Sunday, November 4, 2012

Majibu ya Ndugu Hamudi - Sehemu ya III


Leo ningependa kuendelea na kujibu maswali ya ndugu yetu Hamudi ambayo aliuliza kufuatia makala niliyoandika katika blog hii, yenye kichwa kisemacho Ndugu Waislamu Nisaidieni.


ROHO MTAKATIFU


Hamudi anauliza: Sehemu pekee katika Biblia alipotajwa Roho Mtakatifu ni katika Yohana 14:26; “Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote niliyowaambia. Ni kipi kile ambacho Roho Mtakatifu ameleta au kufundisha kwa miaka 2000 iliyopita?


Jibu langu:
Hamudi, Roho Mtakatifu ametajwa sehemu nyingi sana kuanzia mwanzo kabisa wa kitabu cha Mwanzo hadi Ufunuo. Yohana 14:26 si sehemu pekee alikotajwa kama unavyosema.


Zifuatazo ni baadhi tu ya sehemu anakotajwa Roho Mtakatifu:

 • Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi. Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji; Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji. (Mwanzo 1:1-2).
 • Yesu akarudi kwa nguvu za Roho, akenda Galilaya; habari zake zikaenea katika nchi zote za kandokando. (Luka 4:14).
 • Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu. Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa Roho ni roho. (Yohana 3:5-6).
 • Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli. (Yohana 4:24).
 • Hata siku ya mwisho, siku ile kubwa ya sikukuu, Yesu akasimama, akapaza sauti yake akisema, Mtu akiona kiu, na aje kwangu anywe.  Aniaminiye mimi, kama vile maandiko yalivyonena, mito ya maji yaliyo hai itatoka ndani yake. Na neno hilo alilisema katika habari ya Roho, ambaye wale wamwaminio watampokea baadaye; kwa maana Roho alikuwa hajaja, kwa sababu Yesu alikuwa hajatukuzwa. (Yohana 7:37-39).
 • Yesu anasema: Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu. (Yohana 14:16-17).
 • Kwa maana wale waufuatao mwili huyafikiri mambo ya mwili; bali wale waifuatao roho huyafikiri mambo ya roho. (Warumi 8:5).
 • Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu. (Warumi  8:14).
 • Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote. Tukipendana, Mungu hukaa ndani yetu, na pendo lake limekamilika ndani yetu. Katika hili tunafahamu ya kuwa tunakaa ndani yake, naye ndani yetu, kwa kuwa ametushirikisha Roho wake. (1 Yohana 4:12-13).

Umeuliza kuwa ni mambo gani ambayo Roho Mtakatifu amefanya katika miaka 2000 iliyopita. Ni mambo mengi sana sana. Yafuatayo ni baadhi tu:

 • Analeta mabilioni ya wanadamu kwa Yesu usiku na mchana.
 • Anabadili tabia za wanadamu ambazo hata haiwezekani kwa mtu mwenyewe kujibadili. Kwa mfano, inawezekanaje mtu aliyekuwa mlevi wa kutupa, mtumiaji wa dawa za kulevya, muuaji, mchawi, n.k., akabidilika na kuwa mtu mpole na mpenda watu kabisa na akaanza kuhubiri injili ya Yesu Kristo? – ni kazi ya Roho Mtakatifu.
 • Anatenda  miujiza kama vile kuponya wagonjwa, kufukuza majini ndani ya wanadamu, kufufua wafu, n.k.
 • Anapeleka watu wengi mbinguni na kuwarudisha kuja kutoa ushuhuda kwa sisi tulio duniani juu ya namna mbinguni na hata jehanamu kulivyo.
 • Kuwafundisha watu wake vita vya kiroho, yaani vya kutumia silaha za kiroho badala ya silaha za kimwili, kama vile mapanga na bunduki.
 • Kuwashuhudia wanadamu dhambi zao mioyoni mwao ili wakubali kumgeukia Mwokozi wao na kuokolewa.

NAPENDA NIKUULIZE SWALI


Quran inasema kwamba: We gave Isa, the son of Mariam, veritable signs and strengthened him with the Holy Spirit.


Yaani:
Tulimpatia Isa, mwana wa Mariam, ishara zisizo na shaka na kumtia nguvu kwa Roho Mtakatifu. (Al-Baqarah 2:87)


Je, maana yake ni nini kwako? Kama kuishi kwa Isa duniani alihitaji Roho Mtakatifu, iweje wewe Mwislamu useme kuwa utayaweza maisha haya ambayo yana changamoto nyingi bila msaada wa Roho Mtakatifu? Jihoji sawasawa.


Biblia inasema kwamba: Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu (Matendo 1:8).


Nguvu hii ni kwa ajili ya wanadamu; si kwa ajili ya Wakristo. Mungu aliumba wanadamu; hakuumba Wakristo. Ukristo na Uislamu, n.k. ni mambo ya kibinadamu; si ya kimungu. Mungu anataka akae ndani yako na kukuongoza katika maisha ya baraka alizozikusudia tangu kuumbwa kwa wazazi wetu wa kwanza, Adamu na Eva.


Hamudi anauliza: Wakristo wanasema kwamba Msaidizi maana yake ni Roho Mtakatifu (Yohana 14:26). Yesu alisema katika Yohana 16:7-8. “Lakini mimi nawaambia iliyo kweli; yawafaa ninyi mimi niondoke; kwa maana mimi nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu;” Hii haiwezi kumaanisha Roho Mtakatifu; kwa vile Roho Mtakatifu inasemekana kwamba alikuwapo hata kabla Yesu hajazaliwa kama ilivyo katika Luka 1:41 “Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifu.” Hapa, Roho Mtakatifu vilevile alikuwapo wakati wa Yesu. Sasa vipi hii imaanishe kwamba ni sharti aondoke Yesu ndipo Roho Mtakatifu aweze kuja?


Jibu langu:
Maneno haya ndugu yangu Hamudi yanamaanisha huyohuyo Roho Mtakatifu kabisa. Yesu Kristo unayemnukuu katika Yohana 16:7-8 ndiye anayesema hivyo. Katika Yohana 14:16-17, Bwana Yesu anasema hivi: “Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu.”


Unaona sasa. Huyu ni Roho wa kweli ambaye ulimwengu (yaani watu wasiomwamini Yesu) hawamwoni wala kumtambua. Leo, wale tuliopokea wokovu wa Yesu ni mashahidi kabisa. Tunajua jinsi tulivyokuwa kabla ya kuokoka na jinsi tulivyo sasa – ni watu au tabia mbili tofauti kabisa!


Kuhusu hoja kwamba Roho Mtakatifu alikuwapo tangu nyakati za Yesu (na hata kabla), hilo ni kweli wala halina ubishi. Kimsingi, Roho Mtakatifu Roho Mtakatifu yupo tangu kuumbwa kwa ulimwengu.


Lakini jambo linaloongelewa hapa ni “majukumu” – (duties). Katika ratiba ya Mungu ya nyakati na majira, kabla ya Yesu kuja, Roho Mtakatifu alikuwa anapelekwa kwa watu wachache, kwa malengo maalumu tu. Watu hao walikuwa ni kama vile makuhani, wafalme, manabii, na baadhi ya watu ambao walikabidhiwa majukumu maalumu – kwa mfano:

 • Mama yake Samsoni (Waamuzi sura ya 13)
 • Mama wa Yohana Mbatizaji (Luka sura ya 1)
 • Mariamu mama wa Yesu (Mathayo sura ya 1)

Lakini kwa watu wengine, hawakuwa na Roho Mtakatifu kwa namna iliyo rasmi kama hawa waliokuwa na wajibu maalumu.


Lakini baada ya Yesu Kristo kuja, kufa, na kufufuka, ndipo sasa Roho Mtakatifu ni kwa ajili ya MTU YEYOTE ANAYETAKA.


Ndiyo maana mitume walipoanza kuhubiri Injili hadharani kwa mara ya kwanza, ilikuwa ni baada ya Roho Mtakatifu kumwagwa hadi watu wakadhani kuw amitume wamelewa pombe. Mtume Petro alisimama akasema:


Sivyo mnavyodhani; watu hawa hawakulewa, kwa maana ni saa tatu ya mchana; lakini jambo hili ni lile lililonenwa kwa kinywa cha nabii Yoeli, Itakuwa siku za mwisho, asema Mungu, nitawamwagia watu wote Roho yangu, na wana wenu na binti zenu watatabiri; na vijana wenu wataona maono; na wazee wenu wataota ndoto. Naam, na siku zile nitawamwagia watumishi wangu wanaume na wanawake Roho yangu, nao watatabiri. (Matendo 2:15-18).


Lakini hii haina maana kuwa wale wasiomtaka hashughuliki nao, hapana! Unadhani ni kitu gani kinachokufanya usikie hatia moyoni pale unapofanya makosa? Ni Roho Mtakatifu anasema nawe ili ugeuke na kuacha njia mbaya.

Lakini pale unapompokea Yesu kama Bwana na Mwokozi wako, ndipo Roho Mtakatifu, kwa namna iliyo rasmi kabisa, anakuja kwako na kuanza kudhihirisha mambo kwa namna ya Rohoni ambayo, wewe mwenyewe utakuwa shahidi.


Hamudi anauliza: Katika Yohana 16:7-8, inasema; “Bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu. Naye akiisha kuja, huyo atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu.” Je, hii “Yeye” hapa inamaanisha nini? Je, viwakilishi hivyo havimaanishi mtu mwanamume?


Jibu ni lilelile kama hapo juu.


Hamudi anauliza: Je, Roho Mtakatifu anazungumza na Wakristo wema na waovu vilevile? Je, Roho Mtakatifu yu pamoja nao wakati wote au wakati fulani tu? Je, ni wakati gani anaanza kumtembelea mtu atakaye kuwa Mkristo?


Jibu langu:
Ndiyo. Kama nilivyosema kwa jibu langu la hapo juu. Roho Mtakatifu anazungumza na watu wote – wema na waovu.


Chukulia mfano wa mwalimu anayejua sana kufunsidha awapo darasani. Kwa kawaida huwa si kila mwanafunzi anasikiliza asemacho mwalimu. Lakini mwalimu anawafundisha wote.


Kwa vile mwalimu anafanya kila kinachotakiwa, matokeo ya kazi sasa, yanawategemea wanafunzi. Pale mwanafunzi anapoamua mwenyewe kwamba, “Kuanzia sasa nataka niwe makini na mwalimu,” atapata A. Yule ambaye yuko bize na mawazo mengine, au na simu yake, atapata F, licha ya kwamba mwalimu ni mzuri.


Vivyo hivyo, japo Roho Mtakatifu anasema nasi muda wote, lakini pale mwanadamu anapoamua kwa makusudi kusema, “Yesu Kristo karibu moyoni mwangu,” (Maana Yesu ndiye Roho), ndipo anapoanza kuona kwa namna mpya kabisa mambo yaleyale aliyokuwa anayaona kila siku. Anaingia kwenye ulimwengu mwingine kabisa wa amani, furaha na baraka za mbinguni.


Hamudi anauliza: Utasemaje kuwa wewe ni Mkristo ikiwa Roho Mtakatifu yu ndani ya Mkristo mwingine? Inakuwaje Wakristo wengi wanawapumbaza watu kwa kudai kwamba Roho Mtakatifu yu ndani yao tu! Na baadaye wanabadilisha dini?


Jibu langu:
Ndugu Hamudi, hilini gumu kwako kwa kuwa msingi wa hoja yako ni tofauti na hali halisi. Ukinyoosha msingi huo, wala hakuna utata katika hili hata kidogo.


Usimchukulie Mungu kama mwanadamu. Mwanadamuhawezi kuwa hapa, kisha akawa kule. Lakini si hivyo kwa Mungu. Kwani mabilioni kwa mabilioni kwa mabilioni ya nyota zilizo angani zinawezaje kudumu katika ‘balance’ kwa miaka na miaka bila kuanza kugongana?


Roho Mtakatifu ndiye Mungu Muumba wa mbingu na nchi na wanadamu wote. Ulimwengu ni wake na hakuumba kitu ambacho kitamlemea. Badala ya kukaribisha mapepo/majini ndani yetu, nafasi hiyo inatakiwa ikaliwe na Mungu.


Yeyote aliye tayari kusema, “Bwana Yesu karibu moyoni na maishani mwangu,” atasikiwa na kujibiwa mara moja! Na kwa kuwa Yeye ni Mungu, anaweza bila shida yoyote kuwa ndani ya kila mwanadamu.


Biblia inasema kwamba: Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? (1Wakorintho 6:19).


Hamudi anauliza: Je, Roho Mtakatifu anaamuru kile ambacho Wakristo wanapaswa kukifanya bila ya uhuru wa kuchagua hata kidogo au anawaongoza tu na wao wana uhuru wa kufuata au kutofuata?


Jibu langu:
Mungu ni Mungu mwenye uwezo WOTE! Anaweza kuumba chochote akitakacho. Akitaka uwe mwovu hadi mwisho, ana uwezo huo. Akitaka uwe mwema hadi mwisho, ana uwezo huo. Lakini kama nilivyosema kwenye jibu langu mojawapo huko nyumba, Mungu hana haja na ‘robots’, yaani watu wanaofanya tu kile walichopangiwa bila ya ridhaa yao.


Kwenye mfano wa mwalimu na wanafunzi niliotoa hapo juu, tunafahamu sote kuwa si mwanafunzi anayeamua kitu cha kufundishwa. Mwalimu, au wizara, au mamlaka iliyo juu ndiyo inayojua kile ambacho mwanafunzi anahitaji.


Lakini mamlaka hii, haina uwezo wala sababu ya kushindilia mambo hayo ndani ya akili za wanafunzi. Kazi ya mwalimu ni kufundisha, lakini na kumweleza mwanafunzi umuhimu wa kuwa tayari kujifunza, mbinu na kujifunza, na faida za kujifunza.


Ili kujifunza huko kutokee, inategemea sasa utii wa mwanafunzi.


Vivyo hivyo, Mungu ni Mwalimu wetu. Yeye anajua kile kilicho cha faida kwetu. Ameshatueleza kwenye Biblia kila kitu kinachohitajika. Ili tuweze kufaidika, kazi yetu ni KUTII.


Maandiko yanasema:  


 • Naye Samweli akasema, je! Bwana huzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihu Sawasawa na kuitii sauti ya Bwana? Angalia, kutii ni bora kuliko dhabihu, Na kusikia kuliko mafuta ya beberu. (1 Samweli 15:22).
 • Sasa basi ikiwa mtaitii sauti yangu kweli kweli, na kulishika agano langu, hapo ndipo mtakapokuwa tunu kwangu kuliko makabila yote ya watu; maana dunia yote pia ni mali yangu (Kutoka 19:5)
 • Angalieni, nawawekea mbele yenu hivi leo baraka na laana; baraka ni hapo mtakapoyasikiza (yaani kuyatii) maagizo ya Bwana, Mungu wenu, niwaagizayo leo (Kumbukumbu 11:26-27).
 • Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi (Isaya 1:16).Kwa nini Mungu anaongelea kutii? Ni kwa sababu anaheshimu uamuzi wa mtu binafsi. Anataka uamue mwenyewe kutii amri zake na kuzifuata. Huo ndio utii na upendo wa kweli. Lakini kama “unatii” kwa sababu unaogopa kuchinjwa, kupigwa, au kupigwa, huo ni utii? Hapana! Hapo hakuna utii, bali ni woga.


Ndani ya Kristo kuna uhuru kamili na wa kweli. Unaamua kwa hiyari yako kumsikiliza au kumkataa. Hata siku moja Mungu wetu hamlazimishi mtu kumfuata au kumtii. Alichofanya kukupa maagizo yote kwenye Biblia na kukukumbusha kwa Roho Mtakatifu aliye ndani yako kwamba, “Mwanangu, huku unakoenda si kuzuri. Geuka. Fuata njia hii.”

Inakuwa sasa ni juu yako kufuata au kukataa. Ila tu siku ya mwisho ndiyo sasa unakutana naye kwenye kiti cha hukumu!


Hamudi anauliza: Ikiwa Roho Mtakatifu anaamuru kile Wakristo wanachopaswa kukifanya, kwa nini Wakristo wanafanya maovu na madhambi? Vipi unaweza kuuelezea ubadilishaji wa dini na kuingia dini na imani mbali mbali kunakofanywa na Wakristo wengi? Je, Wanaambiwa kufanya hayo na Roho Mtakatifu?


Jibu langu:
Kwanza, kama nilivyosema, Roho Mtakatifu kamwe HAAMURU jambo la kufanya. Ingekuwa ni hivyo, angetuumba tu tuwe kama roboti moja kwa moja – alikuwa na uwezo huo na anao hata sasa. 


Kitendo cha Wakristo kufanya maovu na kuingia kwenye dini nyingine ni ishara ya wazi ya uhuru ulio ndani Kristo ambao amempa mwanadamu. Roho Mtakatifu hawaambii wafanye hivyo, maana Yeye daima hutushauri kile ambacho kiko kwenye Biblia. Na Biblia haisemi tutende dhambi wala tumwache Kristo, bali inataka tuache dhambi kabisa na tusimame imara na Kristo hadi mwisho wa maisha yetu.


Kama mtu akikengeuka, hiyo ni hiyari yake – kutii au kukaidi ni uamuzi wa mtu binafsi maadamu bado yuko kwenye dunia hii. Lakini kama nilivyosema, ukitoka tu kwenye dunia hii – HAKUNA UHURU TENA –utalipwa sawasawa na kile ulichochagua! Na kile utakacholipwa ndicho kitakuwa chako MILELE!


Kwa mbingu ni za Yesu Kristo, yule ambaye, kwa hiyari yake, aliamua kumkataa Yesu, hatakuwa na sehemu katika mbingu. Basi!


Hamudi anauliza: Ikiwa Roho Mtakatifu anawaongoza Wakristo tu, na wako huru kufanya wanavyotaka, sasa ni vipi tutajua kwamba waandishi wa Biblia hawakufanya makosa wakati walipoziandika?


Jibu langu:
‘Kuwa huru kufanya unavyotaka’ haina maana ya kwamba kila unachofanya kinakubalika. Maana yake ni kuwa uko huru kutii au kukaidi amri ambazo tayari zimeshawekwa.


Kwanza ni lazima iwepo amri ndipo linapokuja tangazo la kwamba uko huru kutii au kukaidi. Tukirudi tena kwenye mfano wetu wa darasani, kwanza wizara inayohusika ni lazima ipeleke walimu, vitabu na silabasi. Ndipo sasa, mwanafunzi anakuwa na uhuru wa kutii (na kufaulu) au kuasi (na kufeli).


Maandiko yako wazi: Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi; bali kama mkikataa na kuasi mtaangamizwa kwa upanga; maana kinywa cha Bwana kimenena haya. (Isaya 1:19-20).


Sasa je, serikali au wizara inaweza kupeleka vitabu au silabasi ambazo inajua kabisa kwamba zina makosa? Jibu ni hapana. Kabla ya kuingizwa shuleni, vitabu na silabasi hizo ni lazima vikaguliwe tena na tena ili kuhakikisha kuwa makosa yote yameondolewa, ndipo wanapelekwa wanafunzi.


Biblia imechukua miaka zaidi ya 4000 katika uandishi wake. Roho Mtakatifu asingeweza kuruhusu kitu ambacho ni kibovu kije kwetu. Imeandikwa kwamba: Maneno ya Bwana ni maneno safi, Ni fedha iliyojaribiwa kalibuni [yaani kwenye tanuru la moto] juu ya nchi; Iliyosafishwa mara saba. (Zaburi 12:6).


Lakini hii haina maana kuwa shetani naye yuko kimya. Hapana. Shetani ni mpinzani wa Mungu siku zote hadi mwisho wa nyakati. Kwa hiyo amekuwa akijaribu tena na tena kuingiza mambo ambayo ni uchafuzi wa kile alichokusudia Mungu. Na uchafu huo upo kabisa hata sasa.


Na hapo ndipo anapoingia Roho Mtakatifu. Ukisoma Biblia mstari mmoja hapa mmoja kule hutajua kitu kwa ukamilifu. Lakini ukiichukulia kama ilivyo, yaani ni Neno la Mungu kwa ujumla wake, ndipo utaona jinsi inavyo-flow toka Mwanzo hadi Ufunuo. Licha ya kwamba imeandikwa kupitia waandishi wengi, na kwa maelfu ya miaka – ujumbe wake unaoana kabisa kuanzia mwanzo hadi mwisho – yaani kwa kifupi ni hadithi ya WOKOVU WA MWANADAMU.


Na unapoielewa sawasawa, ndipo sasa, pale unapokutana na maandiko mbalimbali yaliyopotoshwa, Roho Mtakatifu anaweza kukuambia wazi kwamba hili ni neno la kweli na hili si la kweli.


Sasa, ukishauelewa ule ujumbe wa kweli, ndipo ni rahisi sana kujua kama kuna mwandishi amekosea au hajakosea. Ukiachilia mbali makosa ya kibinadamu katika kunakili - [maana zipo typing errors nyingi tu katika Biblia mbalimbali]- lakini ujumbe wake HAUNA MAKOSA HATA KIDOGO!


Hamudi anauliza: Ikiwa Wakristo wanaamini kwamba Roho Mtakatifu huwajia na kuzungumza nao kila siku, kwanini hawamuulizi Roho Mtakatifu kuhusu chapisho lipi la Biblia wanalopaswa kulifuata kwa vile kuna machapisho mengi?


Jibu langu:
Ndugu yangu Hamudi, kuwapo kwa machapisho mengi wala si tatizo hata kidogo [ingawaje sina uhakika sana una maana gani unaposema ‘machapisho’].


Waislamu wengi wamekuwa na hoja kama hii lakini nahisi kuwa wanachanganya vitu viwili tofauti hapa.


Kwanza, Quran, kwa mfano katika sura 5:13, inasema kuwa Biblia iligeuzwa maneno yake. Sidhani kama hapa inamaanisha machapisho (version) kama vile King James Version, New International Version, n.k. Nafikiri hapa inataka kusema tu kwamba, kuna maneno ya Mungu ambayo ‘Wakristo waliyaacha.’


Lakini pili, Bwana Hamudi wewe sioni kama unaongelea hili. Badala yake wewe unazungumzia kuwapo kwa ‘version’ mbalimbali.


Machapisho tofauti yana lengo tu la kurahisisha welewa wa Maandiko. Kwa mfano, watu wengi huhisi kuwa King James Version ina lugha ngumu. Kwa hiyo, wanapendelea New International version, mathalani. Pia, amplified Bible ni Biblia inayofafanua maandiko kwa upana zaidi, yaani inainyumbua maana kwa upana zaidi. Sasa hili lina tatizo gani hadi nilazimike kumwuliza Roho Mtakatifu?


Kama nilivyosema, ukiujua ujumbe wa Biblia kwa ujumla wake, utatambua tu kama kuna fundisho lililo kinyume na makusudi ya Mungu. Ndiyo kazi ya Roho Mtakatifu ndani yetu. Machapisho mbalimbali si tatizo hata kidogo.


Kama hilo lingekuwa ni jambo la muhimu, basi Biblia ingetakiwa ibakie kwa Kiebrania na Kiyunani na sote tujifunze lugha hizo.


Kwa maneno yako ndugu Hamudi ni kama unataka kusema kuwa Quran haina machapisho mengi. Mimi nimeshakutana na Quran ya Kiingereza iliyochapishwa Lebanoni mwaka 1980, na nyingine iliyochapishwa Iran mwaka 2006. Na hizi zinatofautiana kwenye aya nyingi tu.


Ningependa nami nikuulize swali. Kama Quran kutokuwa na machapisho mengi kama unavyotaka tuamini, kwa nini basi kuna makundi mengi ya Waislamu? Kwa nini kuna wale wa imani kali na wale wa imani ya wastani? Mbona si kila mwislamu ni Wahabi? Kwa nini mna madhehebu? Kama Quran mnayosoma ni ileile, kwa nini msiwe ni kundi moja tu duniani kote badala ya kuwa makundi mengi, tena yanayohasimiana yenyewe kwa yenyewe hadi kufikia kuuana na kuharibiana maeneo ya ibada – kama inavyotokea kule Iraq?


Ninachotaka kusema hapa ni kuwa, japo wewe unaona kuwa Quran ni moja, lakini, ukweli kwamba inazalisha aina mbalimbali za imani ya Kiislamu, ni ushahidi kuwa tayari kuna aina mbalimbali za Quran ndani ya mioyo ya wale wanaojiita Waislamu – na hiyo ndiyo yenye nguvu zaidi kuliko hata hii iliyoandikwa kwenye karatasi!


Kwa hiyo, swali lako linakugeukia wewe mwenyewe: Kwa nini msimuulize Allah ni quran ipi iliyo sahihi? Ni ile ya imani kali au ni ile ya wastani?, n.k.


KAZI YA UJUMBE WA YESU


Hamudi anauliza: Hivi bila ya kuazima kutoka katika dini na mifumo mingine, Ukristo unaweza kuwapa wanadamu mfumo kamili wa maisha? Huku Ukristo ukiwa umefungika kwa maisha ya kiroho tu na hautoi sheria, sasa vipi jamii itaweza kuamua sheria zipi ni sahihi na zipi ni makosa?


Jibu langu:
Ndugu Hamudi, sielewi ni kwa nini unadhani kuwa inatakiwa kila kitu kitoke kwako tu. Je, huko si kuwa mbinafsi na hata dikteta? Kama nilivyosema, Kristo hakuja KULAZIMISHA watu wampende na kumtii kwa nguvu. Kama angesema kuwa ni lazima dunia yote iwe ya Kikristo, atakuwa anapingana na asili yake inayotafuta upendo wa dhati.


Dunia ni lazima iwe na tofautitofauti ili kwamba yule anayempenda Mungu kwa dhati  achague kutoka moyoni mwake kufanya hivyo. Kwa hiyo, ni lazima ziwepo mamlaka ambazo ni za kidunia na Mungu naye awe na ufalme wake ambao haujengwi kwa kulazimishana.


Hicho unachokisema wewe, yaani Ukristo kutoazima chochote, kinakuja kwa wakati wake. Mbinguni hakutakuwa na maisha mengine yoyote zaidi ya kile kilicho kwenye Biblia peke yake.


Hivyo, kwa hapa duniani, kwa wakati huu, UKRISTO NDIYO MAISHA HASA!


Na niseme kuwa, si sahihi kusema kwamba Ukristo hauna sheria. Mara nyingi watu wanachanganya kati ya mambo mawili – sheria kwa ajili ya maisha ya hapa duniani na sheria kwa ajili ya kuingia mbinguni.


Biblia inasema kuwa: kwa sababu hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki mbele zake kwa matendo ya sheria (Warumi 3:20).


Andiko hili linaongelea wokovu  na kupata haki ya kuingia mbinguni. Maana yake ni kuwa, hakuna mwanadamu YEYOTE mwenye uwezo wa kutimiza sheria ya Mungu aliye Mtakatifu kwa 100% (yaani kwa kutenda matendo mema kwa 100% kwenye maisha yake YOTE) kiasi cha kumwezesha kuingia mbinguni kutokana na matendo yake hayo mema. HAYUPO!!


Sababu yake ni rahisi tu – jaribu wewe mwenyewe kuishi kwa UKAMILIFU japo kwa saa moja: usitukane, usitamani, usiwaze mabaya, usione wivu, usiwe na hasira, n.k. – uwe na moyo SAFI KABISA!


Je, utaweza? HUWEZI!!! Sasa, kama huwezi, kwa nini uende mbinguni ambako hakuna dhambi na wewe ni mwenye dhambi? Ndiyo maana basi Mungu katika Biblia akasema kuwa ukitumainia matendo kwamba ndiyo yatakayokufikisha mbinguni, basi uwe na uhakika kwamba umekwama: jehanamu itakuwa ndiko mahali pako.


Imeandikwa: Maana mtu awaye yote atakayeishika sheria yote, ila akajikwaa katika neno moja, amekosa juu ya yote. Kwa maana yeye aliyesema, Usizini, pia alisema, Usiue. Basi ijapokuwa hukuzini, lakini umeua, umekuwa mvunja sheria. (Yakobo 2:10-11).


Hiyo ni kwa upande wa kuingia mbinguni.


Lakini kwa kuwa tunaishi hapa duniani, ni lazima kuna sheria za kuishi katika maisha haya – ila KUZITII HIZO SILO JAMBO LINALOTUPELEKA MBINGUNI!!


Tiketi ya kuingia mbinguni ni moja tu – KUAMINI KUWA YESU ALIKUJA DUNIANI KATIKA MWILI, ALIBEBA DHAMBI ZAKO, YEYE AKAUAWA BADALA YA WEWE MWENYE DHAMBI AMBAYE NDIYE ULITAKIWA KUFA, NA SASA UMESAMEHEWA DHAMBI ZAKO KAMA UTAAMINI HILO, NA UNA TIKETI YA KUINGIA MBINGUNI KWA BABA.


Baada ya hatua hiyo ya iamni, ndipo unaanza sasa kutenda matendo mema kama utii wako kwa Mwokozi wako; maana ameagiza hayo katika amri zake.


Biblia inasema: Mmoja wao, mwana-sheria, akamwuliza, akimjaribu; Mwalimu, katika torati ni amri ipi iliyo kuu? Akamwambia, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote. Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Katika amri hizi mbili hutegemea torati yote na manabii.  (Mathayo 22:35-40).


Anaposema kuwa “Katika amri hizi mbili hutegemea torati yote na manabii,” maana yake ni kuwa, ukizishika amri hizi, umeshatimiza Agano la Kale lote. Ukimpenda jirani yako kama unavyoipenda nafsi yako, hutamchukia, hutamwonea wivu, hutamtukana, hutamwibia, hutapokea rushwa, n.k.


Lakini pia, kwa upande wa mamlaka zilizoko serikalini, Bwana wetu anasema: Uwakumbushe watu kunyenyekea kwa wenye uwezo na mamlaka, na kutii, na kuwa tayari kwa kila kazi njema. (Tito 3:1).


Tiini kila kiamriwacho na watu, kwa ajili ya Bwana; ikiwa ni mfalme, kama mwenye cheo kikubwa; ikiwa ni wakubwa, kama wanaotumwa naye ili kuwalipiza kisasi watenda mabaya na kuwasifu watenda mema. (1 Petro 2:13).


Ukristo ndiyo aina PEKEE ya maisha ambayo ni PRACTICAL; ambayo yanaendana na hali halisi ya maisha ya dunia hii. Huwezi kuwabadilisha wanadamu wote wawe kama wewe – tena kwa nguvu. Hata ukiweza, mwisho wa yote watakuwa wanatenda hayo uliyowalazimisha kwa ‘kukutii’/kukuogopa WEWE na SI Mungu!!

Ninajua kuwa katika nchi za Kiislamu kuna hadi polisi wa kusimamia maadili ya kidini. Lakini mpendwa wangu, kumsimamia mwanadamu utaishia nje tu. Vipi kuhusu moyoni? Wizi au uzinzi au ugomvi, hasa si kile unachokiona kwa nje, ni hali ya moyo. Sasa kule moyoni polisi, sheria au mahakama haiwezi kufika. Huko anafika Roho Mtakatifu PEKE YAKE!!


Upendo na utii WA KWELI unatokana na uamuzi binafsi; na si kulazimishwa!!

Sheria ni mzigo usiobebeka. Mimi nikisema najua nitaonekana sijui ninachokiongea kwa kuwa mimi si Mwislamu. Hebu basi sikiliza video ifuatayo, utaona maana ya maneno haya:Hamudi anauliza: Kwa nini Wakristo wanasema kwamba Yesu alikuja kwa ajili ya ulimwengu mzima wakati yeye alisema kuwa alitumwa kwa Mayahudi tu? Alimwambia yule mwanamke Mkananayo aliyemuomba amtibie bintiye aliyekuwa anasumbuliwa na mapepo: “Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli.” na pia alisema; Si vyema kukitwaa chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.” (Matayo 15:21-28).


Jibu langu:
Ni vizuri kwamba unamnukuu Yesu ili kujenga hoja yako. Basi, ni vizuri usiishie hapo. Hebu tazama pia maneno yake haya mengine:


Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu (Mathayo 28:19).


Akawaambia, Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu; na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu. (Luka 24:46-47).


Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. (Yohana 3:17).


Na mtu akiyasikia maneno yangu, asiyashike, mimi simhukumu; maana sikuja ili niuhukumu ulimwengu, ila niuokoe ulimwengu. (Yohana 12:47).


Nami nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo. Na kondoo wengine ninao, ambao si wa zizi hili; na hao nao imenipasa kuwaleta;  sauti yangu wataisikia; kisha kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja. (Yohana 10:15-16).


Sasa unaweza kuamua. Kama ingekuwa ni kupiga kura, kati ya andiko ulilonukuu na haya niliyokupa, upi ambao ungeuita kuwa ni msimamo wa Yesu? Ni ule wenye andiko moja au ni ule wenye maandiko mengi?


Lakini huenda bado utauliza, “Kwa nini basi alimwambia maneno hayo mwanamke yule Mkananayo?”


Jibu ni kuwa, (kama nilivyosema kwenye jibu langu moja huko nyuma), Mungu amekuwa na kawaida ya kuanza jambo na mtu mmoja.

 • Aliumba mwanadamu mmoja, kisha tukatokea humo wote.
 • Alijifunua kwa taifa moja, kisha tukamjua wote.
 • Alianza na Mwana mmoja (Yesu), kisha tunazaliwa wote kwa imani katika huyo.
 • Vivyo hivyo, alileta wokovu Israeli, kisha ukasambaa kote – ndiyo maana anasema na mwanamke mwingine pale kisimani – “Wokovu watoka kwa Wayahudi.” (Yohana 4:22).

Hali hii ya kuanza na mtu au sehemu moja, ni ushahidi kuwa wale wote wanaojifariji kwa maneno eti “dini mbalimbali ni njia tofauti ambazo zote zinaishia kwa Mungu”, wanapoteza muda na uzima wao wa milele. “Wokovu watoka kwa Wayahudi” – yaani KWA YESU PEKEE!


Sasa, kwa kuwa muda wa kusambaa kwa wokovu huo ulikuwa haujatimia (maana Mungu anakwenda kwa ratiba ya majira na nyakati), ndiyo maana akamwambia yule mwanamke Mkananayo (yaani asiye Myahudi) kuwa hakutumwa ila kwa Israeli.


Lakini utimilifu wa majira ulipofika, yaani alipokufa na kufufuka, ndiyo maana tunaona akiwaagiza sasa mitume wake waende ulimwenguni kote.


Na Biblia inasema wazi:
Kwa ajili ya hayo kumbukeni ya kwamba zamani ninyi, mlio watu wa Mataifa kwa jinsi ya mwili, mnaoitwa Wasiotahiriwa na wale wanaoitwa Waliotahiriwa, yaani, tohara ya mwilini iliyofanyika kwa mikono; kwamba zamani zile mlikuwa hamna Kristo, mmefarakana na jamii ya Israeli, wageni wasio wa maagano ya ahadi ile. Mlikuwa hamna tumaini, hamna Mungu duniani. Lakini sasa, katika Kristo Yesu, ninyi mliokuwa mbali hapo kwanza mmekuwa karibu kwa damu yake Kristo. Kwa maana yeye ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi sote tuliokuwa wawili kuwa mmoja; akakibomoa kiambaza cha kati kilichotutenga. Naye akiisha kuuondoa ule uadui kwa mwili wake; ndiyo sheria ya amri zilizo katika maagizo; ili afanye hao wawili kuwa mtu mpya mmoja ndani ya nafsi yake; akafanya amani. Akawapatanisha wote wawili na Mungu katika mwili mmoja, kwa njia ya msalaba, akiisha kuufisha ule uadui kwa huo msalaba. (Waefeso 2:11-16).


NINA SWALI KWAKO HAMUDI


Je, ni vizuri kuwa mtu bora kabisa au si vizuri? Je, ni watu gani ambao ni bora kuliko wote kwa mujibu wa Quran? Je, ni Wakristo au ni Waislamu?


Imeandikwa katika Quran:


The unbelievers among the People of the Book and the pagans shall burn forever in the fire of Hell. They are the vilest of all the creatures. But those that embrace the faith and do good works are the noblest of all creatures.


Yaani:
Wale wasioamini miongoni mwa Watu wa Kitabu na wapagani wataungua milele katika moto wa jehanamu. Hao ni waovu kuliko viumbe wote. Lakini wale wanaoikumbatia imani na kutenda mema ni waadilifu kuliko viumbe wote. (Al-Bayyina 98:6-7).


Unangoja nini sasa kuingia kwenye kundi la walio bora kuliko viumbe wote? Njoo kwa Mwokozi wako sasa. Mwamini Yesu upate uzima wa milele. Mwite sasa ili aingie moyoni mwako kwa Roho wake Mtakatifu, maana huyo ndiye aliyekuumba. Anajua kipi ni kizuri na kinafaa kwa ajili ya kila mwanadamu. Lakini hatamlazimisha yeyote kumpenda. Ni uamuzi wa kila mtu binafsi, baada ya kusikia maneno ya Kristo na mwaliko wake, kuamua yeye mwenyewe kumkaribisha maishani mwake. Ni baada ya hapo tu ndipo utajua nini maana ya maisha haya; na utapata furaha na amani ya kweli.


Kama Mungu angekuwa na haja na matendo mema, angeumba tu roboti nyingi ambazo zingetenda matendo hayo bila hata kukosea. Matendo yana kitu kingine zaidi tu ya kutendwa!


No comments:

Post a Comment