Sunday, November 17, 2013

Yesu - nitoe humu kuzimu!



(Hii ni picha tu ya mtandaoni - si ya Linda)


Ndugu msomaji, wako watu wengi sana wanaopita kwenye lindi la huzuni ambazo zimesababishwa na aina ya maisha au familia walimojikuta kiasi kwamba inaonekana kama kila kitu kimekwama. Haijalishi tunapita kwenye hali ngumu kiasi gani. Wito wa Bwana wa mabwana, Yesu Kristo bado uko palepale: Njoni kwangu ninyi nyote wenye kulemewa na mizigo nami nitawapumzisha (Mt 11:28). Bwana Yesu yuko kazini saa ishirini na nne. Karibu utiwe moyo na ushuhuda huu wa dada ambaye alishakata tamaa kabisa na kuamini kabisa kuwa tayari alikuwa kuzimu. Lakini Yesu anapoingia, kila kitu kinabadilika.



...............................

Nyumba niliyokulia ilikuwa na fujo nyingi. Maisha yangu yote nilikuwa nikitamani kuwa na familia, mahali penye usalama na ambako ninaweza kupendwa. Baba yangu mara nyingi alitutelekeza huku akimuacha mama atulee sisi binti zake watatu peke yake. Kila baba alipokuwa nyumbani, mara zote nilikuwa nikinyanyaswa kiakili, kihisia, kimwili na kingono. Japokuwa nilijitahidi sana kuwa mtoto mzuri, hakuna nilichofanya kikawa kizuri kiasi cha kutosha.

Dini yetu ilikuwa ni Ubudha na nyumba ya ibada ilikuwa ni sehemu kubwa sana ya maisha yetu. Dini hii ndiyo niliyoifahamu katika kukua kwangu. Nilifundishwa kuwa Yesu alikuwa ni mwanadamu tu ambaye aliishi miaka mingi iliyopita na Wakristo walikuwa ni watu waliopotea, ambao waliishi kwa kufuata sheria nyingi. Nikiwa bado msichana mdogo, nilikuwa ni mtu mwenye aibu sana.

Katika miaka yangu ya mwanzo ya utineja, nilivutiwa na imani za siri (occult). Nilianza kusoma vitabu na kununua vitu kwa ajili ya kuwatupia watu balaa. Nilipata nguvu kwenye imani hizo, na zaidi sana ikawa ni kama nimepata mahali pa kuelekeza maisha yangu. Kwa mara ya kwanza katika maisha yangu, nikawa naweza kujitawala. Kisha nikiwa na miaka 15 nilikata shauri kuyatoa maisha yangu na utashi wangu wote kwa shetani. Kuanzia wakati huo, maisha yangu yalianza kuporomoka. Shetani aliijaza nafsi yangu na akanipa nguvu, lakini wakati huohuo alikuwa akiyafyonza maisha yangu. Niliachana na kila kitu kizuri kuhusiana na mimi …. maadili, mitazamo na imani.

Wakati ningali bado naendelea kujishughulisha na Ubudha, kwa siri nilikuwa ninaabudu mapepo. Nilishiriki katika ‘black magic’ - yaani uganga wa kudhuru; na baadaye white magic – yaani uganga wa kuponya. (Nilidhani ni mambo mazuri – maana havikuwa katika jina la shetani). Ningependa kuongeza, hususan kwa faida ya wale wanaopenda “kujaribujaribu” tu uabudu shetani, kwamba unapofungua mlango kwa uabudu shetani, basi unakuwa umefungua mlango kwenye uovu ambao ni Yesu peke yake anaweza kuufunga.

Nilipofikia utu uzima, nilipokea madhabahu yangu mwenyewe ya Ubudha (gohonzon), kutokana na kuhimizwa na mama yangu, na nikajiingiza sana kwenye ‘new age movement’. Baadaye nikawa hata namfundisha binti yangu mambo hayo.

Kwa kipindi chote hiki, hakuna mtu maishani mwangu mwote aliyekuwa amewahi kunieleza ujumbe wa Kristo. Najua hili linaweza liwe gumu kuamini lakini nashuhudia hili, na natumaini kuwa kuna mtu atatambua kuwa ushuhudiaji una maana kubwa sana. Mtu kuzaliwa Marekani haina maana kuwa amewahi kusikia ujumbe wa Yesu.

Maisha yangu hatimaye yaliishia kwenye hali ya mfadhaiko mkubwa. Nililazwa hospitali mara mbili kutokana na hali hii. Kikundi cha watu niliowaita marafiki walikuwa si wa msaada bali nao walikuwa wanafyonza tu maisha yangu kila wanapokuwa na mimi. Maisha yangu yalikuwa giza kabisa na yenye fadhaa. Ilikuwa ni kama kuzama ndani ya wingu jeusi na hauna nguvu au utashi wa kutoka humo au kupata msaada. Nilifika mahali ambapo nikataa hata kupewa ushauri au dawa maana sikujali kama nitapata nafuu au la! Hatimaye nilifikia kuamini kabisa kuwa nilishaishi maisha yangu, nilishakufa na sasa nilikuwa kuzimu.  

Hii ilikuwa ni kuzimu kabisa. Majaribio ya kujiua yalishindwa kiasi kwamba yakanifanya niamini kuwa siwezi kufa tena, maana tayari nilikuwa mfu.

Jumatatu moja mfanyakazi mwenzangu alinijia. Alikuwa ni kanali wa jeshi na tulikuwa tukimwita Murph. Alisema kuwa wakati wa wikiendi aliwaza sana kuhusu binti yangu, Sara, pamoja na mimi. 

"Kweli???" nikasema.

"Ndiyo," alijibu, "Nilikuwa kanisani na ninyi wawili mlinijia mawazoni mwangu; na nilipenda mfahamu kuwa Bwana ameweka mzigo ndani yangu kuhusiana na ninyi; na ningependa mfahamu kuwa ninawaombea."

Nilipatwa na mshangao na sikujua cha kusema. Sikuwahi kusikia kitu kama hicho kabla ya hapo.

Wakati huo nilikuwa kwenye ndoa yangu ya pili ambayo ilikuwa mara inasimama mara inaanguka, na hatimaye ikaishia na kifo cha baba mkwe wangu. Jina lake aliitwa Chuck na alikuwa anakufa kwa kansa. Tulipendana na tulihitajiana kwa namna yetu. Mimi na mume wangu tulipatana katika kipindi hiki cha shida na sote tulihamia kwenye nyumba yangu. Chuck akawa ni mtu maalum sana kwangu na alikuwa karibu nami sana kwa namna ambayo hata kwa baba yangu sikuipata. Usiku mmoja nilikuwa nazungumza naye kuhusiana na kifo na akasema yeye haogopi kwa sababu alikuwa anaenda mbinguni. Tulishikana mikono na akalala. Nililia na kwa mara ya kwanza nilimwomba Mungu, nikisema: "Mungu, sijui kama unaweza kunisikia kutokea huku kuzimu, lakini kama unaweza, tafadhali naomba unisikie na unijibu maombi yangu. Mimi sikuamini wewe lakini najua kuwa Chuck anakuamini. Najua kuwa mimi nastahili kuwa hapa lakini Chuck hastahili kuwa hapa. Tafadhali mponye au mchukue aje kwako. Hakuna mtu anayetakiwa kuteseka namna hii."

Baada ya saa 36 Chuck alifia nyumbani kwangu. Na baadaye mwili wake ulipoondolewa, mume wangu alionyesha shukrani zake kubwa kwa jinsi nilivyotoa msaada na akaniambia kuwa sasa alikuwa tayari kukamilisha suala letu la talaka.

Dunia yangu yote iliporomoka! Nikawa nikikaa kwenye kona gizani katika bafu langu, ninashika kichwa changu, ninavuta nywele zangu na kulia kwa uchungu sana. Mateso yalikuwa hayasemeki. Nilikuwa natembea kwenye nyumba huku nikimpayukia Mungu wa Chuck.
"MUNGU, niondoe hapa! Sitaki tena kuendelea kuwa hapa! Ulimchukua Chuck pale nilipokuomba, kwa hiyo najua kuwa unanisikia! Niondoe hapa!"

Binti yangu alikuwa akinitazama tu. Alijaribu kunifariji nami ningempayukia na kumsukumia kule. "Hivi wewe huelewi? Mimi sijali! Sina muda na wewe, sina muda na kazi, sijali kuhusu hii nyumba; sijali! Mama yako hataki kuwa hapa tena!"

Uso wake ukawa kama jiwe. Alitembea huku amejiinamia, na akaficha ndani kabisa hisia zake.

Siku moja nilikuwa natafuta chaneli za TV chumbani kwangu. Nikawa nimefungua stesheni ya Kikristo na nikaanza kutazama ingawaje sikuwa naelewa yale waliyokuwa wanasema. Nikawa naiacha inaendelea kuongea kila ninapoenda kwenye ile kona yangu au ninapolala. Sikuweza kusikia mengi kutokana na kelele zilizokuwa kichwani mwangu. Lakini kidogo kidogo nilianza kukaa mbele ya TV. Sikuwa naelewa kile walichokuwa wanazungumza kwa kuwa sikuwa nimewahi kukaa na Wakristo. Hata hivyo, nikaanza kutaka kumjua huyu Yesu ambaye walikuwa wanamzungumzia sana.

Niliporudi kazini baada ya likizo, Murph aliniita ofisini kwake. Nilidhani kuwa nimetenda kosa. Ilishapita miaka miwili na nusu tangu aniambie kuwa alikuwa ananiombea. Alikuwa hajasema chochote kwangu kuhusiana na jambo hilo tangu wakati ule. Niliingia ofisini kwake na kufunga mlango. Alienda kwenye kiti chake na kukaa, kisha akaanza kulia.

Nakumbuka aliniambia, “Linda, Yesu anakupenda sana. Sijawahi kuacha kukuombea pamoja na Sara. Nimekuwa nawaombea kila siku tangu nilipokuambia jambo hili. Bwana anawapenda sana na ninapenda ujue jinsi ambavyo anawapenda. Ana mpango mzuri sana kwa ajili ya maisha yenu na ana shauku kubwa sana ya ninyi kumuamini tu. Tafadhali, tafadhali, muamini Yeye.”

Nilishikwa na mshangao! Hakuna mtu ambaye aliwahi kuniambia maneno kama hayo hapo kabla. Nadhani niliguswa na machozi yake na jinsi alivyoongea kutoka moyoni. Hakuna mtu aliyewahi kulia kwa ajili yangu kabla ya hapo. Baadaye aliongelea televisheni ya Kikristo na kuuliza kama huenda nitaweza kuangalia. Kwa kujivuna kabisa, nilimwambia kuwa tayari nilikuwa ninatazama.

Muda mfupi baada ya tukio lile, Murph alihamia Alabama. Niliendelea kuangalia vipindi hivi vya Kikristo kwa takriban miezi mitatu na kile hasa ninachokumbuka ni kuwa, viliendelea kuzungumza kuhusu Yesu na mambo ya ajabu ambayo ameshayafanya na anaendelea kuyafanya hivi leo. Nilitamani sana kupata imani hii ambayo waliendelea kuizungumzia. Imani kwamba Yesu anaweza kuponya akili yangu. Kila wakati mtu aliposema sala ya toba, nilikuwa nikilia na kuomba. Nilitamani tu kumjua huyu Yesu. Niliomba sala hii kila siku lakini nilijihisi kuwa naendelea kuzama zaidi na zaidi.

Usiku mmoja, wakati nikiwa nimesimama mbele ya TV yangu, nilihisi furaha na amani ambayo si rahisi kuielezea; ni furaha na amani ambayo sikuwa nimedhania nitakuja kuipata. Shetani akaniambia, “Hiyo si halisi. Nimekuwekea tu ili kukudhihaki; ili kukuonyesha kile ambacho ungekuwa umekipata, lakini badala yake ulinipa mimi maisha yako. Wewe uko kuzimu na umekuwa wangu milele.”

Ilikuwa ni kama barafu imepita kwenye mwili wangu na machozi yakaanza kunitiririka usoni. Matumaini yote yakatoweka kabisa. Siwezi kutoka humu. Sina pa kwenda. Siwezi kufa. Siwezi kuishi. Nimekwama!

Nikiwa naelekea sebuleni kwangu, nilimwambia shetani, “Ninajua kuwa mimi ni wako, ninajua kuwa niko kuzimu, lakini siko tayari tena kufanya yale uyatakayo! Ninajua kuwa hii ni himaya yako, lakini sitakutii tena kuanzia sasa. Kama unataka kunitupa nje ya kuzimu hadi mahali ambako hakuna kitu kabisa (ni utupu tu), nitafurahi kwenda huko. Ni bora nikae milele kusikokuwa na kitu kabisa kuliko kukaa na wewe!”

Ndipo kutoka kwenye hiyo hali ya kukata kabisa tamaa, nilisimama katikati ya sebule yangu, nikatazama juu na kuinua mikono yangu kuelekea mbinguni, na kupaza sauti, “Yesu, nitoe humu! Sitaki kuendelea kuwa humu. Ninatubu kutokana na chochote nilichofanya kilichosababisha unilete humu. Ninatubu. Tafadhali, tafadhali nisamehe!”

"Yesu," nilipaza sauti," wanasema kuwa kama nikikuita, utaniokoa. Wanasema kuwa kama nikikukiri Wewe kuwa ni Bwana na Mwokozi utakuja kwenye maisha yangu. Yesu, nitoe humu! Naamini kuwa ni Wewe pekee mwenye uwezo wa kufika hadi kwenye kina cha kuzimu na kuniokoa. Naamini kuwa Wewe ni Mwana wa Mungu. Naamini kuwa ulikufa kwa ajili yangu na ulifufuka kutoka kwa wafu. Nakiri kwa kinywa changu kwamba Wewe ni Bwana na naamini hayo kwa moyo wangu wote. Tafadhali, nisamehe! Tafadhali, niokoe!”

Wakati huu nilikuwa nimepiga magoti. Ghafla, niliacha kulia, nikainuka na kukaa kwenye kiti. Nikaona kuna kitu cha tofauti sana. Sikuwa nacheka au kububujika kwa furaha wakati huo, lakini nilichoona ni kuwa, kwa mara ya kwanza maishani mwangu, zile kelele zilizokuwa kichwani mwangu zilikoma! Kuchanganyikiwa kote kulitoweka! Nikasikia ukimya kwa mara ya kwanza!

Bwana wangu Yesu alinirudishia akili yangu iliyo sawasawa.

Ghafla nilisikia sauti ya tofauti. Sauti ambayo sikuwa nimewahi kuisikia hapo kabla. Alisema, “Huyo ni mwongo.”

Sauti hii ilinishangaza hadi nikakaa na kusema, “Nini?”

“Ni mwongo. Kila kitu alichowahi kukuambia ni uongo mtupu.”

Nilitafakari juu ya hilo kwa muda mfupi kisha nikasema, “Hebu ngoja kidogo. Kama ni mwongo, ina maana hata mimi siko kuzimu! Kama ni mwongo, basi mimi bado sijafa! Kama ni mwongo, basi maisha yangu hayako mwisho bali ndio kwanza yanaanza.”

Nilisimama nikiwa nimejaa ghadhabu kuliko niliyowahi kuwa nayo. Kisha nikapaza sauti, “Shetani! Wewe ni mwongo. Kila ulichowahi kunifundisha ni uongo. Nilikupa maisha yangu nikiwa mtoto na hayakuwa maisha ya kukupa wewe. Nayachukua tena! Maisha yangu ni mali ya Yesu Kristo. Nilikukaribisha maishani mwangu na sasa nakupiga teke hadi nje! Wewe huhitajiki tena humu!”

Nilitumia asubuhi yote iliyofuata nikiwa nimesimama jikoni, nimeangalia mbinguni, ninaimba na kulia. Hatimaye binti yangu alirudi kutoka kwa rafiki yake aliyeenda kumtembelea tangu jana yake. Aliuliza kama kuna kitu nilikuwa ninahitaji. Nilimwita na kuanza kulia, “Yu hai!!! Yu hai!!!”

"Nani yu hai?"

"Yesu. Yesu yu hai. Si mfu. Yeye si hadithi tu au mtu wa kwenye historia tu. Yeye yu hai kabisa!"

"Sawa mama. Chochote utakachosema..." lilikuwa ndilo jibu lake la mshangao.

Niliweka mikono yangu mabegani mwake kwa upole na kusema, "Nisikilize. Hili ni jambo la muhimu sana. Kama hukuwahi kusikiliza jambo lolote nililowahi kukuambia, sikiliza na uamini hili … kila kitu nilichowahi kukufundisha ni uongo mtupu – kila kitu! Nilikuwa niko kwenye makosa sana na nimekuambia uongo maisha yako yote. Kile nilichowahi kukuambia kuhusiana na Wakristo kilikuwa ni makosa. Kile nilichokufundisha kuhusiana na matufe ya kioo (crystals), maono (psychics), roho (spirits), na walimu wabobevu (master-teacher guides) kilikuwa ni uongo. Yesu Kristo ndiye kweli pekee!"

Nilijawa na hofu na kumheshimu Mungu. Sikuwa nimewahi kukutana na jambo kama hili maishani mwangu. Mara moja nilichukua likizo ofisini kwangu. Sikuwa najua ni nini kimenitokea – nilichojua tu ni kuwa, sikuwa yuleyule wa siku zote. Wakati huo nilikuwa nina welewa kidogo sana kuhusu Ukristo, kiasi kwamba ni hadi ulipopita mwezi mzima ndipo nilipotambua kuwa kumbe nilikuwa ‘nimezaliwa upya!’

Binti yangu alienda Alaska kumtembelea baba yake nami nikatumia muda wangu wote kusoma Biblia. Biblia ileile ambayo niliinunua ili kuitumia kinyume na Mungu, ilikuwa sasa inatumika kwa ajili ya utukufu wake. Kila neno lilikuwa linasisimua na liko hai. Bwana alinihudumia kwa namna ya ajabu sana.

Jambo la kukumbuka tu … Kila kitu kinachofanywa kwenye uabudu shetani kinatajwa kwenye Biblia. Kila kitu kuanzia mawe ya vito (gem stones), kuwasiliana na roho zingine (consulting psychics), kuita wafu (conjuring the dead) hadi utoaji sadaka (sacrifices). Shetani amechukua mambo ya kwenye Biblia na kuyapindisha. Nilikuwa natumia Biblia kuwaonyesha watu wenye dini kuwa mambo haya ni sawa tu maana yametajwa hata kwenye Biblia yenu.

Binti yangu alirudi nyumbani lakini bado alikuwa na mashaka.
Linda
Alinitazama kwa makini sana. Lakini alichogundua ni jambo halisi kabisa; ni mama mpya kabisa! Aliniona nikikua ndani ya Kristo. Aliona nguvu mpya na uhai ndani yangu. Akapata mama anayecheka. Akawa na mama anayeweza kumkumbatia na kumpenda. Aliona mtu tofauti kabisa. Hatimaye, aliamua kuwa naye anataka kumfuata Yesu na sote tulibatizwa.

Miezi michache baadaye nilipata fursa ya kuzungumza na Murph. Nilimweleza kilichotokea na kwa kweli alifurahia sana kwa moyo wake wote. Alilia na kubaki tu kusema, “Asifiwe Bwana. Asante Yesu.”

Ningependa kuongezea hapa kuwa, kama Bwana ameweka mzigo moyoni mwako ili kuomba kwa ajili ya mtu fulani, tafadhali, tafadhali, usiache kuomba. Maisha yao ya hapa na yajayo yanaweza kuwa yanategemea maombi yako hayo. Usiache kuomba na tafadhali usikate tamaa juu ya mtu huyo.

Muda mfupi baadaye, Murph alienda kwa nyumbani kwa Bwana. Sikuhuzunika, bali nilifurahia, nikijua kuwa atakuwa amesimama uso kwa uso na Bwana wetu.

Jambo moja zaidi … unakumbuka juu ya madhabahu yangu ya Ubudha? Mara baada ya kuokolewa, nilikuwa ninasafisha takataka zangu zote ikiwa ni pamoja na kuchimbua matufe yangu ya kioo niliyokuwa nimeyachimbia kwenye nyumba yangu. Tulipita kila kona na kutupa nje kila kitu – ikiwa ni pamoja na matufe ya kioo, tarot cards, vifimbo (wands), vitabu, mawe, kengele, mishumaa na kila kitu kinginecho.

Nilifika kwenye madhabahu ile ndani ya kabati na Bwana akaniambia niiache. Kwa hiyo niliiacha. Kwa kama miezi mitatu hivi iliyofuata, nikawa nasikia,  "Si kwa uweza, si kwa nguvu, bali kwa Roho yangu."

Sikuelewa alikuwa anamaanisha nini. Ndipo siku moja, katika sherehe za Halloween, nilikuwa niko jikoni na Bwana akaniambia, "Kumbuka madhabahu."

"Nini?" nilisema kwa mshtuko.

"Kumbuka madhabahu. Irudishe."

Nikamwambia nitaitupa. Lakini akasema niirudishe. Nikamwambia nitaipeleka kwa mama yangu. Akasema tena niirudishe. Nikamwambia sijui pa kuipeleka. Akasema, “Wewe irudishe tu mahali ulikoichukua.”

Kwa kifupi ni kuwa, nilitafuta hekalu kule Dallas. Nilipiga simu ili kuuliza naweza kwenda lini na matokeo yake nikaanza kuzungumza na mwanamume mmoja kwenye simu. Baada ya muda mrefu, nikamwambia anielekeze niipeleke wapi ile madhabahu vinginevyo nitaitupa tu kwenye shimo la taka. 

Aliniuliza jina langu, nikamwambia naye akaniambia jina lake. Ikatokea kwamba alikuwa ni kiongozi wa hekalu kule San Francisco, nilikokulia, ambaye aliwahi kunifundisha kuwa hakujawahi kuwako mtu aliyeitwa Yesu Kristo. Wakati huu alikuwa amehamishiwa kwenye makao makuu mjini Dallas. Alikubali kukutana na mimi huku akisema kuwa anatarajia kunishawishi kuhusiana na kosa nililokuwa ninalifanya.

Nilipofikisha gari kwenye maegesho, nikaanza kuliegesha karibu na gari moja tu lililokuwapo hapo. Bwana akasema, “Hapana. Sio hapa.” Kwa hiyo niliondoka na kuishia kwenda kuegesha uso kwa uso na gari hili. Nilipokaribia jengo, nikamtambua mwanamume yule mara moja. Alikuwa akiongea na watu wengine watatu ambao walionekana kuwa wanakwenda kula chakula cha mchana.

Walipoondoka, nilijitambulisha kwake na akajaribu kuwasimamisha wale wengine watatu – ambao walionekana kuwa ni viongozi wa hekalu. Hawakumsikia. Sote tulienda kwenye gari langu na tulikuwa tumesimama kwenye gari langu wakati watu wale watatu walipokuwa wanaingia kwenye gari lao mbele yangu.

"Subirini, msiondoke! Huyu ndiye mwanamke ambaye nilikuwa nawaeleza habari zake. Walitabasamu na kunipungia mikono na wakaingia kwenye gari lao.

Akapaza sauti, "Hapana. Subirini. Huyu ni mwanamke ambaye anataka kurudisha gohonzon yake. Huyu ni mwanamke ambaye nilitaka mumwone." Walisimama milangoni huku wakitabasamu, wakipunga mikono na kunipongeza. Walisema kuwa walikuwa na furaha juu yangu na wangependa kuongea na mimi wakati mwingine.

Huku akikanyaga miguu yake na kupunga mikono yake, alisema, "Hivi hamnisikii? Au hamnielewi? Huyu mama ANARUDISHA!" Walitabasamu, wakapunga tena mikono na kuingia kwenye gari na kuondoka. Sote tulibakia tumesimama tu pale. Alionyesha uso wa kuchanganyikiwa. Sikuweza kuelewa ni kitu gani kilichokuwa kinatokea hapo. Tulikusanya kila kitu na kuingia kwenye jengo. Aliuliza maswali mengi huku akijaribu kuelewa ni kwa nini hasa nilitaka kuirudisha ile gohonzon.

"Je, kuna watu walikuja nyumbani kwako na kukupatia maandiko ya kusoma?"

"Hapana."

"Je, una mume au rafiki wa kiume anayesababisha ufanye hivi?"
"Hapana."

"Je, ni marafiki wamekuambia kuwa unatakiwa kufanya hivi?"
"Hapana."

Nilicheka na kusema, "Sina marafiki wowote. Nilimpoteza kila mmoja wao pale nilipoamua kuwa Mkristo."

Hatimaye nikamwambia, "Wewe hauelewi. Yesu Kristo mwenyewe alikuja kwenye chumba changu, kule Grand Prairie, Texas, na akanigusa."

Kisha akaanza kuuliza maswali kuhusiana na dini.
"Wewe ni dini gani?"

"Sielewi swali hilo. Sijui dini mbalimbali zilivyo na maana zake.”

"Je, wewe ni Mbaptisti? Mmethodisti? Mkatoliki? Wewe ni Presbiteriani? Je, unajua ni dini gani uliyomo?"

"Hapana. Si yoyote kati ya hizo. Sijui tofauti kati ya dini hizo."

"Sawa. Basi niambie wewe ni mshirika wa kanisa gani."

"Ninaenda kwenye Makanisa yanayompenda Yesu."

Nilipoona kuwa anavurugikiwa na majibu yangu, nikasema, "Samahani kwa kuwa na majibu ya namna hii lakini kusema kweli sielewi maswali unayouliza. Kama ningejua majibu yake, basi ningekujibu. Mimi ni Mkristo.”

"Kama ni Mkristo, basi ni lazima uwe kwenye kundi fulani. Kama ni Mkristo, iweje usiwe kwenye dini?” alisema.

"Sawa... ninachojua mimi tu ni kwamba Yu hai na alikuja kwenye chumba changu na kuokoa maisha yangu. Nimeshasoma Biblia yangu na Kanisa pekee nililokutana nalo ni Mwili wa Kristo. Kama ni lazima niwe kwenye kundi fulani, basi nadhani niseme kuwa mimi ni mshirika wa Mwili wa Kristo.”

Palepale, Bwana akaniambia, "Si kwa nguvu, si kwa uweza, bali kwa Roho yangu uliokolewa. Huu ndio uwe ushuhuda wako."

Na kwa hiyo, huu ndio ushuhuda wangu ninaokuletea leo. Maisha yangu hayakubakia kama yalivyokuwa. Ninamshukuru Bwana Yesu kwa kutonisahau.

Kusema kweli, mimi nilikuwa mdhambi mkubwa kabisa lakini hata hivyo hakunisahau au kuniacha. Licha ya yote niliyotenda, alinisamehe. Bado ninashangaa, na hakuna siku inayopita bila ya mimi kumshukuru kwa kuwa alinikumbuka mimi na kuniokoa. Ni vigumu siku kupita bila mimi kumweleza mtu ushuhuda huu.

Linda na familia yake

Bwana amenibariki kwa kunipa tena mume mwingine, na safari hii, ndoa yetu ni ndani ya Kristo! Picha hii ni ya mimi; mume wangu wa sasa; Olli; binti yangu, Sara; na mjukuu wangu, Jared.

Kusema kweli, Yesu ndiye jambo la thamani sana nililonalo! Bila Yeye najua kuwa mimi nimekufa. Ni kwa sababu yake tu ndiyo maana ninao uzima na hakika ninao tele. 

Asante na Mungu akubariki kwa kutumia muda wako kusoma ushuhuda wangu. Kama kile nilichokisema kimekugusa kwa namna yoyote na ungependa kuwasiliana nami, naweza kupatikana kwenye baruapepe hii: lynlaine@comcast.net  (Tafadhali tumia Kiingereza tu).

………………………….

Mpendwa msomaji, kama ungependa kusoma ushuhuda huu kwa Kiingereza, basi bofya HAPA.

3 comments:

  1. Yesu ni Jibu la Maisha yangu. Nafurahishwa na shuhuda hizi zinanijenga sana. Kila siku naingia humu naona kimya

    ReplyDelete
    Replies
    1. Shalom Juliana. Pole sana kama unakuta kimya. Lakini wakati mwingine ratiba yangu inakuwa na vitu vingi sana kiasi kwamba najikuta sijafanikiwa kukamilisha makala za humu. Wakati mwingine naandaa makala za kwenye blog yangu nyingine: www.waislamukwayesu.com; na makala moja inanichukua muda hadi ikamilike. Mungu akubariki dada yangu usichoke kutembelea. Mungu atatuwezesha tu.

      Delete
  2. BWANA YESU ASIFIWE MILELE NA MILELE

    ReplyDelete