Friday, February 21, 2014

Mwanafunzi wa mchawi - Sehemu ya 2


Yale makucha yalijaribu kunizuia tena lakini yakashindwa. Kwa hiyo, niliikamata ile Biblia na kuiweka kifuani pangu. Biblia ilijifunua yenyewe! Nilitaka kuinyanyua hadi kwenye mwanga wa mshumaa ambao nilikuwa tayari nimeshauwasha. Lakini shetani aliuzima ule mshumaa. Kwa hiyo, sasa kulikuwa na giza kabisa kwenye chumba kile. Na hivyo, sikuweza kusoma chochote kutoka kwenye kitabu hicho na sikuona kilichokuwa kimeandikwa kwenye ukurasa ule ambako Biblia ilijifunua yenyewe kimiujiza. Kulikuwa na giza totoro.


Lakini Mungu ni mwaminifu; anampenda mwanadamu. Ghafla, kulitokea miali mitatu ya mwanga toka juu na kila mmoja ukamulika sehemu maalum kwenye ukurasa wa Biblia uliokuwa umefunguka. Zilikuwa ni aya tatu za sura ya tatu ya Injili ya Yohana:

“Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu.” (Yohana 3:3).

“Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu.” (Yohana 3:5).

“Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.” (Yohana 3:16).

Nilipokuwa nasoma sehemu hii ya mwisho, ndani yangu nilijua kabisa kuwa sasa ninayo kweli pekee iwekayo huru. Kwa muda huo, Mungu aliniwezesha kujua jinsi ya kumpokea Bwana Yesu Kristo maishani mwangu. Nilishasikia mara nyingi kutoka kwa Kim, lakini kila niliposikia, ibilisi alifuta ufahamu huo kutoka akilini mwangu. Kwa muda ule, kila kitu kiliwekwa wazi kabisa kwangu. Mungu aliondoa vile vidole vilivyokuwa vinaziba masikio na moyo wangu.

Nakumbuka sala ya kujikabidhi kwa Mungu na sala ambayo mtu anaomba msamaha wa dhambi, ambayo Kim alikuwa akinieleza. Nilianza kunyanyuka kutoka kitandani na nikawa namwomba Yesu anikomboe na aniokoe. Shetani, kwa kuwa alijua kuwa nina muda mchache tu, na akiona ya kuwa naelekea kuondolewa kuzimu muda wa mwishomwisho,  alifanya kila juhudi kunizuia kuomba. Alijua kuwa kama akiweza kwa namna fulani kunizuia kuomba, roho yangu itaishia mahali ambako sikutaka kwenda. Yalikuwa ni mapambano kwenye ukingo kabisa wa kuzimu! Wakati huo nilijisikia kama shetani ameniwekea uzito mkubwa sana. Nilihisi kama kuna mtu anakata mgongo wangu kwa kisu. Yalikuwa ni maumivu makali sana. Nilijua kuwa natakiwa kupaza sauti kwa Yesu ili aniokoe, kwa hiyo sikujali maumivu yale.

Tayari nimeshaonja mauti na mwanzo wa kuzimu, na sasa ulikuwa ni wakati wangu wa kuonja uzima – uzima mpya na Yesu. Sikuangalia yale maumivu makali, bali nikafanya linipasalo! Nilifunga macho yangu na kusema, “Bwana Yesu, mimi ni mwenye dhambi. Najua kuwa Wewe ni yule Mungu wa kweli, nami ninakuomba, tafadhali ingia kwenye maisha yangu na uyatawale – Sasa!”

Mara moja Mungu alidhihirisha ushindi wake. Nilijua papo hapo kuwa yale mapepo yote ambayo niliyafungulia mlango yamewekwa kando. Kisha yalitupwa kwenye lile shimo pembeni mwa kitanda changu, ambamo mlikuwa mnatokea vile vilio vya kutisha. Ghafla shimo lile lilijifunga; kisha sauti na ile harufu ya kuzimu navyo vilikoma! Ndipo kwenye ile amani iliyoingia hapo ghafla, nilijisikia kama vile naogelea kwenye mafuta. Ilikuwa ni hali ya kutakasa sana. Chumba kile nilimokuwamo, ghafla kilijawa na nuru japokuwa ilikuwa bado ni usiku. Ile nuru ilikuwa ni kali sana kiasi kwamba ilifunika kila kitu. Ilikuwa ni nuru na amani. Huo uwepo wa Mungu pamoja na pendo lake ulikuwa mkubwa sana kiasi kwamba nilipoteza fahamu.

Nilipozinduka asubuhi iliyofuata, nilikuwa nimeoshwa na nimeponywa! Nilikuwa nimevikwa mavazi mapya na moto ulikuwa unawake kwenye stovu! Sehemu ile yote ilikuwa na joto. Homa ya nimonia ilikuwa haipo tena. Udhaifu wote uliondoka kwangu. Kansa nayo ilikuwa imeondoka! Kuungua baridi kwenye miguu nako kuliondoka na nikawa najihisi kuwa nimezaliwa upya. Nilikuwa nimejaa amani na furaha. Nilijua kuwa nimekuwa kiumbe kipya. Nilipofungua macho yangu, nilijihisi kama Adamu, pale alipoamka siku yake ya kwanza paradiso. Nilienda mlangoni na kuangaza macho hukuna kule; na kwa mara ya kwanza kila kitu kilionekana ni kizuri sana!

Lakini ni nani alinikokea moto na kunivika nguo mpya? Nilipoangalia, sikuona nyayo zozote kwenye barafu kuzunguka kile kibanda changu. Ghafla nilisikia ngurumo ya gari la Kim likija kuelekea kwangu kutokea barabarani. Alikuwa anarudi kutokea shuleni kwake. Tulikimbiliana na kukumbatiana. Nikasema, “Nimeshampokea Yesu!”
“Najua,” alisema. “Nilikuwa niko shuleni na Mungu aliniambia kuhusu jambo hilo. Kwa hiyo, vita kwa ajili ya wokovu wako imekwisha.”

Ndege mmoja alianza kuimba kwa sauti ya juu kuliko ndege wengine msituni. Alikuwa amesimama kwenye mlango wa kile kijumba ambako nilitokea kwenda kukutana na Kim. Sote tuligeukia upande ule na ndege yule aliruka na kwenda zake. Lakini palepale alipokuwa amesimama, kukawa na maneno yafuatayo: YOHANA 3:3.

Katika majira ya machipuko yaliyofuata katika mwaka uleule, nilibatizwa katika mto uleule ambako nilikuwa nakata barafu wakati wa baridi ili kupata maji ya kunywa. Pia, katika mwaka huohuo katika kipindi cha mapukutiko, nilioana na Kim na tukahamia kwenye nyumba kubwa zaidi. Sehemu ile kwenye mto ambako nilibatizwa ikawa ni sehemu maalum sana kwangu.

Kulikuwa na mambo mawili ya ajabu tangu niokoke ambayo siwezi kuyaelezea. Kwangu yalikuwa bado ni mafumbo. Mchungaji wangu katika Kanisa ambalo mimi na Kim tunaenda kuabudu aliniambia kuwa nimuulize Mungu moja kwa moja. Mara nyingi huwa naenda kwenye hiyo sehemu maalum, nakaa kwenye jiwe karibu na maji, kisha naanza kuomba.

Wakati fulani nilienda hapo na kuanza kuomba huku namwuliza Mungu, “Bwana, pale nilipokuwa mtumwa wa yule mchawi, na kupitia yeye nikawa nimepagawa na mapepo, kila kitu maishani mwangu kilikuwa ni giza na ndani yangu nikawa nimejawa na hofu. Lakini kwa namna fulani, kwa mbali kulikuwa na hii nuru, ambayo ni mimi tu nilikuwa naweza kuiona. Na kila nilipoitazama ile nuru, ilikuwa kila wakati inanipa amani.” Nilitamani kujua ile nuru ilikuwa ni nini. Kwa hiyo, siku moja nikawa namwuliza Mungu swali hili. Nilipokuwa nikimwuliza ile nuru ya gizani ni nini, ghafla msitu mzima ukawa kimya.  Ndege wote waliacha kutoa sauti; hakuna hata mmoja aliyelia! Pale nilikokuwa, ilikuja amani kubwa na maji kwenye kile kijito mbele yangu nayo yaliacha kutembea. Mkono wa mtu uliokuwa na joto, uliwekwa kwenye bega langu. Sauti nzuri na tamu sana kuliko asali ilianza kusema kwenye sikio langu kwamba, “Hata kabla hujanijua; hata wakati ulipokuwa unapita kwenye magumu, nilikuwa pamoja nawe. Ule Mwale wa mwanga ulikuwa ni Mimi …”

Nilihisi kuwa kulikuwa na nguvu kubwa sana ya Roho Mtakatifu. Nilianguka kifudifudi mbele za Bwana Yesu Kristo na kuanza kulia kutokana tu na furaha iliyozidi, na nikasema, “Baba Mungu, najua kile kilichotokea kabla hujaingilia kati na kunitoa kwenye kile chumba chenye baridi. Lakini, ni nini kilitokea pale nilipokuwa nimepoteza fahamu na kisha nikaja kuamka nikiwa nimeponywa, huku nimevikwa mavazi na kukawa na joto kwenye chumba? Kitu gani kilitokea nilipohisi mafuta ya moto na nikapoteza fahamu?”

Ile sauti ikasema nami tena kwamba, “Ni Mimi peke yangu ndiye niliyeyatoa yale mapepo na kukuponya. Halafu niliwaamuru malaika wakuoshe, wakuvike na kuwasha moto kwenye stovu ili upate joto.”

Nikasema, “Baba Mungu, nitafanya chochote unachotaka nifanye maana sasa ninajua kuwa Wewe ni Mungu pekee wa kweli.”

Akaniambia, “Nenda ukawaambie wengine kile nilichokutendea, ili kwamba na wao waamini kuwa ninakuja hivi karibuni.”

Kwa hiyo, hiyo ndiyo sababu ya mimi kuwapo hapa kwenye Jamhuri ya Cheki nikiwaambia kuwa kuna Mungu mmoja tu, naye ni Bwana Yesu Kristo. ‘New Age movement’, ambako nilikuwa mwanachama wa ngazi ya juu kule Marekani; na dini zote zile zilizopo, kwa mfano yoga na falsafa zingine, ni njia za uongo! Nawatangazia kabisa haya kwa mamlaka ya Bwana Yesu Kristo aliye Mungu wa kweli. Ndiyo, Yesu ni Mungu! Yeye ni ule uzima wa milele!

Mambo yote yanayohusiana na kupiga ramli, ambayo pia yanajumuisha kusoma nyota, kuangalia matufe ya kioo (crystal ball), timazi (pendulum), imani za siri (occult) na njia mbadala za tiba za kishetani; namna zote  kuwasiliana na pepo wachafu (séance), taamuli ya ruiya (transcendental meditation), kumwita Hare Krishna, ubudha na mengineyo mengi – yoye haya yataishia kukupeleka kwenye mauti ya milele. Yote haya ni ahadi za mapepo na ni uongo. Shuleni, mwalimu alipokuwa akinifundisha New Age, niliwekwa kwenye ngazi ya juu kabisa kati ya watu wengine waliokuwa wakijihusisha na ‘New Age’. Nilikuwa kwenye Baraza la Ulimwengu. Nilikuwa nikiwapa mafunzo viongozi wa kisiasa toka nchi zote. Najua kuwa ‘New Age’ inataka kuharibu wanadamu na kama Wakristo hawatasimama kuipinga, mataifa ya ulimwengu yatapoteza uhuru wake na kuangukia kwenye utumwa wa shetani. Sema kitu kupinga New Age – iwe ni mtaani, shuleni, kwa wanasiasa, n.k. Wape taarifa, waamshe watu kwenye jamii, maana ukitaka kuongea dhidi yake kiungwana na kwa upole, itaharibu nchi yako.

Mungu awabariki na asanteni kwa kunisikiliza.

…………………………………………..

Mpendwa msomaji wa blog hii, karibu tena wakati mwingine kwenye sehemu inayofuata ya ushuhuda huu. Bwana Yesu azidi kukubariki.

2 comments:

  1. Mmmmh!!!!!!!!! Mie Regy .....Kwa ushuhuda huu, kama bado humuamini Mungu, basi nadhani usubiri uwe mkuu wa wa New age Mungu akuonekanie, na sidhani kama kwako itatokea kama mume wa Kim, kwani kila mtu anampango madhubuti alio uweka Mungu kwa ajiili ya maisha yako, hivyo ndugu yangu amua leo nakazia Yohana 3:3, Yohana 3:5 hiyo ndio tiketi nyingine hakuna mpendwa, Mungu akubariki Kaka James kwa hii blog yako maana ni mafunuo makubwa Mungu amekupa kwa kweli.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Asante Regy. Bwana Yesu akubariki na aendelee kukuimarisha katika safari ya wokovu.

      Delete