Huu
ni ushuhuda unaotokana na kitabu kinachojulikana kama Baptized by Blazing Fire,
Devine Expose of Heaven and Hell kilichoandikwa na Mchungaji Yong-Doo Kim wa
Korea. Ni ushuhuda mrefu ambao utakupa mafundisho, maonyo, utakutia moyo na
kukuimarisha katika safari yetu ya kuelekea kwa Baba, Mbinguni.
………………………………….
Kutokana na siku 30 za maombi mfululizo wakati wa usiku kwenye
kanisa dogo nchini Korea, waumini walipokea uamsho usio wa kawaida. Wakiwa wameinua
mikono yao juu, huku wakiomba usiku kucha, macho ya kiroho ya waumini hawa
yalikuwa wazi huku na waliona maono, uponyaji, vita vikali vya kiroho, na
kukutana na Yesu kwa jinsi ya ajabu. Huku macho yao yakiwa yamefunguliwa,
waliweza kuona wazi mapambano ya kiroho kwenye ulimwengu wa giza wakati wa
maombi. Walionyeshwa jinsi mashetani
yanavyojaribu kutuondolea uzingativu wetu, kututisha, na kutudanganya wakati
tunapofanya maombi. Kila aina ya hila ya kipepo iliyo kwenye ushuhuda huu
ilitumika dhidi yao ili kuwafanya waache kuomba. Walikabiliana na kupambana na
aina mbalimbali za majoka, wafalme wa kipepo, malaika wa uongo, makristo wa
uongo, mapepo yanayotaka kuhurumiwa, manyonya damu, mapepo yaliyojigeuza kuwa
wanawake warembo, n.k. Pia walipelekwa mbinguni na kuzimu mara nyingi na Yesu.
Ilifunuliwa kuwa maombezi ya usiku, (kukiwamo kunena kwa lugha), yana nguvu
sana, na japo ni magumu kuomba lakini yana matokeo makubwa.
Kuna vitabu vitano vinavyohusu shuhuda hizi. Ushuhuda huu
umefupishwa katika sehemu kadha wa kadha kuliko ulivyo kwenye kitabu chake:
KITABU CHA 1 – SEHEMU YA KWANZA
Yesu amwambia Mchungaji Kim:"Kuanzia sasa, chochote
ambacho wewe na washirika wako mtakiona au kukisikia, lazima mkiandike vizuri.
Kupitia hayo mambo, napenda makanisa yote Korea na duniani kote yaamke. Hii
ndiyo sababu uliletwa duniani. Wakati huu wa sasa, makanisa ya Korea na waumini
wake wanapingana na kile ambacho nimewaandalia. Wachungaji na washirika
wananiabudu kimazoea tu na wananijua kinadharia tu kutokana na yale wanayosoma
vitabuni.”
Mchungaji Kim:
Kanisa letu
linaamini katika nguvu za kunena kwa lugha, hivyo tuliweza kuomba muda mrefu,
kwa moyo, na kwa undani kabisa. Kunena kwa lugha pia kulitusaidia kutuliza
mawazo, hivyo tukapata nguvu kubwa sana zilizotufungua macho yetu ya kiroho.
Mchakato wa kufungua macho ya kiroho ya mtu si tu ni mgumu, bali pia ni lazima
mtu avuke vikwazo vingi. Kwa hiyo, kama wewe ni mzembe, hauzingatii na
haujajipanga sawasawa, utaingia gharama kubwa sana. Sasa, sisi pia tumejiandaa kikamilifu kutuma
mapigo na mashambulizi kwa kujiandaa vilivyo kwa njia ya kusifu, kujaza mioyo
yetu kwa Neno la Yesu, na kutafuta kwa bidii kwa kumlilia Bwana.
Watumishi wa
shetani huja mmojammoja. Kisha akishindwa, wanakuja wawili; kisha wanashambulia
wakiwa kumi, thelathini, hamsini, mia moja au zaidi. Kundi hilo husambaa kila
mara na kujikusanya tena ili kushambulia kulingana na hali ilivyo. Halafu mmoja
akifukuzwa kwa njia ya maombi, pepo hilo linaenda kwa mlengwa mwingine kwa njia
ya dhihaka, vishawishi, na wakati mwingine kwa maneno matamu ya kunong’oneza.
Mwishowe, wanapogundulika, wanakimbia haraka. Watumishi wa shetani huja kwetu
kwa namna na mwonekano tofautitofauti. Wakati mwingine wanajaribu kutunasa kwa
kujipa sura ya msanii maarufu, mtoto mchanga, yesu wa uongo, au kama malaika wa
nuru (2 Kor 11:14). Pia walituchanganya kabisa kwa kutokea kama binti yangu.
Tulipambana na kushinda, lakini pia tulipoteza mapambano mengi dhidi ya pepo
wachafu. Maumivu yalikuwa makali na tuligaragara chini mara nyingi.
Tulipokabiliana na mapepo ya kutisha yenye nguvu sana, yasiyowezekana, Bwana
wetu alimtuma Malaika Mkuu Gabrieli na malaika wengine ili kutusaidia. Bwana
wetu atupendaye anatuhakikishia kuwa hatuko peke yetu pale tunapoita malaika wa
mbinguni kuja kutusaidia tunapochoka kutokana na ugumu wa mapambano.
Yesu
alitukumbusha tujivike uwezo kwa kuomba kila siku (Marko 9:29). Ni muhimu
kuomba kila mara. Yesu anaelezea umuhimu wa maombi ya kukubaliana watu wawili
au zaidi (Mathayo 18:19). Nguvu za giza haziondoki kwa upole. Badala yake
zinaacha makovu na mateso yanaendelea.
Kaulimbiu
yetu ya mwaka 2005 ilikuwa "Pata uamsho kupitia kuomba," na tulianza
maombi yetu Januari 2. Maombi yaliendelea kwa siku thelathini. Tulikuwa
watu kumi. Siku ya kwanza, baada ya ibada ya Jumapili jioni, tulikuwa na
kipindi cha kuomba. Siku ya pili, (Januari 3), tuliona uwepo wa nguvu wa Roho
Mtakatifu. Maombi ya pamoja na pia maombi ya mmojammoja yalilipuka na kuendelea
hadi saa 1:30 asubuhi iliyofuata. Baada ya maombi kwisha, tulikaa kwenye duara
ili kusikia shuhuda na jinsi kukutana na Yesu kulivyokuwa. Muda wa maombi yetu
uliendelea kuwa mrefu zaidi na zaidi. Maombi ya Jumatano jioni yalianza saa
1:30 jioni na kwisha karibu saa 2:00 asubuhi iliyofuata. Alhamisi ilikuwa ni
saa 3:00 jioni hadi saa 4:00 asubuhi.
Mungu
aligeuza kabisa mawazo yetu. Kadiri tulivyozidi kuomba, ndivyo Bwana
alivyotupatia mambo ya kushangaza zaidi. Japokuwa maombi yetu yalidumu usiku
kucha, hakuna aliyelalamika. Badala yake, njaa ya chakula cha kiroho ilizidi
kuongezeka. Bwana alikuja kututembelea wakati tunaomba. Tulimwona kwa njia ya
macho yetu ya kiroho, lakini kuna wakati ambapo tulimwona kwa macho yetu ya
nyama kabisa!
Kadiri
watoto walivyoweza kumwona Yesu, kukosa utii kuliisha na wakawa watumishi
wanyenyekevu na waaminifu. Washirika wetu wawili, baada ya kuona Mbingu na
kuzimu, walilia sana na kupiga magoti na kuomba msamaha kwa mambo mabaya ambayo
walikuwa wamenifanyia mara nyingi. Licha ya kwamba kulikuwa na baridi kali sana
chini ya nyuzi sifuri, walitoka kwenda kushuhudia. Walitoka saa 10 mchana na
hawarudi hadi saa 2:30 usiku, huku mikono na miguu yao ikiwa imeganda kwa
baridi kali. Walitambua kuwa wanatakiwa kuwa na bidii kwa sababu waliona hazina
zao zikitunzwa mbinguni. Meena, msichana wa miaka 5, huomba kwa kunena kwa
lugha huku mikono yake imeinuliwa juu kwa saa 2 hadi 3! Kusanyiko letu
lilipokea karama za kiungu za unabii, kupambanua roho, kunena kwa lugha,
maarifa, hekima na imani ya kiungu.
Hakuna
maneno ya uongo kwenye kitabu hiki; bali ni mambo ambayo washirika waliyapitia
kibinafsi wakati wa mwito wa kufanya maombi.
Washirika wa
Kanisa la Bwana walioshiriki ni hawa: [Mchungaji Kim] [Kang,
Hyun-ja] [Kim, Joseph] [Kim, Joo-Eun] [Dada Baek,
Bong-Nyo] [Lee, Haak-Sung] [Lee, Yoo-Kyung] [Meena]
[Oh, Jong-Suk] [Shemasi Shin, Sung-Kyung] [Oh, Jung-Min]
==== SIKU YA 1 ==== [Ukiona hivi maana yake sehemu
hii imepunguzwa]
==== SIKU YA 2 ====
Mchungaji Kim:
Baada ya
Roho Mtakatifu kuingilia kwa namna ya kipekee, ilikuwa ni kama tumepata moto
wakati tukiomba. Japokuwa maombi yaliisha saa 1 asubuhi iliyofuata, tulijiona
kama vile hatukupata muda wa kutosha.
Lee, Yoo-Kyung:
Niliingiwa
na shauku kubwa sana na kwa nguvu zangu zote nilimwita Bwana, "Yesu,
Yesu, Yesu nakupenda. Naomba nikuone. Jidhihirishe kwangu." Nilipaza sauti
na kuomba kwa lugha kwa bidii. Karibu saa moja ilishapita ndipo mwanga mkali
uliwaka ghafla, na kuna mtu alikuwa amesimama katikati yake. Nilifungua macho
yangu na kupatwa na mshtuko, lakini sikuona chochote. Nilipofunga tena macho
yangu, niliweza kuona wazi, kwa hiyo nilibaki nimeyafunga. Yesu alisimama mbele
yangu huku amevaa vazi zuri linalong’aa.
"Yoo-Kyung,
nakupenda," Yesu alisema maneno haya, kisha alisogea karibu
yangu na kukaa mbele yangu. Sidhani kama nimewahi kuona mtu mzuri kama Yeye.
Nywele za Yesu zilikuwa za rangi ya dhahabu na alikuwa na macho mazuri,
makubwa. Alinipapasa nywele zangu taratibu na kusema, "Yoo-Kyung, nakupenda."
Nilianza kulia na moyo wangu uliyeyuka. "Nataka nikuonyeshe Mbingu ilivyo." Mara
tuliondoka. Kulikuwa na nuru kali sana kiasi kwamba sikuweza kufungua macho
yangu. Niliwaza, "Lazima hapa patakuwa ni Mbinguni." Tulipofika,
malaika wenye mabawa wasio na idadi walitukaribisha, na Yesu akaanza
kunitembeza, huku akinitambulisha kwa malaika wengi. Baadaye Yesu aliniuliza, "Yoo-Kyung, unafurahia kutembelea
Mbinguni?" "Ndiyo, Yesu. Nina furaha kubwa sana,"
nilijibu. Yesu akasema, "Omba kwa bidii, mtii Mchungaji Kim, na hudhuria ibada vizuri, nami
nitakuchukua kuja kutembelea Mbinguni mara kwa mara. Kwa hiyo, uwe na bidii.”
Baada ya
haya kwisha, nilisimulia ushuhuda wangu wa kukutana na Yesu na kutembelea
Mbinguni.
Baek, Bong-Nyo:
Kila mmoja
wetu alikuwa amepiga magoti kwenye mto ili kuomba. Pembeni yangu alikuwapo mke
wa mchungaji, ambaye alikuwa anacheza, akiwa amejawa na Roho Mtakatifu.
Uchezaji wake ulikuwa laini kama kutiririka kwa maji. Alikuwa anang’aa na
kucheza vizuri kadiri Roho Mtakatifu alivyomwongoza.
Niliendelea
kuomba kwa lugha. Ghafla, mwangaza wa rangi ya dhahabu uliangaza, na mbele
yangu akawa amesimama Yesu amevaa vazi jeupe linalong’aa. "Bong-Nyo. Nakupenda."
Sina maneno ya kuelezea furaha kubwa niliyopata kwa kukutana na Bwana. Nilikuwa
na maswali mengi kwake, naye aliyajibu mara moja.
Lee, Haak-Sung:
Nilizama
zaidi kwenye kuomba kwa lugha, bila mimi kujua, na maombi yangu yalijawa na
mamlaka kadiri sauti yangu ilivyopata nguvu. Mwili wangu ulikuwa unawaka kama
moto, na ilibidi nivue nguo yangu ya juu. Baadaye, hata shati langu nalo
lililowa jasho. Sikuwa nimewahi kukutana na moto huu wa Roho Mtakatifu maishani
mwangu. Nilijawa na furaha na nikapenda kuomba. Niliomba nikiwa nimepiga
magoti, na kutokana na maumivu ya kupooza, miguu yangu ilikufa ganzi.
Mke wa Mchungaji, Kang, Hyun-ja:
Nilikuwa
sijaomba maombi ya kwelikweli kwa muda mrefu, kwa hiyo nilikuwa najisikia
shauku hiyo. Wakati nikiomba, kama kulikuwa na hali ya kiroho iliyojitokeza
isiyo ya kawaida, Bwana alishughulika na kila mmoja kibinafsi kwa mamlaka yenye
moto. Upako wa uchezaji wa kiroho ambao Mrs. Choo
Thomas alikuwa nao, nilikuwa na shaku ya kuupata. Nilitamani kupokea. Na
baadaye, kwa mara ya kwanza niliweza kucheza uchezaji ule mtakatifu bila ya
kusitasita. Kwa kitambo fulani, nilificha kipawa hiki, lakini hivi sasa siwezi
kukimbia tena mwongozo wa Roho Mtakatifu. Mwili wangu ulikuwa umepakwa mafuta
kama moto kadiri mikono yangu ilivyoenda na muziki.
==== SIKU YA 3 ====
==== SIKU YA 4====
Lee, Yoo-Kyung:
Nilikuwa
naomba kwa nguvu zangu zote na kwa ghafla, niliona pepo ambalo ilionekana kama
vile limetokea kwenye sinema. Lilivaa vazi jeupe na nywele ndefu, likaja kuelekea
kwangu huku likicheza na kuongea kwa sauti mbaya, "Hahahahaha Hehehehehe." Nilipooza kwa hofu.
"Ewe shetani mwovu na uliyelaaniwa, nakuamuru kwa Jina la Yesu uondoke
kwangu!" Lakini lilizidi kunisogelea hata zaidi huku likipiga kelele,
"Hehehehe, Niondoke kwa nini? Si tu kwamba
niko hapa kukuzuia kuomba, lakini pia nitakupa ugonjwa mwilini mwako." Kisha
Mchungaji Kim aliweka mikono yake kichwani mwangu na kuomba kwa sauti, "Ewe
shetani mchafu. Nakuamuru kwa Jina la Yesu, kimbia!" Shetani
lile lilitoweka. Mchungaji alituambia kuwa ni lazima tujiamini tunapoomba.
Niliendelea
na maombi, huku nikipaza sauti, "Yesu, nisaidie! Nisaidie!"
Niliendelea kumwita kwa muda, ndipo alipotokea kwenye mwanga mkali. Akaniambia,
"Yoo-Kyung, usiogope. Nitakulinda … Haijalishi ni
aina gani ya pepo atakushambulia, usiogope. Kwa nguvu zako zote, niite Mimi
nami nitakuja na kulitoa pepo. Kwa hiyo, usihofu bali uwe na ujasiri."
==== SIKU YA 5 ====
[Maelezo
ya mwandishi: Harusi
kati ya Dada Bong-Nyo na Yesu ni ishara ya uhusiano kati ya Mwokozi na wenye
dhambi aliowaokoa. Alitaka kuonyesha hili kwa mwongofu mpya, Dada Baek.]
Baek, Bong-Nyo:
Baada ya
ibada, nilianza kuomba kwa lugha kwa bidii na Bwana alinitokea na kusema, "Bong-Nyo, twende Mbinguni."
Alinishika mkono na kuanza kuniongoza. Mara nikajikuta nimesimama mbele ya kiti
cha kifalme cha Baba yetu wa Mbinguni. Yesu alieleza kwa hisia sana sababu ya
mimi kupelekwa Mbinguni. "Bong-Nyo, natamani kuwa na harusi nzuri na wewe Mbinguni leo, na hiyo
ndiyo sababu tuko hapa." Mara malaika walianza kuandaa gauni
langu na wakanipamba kwa vito vingi. Sijawahi kuona kitu kinachofanana na gauni
la dhahabu lililoandaliwa kwa ajili yangu kule. Nilijawa na furaha sana. Malaika
wengi na wakaaji wengi wa Mbinguni walipongeza harusi yetu, na sitakaa nisahau
jambo hilo. Hapohapo nikawa naona kiti cha enzi cha Baba wa Mbinguni
kikiyumbayumba taratibu. Kila kilipofanya hivyo, maana Mungu alifurahia sana,
rangi tano nzuri zilitokea pale. Baada ya sherehe ile, nilisafiri kote Mbinguni
huku nimemshika Bwana mkono. Nilikuwa nina furaha isiyo kifani.
Lee, Haak-Sung:
Huku nikiwa
nimeamua kwelikweli, nilianza kuomba kwa lugha. Ghafla, msalaba ulioko nyuma ya
madhabahu ulitoa nuru kali, kisha mlango wa duara ulitokea. Baadaye kidogo,
Yesu alitokea. "Haak-Sung.
nakupenda." Sikuwa na uwezo wa kustahimili furaha kubwa
niliyojisikia. "Haak-Sung, kuna
mahali nataka uende nami. Kwa hiyo, tuondoke." Mara Yesu
aliponishika mkono, mwili wangu ulielea hewani kwa wepesi kama unyoya.
Tulipofika tulikokuwa tunaenda, kulikuwa na harufu ya ajabu, na ilikuwa ni
mbaya sana! Sikuweza hata kupumua kutokana na harufu ile. "Yesu, mpendwa wangu Yesu. Tunakwenda
wapi? Mbona sioni vizuri mbele yangu?" nilipaza sauti, lakini Yesu
akasema, "Haak-Sung,
usiogope. Hapa ni kuzimu. Nitakulinda, kwa hiyo usiwe na hofu. Lakini angalia
kwa makini."
Moto
ulisababisha joto kwenye lango la kuzimu hadi likawa jekundu! Na kuingia
kulisababisha joto kali hata zaidi. Ilibidi nigeuze uso wangu kwa sababu ya
joto lile. Nikauliza, "Yesu, tutaingiaje humu kwenye shimo hili la
moto? Sidhani kama naweza kufanya hivyo." Tulienda mahali ambako
kulikuwa na giza totoro na sikuweza kuona chochote. Kisha mara Yesu alipogusa
macho yangu, niliweza kuona waziwazi. Kulikuwa na bibi mmoja akionekana amekata
tamaa, amekaa bila kusogea huku amevaa vazi la kitamaduni la Kikorea. Yesu
kasema, "Haak-Sung, tazama kwa
makini." Kwa hiyo nilimtazama yule bibi kwa karibu zaidi. Alikuwa ni
bibi yangu mzaa mama, ambaye alishakufa miaka michache iliyopita! Mama yangu
alipoondoka nyumbani, bibi yangu huyo ndiye aliyenilea. Bibi yangu alitupenda.
Nilijisikia vibaya kumkuta bibi yangu kuzimu. Kwa mshangao nilipaza sauti
nikisema, "Bibi, ni mimi, Haak-Sung. Yawezekanaje mtu mpole na
mkarimu aishie huku? Fanya haraka, njoo huku!" Bibi yangu
alinitambua mara moja, na kwa mshangao aliuliza, "Haak-Sung, kwa nini
uko hapa? Umekujaje huku?" Nikajibu, "Yesu amenileta hapa.
Bibi, fanya haraka utoke humu!" Bibi yangu alilia kwa sauti akisema,
"Haak-Sung, japokuwa nataka sana kutoka humu, huwezi kufanya hicho
unachotaka kufanya. Usikubali kuja huku. Ondoka mara moja." Kwa
machozi, nilimwomba Yesu, "Yesu, tafadhali msaidie bibi yangu atoke
humu. Bibi yangu aliishi maisha ya huzuni." Papo hapo, joka kubwa
lilitokea chini ya mguu wa bibi yangu na kuanza kujiviringa mwilini mwake.
Nilipiga kelele kubwa, "Ahh." Bibi yangu alipiga kelele
kwa hofu, "Niokoe, tafadhali," lakini hakukuwa na msaada.
"Yesu, mpendwa wangu Yesu, mimi ndiye niliyetenda maovu mengi,"
nililia. "Tafadhali fanya kitu, tafadhali!" Yesu
hakusema hata neno moja, lakini moyo wake ulikuwa unaumia akiangalia. Nililia
na kulia na kusihi, lakini wapi! Hata katikati ya mateso hayo, bibi aliuliza
juu ya hali ya familia na alikuwa akihofia juu yao. "Haak-Sung, dada
zako wanaendeleaje? Vipi mama yako?" Nikajibu, "Kila mmoja
anaendelea vizuri," na wakati nikimjibu, joka lile lilimviringa kwa
nguvu zaidi. Kilio cha bibi yangu kiliongezeka zaidi na zaidi. Yesu alinishika
mkono na kuniongoza na kusema, "Haak-Sung, ni wakati wa kuondoka sasa." Niliacha vilio
vya bibi yangu nyuma na tukatoka kuzimu. Yesu akasema, "Kuzimu, ukilinganisha na duniani,
hisia zako zote zinakuwa zinahisi sana ... Haa-Sung, usilie. Umeona waziwazi.
Kwa hiyo, nenda ukamtumikie Bwana kwa uaminifu. Je, unaelewa?"
Baadaye Yesu
aliniita, "Haak-Sung.
Kuzimu ni kubaya sana, si ndiyo? Nataka nikuonyeshe Mbinguni leo."
Kwa muda mfupi, tulikuwa tayari tuko Mbinguni. Makundi ya malaika na watu wengi
waliokwishafika Mbinguni kabla yangu walitoka kuja kunikaribisha. Malaika
waliozunguka pamoja na Yesu walishikana mikono na kuanza kucheza pamoja kwa
furaha. Kila kitu Mbinguni kilikuwa tofauti kabisa na kule kuzimu. Nilichoona
Mbinguni kilionekana kipya, cha kushangaza na si rahisi kuamini hata kidogo.
Nikiwa Mbinguni, nilitoa ombi kwa Yesu, "Yesu,
mtoto wa mchungaji, Joseph—mguu wake umefunikwa na vidonda vyenye maumivu na
hawezi kutembea vizuri. Tafadhali, mponye. Na mama yangu anaumwa na mgongo.
Msaidie kaka Oh, Jong-Suk, ambaye anaishi kwenye ofisi ya kanisa apate kazi. Na
mwisho, tusaidie kupata uamsho kwenye Kanisa letu." Yesu alijibu
kwa furaha, "Ndiyo,
sawasawa." Yesu alinitazama na kusema, "Haak-Sung, inatosha kwa leo.
Tuondoke." Yesu aliponishika mkono wangu, tulipaa angani
na kurudi kwenye kanisa letu.
Niliendelea
kuomba kwa bidii. Sikuweza kumsahau bibi
yangu ambaye alikuwa akiteseka kuzimu, na machozi yananitoka. Nilikuwa kwenye
maumivu na huzuni kubwa. Nililia sana huku nikipiga mateke na kupaza sauti, "Bwana,
nifanye nini? Bibi yangu alikufa kwa sababu yangu. Maumivu haya moyoni mwangu
ni makali sana. Bibi. Maskini bibi yangu!” Nililia hadi nikachoka. Kisha
nikaanza tena. Nikamwita Bwana. Ni nadra sana mimi kulia, lakini sikuamini
machozi yaliyonitoka kwa saa 2, saa 3, na kisha saa 4! Ngwe ya kwanza ya maombi
iliisha, lakini bado sikuweza kudhibiti huzuni yangu. Niliwashirikisha wenzangu
kile nilichoona Mbinguni na kuzimu. Kisha saa 11 alfajiri tulianza ngwe ya pili
ya maombi yetu, ambayo iliisha baada ya masaa 5. Wakati mchungaji akitoa
mahubiri yake, Yesu alitokea, halafu mahubiri ya mchungaji yakawa na nguvu
zaidi. Malaika walishuka toka mbinguni, wakajipanga pembeni ya madhabahu, na
wengine walikuwa na mabakuli. Walichukua sala za kila mmoja wetu na kuzitia
humo. Na waliimba "Amina. Amina."
Hata baada
ya ibada kwisha, sikuweza kujizuia kusikitishwa na bibi yangu aliyeko kuzimu.
ITAENDELEA ….
tuishi maisha ya kumpendeza mungu.......
ReplyDeletemaana hatujui siku wala saa.
Pasipo utakatifu hakuna atakaye mwona Mungu Ebrania 12:14.Asante sana kwa Ushuuda huu.Mimi naitwa Wane John Msukwa.
Deletetena hakuna jina liokoalo isipokuwa jina la yesu peke yake.
DeleteAmen. Ni kweli kabisa.
DeleteShalom ✋ Tafadhali naomba kitabu kiitwacho kubatizwa kwa moto uwakao
ReplyDeletepastoradriano78@gmail.com
ReplyDelete