Zak Gariba ni mtoto wa pili kuzaliwa katika familia yao. Kwa sababu ya
kulitaja jina la Yesu msikitini, Zak Gariba, ambaye alikuwa ni imam alitupwa si
tu nje ya msikiti, bali pia nje ya familia yake. Alikataliwa na kujikuta hana
tena ndugu; na akapoteza kila kitu. Matokeo yake alifika mahali ambapo aliamua
kujiua. Lakini Yesu Kristo mwenyewe alienda kugonga mlango wa nyumba yake na akayabadili
kabisa maisha yake kutoka mautini na kumwingiza uzimani.
Kwa maneno yake mwenyewe, Zak anasema:
“Nilizaliwa katika familia ya Kiislamu na kulelewa katika Uislamu na wazazi
wangu walinichagua niweze kupata mafunzo ili nije kuwa imam. Nilienda kwenye
shule na nikajifunza pia lugha na utamaduni wa Kiarabu.
Nilisomea masomo ya kuwa imam. Baadaye nilienda Nigeria na nikawa imam wa
msikiti mmoja. Nilipenda kile nilichokuwa nakifanya.
Kuna wakati nilikutana na Wakristo fulani marafiki zangu ambao walikuja na
Biblia zao na tukaanza kubishana, huku nikiwaambia kuwa Quran ina nguvu kuliko
Biblia. Tuliendelea kubishana na ikafika mahali nikawapiga. Nikafikia pia
wakati ambao nikawa nimewachoka; nikawa nataka waende zao, maana wao walikuwa
ni watu wakimya. Nikawa natafuta namna
ya kuwaondoa.
Baadaye waliniomba kama naweza kuwabeba kwa gari hadi mahali fulani ambako
kulikuwa na mkutano wa injili. Nikasema, kama hilo ndilo mnalotaka,
nitawapeleka – maana niliona hiyo ni njia itakayonisaidia kuachana nao.
Mama mwenye nyumba yangu alikuwa na msichana mdogo ambaye, tangu kuzaliwa, alikuwa amepooza kuanzia kiunoni kuja chini. Waliniomba
nimbebe ili kumpeleka kwenye mkutano. Nilimbeba hadi kwenye huo mkutano uliokuwa
unafanyika kwenye uwanja mkubwa.
Niliegesha gari nyuma ya uwanja na kulikuwa na spika kubwa imeelekea
kulekule; na kuna mtu akawa anasema Yesu, Yesu!
Baada ya kuegesha gari, watu wengine wenye magari nao walikuja. Nikajikuta nimezingirwa
na magari mengine kiasi kwamba haikuwezekana kutoka tena.
Msichana yule akataka kutoka kwenye gari. Ikabidi nimbeba mikononi ili
nimpeleke kwenye benchi mojawapo. Na yule mtu wa kwenye spika naye aliendelea tu
kusema Yesu, Yesu. Na mimi nikawa ninatamani kufunga masikio yangu ili
nisisikie lakini siwezi, maana nimembeba huyu msichana.
Lakini wakati kuo kitu cha ajabu kilitokea. Mguu wa huyu msichana ulisogea
kwa namna isiyo ya kawaida. Nikawaza, ‘Ha! Nini hiki tena? Bila shaka hii ni
voodoo! Huu utakuwa ni uchawi tu!’
Na kadiri yule msemaji alivyoendelea kusema Yesu, Yesu, miguu ya msichana
huyu iliendelea kusogea zaidi na zaidi. Nikawa kama nimechanganyikiwa. Kisha huyu
msichana akasema, ‘Nataka kutembea.’
Nikamwambia, ‘Hutaweza.’
Matokeo yake, aliniuma. Ninalo kovu hapa(kwenye mkono). Ikabidi nimwachie hadi
chini. Na mbele ya macho yangu, nilimwona msichana huyu akitembea!
Nami nikawa najiuliza, ‘Inawezekanaje mtu mmoja ataje jina la Yesu na mtu
mwingine apone kabisa? Nikaanza kuwaza kuwa, ni lazima kuna kitu hapa kwenye
kitendo tu cha kutaja jina hili la Yesu.
Baadaye nilirudi nyumbani na jioni ile, kama kawaida, nilienda msikitini. Nilipokuwa
msikitini nikiongoza swala, sijui ni kwa vipi, lakini kwa namna nisiyoelewa,
ghafla maneno yalinitoka mdomoni ambayo hata sijui yalitoka wapi. Badala ya
kusema, Muhammad-sallal-laahu-alaihi-wasallam,
nilijikuta tu nasema kwenye spika za msikitini pale, ‘Yesu Kristo wa Nazareti!’
Katikati ya msikiti! Katikati ya waumini wengi! Nilichanganyikiwa. Matokeo yake
waumini wakanitoa nje. Walitaka hata kuniua!
Na huo ukawa ni mwanzo wa matatizo yangu.
Baada ya hapo, kaka yangu mkubwa alinisaidia kuja Kanada kusoma. Nilipokuja
huku, niliazimia kuwa nitaishi maisha ya kipagani kabisa. Sikutaka kuwa Mkristo
wala kuwa Mwislamu!
Lakini nakumbuka tarehe 3 Januari 1997 nilikuwa chumbani kwangu na nilikuwa
nimepanga kujiua. Nilikuwa nimefika mwisho wa maisha yangu kabisa. Wazazi wangu
walishanikataa; na hata walishafanya msiba kwa ajili yangu. Kila kitu kilikuwa
hovyo kwangu. Nilikuwa nimeshaandaa vidonge na kila kitu.
Ilipofika saa 3:00 asubuhi nilisikia mlango ukigongwa. Nilipandwa na hasira
sana. Nikaenda kuangalia, lakini hakukuwa na mtu. Nikawaza, hii ni ajabu! Yaani
Kanada? Mbona hapa watu wana simu wanaweza kukupigia kabla ya kuja kwako!
Nikarudi ndani. Lakini nikasikia mtu anagonga tena. Nilipofungua, sikuona
mtu tena. Nikafunga mlango na kuwaza, ‘Labda atagonga tena mara ya tatu.’ Kwa hiyo,
nikanyagakanyaga sakafu kama vile natembea – ili kwamba huyo mtu afikiri kuwa
nimeenda ndani. Lakini nikawa nimesimama palepale karibu na mlango.
Mara kweli nikasikia amegonga tena. Nilipofungua, hakukuwa na mtu; lakini nikasikia
sauti ambayo sijawahi kuisikia maishani mwangu. Ilisema, “Mama na baba yako
wamekuacha, lakini mimi nitakuwa pamoja
nawe.”
Nikatazama huku na huku na kuwaza, ‘Yaani sasa nimeanza hata kusikia sauti!’
‘Wewe ni nani? Wewe ni nani?’ niliuliza.
Sauti ile ikasema, ‘Mimi ni Yesu. Sasa nakuita kufanya jambo jingine.’
Nikasema, ‘Hebu ngoja kidogo. Nilitaja jina la Yesu wa Nazareti msikitini
matokeo yake nikaingia kwenye matatizo makubwa kiasi hiki ...! Sitaki kujihusisha
na chochote kinachohusiana na wewe!’
Akasema, “Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo. Niko tayari
kukusaidia.’
Na huo ndio ukawa mwanzo wa maisha yangu.
****************
Zak Gariba, kwa neema ya Mungu, pamoja na kukataliwa na ndugu na kila mtu, alimpata
Mungu wa kweli. Hivi sasa yeye ni mchungaji. Unaweza kusoma zaidi habari za kanisa
lake kwenye www.orilliajubileecc.org.
Yesu yuko tayari kukuokoa na wewe sasa. Usichelewe kumwita na kumkaribisha
moyoni mwako. Kanuni ya msingi ya wokovu ni kwa mtu kuamua moyoni mwake na
kuchukua hatua ya kusema, ‘Bwana Yesu karibu moyoni mwangu ili unipe uzima wako
wa milele.’ Kuna watu wachache tu ambao Bwana Yesu, kwa kuamua mwenyewe, huwaendea uso kwa uso na kuwatoa kwenye upotevu na kuwaingiza uzimani. Kwa hiyo, usije ukasema, nitangoja hadi Yesu atakapokuja kugonga mlango wa nyumba yangu kama alivyofanya kwa Zak Gariba ndipo nitaokoka. Anaweza asije kabisa hadi mwisho kwa namna hiyo; maana hiyo si kanuni ya msingi ya wokovu. Lakini usiku na mchana anagonga kwenye moyo wako kwa njia ya Roho Mtakatifu ambaye husema na dhamiri zetu muda wote.
Uzima wa milele haupatikani kwenye dini yoyote – iwe ya Kikristo au isiyo
ya Kikristo. Uzima wa milele unapatikana kwa Yesu Kristo pekee. Yesu hakuja
kuokoa Wakristo – maana wakati alipokuja duniani hadi anaondoka, wala hakukuwa
na Ukristo. Yesu alikuja kwa ajili ya dhambi za wanadamu wote. Yeye ni Mwokozi
wa ulimwengu wote – si Mwokozi wa Wakristo.
Tatizo la dhambi ni tatizo la wanadamu wote. Na hilo ndilo tatizo pekee
linalomfanya mwanadamu yeyote aikose mbingu na kuingia jehanamu ya milele. Lakini
tumepewa njia rahisi na ya uhakika ya kupona na kuokoka; nayo ni kumwamini Yesu
ambaye alikufa ili awe sadaka kwa ajili ya dhambi zetu. Hii ni kwa sababu sisi hatuna
kabisa uwezo wa kuishi maisha matakatifu kwa nguvu zetu wenyewe kiasi cha
kufikia utakatifu wa Mungu mwenyewe. Maana bila utakatifu, HAKUNA yeyote
atakayeingia mbinguni. Na ni mwanadamu gani basi anayeweza kusema kuwa yeye ana
maisha matakatifu? Bila shaka hakuna hata mmoja.
Ndiyo maana Yesu aliye Mungu, alikuja kuishi maisha ya kibinadamu, lakini
kwa ukamilifu wa kiungu ili kwamba, kwa kule tu kumwamini, sisi si tu tunahesabiwa
haki ya kuwa wana wa Mungu, lakini pia tunapewa neema ya kuishi maisha
matakatifu.
Amua leo!
Karibu pia usome zaidi Kwa Nini Yesu Alikufa.
Ubarikiwe na Bwana Yesu.
I wanted to thank you yet again for this amazing web-site you have designed here. It's full of ideas for those who are definitely interested in this subject, especially this very post. You're really all absolutely sweet and thoughtful of others plus reading your blog posts is a superb delight if you ask me. And what a generous gift! Ben and I are going to have fun making use of your points in what we should instead do next week. Our list is a mile long and tips might be put to good use.
ReplyDeleteHello there. I'd like to thank you again for visiting this little site. May the good Lord be with you always. He is good to us. He loves us and He is there for us all the time. Send my greeting in Jesus name to your family. Be blessed.
ReplyDelete