yanayosema “Ndugu Waislamu Nisaidieni.” Nashukuru kwamba ndugu Hamudi amejitokeza kujibu maswali yangu kadhaa niliyokuwa nimeuliza. Lakini pia, baada ya kufanya hivyo, ndugu Hamudi ameuliza maswali si machache. Nami nimeona kuwa niyaweke hapa pamoja na kile nilichojibu, kama makala ili kwamba, hata mtu mwingine anayependa kuchangia, afanye hivyo.

Ndugu Hamudi, asante tena kwa maswali yako yenye kutikisa akili na fahamu za mtu. Ni lazima nikiri kuwa haya ni maswali ambayo, hakika, kama hujui sawasawa kile unachokiamini, ni lazima ama utachanganyikiwa au utakimbia.


Umeweka maswali yako katika mafungu kadhaa. Kuna maswali kuhusu utatu, wokovu, Roho Mtakatifu, n.k. Nitajibu fungu moja baada ya jingine katika makala tofauti tofauti.

Japokuwa si sahihi sana kujibu maswali haya mojamoja, maana yanakosa kuona picha na makusudi ya jumla ya mpango wa Mungu kwa mwanadamu, lakini acha nifanye hivyo, kisha nitatoa jibu la jumla mwishoni kabisa ili kuweza kuona kila kitu kwa ukamilifu wake:


UTATU


1.Hamudi anasema: Kwa mujibu wa Wakristo wengi, Yesu amekuwa ni Mungu-mtu, mtu kamili na Mungu kamili. Je, kitu chenye mwisho na kile kisicho na mwisho vinaweza kuwa ni kimoja? Kuwa “Mungu kamili” maana yake ni kutokuwa na mwisho na kutohitajia msaada, na kuwa “mtu kamili” maana yake ni kutokuwa na uungu.


Nianze kwa kusema kuwa, umungu-mtu wa Yesu si kwa mujibu wa Wakristo, bali ni kwa mujibu wa Biblia yenyewe. Imeandikwa: Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. (Yohana 1:1). Kisha ikaandikwa: Alikuja kwake (yaani duaniani), wala walio wake hawakumpokea. (Yoh. 1:11).
Umeuliza iwapo chenye mwisho kinaweza kuwa kimoja na kisicho na mwisho. Hamidu, naomba nikuulize: Je, wewe una mwisho? Napenda nikutaarifu kuwa, wewe na mimi hatuna mwisho. Sisi ni viumbe wa milele na milele yote! Najua hapa bado sijakamilisha jibu lako, lakini nivumilie hadi nitakapofika kwenye jibu la jumla.

2.Hamudi anasema: Kuwa mtoto ni kuwa chini ya daraja ya uungu na kuwa na uungu ni kutokuwa mtoto wa yoyote. Vipi Yesu atakuwa na sifa ya utoto na uungu kwa wakati mmoja?


Ni kweli Yesu alikuwa na sifa ya utoto na kuwa chini ya daraja. Biblia inasema: umemfanya mdogo punde  kuliko malaika (Waebrania 2:7). Yaani, alikuwa mkuu, lakini ukamshusha daraja hadi chini kidogo ya daraja la malaika. Sababu yake nitakutajia mwishoni.


3.Hamudi anasema: Wakristo wanadai kwamba Yesu alidai kuwa yeye ni Mungu wakati walipomnukuu katika Yohana 14:9: “…Aliyeniona mimi amemwona Baba…” Je, Yesu hakusema wazi wazi kwamba: kamwe watu hawakumuona Mungu, kama inavyosema Yohana 5:37: “Naye Baba aliyenipeleka amenishuhudia. Sauti yake hamkuisikia wakati wowote, wala sura yake hamkuiona”?


Kimsingi kabisa, Mungu ni roho. Hata mimi na wewe, kimsingi ni roho. Kwa sababu hiyo, wewe unajijua na wakati huohuo hujijui. Unajijua kwa maana ya mwili wa nje unaoonekana. Lakini wewe halisi, yaani roho, wala hujui ulivyo. Kumjua Mungu, wakati tungalipo duniani, ni kwa imani. Katika Yoh. 14:9, Bwana Yesu anatumia neno ‘kusadiki’. Hapa anaongelea si tu kuwa Filipo na mitume wenzake wamemwona kimwili, kwa macho ya nyama, bali pia wamesadiki (wameamini) kuwa yeye ni Mungu. Katika Yoh. 5:37 anatumia neno lilelile anapowaambia watu kuwa hawakumwona Mungu wakati wowote. Yaani anasema: kwa kuwa ninyi hammwamini yule aliyetumwa na yeye. Kuamini = kusadiki. Hivyo, wenye imani hapa duniani wanamwona Mungu. Wasio na imani hawamwoni, hata kama wote hawa wanasikia ujumbe uleule.


4.Hamudi anasema: Wakristo wanasema kwamba Yesu alikuwa ni Mungu kwa sababu alikuwa anaitwa mtoto wa Mungu, Mtoto wa mwanadamu, Masiha, na “mwokozi.” Ezekieli aliandikwa katika Biblia kama ni mtoto wa Mungu. Yesu alinena kuhusu “waletao amani” kuwa ni watoto wa Mungu. Mtu yoyote aliyefuata matakwa na mipango ya Mungu alikuwa akiitwa MTOTO WA MUNGU katika utamaduni wa Kiyahudi na katika lugha yao (Mwanzo 6:2,4; Kutoka 4:22; Zaburi 2:7, Warumi 8:14). Neno “Messiah” ambalo kwa Kiebrania linamaanisha “Mpakwa Mafuta wa Mungu” sio “Kristo”, wala “Cyrus” na mtu huitwa “Messiah” au “mpakwa mafuta”. Ama kuhusu neno “mwokozi” lililopo katika Wafalme wa pili 13:5, watu wengine walipewa jina hilo vilevile bila ya kuwa miungu. Kwa hivyo, katika maneno hayo uko wapi uthibitisho unaoonesha kuwa Yesu ni Mungu wakati neno mtoto halikutumiwa kwake peke yake?


Naamini kuwa mtu mzima yeyote akikutana na mtoto anaweza kusema, “Hujambo mwanangu?” au sivyo Hamudi. Lakini, je, tendo hilo linamfanya aliyeitwa ‘mwanangu’ awe sawa na mtoto wa kuzaliwa? Bila shaka jibu ni hapana. Hizi ni maana mbili tofauti; na tofauti yake iko wazi tu. ‘Mwanangu’ wa kuzaa na ‘mwanangu’ wa kuitwa kwa sababu ya umri mdogo kwangu ni neno lilelile lakini maana tofauti, japo zina uhusiano. Nakubaliana kabisa na wewe kwamba mtu yeyote anayemtii Mungu anaitwa mtoto wa Mungu. Lakini tunafahamu pia kuwa kila mwanadamu ametoka kwa baba na mama yake. Mama wa Yesu tunamjua – ni Mariamu. Baba yake ni nani? Najua kuwa kwa swali hili, Waislamu huwa mnatoa hoja kwamba hata Adamu naye hakuwa na baba kama sisi. Ndiyo. Lakini Yesu alikuwa na mama. Adamu hakuwa na mama. Yesu alikaa tumboni miezi 9 na kuzaliwa kama sisi; haikuwa hivyo kwa Adamu. Kuwapo kwa Yesu, kulikuwa na mchango wa mbegu ya mwanamke, lakini si kwa Adamu. Sasa, kama Yesu alitokana na mbegu ya kike – baba yake alikuwa ni nani? Jibu liko wazi tu, Hamudi.


Unasema kuwa  neno ‘messiah’ kwa Kiebrania ni ‘mpakwa mafuta’ ila sio ‘Kristo’. Sijui kwa nini unasema hivyo kwa sababu ‘messiah’ ni Kiingereza, ‘masih’ ni Kiebrania na kwa Kiyunani ni ‘kristos’, ambalo linatupatia ‘Christ’ na ‘Kristo.’. Neno ‘Cyrus’ wala halihusiani na ‘Kristo’. Sijajua ni kwa nini umeliweka hapa. Lakini hili ni jina linalomaanisha ‘jua’. Ni kitu kingine kabisa mbali na ‘masih’. Kuhusu neno ‘mwokozi’ ni kweli kwamba hili si jina la Yesu pekee. Lakini swali ni kuwa unaongelea kuokoa kutoka kwenye nini? Nyumba ya jirani yako ikiwaka moto ukawahi kuwatoa watoto wake nje, hakuna shaka yoyote kwamba wewe umekuwa ni mwokozi wao. Sasa katika 2 Wafalme 13:5, inaongelea mtu aliyewatoa Israeli mikononi mwa Washami. Ndiyo, huyo aliwaokoa Israeli; alikuwa ni mwokozi wao. Lakini kumbuka kuwa Yesu si mwokozi wa kuwatoa watu kwenye mambo ya kimwili. Uokozi wake ni wa jambo kuu kabisa; la juu zaidi – Yeye amewaokoa wanadamu kutoka kwenye JEHANAMU YA MOTO na KUTENGWA NA MUNGU MILELE! Ametulipia dhambi zetu kwa kujitoa sadaka hadi kufa ili sisi tusife kwa dhambi zetu, bali tuokolewe kwa kuamini na kukubali sadaka aliyotoa kwa niaba yetu. Hiyo si kazi ya mwanadamu yeyote.


Wale wote waliomwamini Yesu na kupokea wokovu wake watakapofika mbinguni, na Mungu akawaonyesha jehanamu ya moto ilivyo, hapo ndipo watakapotambua kwa usahihi jinsi ilivyo kuu sadaka ya Yesu aliyoitoa kwa ajili ya sisi wanadamu. Lakini wale walioikataa sadaka yake – wakakataa kuokoka kwa njia rahisi sana ya imani – wakidhani kuwa kwa matendo yao wanaweza kununua nafasi zao kwenye mbingu takatifu za Mungu aliye hai – oh! Ni uchungu na kilio kikuu cha milele! – maana hawajaweza na hawataweza – kwa kuwa mwanadamu hajaumbwa kuweza kutimiza sheria ya Mungu kwa asilimia zote kwa nguvu zake mwenyewe! Sijui ndugu Hamudi kama wewe umeweza?


5.Hamudi anasema: Wakristo wanadai kwamba Yesu alikiri kwamba yeye na Mungu walikuwa ni kitu kimoja kwa maana ya kimaumbile pale anaposema katika Yohana 10:30; “Mimi na Baba tu umoja.”  Baadaye katika Yohana 17:21-23, Yesu alinena kwamba wafuasi wake, yeye mwenyewe na Mungu ni kitu kimoja katika sehemu tano. Sasa kwa nini walipe neno “Kitu kimoja” la kwanza maana nyingine tofauti na yale maneno “kitu kimoja” katika sehemu tano nyinginezo?


Kama nilivyosema, kujibu swali moja moja, kimsingi hakutoi picha nzuri ya kueleweka. Hivyo, katika jibu langu la jumla mwishoni, swali hili nalo litajibiwa. Lakini pia niseme hapa kuwa, hakuna Mkristo hata mmoja anayesema kuwa Yesu na Mungu ni kitu kimoja, nikinukuu maneno yako, “kwa maana ya kimaumbile.” Hiyo habari ya kimaumbile haipo kabisa! Biblia wakati wote msisitizo wake  kimsingi ni ujumbe wa rohoni si mwilini.


6.Hamudi anasema: Je, Mungu ni watatu-katika-mmoja na ni mmoja katika watatu kwa wakati mmoja au ni mmoja kwa wakati huo huo?


Mungu wetu si watatu katika mmoja; wala si mmoja katika watatu; bali ni mmoja katika utatu.


Ningependa uniambie unaelewa nini katika maneno haya:

Sura ya Al-Nisa 4:171
Al-Masih, Isa son of Mariam, was no more than Allahs Apostle and His Word which He cast to Mariam; a spirit from Him.
Yaani: Masih,
Isa mwana wa Mariam, alikuwa ni Mtume wa Allah na Neno Lake alilolituma kwa Mariam; roho kutoka Kwake, na si zaidi ya hapo. (Al-Nisa 4:171).
Katika swali namba 10 hapa chini umenitolea mantiki hii: B = G, M = G na R = G; kwa kufuatanisha inakuwa B = M = R. Nami ningependa niulize kwa kutumia mantiki kama ifuatavyo:
Kama Isa ni Neno (N) la Allah (A);
Na kama Isa ni roho (R) ya Allah;
Je, N si = A? A si = R? R si = A?
Je, wewe na roho yako mko tofauti?
Je, neno lako na wewe ni tofauti?

Naamini unafahamu na unakubaliana na Quran kuwa unatakiwa kusoma Injili (Tazama sura Al - Imran 3:2-3) ili kufahamu ujumbe wa kweli wa Mungu aliye hai. Pia Quran inakuagiza katika Sura ya Yunus 10:94 kuwa, Kama mna shaka juu ya yale tuyowafunulia, waulizeni wale waliokisoma Kitabu (Biblia) kabla yenu. Sina uhakika ni Waislamu wangapi wanasoma Biblia ili kupata uzima. Lakini nina uhakika wako wengi wanasoma Biblia ili kutafuta makosa. Sana sana, wengi wameshikilia kuwa Biblia imepotoshwa; Biblia imepotoshwa. Je, Mungu anayejua mambo yajayo angeweza kuwaagiza msome jambo ambalo alijua kuwa baadaye lingepotoshwa?

Kitabu cha injili kinasema nini sasa? Kinasema kwamba: Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. (Yohana 1:1).

Na unaposoma kuhusu Mariamu kutembelewa na malaika Gabrieli, na kuletewa habari za yeye kumzaa Yesu, maandiko yanasema kuwa malaika alisema na Mariamu baada ya kuulizwa swali:

Litakuwaje neno hili, maana sijui mume?
Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu.   (Luka 1:34-35).

Kumbe hapa tunakutana na maneno yaleyale kama kwenye Al - Imran 3:2-3: Aliye juu; Roho Mtakatifu;  Neno. NI MUNGU YULEYULE! Tofauti tu ni kuwa haya yanaenda mbele zaidi na kusema wazi kuwa Neno alikuwa ni Mungu!

7.Hamudi anasema: Ikiwa Mungu ni mmoja na watatu kwa wakati mmoja, kwa hiyo hakuna hata mmoja kati ya hao watatu ambaye ni Mungu kamili. Tukikubali kwamba huo ndio ukweli, sasa je, wakati Yesu alipokuwa duniani, hakuwa Mungu kamili, wala “Baba aliye mbinguni” hakuwa Mungu kamili. Je, hilo halileti mkanganyiko kwa kile alichokuwa akikisema Yesu kila siku kuhusu Mungu wake na Mungu wetu aliye mbinguni, Bwana wake na Bwana wetu? Je, hilo vilevile halimaanishi kwamba hakukuwa na Mungu kamili, katika kipindi cha kati ya dai la kusulubiwa na dai la kufufuka?


Nakubaliana nawe Hamudi kuwa hili linaleta mkanganyiko kwa namna ya kimwili. Lakini kwa namna ya rohoni hakuna kabisa mkanganyiko hata kidogo. Hapa tunaongelea Mungu awezaye mambo yote; aliyekuwa amekuja kutimiza makusudi fulani katika ulimwengu huu. Kuona kuwa hili haliwezekani hakuna tofauti na kuhoji kwamba: “Inakuwaje watu milioni moja wanamwomba Mungu Marekani na milioni kumi wako Indonesia; milioni hamsini wako China, n.k. halafu wote wasikilizwe?” Jibu ni rahisi tu. Anayeombwa ni Mungu si mwanadamu!


8.Hamudi anasema: Ikiwa Mungu ni mmoja na watatu kwa wakati mmoja, sasa nani aliyekuwa Mungu huko mbinguni wakati Yesu alipokuwa aridhini? Je, hili halileti mkanganyiko na yale aliyokuwa akiyasema mara nyingi juu ya kuwa Mungu aliyembinguni ndiye aliyemtuma?


Jibu ni kama namba 6 hapo juu.


9.Hamudi anasema: Ikiwa Mungu ni mmoja na watatu kwa wakati mmoja, je, nani aliyekuwa Mungu huko mbinguni katika zile siku tatu zilizo kati ya dai la kusulubiwa na dai la kufufuka?


Jibu ni kama namba 6 hapo juu.


10.      Hamudi anasema: Wakristo husema kwamba: “Baba (B) ni Mungu, Mwana (M) ni Mungu na Roho Mtakatifu (R) ni Mungu, lakini Baba si mwana, na Mwana si Roho Mtakatifu, na Roho Mtakatifu si Baba”. Kwa hesabu rahisi na kwa kanuni inakuwa hivi, ikiwa B = G, M = G na R = G; kwa kufuatanisha inakuwa B = M = R, wakati sehemu ya pili ya maelezo hayo inaonesha kuwa B№ M№ R (inamaanisha haziko sawa). Sasa je, huo si mkanganyiko na imani ya Wakristo juu ya utatu wenyewe?


Jibu kinyume chake. Biblia haisemi kamwe kuwa Baba si Mwana; Mwana si Roho Mtakatifu; Roho Mtakatifu si Baba. Bali inasema kuwa Baba ni Mwana; Mwana ni Roho Mtakatifu; na Roho Mtakatifu ni Baba. Hivyo, hakuna mkanganyiko hata kidogo.


11.      Hamudi anasema: Ikiwa Yesu alikuwa Mungu, kwa nini alimwambia yule mtu aliemwita Yesu “Bwana Mwema” kuwa asimwite “mwema” kwa sababu hakuna mwema ila Mungu wake aliye mbinguni peke yake?


Ukiwa mwenyekiti wa mkutano halafu mtu akakwambia “Bwana Hamudi naomba niseme jambo” bila shaka utamwambia asiseme na Hamidu bali aseme na mwenyekiti (au aseme na kiti), japo ni wewe huyohuyo. Je, hapo kutakuwa na Hamudi wawili? Yesu alikuja kama Mwana, lakini alitaka tutambue kuwa mwisho wa yote, kila kitu kinatoka kwa Baba. Baba ndiye Mkuu; ingawaje ni Yeye huyohuyo. Ni suala tu la protokali.


12.      Hamudi anasema: Kwa nini Wakristo wanasema kwamba Mungu ni watatu katika mmoja na mmoja katika watatu, wakati Yesu alisema katika Marko 12:29. “Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja” kama ilivyo katika sehemu nyingi ndani ya Biblia.


Uko sahihi kabisa kwamba Mungu ni mmoja. Ni lazima utambue kwamba ni wengine, hasa ninyi Waislamu, ndio mnaotuwekea maneno hayo midomoni mwetu kana kwamba ni sisi tulioyasema. Sisi hatujawahi kusema kuwa Mungu ni watatu na hatutasema hivyo. Siku zote na daima Mungu ni mmoja; na huo ndio msimamo wa Biblia na imani ya Kikristo. Rais wa Tanzania ni rais wa nchi lakini pia ni mwenyekiti wa chama chake cha mapinduzi. Je, yeye ni wawili katika mmoja? Hapana.


13.      Hamudi anasema: Ikiwa kuamini utatu lilikuwa ni jambo la lazima ili uwe Mkristo, kwa nini Yesu hakulifundisha na wala hakulisisitiza jambo hilo kwa Wakristo katika zama zake? Je, vipi hao wafuasi wa Yesu wachukuliwe kuwa ni Wakristo bila ya kulisikia neno utatu? Kama ingekuwa utatu ndio uti wa mgongo wa Ukristo, Yesu angeliufundisha na angeliusisitizia na angeliufafanua kwa watu wake kikamilifu.


Sielewi Hamudi kwako ili kuonekane ni kusisitiza kunatakiwa kuwe mara ngapii? Biblia inasema kuwa kila neno lenye pumzi ya Mungu, (2 Timotheo 3:16) yaani Biblia yote, lafaa kwa mafundisho, hata kama lingesemwa mara moja tu. Sasa sijui inatakiwa lisemwe mara ngapi ndipo liwe na umuhimu. Lakini mimi nikwambie ukweli, Roho Mtakatifu amesemwa sana na Bwana Yesu. Kwa mfano:

Si kwa uwezo, wala si kwa nguvu, bali ni kwa roho yangu, asema Bwana wa majeshi. (Zekaria 4:6). Yaani huwezi kufanya lolote la kufaa mbele za Mungu kama haliwezeshwi na Roho Mtakatifu.


Na ndiyo maana hata Quran inasema: Tulimpatia Isa, mwana wa Mariam, ishara zisizo na shaka na kumtia nguvu kwa Roho Mtakatifu. (Al-Baqarah 2:87). Bila Roho Mtakatifu hufui dafu mbele ya shetani Hamudi. Utakuwa unapoteza muda na mwisho wake utakuwa mbaya rafiki.


Unaweza kuangalia pia Mathayo 10:20, 12:28. Luka 4:14, 4:18, 11:13. Yohana 3:5-8, 7:39, 14:17, 15:26, 16:13. Matendo 2:4, na kadhalika.


14.      Hamudi anasema: Wakristo wanadai kwamba Yesu alikuwa Mungu kama walivyomnukuu katika Yohana 1:1 “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu.” Hayo ni maneno ya Yohana na si maneno ya Yesu, vilevile, neno la kwanza la Kigiriki kwa ajili ya Mungu ni “HOTHEOS” ambalo linamaanisha “Mungu” likiwa na M kubwa, wakati neno la pili la Kigiriki kwa ajili ya Mungu ni “TONTHEOS” ambalo linamaanisha “mungu” likiwa na “m” ndogo. Je, huko si kukosa uaminifu kwa wale waliotafsiri Biblia ya Kigiriki? Je, nukuu hiyo ya Yohana 1:1 iliyotambuliwa na kila mwanazuoni wa Kikristo aliyeisoma Biblia kwamba imeandikwa na Myahudi aitwae Philo Alexandria kabla ya Yesu na Yohana?


Kuhusu swali lako la 14, soma HAPA.


15.      Hamudi anasema: Je, neno “god” au “TONTHEOS” pia halikutumika kuashiria wengine kama ilivyo katika Wakorinto 2 4:4 (Na Shetani ndiye) mungu wa ulimwengu huu na katika Kutoka 7:1 “Angalia, nimekufanya wewe kuwa kama Mungu kwa Farao”?


Jibu ni lilelile kwenye namba 13.


Katika makala yatakayofuata, nitaendelea na kujibu fungu la pili la maswali kuhusiana na wokovu.2 comments:

 1. Mungu Aliye Hai Kwa Jina Lako Lililo Kuu Kuliko majina yote Yesu Usifiwe. Nimefuatilia majibu kwa Ndugu Hamidu toka sehemu hii ya kwanza hata ya pili, naomba niseme haya yafuatayo.
  Mtu anapokuwa na maswali kama haya ya Hamidu na akakaa kimya ni hasara kubwa katika Ufalme Wa Bwana Yesu. Na inapotokea ameamua kuyatapika yote ambayo yamekuwa yamemtatiza ni nafasi nzuri/na faida kubwa kwa Ufalme wa Bwana Yesu. SASA BASI naomba tukumbushane maana kwafaa sana kuwa Kuwa Neno la Mungu limehakikishwa kwa moto, tena Kweli,Uzima na Njia na hakuna anayeweza akayafananisha maandiko haya na maandiko mengine yoyote, haijalishi yameandikwa kwa hekima ipi.
  Hivyo majibu yote yanapatikana ndani ya Biblia Takatifu na si kwingineko, kwanini nasema hivyo ni kwa sababu naliona Jibu lililo kamili lisilo na mashaka unalolitoa lakini mara kadhaa nimeona reference toka kwenye kitabu kingine. Hii haiwezi kukubalika hata kidogo. Mungu ahitaji msaada wa hekima nyingine ili ajieleze. Tumepewa uelewa na Roho Mtakatifu tuutumie pasipo kutafuta reference ambazo zitamfanya mtu aendelee kuamini kuwa alipo angalau pana neno moja linafanafana na la huko na hivyo kuendelea kubaki katika hali ileile na kushindwa kupona.
  Naomba majibu yetu yawe pure toka ndani ya Maandiko Matakatifu na ndipo Roho wa Mungu Hatahuzunika kwa kuwa atabaki akicheza kwenye uwanja Wake ule ule na wengi watafunguka. Neno lilivyoletwa ni upanga linatakiwa liwe upanga Kwelu hata kama mtu ataumia lakini nafsi yake itafunguka na Bwana wa Mavuno atavuna.
  Ameni Ubarikiwe na Bwana Yesu.

  ReplyDelete
 2. Shalom brother Revocatus. Asante kwa kuwa mfuatiliaji mzuri; asante pia kwa maoni na ushauri wako ambao naupokea kwa mikono miwili kabisa.

  Hata hivyo, kwa maoni yangu, ninafikiri kuwa upo upande wa pili. Ndugu yetu Paulo anasema: Maana, ingawa nimekuwa huru kwa watu wote, nalijifanya mtumwa wa wote, ili nipate watu wengi zaidi. Nalikuwa kama Myahudi kwa Wayahudi, ili niwapate Wayahudi; kwa wale walio chini ya sheria, nalikuwa kama chini ya sheria, (ingawa mimi mwenyewe si chini ya sheria), ili niwapate walio chini ya sheria. Kwa wale wasio na sheria nalikuwa kama sina sheria, (si kwamba sina sheria mbele za Mungu, bali mwenye sheria mbele za Kristo), ili niwapate hao wasio na sheria. Kwa wanyonge nalikuwa mnyonge, ili niwapate wanyonge. Nimekuwa hali zote kwa watu wote, ili kwa njia zote nipate kuwaokoa watu. Nami nafanya mambo yote kwa ajili ya Injili ili kuishiriki pamoja na wengine. (1Co 9:19-23).

  Msimamo wa kweli wa uzima wa milele ni kupitia Neno la Kristo lililo katika Biblia. Lakini pamoja na kwamba neno ni UWEZA, bado Mungu wetu hamlazimishi yeyote kuamini. Sasa nitafanyaje kumsaidia asiyeamini aamini? Njia mojawapo, japo si pekee, ni kuongea lugha yake; kama ambayo nay eye anaweza kuongea lugha yangu ili niamini upande wake.

  Ndiyo maana pia, Paulo akawaambia Waathene: “Enyi watu wa Athene, katika mambo yote naona ya kuwa ninyi ni watu wa kutafakari sana mambo ya dini.” (Mdo 17:22).

  Lakini ni nini hasa walichokuwa wakitafakari? Mstari wa 23 unatupa jibu. “Kwa sababu nilipokuwa nikipita huko na huko na kuyaona mambo ya ibada yenu, naliona madhabahu iliyoandikwa maneno haya, KWA MUNGU ASIYEJULIKANA. Basi mimi nawahubirini habari zake yeye ambaye ninyi mnamwabudu bila kumjua.”

  Mungu akubariki Revocatus.

  ReplyDelete