Dada
Liyan ni mwenyeji wa China. Bwana alisema naye kwa njia ya maono na hata
kumpeleka mbinguni na kuzimu. Anayo mafunuo mengi ya muhimu sana ambayo
tunayahitaji mno, hasa katika nyakati hizi za mwisho. Tafadhali fuatana naye
katika ushuhuda huu muhimu na Bwana atasema na moyo wako kwa namna ya ajabu
sana.
……………………..
Hivi
karibuni nimekuwa nikipata maono mengi kutoka kwa Mungu.
Hebu nianze
kukushirikisha yale ambayo nimeyaona kwenye miaka michache iliyopita.
Tangu
1996, nimekuwa nikimjua Bwana, na nimekuwa nikiona ukweli wake. Mimi nimekulia
kwenye familia ya Kikristo, huku nikimwamini Yesu Kristo, lakini kusema kweli
sikuwa nikimjua kiukweli. Kuwa na imani katika Yesu ni tofauti na kumjua Yesu.
Katika 1 Samweli 3:7, licha ya kukulia kwenye Hekalu, Samweli hakumjua Bwana.
Kama ilivyokuwa kwa Samweli, mimi nami sikumjua Bwana hadi mwaka 1996
nilipokuwa na umri wa miaka 16.
Tangu
nilipokuwa mtoto, nilikuwa nina matatizo ya kiafya, tofauti na mama na dada
yangu. Mama yangu ni mtu mwenye bidii sana nyumbani na hata kazini. Mara nyingi
alinikasirikia kutokana na kuumwa kwangu kila wakati, na hakujua ni kwa nini
nilikuwa hivyo, ilhali dada yangu alikuwa ni mtu mwenye afya tu. Nyumbani sikuweza
kusaidia kazi yoyote, hata kupika, maana nilikuwa nikianguka na kupoteza fahamu
mara kwa mara. Madaktari hawakuweza kugundua ugonjwa wangu hadi nilipofanyiwa
kipimo cha CT scan, ambacho kilionyesha kuwa nilikuwa na magonjwa sugu ya gastritis, sinusitis, na periostitis. Lakini hata
baada ya ugunduzi huo, madaktari hawakuweza kunitibu. Magonjwa haya yalinizuia
kuwa wa msaada pale nyumbani. Kwa hiyo, hata mama yangu aliniona sifai, jambo
ambalo liliyafanya maisha yangu kuwa machungu hata zaidi.
Nilipofikisha miaka 16, nilikuwa
bado ziwezi kusaidia kazi za nyumbani. Kwa hiyo, mara kwa mara mama yangu
alinitishia kwa kusema, "Kama
utakufa, basi ni bora ufe tu mapema utupunguzie matatizo. Hebu jiangalie. Huna
maana yoyote kwenye dunia hii. Huna uwezo wa kuyaondoa maisha yako wala kuishi
maisha mazuri. Tukufanyie nini sasa?” Hata
mimi mwenyewe nako sikuwa na jibu. Kuanzia hapo, nilianza kumwomba Mungu: "Ee
Mungu, kama kweli wewe upo, tafadhali nisaidie kuondoa uhai wangu hapa
duniani.” Mara nyingi niliwaza juu ya kujiua – kwa mfano kwa kujinyonga,
kunywa sumu na kuruka kutoka kwenye ghorofa – lakini kila mara wazo la kujiua
lilinitia hofu. Nilikuwa nikiwaza, “Vipi
kama nitajaribu halafu nisife?” Nilijua kuwa, kama hilo litatokea, basi
hali yangu itakuwa mbaya zaidi. Kwa hiyo, sikujaribu kujiua. Baadaye
nilikumbuka jinsi Biblia inavyosema, “Kama mtu
akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la
Mungu ni takatifu, ambalo ni ninyi.” [1 Kor. 3:17]; kitu
kinachomaanisha kwamba mtu akijiua hawezi kuokoka.
Tarehe
1 Juni, sikufanya maombi yoyote maalum, lakini nilisema tu, "Mungu,
kama wewe kweli upo, tafadhali niondolee uhai wangu Bwana; tafadhali pokea roho
yangu." Mama yangu alipoondoka saa 9:30 mchana kwenda kazini, nilipiga
magoti pembeni mwa kitanda changu na kuendelea kuomba. Ghafla, roho yangu
ilitoka kwenye mwili na nikawa nauona mwili wangu ukiwa unaendelea kuomba
lakini ukaanguka. Roho yangu ikaendelea kuwapo pale. Wakati huo, sikuwa
ninaogopa. Badala yake, nilijisikia tu vizuri kwa kuwa sasa sikuwa nahisi tena
maumivu yoyote au kuumwa na kichwa. Hapo nilielewa pale Biblia inaposema kuwa
roho ndiyo itiayo uzima na mwili haufai kitu (Yohana 6:63). Sikujisikia kuwa
nauhitaji tena mwili wangu badala yake nikawa najisikia vizuri sana.
Roho
yangu ilipotoka kwenye mwili, nilijua hakika kuwa naenda
mbinguni; maana
nilidhani kuwa wale wanaomwamini Yesu wana uhakika wa kwenda mbinguni baada ya
kufa. Pia niliamini kuwa njia ya kwenda mbinguni inaelekea juu huku ile ya
kwenda kuzimu ikieleka chini. Roho yangu ilipaa na kutoka nje kupitia dirishani
na ikaendelea kupaa kwenda juu mbinguni. Ah! Kulikuwa kuzuri mno! Nilikuwa
naelekea mbinguni! Sikujisikia kuwakumbuka familia yangu hata kidogo.
Giza la Nje
Kisha
roho yangu ilienda kwenye sehemu yenye giza. Giza la pale ni tofauti na giza la
hapa duniani. Giza hilo litaishtua roho yako kiasi kwamba hutaweza hata kuiona
mikono yako hata kama ukiiweka karibu kabisa na macho yako! Nilikuwa na uhakika
kabisa kwamba hapa hakukuwa mbinguni, japokuwa sikuwa nimewahi kwenda huko. Nilijua
kuwa mbinguni hakutakiwi kuwa na giza; kunatakiwa kuwe kumejaa nuru. Niliwaza, “Hapana!
Ina maana hapa ni kuzimu?” Sikuweza kujua pale ni mahali gani maana
nilipokuwa mdogo nilisikia kuwa kuzimu kuna moto; lakini hapa hakukuwa na moto,
ni giza tu. Nikasema, "Ni mahali gani humu?" Nikawasikia watu
wengi wakilia [Mt 25:30], lakini sikuweza kutambua walikuwa wako wapi. Ghafla,
nilisikia sauti iliyosema kwa kurudiarudia, "Endelea mbele, endelea
mbele.”
Nilitembea
kwenye giza lile na kadiri nilivyoendelea kutembea, vilio vya watu vikasikika
kwa karibu zaidi kiasi kwamba ingetakiwa niweze kuona nyuso zao; lakini bado
nilikuwa siwezi kuona chochote! Mara niliweza kutambua sauti ya minyororo ya
chuma, na nikasikia kufuli likifunguliwa. Ghafla mlango ulifunguka na kulikuwa
na chumba mbele yangu ambacho kilikuwa
kina mwanga kwa mbali. Niliona watu wengi, na ninapotafakari, naona walikuwa ni
Wakristo. Wazo lililonijia kwanza lilikuwa kwamba Ukristo ulikuwa ni uongo;
maana Wakristo wale hawakwenda kamwe mbinguni. Walikuwa wako gizani; na sehemu
hii ilikuwa imejaa Wakristo. Kwa nini wote walikuwa hapa? Baadhi walikuwa ni
Wakristo wanawake kutoka kijijini kwangu ambao walishakufa na niliwafahamu
fika; lakini kumbe wamekuja kuishia humu!
Kisha
sauti iliniambia: "Ingia ndani." Nikajibu, "Hapana
kabisa! Sitaingia kamwe kwenye sehemu hii." Nilijua kuwa mara
nitakapoingia, nitajiunga na kundi lile la wafu waliokuwa wanaangua vilio. Watu
humo walikuwa wakilia mfululizo na mavazi yao yalikuwa ya rangi ya udongo na machakavu.
Mara kulitokea nguvu fulani iliyonisukumia ndani, lakini mkono wangu ulibakia
umeng’ang’ania mlango, na niligoma kuingia kwenye chumba kile. Kwa hiyo,
nilipiga magoti na kulia kwa sauti, “Bwana, sitataka kujiua tena; tafadhali
nirudishie uhai na uniruhusu kuishi tena. Kama sehemu yenyewe ninayokuja kuishi
ni hii, basi bora nibakie duniani hata kama nitakuwa mgonjwa kwa miaka kadhaa.
Kwa nini nije hapa? Hapana!” Wakati huo nilikuwa nikijiuliza swali ndani
yangu, maana niliwaza kuwa hakuna kitu kama mbinguni na kuzimu; yote yalikuwa
ni uongo. Wale wote walkoonekana kumwamini Yesu kule duniani, wote waliishia
hapa. Kila mara niliwaza – hakuna mbingu wala kuzimu.
Niliuliza,
"Hapa ni mahali gani?" Ghafla sauti ilinijibu: "Hapa
ni mahali
pa kilio na kusaga meno.” Nilimsikia mtu akiongea lakini sikuweza
kumwona. Niliendelea kuuliza, "Nini? Hapa ni mahali pa kilio na kusaga
meno? Mbona basi watu wote hawa ni Wakristo?" Akasema, "Watu
hawa walimwamini Yesu bila kuwa na toba." Nikajibu, "Vipi sasa
kuhusu wasioamini?" Akasema, “Wasioamini wanaenda moja kwa moja
kuzimu." Kisha ghafla nilijikuta ninaelekea kuzimu.
Kuzimu
Sehemu
ya kutisha waliko wasioamini haiwezi kulinganishwa na pale waliko wale
waliomwamini Yesu bila ya toba. Niliwasikia watu kule kuzimu wakilia sana kwa
maumivu makali. Kila mmoja pale alisema: "Ni
joto sana! Nina kiu sana!" Niliona moto ukiwaka ndani ya miili
yao. Na kila moto ulipounguza mwili, mtu alipiga kelele sana. Cha ajabu, minyoo
ambayo haiathiriwi na moto, iliendelea kutoboa na kuingia na kutoka ndani ya
mifupa yao. Kila ilipofanya hivyo, ilimsababishia mtu maumivu makali sana.
Mateso
ya roho ya mtu ni mabaya sana kuliko mateso ya mwili. Nilipotambua hili,
nikajiambia, “Ni afadhali kumwamini Yesu bila toba kuliko kutomwamini na
kwenda moja kwa moja kuzimu,” ukitilia maanani mahali pa kilio na kusaga
meno, ambako kuna unafuu kuliko kuzimu.
Mbinguni
Niliwaza,
hivi mbingu kweli ipo? Mara swali hili lilipoingia mawazoni mwangu, nilijihisi
roho yangu ikielekea Mbinguni. Ha! Kulikuwa kuzuri! Uzuri wa mbinguni
hauelezeki. Niliona maji yakitiririka, majani, milima, na maua. Mitaa ilikuwa
mizuri mno kuliko mitaa yoyote iliyojengwa na wanadamu duniani. Milima ilitengenezwa
kwa vito vya thamani; maji yalionekana kama vito vya lulu na shohamu (onyx);
mitaa ilisakafiwa kwa dhahabu safi, na kuta zilijengwa kwa yaspi, rubi, yakuti
samawi (sapphire), na zumaridi (emerald).
Nilipigwa na butwaa na uzuri ule! Nikajisemea, "Siondoki hapa! Nataka
kukaa mahali kama hapa."
Ghafla alitokea malaika na akaongea na mimi
akisema, "Kulingana na
kiwango cha imani yako, unastahili kuwa kwenye
mahali pa kilio na kusaga meno. Hautakiwi kuingia humu.” Nikasema, "Siondoki
humu." Kisha malaika akasema, "Hapana! Ni lazima uondoke."
Nikajibu, "Je, natakiwa kuteseka kwa maumivu ya ugonjwa wangu duniani
tena?" Akasema, "Kama hauko tayari kurudi tena duniani, basi
sehemu pekee nyingine unayostahili ni kubakia kwenye mahali pa kilio na kusaga
meno." Nikasema, "Kama sehemu pekee nyingine ninayostahili
kwenda ni kule kwenye giza, basi bora nirudi kwenye mwili wangu ulio mgonjwa
kule duniani na kuendelea kuteseka kwa ugonjwa." Nilichagua kurudi
duniani. Sekunde iliyofuata nilikuwa tayari nimesharudi nyumbani.
Roho
yangu iliondoka kwenye mwili wangu kwenye saa 10:10 jioni; na ilikuwa ni saa
4:30 usiku ndipo iliporudi. Saa za mama yangu kufanya kazi zilikuwa ni kuanzia
saa 10:30 jioni hadi usiku wa manane. Muda huu dada na mama yangu walikuwa
tayari wameshalala. Mwili wangu ambao haukuwa na ufahamu, ulikuwa uko chini,
huku umepiga magoti pembeni mwa kitanda. Inasikitisha! Hawakujali kama nimekula
au la – jambo linaloonyesha kiwango kilichokuwapo cha cha kutonijali kwao.
Nikawaza, “Dada yangu! Yaani dada yako mkubwa, pembeni yako, amekufa na wewe
hata haujali! Ulipanda tu kitandani na kulala?" Roho yangu iliendelea
kurandaranda kwenye nyumba, na bila ya ugonjwa ilikuwa inajisikia vizuri. Nilikuwa nasitasita kweli kurudi kwenye mwili
wangu mgonjwa, maana nilijua kuwa mara nitakapoingia humo, nitaanza kupata
maumivu tena; lakini pia kama nikikataa kuingia kwenye mwili wangu, nitarudi
kwenye sehemu ya kilio na kusaga meno. Kwa hiyo, nikajua kuwa ni bora nirudi
kwenye mwili wangu kuliko kwenye yale mateso niliyoyaona.
Roho
yangu ilienda kwenye mwili wangu, kisha niliamka, lakini mwili wangu wote
ulikuwa hauna hisia. Nikagundua kuwa uso wangu umejaa machozi. Baada ya
kusubiri kwa takriban dakika kumi hivi, miguu yangu ilianza kujisikia ganzi
kidogo. Roho yangu ilipoondoka kwenye mwili, damu ilisimama mwilini. Nilianza
kujisogeza kidogo na nikaanguka kutoka kitandani; machozi yalikuwa
yakinitiririka. Nilishukuru sana na kusema, "Bwana, nakushukuru.
Asante, asante kwa kunirudisha tena duniani." Roho yangu iliporudi,
Mungu alinipatia maneno machache. Alisema, "Mwanangu,
rudi. Umebakiwa na muda kidogo. Muda mfupi ujao utakuja mahali hapa
nilipopaandaa kwa ajili ya watu wangu. Ukirudi duniani, ni lazima ukawaambie
kile ulichokiona.” Niliposikia maneno yake akisema, “Umebakiwa na muda kidogo,” nilidhani
ingekuwa ni siku chache tu. Nilifikiri angerudi mapema sana. Nikasema, "Oh!Hakika! Ilmradi tu kama
utaniruhusu kuja mbinguni, basi nitawaeleza nilichokiona.”
Wakati
ule nilipopokea ujumbe, nilidhani kuwa angekuja ndani ya siku chache, nami
ningekutana naye mbinguni tena. Sikutarajia kuwa ningeolewa na kuwa na watoto
wangu. Niliporudi duniani, nilikuwa nimejawa na pendo la Mungu na nilianza
kuhubiri Injili. Nilianza na wasioamini kwa sababu walioamini hawakutilia
maanani sana ushuhuda wangu. Wa kwanza kumweleza alikuwa ni mama yangu. Wakati
huo tulikuwa sote tuko nyumbani nami nilikuwa narukaruka kwa msisimko. Mama
yangu aliporudi nyumbani kutoka kazini saa kumi na mbili, nilimwambia, "Mama,
nilikufa na roho yangu ikatoka kwenye mwili." Akasema, "Hivi
siku nzima ya leo ulikuwa kwenye hali hiihii? Hauko sawa wewe; una wazimu!"
Niliwaza, kama mama yangu tu haniamini, ni nani mwingine ataniamini? Nakumbuka nilienda kumshirikisha dada mmoja
wa kanisani ushuhuda wangu. Mara moja alisema, "Liyan! Hakika kuna
tatizo kwako. Hilo haliwezekani! Hata siwezi kuamini.” Kwa hiyo, niliacha
kuwashirikisha waumini wenzangu ushuhuda wangu.
Nilipowashirikisha
wasioamini, mmoja baada ya mwingine walikuja kwa Yesu. Nilipowasimulia watu
mbalimbali kwenye treni, wengi waliyatoa maisha yao kwa Bwana. Bwana asifiwe!
Nilijua kuwa hii ilikuwa ni kazi ya Mungu. Hata hivyo, sijawahi kwenda shuleni
na ninajihesabu kuwa mtu asiyesoma. Nilimwambia Mungu, "Unaenda
kunitumia mimi; lakini sijasoma." Wakati fulani nilisikiliza mahubiri
kuhusiana na kufufuka kwa Lazaro, ambaye alikufa na kukaa kaburini siku nne
hadi akawa ananuka. Lakini Yesu alipotamka neno moja tu, Lazaro alirudi kutoka
kwa wafu [Yohana 11:43]. Niliguswa sana na hadithi hiyo na nikajisemea, “Kama
Lazaro alikuwa amekufa kwa siku nne, alikuwa amezikwa na hata kunuka vibaya,
lakini bado alifufuliwa, vipi kama Bwana atataka nijifunze kusoma? Bila shaka
itakuwa ni jambo rahisi zaidi.” Kuanzia hapo nilipata shauku kubwa ya kujifunza
jinsi ya kusoma. Matokeo yake, sala zangu zikawa ndefu zaidi. Kila usiku
niliomba hadi saa saba au nane usiku.
Nakumbuka
ilikuwa saa nane usiku kwenye mwezi wa kumi na mbili, nilipokuwa nimemaliza
kuomba, nililala kisha nikaanza kuota ndoto. Ghafla, nilimwona mtu amevaa nguo
nyeupe ambaye alikuwa anang’aa sana. Alikuwa na mng’ao ambao sijawahi kuuona
duniani. Alisimama kwenye dirisha langu na kuniita, "Mwanangu, njoo kwangu." Uso wake
uliangaza kama jua, na sikuweza kuuona sawasawa. Kisha alinitoa kwenye blangeti
langu na kunikumbatia kama mtoto mchanga. Akasema, "Kuanzia leo na kuendelea nitakufundisha jinsi ya kusoma."
Nikajibu, "Safi sana! Nina shauku sana. Nianzie wapi?" "Tutaanzia kwenye Injili ya Yohana." Alifungua
Biblia kwenye Yohana 21:15 na kuanza kusoma, "Basi
walipokwisha kula, Yesu akamwambia Simoni Petro, Je! Simoni wa Yohana, wewe
wanipenda kuliko hawa? Akamwambia, Naam, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda.
Akamwambia, Lisha wana-kondoo wangu.” Kadiri tulivyoendelea kusoma,
jina la Petro lilikuwa limeshabadilika na kuwapo jina langu; hata hivyo, wakati
huo sikutambua jina langu wakati wa kusoma na Bwana aliendelea kunifundisha
jinsi ya kusoma. Alisema, “Liyan, je,
wanipenda kuliko haya?” Nikasema, “Unamaanisha nini?"
Kisha akasema, "Ninaongelea mambo ya
dunia; je, unanipenda kuliko haya?" Nikasema, "Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda.” Tuliendelea
kusoma hadi kulipopambazuka.
Kulipokucha,
niliamka na kukuta kwamba niliendelea kusoma na kujikuta bado niko kitandani.
Haraka nilichukua Biblia na kufungua kwenye Yohana 21:15. Nikasema, "Ha!
Hiki ni kitabu cha Yohana." Lakini nilikuwa naogopa kufanya makosa,
kwa sababu wakati huo baba yangu, mdogo wangu wa kike na kaka yangu walikuwa
wote wapo. Nikamwambia mdogo wangu wa kike na wa kiume, "Njoni hapa.
Leo nitawasomea baadhi ya aya za Biblia.” Wakasema, "Haya, soma.”
“Kitabu cha Yohana, siyo?" nikauliza. Wote walinitazama na kusema,
"Ndiyo, ndiyo. Umepatia kabisa." Nikasema, "Nitasoma
Zaidi kidogo. "Basi walipokwisha kula, Yesu akamwambia Simoni
Petro, Je! Simoni wa Yohana, wewe wanipenda kuliko hawa? " Walishikwa
na mshangao na kusema, "Dada, umejifunza wapi namna ya kusoma maneno
haya?" Nikajibu, "Ninachowaza zaidi mimi ni endapo nimesoma
kwa usahihi." Wakasema, "Ndiyo, ndiyo, kila neno. Umesoma maneno hayo kwa
usahihi kabisa!”
Taratibu,
nilianza kutambua kila neno kwenye Biblia. Hata hivyo, sikuweza kutambua maneno
kwenye kitabu kingine kisichokuwa Biblia, hata vitabu vya kiroho vinavyoongelea
Kitabu cha Yohana. Maneno yalionekana nayajua, lakini sikuyaelewa. Matokeo
yake, kwa miaka kadhaa Mungu aliendelea kunifundisha jinsi ya kujifunza Biblia,
ambayo ilifanyika maji yangu ya uzima ya kiroho; na nilijifunza kwa bidii sana.
Kasi yangu ya kusoma ilikuwa ndogo. Wakati mwingine ilinichukua siku kadhaa
kumaliza mstari mmoja; lakini nilipokea ufunuo mwingi kutoka kwa Roho
Mtakatifu. Kila siku nilitafakari, niliomba na kusoma. Kwa hiyo, maisha yangu
yakawa yamejawa utajiri wa kiroho. Hivyo ndivyo nilivyojenga uhusiano na Yesu
Kristo.
Kisha
nilijiunga na kanisa na kufanya kazi ya Bwana kwa miaka miwili. Ulikuwa ni
uzoefu wenye matunda sana na ulinisaidia mimi pamoja na ndugu wengine katika
maisha yetu ya kiroho. Lakini Bwana hakuridhishwa na kazi yangu katika miaka
hiyo miwili. Hivyo, karama za rohoni wala miujiza haikubainisha maisha yangu ya
kiroho. Kama alivyosema Paulo, “isiwe,
nikiisha kuwahubiri wengine, mwenyewe niwe mtu wa kukataliwa.” [1 Kor
9:27]. Ilikuwa ni mwaka 2004 ndipo nilipoungana na mchungaji mmoja kuanzisha
kanisa kwenye nyumba yangu. Tulidhani tumefanya kazi nzuri.
Kwenye
siku ya pili ya mwaka 2006, Mungu alianza kufunua jambo ambalo lingenitokea
mimi siku iliyofuata, na jambo hilo kweli lilitokea. Siku ya tatu nilipokuwa
najiandaa kulala, Bwana aliniambia, "Kesho
asubuhi, kuna mtu atakuja kukuomba ukamwombee bibi yake, nawe ni lazima uende."
Siku ya nne nilianza kungoja nyumbani kuanzia saa 2 hadi saa 4 asubuhi, ndipo
alipotokea huyo mwanamume. Nilishangaa kumwona akiwa kama vilevile nilivyoona
kwenye ndoto. Kwa hiyo nilienda naye kumwombea bibi yake.
Siku
ya tano, nilishangazwa na ufunuo mwingine wa ghafla kutoka ndotoni. Mungu
alisema, "Ninarudi, na ni lazima utubu!"
Nilishtuka na kujibu, "Unarudi na ni lazima nitubu? Vipi kuhusu
mchungaji ambaye tuko pamoja?" Akasema, "Hakuhusu. Mimi ninarudi na ni lazima utubu!"
Nikawaza, "Nitubu kuhusiana na nini? Nimekuwa najibidisha kulea kanisa
hili. Sasa, kwa nini nahitaji kutubu?” Akasema, "Nifuate Mimi, ninapenda nikuonyeshe mahali."
Moyo
Kufumba
na kufumbua, nilifika kwenye nyumba moja ambayo kuta
zake na sakafu vilikuwa
vichafu sana. Vilikuwa vichafu kiasi kwamba ilikuwa haiwezekani kuingia ndani.
Nikauliza, “Hii ni sehemu gani? Mbona ni chafu kiasi hiki?” Bwana
akasema, “Unajua kwamba huu ni moyo wako?”
Kwa kweli sijui. Nilidhani nilikuwa ninamtumikia Bwana na kwamba ningekuwa niko
safi. Kusema kweli, nilikuwa ninapingana na Bwana. Nikauliza, "Ni lini
nilitenda dhambi nyingi kiasi hiki na sikutubu?" Ndipo akanifunulia
dhambi hizo moja baada ya nyingine. Akasema, “Unatakiwa
kukiri dhambi zako moja baada ya nyingine ili kwamba niweze kukusamehe dhambi
hizo moja baada ya nyingine."
Mara
niliona chombo safi cheupe kilichojaa damu. Yesu alivaa vazi jeupe na
akashikilia brashi kama ile ya kupakia rangi. Akaniambia, “Kiri dhambi zako moja baada ya nyingine.” Nikasema,
“Tafadhali ninaomba unifunulie ni lini nilitenda dhambi hizi?" Akaanza
kunifunulia dhambi zangu kana kwamba nilikuwa ninaangalia sinema. Nikaanza mara
moja kukiri dhambi zangu; na kila nilipofanya hivyo, alitumbukiza brashi ile
kwenye chombo chenye damu na kufuta dhambi zangu.
Baada
ya kutubu dhambi zangu zote moja moja, nyumba yote ilipakwa
damu. Cha
kushangaza, mahali pale ghafla, pakawa peupe na panapong'aa sana. Hapo, nikajua
kuwa niko safi. Akasema, "Usianzishe kanisa hapa. Unatakiwa uachane na kazi ya
kanisa. Sitazikumbuka kazi ulizofanya kwa miaka hii miwili iliyopita."
Nikasema, "Kama Bwana hatazikumbuka kazi zangu, basi ninafanya nini
hapa?”
Ghafla
niliamka. Nilikuwa natokwa na jasho jingi na nguo zangu zote zililowana. Kwa
kawaida familia yangu huamka mapema kila asubuhi ili kujifunza Biblia,
isipokuwa siku ile. Ilitarajiwa kwamba mafunuo ya Bwana niliyokuwa nikipokea
kila usiku yangetimia siku iliyofuata, na nilihofia kwamba ufunuo huu nao
ungetimia, kwamba Bwana anarudi. “Natakiwa nifanye nini?” Nilikuwa nina
wasiwasi na nikasema, "Kwa nini hamkuamka na kujifunza Biblia. Siku
nyingine ni sawa, lakini sio leo! Hamjui ya kuwa Bwana anarudi?” Mama yangu
alidhani ninachanganyikiwa tena; kwa hiyo alienda kuomba. Nilikuwa ninatetemeka
kwa hofu nikidhani kwamba Bwana angerudi siku inayofuata. Niliamua kukaa tu nyumbani
na kutubu. Kwa hiyo, niliahirisha usomaji wa Biblia na mkutano kanisani.
Mchungaji aliniuliza, "Kwa nini
tuahirishe mkutano wa kanisani?" Nikasema, "Mara nyingi, baada
ya watu kumwamini Bwana, maisha yao hubadilika na kufanywa upya. Lakini najua
sasa kwamba Mungu anashughulika na mimi na moyo wangu. Tuahirishe mkutano kwa
sababu Mungu hataukumbuka mkutano huu. Hatuwezi kuendelea.” Baada ya hapo,
kama inavyosema Biblia, kuhubiri kwenye madhabahu si jambo la msingi [Mt 23:3].
Cha muhimu kabisa ni jinsi unavyoendesha uhusiano wako na Mungu; pia na watu
mara unapoondoka kwenye viwanja vya kanisa. Sikutarajia kuwa Mungu
angeshughulika na mimi kuhusiana na nyumbani kwangu.
Nikasema,
"Bwana, niambie kinachokupendeza nami nitakifanya. Ni kazi zipi ambazo
ni kazi za dhahabu, fedha na mawe ya thamani, niambie tafadhali!" [1
Kor. 3:12]. Bwana akasema, “Ni kweli kabisa
unataka kufanya mambo yanayonipendeza?" "Ndiyo!"
nikajibu. Bwana akasema, "Sawa, nenda
ukawajali watoto wako na mume wako na kuifanya nyumba yako iwe safi. Hilo ndilo
unalotakiwa kulifanya." Kwa kweli sikuamini kwa nguvu sana
kwamba kuwa hili limetoka kwa Mungu, maana nilikuwa najibidisha sana na kazi za
kanisa kiasi kwamba nilikuwa nikifua nguo zangu lakini si za mume wangu.
Nilikuwa na kazi nyingi kiasi kwamba sikuwa hata na muda wa kufua soksi zake
maana ilinibidi kuangalia watoto na kuandaa mikutano ya kanisa. Nilikuwa na
kazi nyingi mno! Mume wangu alifua nguo zake mwenyewe nami nilifua zangu. Baada
ya kurudi kutoka kwenye kazi za siku nzima, mume wangu alilazimika kufua nguo
zake na kufagia nyumba, ambayo kila mara ilikuwa imevurugikavurugika.
Nikawaza,
"Ee Bwana, hivi haya yanatoka kwako kweli? Hivi niache kufanya kazi
yako, nikafanye mambo haya, kweli?" Bwana akasema, "Ndiyo!" Hatimaye, nilianza kufua nguo
za mume wangu. Nilipofanya hivyo, Bwana aliendelea kunifundisha. Aliendelea
kugusa moyo wangu, na kusema: "Unajua
kuwa kufua hii soksi moja ni kazi ya dhahabu, fedha na mawe ya thamani, ambayo
ninaikumbuka?" Hilo lilinishangaza kweli. Nikamwambia mume
wangu, "Kuanzia sasa nipatie soksi zako zote chafu; nitazifua!”
Mume wangu alionekana kushtuka na kuogopa. Akaniambia, "Kwa nini
umebadilika ghafla kiasi hiki? Umekuwa mwema ghafla." Nikasema, "Kwa
kweli, nimefundishwa na Mungu. Kuanzia sasa, sitakuruhusu ufue nguo zozote.”
Kisha mikutano yote kanisani ilifutwa na nikaanza kukaa nyumbani muda wote.
Sikutarajia kwamba Mungu angegeuza maisha yangu kwa namna ile. Kusema kweli, nilipokea
upako wangu mwingi kutokana na kule kufutwa kwa vikao vya kujifunza Biblia na
ile mikutano ya kanisani katika kipindi kile.
Ni
wazi kuwa hii haikutosha. Baadaye, Mungu alinipeleka kwenye nyumba ya mama mkwe
wangu. Niliishi Yongnian Handan, na mama mkwe wangu aliishi kwenye nyumba
iliyokuwa Cangzhou, kama km 600 kutoka kwangu. Kwa kuwa wao hawakuwa waamini,
nilipata manyanyaso sana kutoka kwao.
Nakumbuka
nilipanda basi kwa siku nzima ili kufika kule aliko mama mkwe. Niliwasili
wakiwa ndio wakiwa tayari kula. Kila mara nilimfundisha binti yangu kuomba
kabla ya kula. Kwa hiyo, kama familia, mara zote tuliomba kabla ya kula. Kwa
wakwe zangu, baada ya kuandaa chakula na kumwita kila mmoja, binti yangu wa
miaka 2 alisema, "Mama, tuongoze kwenye sala." Babu yake
hakuelewa kile binti yangu alichokuwa anasema. Hivyo akauliza, "Liyan, anasema
nini?" Nikajibu, "Oh, amesema tuombe, vinginevyo hatakula."
Baba mkwe wangu mara moja alimwambia wifi yangu, "Yunyun! Nenda kalete
chombo cha ubani. Mwaga mchanga ulio kwenye chombo hicho, kioshe kisha ukijaze
tambi kwa ajili ya wifi yako."
Hiyo
ndiyo aina ya manyanyaso waliyonipa. Basi, akaniletea chombo kile kikiwa na
tambi na kusema, "Haya, chukua ule kutoka kwenye chombo hiki ambacho
kina baraka nyingi sana." Ukweli ni kuwa walikuwa kinyume nami.
Japokuwa ndio nilitoka tu kuolewa kwenye familia yao, walinitendea kwa namna
hiyo. Nikamwuliza Bwana, "Bwana, nifanye nini sasa?" Bwana
akasema nami, "Sanamu si lolote; vivyo
hivyo chombo kinachotumika kuchoma ubani kwa ajili ya sanamu nacho si lolote."
Nikasema, "Bwana asifiwe. Mambo haya si lolote!"
Binti
yangu aliendelea kusema, "Mama, omba basi!" Nilikuwa nafikiri,
niombe nini sasa? Tayari walishaniwekea chakula kwenye chombo wanachotumia
kuabudia sanamu. Nikasema, "Haya! Tuombe! Bwana Yesu, nakupa shukrani
na sifa." Mwanzoni nilikuwa nina hofu ya kuomba, lakini kadiri
walivyozidi kuniwekea vikwazo, ndivyo nilivyoomba kwa ujasiri. Maneno kutoka
kwenye Biblia yalikuja kwenye akili yangu, "usali
mbele ya Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi.”
[Mt. 6:6]. Mungu akasema nami, “Hii ndiyo kazi
ya dhahabu, fedha, na mawe ya thamani.” “Ha, kweli?” nikasema.
Vijiti vyangu vya kulia (chopsticks) vilitupwa chini na mtu.Na hii nayo ni kazi
ya dhahabu, fedha, na mawe ya thamani? Nikasema, "Sifa kwa Bwana."
Nilisimama haraka na kufuta machozi yangu, na mara moja mateso na hasira
iliyokuwa ndani yangu vilitoweka. Hakika Neno la Bwana ni faraja kubwa. Kwa
hiyo, nilianza kutafuta vijiti vyangu vya kulia sakafuni na nikavipata. Baada
ya kula, nilikuwa nikiosha vyombo mara moja tu, lakini safari hii niliosha mara
3, maana Bwana aliniambia kuwa hii ilikuwa ni kazi ya dhahabu, fedha, na mawe
ya thamani. Kwa hiyo, nilitaka kuviosha viwe safi kabisa. Na kadiri
nilivyoviosha, ndivyo furaha ilivyozidi ndani yangu.
Halafu,
mume wangu alikuja kututembelea bila kutarajiwa. Aliona jinsi nilivyojishughulisha
na mapishi na usafi na ndugu zake walikuwa hawafanyi chochote zaidi ya kucheza
tu mahjong na kamari. Mume wangu hakuweza kustahimili kile alichokiona; kwa
hiyo aliwakasirikia sana familia yake. Kwa kweli, kustahimili mateso imekuwa ni
kama jambo la kawaida kwangu. Nikamjibu, "Hakuna tatizo!" Akasema,
"Acha kufanya kazi zote za ndani." Nikasema, "Sikuwa
nazifanya kwa ajili yao." Akasema, "Tuondoke zetu!"
Nikamjibu, "Hapana, hii ni kazi ya dhahabu, fedha, na mawe ya thamani mbele za Mungu." Hakuelewa nilichokuwa nasema. Alitaka
niondoke pamoja naye, lakini nilikataa. Kwa hiyo akaenda kunywa mvinyo.
Baadaye
alirudi na kukawa na mvutano mkubwa kati yake na wazazi wake. Nikajisemea, “Bwana!
Kazi ya dhahabu na fedha itafikia mwisho hivi karibuni.” Mwanzoni,
tungeweza kuondoka mahali hapa pamoja kwa furaha, lakini ghafla mume wangu
akaamua kuvutana na ndugu zake kwa namna ile. Kutakuwaje na mwisho mwema? Mume
wangu alipomaliza kubishana na baba yake, alisema, “Liyan, fuatana nami. Hatutarudi
tena kwenye nyumba hii na sitaingia tena kwenye chumba hiki. Kama nitakanyaga
tena kwenye chumba hiki, basi sitakuwa mwanafamilia hii." Lakini Bwana
akaniambia, "Hapana, huwezi kuondoka sasa."
Nilimwambia mume wangu naye alikasirika sana kutokana na jibu hilo na akasema,
“Kwa sababu yako, wazazi wangu wananilaani.” Nikasema, "Bwana
aliniongoza kuja kuwa sehemu ya familia yenu. Inanibidi nitii mwongozo wa Bwana
wangu. Kwa hiyo, unaweza kuondoka." Kisha akasema, "Sawa,
nitaondoka. Unaweza kukaa hapa milele na usiondoke kamwe!" Nikasema,
"Nitaondoka Bwana atakaponiongoza kufanya hivyo."
Mume
wangu aliondoka kwa hasira na kuniacha mimi kwenye nyumba ya wakwe zangu.
Nikauliza, "Ee Bwana, nitaondoka lini kwenye nyumba hii?"
Bwana akasema, "Subiri kwa muda. Bado si
muda mwafaka." Nikasema, "Sawa!"
Kila
wakwe zangu walipotoa nguo zao, haraka nilienda kuzifua. Kisha ghafla, kwa
namna fulani, Mungu akafungua mioyo yao na wakatambua kwamba kazi zote za
nyumbani hazikutakiwa zifanywe na mimi peke yangu. Walikuwa wakiwaza, “Huyu
mwanamke ameolewa kwenye familia yetu kutoka mbali. Hizi kazi za kufua
zinatakiwa kufanywa na binti yetu maana ni wajibu wake kwa kuwa yeye ndiye
tuliyemzaa na kumlea.” Baadaye, wakwe zangu ghafla walianza kuwa wema
kwangu, kitu ambacho kilinishangaza sana. Nilipokuwa nje nikifua, mama mkwe
wangu alitoka na kuja kunifunika kwa nguo, maana kulianza kuwa baridi zaidi.
Alisema, “Liyan, hebu jifunike nguo hizi." Baba mkwe wangu
aliniletea kikombe cha chai ya moto na kusema, “Njoo, njoo. Kunywa chai ya
moto." Nilishangaa sana maana mara zote walikuwa wakininyanyasa;
lakini ghafla wakawa wamegeuka na kuwa wema kwangu. Hili lilikuwa jambo gumu
kulizoea. Nilijiuliza ni kwa nini wamegeuka ghafla kiasi hicho na kuwa wema
kwangu. Baba mkwe hata aliniuliza ni mablangeti mangapi nilikuwa ninahitaji
nyumbani. Alisema, “Nitayaandaa kwa
ajili yako. Kama ukiona kitu chochote katika nyumba hii ambacho unakihitaji,
wewe kichukue tu. Tutajisikia furaha kukupatia." Nikasema, "hapana,
hakuna ulazima wa kufanya hivyo. Sihitaji kitu chochote." Ghafla Bwana
akasema nami, "Ni muda umefika. Ondoka
mapema kesho." Kulikuwa na tofauti ya siku moja tu kabla
Bwana hajaniambia kuondoka; mume wangu aliondoka siku moja kabla na mimi
niliondoka siku iliyofuata.
Muda
wangu wa kuondoka ulikuwa wa kimiujiza. Watu wa kijiji chote walikuja kuniaga
na walinichukulia ungedhani ni mtu maarufu tajiri aliyekuja kutembelea
kijijini. Kila mtu alisema kuwa huyu mkamwana ameteseka sana. Ndani ya zile
siku 2, alifanya kazi nje na ndani ya nyumba. Ghafla Bwana akasema, "Ole wako, watu wanapokusifu." Nikasema
, "Bwana, sikuweza kufanya lolote bila ya neno lako kunitia nguvu. Yote
ni kwa sababu ya msaada wako usiokoma. Nisingeweza kuyafanya hayo kwa kiwango
kile mimi mwenyewe. Wanakusifu Wewe nami napenda nirudishe utukufu wote kwako."
Safari ya Basi
Baba
mkwe wangu alituangalia tukipanda basi ili kurudi ShiJiaZhuang. Tulipanda basi
la masafa marefu. Basi lilijaa watu, maana ulikuwa ni msimu wa wanafunzi kurudi
mashuleni. Nilipokuwa kwa wakwe zangu, moyo wangu ulipata nguvu, na kulikuwa na
upako wenye mamlaka. Wakati nimekaa kwenye basi, niliona kwamba kulikuwa na
kipindi kwenye TV chenye lugha chafu. Nilijisikia kinyaa na kusimama. Lakini
nilipowaangalia watu walivyo wengi, nilirudi kukaa. Nilifanya hivi mara tatu.
Nilifumba macho yangu na kuomba, "Ee! Bwana, nina aibu. Nifanye nini?"
Ghafla Bwana alinipa maono ya Yesu ndani ya hekalu, akiwa na hasira ya haki,
akisokota kamba ili kulitakasa hekalu. Nilipoyaona maono hayo, sikuvumilia
tena. Ghafla, nilisimama na kumwambia dereva wa basi, "Dereva wa basi! Zima
TV yako! Unawezaje kuonyesha video ya aina hii mbele za watu? Unaweza kwenda
kuiangalia huko nyumbani kwako; lakini je, ni sahihi kuionyesha hapa?"
Dereva
yule alishtuka. Yeye na mwanamke wa tiketi wa humo ndani ya basi walitazamana.
Dereva akauliza, "Kitu gani kimetokea kwake?" Yule mwanamke
akasema, "Sijui." Dereva akasema, “Wewe ni nani?" Nikajibu,
"Wacha nikuambie. Huhitaji kuuliza mimi ni nani. Kama ukijua mimi ni
nani, nitaivunja TV yako na CD yako, nawe utahitaji kulipwa faini!"
Sikujua ni kwa nini nilipata ujasiri kiasi hicho. Dereva alipigwa butwaa na
kasema, "Haya! Haya! Naizima! Naizima!" Mara moja alizima TV
na kuisukumia pembeni. Dada wa tiketi alikaa chini na hakusogea. Kukawa na
ukimya mkubwa kwenye basi; mtu angeweza hata kusikia pini ikidondoshwa. Basi
lilifika Hengshui, kituo cha kupumzikia, ili kuruhusu abiria kwenda maliwatoni.
Watu walipotoka kwenye basi, wengi wao walinitupia jicho huku wakibasamu. Nami
pia nilitabasamu. Ilionekana kwamba kila mmoja alikubali kuwa haikuwa sahihi
kuonyesha video kama ile pale, lakini hakukuwa na mtu wa kusema, maana dunia na
jamii zimeshaporomoka kimaadili hadi kiasi hicho.
Baadaye,
mama mkwe wangu alikuja kukaa nasi. Nilimwongoza sala ya kumkubali Yesu kama
Mwokozi wake. Ilikuwa ni Julai, wifi yangu akiwa chuoni alibishana nami sana.
Miezi mitatu baadaye, alikuwa kwenye mfadhaiko mkubwa baada ya kuachana na
rafiki yake wa kiume. Alijaribu mara nyingi kujiua. Kila mara alibishana nami
kuhusiana na masuala ya imani yake. Alijua kuwa ninaweza kumsaidia, lakini
alikuwa anasikia aibu kuniomba msaada. Hatimaye baadaye alinipigia simu na
kusema, "Wifi, njoo unisaidie. Wewe peke yako ndiye unaweza kuniokoa."
Nikasema, "Mimi siwezi kukuokoa. Ni Mungu tu ndiye mwenye uwezo wa
kukuokoa. Ungependa kuomba nami ili umpokee Yesu kama Mwokozi wako?"
Akasema, "Ndiyo!" Kisha nikaomba naye ili ampokee Yesu Kristo
kama Mwokozi wake. Mambo haya yote yalinionyesha kwamba baada ya kuwa kwenye
ndoa kwa miaka mingi, kupigana na kubishana hakukumbadilisha yeyote. Lakini
nilipoanza kujinyenyekeza, Mungu aliendelea kunishusha ili kwamba siku moja
aweze kuniinua.
Maneno
niliyotamka kwenye basi yalikuwa ni matokeo ya mafunzo yangu ya kiroho kwenye
nyumba ya mama mkwe wangu wakati nikiosha vyombo, nikifua nguo na kufanya kazi
zote za ndani. Mafunzo yangu yote yalitokea kipindi hicho. Nilitambua kuwa kile
ambacho ninashughulika na kushindana nacho si mwili wa nje bali ni roho iliyo
ndani. Unapotambua kuwa Mungu ndiye nguvu ya moyo wako, nguvu hiyo ni kubwa
sana. Nilipambana na magonjwa mengi kwa muda mrefu, lakini mara moyo wangu
ulipoungamanishwa na Bwana, magonjwa yote yaliondoka mwilini. Hivyo ndivyo
Bwana alivyo halisi!!
Nakumbuka
zamani kila nilipopata ugonjwa, Bwana alikuwa pamoja nami. Hivyo, hata
nilipoumwa, nilikuwa nimejawa na furaha tu. Wapendwa wengi kanisani walidhani
nina wazimu. Baadaye, niliwaza labda kulikuwa na tatizo kwenye maneno: “furahini
katika mateso”. Wiki mbili za mwisho katika mwezi, nilipokuwa na ushirika
na Bwana, nilijumuisha maneno: “Sifurahii mateso, lakini nafurahia uwepo
wa Bwana wakati ninapopitia mateso.” Niliwaza: Ni lini huwa ninakuwa na
uhusiano wa karibu na Bwana? Jibu ni wakati ninapopitia mateso. Kwa hiyo,
ninamsifu Mungu kwa ajili ya mateso yote. Nilicheza na kupiga ngoma nyumbani
wakati ninamsifu Mungu.
Usiku
mmoja, nilikuwa na shauku kubwa ya kuwa na ushirika na Bwana kiasi kwamba
nilikuwa ninashindana na Bwana na kukataa kabisa kumwacha aondoke. Siku
iliyofuata nilipoamka, sikuweza hata kusogeza miguu yangu maana misuli yote
ilikuwa imekufa ganzi, kitu ambacho kilinikumbusha habari ya Yakobo juu ya
kushindana na Bwana. Bwana aliniwezesha kutambua hilo kidogo kidogo. Ni lazima
nimsifu Mungu kwa ajili ya mateso yangu yote. Nilisema, "Ee Bwana,
sikujua kuwa umejaa hekima.” Unapomsifu Mungu kwa ajili ya mateso yote unayopitia,
ni hekima kutoka kwa Mungu kwa sababu, hekima ya Mungu siku zote huwa juu ya
hekima yetu. Alimtuma Mwanawe wa pekee kuja kufa kwa ajili yetu; na alikufa
msalabani. Ni hekima ya Mungu na nguvu ya Mungu! Machoni petu, ni jambo la aibu
na la kipumbavu; lakini machoni pa Mungu, ni hekima ya kutuokoa sisi sote.
Safari ya Treni
Nakumbuka
wakati fulani nilisafiri hadi kaskazini mashariki mwa China pamoja na watoto
wetu. Basi lilichelewa kuja. Lilitakiwa kufika saa mbili, lakini lilifika saa
tatu. Wanangu walichoka na kulala. Tulipokuwa tunaingia kwenye basi, wanangu
waliamka ghafla na kusema kwa kilio, “Nataka kulala. Nataka kwenda nyumbani!”
Mume wangu akanipa changamoto kwa kusema, "Hata hivyo, hakuna viti
vilivyobaki wazi. Bora tu kurudi nyumbani na kwenda kulala. Tuondoke zetu."
Wakati huo, kwa kweli sikujua cha kufanya. Kusema kweli nilisikia kusukumwa na
Mungu niondoke. Nikasema, "Bwana,
maisha yangu yote ni kwa ajili yako. Sijali juu ya maisha yangu, lakini
nisingependa mume wangu na wanangu wateseke pamoja nami." Ghafla Bwana
akasema nami, "Unajua nitakavyokuja
kuwapa thawabu hapo baadaye? Nataka na wao waje wapate thawabu sawasawa na wewe."
Kisha mume wangu akasema, "Ama twendeni nyumbani au tukakate tiketi."
Bwana alinipa neno, kwa hiyo nikasema, "Twendeni tukakate tiketi."
Mwishowe,
tulijipenyeza hadi tukaingia ndani ya treni. Lakini kulikuwa na watu wengi
sana. Hivyo, tuliweza tu kusimama mlangoni. Ghafla Bwana akasema, "Liyan, nisifu Mimi. Nataka kusikia ukinisifu Mimi!"
Nikasema, "Ee Bwana, usinitanie. Nawezaje kukusifu wewe kwa sauti
kwenye muda kama huu?" Bwana akanipa changamoto akisema, "Jaribu na unisifu Mimi. Nataka kusikia."
Nikasema, “Bwana, hapana." Bwana akasema, "Ndiyo. Nisifu Mimi!” Nikasema, "Bwana,
hata kama nikikusifu Wewe, nakwambia ukweli, nitakuwa naongopa. Sifa hizo
hazitatoka moyoni mwangu." Kisha Bwana akasema, "Hata kama si kutoka moyoni mwako, hakika bado nataka
kusikia sifa kutoka kwako; na nataka kusikia ukinisifu Mimi katika muda kama
huu." Nikasema, "Bwana, ina maana unaniruhusu
kukudanganya? Sina sifa zozote ndani yangu." Hapo Bwana alizungumza
kutokea ndani yangu akisema, "Kama hunisifu
Mimi katika hali kama hii, basi hauna tofauti na watu wengine. Una tofauti gani
na wasioamini? Hao wasioamini humshukuru Mungu kwa kufanikiwa kuingia kwenye
treni. Kuna tofauti gani kati yako na wao?" "Ndiyo,
niko tofauti na wao … Ee Bwana. Mimi ninakusifu Wewe!"
Wakati
nikijaribu kumsifu Mungu, kulikuwa na watoto wakilia, watu wamejaa, kuna harufu
mbaya kila mahali, na jasho la moto kwenye ngozi yangu. Nikasema, "Bwana,
ninakusifu Wewe kwa sababu ninaweza kujipenyeza kwenye treni hii." Mara
nilipoanza kumsifu Mungu, moyo wangu ulitulia. Nikasema, "Bwana, nasifu
hekima Yako kwa sisi kutopata viti. Naamini utanipa nguvu ya kusimama hadi
mwisho wa safari na ninaamini unazo nguvu nyingi." Kadiri nilivyozidi
kumsifu Mungu, ndivyo watoto walivyopunguza kulia. Kadiri nilivyoendelea
kusifu, ndivyo furaha ilivyoongezeka ndani yangu. Kisha Mungu akanipa
changamoto wakati nimesimama kwenye mlango wa choo nikiwa nimemshikilia
mwanangu mikononi; na nikaanza kurukaruka na kusema, “Bwana, pokea sifa. Nakushukuru.
Nakupenda. Yehova Mungu ni nguvu zangu. Nakupenda. Nakusifu. Nakusifu."
Nilisifu mfululizo. Kulikuwa na watu wa kila aina wamenizunguka kwenye treni,
lakini hawakusikia nilichokuwa nasema. Niliendelea kusifu na kusifu.
Baada
ya muda, mume wangu akaniambia kuwa alitaka kutafuta tiketi ya daraja la juu zaidi
ili aone kama tunaweza kupata sehemu yenye kiti cha kitanda. Ukweli wakati huo moyo
wangu haukujali kama tutapata au la. “Ee
Bwana, Wewe uko na mimi. Utanisaidia kusimama hadi mwisho wa safari. Nina imani
kubwa ndani yangu. Ninakushukuru sana.” Watu wengi walisimama mstari ili
kupata tiketi hizo. Hatimaye, mume wangu akasema, "Sifa kwa Bwana!"
Nikasema, "Nguvu ya ndani ya kutoa shukrani kwa kupata kiti cha kitanda
ni kubwa; lakini nguvu ya ndani ya kutoa shukrani ni kubwa zaidi kama
nisingepata hicho kiti."
Wakati
maisha ya kiroho ya watu wengine yanapokuwa hayajafikia ngazi sawa na ya kwako,
utakuta kwamba maisha yako ya kiroho yako juu zaidi. Maisha yako ya kiroho
yanapofikia ngazi ya juu zaidi, unafanya nini? Utaona mbali zaidi! Mateso yote
mbele za macho yako yanakuwa ni jambo dogo sana. Mateso ni chakula cha kiroho. Ni
virutubisho vya maisha ya kiroho. Njoo ule na mwili wako utakuwa na afya. Kwa hiyo,
hivi karibuni nilipokuwa niko nyumbani, nilijisikia maumivu kwenye mguu na
kiunoni. Kwa kawaida, kunapokuwa na maumivu, huwa nayafukuza maumivu hayo kwa jina
la Yesu. Hivyo niliyakemea maumivu hayo, “kwa kupigwa kwa Yesu Kristo,
nimepona!” Kila mara ninaposema hivyo, maumivu huondoka mara moja. Lakini safari
hii hakuna kilichotokea. “Ni kwa nini?” nikajiuliza. Kisha nikaingia
kwenye maombi mazito, na nikamwuliza Bwana kwa njia ya Roho Mtakatifu. Bwana akasema,
"Unajua jinsi ambavyo hauna utii? Kwa nini
una maumivu ya mguu? Unahitaji kumsifu Mungu! Kwa nini una maumivu ya kiuno? Unahitaji
kumsifu Mungu!" Ndipo nikaelewa kwamba nilikuwa sitoi
ushirikiano. Nikasimama, nikajinyosha miguu yangu na kunyonga kiuno changu,
maana mwili wangu wote utamsifu Bwana wangu! Nikajibiringisha kwenye sakafu. Nilifunga
mlango ili mume wangu asinione akadhani nimechanganyikiwa. Mara nyingi huwa
namsifu Bwana kama mtu mwenye wazimu. Nilipokuwa nabiringika sakafuni nikimsifu
Mungu, ghafla nilibaini ukweli, pale Bwana aliposema, "Haujaona waigizaji kwenye jukwaa hutumia kila njia kuigiza
ili waweze kupigiwa makofi na kutiwa moyo kila mtu? Je, unajua jinsi
ninavyojawa na furaha pale unaponisifu Mimi?”
Mara
nyingi huwa namsifu Mungu nikiwa na dada mmoja hadi usiku wa
manane tukiwa sehemu
fulani mbali na mji; mahali ambako tunaweza kumsifu Mungu kwa uhuru. Usiku mmoja,
tulimsifu Mungu na kumwomba hadi saa 8 usiku, na dada yule akalala. Niliendelea
kuomba kwa nusu saa nyingine ndipo nikaona maono. Niliona malaika wawili, kila
mmoja ameshikilia kikombe cha dhahabu kikubwa sana. Malaika wale walikuwa
wanadaka vitu kutoka kwetu. Wakati huo, sikuelewa kile ambacho malaika walikuwa
wakikamata, lakini nilisisimka kweli kuwaona na nikawa nasifu na kuomba zaidi
na zaidi. Niliimba nyimbo katika roho na malaika wale waliendelea kushikilia
vikombe vile vya dhahabu na kukamata vitu kutoka kwetu…. Niliomba kwa muda
mrefu hadi sauti yangu ikaanza kupungua, nilipoona kuna kitu kimejaa na
kufurika kwenye kikombe kile; nami nikaacha kuomba. Nilikuwa na shauku ya kuona
kuna nini ndani ya vikombe vya dhahabu. Nilidhani labda ni machozi, mvuke, au
kitu kama hicho! Lakini nilioangalia kikombe kimojawapo, kilikuwa kimejaa
manukato, huku kikombe cha malaika mwingine kikiwa kitupu. Kilikuja kitupu na
kikarudi kitupu. Nilishangaa sana. Kulipokucha, nilijilaza na kupata usingizi
kwa muda. Sikumwambia yule dada kile kilichotokea usiku ule. Alisema, "Nilijisikia
usingizi sana, lakini nilikuwa nikikusikia ukiomba kwa bidii. Je, uliona maono?"
Baadaye,
nilipopiga magoti pembeni mwa kitanda changu kumuuliza Bwana, ghafla Bwana alifungua
ufahamu wangu na kusema, "Ewe mwenye
welewa kidogo. Kuna malaika wawili. Mmoja wa kwako na wa pili wa rafiki yako.”
Nikamwuliza Bwana, "Kwa nini malaika ameshikilia kikombe?"
Bwana akajibu, "Ili kukamata maombi yako."
Kisha nikaendelea kuuliza, "Kwa nini kikombe changu kimejaa na
kufurika, na kwa nini kingine kilikuwa kitupu?" Bwana akajibu, "Mwenzako alilala usingizi." Nikasema,
"Kirahisi hivyo?" Bwana akasema, "Ndiyo, kikombe kinajazwa na maombi yako. Malaika atakiinua
mbele za Mungu. Mungu atatumia maombi yako kutengeneza upako na kuumimina. Kwa hiyo,
maombi yanaweza kabisa kuharibu ufalme wa ugonjwa, hata kama ni kansa, kwa
sababu upako unatengenezwa na Mungu, na unapomiminwa kutoka kwa Mungu, unakuwa
na nguvu sana, na unaweza kuharibu mamia ya falme za shetani."
Mara
nilipotambua jinsi upako unavyotokea, niliyapenda maombi ya usiku kuliko
mwanzo, na nikawa naomba bila kukoma. Wakati mwingine mwili unapolemewa, Bwana
anasema ghafla, "Liyan, amka."
Nami ninasema, "Nahitaji kulala kidogo." Bwana aliuliza,
"Utatengeneza nini kutokana na usingizi? Je,
unaweza kuzalisha upako kutokana na usingizi?" Nikasema,
"Hapana." Bwana akauliza, "Unaweza
kuzalisha imani kutokana na usingizi?" Nikasema, "Hapana."
Bwana akauliza, " Unaweza kuzalisha upendo
kutokana na usingizi?" Nikasema, "hapana."
Bwana akasema, "Vitu hivi vyote viko wapi?
Viko ndani ya maombi yako." Mara moja nilielewa, na
nikainuka na kupiga magoti sakafuni na kuomba. Nikaendelea kuomba ili upako huo
wenye nguvu uje. Niligundua kwamba upako huo ni halisi kabisa.
Kwa
hiyo, ni lazima tujenge madhabahu nyumbani, katika siku hizi za mwisho, maana
Mungu anataka kutupatia baraka nyingi sana. Huu ndio ufunuo niliopokea pale
nilipojifungia kwa siku nyingi na kuomba. Bwana alisema, "Hakuna kusubiri tena. Tuko kwenye kipindi cha kitabu cha
Yoeli." Kitabu cha Yoeli kinasema: Hata itakuwa, baada ya hayo, ya kwamba nitamimina roho yangu juu ya
wote wenye mwili. Usingoje zaidi; huu ndio wakati wenyewe. Hivi sasa Roho
wa Mungu anamiminwa, na Bwana alisema kwamba katika siku hizi za mwisho anazo baraka
nyingi. Baraka hizo si za mali za kimwili, bali mafunuo juu ya nyakati za
mwisho. Kwa waamini, kujua mafunuo ya nyakati za mwisho kutaleta uamsho wa
kanisa zima. Mara uamsho utakapokuja, ufalme wa Mungu utakuja mapema baada ya
hapo. Kupitia sisi, ufalme wa Mungu utaenea kote.
Hivi
sasa tunaingia kwenye siku za mwisho. Tumia muda mwingi zaidi ukijenga uhusiano
wako na Bwana, Mwokozi wako. Bwana anatamani kumpa kila mmoja ujumbe wa namna
hii; na anatarajia kuwa kila mmoja ataamka. Huu pia ni ujumbe niliopokea siku
chache zilizopita nikiwa peke yangu, katika ushirika na Bwana huku nikiomba
mahali pangu pa siri. Roho wa Bwana atamiminwa kwa wote wenye mwili, ili kwamba
sote tuweze kwenda na mwendo ya Roho Mtakatifu. Kama huwezi kwenye na mwendo ya
Roho Mtakatifu, utaanguka; na mara ukianguka, umaskini, magonjwa na majanga ya
dunia yataongezeka zaidi na zaidi. Utapata mateso kwenye kipindi cha mwisho, na
hali itakuwa ngumu sana kwako!
………………………………………
Mpendwa
msomaji wa blog hii, asante kwa kusoma Makala haya na Bwana atutie nguvu ili
tuweze kusimama katika nyakati hizi za mwisho. Tutafute chakula, mavazi, nyumba
na kadhalika, lakini tusisahau kuwa hivyo vyote ni vitu vidogo sana; si
kipaumbele cha kwanza. Kristo na uzima wa milele wa roho zetu pamoja na
utakatifu ndivyo kipaumbele namba wani.
Kama
ungependa kusoma ushuhuda huu kwa Kiingereza, basi bofya HAPA.
Bwana
akubariki, akushikilie na kukutia nguvu, katika Jina la Yesu.
God Bless you
ReplyDeleteBe blessed too Nicky
DeleteBarikiwa na Bwana mpendwa kwa kutuwekea shuhuda zenye kuimarisha imani yetu. Kwa kweli tumaini letu ni YESU TU
ReplyDeleteAmen. Nawe pia Bwana akubariki.
DeleteUbarikiwe sana James ushuhuda huu umenijenga sana nimegundua kuwa kumbe Huduma tunazofanya tunatakiwa Mungu azihakikishe
ReplyDeleteAmen mpendwa. Zidi kubarikiwa na kuinuliwa na Mzee wa Siku, Yesu Kristo.
Deleteubarikiwe sana mtumishi wa MUNGU
ReplyDeleteBwana atutie nguvu katika safari yetu.
ReplyDeleteAmen
ReplyDelete