Saturday, July 19, 2014

Kubatizwa kwa Moto Uwakao - 3


Huu ni ushuhuda unaotokana na kitabu kinachojulikana kama Baptized by Blazing Fire, Devine Expose of Heaven and Hell kilichoandikwa na Mchungaji Yong-Doo Kim wa Korea. Ni ushuhuda mrefu ambao utakupa mafundisho, maonyo, utakutia moyo na kukuimarisha katika safari yetu ya kuelekea kwa Baba, Mbinguni.


====  SIKU YA 8  ====

Pastor Kim, Yong-Doo 
Ilishapita kama wiki nzima tangu tuazimie kufanya maombi. Mapambano yetu kwenye ulimwengu wa roho yaliongezeka, na majaribu yetu ya kimwili nayo yaliendelea kila siku. Shujaa wa maombi mmoja baada ya mwingine alifunguliwa macho ya rohoni na alijazwa kwa Roho Mtakatifu. Nguvu za kipepo zilifanya mashambulizi makubwa. Hali mbalimbali za kibinafsi ziliinuka, huku zikijaribu hasira zetu. Siku ya kwanza, tairi moja la gari langu lilipasuka. Siku iliyofuata, tairi la mbele nalo lilipasuka. Hali ile ilinichanganya sana. Hata hivyo, sikumlalamikia Mungu, badala yake nilipaza sauti  "Haleluya" kwa moyo wa shukrani. Siku iliyofuata gari la breakdown liliondoka na gari langu. Jambo hili kwa kweli kidogo linitoe kwenye mstari sahihi. Lakini mke wangu pamoja na washirika wenzangu walinikumbusha wakisema,  "Mchungaji, ni lazima uvumilie katika hili." Baadaye, kuna mtu alivunja taa za gari, na siku iliyofuata, mtu mwingine alilikwaruza kwa kitu kikali.

Ibada iliendelea kadiri Roho Mtakatifu alivyotuongoza. Hadi wakati huo, kichwa cha habari  kwenye ubao wa matangazo wa kanisa kilisomeka: "Saa ya Mazingira Yaliyojaa Uwepo wa Roho Mtakatifu," lakini kilibadilishwa na kuwa, "Ibada Halisi Inayoongozwa na Roho Mtakatifu." Taratibu zote za kuabudu, kuomba, mahubiri na matoleo ziliondolewa, tukawa tunafuata mwongozo wa Roho Mtakatifu – Yeye ndiye aongoze namna tutakavyoabudu, tutakavyoomba, na mahubiri yatakavyotolewa. Mahubiri yangeweza kuendelea maana hatukuwa na haraka ya kumaliza ndani ya muda maalum. 

Kila shujaa wa maombi alikuwa anaona uwepo wa Yesu wakati wa maombi ya mkesha wa usiku kucha. Kwa hiyo, walikuwa hawajisikii kuchoka japokuwa ibada iliendelea hadi asubuhi inayofuata. Saa zote tulikuwa macho na hakukuwa na muda wa kuzubaa maana mapepo yanashambulia bila kupumzika. 

Kim, Joo-Eun 
Nilikuwa naomba kwa lugha pale Yesu alipokuja kwangu na kusema, "Joo-Eun, nakupenda." Akaendelea kusema, "Joo-Eun, omba kwa bidii, nami nitakwenda nawe hadi Mbinguni. Omba bila kukoma. Nitakuonyesha Mbingu. Je, unanielewa?"

Baadaye usiku ule, mashetani yalitokea kwa makundi. Mojawapo lilionekana likipigapiga mabawa yake kama popo, huku likiwa na pembe ndogo kwenye vichwa na macho yake kama paka. Shetani hilo liliruka kuelekea kwangu ilhali limepanua kinywa, huku ute unaonata ukimwagika toka mdomoni mwake. Macho yake yalikuwa mekundu sana. Nikasema kwa sauti,  "Katika Jina la Yesu, nakuamuru ewe pepo mchafu, ondoka kwangu!" Niliposema hivyo, lilitoweka. Baada ya muda mfupi, pepo jingine lenye uso wa buluu na macho madogo likawa linanijia. Nikapiga kelele, "Kwa jina la Yesu, ondoka kwangu." Lakini shetani lile wala halikushituka! Badala yake liliendelea tu kunikodolea macho. Nilipaza sauti kwa nguvu zaidi na nikajawa na hofu ndipo Dada Baek, Bong-Nyo, ambaye alikuwa amekaa pembeni yangu, aliungana nami kupaza sauti, "Kwa Jina la Yesu, ondoka kwetu!" Hapo tu ndipo lilipokimbia. 

Niliendelea na maombi hatimaye joka kubwa jekundu likawa linaruka kuelekea kwangu. Macho yake yalikuwa ya kijani. Kichwani kulikuwa na pembe ndefu, kali. Moshi ulikuwa unatoka puani mwake. Lilikuja kwangu kwa nguvu kama vile lilitaka kunimeza hai. Sikutetereka! Nilisimama kwa ujasiri, huku nikiomba kwa bidii kwa lugha kwa Jina la Yesu. Ghafla likatoweka. Nilijisikia vizuri sana. Sikuwa najua uwezo uliomo ndani ya Jina la Yesu kabla ya hapo. Safari nyingine, pepo baya, la kutisha lenye kichwa ambacho ni fuvu lilicheka mbele ya uso wangu kana kwamba lilikuwa likinidhihaki. Safari hii tena niliomba kwa lugha huku nikitumia Jina la Yesu kulifukuza.

Baadaye, nilikuwa nawaza juu ya Yesu akiwa amening’inia msalabani, ndipo alinitokea, huku akinitia moyo, akisema, "Joo-Eun, hebu zaidi kidogo, omba kwa muda zaidi kidogo tena."

====  SIKU YA 9  ====

Lee, Haak-Sung 
Mashambulizi makali ya mashetani yalianza. Joka jekundu ambalo Joo-Eun alinisimulia lilinitokea na mimi pia. Ukubwa wake uliniogopesha. Lilikuwa na macho ya kijani, na moshi mweusi ulitoka puani mwake. Meno yake yalikuwa makali kama pembe; kucha zake zimechongoka na mkia wake ulikuwa mrefu sana. Hata hivyo, niliomba kwa bidii, nalo likatoweka! Muda mfupi baadaye, shetani la kike likatokea huku likipiga kelele, "Hee-hee-hee!" Mdomo wake ulijaa meno kama ya mbweha. Kisha nikaanza kusikia sauti ya mabuti ya jeshi vikitembea nyuma yangu. Na mara vivuli vyeusi vikanifunika. Makelele ya mashetani na sauti ya mabuti vilinitisha, kwa hiyo nikaanza kulia, "Bwana, nisaidie! Tafadhali nisaidie!" Nilikuwa namwita Bwana ndipo Yesu akatokea kwenye nuru kali. Mapepo yakatoweka mara Yesu alipotokea! Yesu alinishika mkono, nami nikaimba na kucheza pamoja naye.

Baadaye, Yesu aliniita, "Mpendwa wangu, Haak-Sung, unataka kutembelea Mbinguni?" Mara aliponishika mkono, mwili wangu ukawa umevikwa vazi jeupe. Nilielea hewani, na tukawa tunapaa kuelekea kwa malaika wa Mbinguni waliokuwa wakitusubiri. Sikuweza kuinua kichwa changu sawasawa kutokana na ukali wa nuru. Mbingu inaweza kuelezwa kama sehemu iliyojaa nyota. Nilidhani ninaota, lakini Mbingu ilikuwa ni halisi kuliko hata dunia. Mbingu yote ilikuwa imefunikwa kwa dhahabu. Hakukuwa na sehemu ambayo haitoi nuru. Malaika na watakatifu wengi walikuwa wakipita huku na kule, na malaika walinisalimu kwa furaha. Nikasema,  "Yesu, nataka kujua kama kuna nyumba yangu hapa." Kisha Yesu akatuma malaika wawili wanisindikize hadi iliko nyumba yangu. Nyumba yangu haikuwa kubwa, lakini kuta zake zilikuwa za matofali ya dhahabu! Niliona bustani kubwa sana ya maua ambayo ilijaa maua ya aina mbalimbali. Nilitamani kurukia humo ndani na kuanza kubiringika. Kutokana na harufu nzuri ya maua, nilijawa na furaha na nikarukaruka kama mtoto.

Lee, Yoo-Kyung 
Nilikuwa naomba kwa lugha ndipo shetani likanijia. Kulikuwa kovu la X la mishono kwenye jicho lake la kulia na la kushoto lilionekana kama doa jeusi. Pepo hilo lilionekana kama ni la kiume. Nikapaza sauti,  "Kwa Jina la Yesu, toweka!" Baadaye, lilikuja pepo ambalo lilikuwa na mabawa kama ya popo. "Nilikukosea nini hadi unighasi kiasi hiki?" lilinisihi, "Hey, sitarudi tena kama utaniruhusu niingie ndani yako na kutoka mara moja tu." Nikasema, "Ewe pepo mchafu; kwa Jina la Yesu, ondoka mbele yangu!" Niliposema hivyo, likatoweka. Baada ya hapo, nilipambana na mapepo mengine matatu au manne hivi tofauti. Kisha ghafla, nilihisi harufu nzuri imenizunguka. Yesu alikuja na kuniita jina langu. "Mpendwa wangu, Yoo-Kyung, nipe mkono wako." Kwa hiyo, nikanyoosha mkono wangu na Yesu akanishika mikono yangu kwa mikono yake kwa upole. Nikasema, "Yesu, bega langu linauma sana," na Yesu akaweka mkono wake juu ya mabega yangu, na maumivu yakaondoka. 

Yesu alimpa kila shujaa wa maombi jina la utani. Ilikuwa ni furaha sana. Yesu aliniita mimi "Speckle face" (Usomadoa) kwa sababu uso wangu una madoadoa mengi. Joo-Eun alipewa jina la "Sesame" au "Freckles" (Mabaka) kwa sababu amefunikwa na mabakamabaka.

Baadaye, Yesu alinifariji kwa sababu ya maumivu yote niliyopitia kutokana na kuwaona ndugu zangu kule kuzimu. Alisema, "Mpendwa wangu, Yoo-Kyung, ulilia sana baada ya kukutana na bibi yako kule kuzimu." Bwana akanikumbusha, "Yoo-Kyung, nitakapokupeleka kutembelea kuzimu, usitoe msaada kwa mtu yeyote, hata kama ni bibi yako mpendwa. Usije kujaribu kushika mkono wa mtu yeyote kule."

Baadaye Yesu alinipeleka tena kutembelea kuzimu. Safari hii nilimwona baba yangu na mdogo wangu wa kiume wa miaka 26. Huyu alijiua kwa kunywa sumu. Wote walikuwa uchi. Macho yao yaligongana na yangu.  "Dada yangu mkubwa, Bong-Nyo, umefikaje huku? Huku si mahali pako. Dada, mwombe Bwana. Fanya haraka umwombe anitoe humu. Nisaidie niende Mbinguni. Sasa!" Kutokana na kilio na kusihi kwake, kaka yangu alitupwa kwenye mtungi wa kitu kama maji yaliyokuwa yakichemka. Sikusikia yakichemka.

Tangu nikiwa mdogo, baba yangu alinidharau, na chuki hiyo iliongezeka mwaka hadi mwaka. Tulipoonana kuzimu, baba yangu akasema, "Bong-Nyo, nilipokuwa hai, nilitenda mambo mengi mabaya ambayo nayajutia sasa. Nadhani ndiyo sababu niko hapa sasa. Ninatubu sana kwa hayo yote." Nikamwuliza Yesu, "Bwana, kwa nini baba yangu yuko hapa?" Akasema, "Baba yako ametenda dhambi sana. Hakuniamini Mimi, lakini pia alikuwa akicheza kamari kila siku bila kukosa hata siku moja. Mama yako alipokuwa ana ujauzito wa mdogo wako huku bado mwezi mmoja ajifungue akiwa mwenye afya na kwa njia ya kawaida, baba yako aliondoa uhai ule wa thamani kwa kumpiga mama yako ngumi tumboni. Mtoto  aliumia tumboni na kufa. Baba yako pia alikulazimisha wewe kuzika kitoto kikiwa bado hai mlimani. Kwani huyajui hayo? Baada ya kutenda dhambi hiyo mbaya, hakuwahi kukiri wala kutubu. Ni sahihi yeye kuwapo hapa kuzimu!" Sauti ya Yesu ilijaa ghadhabu. 

Niliona sura nyingine ninayoifahamu. Ilikuwa ya mama mkwe wa mdogo wangu wa kike. Aliomba kabisa kwamba nitakaporudi duniani, nimwambie mkwe wake na familia yake wamwamini Yesu Kristo, waombe kwa bidii, ili kwamba wote waende Mbinguni. Akasema, "Kwa kweli sikujua kuwa kuna kuzimu, au jinsi kulivyo kwa moto na kubaya hapa. Nilikuwa ni shemasi kanisani, lakini sikuwa nikitumika kanisani. Nilikuwa na miungu mingi duniani, nayo ilininajisi. Ndiyo maana niko hapa. Najuta sana," alisema kwa sauti.  Kisha alitupwa kwenye yale maji ya moto vilevile.

Niliogopa na kuhuzunika sana. Sikuweza kustahimili tena. Uso wangu ulijaa machozi, na harufu ya kuungua ilifanya kupumua kwangu kuwe kwa shida. Yesu naye aliendelea kutoa machozi. Bwana alikuwa na somo la muhimu kwa ajili yangu: "Una nafasi moja tu Mbinguni; na hiyo ni wakati ukiwa bado hai kimwili." Sikuwa na cha kufanya zaidi ya kuwaangalia wakiteseka. Moto wa kuzimu hauwezi kulinganishwa na moto wa duniani.

Lee, Yoo-Kyung 
Baada ya kuomba hadi saa 1:30 asubuhi, nilirudi nyumbani nikitumaini kulala kidogo, lakini nilihisi uwepo fulani chumbani. Nilifungua macho yangu, lakini sikuona chochote. Nilipofunga tena macho yangu, “Yesu” alikuwa amekaa pembeni yangu. Hofu ya ghafla iliniingia. Niliomba kwa lugha kwa ujasiri. Ghafla, yule ambaye nilidhani ni Yesu aligeuka na kuwa pepo jeusi, likiwa na macho ya buluu nyeusi! Pepo lile lilizungusha macho yake, na huku limeinua mkono wake, lilijaribu kusema Sala ya Bwana. Kisha lilipaza sauti, "Mapepo yote inukeni!" Niliogopa sana. Kwa sauti yenye amri nilisema, "Ewe shetani, kwa Jina la Yesu, ondoka!" Mara moja lile pepo lilitoweka.  

ITAENDELEA ...

No comments:

Post a Comment