Wewe hujawahi kujiona hata siku moja!
Biblia inasema kwamba sisi tumeumbwa kwa mfano wa Mungu. Mungu alipopanga
kumwumba mwanadamu alisema, Na tumfanye mtu kwa
mfano wetu, kwa sura yetu. (Mwa. 1:26).
Biblia pia inasema: BWANA Mungu
akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi. (Mwa. 2:7). Na tena: Mungu ni Roho.
(John 4:24).
Maandiko haya mawili yanatuonyesha
mambo kadhaa kuhusu mwanadamu:
- Mwanadamu ana sura ya Mungu (yaani anafanana na Mungu).
- Mwanadamu ni udongo.
- Mungu ni Roho; si udongo.
- Pale ninapojitazama, kile ninachoona ni udongo (mwili).
- Kwa vile Mungu si udongo, basi yule mtu ambaye Mungu alisema ni mfano wake si hiki ninachokiona, yaani udongo.
Mimi halisi lazima nitakuwa roho pia
kama alivyo Mungu; si mwili. Kimsingi, baada ya Mungu kuumba, hata maandiko
yanasema: akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa
nafsi hai. (Mwa. 2:7b).
Mimi halisi (ile roho ambayo ndiyo sura
ya Mungu) ninaishi ndani ya huu udongo ninaouona.
Kwa vile mimi ni roho, kibiblia mwili
wangu unaitwa nyumba ya maskani yetu iliyo ya dunia.
(2 Kor. 5:1).
Nitakapotoka nje ya mwili huu ndipo
nitakapokuwa katika ngazi ileile sawa na Mungu, malaika na hata mapepo, yaani
nitakuwa ni roho kama wao walivyo roho. Hapo ndipo nitakuwa mimi halisi.
Nitakapokuwa nje ya mwili huu, bado
nitakuwa ni mtu kamili kabisa, tofauti na watu wengine kama sasa. Hebu tuone
anachosema mtume Paulo juu ya kuwa nje ya mwili: Namjua mtu mmoja katika
Kristo, yapata sasa miaka kumi na minne, kwamba alikuwa katika mwili sijui;
kwamba alikuwa nje ya mwili sijui; Mungu ajua. (2 Kor. 12:2).
Ukisoma aya zilizo kabla na baada ya
aya hii, utagundua kuwa Paulo anajiongelea yeye mwenyewe. Sote tunafahamu kuwa
mtu hawezi kwenda mbinguni na mwili huu wa udongo. Mungu anasema wazi kwamba: kwa
maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi. (Mwa. 3:19).
Ni roho, yaani yule mtu wa ndani; yule
mtu halisi ambaye ndiye ana uwezo wa kuingia kwenye ulimwengu wa roho. Kwa
hiyo, haikuwa ni Paulo-udongo aliyeenda mbinguni bali ni Paulo-roho. Ukiwa nje
ya mwili, bado unakuwa na ufahamu wako wote. Paulo anatuambia: akasikia maneno
yasiyotamkika, ambayo haijuzu mwanadamu ayanene. (2 Kor. 12:4). Aliweza
kusikia na kuelewa mambo yaliyosemwa kule mbinguni; lakini wakati huo mwili na
masikio yake ya udongo yalikuwa hapa duniani.
Sasa basi, ile roho, ambayo ndiyo mimi
halisi ndiyo:
Inayoupa mwili wangu uhai. Ukiondoa
mwili wangu kutoka kwangu, bado nitaendelea kuwa hai kabisa; lakini ukiondoa
roho yangu kutoka kwenye mwili, mwili unakufa mara moja! Mungu anasema: … mwili
pasipo roho umekufa, ... (Yak. 2:26).
- Mimi-roho ni halisi zaidi kuliko mimi-udongo.
- Roho itakuwa hai milele.
- Roho ndiyo sehemu yangu ya muhimu ninayotakiwa kuitilia maanani zaidi.
- Roho ndiyo ambayo shetani anatumia juhudi zake zote kuiharibu na kuitenga na Mungu milele.
Kile anachofanya shetani
Kwa kuwa shetani na malaika zake walishahukumiwa milele
na hawana tena tumaini la wokovu, wanajibidisha usiku na mchana kutekeleza
jambo moja tu – kutumia kila njia kumharibu mwanadamu! Mungu anatueleza wazi: Mwivi haji ila aibe na kuchinja na
kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele. (Yohana 10:10).
Ili kutekeleza lengo hili, shetani
anafanya kile awezalo kutufanya tusielekeze macho yetu kwenye roho (mimi
halisi); badala yake nielekeze macho yangu kwenye mimi-udongo. Matokeo yake,
tunatumia muda mwingi sana tukijaribu kutimiza tamaa mbalimbali za mwili, ilhali
mwili hauwezi kamwe kuridhishwa na kitu chochote – huku ndiko kutia maji kwenye
gunia hasa! Kamwe haliwezi kujaa! Imeandikwa: Kwa sababu mwili hutamani
ukishindana na Roho, na Roho hushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana,
hata hamwezi kufanya mnayotaka. (Gal. 5:17). Matokeo ya haya ni kuwa: Maana yeye
apandaye kwa mwili wake, katika mwili wake atavuna uharibifu. (Gal.
6:8).
Ili kutekeleza kusudi hilo, majeshi
yaliyo kwenye ufalme wa giza yanahakikisha kuwa tunahangaishwa kila uchao na
mambo kama vile ulevi, uzinzi, kusaka fedha, kusaka umaarufu, ulipizaji kisasi,
muziki wa kidunia, dawa za kulevya, uchawi, ... nk, nk.
Tunapofungwa na mambo haya, tunakuwa vipofu na viziwi kabisa! Hatuwezi tena
kusikia, kuona au kukubali wazo kwamba yapo maisha mengine bora zaidi ya yale
tunayoendesha. Huu ndio ukweli halisi! Tunakuwa tunadhani hapo ndipo tumefika.
Kisha pale maisha ya mtu yanapofika mwisho, mara tu anapokufa, palepale
anatambua jinsi ambavyo alikuwa akiishi kwenye uongo na udanganyifu siku zote.
Na hapo ndipo anapotambua kuwa siku zote hakuwa anajifahamu yeye ni nani hasa.
Anagundua kuwa kumbe alikuwa anahangaikia mwili usio na maana, huku akiwa
ametelekeza sehemu ya muhimu kabisa, yaani yeye halisi (roho). Na hapo anakuwa
ameshachelewa kabisa!
Unakuwa kama ilivyokuwa kwa tajiri katika Biblia; akili zake zilikuwa
timamu kabisa na tena anaonyesha ufahamu na hekima kubwa; isipokuwa ni mahali
ambapo hekima na ufahamu huo haukumsaida tena. Alitakiwa kuutumia angali
duniani, kama ilivyo kwa sisi leo. Huyu tajiri alimwambia Ibrahimu: nihurumie,
umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake majini, auburudishe ulimi wangu; kwa
sababu ninateswa katika moto huu. (Lk. 16:24).
Tunaporuhusu mambo yafike hapa, Mungu anasema: Ndipo watakaponiita, lakini
sitaitika; watanitafuta kwa bidii, wasinione. Kwa kuwa walichukia maarifa, wala
hawakuchagua kumcha BWANA. Hawakukubali mashauri yangu, wakayadharau maonyo
yangu yote. Kwa hiyo watakula matunda ya njia yao, watashiba mashauri yao
wenyewe. Maana kurudi nyuma kwao wajinga kutawaua, na kufanikiwa kwao wapumbavu
kutawaangamiza. Bali kila anisikilizaye atakaa salama, naye atatulia bila
kuogopa mabaya. (Prov. 1:28-33).
Wakati mtu anapokuwa duniani, anadhani kuwa haiwezekani kuishi bila kutumia
dawa za kulevya, pombe, uzinzi, uongo, hasira, nk. Lakini akishatumbukia
upotevuni, anatamani apate japo hata tone moja la maji – ingawaje sasa hata
hilo halipati! Hebu tafakari juu ya hilo! Kumbuka, kiu hii haitakuwa ya siku
moja au mbili. Itakuwa ndio maisha yako milele na milele!!
Je, ni vibaya kuwa na
maisha mazuri?
Sisemi hata kidogo kwamba kuwa tajiri ni dhambi. Kimsingi, hata Biblia
inasema: Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini
kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa
umaskini wake. (2 Kor. 8:9).
Tena Mungu anasema: Leteni zaka kamili
ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo,
asema BWANA wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na
kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la. (Mal. 3:10). Mungu
anapenda kabisa tuwe matajiri, tena matajiri wakubwa!
Suala la msingi ni kuwa, je, umemkaribisha Bwana Yesu moyoni mwako na kumpa
nafasi ya kwanza katika kila jambo ikiwa ni pamoja na mambo yako ya kusaka
maisha? Utajiri na heshima vinatakiwa vitoke kwake. Tukitanguliza dunia na
mwili mbele, bado tutakuwa matajiri kulingana na juhudi tulizo nazo, lakini
mara tutakapotoka kwenye maisha haya ndipo tutakapojiona jinsi ambavyo tu
maskini wa kutupwa.
Bwana Yesu anasema: Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala
sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na
maskini, na kipofu, na uchi. Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa
kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako
isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona. (Ufu.
3:17-18).
Sasa je, unaishi kulingana na sheria ya Mungu au unaishi kulingana na sheria
ya mwili na dunia? Umeelekeza macho yako kwenye wewe-roho unayedumu milele au
kwenye wewe-udongo uliye wa kitambo tu?
Jukumu letu
Bwana Yesu anasema:
Linda sana moyo wako kuliko yote uyalindayo; maana ndiko zitokako chemchemi za
uzima. (Mithali 4:23).
Tukifuata tu mambo ya dunia kwa sababu tu yamepewa umaarufu na vyombo vya
habari; au kwa kuwa tu eti watu fulani maarufu wanaonekana kuyafuata; kama
mambo hayo yako kinyume na Neno la Mungu, hayo si lolote si chochote bali ni
hila na uongo kutoka kuzimu ambao umepangwa kwa ustadi mkubwa ili kukunasa na
kukuua milele!
Ibilisi yuko kazini ndugu. Yeye hana mchezo na malengo yake. Lakini wewe
unachezacheza tu na maisha wala hukai uwaze unakoelekea. Maandiko yanasema:
Wenye kiburi wamenifichia mtego na kamba; wametandika wavu kando ya njia;
wameniwekea matanzi. (Zab. 140:5). Pia imeandikwa: Miiba na mitego huwa katika
njia ya mshupavu; yeye aitunzaye nafsi yake atakuwa mbali nayo. (Mith. 21:5).
Rafiki, haya mambo ni halisi kabisa. Hakuna mwindaji atakayetega mtego waziwazi.
Ni lazima ataufunika ili yule aliyetegwa asiutambue. Yale mambo ambayo wewe
unadhani ni kula raha, yamewekewa hiyo hali ya raha ili wewe usishituke - iwe ni
pombe, disko, kukesha kusaka utajiri, nk. Huo ni mtego kabisa wa adui. Huwezi
kupona nje ya Kristo. Huwezi kamwe!
Rudi tena utwae usukani wa maisha yako kutoka mikononi mwa dereva muuaji,
kisha uanze kutawala hayo maisha aliyokupa Mungu ambayo ni ya thamani kuliko
unavyoweza kufikiri. Bwana Yesu yuko tayari kabisa kukuongoza kwa usalama hadi
ufike nyumbani, mbinguni.
Tafadhali, tafadhali, tafakari juu ya mambo haya. Japokuwa yanaonekana ni
ya kipuuzi kwa wengi, lakini jambo moja ni dhahiri – kila mmoja atakufa siku
moja! Nini kitafuata kwako baada ya hapo?
Wewe halisi (yule mtu wa ndani) haishi kwa kula wali na ugali. Anaishi kwa
kula Neno la Mungu lililoandikwa kwenye Biblia. Bwana wetu Yesu anasema: Mtu
hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu. (Mt. 4:4).
Mambo ya rohoni ni halisi kabisa lakini yako kwa namna ambayo ni vigumu
sana kuyaelewa kwa akili za kibinadamu. Ndiyo maana imeandikwa: Basi mwanadamu
wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuuzi,
wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni. (1 Kor.
2:14).
Ndugu, kama unangoja akili zako zielewe ndipo uamini, hautaamini kamwe. Kwa
maana nyingine, hapo tayari adui ameshakushika na kukutoa nje ya mstari.
Ni lazima tufahamu kwamba, japokuwa Mungu ana nguvu zote, kamwe
hatamlazimisha mtu yeyote kumwamini. Badala yake yeye anaomba ruhusa ya kuingia
moyoni mwako. Hakika Mungu wetu ni wa ajabu! Anasema: Tazama, nasimama
mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia
kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami. (Ufunuo 3:16). Ni pale tu tunaponyenyekea na kusema, “Karibu moyoni mwangu Bwana Yesu”
ndipo mambo yanaanza kueleweka.
Usitafute sababu zinazoonyesha kwamba haiwezekani. Ukifanya hivyo,
utazipata maana ziko nyingi sana. Badala yake, mwamini Bwana Yesu; mkaribishe
moyoni mwako leo; amini ahadi zake maana yeye ndiye njia, kweli na uzima!
Hakika Mungu ni mwema kwani anawatumia watu wake ambao ni kazi ya mikono yake ili kuwahokoa wale waliofungwa na nguvu za mwili.
ReplyDeleteAhsante sana kwa somo zuri Mungu akupe neema yake katika utumishi. AMINA
By Vaileth Kiiza
Amina dada Vaileth. Ubarikiwe na Bwana. Endelea kusimama naye hadi mwisho.
ReplyDeleteHABARI UPO HMPAKA HUKU
Deletemh!
ReplyDeleteemback mbona mguno huu unanitisha. ha ha ha. Hebu niambie ulivyoliona somo hili, hata kama kuna kitu unadhani hakiko sawa na maandiko.
ReplyDeletehalelluya! Hakika ukikaa ndani ya Neno la Mungu ndipo utakapojua siri zilizositirika-ni jipya kila wakati. Mungu akuzidishie kuona katika Jina la Yesu.
ReplyDeleteAmina Revocatus. Ni kweli kabisa. Kwenye Biblia ziko siri nyingi, nyingi mno ambazo hadi tunamaliza safariyetu hapa duniani, hatutazijua zote. Kwa hiyo, kadiri tunavyochimbua humo, ni kweli kabisa Roho Mtakatifu anakuwa anatuonyesha mambo mengi ya kushangaza.
ReplyDeleteMaandiko yanasema katika Mithali 2:1-5:
Mwanangu, kama ukiyakubali maneno yangu, Na kuyaweka akiba maagizo yangu;
Hata ukatega sikio lako kusikia hekima, Ukauelekeza moyo wako upate kufahamu;
Naam, ukiita busara, Na kupaza sauti yako upate ufahamu;
Ukiutafuta kama fedha, Na kuutafutia kama hazina iliyositirika;
Ndipo utakapofahamu kumcha Bwana, Na kupata kumjua Mungu.
great to meet you injiliyakweli.blogspot.com owner discovered your blog via search engine but it was hard to find and I see you could have more visitors because there are not so many comments yet. I have found site which offer to dramatically increase traffic to your website http://xrumer-services.net they claim they managed to get close to 4000 visitors/day using their services you could also get lot more targeted traffic from search engines as you have now. I used their services and got significantly more visitors to my blog. Hope this helps :) They offer most cost effective services to increase website traffic Take care. Roberto
ReplyDeleteHi Roberto,
ReplyDeleteThank you so much for taking your time to visit this little blog. Thank you too for your suggestion. God bless you a lot.