Wednesday, February 26, 2014

Mwanafunzi wa mchawi - Sehemu ya 3




Katika Sehemu ya 1 na ya 2 tuliona jinsi ambavyo Jim McCoy aliingizwa kwenye vifungo vya kipepo na mwanamke mchawi (lakini kwa ridhaa ya McCoy mwenyewe); lakini akajikuta kwenye mateso mengi. Hatimaye Bwana Yesu alimhurumia na kumtoa kwenye vifungo hivyo.

Katika sehemu hii, McCoy anaendelea kueleza mbinu na hila zinazotumika leo duniani; ambazo shetani na maajenti wake wanafanya juhudi za kuzieneza kote duniani ili, sit u watu wanaomkataa Yesu, bali hata Wakristo waweze kunaswa katika mtego na kuishia jehanamu.


Huu ni ushuhuda wa Jim McCoy alioutoa siku nyingine katika semina aliyofanya kuhusiana na kundi au vuguvugu la New Age kule kwenye Jamhuri ya Cheki. Mambo anayoeleza yapo na yanaanza kuingizwa sehemu mbalimbali duniani kwa lengo la kuwatoa watu kwenye uwezekano wa kumkubali Yesu Kristo na kupokea wokovu wake; ili kwamba shetani apate nafasi ya kuja kutawala hapa duniani nan a hatimaye kupata watu wengi iwezekanavyo wa kwenda naye jehanamu. Kila mwanadamu amepewa nafasi ya bure ya kupokea wokovu wa Yesu Kristo. Je, una uhakika haujadanganywa? Unamsikiliza nani – Yesu au mwanadamu au dini?
 
New Age na Kanisa la Bwana Yesu Kristo

Kuna aya tatu ambazo Mungu alizitumia kuniweka huru toka kwenye utumwa wa kipepo (Yohana 3:3, Yohana 3:5, Yohana 3:16). Mungu alinifunulia aya hizi wakati nilipokuwa ndani ya kundi la New Age. Sikuwa najua chochote kuhusiana na Mungu. Kila mmoja wetu anatafuta majibu ya maswali yaliyomo mioyoni mwetu. Nami nilikuwa nikiyatafuta, matokeo yake nikaishia kudanganywa na kundi la New Age. Si hivyo tu, lakini niliweza kupanda ngazi hadi nikafikia uongozi wa juu kabisa, ndani ya kikundi ambacho hupanga mbinu za kuwadanganya watu, na hasa Wakristo. 

Nilikuwa nina bidii sana katika Baraza la Umoja wa Mataifa, linalojishughulisha na mipango ya kuwadanganya watu na kueneza mafundisho ya kundi la New Age duniani [Maelezo ya blogger: New Age au ‘Enzi Mpya’ ni mkusanyiko wa falsafa na imani mbalimbali kutoka dini mbalimbali zenye nia ya kuunda dini moja kwa ulimwengu wote kwa kisingizio cha kuleta maelewano na kuondoa mifarakano ya kidini, lakini msingi wake ni ushetani]. Kazi yangu ilikuwa ni kufundisha kweli za msingi za New Age duniani. Je, kundi hili ni nini? Mbinu gani wanatumia? Na ni hila ipi kubwa kabisa wanayotumia kuwadanganya watu?   Nitafafanua baadhi ya mambo haya.

Nilikuwa na diploma ya ufundishaji kuhusu New Age. Nilifundisha kwenye shule zilizoanzishwa na serikali, na lengo kuu la mafundisho hayo ni kuharibu kweli za msingi za Imani ya Kikristo. Je, hili litatokea kwa namna gani? Hili linafanyikaje? Nieleze kwa ufupi kuwa niliwafundisha watu kuongea na kutenda kama Wakristo ili waweze kuingia ndani ya wale wanaoishi katika ushirika wa Kikristo na kwenye makanisa ya aina mbalimbali ili hatimaye waweze kuwaangusha. Lakini Mungu ameninyakua kutoka kwenye kundi hilo na kwenye utumwa wa mchawi mmoja; na sasa ninafundisha kinyume na yale niliyofundisha mwanzo ili kuwaonyesha Wakristo malengo ya kundi hili, ambalo nilikuwa mwanachama mwenye bidii sana. 

Kwa kifupi, New Age ni nini? Ni mkusanyiko wa dini zote; matendo mbalimbali ya kidini, ambayo lengo lake ni kumfanya mwanadamu awe mungu. Ni mwavuli ambao chini yake dini zote zinaweza kujificha, ingawaje mafundisho yanaweza kuwa kinyume kabisa na Injili ya Bwana Yesu Kristo.

Yako mafundisho na dini ambazo asili yake ni ubudha, imani za siri za kishetani, uislamu, na hata baadhi ya dini ambazo zina mafundisho ya msingi ya Kikristo, kwa mfano kanisa la Moon na Mashahidi wa Yehova, Wana wa Mungu au kile kinachoitwa ‘Sayansi ya Kikristo’.

Ziko falsafa: Ukonfyushasi wa Kichina (Chinese Confucianism), imani za siri (occult) na mafundisho ya unajimu, mashamani, ma-guru, Krishna, n.k. Makundi haya na mengineyo yanatengeneza namna ya kundi moja ambalo kiini chake hasa ni ushetani. Nguvu zingine zote za kichawi na imani za siri zinatokea hapa. Pamoja na hayo, ni watu wachache sana waliomo ndani ya New Age wanaofahamu juu ya ukweli huu. Ndiyo sababu kuna Wakristo wengi walio kwenye kundi hili.

Kwa kuwa, kwa nje kundi hili linaonekana ni la kiutu na ni chanya, hiki ni kishawishi kwa Wakristo, na malengo yake yaliundwa kwa ajili hasa ya  Wakristo walio wanachama, ili kwamba wazimwe nguvu zao; na waweze kupelekwa mbali na Yesu Kristo na Injili Kamili. Baadhi ya mambo yanayofanyika ni yoga, kutoka katika mwili (astral projection), kuelea (levitating), namna zote za uchawi na upigani bao. Mambo haya ni vishawishi. Wanaanza kwa kufundisha kwamba Wakristo wanatakiwa kuwa wavumilivu kwa makundi mengine, kwa mfano, kwa ajili ya maslahi ya wanadamu na amani ya dunia. Maneno yanayohusiana na upendo yanaweza kuwadanganya kirahisi Wakristo wengi.

Ni kwa nini Wakristo hawatakiwi kujihusisha kabisa na New Age? Bwana amenituma mimi kwenye Jamhuri ya Cheki ili kuwaonya Wakristo. Mmeshapata uhuru wa kisiasa na wa wananchi; lakini unaweza kupotea na mnaweza kuwa chini ya nira na vifungo vya aina nyingine, kama hamtataka kuelewa kile ninachowaeleza. Haikuwa ni siasa iliyowaweka huru mbali na ukomunisti. Ulikuwa ni mkono wa Yesu Kristo uliozifanya siasa zile zibadilike. Bwana Mungu anataka niwaambie kuwa, kama Jamhuri ya Cheki haitaki kurudi kwenye uongozi wa Bwana Yesu Kristo, Mungu Aliye Hai, mtarudi kwenye utumwa ulio mbaya zaidi. Kama hautaki kuwasamehe wengine lakini wewe mwenyewe unataka kusamehewa, basi wewe utaingia kwenye hivi vifungo vipya. Wako watumishi wengi wa Mungu wanaokuja kwenye nchi yenu ambao watahubiri Injili. Lakini pia wako watu kutoka kundi la New Age, wanaojiita guru, ambao nao wanakuja. Na kama mtasikiliza mafundisho yao na kutenda yale watakayowafundisha, basi Bwana atageuzia uso wake mbali na nchi hii. Mungu ameniamuru nizungumzie hilo kwa sababu ni jambo la muhimu na zito sana kwa mtazamo wa Kibiblia.   

Nisisitize tena kwamba, matendo na mafundisho haya ya kundi la New Age yanaweza kuharibu nchi yenu, lakini baya zaidi ni kuwa, yanaweza kuharibu roho yako. Binafsi nimeshashuhudia Wakristo waliorudi nyuma na kumwacha Mungu aliye hai. Ziko njia nyingi na matendo mengi ambayo Wakristo huingizwa humo. Kwa mfano, yoga, na hasa hatha-yoga, ambayo inajumuisha mazoezi ya viungo na kupumua. Wako Wakristo wengi Marekani na kwenye nchi yenu ambao wanajihusisha na jambo hili.

Yoga ni nini? Ni mfumo wa vitendo vya kidini kwa ajili ya mtu kurudi tena baada ya kufa (reincarnation). Neno la Mungu linasema kuwa: Na kama vile watu walivyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu (Ebr. 9:27). Hakuna mtu anayeweza kurudi tena duniani kwa njia nyingine baada ya kufa.  Yoga asili yake ni Uhindu, na ni mfumo wa vitendo vya dini nyingi. Vitendo hivi vinaaminika kuwa vinavunja nira kwenye maisha yako, ambazo, kwa imani zao, zitaanzisha mchakato wa “kuzaliwa tena baada ya kufa”. Kwa hiyo, kupitia yoga, tunafungulia mlango kwa mapepo ya Kihindu.

Wakristo walegevu husema kuwa hawaamini juu ya mambo hayo bali kwamba hatha-yoga ni mazoezi tu mazuri kwa ajili ya mwili. Kwa kusema hivyo, tayari wameshaamini uongo wa ibilisi. Shetani atakuruhusu ujenge mwili wako, na kujisikia vizuri, maana anajua kuwa Wakristo kama hao hawawezi kuona kilicho nyuma katika ulimwengu wa roho.  Ni nini basi kitatokea? Matokeo yote ya kimwili na kiroho yanajengwa juu ya nguvu iitwayo Shiva. Hili ni pepo la Kihindu, ambalo wanalifungulia mlango.

Katika upande wa chini wa uti wa mgongo wetu, kuna nafasi wanayoiita “nguvu ya nyoka”. Unapofanya mazoezi ya yoga, unakuwa kimsingi unasujudu kwa huyu Shiva; ile nguvu ya nyoka inaamshwa kwenye mwili wako. Inapokuwa kubwa, watu wanapata na uwezo fulani usiokuwa wa kibinadamu.

Mambo haya hayatoki kwa Mungu aliye hai. Asili yake ni kwenye ulimwengu wa giza wa kipepo. Kwa hiyo, kumbuka kuwa mambo yote tunayofanya kimwili wakati wa yoga yana asili ya ulimwengu wa giza wa kipepo; haijalishi tunafikia ngazi gani. Hata hatua za kwanza kabisa zinakuwa zinaelekea kwenye vifungo hivyo – tuwe tunakubaliana au hatukubaliani.

Namna ya pili ambayo ni kishawishi kwa Wakristo, hata walio makanisani – na imeenea sana nchi za magharibi – ni  “kutoka nje ya mwili” (astral projection). Hii ni aina ya mazoezi ambayo yanaweze kufanya roho ya mtu ikatengana na mwili. Kwa uamuzi wako mwenyewe, unaweza kupeleka roho yako kwenye mahali au wakati wowote, kwa mfano ukarudi nyuma ya wakati kwenye maisha yaliyopita, ukaenda kwenye anga au kokote kwingineko.

Mara nyingi hili linawezekana, lakini ambacho watu wa namna hii hawatambui ni kuwa, roho zao zinakuwa haziingii kwenye ufalme wa Mungu bali wa mapepo. Nilipokuwa niko chini ya kifungo cha yule mchawi katika kundi la New Age, nilifanya ‘astral projection’. Roho yangu ilikuwa ikipelekwa kwenye ngazi mbalimbali na aina mbalimbali za ulimwengu.

Kwa njia hii, unafungulia mlango kwa viumbe wengine wa kiroho wasioonekana. Shetani ameweka tayari mtego wake kwa ajili yako pale. Watu wanapoanza kufanya mambo haya, kwa mara ya kwanza wanakuwa na hisia nzuri za kunyanyuliwa. Hisia hizi zinatoka kwenye asili ya dhambi. Kuna hatari kubwa hapa. Kwa kitambo kidogo unakuwa unaweza kuitawala hali hiyo, lakini baada ya kufikia mahali fulani, unaanza kupoteza udhibiti wa mwili wako na unakuwa ni uwanja wa mapepo kufanya kila watakacho. Wengi walipoteza hata uwezo wao wa kurudi.

2 comments:

  1. Mtumishi James nakusalimu katika Jina la Yesu. Asante kwa ushuhuda mkubwa kwa mara nyingine. Ni hatari kwa walio ndani ya kanisa kuliko aliye nje katika zama hizi za mwisho. Watu ndani ya kanisa wamevamiwa na roho za mazoea na hivyo ni rahisi tu kumuona shetani akiwachezea na hata kuwavika hofu ya kuzimu na mauti.

    Mfano mahali pale Sauli mfalme na jeshi lake wamekaa kwenye mlima upande mmoja na Goliati ajenti wa shetani kwenye mlima upande mwingine (1Samweli 17) na katikati kuna bonde la Ela na shetani analitumia bonde hili kila siku asubuhi na jioni kulitukana kanisa na kulitia hofu kwa SIKU AROBAINI maajabu sana.

    Mpaka anatokea Daudi asiyezoelea, asiyeenda vitani kwa mazoea maana naye walitaka kumpa SILAHA walizozizoea. Yeye alitumia Neno la Mungu na nguvu ya Mungu akimwangusha shetani na majeshi yake.

    1 SAM. 17:45-47 SUV

    "Ndipo Daudi akamwambia yule Mfilisti, Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la BWANA wa majeshi, Mungu wa majeshi ya Israeli uliowatukana. Siku hii ya leo BWANA atakuua mkononi mwangu, nami nitakupiga, na kukuondolea kichwa chako, nami leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya majeshi ya Wafilisti, ili kwamba dunia nzima wajue ya kuwa yuko Mungu katika Israeli. Nao jamii ya watu wote pia wajue ya kwamba BWANA haokoi kwa upanga wala kwa mkuki; maana vita ni vya BWANA, naye atawatia ninyi mikononi mwetu."

    Ni maombi yangu ya kuwa tuache mazoea, Mungu wetu anatupenda na anatumia kila aina ya anachoweza kuona tunafika kwake tukiwa salama tena bila madoa wala mawaa. Tunapata kuona ukuu wa Mungu kwa namna mbalimbali kama huu lakini shida yetu ni mazoea mazoea. Kwa hili tutaadhirika hapa duniani na mbinguni pia.

    Unaona Daudi hakuadhirika kwasababu alikataa mazoea akamwambia mfalme. 1 SAM. 17:39 SUV

    "Naye Daudi akajifunga upanga juu ya mavazi yake, akajaribu kwenda; maana alikuwa hajavijaribu. Daudi akamwambia Sauli, Siwezi kwenda na vitu hivi, maana sikuvijaribu. Basi Daudi akavivua."

    Daudi alipata heshima hapa duniani na mbele za Baba wa Mbinguni hata leo. Mungu ametuwekea vyote hivi, hivyo basi tulitafute Neno na kulijua hatimaye hatutakaa na kujiingiza kwenye mashimo ya shetani ya mfano wa "new age" barikiwa sana mtumishi James kwa utumishi huu.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Amen, amen brother Kishiwa. Asante sana na Bwana Yesu azidi kukuinua katika hekima na maarifa yote.

      Delete