Tuesday, October 23, 2012

Majibu ya Ndugu Hamudi - Sehemu ya II



Katika sehemu hii ya pili, ninaendelea na kujibu maswali aliyouliza ndugu Hamudi kutokana na makala yangu niliyotoa katika blog hii yenye kichwa: Ndugu Waislamu Nisaidieni.

Kwa kuwa Bwana Hamudi aliuliza maswali mengi, nimeona ni vema niwe nayajibu kwa mafungu kulingana na yeye alivyoyaweka katika mafungu. Leo tutaangalia fungu la pili la maswali hayo.



Maswali kuhusu wokovu


1.    Hamudi anauliza: Wakristo wanasema kwamba “MUNGU AEMTOA” mwanawe wa pekee ili kutuokoa sisi.” Je, Mungu alimtoa Yesu kumpa nani wakati yeye Mungu ndiye mmiliki wa ulimwengu wote?


Kama nilivyoanza kusema tangu kwenye majibu yangu ya mwanzo, kujibu swali mojamoja hakutoi fursa nzuri sana ya kuona picha kamili. Lakini kwa kifupi ni kuwa, Waislamu huwa mnasema kuwa sisi Wakristo tumepotosha maandiko ya asili ya Biblia na kuingiza mambo mengine.


Na kwa kuwa mnaamini torati, naamini kuwa unafahamu kwamba suala la sadaka ya kuchinja lilianza zamani kabla ya Ukristo na Uislamu. Makuhani wa Israeli walikuwa wanachinja wanyama na kutoa damu hiyo kama sadaka, hususani kwa ajili ya kusamehewa dhambi. Je, walikuwa wanazitoa kwa nani?


Ninapenda nikuarifu kuwa, agano la kale ni kivuli au mfano wa kile ambacho kilikuwa kinangojewa; kile kilicho kikamilifu; yaani sadaka ya kweli iondoayo dhambi kwelikweli. Sadaka hiyo ni Yesu. Ndiyo maana anaitwa Mwana-Kondoo wa Mungu.


Naamini pia unafahamu kuwa Israeli walikuwa utumwani Misri, maana hata Quran inakiri hilo. Kabla ya kutolewa utumwani mwa farao, waliambiwa KWANZA kila familia ichinje mnyama na kupaka damu yake kwenye milango ya nyumba zao. Baada ya hapo, ndipo malaika alipita usiku na kuwaua wazaliwa  wa kwanza wote wa Misri, yaani wa nyumba ambazo milango yake haikuwa na damu. Na Israeli WOTE walipona.


Israeli hawakupona kwa sababu wao ni Waisraeli. Walipona kwa sababu walichinja mwanakondoo wa pasaka. Kama katika nyumba yoyote ya Mwisraeli wasingefanya hivyo, wao nao mauti ile ingewatembelea.


Farao ni mfano wa shetani. Utumwa wa Israeli ni mfano wa utumwa wetu wa dhambi. Mwanakondoo wa pasaka aliyechinjwa ni mfano wa Yesu aliyetoa uhai wake ili sisi tusiuawe/tusife kiroho. Na kuokolewa kwa Israeli kupitia damu ile ni mfano wa kila mwanadamu aliyeamini sadaka ya Yesu, hivyo kupona kufa, yaani kutupwa jehanamu ya milele.


Sasa, kwa kuwa yule mwanakondoo wa pasaka na hata wanyama wengine waliochinjwa kama sadaka walitolewa kwa Mungu, jibu la swali lako kwamba “Je, Mungu alimtoa Yesu kumpa nani wakati yeye Mungu ndiye mmiliki wa ulimwengu wote?” ni kuwa,  Mungu alimtoa Yesu ili kujipa yeye mwenyewe sadaka itakayokuwa ni malipo ya dhambi za ulimwengu wote ili sisi wanadamu badala ya kuhangaika kutaka kutimiza sheria ya Mungu, jambo ambalo hatujawahi kuliweza na hatutakaa tuliweze KAMWE, tuweze kuokoka kwa njia rahisi tu, yaani kuamini kuwa Yesu alikufa kwa niaba yangu mimi mtenda dhambi, akalipa adhabu ya dhambi zangu, ili mimi niweze kuhesabiwa haki bure ya kuingia mbinguni na kuishi milele na Mungu kwa imani TU!


2.    Hamudi anauliza: Ikiwa ilikubalika kwa utukufu wa Mungu kuwa awe na watoto, basi angeumba mamilioni ya watoto kama Yesu. Sasa kuna jambo gani kubwa kumhusu huyu mtoto wa pekee?


Hamudi, swali lako halitatui suala lililopo. Nina uhakika kabisa kama Mungu angeumba hao unaowaita mamilioni, bado ungeuliza, “Kwa nini hakuanza na mmoja?”


Lakini hata hivyo, jibu lake ni hili. Mungu hahitaji ‘robots’ zinazomtii bila kufikiri au kupenda. Hata wewe, ingawaje mwanao anaweza kuwa ameshakaidi amri zako mara nyingi, naamini unampenda mwanao zaidi kuliko kiti chako cha kukalia japo kiti hakijawahi kugombana na wewe; hakijawahi kukugomea; hakijawahi kukukimbia. Siku zote “kinakutii” katika yale unayotaka kikutendee - kama unaweza kuita kuwa huo ni utii. Kwa nini inakuwa hivi? Ni kwa sababu kiti hakina utashi wala ufahamu. Kwa hiyo, kufanya kwake yale uyatakayo si utii bali hali ambayo ni ‘automatiki’ tu. Haiwezi kugusa hisia zako kiasi kwamba ukawa na upendo kwa kiti kile kama ulio nao kwa mwanao.


Kwa hiyo, hoja yako kwamba Mungu angetengeneza mamilioni ya watoto kama Yesu, wasio na dhambi, walio watii kwa 100%, ni sawa na kusema kuwa Mungu alitakiwa aumbe ‘robots’ ambazo haziwezi kufanya vingine zaidi ya vile ambavyo ziko ‘programmed’. Huo si utii wala upendo. Utii na upendo kamili ni ule ambao anayeuonyesha, anakuwa ana uchaguzi wa kutenda vinginevyo, lakini anaamua kuacha hayo mengine na kutii au kupenda.


Dhambi na makwazo yanayotuzunguka ndicho kipimo halisi cha utii. Miili yetu inatuvuta kwa tamaa, hasira, wivu, chuki, n.k., si kwa bahati mbaya,  bali ili tuwe na fursa ya kuamua wenyewe ama kumtii Mungu aliye hai au kuzitii tamaa hizo. Kama zisingekuwapo, hakuna utii hapo. Kitakachobaki ni ‘robots’ tu! Lakini pale tunapoamua kumtii Mungu na kuzikataa tamaa, huo hasa ndio utii na upendo kwa Mungu.


Labda unasema, “James, una maana kuwa Yesu alikuwa ni robot?” Jibu ni hapana. Yesu alikuwa ni Mungu mwenyewe. Aliamua kuja kuishi maisha kama yetu hapa duniani, akashindana na dhambi na kuzishinda (yaani hakutenda dhambi hata moja), badala yake akabeba za kwetu mabegani mwake, kisha akauawa ili iwe ni malipo kwa ajili ya dhambi zetu.


Kwa hiyo, kwa kule kuja kama Mwana pekee, alianzisha ‘line’ ya uzao ambao kila anayetaka kuwa mwana wa Mungu, akubali kufuata njia ya Yesu na kuamini kazi aliyofanya.


Napenda nichukue fursa hii kukuhakikishia kabisa (na hili ni jambo ambalo mantiki yake iko wazi tu) kwamba, uhalali PEKEE wa Uislamu unategemea jambo hili. Kama Yesu hakufa, basi Uislamu unayo nafasi ya kudai kuwa ni dini inayoweza kumpeleka mtu mbinguni. Lakini kama Yesu alikufa (na hivyo ndivyo ilivyo) Uislamu hauna KAMWE uwezo wa kumpeleka mwanadamu awaye yote kwenye mbingu za Mungu aliye hai. Si Uislamu tu, bali na dini yoyote ile inayokataa dhabihu ya Yesu Kristo.


Kama kweli ninyi mnaamini torati kama mnavyosema, mbona hamchinji wanyama kwa ajili ya kusamehewa dhambi?


Kwa hiyo, nimalizie kujibu swali lako hili kwa kusema kwamba, jambo kubwa la pekee kumhusu Yesu ni kuwa wanyama waliochinjwa na Waisraeli kama dhabihu kwa Mungu walikuwa ni mfano au utangulizi wa lile lililokuwa likisubiriwa; Yesu ndiye utimilifu wa mfano ule. Yeye ndiye dhabihu Kamili, ya kweli, takatifu! Damu yake ndiyo PEKEE itakasayo dhambi.


3.    Hamudi anauliza: Kwa nini Biblia inasema kwamba Yesu alitaka kufa msalabani, huku yule mtu aliyesulubiwa pale msalabani alikuwa anapiga kelele “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?” kwa mujibu wa Matayo 27:45 na Marko 15:33?


Nadhani swali hili nimeshalijibu.  Hapa tunaongelea Mungu; si mwanadamu. Ukitaka kumpa Mungu sifa za kibinadamu, ni LAZIMA utakwama tu. Swali lako linamaanisha kuwa Mungu asingeweza kuwa msalabani na pia akawa mbinguni. Mungu yuko kila mahali kwa wakati uleule. Na anafanya mambo tofautitofauti kwa wakati huohuo. Kuna ajabu gani basi Yeye kuwa msalabani na papo hapo akawa mbinguni?


Vilevile, Yesu si tu alikuja kumwokoa mwanadamu, lakini pia alikuja kutupa kielelezo cha maisha tunayotakiwa kuyaishi. Kama Yeye alivyokuwa mnyenyekevu na mtii kwa Mungu Baba ndivyo na sisi tunatakiwa kuwa wanyenyekevu na watii. Na tunapofanya hivyo, mwisho wa siku tunakuwa tunamtii na kumnyenyekea Yesu huyohuyo.


4.    Hamudi anauliza: Ikiwa Mungu alitaka kutuokoa, je, angeshindwa kutuokoa bila kumtoa muhanga Yesu?


Jibu ni HAPANA. ASINGESHINDWA HATA KIDOGO! Lakini swali lako ni sawa na kusema “Kama Mungu angetaka tuwe na macho mgongoni na masikio kifuani angeshindwa?” Jibu ni wazi. Asingeshindwa! Lakini sasa hatuko hivyo sasa. Inanisaidia nini kuanza kusema, “Kama ningekuwa rais, ningekuwa na furaha sana,” wakati mimi si rais. Badala ya kujihangaisha na mawazo ambayo ni ‘impractical’ kwa nini nisijipange ndani ya hali HALISI iliyopo? Yaani ndani ya ukweli kwamba mimi si rais, kisha nitafute kile ninachotakiwa kufanya ili nipate hiyo furaha ninayoitaka katika hali hiihii ya kutokuwa kwangu rais?


Kwa hiyo, ni kweli kabisa kwamba, kama Mungu angetaka kutuokoa kwa njia nyingine, angeweza. Lakini HAKUTAKA SASA? NJIA ALIYOITAKA NDIYO HII. Na kama nilivyokujibu swali lako la 2 hapo juu, nina uhakika kabisa kuwa hata kama Mungu angetumia hiyo unayoita “njia nyingine” bado ungeuliza swali hilihili – kwamba “Kwani Mungu hakuwa na njia nyingine?” Na njia hii ilianza kuandaliwa tangu kuwekwa kwa misingi ya ulimwengu. Na hata siku Adam na Hawa walipofukuzwa Edeni, Mungu alimwambia ibilisi: “… nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino.” (Mwanzo 3:15). Uzao siku zote huhesabiwa kwa manamume, lakini hapa shetani anaambiwa kutakuwa na uadui kati ya uzao wake (mashetani/majini wote) na uzao WA MWANAMKE (si wa mwanamume). Ni nani aliye uzao wa mwanamke? NI YESU!



Je, Hamudi, Quran haisemi katika sura 5:32 kwamba ukiua nafsi unahesabiwa kuwa umeua wanadamu wote na ukiokoa nafsi unahesabiwa umeokoa wanadamu wote? Hicho ndicho alichokuja kufanya Yesu.



Sasa mpendwa wangu Hamudi, kwa kuwa tayari Mungu ameshachagua njia hii, huna udhuru wala utetezi. Kukubali au kukataa kwetu hakutabadilisha mpango wa Mungu. Kutamani kwetu kwamba kungekuwapo na njia mbadala ni kupoteza muda, nafasi, na uzima! Ama tunakubali njia iliyowekwa na kupona au tunaikataa na kuangamia! Basi!


5.    Hamudi anauliza: Mungu yeye mwenyewe ni haki, na haki inataka kusiwepo na mtu anayepaswa kuadhibiwa kwa madhambi ya wengine, vilevile haipaswi kuadhibiwa watu wengine kwa kuwaokoa wengine: Je! Dai la kwamba Mungu amemtoa muhanga Yesu ili kutuokoa halileti mkanganyiko kama kweli Mungu ni mpenda haki? Je, dai hilo halitofautiani na maana halisi ya haki?


Sielewi ni kwa kadiri ya nani au kadiri ya nini kwamba  “haki inataka kusiwepo na mtu anayepaswa kuadhibiwa kwa madhambi ya wengine, au vilevile haipaswi kuadhibiwa watu wengine kwa kuwaokoa wengine.”


Je, mwanao akivunja kioo cha gari cha mtu mwingine utamwacha akafungwe jela kwa sababu si wewe uliyevunja kioo hicho? Naamini utakubali kulipa gharama za kioo kwa ajili ya mwanao umpendaye. Lakini pia ukishalipa, je, hiyo itamaanisha kuwa wewe ndiye mkosaji sasa? Bila shaka jibu ni hapana. Mkosaji anabakia kuwa ni mwanao huyohuyo. Lakini wewe unakuwa umefanyika mwokozi wake, japokuwa umebeba kosa lake mabegani mwake.


Sisi kama wanadamu ni wenye dhambi. Tumemwasi Mungu, tumevunja sheria zake kila siku. Kwa hiyo, bila shaka yoyote, kutokana na kwamba Mungu ni mwenye haki, kama unavyosema, na mimi nakubaliana na wewe katika hilo, kila dhambi, hata kama ni ndogo kiasi gani, ni lazima iadhibiwe. LAZIMA! Sheria ya Mungu inasema wazi: Mshahara wa dhambi ni mauti (Warumi 6:23). Haisemi mshahara wa dhambi kubwa au nyingi. Ni mshahara wa dhambi yoyote, kwa kiasi chochote. Mshahara huo au mauti hiyo ni nini? – NI JEHANAMU YA MILELE!


Kwa hiyo, dai la kumtoa Yesu halina mkanganyiko KAMWE bali limejaa UPENDO wa ajabu. Kwa sababu haki inadai adhabu kwa kila mtenda dhambi; ambayo ni sawa na kusema, kwa kila mwanadamu; lakini UPENDO WA MUNGU ukasema, “Hapana. Nitakwenda mwenyewe kama Yesu. Kisha nitakufa kwa ajili yao ili kwamba, kwa vile wamevunja kioo cha gari ya jirani, mimi ndio niwe wa kubeba adhabu hiyo ili wanangu niwapendao wapone.” Si kwamba kosa limefumbiwa macho, la hasha, bali limelipwa KIKAMILIFU kama sheria inavyotaka!!


Hiyo ndiyo haki Hamudi. Tumetenda dhambi lakini Mungu hasemi kirahisi, “Waache tu.” Waache kivipi wakati haki ya kisheria inadai hukumu? Ni lazima hukumu itolewe kwa kila kosa lililotendwa. Hiyo ndiyo haki!


Sasa hebu niambie wewe uliye Mwislamu. Unafahamu kuwa Quran inakuambia kwamba Israeli waliadhibiwa na Mungu kwa sababu ya uasi na dhambi zao. Je, wewe hutendi dhambi? Kama unatenda dhambi, ni kwa nini yuleyule aliyewaadhibu Israeli asikuadhibu na wewe wakati wewe nawe hauna tofauti na wale?


Je, akikusamehe wewe kwa makosa yaleyale atakuwa ni Mungu mwenye haki au ni mwonevu na mwenye upendeleo?


6.    Hamudi anauliza: Watu wanatoa muhanga vitu vyao ili kupata vitu vingine wasivyokuwa navyo ikiwa haiwezekani kuwa navyo vyote viwili kwa wakati mmoja. Wakristo wanasema kwamba “Mungu alimtoa muhanga mtoto wake wa pekee ili kutuokoa; Tunajua kwamba Mungu ni Mwenye nguvu; Mungu alimtoa Muhanga Yesu kwa nani?


Jibu liko hapo juu kwenye swali namba 5 hapo juu.


7.    Hamudi anauliza: Kutoa muhanga kitu maana yake ni kwamba huwezi kukipata tena kile ulichokitoa; sasa kuna siri gani katika kutolewa Muhanga Yesu wakati Mungu aliweza kumrudisha Yesu baada ya kusulubiwa (kwa mujibu wa maneno ya Wakristo)?


Sielewi hili neno “kutoa muhanga” unalitoa wapi. Ninavyofahamu mimi, Biblia haiongelei juu ya Yesu kutolewa muhanga. Inaongelea juu ya kutolewa sadaka.


Hata hivyo, siri iliyopo Hamudi ni kuwa, hangaika uwezavyo, jitahidi uwezavyo, jibidishe uwezavyo – wewe na mimi kama wanadamu KAMWE hatutaweza kuishi kwa utakatifu unaotakiwa ili Mungu aweze kuturuhusu kuingia mbinguni. Hili si jambo la kinadharia tu. Jichunguze wewe mwenyewe kwa makini japo kwa siku moja; au hata nusu siku kama kweli unaweza kuishi kikamilifu. Kama Adam na Hawa walikataliwa kwa dhambi MOJA, je, wewe na mimi itakuwaje?


Kwa hiyo, kwa sababu mimi na wewe hatuwezi, ndiyo maana ilibidi Mungu mwenyewe (akiwa kama Yesu) aje kuishi maisha hayahaya ya kibinadamu lakini bila kutenda dhambi yoyote. Lakini kwa kuwa sheria inasema kuwa mshahara wa dhambi ni mauti, Yeye aliamua kwa upendo wake kuzibeba dhambi zetu, halafu akauawa, badala ya sisi wenye dhambi hizo kuuawa! Nadhani unakumbuka mfano wa mtoto aliyevunja kioo cha gari kwenye swali namba 5 hapo juu. Kama utalipa gharama za kioo kisha baada ya siku moja mwenye gari akaja kusema, “Nataka mwanao aende jela kwa sababu amevunja kioo cha gari yangu,” je, utamwambia nini? Bila shaka unaweza kumwambia, “Huna unachodai hapa. Nimeshakulipa fedha yako. Hiki unachokitaka si haki yako. Haki yako ilikuwa ni huyu mtoto alipie kosa lake, na mimi baba yake nimeamua kubeba kosa hilo nikamlipia deni lake. Kwa hiyo, hivi sasa yuko huru.”


Kwa kitendo alichofanya Yesu vilevile, haki inasema kwamba, “Mwanadamu ni mwenye dhambi. Anatakiwa kwenda jehanamu.” Lakini Bwana wangu Yesu atasema, “Ni kweli ametenda dhambi, lakini mimi nilishabeba adhabu yake. Na yeye kwa sababu ameniamini na kutubu  dhambi zake, hadaiwi chochote.” Hii Hamudi ndiyo raha na UHAKIKA wa wokovu wa Yesu. Mtu aliye nje ya Yesu hana hata uhakika kama atakwenda mbinguni. Anajaribu tu kufanya hiki na kile akidhani ndio atamfurahisha Mungu. Huko ni kupoteza muda ndugu yangu. Wewe mwenyewe ni shahidi wa maisha yako binafsi kwamba hujawahi kuweza; na hutaweza!


8.    Hamudi anauliza: Ikiwa Wakristo wote wameokoka kwa kupitia Yesu na wanakwenda peponi (kwenye uzima wa milele) bila kujali matendo yao, kwa hiyo mafundisho ya Yesu hayana umuhimu wowote na maana ya maneno “uovu” au “wema” hayana umuhimu wowote. Ikiwa hali sivyo hivyo, kwa hiyo wale Wakristo ambao wanamwamini Yesu lakini hawafuati mafundisho yake wala hawajatubu watakwenda motoni?


Kwanza si sahihi hata kidogo kusema kwamba Wakristo wote wameokoka na wanakwenda peponi. Maneno ya Bwana Yesu yako wazi kabisa. “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.” (Mathayo 7:21).


Kwanza ni lazima ieleweke kwamba Yesu hakuja kwa ajili ya Wakristo. Wakati akiwa hapa duniani hadi anaondoka, wala hakukuwa na Ukristo. Majina ya kidini yalikuja baadaye. Yesu alikuja kama Mwokozi wa wanadamu WOTE! Yeye ndiye alikuumba wewe na mimi na kila mtu. Upendo wake si kwa Wakristo bali ni kwa wanadamu.


Kwa hiyo, kinachompeleka mtu mbinguni si Ukristo bali ni kuamini na kupokea sadaka ya Yesu. Yaani kuamini kwamba Yesu alikufa kwa ajili yake na kuishi kadiri ya maagizo na amri za Bwana Yesu.


Mwanadamu YEYOTE ambaye hadi anakufa atakuwa amemkataa Yesu au hakumwamini au hakuishi sawasawa na amri zake – kituo chake cha milele ni JEHANAMU YA MOTO. Kuhusu kipengele cha matendo, soma jibu linalofuata hapa chini.


9.    Hamudi anauliza: Vipi Wakristo wanayachukulia matendo kama kitu kisicho na umuhimu baada ya kuwa kitu kimoja wakati Yesu aliposema katika Matayo 12:36; “Basi, nawaambia, Kila neno lisilo maana, watakalolinena wanadamu, watatoa hesabu ya neno hilo siku ya hukumu”?


Hamudi, matendo ni kitu cha muhimu sana. Hata Biblia inasema kuwa imani pasipo matendo imekufa. (Yakobo 2:17). Lakini kile ambacho Biblia inasema ni hiki. …. mwanadamu hahesabiwi haki kwa matendo ya sheria, bali kwa imani ya Kristo Yesu (Wagalatia 2:16).


Maana yake ni kuwa, hakuna mwanadamu hata mmoja atakayeingia mbinguni kwa sababu eti akiwa duniani alitenda matendo mema. Hata kama ukitoa sadaka kwa maskini kila siku, ukawalisha yatima wote kila siku, ukauza nyumba na kila kitu ili kuwahudumia maskini – lakini hujaamini kuwa Yesu alikufa kwa ajili yako - kama hicho ndicho unadhani kitakupa tiketi ya kuingia mbinguni, basi fahamu kuwa umepotea kabisa!! Mwisho wako ni jehanamu ya moto. Hili wala halina swali au kujiumauma. Na wala hii si hukumu; maana watu wengi watakimbilia kusema, “Wewe unatuhukumu kama nani?” Hii ni sheria ya mbinguni ndugu yangu.


Sababu yake ni hii. Utakatifu wa Mungu hauchangamani na dhambi hata iwe ndogo kiasi gani. Na kwa sababu wewe na mimi ni wanadamu, hata tukijitahidi kutenda mema kiasi gani, hatuna uwezo wa kuwa wema kwa 100%. Hili ni jambo lililo wazi tu.
    

Neno la Mungu linasema wazi: “Kwa maana sisi sote tumekuwa kama mtu aliye mchafu, na matendo yetu yote ya haki yamekuwa kama nguo iliyotiwa unajisi.” (Isaya 64:6).


Sasa, kama ukikosea katika jambo moja, yale mengine yote uliyoyafanya ni kazi bure. Kama unaweza kuwa na matendo mema na ukawa mkamilifu kwa asilimia mia moja, uwe na uhakika kabisa kwamba mlango wa mbinguni uko wazi kwa ajili yako. Lakini kama utafanya matendo mema kwa asilimia 99.9, kisha ukaja kukosea kwa 0.1%, mlango wa mbinguni umefungwa kwako! Na je, kuna mwanadamu anayeweza kufanya mema japo kwa asilimia 2 ya maisha yake yote hapa duniani? Jibu liko wazi.


Kwa hiyo, ndiyo maana tiketi ya kwenda mbinguni ni kwa kuamini sadaka ya dhambi ya Mwana-Kondoo wa kweli wa Mungu, yaani Yesu Kristo. Kisha baada ya kuamini, matendo mema tunafanya kwa kumtii Yesu; si kwa lengo la kupata tiketi ya kwenda mbinguni.


Kwa upande wa pili, kama utamwamini Yesu, kisha ukasema, “Si nimeshaokoka. Wacha niponde tu maisha.” Ukaanza kutenda matendo maovu kwa sababu eti tayari umeshaweka tiketi ya mbinguni mfukoni, hapo mwisho wako ni uleule – jehanamu!


Hebu niambie Hamudi; kama Mungu angekuwa kweli na haja na matendo kama ninyi mnavyosema, je, kati ya sisi wanadamu na viumbe wengine kama wanyama na miti, ni nani ambaye anatimiza matendo yake kama Mungu alivyoagiza? Je, si wazi kwamba wanyama na miti wanaishi sawasawa na Mungu alivyowaumba? Kama ni kuzaa, wanazaa kwa misimu yao sawasawa; kama ni kula, wanakula kwa kadiri ya maumbile yao – uliona wapi ng’ombe mlevi au anayetumia dawa za kulevya? Sasa, kama wao wanatenda sawasawa kabisa na amri ya Mungu iliyo juu yao, je, watakwenda mbinguni?


Ndugu, Mungu hana haja na matendo yako mema kwa sababu tu ni matendo; kuna zaidi ya hapo!!!


10. Hamudi anauliza: Wakristo wanasema kwamba watu wanakwenda peponi kwa kupitia Yesu tu! Wakati Paulo anasema katika 1 Wakorintho 7:8-16 kwamba Mume asiyeamini anakubalika kwa Mungu kwa sababu anaunganishwa na mke wake na kinyume chake, na watoto wao wasio na dini vilevile wanakubalika kwa Mungu. Kwa hivyo, kumbe watu wanaweza kwenda peponi bila ya kumwamini Yesu; kutokana na maneno hayo.


Kinachomaanishwa hapa ni kuwa, anakubalika kuwa mume wa huyo mke, na si kukubalika kuwa mtakatifu wa kwenda mbinguni. Yaani, Mungu anakubali kuwa huyo ni mume halali wa mke huyo.


Kwenda mbinguni ni uamuzi wa mtu mmojammoja kibinafsi. Huwezi kwenda mbinguni kwa imani ya mtu mwingine. Mtoto hawezi kwenda mbinguni kwa imani ya mzazi wake, wala mume kwa imani ya mkewe, n.k.


Kanuni ya kuingia mbinguni ni hii: “Ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana, kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu.” (Waebrania 10:9-10).


Ndiyo maana Ukristo haumlazimishi mtu kwa nguvu wala hauna haja ya kuwa na polisi wa kuhakikisha kuwa eti watu hawanywi pombe au hawafanyi uzinzi. Injili ya Yesu inahubiriwa, kisha ni uamuzi wa mtu mwenyewe kuiamini na kuitii au kuikataa.


Hakuna lifti au kulazimishana kwa habari ya kwenda mbinguni, rafiki yangu Hamudi. Lakini hata kama mtu akikataa, mwisho wa safari ndipo sasa anakutana na Bwana Mkubwa Yesu – hapo akiwa si tena Mwanakondoo bali Hakimu!



11. Hamudi anasema: Vipi Biblia inasema kwamba Waisraeli wote wameokoka ingawa hawamwamini Yesu? Je, Hili halipingani na dai la Biblia ya kuwa njia ya pekee ya kwenda Peponi ni kwa kupitia Yesu tu?



Hakuna sehemu katika Biblia inayosema kuwa Waisraeli wote wameokoka. Isipokuwa kuna mahali panaposema: “Kwa maana, ndugu zangu, sipendi msiijue siri hii, ili msijione kuwa wenye akili; ya kwamba kwa sehemu ugumu umewapata Israeli, mpaka utimilifu wa Mataifa uwasili. Hivyo Israeli wote wataokoka; kama ilivyoandikwa, Mwokozi atakuja kutoka Sayuni; Atamtenga Yakobo na maasia yake.” (Warumi 11:25-26).


Kwa hiyo, maandiko yanasema kuwa wata- siyo wame-. Na hili litatimia lini? Ni mpaka utimilifu wa mataifa utimie.


Maana yake ni hii. Kabila PEKEE duniani lililomjua Mungu wa kweli tangu mwanzo wa kuwako kwake ni Israeli. Wengine wote tulikuwa kwa asili ni waabudu mizimu na mashetani. Iwe ni Mwafrika, Mwarabu,  Mhindi, Mzungu, n.k.


Lakini kwa vile wao Israeli walikabidhiwa torati, ambayo ilikuwa ni mfano wa yale yaliyokuwa yakisubiriwa, pale utimilifu ulipofika kwa Yesu kuja, hawakuelewa. Matokeo yake walimkataa yuleyule waliyekuwa wamemngojea kwa maelfu ya miaka.


Sasa wakati ambapo wao wamemkataa, wale ambao mwanzoni walikuwa waabudu mashetani (yaani sisi watu wa Mataifa) tukampokea na kumkubali. Lakini kwa kuwa bado si watu wa Mataifa wote wamempokea (maana bado kuna watu kama wewe Hamudi hamumtaki), ndiyo maana Biblia inasema kwamba, kutokuamini kwa Israeli kutaendelea hadi utimilifu wa mataifa utimie. Yaani, mpaka akina Hamudi nao wamwamini Yesu.


Baada ya hapo, Israeli sasa nao watamwamini Yesu na kuokolewa. (bila shaka ni wale watakaokuwapo wakati huo). Maana hata sasa wao bado wanamngojea Masihi, lakini utafika wakati ambapo watagundua, “Ala kumbe Masihi ni huyu tuliyemkataa!”


Kwa hiyo, kulingana na swali lako, hakuna upinzani wowote kwa sababu bado kuokolewa kwao nako kutakuwa  ni lazima kufuate kanuni ileile – yaani kumwamini Yesu Kristo ambaye ndiye LANGO PEKEE la kuingia mbinguni.


12. Hamudi anauliza: Kwa mujibu wa Wakristo, wale wote ambao hawakubatizwa watakwenda motoni. Kwa hivyo, hata watoto wachanga nao watakwenda motoni kwa vile walikufa kabla ya kubatizwa; kwa vile walizaliwa na dhambi la asili la kurithi? Je, hili halipingani na maana ya neno haki; kwa nini Mungu awaadhibu watu kwa madhambi wasiyoyatenda?


Biblia hata haiagizi watoto wachanga wabatizwe, bali ni baadhi ya makanisa ambayo yamejiundia injili zao zisizotokana na Bwana Yesu. Badala yake Biblia inasema kwamba: “Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa.” (Marko 16:16).


Kubatizwa ni lazima kutanguliwe na kuamini. Mtoto mchanga hana uwezo wa kuamini. Kwa hiyo, hana haja ya kubatizwa hadi atakapopata akili na uwezo wa kuelewa, kuamini na kuamua.


Lakini kuhusu watoto, Bwana wetu Yesu anasema wazi: “Waacheni watoto wadogo waje kwangu; wala msiwazuie; kwa maana walio mfano wa hao, ufalme wa mbinguni ni wao.” (Mathayo 19:14). Watoto wadogo, wakiwa bado hawajafikia ule umri wa kufanya maamuzi yao binafsi, wana tiketi ya moja kwa moja ya kuingia mbinguni - wawe wamezaliwa kwenye familia za Wakristo, Waislamu, wapagani, waabudu shetani, nk. Mungu si dhalimu.


Hitimisho la sehemu hii

Ndugu yangu Hamudi, pamoja na Waislamu wote, hakuna wokovu nje ya Yesu. Yesu hakuja kuleta dini bali alikuja kuleta suluhisho la dhambi kwa mwanadamu ili kumpatanisha na Muumba wake.
Adamu hakuwa Mkristo, bali alikuwa mwanadamu. Hakufukuzwa kwenye Bustani ya Edeni kwa sababu ya kutokuwa Mkristo mzuri, la hasha! Alifukuzwa kwa sababu ya dhambi.


Kama Mungu angekuwa anahesabia watu haki kwa matendo mema, kwa nini basi hakumwambia Adamu na mke wake watende matendo mema ili awarejeshe tena Edeni?

Acha kusita, njoo kwa Yesu upate wokovu.

Tangu asili, Mungu amekuwa akianza na mtu mmoja kwa habari ya mambo yahusuyo wanadamu.

  • Alianza na Adamu ambaye kutoka kwa huyo tumekuwa mabilioni kwa mabilioni. 
  • Dhambi ilianza na Eva, kisha ikaingia kwa kila mwanadamu. 
  •  Uana (yaani kuitwa mwana), kulianza na Yesu, kisha kupitia Yeye, kilaa aaminiye anazaliwa katika familia ya kiroho ya Mungu na kuwa mwana wa Mungu. 
  •  Wokovu umeanza na Yesu, kisha ukaingia kwa kila mwanadamu anayeutaka.

Hakuna wokovu nje ya Yesu Kristo!

Quran inawaagiza Waislamu wote wamfuate Yesu Kristo. Imeandikwa kwamba: “I have come to you with wisdom and to make plain to you some of the things about which you differ. Fear Allah and follow me.” (Al-Zukhruf 43:64.)

2 comments:

  1. Thank you for your thoughtful present of having written this article. The message seems to be given to me specifically. Our son also had a lot to learn from this – though he was the individual that found your site first. Most of us can't imagine a more superb present than a gift to encourage that you do more.

    ReplyDelete
  2. Hi, be so blessed for visiting my site. Thank you so much too for your encouraging words. To know that someone has benefited from what you did is truly very empowering. May the Lord keep strengthening you and your family.

    ReplyDelete