Monday, July 14, 2014

Kubatizwa kwa Moto Uwakao - 1




Huu ni ushuhuda unaotokana na kitabu kinachojulikana kama Baptized by Blazing Fire, Devine Expose of Heaven and Hell kilichoandikwa na Mchungaji Yong-Doo Kim wa Korea. Ni ushuhuda mrefu ambao utakupa mafundisho, maonyo, utakutia moyo na kukuimarisha katika safari yetu ya kuelekea kwa Baba, Mbinguni.


………………………………….

Kutokana na siku 30 za maombi mfululizo wakati wa usiku kwenye kanisa dogo nchini Korea, waumini walipokea uamsho usio wa kawaida. Wakiwa wameinua mikono yao juu, huku wakiomba usiku kucha, macho ya kiroho ya waumini hawa yalikuwa wazi huku na waliona maono, uponyaji, vita vikali vya kiroho, na kukutana na Yesu kwa jinsi ya ajabu. Huku macho yao yakiwa yamefunguliwa, waliweza kuona wazi mapambano ya kiroho kwenye ulimwengu wa giza wakati wa maombi.  Walionyeshwa jinsi mashetani yanavyojaribu kutuondolea uzingativu wetu, kututisha, na kutudanganya wakati tunapofanya maombi. Kila aina ya hila ya kipepo iliyo kwenye ushuhuda huu ilitumika dhidi yao ili kuwafanya waache kuomba. Walikabiliana na kupambana na aina mbalimbali za majoka, wafalme wa kipepo, malaika wa uongo, makristo wa uongo, mapepo yanayotaka kuhurumiwa, manyonya damu, mapepo yaliyojigeuza kuwa wanawake warembo, n.k. Pia walipelekwa mbinguni na kuzimu mara nyingi na Yesu. Ilifunuliwa kuwa maombezi ya usiku, (kukiwamo kunena kwa lugha), yana nguvu sana, na japo ni magumu kuomba lakini yana matokeo makubwa.

Kuna vitabu vitano vinavyohusu shuhuda hizi. Ushuhuda huu umefupishwa katika sehemu kadha wa kadha kuliko ulivyo kwenye kitabu chake:

KITABU CHA 1 – SEHEMU YA KWANZA
Yesu amwambia Mchungaji Kim:"Kuanzia sasa, chochote ambacho wewe na washirika wako mtakiona au kukisikia, lazima mkiandike vizuri. Kupitia hayo mambo, napenda makanisa yote Korea na duniani kote yaamke. Hii ndiyo sababu uliletwa duniani. Wakati huu wa sasa, makanisa ya Korea na waumini wake wanapingana na kile ambacho nimewaandalia. Wachungaji na washirika wananiabudu kimazoea tu na wananijua kinadharia tu kutokana na yale wanayosoma vitabuni.”

Mchungaji Kim:
Kanisa letu linaamini katika nguvu za kunena kwa lugha, hivyo tuliweza kuomba muda mrefu, kwa moyo, na kwa undani kabisa. Kunena kwa lugha pia kulitusaidia kutuliza mawazo, hivyo tukapata nguvu kubwa sana zilizotufungua macho yetu ya kiroho. Mchakato wa kufungua macho ya kiroho ya mtu si tu ni mgumu, bali pia ni lazima mtu avuke vikwazo vingi. Kwa hiyo, kama wewe ni mzembe, hauzingatii na haujajipanga sawasawa, utaingia gharama kubwa sana.  Sasa, sisi pia tumejiandaa kikamilifu kutuma mapigo na mashambulizi kwa kujiandaa vilivyo kwa njia ya kusifu, kujaza mioyo yetu kwa Neno la Yesu, na kutafuta kwa bidii kwa kumlilia Bwana.

Watumishi wa shetani huja mmojammoja. Kisha akishindwa, wanakuja wawili; kisha wanashambulia wakiwa kumi, thelathini, hamsini, mia moja au zaidi. Kundi hilo husambaa kila mara na kujikusanya tena ili kushambulia kulingana na hali ilivyo. Halafu mmoja akifukuzwa kwa njia ya maombi, pepo hilo linaenda kwa mlengwa mwingine kwa njia ya dhihaka, vishawishi, na wakati mwingine kwa maneno matamu ya kunong’oneza. Mwishowe, wanapogundulika, wanakimbia haraka. Watumishi wa shetani huja kwetu kwa namna na mwonekano tofautitofauti. Wakati mwingine wanajaribu kutunasa kwa kujipa sura ya msanii maarufu, mtoto mchanga, yesu wa uongo, au kama malaika wa nuru (2 Kor 11:14). Pia walituchanganya kabisa kwa kutokea kama binti yangu. Tulipambana na kushinda, lakini pia tulipoteza mapambano mengi dhidi ya pepo wachafu. Maumivu yalikuwa makali na tuligaragara chini mara nyingi. Tulipokabiliana na mapepo ya kutisha yenye nguvu sana, yasiyowezekana, Bwana wetu alimtuma Malaika Mkuu Gabrieli na malaika wengine ili kutusaidia. Bwana wetu atupendaye anatuhakikishia kuwa hatuko peke yetu pale tunapoita malaika wa mbinguni kuja kutusaidia tunapochoka kutokana na ugumu wa mapambano.

Yesu alitukumbusha tujivike uwezo kwa kuomba kila siku (Marko 9:29).  Ni muhimu kuomba kila mara. Yesu anaelezea umuhimu wa maombi ya kukubaliana watu wawili au zaidi (Mathayo 18:19). Nguvu za giza haziondoki kwa upole. Badala yake zinaacha makovu na mateso yanaendelea.

Kaulimbiu yetu ya mwaka 2005 ilikuwa "Pata uamsho kupitia kuomba," na tulianza maombi yetu Januari 2.  Maombi yaliendelea kwa siku thelathini. Tulikuwa watu kumi. Siku ya kwanza, baada ya ibada ya Jumapili jioni, tulikuwa na kipindi cha kuomba. Siku ya pili, (Januari 3), tuliona uwepo wa nguvu wa Roho Mtakatifu. Maombi ya pamoja na pia maombi ya mmojammoja yalilipuka na kuendelea hadi saa 1:30 asubuhi iliyofuata. Baada ya maombi kwisha, tulikaa kwenye duara ili kusikia shuhuda na jinsi kukutana na Yesu kulivyokuwa. Muda wa maombi yetu uliendelea kuwa mrefu zaidi na zaidi. Maombi ya Jumatano jioni yalianza saa 1:30 jioni na kwisha karibu saa 2:00 asubuhi iliyofuata. Alhamisi ilikuwa ni saa 3:00 jioni hadi saa 4:00 asubuhi.  

Mungu aligeuza kabisa mawazo yetu. Kadiri tulivyozidi kuomba, ndivyo Bwana alivyotupatia mambo ya kushangaza zaidi. Japokuwa maombi yetu yalidumu usiku kucha, hakuna aliyelalamika. Badala yake, njaa ya chakula cha kiroho ilizidi kuongezeka. Bwana alikuja kututembelea wakati tunaomba. Tulimwona kwa njia ya macho yetu ya kiroho, lakini kuna wakati ambapo tulimwona kwa macho yetu ya nyama kabisa!

Kadiri watoto walivyoweza kumwona Yesu, kukosa utii kuliisha na wakawa watumishi wanyenyekevu na waaminifu. Washirika wetu wawili, baada ya kuona Mbingu na kuzimu, walilia sana na kupiga magoti na kuomba msamaha kwa mambo mabaya ambayo walikuwa wamenifanyia mara nyingi. Licha ya kwamba kulikuwa na baridi kali sana chini ya nyuzi sifuri, walitoka kwenda kushuhudia. Walitoka saa 10 mchana na hawarudi hadi saa 2:30 usiku, huku mikono na miguu yao ikiwa imeganda kwa baridi kali. Walitambua kuwa wanatakiwa kuwa na bidii kwa sababu waliona hazina zao zikitunzwa mbinguni. Meena, msichana wa miaka 5, huomba kwa kunena kwa lugha huku mikono yake imeinuliwa juu kwa saa 2 hadi 3! Kusanyiko letu lilipokea karama za kiungu za unabii, kupambanua roho, kunena kwa lugha, maarifa, hekima na imani ya kiungu.

Hakuna maneno ya uongo kwenye kitabu hiki; bali ni mambo ambayo washirika waliyapitia kibinafsi wakati wa mwito wa kufanya maombi.

Washirika wa Kanisa la Bwana walioshiriki ni hawa: [Mchungaji Kim]  [Kang, Hyun-ja]  [Kim, Joseph]  [Kim, Joo-Eun]  [Dada Baek, Bong-Nyo]  [Lee, Haak-Sung]  [Lee, Yoo-Kyung]  [Meena]  [Oh, Jong-Suk] [Shemasi Shin, Sung-Kyung]  [Oh, Jung-Min]

====  SIKU YA 1  ==== [Ukiona hivi maana yake sehemu hii imepunguzwa]
====  SIKU YA 2  ====
Mchungaji Kim
Baada ya Roho Mtakatifu kuingilia kwa namna ya kipekee, ilikuwa ni kama tumepata moto wakati tukiomba. Japokuwa maombi yaliisha saa 1 asubuhi iliyofuata, tulijiona kama vile hatukupata muda wa kutosha.

Lee, Yoo-Kyung:
Niliingiwa na shauku kubwa sana na kwa nguvu zangu zote nilimwita Bwana, "Yesu, Yesu, Yesu nakupenda. Naomba nikuone. Jidhihirishe kwangu." Nilipaza sauti na kuomba kwa lugha kwa bidii. Karibu saa moja ilishapita ndipo mwanga mkali uliwaka ghafla, na kuna mtu alikuwa amesimama katikati yake. Nilifungua macho yangu na kupatwa na mshtuko, lakini sikuona chochote. Nilipofunga tena macho yangu, niliweza kuona wazi, kwa hiyo nilibaki nimeyafunga. Yesu alisimama mbele yangu huku amevaa vazi zuri linalong’aa.  "Yoo-Kyung, nakupenda," Yesu alisema maneno haya, kisha alisogea karibu yangu na kukaa mbele yangu. Sidhani kama nimewahi kuona mtu mzuri kama Yeye. Nywele za Yesu zilikuwa za rangi ya dhahabu na alikuwa na macho mazuri, makubwa. Alinipapasa nywele zangu taratibu na kusema, "Yoo-Kyung, nakupenda."  Nilianza kulia na moyo wangu uliyeyuka.  "Nataka nikuonyeshe Mbingu ilivyo." Mara tuliondoka. Kulikuwa na nuru kali sana kiasi kwamba sikuweza kufungua macho yangu. Niliwaza, "Lazima hapa patakuwa ni Mbinguni."  Tulipofika, malaika wenye mabawa wasio na idadi walitukaribisha, na Yesu akaanza kunitembeza, huku akinitambulisha kwa malaika wengi. Baadaye Yesu aliniuliza, "Yoo-Kyung, unafurahia kutembelea Mbinguni?"  "Ndiyo, Yesu. Nina furaha kubwa sana," nilijibu.  Yesu akasema, "Omba kwa bidii, mtii Mchungaji Kim, na hudhuria ibada vizuri, nami nitakuchukua kuja kutembelea Mbinguni mara kwa mara. Kwa hiyo, uwe na bidii.”
Baada ya haya kwisha, nilisimulia ushuhuda wangu wa kukutana na Yesu na kutembelea Mbinguni.

Baek, Bong-Nyo:
Kila mmoja wetu alikuwa amepiga magoti kwenye mto ili kuomba. Pembeni yangu alikuwapo mke wa mchungaji, ambaye alikuwa anacheza, akiwa amejawa na Roho Mtakatifu. Uchezaji wake ulikuwa laini kama kutiririka kwa maji. Alikuwa anang’aa na kucheza vizuri kadiri Roho Mtakatifu alivyomwongoza.

Niliendelea kuomba kwa lugha. Ghafla, mwangaza wa rangi ya dhahabu uliangaza, na mbele yangu akawa amesimama Yesu amevaa vazi jeupe linalong’aa. "Bong-Nyo. Nakupenda." Sina maneno ya kuelezea furaha kubwa niliyopata kwa kukutana na Bwana. Nilikuwa na maswali mengi kwake, naye aliyajibu mara moja.

Lee, Haak-Sung:
Nilizama zaidi kwenye kuomba kwa lugha, bila mimi kujua, na maombi yangu yalijawa na mamlaka kadiri sauti yangu ilivyopata nguvu. Mwili wangu ulikuwa unawaka kama moto, na ilibidi nivue nguo yangu ya juu. Baadaye, hata shati langu nalo lililowa jasho. Sikuwa nimewahi kukutana na moto huu wa Roho Mtakatifu maishani mwangu. Nilijawa na furaha na nikapenda kuomba. Niliomba nikiwa nimepiga magoti, na kutokana na maumivu ya kupooza, miguu yangu ilikufa ganzi.

Mke wa Mchungaji, Kang, Hyun-ja:
Nilikuwa sijaomba maombi ya kwelikweli kwa muda mrefu, kwa hiyo nilikuwa najisikia shauku hiyo. Wakati nikiomba, kama kulikuwa na hali ya kiroho iliyojitokeza isiyo ya kawaida, Bwana alishughulika na kila mmoja kibinafsi kwa mamlaka yenye moto. Upako wa uchezaji wa kiroho ambao Mrs. Choo Thomas alikuwa nao, nilikuwa na shaku ya kuupata. Nilitamani kupokea. Na baadaye, kwa mara ya kwanza niliweza kucheza uchezaji ule mtakatifu bila ya kusitasita. Kwa kitambo fulani, nilificha kipawa hiki, lakini hivi sasa siwezi kukimbia tena mwongozo wa Roho Mtakatifu. Mwili wangu ulikuwa umepakwa mafuta kama moto kadiri mikono yangu ilivyoenda na muziki.  

====  SIKU YA 3  ====
====  SIKU YA 4====

Lee, Yoo-Kyung: 
Nilikuwa naomba kwa nguvu zangu zote na kwa ghafla, niliona pepo ambalo ilionekana kama vile limetokea kwenye sinema. Lilivaa vazi jeupe na nywele ndefu, likaja kuelekea kwangu huku likicheza na kuongea kwa sauti mbaya, "Hahahahaha Hehehehehe." Nilipooza kwa hofu.  "Ewe shetani mwovu na uliyelaaniwa, nakuamuru kwa Jina la Yesu uondoke kwangu!" Lakini lilizidi kunisogelea hata zaidi huku likipiga kelele, "Hehehehe, Niondoke kwa nini? Si tu kwamba niko hapa kukuzuia kuomba, lakini pia nitakupa ugonjwa mwilini mwako." Kisha Mchungaji Kim aliweka mikono yake kichwani mwangu na kuomba kwa sauti, "Ewe shetani mchafu. Nakuamuru kwa Jina la Yesu, kimbia!"  Shetani lile lilitoweka. Mchungaji alituambia kuwa ni lazima tujiamini tunapoomba.

Niliendelea na maombi, huku nikipaza sauti, "Yesu, nisaidie! Nisaidie!" Niliendelea kumwita kwa muda, ndipo alipotokea kwenye mwanga mkali. Akaniambia,  "Yoo-Kyung, usiogope. Nitakulinda … Haijalishi ni aina gani ya pepo atakushambulia, usiogope. Kwa nguvu zako zote, niite Mimi nami nitakuja na kulitoa pepo. Kwa hiyo, usihofu bali uwe na ujasiri.

====  SIKU YA 5  ====
[Maelezo ya mwandishi: Harusi kati ya Dada Bong-Nyo na Yesu ni ishara ya uhusiano kati ya Mwokozi na wenye dhambi aliowaokoa. Alitaka kuonyesha hili kwa mwongofu mpya, Dada Baek.]

Baek,   Bong-Nyo:
Baada ya ibada, nilianza kuomba kwa lugha kwa bidii na Bwana alinitokea na kusema, "Bong-Nyo, twende Mbinguni." Alinishika mkono na kuanza kuniongoza. Mara nikajikuta nimesimama mbele ya kiti cha kifalme cha Baba yetu wa Mbinguni. Yesu alieleza kwa hisia sana sababu ya mimi kupelekwa Mbinguni. "Bong-Nyo, natamani kuwa na harusi nzuri na wewe Mbinguni leo, na hiyo ndiyo sababu tuko hapa." Mara malaika walianza kuandaa gauni langu na wakanipamba kwa vito vingi. Sijawahi kuona kitu kinachofanana na gauni la dhahabu lililoandaliwa kwa ajili yangu kule. Nilijawa na furaha sana. Malaika wengi na wakaaji wengi wa Mbinguni walipongeza harusi yetu, na sitakaa nisahau jambo hilo. Hapohapo nikawa naona kiti cha enzi cha Baba wa Mbinguni kikiyumbayumba taratibu. Kila kilipofanya hivyo, maana Mungu alifurahia sana, rangi tano nzuri zilitokea pale. Baada ya sherehe ile, nilisafiri kote Mbinguni huku nimemshika Bwana mkono. Nilikuwa nina furaha isiyo kifani. 

Lee, Haak-Sung:
Huku nikiwa nimeamua kwelikweli, nilianza kuomba kwa lugha. Ghafla, msalaba ulioko nyuma ya madhabahu ulitoa nuru kali, kisha mlango wa duara ulitokea. Baadaye kidogo, Yesu alitokea. "Haak-Sung.  nakupenda." Sikuwa na uwezo wa kustahimili furaha kubwa niliyojisikia.  "Haak-Sung, kuna mahali nataka uende nami. Kwa hiyo, tuondoke." Mara Yesu aliponishika mkono, mwili wangu ulielea hewani kwa wepesi kama unyoya. Tulipofika tulikokuwa tunaenda, kulikuwa na harufu ya ajabu, na ilikuwa ni mbaya sana! Sikuweza hata kupumua kutokana na harufu ile.  "Yesu, mpendwa wangu Yesu. Tunakwenda wapi? Mbona sioni vizuri mbele yangu?" nilipaza sauti, lakini Yesu akasema, "Haak-Sung, usiogope. Hapa ni kuzimu. Nitakulinda, kwa hiyo usiwe na hofu. Lakini angalia kwa makini."

Moto ulisababisha joto kwenye lango la kuzimu hadi likawa jekundu! Na kuingia kulisababisha joto kali hata zaidi. Ilibidi nigeuze uso wangu kwa sababu ya joto lile. Nikauliza, "Yesu, tutaingiaje humu kwenye shimo hili la moto? Sidhani kama naweza kufanya hivyo." Tulienda mahali ambako kulikuwa na giza totoro na sikuweza kuona chochote. Kisha mara Yesu alipogusa macho yangu, niliweza kuona waziwazi. Kulikuwa na bibi mmoja akionekana amekata tamaa, amekaa bila kusogea huku amevaa vazi la kitamaduni la Kikorea. Yesu kasema,  "Haak-Sung, tazama kwa makini." Kwa hiyo nilimtazama yule bibi kwa karibu zaidi. Alikuwa ni bibi yangu mzaa mama, ambaye alishakufa miaka michache iliyopita! Mama yangu alipoondoka nyumbani, bibi yangu huyo ndiye aliyenilea. Bibi yangu alitupenda. Nilijisikia vibaya kumkuta bibi yangu kuzimu. Kwa mshangao nilipaza sauti nikisema, "Bibi, ni mimi, Haak-Sung.  Yawezekanaje mtu mpole na mkarimu aishie huku? Fanya haraka, njoo huku!"  Bibi yangu alinitambua mara moja, na kwa mshangao aliuliza, "Haak-Sung, kwa nini uko hapa? Umekujaje huku?" Nikajibu, "Yesu amenileta hapa. Bibi, fanya haraka utoke humu!" Bibi yangu alilia kwa sauti akisema, "Haak-Sung, japokuwa nataka sana kutoka humu, huwezi kufanya hicho unachotaka kufanya. Usikubali kuja huku. Ondoka mara moja."  Kwa machozi, nilimwomba Yesu, "Yesu, tafadhali msaidie bibi yangu atoke humu. Bibi yangu aliishi maisha ya huzuni." Papo hapo, joka kubwa lilitokea chini ya mguu wa bibi yangu na kuanza kujiviringa mwilini mwake. Nilipiga kelele kubwa, "Ahh."  Bibi yangu alipiga kelele kwa hofu, "Niokoe, tafadhali," lakini hakukuwa na msaada.  "Yesu, mpendwa wangu Yesu, mimi ndiye niliyetenda maovu mengi," nililia.  "Tafadhali fanya kitu, tafadhali!" Yesu hakusema hata neno moja, lakini moyo wake ulikuwa unaumia akiangalia. Nililia na kulia na kusihi, lakini wapi! Hata katikati ya mateso hayo, bibi aliuliza juu ya hali ya familia na alikuwa akihofia juu yao.  "Haak-Sung, dada zako wanaendeleaje? Vipi mama yako?" Nikajibu, "Kila mmoja anaendelea vizuri," na wakati nikimjibu, joka lile lilimviringa kwa nguvu zaidi. Kilio cha bibi yangu kiliongezeka zaidi na zaidi. Yesu alinishika mkono na kuniongoza na kusema, "Haak-Sung, ni wakati wa kuondoka sasa." Niliacha vilio vya bibi yangu nyuma na tukatoka kuzimu. Yesu akasema, "Kuzimu, ukilinganisha na duniani, hisia zako zote zinakuwa zinahisi sana ... Haa-Sung, usilie. Umeona waziwazi. Kwa hiyo, nenda ukamtumikie Bwana kwa uaminifu. Je, unaelewa?"
Baadaye Yesu aliniita, "Haak-Sung.  Kuzimu ni kubaya sana, si ndiyo? Nataka nikuonyeshe Mbinguni leo."  Kwa muda mfupi, tulikuwa tayari tuko Mbinguni. Makundi ya malaika na watu wengi waliokwishafika Mbinguni kabla yangu walitoka kuja kunikaribisha. Malaika waliozunguka pamoja na Yesu walishikana mikono na kuanza kucheza pamoja kwa furaha. Kila kitu Mbinguni kilikuwa tofauti kabisa na kule kuzimu. Nilichoona Mbinguni kilionekana kipya, cha kushangaza na si rahisi kuamini hata kidogo. Nikiwa Mbinguni, nilitoa ombi kwa Yesu,  "Yesu, mtoto wa mchungaji, Joseph—mguu wake umefunikwa na vidonda vyenye maumivu na hawezi kutembea vizuri. Tafadhali, mponye. Na mama yangu anaumwa na mgongo. Msaidie kaka Oh, Jong-Suk, ambaye anaishi kwenye ofisi ya kanisa apate kazi. Na mwisho, tusaidie kupata uamsho kwenye Kanisa letu."  Yesu alijibu kwa furaha, "Ndiyo, sawasawa." Yesu alinitazama na kusema, "Haak-Sung, inatosha kwa leo. Tuondoke."  Yesu aliponishika mkono wangu, tulipaa angani na kurudi kwenye kanisa letu.

Niliendelea kuomba kwa bidii.  Sikuweza kumsahau bibi yangu ambaye alikuwa akiteseka kuzimu, na machozi yananitoka. Nilikuwa kwenye maumivu na huzuni kubwa. Nililia sana huku nikipiga mateke na kupaza sauti, "Bwana, nifanye nini? Bibi yangu alikufa kwa sababu yangu. Maumivu haya moyoni mwangu ni makali sana. Bibi. Maskini bibi yangu!” Nililia hadi nikachoka. Kisha nikaanza tena. Nikamwita Bwana. Ni nadra sana mimi kulia, lakini sikuamini machozi yaliyonitoka kwa saa 2, saa 3, na kisha saa 4! Ngwe ya kwanza ya maombi iliisha, lakini bado sikuweza kudhibiti huzuni yangu. Niliwashirikisha wenzangu kile nilichoona Mbinguni na kuzimu. Kisha saa 11 alfajiri tulianza ngwe ya pili ya maombi yetu, ambayo iliisha baada ya masaa 5. Wakati mchungaji akitoa mahubiri yake, Yesu alitokea, halafu mahubiri ya mchungaji yakawa na nguvu zaidi. Malaika walishuka toka mbinguni, wakajipanga pembeni ya madhabahu, na wengine walikuwa na mabakuli. Walichukua sala za kila mmoja wetu na kuzitia humo. Na waliimba  "Amina.  Amina."  

Hata baada ya ibada kwisha, sikuweza kujizuia kusikitishwa na bibi yangu aliyeko kuzimu. 

ITAENDELEA ….

6 comments:

  1. tuishi maisha ya kumpendeza mungu.......
    maana hatujui siku wala saa.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Pasipo utakatifu hakuna atakaye mwona Mungu Ebrania 12:14.Asante sana kwa Ushuuda huu.Mimi naitwa Wane John Msukwa.

      Delete
    2. tena hakuna jina liokoalo isipokuwa jina la yesu peke yake.

      Delete
  2. Shalom ✋ Tafadhali naomba kitabu kiitwacho kubatizwa kwa moto uwakao

    ReplyDelete
  3. pastoradriano78@gmail.com

    ReplyDelete