Jim McCoy alikuwa ni mwanafunzi wa mchawi mkubwa wa Kimarekani. Ufuatao
ni ushuhuda wake ambao aliutoa kwenye mkutano kuhusiana na
New Age, kule Jamhuri ya Cheki kwenye mwaka 1995, miaka michache baada
ya kuanguka kwa ukomunisti.
Bwana alimwambia, “Nenda kawaambie na wengine
kile ambacho nimekutendea wewe, ili kwamba waweze kuamini kuwa ninakuja tena
hivi karibuni.”
……………………………………
Jina langu ni Jim McCoy. Nilizaliwa na
kukulia kwenye jiji dogo kule Marekani. Wazazi wangu hawakujua sana habari za
Mungu. Kwenye nyumba yetu hatukuzungumzia habari za Mungu hata kidogo. Hata hivyo, nilikuwa nina njaa fulani ya ajabu
ndani yangu – nilitaka kujua maana hasa ya maisha. Kwa hiyo, niligeukia kwenye
dunia na kila kitu inachotoa, ili niweze kushibisha njaa hiyo. Kwa njia hiyo,
niliweza kukutana na kila aina ya imani na dini. Na kwa kuwa sikujua chochote
kuhusu Ukristo, na wala sikujua ukweli wa Biblia, nilifanya mambo ambayo
nilidhani mtu anatakiwa kuyafanya; huku nikiamini kuwa kufanya hayo ndio
kumtafuta Mungu. Ilikuwa ni shauku ya kuijua kweli. Lakini, kila dini niliyojihusisha
nayo iliniacha nikiwa na utupu ndani yangu. Nilijihusisha na yoga, uhindu,
ubudha, voodoo, uchawi, ‘humanism’ (yaani falsafa inayozingatia zaidi mawazo
binafsi ya binadamu na ushahidi wa kisayansi kuliko Imani za kidini) – na zote
hizi ziliniacha mtupu kabisa ndani yangu!
Nilikuwa pia nina matatizo makubwa
maishani mwangu. Siku moja wazazi wangu
walifikia mwisho wa uvumilivu na kuamua kunifukuza nyumbani. Nilikuwa sina
msimamo na mara kwa mara nilikuwa ninatafuta kazi mpya. Pia nilibadilisha
marafiki zangu wa kike mara kwa mara.
Nilihamia sehemu nyingine Marekani
nikidhani kwamba hii ingenisaidia. Kwa hiyo, nilikuja hadi New York. Hapo nilikutana
na mtu kazini kwangu ambaye sitamsahau. Aliniambia kuwa alikuwa anamjua
mwanamke mmoja ambaye alikuwa ana majibu ya maswali yote kwenye maisha yangu.
Jina lake lilikuwa ni Nels. Alikuwa ni mchawi aliyesajiliwa na serikali.
Wanawake kama huyu wanajulikana duniani
kote kupitia chama chao cha OSN na kazi yake ilikuwa ni kuwafundisha watu
maarufu mbalimbali ili waungane pamoja katika dini hii moja. “Shule yake ya
kidini” ilikuwa kwenye sehemu moja inayokaliwa na Wahindi. Nilipoingia pale,
nilishangazwa na idadi kubwa ya vijana waliokuwa wakitabasamu na kuonekana
wenye furaha. Hata hivyo, ndani ya macho ya watu hawa kulikuwa na namna fulani
ya utupu.
Wakati ule sikugundua kuwa ile ilikuwa ni
ishara ya maonyo. Nilimwomba yule mwanamke kama ningeweza kukaa pale kwake na
kuwa chini yake. Sikuwa na fedha za kutosha pale kama wanafunzi wengine.
Aliniambia kuwa naweza kukaa lakini kwa masharti kuwa niwe mfuasi wake, na
kwamba nitakuwa nikijifunza kila kitu ambacho wanafunzi wake walikuwa
wakijifunza.
Siku moja alinijia na kuniambia, “Roho
inayoniongoza imeniambia kuwa sasa nikufanye kuwa mfuasi wangu.” Nilikubaliana
na hili. Alinipeleka kwenye nyumba yake. Nyuma ya nyumba kulikuwa na maktaba
yake binafsi. Katikati ya chumba hiki kulikuwa na meza ya umbo la pembetano.
Ukutani kulikuwa na vitabu vingi kuanzia sakafuni hadi darini. Vilikuwa
vinahusu jinsi ya kila aina ya ‘occult’ (imani za siri za kishetani) pamoja na mafundisho
mbalimbali ya ‘New Age’ (aina ya dini inayochanganya imani za mashariki ndani yake).
Baadhi ya vitabu vilionekana ni vya zamani sana. Viliandikwa kwa mkono na
wachawi wa kutoka zamani sana – miaka mia mbili au mia tatu nyuma katika nchi
za Ulaya. Nilifungiwa ndani ya jengo lile na niliruhusiwa kuonana na yeye tu.
Ilipofika siku ya thelathini, alikuja na kuniambia kuwa ile ‘roho inayomwongoza’
imemwambia kuwa na mimi pia natakiwa kupewa roho ya kuniongoza.
Tulienda mahali fulani nje ambalko
kulikuwa na kijumba kidogo. Kilikuwa ni namna ya madhabahu yake, ambako hakuna
aliyeruhusiwa kuingia isipokuwa yeye; na hapo ndipo alipofanyia uchawi wake.
Mara tu alipofungua mlango, niliweza kuona kwa macho yangu ya nyama kwamba
kulikuwa na kitu fulani kilichofunika mahali pale. Tulipoingia, nikagundua kuwa
hakukuwa na madirisha. Katikati ya chumba kile kulikuwa na meza yenye viti vine
na kimoja kilikuwa kikubwa – tuseme ndiyo kama kiti chake cha enzi. Akakaa
pale. Mezani kulikuwa na tufe la kioo. Alikaa kwenye kiti na kunikaribisha
ndani.
Aliniambia kuwa, atakapofanya mambo
fulanifulani – ambayo sikuyaelewa – lile tufe la kioo litaanza kung’aa; mwanga
wake utakuwa unawake na kupungua. Kisha hiyo ‘roho’ itajidhihirisha. Akaniambia
kuwa roho hii itaniambia kuwa imekuja kutokea kwenye maisha yangu mwenyewe na
kwamba itakuwa ikinisaidia. Na akaniambia pia kuwa, hiyo roho itakapokuja, natakiwa
kusema “Ndiyo.” Nikakubaliana naye. Akaanza kuimba. Ghafla, mlango wa nyumba
ile ukajifunga wenyewe. Tulikuwa ndani humo wenyewe tu. Lakini bado humo ndani
niliweza kusikia sauti nyingi na sikujua zinatokea wapi. Ilikuwa ni ajabu sana.
Baadaye aliniambia kuwa hizo zilikuwa ni sauti za watu waliokufa ambao roho zao
zilikuja kutokea ulimwengu wa chini. Mara tu alipoanza kuimba, kweli lile tufe
likaanza kung’aa na kupunguza mwanga. Ghafla, ile roho ikaanza kujidhihirisha
kutokea kwenye lile tufe. Ikaniuliza kama inaweza kuingia ndani yangu.
Nikajibu, “Ndiyo,” hivyo ikaingia.
Kuanzia hapo nilipoteza kabisa uwezo wa
kujidhibiti mwili wangu. Kuanzia hapo, kila nilichosema, nilichowaza na
nilichotenda, sikuwa na udhibiti nacho tena. Hii ilifungua mlango kwa mapepo
mengine mengi, ambayo nayo yaliniingia. Nikawa nimepagawa kabisa na pepo.
Nikawa ni roboti tu ya ‘New Age’. Kila alichoniambia mwalimu wangu ndicho
nilichokitenda.
Wakati fulani alinionyesha familia moja
iliyoishi jirani. Aliniambia, “Unamwona yule binti?” Nikasema, “Ndiyo.”
Akasema, Yeyote atakayemwoa, atapewa moja ya tatu ya urithi kutoka kwa wazazi
wake.” Mwalimu wangu alikuwa anawazia kile ambacho binti huyo angepewa kama
mahari kwa vile alikuwa ni binti wa familia ya kihindi. Akaniambia, “Nataka
umwendee, mpendane na kisha umuoe.” Hata katika hili, nilitii. Nilienda na
kufanya vilevile. Kisha mali ile ililetwa kwangu. Lakini familia ya yule binti
haiukukubaliana na hilo. Ndiyo maana mwalimu wangu aliniambia nimpeleke yule
binti kwenye mji wangu. Alidhani kuwa wazazi na ndugu wa binti hawatapinga
hilo. Nilifanya hivyo. Pale kwenye mji wangu, ulifika wakati ambapo mahali ile
ilitakiwa kuandikwa kwa jina langu.
Siku moja ilitokea kwamba nikapoteza zile
nguvu zangu na lile pazia la kifungo cha kipepo likawa limepasuka katikati.
Mara moja nikarudi kwenye hali ya kawaida kama awali na nikaweza kufikiri na
kufanya maamuzi mwenyewe. Nilitambua kuwa hali hii ingekuwa ni ya muda mfupi
tu; ilikuwa ni jambo la saa chache. Ilinibidi nichukue hatua haraka. Mara moja
nilimpandisha binti yule kwenye basin a kumrudisha kwao, huku nikimpa barua
apelike kwa wazazi wake, ambamo nilieleza jinsi ambavyo kukutana kwetu
kulivyoanza hasa; na kwamba yote hii ilikuwa ni mipango ya mwalimu wangu. Mara
moja niliamua kumpa talaka. Niliporudi kwenye nyumba yangu, nilianza kujisikia
hasira kali sana dhidi yangu mwenyewe. Nilijua kuwa nimekosa utii kwa mwalimu
wangu – mchawi.
Nilikaa mezani na sikutaka kumsikia mtu
yeyote. Nilijua kuwa, kwa uasi huu nilikuwa nimejiweka kwenye matatizo makubwa.
Nikaanza kulia. Nikaanza pia kusikia sauti za wazi ya roho fulani ambayo
ilikuwa inaongea na mimi. Ikazema, “Ewe
mjinga! Vyovyote iwavyo, mwalimu wako, ambaye ni mtu wangu, bado
amekushikilia.” Ghafla nilikaanza kuhisi kuwa ile roho ilikuwa ikinishambulia.
Nikashika kisu kilichokuwa mezani. Lakini ile roho ikaanza kunishambulia kwa
kutumia kile kisu. Ilininyanyua juu kutoka kwenye kiti; ikaanza kunitoa kwa
nguvu nje ya nyumba na ikawa inaniburuta kuelekea kwenye gari. Nikaanza kupiga
kelele kuomba msaada.
Hatimaye ile roho ilinifikisha kwenye gari
na kuliwasha. Ikaanza kuniendesha kuelekea nje ya mji hadi kwenye bwawa fulani.
Tulipofika pale, gari lilisimama ghafla nami nikatupwa nje ya gari lile. Kisha ile
roho ikaanza kuniburuta kuelekea kwenye maji. Wakati ikiniburuta, nikaanza tena
kupiga kelele kuomba msaada, na wakati huohuo nikamwita Mungu anisaidie.
Wakati ikiniburuta kuelekea kwenye maji, ilinisababishia
maumivu makali sana na kuhatarisha maisha yangu kwa kile kisu ambacho nilikuwa
nimekishikilia mkononi mwangu. Iliniambia kuwa itakuwa ikinitesa. Nilitambua kuwa
ilitaka kunizamisha majini.
Tulipofika umbali nusu kati ya gari na
maji, nilipaza sauti, “Mungu, kama upo, tafadhali nisaidie!” Hapo, alitokea
mbwa mkubwa upande wa majini na akaanza kukimbia kuelekea kwangu. Mbwa huyu
alipokuwa karibu kabisa nami, nilihisi hii roho ikiingia ndani ya mwili wangu, (kana
kwamba ilikuwa ikimwogopa yule mbwa). Mbwa yule aliniuma kwenye mkono uliokuwa
umeshikilia kile kisu. Kisu kilidondoka chini. Sasa mbwa alikuwa akinisukumia
majini; na tukawa sote kwenye maji. Mbwa yule akawa ananivuta kuelekea kwa
binti mmoja ambaye alikuwa amesimama kwenye maji huku mgongo wake umeelekea
kwangu. Leo binti yule ni mke wangu.
Nikiwa nimesimama pale, sikuweza hata
kusogea. Kim, ambalo ni jina la mke wangu leo, alikuwa amesimama pale kwa muda
akiwa anamwomba Mungu. Aligeuka na kuniona mimi; kisha akanigeuzia tena mgongo
na akawa anamwambia Mungu jambo. Baada ya hapo alinijia. Sijui alikuwa
akiniambia nini, lakini palepale nilijua kuwa nimepona. Baadaye alikuja
kuniambia kuwa alikuwa akishindana na Mungu katika maombi kwa habari ya mahusiano
aliyokuwa nayo na mwanamume mmoja, ambayo yaliishia kuvunjika. Wakati huo
alishafikia ukomo. Alikuwa amesimama pale kwenye maji huku akimwita Mungu na
kumwambia, “Bwana Yesu, niletee mwanamume ambaye atakuwa mume wangu.” Mara alipomaliza
kuomba hivi, ndipo alipogeuka na kuniona mimi nimesimama pale majini.
Kwa upande wake, aliona ni tu kitu
kinachofanana na mwanamume au mzimu wa mwanamume, lakini si mtu aliyekuwa akimtarajia
moyoni mwake. Alimgeukia Mungu na kulia kwa sauti, “Mungu, sidhani kama
unamaanisha kuwa huyu ndiye mwanamume mwenyewe!”
Kusema kweli nilikuwa ninatisha. Ilikuwa ni
mateso hata kunitazama. Nilikuwa na nywele ndefu, fulana ya ngozi, sina shati,
kifuani nimejaa michoro ya kishetani na shingoni mwangu nimening’iniza tufe la
kioo, huku miguuni nimevaa viatu vinavyonuka.
Aliponiangalia, aliona kuwa nilikuwa nina
saratani kinywani mwangu, ambayo ilisababishwa na kutafuna tumbaku. Alianza kutembea
kuja kwangu kwa sababu tu alikuwa akimtii Mungu kwa nguvu sana; maana, mara tu
aliponiona, moyoni mwake hakutaka kamwe kujihusisha nami kwa namna yoyote ile. Tulianza
kuzungumza. Hatimaye, alihisi kuwa kuna muunganiko fulani kati yetu, ambao
uliletwa na Roho Mtakatifu.
Alinichukua hadi nyumbani kwa wazazi wake.
Alipofungua tu mlango na kunitambulisha kwao, baba yake alishtuka sana; maana
yeye alimwambia, “Baba, ona ni nani nimemleta nyumbani kwetu.” Baba alibamiza
mlango na kwenda kwenye simu na kuwaita baadhi ya ndugu waje kuomba, maana
binti yake alileta nyumbani kitu cha kutisha. Kim alikuwa ndiye mtu pekee
aliyezungumza nami. Mimi nilijua kuwa, kwa sababu ya ile saratani, nilikuwa
ninaelekea mautini polepole.
Nilipoteza kila kitu na sasa nilikuwa
naishi mtaani. Hata hivyo, bado nilikuwa najihusisha na ‘New Age’. Kwa upande
mwingine, Kim alikuwa bado akiongea nami kuhusiana na Mungu na Bwana Yesu. Nilimpinga
kwa kutumia nadharia zangu nilizojifunza, na nilikuwa mbishi sana.
Katika nchi ile na mji ule nilikokuwa
nikikaa, kuna wakati kilikuja kipindi cha baridi kali mno. Sikuwa na mahali pa
kuishi. Nilimwendea Kim na kumwuliza, “Niende wapi sasa?” Wazazi wake walikuwa na
kibanda cha magogo kwenye msitu katika eneo la karibu la New Eucher kwenye
mbuga ya wanyama. Lilikuwa ni eneo la upweke sana msituni takriban kilometa 22
(maili 13) kutoka mjini. Hakukuwa na umeme wala maji. Chanzo pekee cha joto
kilikuwa ni stovu. Tarehe moja Januari, ilianguka barafu nyingi sana ambayo
ilirundikana ardhini kwa kiasi cha sentimeta 180 (takriban furi 5), huku mimi
nikiwa pale peke yangu. Kim alikuwa anakuja kuniangalia wakati wa wikiendi tu. Muda
mwingine wote alikuwa shuleni.
Ndani ya kibanda kile kulikuwa na vyumba
viwili. Nilitakiwa kutumia chumba kidogo. Kim anapokuja, alitumia kikubwa. Alinihudumia;
na alizungumza nami kuhusiana na Bwana Yesu. Alikuwa ndiye mtu pekee niliyemjua
kwenye eneo lile. Ilinibidi kutembea kilometa ipatayo moja kwenda kukata pande
la barafu iliyokuwa imeganda kwenye mto ili niweze kupata maji. Pia nilitembea
msituni nikiwa na msumeno ili niweze kutengeneza moto. Sikuwa na fedha za
kununulia chakula. Kulikuwa na upweke mkubwa sana pale msituni. Sikuwa na gari
la kuniwezesha kufika mjini. Kim alikuwa akiniletea chakula kila wikiendi. Ilikuwa
ni maziwa na namna fulani ya maandazi na nilikula mara mbili tu kwa wiki.
Kwa sababu sikula mara kwa mara na
nilikuwa pale peke yangu tu, nilikuwa zaidi chini ya nguvu za mapepo. Hivyo,
afya yangu ilikuwa ikiharibika siku hadi siku. Nilidhoofika sana kiasi kwamba
nilibakia tu kitandani nisiweze kutoka. Kim alitaka kunipeleka kwa daktari,
lakini tayari Mungu alishamwambia, “Hapana!” Mungu alitaka kuniokoa kwa njia
nyingine.
Jumapili moja nilikuwa mgonjwa sana kiasi
kwamba nilijihisi ninakufa. Bwana alishamwambia Kim kuwa hataki arudi tena
kwenye kile kibanda hadi atakapomwambia. Mchakato wa mabadiliko yangu ulikuwa
umeanza. Kim alikuwa ananiacha huku analia na akarudi zake shuleni, ambako ni
mbali. Mungu alikuwa anaanda mpango wake mwenyewe. Kabla Kim hajaondoka,
alinikokea moto. Sikuwa naweza kutoka kitandani, na nje tayari kulikuwa na
baridi nyuzijoto 20 chini ya sifuri. Hakika, hapa ndipo nilipoachwa peke yangu
kabisa.
Moto ule uliisha baada ya muda mfupi tu. Sikuwa
na nguvu za kuinuka na kuukoleza tena. Niliathiriwa na baridi na mwili wangu
ulidhoofika zaidi na zaidi. Nilikuwa nakufa polepole. Chumba kiliendelea kuwa
baridi zaidi na zaidi, huku nikihisi uvuli wa mauti nao ukinifunika.
Nikiwa nimelala pale bila msaada, nilianza
kuhisi kuwa roho yangu na mwili wangu vilikuwa vinatengana. Hofu kuu
iliniangukia. Zile “kweli” zote nilizokuwa napokea hadi wakati huo, ghafla
niliziona kama ni uongo na nikatambua kuwa niliishi katika ubatili mkubwa.
Ghafla niliona kwa macho yangu kabisa hapo
pembeni mwa kitanda shimo refu limefunuka na nikaiona kuzimu. Mara moja chumba
kilijaa harufu ya kiberiti (Ufu 21:8) na miili ya watu iliyoungua; na nikasikia
vilio vya kutisha vya maelfu ya watu vikitokea kwenye lile shimo. Walikuwa ni
makundi kwa makundi ya watu wakilia kutokana na mateso. Roho yangu ilianza
kushuka kwenye lile shimo.
Nilianza kupiga kelele kwa sababu papohapo
nilitambua kuwa naenda kuishi milele kuzimu. Hapo pia, mafundisho, mahubiri na
shuhuda zote alizokuwa akinipa Kim zikawa wazi kabisa. Niliweza kuona wazi akilini mwangu. Kwenye ukingo
wa kuzimu, Mungu alianza kumwagilia ile mbegu ndogo ya Neno la Mungu ambalo Kim
alinieleza. Wakati huo nilitambua kuwa Biblia, ambayo ilikuwa pembeni tu yangu
ambayo Kim aliiacha pale kabla ya kuondoka, ilikuwa na kitu kuhusiana na hali
yangu kuwa bora; na kwamba, ni kwenye kitabu hicho tu ndimo penye wokovu pekee.
Nilikuwa na mshumaa mdogo kwenye kile
chumba kwa ajili ya mwanga. Mwangaza wa kutoka kwenye shimo la kuzimu haukuweza
kuangaza chumba kile. Kwa hiyo nikawa natafuta kwa mkono wangu ule mshumaa na
kiberiti viliko. Pia nilinyoosha mkono ili nichukue ile Biblia. Mara niliponyoosha
mkono kuelekea kwenye Biblia, yakatokea makucha ambayo yalinikamata mkono wangu
na kunizuia. Ghafla chumba kilijawa na namna fulani ya uwepo wa mamlaka ya
kipepo; na sauti moja nzito sana ikaniambia, “Mjinga wewe! Mbumbumbu wewe! Uliamini
kila kitu nilichokwambia na ndio maana sasa wewe ni mali yangu!” Kisha ile roho
ikaweka mkono wake kifuani pangu.
Kutokana na kukata tamaa, nilianza kulia,
maana roho yangu ilikuwa inaendelea kuelekea chini kuzimu bila uwezo wa
kujizuia. Sasa mwili wangu na roho yangu
vilishatengana. Nikawaza, ni lazima nipate njia ya kusimamisha hali hii. Ufahamu
wangu ulikuwa bado upo, na nikajua kuwa natakiwa mara moja kumpokea Yesu Kristo
kama Bwana na Mwokozi wangu, kama ambavyo Kim amekuwa akiniambia. Nilijua kuwa
hilo lilitakiwa kutendeka kabla roho yangu haijatengana daima na mwili wangu,
na kabla haijavutwa kuingia kabisa kuzimu. Shetani naye alijua hilo pia. Ilikuwa
ni vita kwa kweli katika kila sehemu ya sekunde. Nilihisi kuwa Mungu alikuwa
upande wangu na alikuwa akinitia nguvu ili niweze kuifikia tena Biblia. Nilihisi
wazi kabisa kuwa kuna nguvu ya Mungu kwa ajili ya tendo hili. Kwa hiyo
nilijaribu kwa mara nyingine tena.
……………………….
Mpendwa msomaji wa blog hii, nini
kiliendelea baada ya hapo. Karibu ufuatilie ushuhuda huu kwenye sehemu ya 2
katika toleo linalofuata. Bwana akubariki na kuzidi kukutia nguvu katika safari
yetu ya kiroho, ambayo iko kwenye ukurasa wa mwisho wa majira na nyakati.
No comments:
Post a Comment