Sabato ilianzia wakati wa uumbaji ambapo baada ya siku sita za uumbaji,
Mungu alipumzika siku ya saba.
Imeandikwa: Na siku ya saba Mungu alimaliza
kazi yake yote aliyoifanya, akastarehe siku ya saba, akaacha
kufanya kazi yake yote aliyoifanya. Mungu
akaibarikia siku ya saba, akaitakasa kwa sababu katika siku hiyo Mungu alistarehe, akaacha kufanya kazi
yake yote aliyoiumba na kuifanya. (Mwa. 2:2-3).
Hatimaye ulifika wakati ambapo Mungu aliwatoa wana wa Israeli kutoka
utumwani Misri; ndipo aliwapa amri juu ya sabato.
Imeandikwa: Ikumbuke siku ya sabato uitakase. Siku sita fanya
kazi, utende mambo yako yote; lakini siku ya saba ni sabato ya BWANA, Mungu
wako, siku hiyo usifanye kazi yo
yote ... (Kut. 20:8-9).
MAANA YA NENO ‘SABATO’
Sabato ni neno linalotokana na neno la Kiebrania ‘shabbat’ ambalo lina maana
ya kusimamisha, kukomesha, kuacha, au kupumzika. Hii ina maana ya kusimamisha jambo fulani, kulifanya likome kuendelea,
au kuacha kutenda kitu fulani.
Kwa hiyo, kwa upande wa maisha ya kila siku ilimaanisha kwamba ikifika
siku ya sabato, kazi zote zikome; watu wasimame au waache kufanya kazi zao
ambazo walikuwa wanazifanya kwa siku sita zilizotangulia. Ilimaanisha kuwa watu
wapumzike.
NAMNA SABATO ILIVYOTUNZWA
Katika kutekeleza amri ya Mungu, yalikuwapo mambo mengi yaliyoambatana
na utunzaji wa sabato, ambayo kwa ujumla wake yamebebwa na maneno “usifanye
kazi yoyote” (Kut. 20:10) , au kwa namna nyingine “pumzika” au “starehe”.
Imeandikwa: Kazi itafanywa siku sita; lakini
siku ya saba ni Sabato ya kustarehe kabisa takatifu kwa BWANA. (Kut. 31:15).
Sasa, mambo ambayo yaliambatana na huo utunzaji wa sabato, yaani ambayo
yalizuiwa kufanywa, ni pamoja na haya yafuatayo:
Kufanya biashara
Tena wakakaa humo watu wa Tiro, walioleta samaki,
na biashara za kila namna, wakawauzia wana wa Yuda siku ya sabato, na mumo humo
Yerusalemu. Ndipo nikagombana na wakuu wa Yuda, nikawaambia, Ni neno baya gani
hili mnalofanya ninyi, na kuinajisi siku ya sabato? (Neh. 13:16-17).
Kubeba mizigo
Bwana asema hivi, Jihadharini nafsi zenu, msichukue
mzigo wowote siku ya sabato. (Yer. 17:21).
Ndiyo maana Bwana Yesu alipomponya mtu aliyekuwa hawezi kwa muda wa
miaka thelathini na nane na kumwambia, Simama,
jitwike godoro lako, uende. (Yoh. 5:8), Wayahudi walipomwona mtu huyo walimwabia,
Leo ni siku ya sabato, wala si halali kwako
kujitwika godoro. (Yoh. 5:10).
Kukusanya kuni
Kisha wakati huo wana wa Israeli walipokuwapo
jangwani, wakamwona mtu mmoja akikusanya kuni siku ya sabato ... wakamleta kwa
Musa ... BWANA akamwambia Musa, Mtu huyo
lazima atauawa. (Hes. 15:32-35).
Kuwasha moto/kupika
Hamtawasha moto katika nyumba zenu kwa siku ya
Sabato. Hii ina maana kwamba
haikuruhusiwa kupika vyakula siku ya sabato. (Kut. 35:3).
Kutembea mwendo mrefu
Kaeni kila mtu mahali pake, mtu awaye yote
asiondoke mahali pake kwa siku ya saba. (Kut. 16:29).
Kulikuwa na kiasi kinachoruhusiwa cha mtu kutembea inapofika siku ya
sabato (Mdo 1:12). Ilikuwa ni makosa kwa mtu kwenda mwendo unaozidi kiasi
hicho.
ADHABU YA KUVUNJA SABATO
Mtu ambaye aliasi sheria ya sabato, adhabu yake ilikuwa ni kuuawa.
Maandiko yanasema: Kila mtu atakayefanya
kazi yoyote siku ya sabato, hakika yake atauawa. (Kut. 31:15b).
VIPINDI VITATU VYA MAISHA YA MWANADAMU
Mungu ameweka safari yetu yote ya kiroho katika nyakati au vipindi vikuu
vitatu. Tunaweza kuviita vipindi hivyo kuwa ni: kipindi cha mfano, kipindi cha
uhalisia wa kwanza, na kipindi cha utimilifu wa yote.
KIPINDI CHA MFANO
Hiki ni kipindi ambacho kilihusu utimizaji wa maagizo ya Mungu kimwili.
Kilikuwa ni kipindi cha maisha ya wana wa Israeli katika nyakati za Biblia.
Maandiko yanasema juu ya kipindi hiki kwamba: Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano,
yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani. (1Kor. 10:11).
Hii inamaanisha
kwamba, maisha ya wana wa Israeli waliyoishi kimwili yalikuwa ni mfano wa mambo
ya rohoni ambayo Mungu aliyakusudia kwa ajili yetu tangu kuumbwa kwa ulimwengu.
Lakini kabla hajayadhihirisha kwa ulimwengu wote makusudi yake hayo ya kiroho,
aliyaonyesha kwanza kimwili kwa kutumia maisha halisi ya watu wachache, yaani
Waisraeli.
Pia imeandikwa: Basi torati, kwa kuwa ni kivuli cha mema yatakayokuwa, wala si sura yenyewe ya mambo hayo, kwa dhabihu zilezile wanazozitoa kila mwaka daima,
haiwezi wakati wowote kuwakamilisha wakaribiao. (Ebr. 20:1).
Maisha ya wana wa
Israeli yaliongozwa na torati ambayo walifundishwa na Mungu kupitia Musa. Torati
hiyo haikuwa jambo lenyewe halisi, bali ilikuwa ni taswira au picha ya kile
ambacho ndicho hasa alikusudia Mungu, si tu kwa Israeli, bali kwa ulimwengu
wote.
Katika kipindi hiki,
watu walihesabiwa haki kwa kutenda matendo ya sheria (torati) kimwili kabisa.
Ndiyo maana Mungu akasema: ... mtazishika amri
zangu na hukumu zangu; ambazo mtu akizitumia ataishi kwa hizo; mimi ndimi
BWANA. (Law. 18:5).
Pia imeandikwa: Na torati haikuja kwa imani, bali, Ayatendaye hayo
ataishi katika hayo. (Gal. 3:12).
Maana ya maneno haya
ni kuwa, ukitaka uishi unaweza kufanya hivyo kwa kuitimiza torati YOTE! Ukiishi
kwa torati halafu ukaivunja, basi utakufa. Na wakati huo watu walikufa kimwili
kabisa, kwa mfano kwa kupigwa kwa mawe.
Tumesema kwamba torati
ilikuwa ni sheria ya Mungu ambayo ilitekelezwa kimwili. Kabla hatujaangalia
jinsi ambavyo sabato nayo ilikuwa ni ya kimwili, ifuatayo ni mifano mbalimbali ya
jinsi Waisraeli walivyotekeleza torati kimwili:
Msamaha wa dhambi
Mtu alipotenda dhambi,
ili aweze kusamehewa dhambi zake, ilimbidi aende kwa kuhani na mnyama halisi.
… nami
nimewapa ninyi hiyo damu juu ya madhabahu, ili kufanya upatanisho juu ya nafsi
zenu; kwani ni hiyo damu ifanyayo upatanisho kwa ajili ya nafsi. (Law.17:11).
Mavazi
Imeandikwa: ... wala usivae mwilini mwako nguo ya namna mbili
zilizochanganywa pamoja. (Law. 19:19b). Usivae
nguo iliyochanganyikana sufu na kitani pamoja. (Kumb. 22:11). Hii
ilikuwa ni amri iliyohusu nguo halisi kabisa zinazovaliwa mwilini.
Kutembelewa na Bwana
Bwana alipotaka
kuwatembelea watu wake, watu walifua nguo halisi kabisa walizovaa mwilini.
Imeandikwa: Bwana akamwambia Musa, Enenda kwa watu
hawa, ukawatakase leo na kesho, wakazifue nguo zao, wawe tayari kwa siku ya
tatu; maana siku ya tatu BWANA atashuka katika mlima wa Sinai machoni pa watu
hawa wote. (Kut. 19:10-11).
Vyakula
Haikuruhusiwa kula
baadhi ya vyakula kwa kuwa vilitajwa kuwa ni najisi. Imeandikwa: Usile kitu
chochote kichukizacho. ... msile katika wale wenye
kucheua, na hao waliopasuliwa ukwato; ngamia, na sungura, na kwang’a, kwa kuwa
hucheua, lakini hawakupasuliwa kwato, ni najisi kwenu; na nguruwe, kwa kuwa
amepasuliwa ukwato lakini hacheui, huyu ni najisi kwenu, msile nyama zao, wala
mizoga yao msiiguse. (Kumb. 14:3,7,8).
Kutoka utumwani
Waisraeli walitoka
utumwani kwenye nchi Misri ya kimwili yenye Farao wa kimwili, wakapita kwenye
jangwa la kimwili, na hatimaye wakaelekea kwenye Kanaani ya kimwili.
Imeandikwa: Bali aliwaongoza watu wake kama kondoo, akawachunga kama
kundi jangwani. Hao akawachukua salama wala hawakuogopa, bali bahari
iliwafunikiza adui zao. Akawapeleka hadi mpaka wake mtakatifu, mlima alioununua
kwa mkono wake wa kuume. Akawafukuza mataifa mbele yao, akawapimia urithi kwa
kamba, na kuwakalisha kabila za Israeli katika hema zao. (Zab.
78:52-55).
KIPINDI CHA UHALISIA WA KWANZA
Hiki ni kipindi cha kupokea ahadi za Mungu na kuishi kwa imani. Kile
kilichokuwa mfano, kinakuwa ni kitu halisi. Hata hivyo, uhalisi huu si
utimilifu wa kudumu kwa sababu kipindi hiki nacho kitabadilika na kuwa bora
zaidi.
Hapa mambo yale ya Agano la Kale bado yanatendeka vilevile kama zamani, lakini
si kimwili tena, bali ni kiroho. Kipindi hiki kilianza na ujio wa Bwana Yesu
hapa duniani, na kinaendelea hadi sasa.
Hebu tuangalie jinsi mambo tuliyoongelea hapo juu yanavyotendeka katika
kipindi hiki:
Msamaha wa dhambi
Bado sheria ni ileile
kabisa. Hata leo bado tunatoa kafara ya damu ili kusamehewa dhambi zetu. Tofauti
tu ni kwamba hatutoi tena wanyama halisi kama zamani. Wanyama waliotolewa
kafara katika Agano la Kale walikuwa ni kivuli au taswira ya kafara timilifu, yaani
Mwana-Kondoo wa Mungu, Yesu Kristo.
Yohana alipomwona Yesu alisema: Tazama
Mwana-Kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu. (Yoh. 1:29). Kama
ambavyo zamani wanyama waliuawa kwa niaba ya mtenda dhambi, yaani walibebeshwa
dhambi zake, ndivyo ambavyo Mwana-Kondoo wa Mungu alivyobebeshwa dhambi ya
ulimwengu wote, kisha akatolewa kafara kwa niaba ya ulimwengu wote.
Ndiyo maana maandiko yanamwongelea
Bwana Yesu kuwa ni: Yeye atupendaye na kutuosha
dhambi zetu katika damu yake. (Ufu. 1:5).
Mavazi
Hata leo sheria ya
kutovaa mavazi yaliyochanganya rangi bado iko palepale.
Pia imeandikwa: Nitafurahi sana katika BWANA, nafsi yangu itashangilia
katika Mungu wangu; maana amenivika mavazi ya wokovu, amenifunika vazi la haki
... (Isa. 61:10).
Mavazi ni ishara ya
wokovu. Wokovu ni mmoja tu. Hauwezi kupatikana kwa njia nyingine tofauti na
iliyowekwa na Mungu.
Maandiko yanasema: Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu
walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo. (Mdo. 4:12), yaani
ni jina la Yesu pekee. Kutafuta wokovu kwa
kutumia dini, imani au jambo jingine lolote nje ya Yesu ni kujivika mavazi ya
rangi nyingi. Vazi la wokovu ni la rangi moja tu; nyeupe!
Kutembelewa na Bwana
Bwana alipokuwa
anamuandaa Paulo kwa utumishi, Anania anamwambia Paulo: Basi sasa, unakawilia nini? Simama, ubatizwe, ukaoshe dhambi zako, ukiliitia
jina lake. (Mdo. 22:16).
Halikuwa tena suala la
kumwambia Paulo asimame akafue nguo alizovaa mwilini mwake.
Biblia pia inasema juu
yetu kwamba: Na baadhi yenu mlikuwa watu wa namna
hii; lakini mlioshwa, lakini mlitakaswa, lakini mlihesabiwa haki katika jina la Bwana Yesu
Kristo, na katika Roho wa Mungu wetu. (1 Kor. 6:11).
Hii inaonyesha kwamba suala
la kuosha au kufua bado liko palepale. Isipokuwa sasa kinachooshwa si nguo
zilizoko mwilini bali ni uchafu uliomo moyoni, yaani dhambi. Na kinachoosha si
tena maji ya kimwili, bali ni damu ya Yesu na Neno lake.
Vyakula
Chakula kazi yake ni
kutia uzima kwenye mwili. Kama ilivyokuwa katika Agano la Kale, hata sasa kuna
vyakula vilivyo safi na vyakula visivyo safi, yaani ambavyo ni najisi.
Bwana anasema wazi kwamba: Mimi
ndimi chakula chenye uzima kishukacho toka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi
milele. Na chakula nitakachotoa ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa
ulimwengu. (Yoh. 6:51).
Tunafahamu kwamba Yesu
ni Neno la Mungu (Yoh. 1:1). Kwa hiyo, kula chakula najisi ni kuingiza moyoni
maneno yasiyo ya Mungu kiasi kwamba nafsi inajaa takataka na uchafu; mawazo
mabaya, hisia mbaya, n.k.
Ndiyo maana Bwana akaongea wazi kwamba: Sikilizeni,
mfahamu; Sicho kiingiacho kinywani kimtiacho mtu unajisi; bali kitokacho
kinywani ndicho kimtiacho mtu unajisi. (Mt. 15:11).
Uovu wa mtu haufiki rohoni kupitia tumboni kwa njia ya chakula. Pia roho ya
mtu haili wali au nyama au ugali, bali hula Neno. Biblia inasema: Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu;
maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima. (Yoh. 6:63).
Yakiingia maneno ya Kristo moyoni, unapata uzima na afya ya kiroho, lakini
yakiingia maneno mengine, hicho ni chakula najisi.
Lakini kuhusu chakula cha kimwili, Biblia
inasema: Lakini chakula hakituhudhurishi mbele za
Mungu; maana, tusipokula hatupunguziwi kitu,
wala tukila, hatuongezewi kitu. (1 Kor. 8:8).
Kutolewa utumwani
Waisraeli walitolewa
katika nchi ya utumwa kwa mkono hodari
wa Mungu aliye hai. Haikuwa ni kwa uwezo wao wenyewe, maana wangekuwa na
uwezo wasingekaa utumwani kwa miaka mia nne na thelathini.
Bwana anamwambia Musa:
Mimi ni YEHOVA, nami
nitawatoa ninyi mtoke chini ya mizigo ya
Wamisri, nami nitawaokoa na utumwa wao, nami nitawakomboa kwa mkono
ulionyoshwa, na kwa hukumu kubwa, nami nitawatwaeni kuwa watu wangu. (Kut. 6: 6-7). Na hivyo ndivyo Bwana
alivyofanya.
Hata leo hali iko
vilevile. Hakuna mtu anayetaka kuishi sawasawa na sheria ya Mungu. Kila mtu
anavutwa na hali ya dhambi iliyoko ndani yetu. Lakini unafika wakati ambapo mtu
anachoka, na kutokea ndani ya moyo wake anaanza kumlilia Mungu. Naye Bwana
anamimina neema ya wokovu juu yake.
Maandiko yanasema: Lakini Mungu, kwa kuwa ni mwingi wa rehema, kwa mapenzi
yake makuu aliyotupenda; hata wakati ule tulipokuwa wafu kwa sababu ya makosa
yetu; alituhuisha pamoja na Kristo; yaani, tumeokolewa
kwa neema. (Efe. 2:4-5).
Hakuna mtu anayeweza
kujisifia kuokoka. Ni neema ya Mungu tu. Bwana anasema: Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa. (Tito
2:11). Ukiwa dhambini kutoka humo si
jambo rahisi, ni kifungo kigumu mno!
Kuokoka, yaani
kumwamini Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wako binafsi ndio kutolewa kwenye utumwa
wa Farao mtesaji, yaani ibilisi.
KIPINDI CHA UTIMILIFU WA YOTE
Hiki ni kipindi ambacho tutakuwa katika miili ya utukufu, yaani ni baada
ya maisha haya ya duniani. Tutakuwa katika Yerusalemu mpya na hatutahitaji tena
imani maana kile tulichokuwa tukikiamini kitaonekana wazi na tutakiishi jinsi
kilivyo milele na milele!
Biblia inasema kwamba: Maana wakati wa sasa tunaona kwa kioo kwa jinsi ya fumbo;
wakati ule tutaona uso kwa uso; wakati wa sasa nafamu kwa sehemu; wakati ule
nitajua sana kama mimi nami ninavyojuliwa sana. (1 Kor. 13:12).
Hebu tuangalie baadhi ya vipengele ambavyo tumekuwa tunaviongelea kwenye vipindi viwili vya mwanzo hapo juu jinsi ambavyo vitakuwa katika kipindi cha utimilifu wa mambo yote.
Msamaha wa dhambi
Katika kipindi cha
kwanza mtu aliyetenda dhambi alitoa mnyama wa kafara ambaye alikufa kwa niaba
yake. Katika kipindi cha pili, tunatoa damu ya Yesu kwa imani. Hata hivyo,
katika kipindi cha ukamilifu, wale walio mbinguni hawatakuwa tena na kazi ya
kuomba msamaha maana kule hawatendi tena dhambi.
Maandiko yanasema
kuhusu Yerusalemu mpya: Na
ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge, wala yeye afanyaye
machukizo na uongo, bali wale walioandikwa katika kitabu cha uzima cha
Mwana-Kondoo. (Ufunuo 21:27).
Tuwapo hapa duniani tunao unyonge wa dhambi ndiyo maana Bwana anasema: mtakatifu na azidi
kutakaswa. (Ufu. 22:11). Wewe ni mtakatifu tayari kwa njia ya wokovu
ulio katika Kristo Yesu. Lakini, kutokana na kwamba bado uko duniani, utafanya
kosa hili na lile. Ndiyo maana Bwana anasema ‘mtakatifu na azidi’ kujitakasa.
Mavazi
Katika kipindi cha
kwanza haikuruhusiwa kuvaa mavazi halisi yenye rangi tofautitofauti.
Katika kipindi cha pili, mavazi ni wokovu. Hivyo, kuwa
na vazi la aina moja ni kusimama na wokovu halisi wa Yesu Kristo bila
kuuchanganya na mambo ya kidunia.
Hata hivyo, katika
kipindi cha utimilifu wa yote, mbinguni kuna mavazi halisi ya haki yaliyo ya
milele, ambayo yatakuwa safi siku zote; milele na milele.
Imeandikwa: Baada ya hayo nikaona, na tazama, mkutano mkubwa sana
ambao hapana mtu awezaye kuuhesabu, watu wa kila taifa, na kabila, na jamaa, na
lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi, na mbele za Mwana-Kondoo, wamevikwa mavazi meupe
... (Ufu. 7:9). Haya ni mavazi ambayo
yameoshwa kwa damu ya Mwana-Kondoo wa Mungu.
Kutembelewa na Bwana
Katika kipindi cha
kwanza, watu walifua mavazi yao halisi ya mwilini ndipo Bwana alikuja kusema
nao. Mavazi hayo yalifuliwa kwa maji halisi.
Katika kipindi cha
pili, kinachooshwa si mavazi halisi ya mwilini, bali ni dhambi katika mioyo
yetu. Dhambi hizo zinaoshwa kwa njia ya damu ya Yesu Kristo.
Katika kipindi cha
tatu, yaani cha utimilifu kwa yote, si tu kwamba hakutakuwa tena na haja ya
kuoshwa (maana wote watakuwa watakatifu milele), lakini pia hakutakuwa na kusema
kuwa kuna kutembelewa na Bwana, maana watakatifu watakuwa naye siku zote.
Imeandikwa: Nao watamwona uso wake, na jina lake litakuwa katika
vipaji vya nyuso zao. wala hapatakuwa na
usiku tena; wala hawana haja ya taa wala ya nuru ya jua; kwa kuwa Bwana Mungu
huwatia nuru, nao watatawala milele na milele. (Ufu. 22:4-5).
VIPINDI VITATU VYA SABATO
Baada ya kuangalia vipindi
vikuu vitatu vya uumbaji kuhusiana na mwanadamu kwa kirefu namna hiyo, hebu
tuangalie sasa kama sabato nayo inapita katika vipindi hivyo vitatu.
Kipindi cha
mfano
Kama ilivyo kwa mambo mengine,
sabato nayo ilianza na kipindi cha mfano. Hiki kilikuwa ni kipindi cha Agano la
Kale ambacho kilitekelezwa kwa kupitia watu kupumzika kimwili kabisa.
Hii haikuwa ni hali ambayo
Mungu alipanga iendelee hivyo hivyo siku zote, bali alikusudia tulione kusudi
lake lililo kuu zaidi kupitia kipindi hicho cha mfano.
Kupitia sabato Mungu alikuwa
anasema nasi juu ya kitu kingine bora zaidi. Si makusudi yake mawazo yetu
yaishie tu kwenye kupumzika kimwili, kujizuia kazi za kimwili, n.k. Ndiyo maana
anasema: Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula
au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato; mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo. (Kol. 2:16-17).
Kipindi cha
uhalisia wa kwanza
Hiki ni kipindi ambacho ni cha
kiimani zaidi. Kimsingi hiki ni kipindi ambacho kinaendelea hadi sasa. Huu ni wakati
wa kupumzika kazi za mwili za uovu, yaani kuacha dhambi na kuishi kwa
kumtegemea Kristo. Ni maisha ya imani.
Imeandikwa: Njoni kwangu ninyi nyote wenye kulemewa na mizigo nami nitawapumzisha. (Mt. 11.28), yaani, nitawapa ‘sabato’. Pia ndiyo maana ya andiko lisemalo: Kwa maana Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato.
(Mt. 12:8). Sabato iko kwake, si kwenye siku.
Ni maisha ya kujiachia
mikononi mwa Mungu ambaye yeye ndiye anayeshughulikia kila kitu katika maisha
yetu. Kazi yetu ni kuamini tu kuwa atafanya; naye hakika anafanya. Hilo ndilo
pumziko! Hiyo ndiyo raha! Hiyo ndiyo starehe! Hiyo ndiyo sabato!
Kipindi cha utimilifu wa yote
Hiki ni kipindi cha
maisha ya mbinguni. Huo utakuwa ni utimilifu wa yote kwa sababu, mara
tutakapoingia humo, tutakuwa tukitekeleza sabato halisi milele na milele.
SABATO SI SIKU
Upo ushahidi wa kutosha katika Biblia unaoonyesha kwamba sabato si siku
katika juma. Bwana anapoongelea kuhusu safari ya wana wa Israeli anasema:
Kwa hiyo nalichukizwa na kizazi hiki, nikasema,
Siku zote ni watu waliopotoka mioyo hawa ... hawataingia rahani mwangu. (Ebr. 3:10-11).
Pia imeandikwa: Maana ameinena siku ya saba
mahali fulani hivi, Mungu alistarehe siku ya
saba, akaziacha kazi zake zote; na hapa napo, Hawataingia rahani mwangu. (Ebr. 4:4-5).
Katika maandiko haya Mungu anasema kwamba, kutokana na kukasirishwa na
uasi wa wana wa Israeli kule jangwani, alimua kwamba hawataingia
kwenye raha aliyokuwa amewaandalia. Neno rahani
hapa, au kwa Kiingereza rest, ndilo hilohilo
sabato. Ndiyo maana hapo juu katika Ebr.
4:4-5, anahusisha siku ya saba na kuingia rahani.
Lakini hebu tujiulize maswali yafuatayo ili tuweze kupiga hatua zaidi.
- Je, Israeli walipokuwa jangwani kwani hawakuwa wakitunza sabato kama siku? Jibu ni ndiyo, waliitunza. Biblia inasema: Basi ikawa siku ya sita wakaokota kile chakula sehemu mara dufu, kila mtu pishi mbili; na wazee wote wa mkutano wakaenda na kumwambia Musa. Akawaambia, Ndilo neno alilonena BWANA,Kesho ni starehe takatifu, Sabato takatifu kwa BWANA ... (Kut. 16:22-23).
- Kama basi waliitunza sabato, iweje tena Mungu aseme, ‘Hawataingia rahani mwangu’? Kama ingekuwa ni kumwuliza Mungu, mtu ungesema, “Bwana, unasemaje hawataingia rahani mwako wakati kila siku ya saba wanapumzika?” Hii ni ishara ya wazi kwamba sabato hasa si kupumzika au kutofanya kazi kimwili katika siku ya saba. Sabato ni jambo jingine tofauti na siku ya saba. Iko sabato halisi ambayo siku ya saba na kupumzika kwake vilikuwa ni kivuli chake tu.
- Jambo jingine la kujiuliza ni kwamba, japo ni kweli kwamba wale ambao Mungu alisema hawataingia rahani mwake walifia wote jangwani, lakini walikuwapo wengine wengi walioingia, yaani watoto wao. Sasa je, hao walioingia waliipata hiyo raha (sabato)?
Mtu anaweza kujibu, Ndiyo, maana sote tunajua
kuwa hata wakati alipokuja Bwana Yesu, alikuwa akifundisha mara nyingi kwenye
masinagogi 'siku ya sabato'. Kwa hiyo, mtu anaweza kusema, ‘Ndiyo, waliingia
kwenye raha au kwenye sabato.’
Lakini Mungu ambaye ndiye mwenye usemi wa mwisho
juu ya mambo yake mwenyewe anasema:
Basi kwa kuwa neno hili
limebaki kwamba wako watu watakaoingia humo, na wale waliohubiriwa habari ile
zamani walikosa kuingia kwa sababu ya kuasi kwao, aweka tena siku fulani, akisema katika Daudi baada ya
muda mwingi namna hii, Leo; kama ilivyonenwa tangu zamani, Leo, kama mtaisikia sauti yake,
msifanye migumu mioyo yenu. Maana kama Yoshua angaliwapa raha (yaani sabato),
asingaliinena siku nyingine baadaye. Basi imesalia raha ya
sabato kwa watu wa Mungu. (Ebr. 4:4-9).
Yaani, hawa watu licha ya kwamba kila mwisho wa
wiki walikuwa wakipumzika, bado Mungu anasema ‘walikosa kuingia.’ Lakini cha
kushangaza zaidi ni kwamba, kumbe hata siku yenyewe ilibadilishwa! Je, umeona
hayo maneno ‘aweka tena siku fulani’? Pia
hapo mwishoni nako anasema, ‘siku nyingine baadaye’!!
Hebu jiulize, inakuwaje siku nyingine wakati
tumesema kwamba hadi Yesu anakuja watu hao walikuwa wakipumzika kila mwisho wa
wiki?
Jibu ni wazi kwamba ‘siku nyingine’ hapa
haimaanishi siku katika juma – maana hiyo haikuwahi kuachwa! Kwa hiyo, ni wazi
kwamba, hii ni ‘siku ya sabato’ tofauti na ile iliyojulikana na kufuatwa tangu
siku za Musa!
HOJA YA SABATO KUTOKA KINYWANI MWA MUNGU
Iko hoja kwamba sabato
ni amri ya muhimu sana kwa sababu ilitoka moja kwa moja kinywani mwa Mungu
tofauti na amri zingine ambazo zililetwa kupitia manabii au mitume.
Hoja hii haina uzito
kwa sababu kuu mbili:
1.
Biblia kwa ujumla wake
ni Neno la Mungu ambalo limetoka kinywani mwake lote. Na maandiko yako wazi
kwamba: Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa
kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa
kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa, apate
kutenda kila tendo jema. (2 Tim. 3:16-17).
Na kimsingi maandiko haya, ukisoma kwenye Biblia ya Kiingereza, hayasemi
“Kila andiko lenye pumzi ya Mungu”. Badala yake yanasema: All Scripture is God-breathed (NIV); au All scripture is given by inspiration of God (KJV). Hii ina maana kwamba: Maandiko
yote yametokana na pumzi ya Mungu.
Kwa hiyo, hakuna mantiki kusema kwamba
andiko hili lina maana zaidi kuliko lile kwa kuwa hili alitamka Mungu mwenyewe.
Yote yana nguvu ileile; yote yametoka kwa Mungu yuleyule.
2.
Sababu ya pili ni kuwa, Bwana Yesu alisema: Awapokeaye
ninyi, anipokea mimi; naye anipokeaye mimi, ampokea yeye aliyenituma.
(Mt. 10:40).
Maana yake ni kuwa Musa au nabii yeyote hakusema
kwa niaba yake au kwa nafsi yake mwenyewe. Maneno waliyoyasema na kuyaandika
hayakuwa yao.
Ukimpokea Musa au Paulo na maneno yake, unakuwa
umempokea Kristo, na hatimaye Mungu Baba
mwenyewe.
Kwa hiyo, si sahihi kudhani kuwa maneno ya Musa
au ya Paulo ni yake yeye, na kwamba yana uzito wa chini kuliko yale yaliyotoka
kinywani mwa Mungu moja kwa moja kuhusiana na sabato.
KWA NINI YESU ‘ALIVUNJA’ SABATO?
Hebu tuangalie mifano kadhaa hapa:
Mfano wa 1
Yesu alipomponya mtu ambaye alikuwa hawezi kwa muda wa miaka 38,
alimwambia ‘jitwike godoro lako, uende.’ (Yoh.
58). Hii ilikuwa ni siku ya sabato.
Lakini tunaona kwamba Wayahudi walipomwona mtu huyo walimwambia, Leo ni sabato, wala si halali kwako kujitwika godoro.
(Yoh. 5:10). Bila shaka walisema hivi kwa kuwa walifahamu fika jinsi sabato
inavyotakiwa kutunzwa.
Hii ni kusema kwamba, kwa kadiri ya kanuni za utekelezaji wa sabato,
hili lilikuwa ni kosa. Sasa, swali ni kwamba, kwa nini Yesu alivunja sabato kwa
kumruhusu yule mtu abebe godoro?
Mfano wa 2
Wayahudi walipomkasirikia Yesu kwa sababu ya kumruhusu yule mtu kubeba
godoro siku ya sabato, Bwana Yesu aliwajibu kwamba: Baba
yangu anatenda kazi hata sasa, nami ninatenda kazi. (Yoh. 5:17). Haya ni
maneno ya ajabu sana. Wewe uliye Mungu ulituambia kwamba siku ya sabato
tusifanye kazi bali tupumzike; tumemwona mtu anafanya kazi ya kubeba godoro,
tumekuja kwako, lakini wewe si tu kwamba hukumkemea, bali unasema tena kwamba
na wewe unafanya kazi hata sasa (siku ya sabato)!
Kama sabato hasa ni kuacha kufanya kazi, iweje tena Yesu atamke jambo
ambalo ni wazi kabisa linavunja sheria aliyoiweka mwenyewe ya kutofanya kazi;
yaani aseme kuwa hata sasa yeye anafanya kazi?
Mfano wa 3
Siku moja Yesu aliingia kwenye sinagogi ambamo mlikuwamo mwanamke mwenye
pepo wa udhaifu. Yesu alimponya mama yule.
Hata hivyo, Biblia inasema: Basi mkuu wa
sinagogi alikasirika kwa sababu Yesu amemponya mtu siku ya sabato, akajibu,
akawaambia mkutano, Kuna siku sita zifaazo kufanya kazi, basi njoni mponywe
katika siku hizo, wala si katika siku ya sabato. (Lk. 13:14).
Maneno haya ya mkuu wa sinagogi yanatuonyesha kwamba, jambo alilofanya
Yesu lilikuwa ni kuvunja sabato. Swali ni lilelile, kwa nini Yesu alivunja
sabato?
Tunafahamu kuwa maandiko yanasema kwamba kuvunja sabato ni dhambi, tena
ambayo iliadhibiwa vikali sana. Na katika mifano hiyo hapo juu, tunaona kwamba
Yesu alivunja sabato kwa kufanya mambo ambayo jamii nzima ilikuwa haiyafanyi
siku ya sabato. Kwa harakaharaka, mtu anaweza kusema kwamba, Yesu alitenda
dhambi.
Lakini wakati huohuo, maandiko yanasema kwamba, katika kuishi kwake kote
hapa duniani, Bwana Yesu hakuwahi kutenda dhambi. (Ebr. 4:15).
Swali la kujiuliza hapa ni kwamba, iweje uvunje sabato, jambo ambalo ni
dhambi, halafu uhesabiwe kuwa hujatenda dhambi? Pili, iweje wewe ambaye ndiye
ulisema watu wapumzike siku ya sabato, ndio uwe wa kufanya kinyume na agizo
lako mwenyewe? (Maana Yesu ndiye Mungu aliyeagiza sheria ya sabato ifuatwe).
Iweje hapa yeye ndiye awe wa kuivunja?
Hapa jibu ni moja tu. Sabato si siku katika
juma! Kama sabato ingekuwa ni siku katika juma, Bwana Yesu angekuwa na
hatia ya kuvunja sabato, maana ni wazi kuwa alitenda mambo ambayo ni kinyume na
sabato kama siku!
Lakini kwa sababu sabato ina maana tofauti na siku, ndiyo maana
aliruhusu mtu yule abebe godoro siku sabato; ndiyo maana hakuwa na tatizo na
uponyaji siku ya sabato; ndiyo maana hakuwa na tatizo na wanafunzi kukwanyua
masuke mashambani!
MAANA HALISI YA SABATO
Sabato ni kitu gani basi kama si siku katika juma?
Maandiko yanasema: Basi imesalia raha ya
sabato kwa watu wa Mungu. Kwa maana yeye (yaani mwanadamu) aliyeingia katika raha yake (yaani raha ya Mungu) amestarehe mwenyewe katika
kazi yake, kama vile Mungu alivyostarehe
katika kazi zake. (Ebr. 4:10).
Aha! Kumbe sabato si kupumzisha damu na nyama katika siku mojawapo ya
wiki; si kujizuia kukoka moto, kubeba mzigo au kusafiri mwendo mrefu kimwili!
Sabato ni kitendo au hali ya mwanadamu kuacha ‘kazi
zake’ kama Mungu alivyoacha zake. Mungu ni mtakatifu, kwa hiyo kazi zake
ni takatifu na kamilifu. Mwanadamu ni mpungufu, kwa hiyo kazi zake ni uasi,
yaani dhambi. Hizo ndizo anazotakiwa kupumzika kwazo, yaani kuziacha na
kumgeukia Mungu.
Ili kuweza kuingia rahani mwa Bwana, yaani kwenye sabato yake, Bwana
akasema: Njoni kwangu ninyi nyote wenye kulemewa
na mizigo nami nitawapumzisha. (Matayo 11.28).
Pumziko au raha au
sabato hiyo si kupumzisha damu na nyama katika siku fulani ya wiki, bali Bwana
anasema: Nanyi mtapata raha (sabato) nafsini mwenu. (Mt. 11:29) – si kwenye miili yenu!
Na pale unapowezeshwa
kuacha dhambi na ukamgeukia Bwana na kumfuata maishani mwako, ndipo raha au
sabato hiyo inapokuwa ni kwa faida au kwa ajili yako, yaani sabato inakuwa ni
kwa ajili ya mwanadamu. Lakini ukishikilia kutunza siku, hapo wewe ni kwa ajili
ya siku (sabato) na wala si sabato kwa ajili yako.
Kwa hiyo, sabato si
siku bali ni pumziko, raha na starehe ndani ya Kristo katika Roho Mtakatifu.
Imeandikwa: Maana ufalme wa Mungu si kula wala
kunywa, bali ni haki na amani na furaha katika Roho Mtakatifu. (Rum. 14:17).
HITIMISHO
Tumalizie kwa kujiuliza
swali hili. Je, kuabudu siku ya sabato au jumamosi ni vibaya?
Yapo mambo mawili ya
kutofautisha hapa. Kuna kushika siku kama siku tu; na kushika siku kama sehemu
ya utekelezaji wa sheria.
Ukishika siku kama
siku tu, unaweza kumwabudu Mungu katika siku yoyote upendayo maana siku zote ni
sawa tu.
Lakini ukishika siku
kama sheria, hutaweza kuabudu katika siku yoyote, maana sheria ina siku yake
maalumu.
Kuabudu katika siku ya
sabato (jumamosi) kama siku tu haina tatizo hata kidogo. Lakini kuabudu katika siku hiyo kama sheria kunaweza kuwa na
maswali.
Tumeshaona kwa
ushahidi mwingi kwamba, sabato ilikuwa ni kivuli au mfano au taswira ya kitu
kingine.
Unapopita barabarani,
utaona vibao vinavyotaja majina ya sehemu na umbali wake. Mathali unaweza
kuona: ARUSHA, KM 350.
Kama wewe utaamua
kushusha mizigo na kukaa kwenye kibao hicho kisa tu kimeandikwa Arusha ambako
ndiko ulikokuwa unaenda, basi hapo liko tatizo.
Kibao ni ishara tu ya
hiyo Arusha. Lakini iko Arusha yenyewe halisi. Kazi ya kibao ni kukuelekeza
kwenye lengo au kusudi halisi la safari. Chenyewe si kusudi lenyewe.
Sabato iliwekwa ili
iwe ni kibao cha kutuelekeza kwenye kusudi. Sasa wewe ukiing’ang’ania yenyewe
ukaacha kusudi, basi hapo ndipo ilipo shida.Na kama utafika kwenye
kusudi lenyewe, je, utang’ang’ania kibao cha nini tena?
Jambo la msingi ni
kuwa, sabato au pumziko halisi ni kuwa ndani ya Yesu, yaani kuokoka. Ukishaingia
ndani ya Yesu, haijalishi tena endapo utamwabudu siku ya kwanza, ya pili au ya
mwisho ya juma.
Biblia inasema: Mtu mmoja afanya tofauti kati ya siku na siku, mwingine
aona kuwa siku zote kuwa sawasawa. Kila mtu na athibitike katika akili zake
mwenyewe. Yeye aadhimishaye siku,
huiadhimisha kwa Bwana; naye alaye, hula kwa Bwana, kwa maana amshukuru Mungu;
tena asiyekula, hali kwa Bwana, naye pia amshukuru Mungu. (Rum. 14:5-6).
Tena imeandikwa: Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji,
au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato; mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo. (Kol. 2:16-17).
Vilevile imeandikwa: Bali sasa mkiisha kumjua Mungu, au zaidi kujulikana na
Mungu, kwa nini kuyarejea tena mafundisho ya
kwanza yaliyo manyonge, yenye upungufu,
ambayo mnataka kuyatumikia tena? Mnashika
siku, na miezi, na nyakati, na miaka.
Nawachelea, isiwe labda nimejitaabisha bure kwa ajili yenu. (Gal.
4:9-11).
Je, umeokoka? Kama
jibu ni ndiyo na unapenda kumwabudu Bwana wa sabato (pumziko) siku ya jumamosi,
basi songa mbele katika hilo, maana siku kama siku haikuongezei wala
kukupunguzia chochote.
Je, hujaokoka? Kama
jibu ni ndiyo, nasikitika kusema kwamba kushika kwako siku hakutakusaidia,
maana hapo hakuna tofauti na kung’ang’ania mfano au kibao na kuacha jambo
lenyewe ambalo hasa ndilo lililolengwa na kibao au mfano huo.
Mtu akiwa mwizi, wizi
wake hautoki kwa sababu ameabudu katika siku fulani ya juma. Na mtu mtakatifu,
utakatifu wake hauji kutokana na kuabudu katika siku fulani. Utakatifu unatoka
kwa Bwana wa sabato, Yesu Kristo mwenyewe.
Umeona mwenyewe hapo
juu kwamba Mungu anaita ‘kushika siku’ kuwa ni ‘mafundisho ya kwanza yaliyo
manyonge!’
Achana na mambo ya
kimwili maana wakati wake ulishapita! Bwana Yesu alisema
wazi: Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo
waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta
watu kama hao wamwabudu. Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu
katika roho na kweli. (Yoh. 4:23-24).
Si katika mwili!!
Asante sana mtumishi wa Mungu nimebarikiwa sana na neno hili.Mungu akutangulie uzidi kusonga mbele katika kuujenga mwili wa Kristo (Baba wa sabato)
ReplyDeleteAmina ndugu. Ubarikiwe na Bwana pia.
ReplyDeleteGODFRAY -TANZANIA,
ReplyDeleteMungu akubariki mtumishi. kwa kweli somo hili linafungua kwa mapana na marefu. naamini linamtoa mtu katika mgando wa kiakili na kumfyatua kuelekea kwenye ukombozi halisi, kama Paulo mwenyewe alivyookolewa. Mungu akubariki.
Amen, Godfray. Bwana Yesu akubariki nawe pia. Ashukuriwe Bwana kama umeweza kupokea kitu kutoka kwake kupitia somo hili.
Deletekuna haja gan ya kutafuta siku nyingine ili upumzike ile hali siku ya jumamosi aliyopumzika mungu ingali ipo? si bora tuendelee kupumzika ile ile cku kulko kujijengea siku nyngne. #Kireri
ReplyDeleteshalom Kireri.
DeleteMimi nionavyo, lengo wala halitakiwi kuwa SIKU. Lengo letu ni Bwana wa Sabato mwenyewe. Yaani ukimpata huyo, suala la siku SI KIPAUMBELE. Yaani, uitafute au usiitafute hiyo siku - haijalishi. Suala ni kwamba nimepeleka mizigo yangu kwa Yesu kama alivyotoa mwito? yaani nimeokolewa?
Kama nimefanya hivyo, na nikaendelea kudumu katika uongozi wa Roho wake, tayari niko ndani ya sabato.
Hapo haijalishi jina la siku halisi ninayoabudu - iwe jumatatu, jumamosi au jumapili au kila siku - haijalishi.
Kwa hiyo, suala kwa kweli, SIO KUTAFUTA SIKU NYINGINE au KUTOTAFUTA.
kuna haja gan ya kutafuta siku nyingine ili upumzike ile hali siku ya jumamosi aliyopumzika mungu ingali ipo? si bora tuendelee kupumzika ile ile cku kulko kujijengea siku nyngne. #Kireri
ReplyDeleteNimeguswa sana na ufafanuzi wako wa kina, hasa kwa ushahidi wa maandiko matakatifu. Naomba Mungu azidi kukutumia ili wanadamu wa leo tuachane na mafundisho ya AWALI ya ulimwengu ambayo yanafundisha si kwa jinsi ya KRISTO.........(Wakolosai 2:8)
ReplyDeleteAmen. Bwana akubariki mpendwa katika Kristo.
DeleteWewe Muongo. Hujafafanua vyema maandiko hayo. Sabato ya Siku ya Saba ni agizo la Bwana Mungu kwaajili ya Watu wake wote. Kutoka 20:8-11 "lakini siku ya saba ni Sabato ya Bwana Mungu wako" Biblia haijasema ni Sabato ya Wayahudi. Pia Hata yesu alivyokuja aliitunza Sabato, baada ya Kupaa Mitume waliendelea kuitunza. Kanisa la RC ndio lilibadili Agizo la Mungu takriban miaka 300s baada ya kristo kipindi cha Mfalme Costantio, Rejea historia.
ReplyDeleteYesu aliitunza vipi wakati walimtuhumu kila siku kuwa anavunja sabato. Kwa mfano alimwambia yule mtu aliyekuwa kilema kwa miaka 38 abebe godoro siku ya sabato. Kisha Biblia inasema-------------(Yoh 5:10) Kwa sababu hiyo Wayahudi wakamwambia yule aliyeponywa, LEO NI SABATO, WALA SI HALALI KWAKO KUJITWIKA GODORO.
DeleteKwa nini Yesu alifanya jambo kama hilo?
nimesoma nusu tu nitamalizia,ufafanuzi ni mzuri,Agano la kale limetusaidia kutuleta kwenye agano jipya.kama kitu halisi nakiona kwanini niendelee kukumbatia kivuli?
ReplyDeleteMtumishi kafafanua vizuri kwa uelewa wake mdogo.maana hajafafaunua kuwa kuna aina ngapiza sabato.je sabato ya kivuli ndio ipo kwenye amri kumi? Je sabato ya miaka saba ni ipi hapo?usichanganye mambo hapo,kuwa muwazi sio kutafuta kichaka au uchochoro wa kuhalalisha ujanja wa shetani wa kuoanisha hoja zifanane na za Mungu
ReplyDeleteThis comment has been removed by the author.
DeleteMuongooo
ReplyDeleteAfu Mungu anawaona soma warumi 7:12-13
ReplyDeleteAfu sabato ni kufanya kazi ya Mungu na sio kazi ndo maana yesu alikua anafanya kazi ya Baba yake yaani kuponya wagonjwa.... afu mzigo cio nyie mnavyo tafasiri bali siku iyo usije ukabeba dhambi yeyoyote ambao ukawa mzigo rohoni mwako
ReplyDeleteNi wazi unesoma heading tu lakini hujui nini kimeandikwa humo
DeleteNa ndio maana akamwambia jitwike godoro na uwende kwani kubeba godoro ni dhambi... niwaulize nyie au soma Marko 3:1-7 Yesu anauliza ni halali kutenda mema au mabaya katika siku ya sabato.... yaani kuponya au kuuwa na mimi nawauliza kipi ni halali kufanya... yesu alikuja kuwaonyesha namna sabato inavyo fanywa... alafu sabato ni amri ya Mungu leo mnajiita wakristo mmeiacha na Mungu anawaona...
ReplyDeleteInavyoonekana unesoma kichwa cha habari tu hata hujui nini kineandikwa
ReplyDelete