Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa
mfano wetu,
kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini,
na ndege wa angani, na wanyama, na nchi
yote pia,
na kila chenye kutambaa kitambaacho juu
ya nchi.
(Mwanzo 1:26).
Tazama nimewapa amri
ya kukanyaga nyoka na nge,
na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu
kitakachowadhuru. (Luka 10:19).
‘Kutawala’ ni kuwa na
mamlaka, amri au usemi wa mwisho juu ya jambo au hali. Hii ina maana kwamba
chochote kilicho chini ya mamlaka hayo hakiwezi kufanya kilicho juu ya mamlaka
hayo iwapo mamlaka yenyewe yamesimama sawasawa.
Biblia inasema: Basi imani, chanzo chake ni kusikia;
na kusikia huja kwa neno la Kristo (Warumi 10:17).
Lakini swali la
msingi ni kwamba, je, hatujasikia? Je,
wanaoumwa ni wale ambao hawajawahi kusikia Neno lisemalo: Kwa kupigwa kwake sisi tumepona (Isaya 53:5)? Je, wenye hofu ni wale tu
ambao hawajasikia kwamba Bwana ameshasema: Maana Mungu hakutupa roho ya woga,
bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi (2 Timotheo 1:7)?
Jibu ni HAPANA! Tayari tumeshasikia na kusikia na kusikia ....!
Inakuwaje basi lisitimie kwetu neno lisemalo: Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa
neno la Kristo; ili kwamba imani hiyo ituwezeshe kushinda katika kila jambo? Mbona
tunazidi kulemewa na shida za dunia hadi tunakata tamaa na hata kufikia
kumwacha Kristo? Au huku kusikia kunakotajwa kwenye Warumi 10:17 ni tofauti na
maana tunayoijua ya neno hilo?
Imeandikwa kwamba: Bali vitokavyo kinywani vyatoka moyoni; navyo ndivyo vimtiavyo mtu
unajisi. (Mathayo 15:18).
Na tena: … Maana, kinywa cha mtu huyanena yaujazayo moyo wake. Mtu mwema
katika akiba njema hutoa mema; na mtu mbaya katika akiba mbaya hutoa mabaya. (Mathayo
12:34-35)
Kwa kuwa: Yote yawezekana kwake aaminiye (Marko 9:23), basi, kushindwa
kwangu kuna maana kwamba sina imani; pia sijasikia
kwa jinsi ambayo itaniwezesha kupata hiyo imani inayoweza yote!
Na kwa kuwa Bwana anasema katika Waefeso 3:20 Basi atukuzwe yeye
awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa
kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani
yetu, (na si kwa kadiri ya nguvu itokayo juu mbinguni), ina maana kwamba
tatizo limo ndani yangu, yaani kwenye moyo.
Ukiniuliza kuhusu maandiko mbalimbali na ahadi za Mungu,
ninaweza kukutajia moja baada ya jingine. Lakini iwapo sina nguvu ya kugeuza
hali yangu, ina maana kuwa ninajua tu kwa akili lakini si kwa moyo. Ni nguvu itokayo
moyoni tu ndiyo inayobadili mambo! Kwa hiyo, kama Neno la Kristo halimo moyoni
mwangu, basi humo kuna neno la mwingine!
Kwa nini nimejawa na hofu, mashaka, wasiwasi, huzuni, kukata
tamaa, n.k. ilhali hakuna kokote kwenye Biblia ninakoagizwa kuwa hivyo? Ni kwa
sababu hayo ndiyo yaujazayo moyo wangu – ndiyo maana yananitoka muda wote.
Kumbe basi imani ninayo; isipokuwa tu nina imani na neno la
adui. Nimesikia neno la adui – na hilo ndilo ambalo limeujaza moyo wangu.
Neno la adui linasemaje? Linasema:
Huwezi!
Hufai!
Umeshindwa!
Hauna nguvu!
Haufiki popote!
Una dhambi!
Wewe ni maskini!
Hautapona!
Maisha ni magumu!
Hawakupendi!
Hujasoma!
Utashindwa tu!
Unapoteza tu muda!
Kazi hazipatikani kirahisi!
Bila kutoa kitu kidogo hutafanikiwa!
Wengi walishajaribu wakashindwa!
n.k, n.k, n.k …..!
Neno hili linatokea wapi? Mungu ana kitabu cha Biblia lakini
shetani hana kitabu kilicho wazi. Lakini anayo ‘injili’ yake mbaya. Neno lake
linakuja kwetu tangu tunapozaliwa. Neno hilo linatokea kwa wazazi, ndugu, walezi,
majirani, marafiki, redio, televisheni, muziki, magazeti, wanasiasa, wapita njia,
n.k.
Tunalisikia neno hili karibu muda wote. Matokeo yake, bila
hata sisi kujua, neno hili limejaa tele mioyoni mwetu na ndilo limekuwa sehemu
ya mawazo yetu na miwani ambayo kwayo tunayaona na kuyapima maisha.
Je, Mungu ni mwongo? Hapana!
Je, Mungu hajui anachokisema? Hapana!
Je, Mungu ana uhakika kabisa
na kile anachosema? Ndiyo!
Kama basi ni kweli amenipa mamlaka au amri juu ya vyote kama
anavyosema kwenye Mwanzo 1:26, je, ina maana kwamba ninayo amri juu ya nyoka, samba,
nge, moto, mafuriko, mvua, ukimwi, utasa, ajali na hata mauti?
Kwa kuwa Mungu si mwongo, jibu ni NDIYO!!!!
Kama hivi ndivyo, basi tatizo si Mungu; wala tatizo si Neno
lake, bali ni habari ya ndani ya moyo wangu; maana imeandikwa: … atukuzwe yeye
awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani
yetu (Waefeso 3:20).
Kusikia kunakotajwa kwenye Warumi 10:17 si suala tu la sauti
ya muhubiri kupenya ndani ya masikio yangu. Hapana! Ni zaidi ya hapo.
Udongo mgumu ukinyeshewa na mvua kwa mara moja kisha jua
likauwakia kwa siku 7, utaukuta ni mkavu – lakini kuna mvua iliunyeshea! Lakini
ukinyeshewa kwa siku 7 na kuwakiwa na jua kwa siku moja, utaukuta ni mbichi.
Sisi nasi, kama udongo, tumeshasikia na kusikiliza
(kutafakari) mambo mabaya (neno la adui) tena na tena maishani mwetu kuliko
tulivyofanya kwa Neno la Kristo. Hivyo, mvua ya neno la adui imeweza kupenya
ndani sana kwenye mioyo yetu. Kwa hiyo, ile nguvu itendayo kazi ndani yetu ni
nguvu ya adui, ambayo ni nguvu ya uharibifu na kushindwa. Imani chanzo chake ni
kusikia. Imani ya kushindwa imejaa kwetu na kuwa na nguvu kutokana na kusikia
zaidi neno la adui!
Pamoja na kwamba tumeshasikia karibu kila Neno la Bwana wetu
Yesu, maandiko hayo hayajatufaa sana maana kinachoendelea ni kama kunyeshewa na
mvua ya siku moja ya neno la Bwana na kuwakiwa na jua la siku 7 la neno la
adui.
Hebu tujipime kama tunatenda sawasawa na vile inavyotakiwa. Je,
Bwana mwenyewe anasemaje?
- Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana (Yoshua 1: 8).
- Mwanangu, kama ukiyakubali maneno yangu, Na kuyaweka akiba maagizo yangu; hata ukatega sikio lako kusikia hekima, Ukauelekeza moyo wako upate kufahamu; naam, ukiita busara, Na kupaza sauti yako upate ufahamu; ukiutafuta kama fedha, Na kuutafutia kama hazina iliyositirika; ndipo utakapofahamu kumcha Bwana, Na kupata kumjua Mungu (Mithali 2:1-5).
- Nawapenda wale wanipendao, na wake wanitafutao kwa bidii wataniona (Mithali 8:17).
- Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakarini hayo. (Wafilipi 4:8).
- Akawaambia, Kwamba utaisikiza kwa bidii sauti ya Bwana, Mungu wako, na kuyafanya yaliyoelekea mbele zake, na kutega masikio usikie maagizo yake, na kuzishika amri zake, mimi sitatia juu yako maradhi yo yote niliyowatia Wamisri; kwa kuwa Mimi ndimi Bwana nikuponyaye (Kutoka 15:26).
Naamini wengi wetu tutakubaliana kwamba kipengele cha bidii katika kusikiliza, kusoma na kutafakari Neno la Kristo
kimekosekana kwetu. Sasa, kama hakipo inawezekana Neno hilo likafika moyoni
ambako ndiko linatakiwa kuzalisha nguvu ya kutushindia?
Mimi ninapotembea njiani, ninapokuwa kwenye daladala, n.k., huwa nasikia
mechi za mpira zikitangazwa. Lakini kwa kuwa mimi si shabiki wa mpira maneno
hayo huwa tu ni kama mvua ya siku moja kwenye udongo mgumu. Hata timu inapofunga
na watu wanaruka na kushangilia kwa kelele nyingi, kwangu hata kamsisimko
kadogo sipati kabisa – lakini ninakuwa nimesikia mtangazaji akisema, “Gooooo!”
Ni masikioni tu, lakini neno lake halivuki zaidi ya hapo.
Lakini hebu mwangalie shabiki mwenyewe wa mpira. Yuko makini kusikiliza na
kufuatilia kila neno la mtangazaji. Hata ukimsemesha, anaweza akakasirika kwa
hasira ya kweli kabisa! Kwa nini? Hataki apitwe hata na neno moja. Yuko makini
kweli kusikiliza kila kitu. Anasikiliza kwa bidii.
Kwa umakini huo, ni lazima kile
anachosikia kinapenya moja kwa moja hadi ndani kabisa. Ndiyo maana kinazalisha
hata nguvu ya kuruka na kupiga kelele pale timu yake inapofunga; au nguvu ya
kulia na kushindwa kula timu hiyo inapofungwa. Kwa nini? Ni kwa sababu kile
anachokisiliza anakipa nafasi yote ya kufika hadi ndani kabisa kwenye mtambo wa
kuzalishia nguvu – yaani moyo.
Neno la Kristo lina nguvu kubwa sana ya kutenda chochote alichoahidi Bwana
pale tu tutakapolipa nafasi ya kufika kwenye moyo – si kwenye ubongo (akili)!
Je, shabiki wa mpira hufanya mazoezi ya kushangilia au kulia kabla ya
kuanza kusikiliza mechi? Hapana! Anachofanya ni kutoa tu umakini; kusikiliza
kwa bidii kile kinachotangazwa. Kisha lile neno la mtangazaji lenyewe
linazalisha nguvu ama ya kukasirika, kushangilia au kulia.
Imani chanzo chake ni kusikia neno kwa bidii zote. Yaani, kile
tunachosikia, kikifika tu moyoni, kinageuka na kuwa imani ‘automatically’. Kwa hiyo,
kama bidii yetu tumeiweka kwenye kusikia zaidi neno la adui, itazaliwa imani ya
kushindwa. Kama bidii yetu ni katika Neno la Kristo, itazaliwa imani ya
kushinda.
Mpendwa, usifanye bidii kutafuta imani. Fanya bidii kutafuta Neno. Hata Biblia
nayo inasema: Mitume wakamwambia Bwana, Tuongezee imani (Luka 17:5).
Lakini Bwana alifanya nini? Badala ya kuwaongezea, aliwaambia: Kama mngekuwa na imani kiasi cha chembe ya haradali, mngeuambia
mkuyu huu, Ng'oka, ukapandwe baharini, nao ungewatii (Luka 17:6).
Imani haiongezwi kutoka kwa Bwana. Imani inatokea ndani pale Neno
linapopewa nafasi kufika hadi moyoni. Bidii kubwa kwetu iwe ni katika kuingiza
Neno la Bwana wetu kwenye mioyo yetu. Imeandikwa: Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu (Wakolosai
3:16).
Hatuwezi kupiga hatua yoyote ya maana kama muda mwingi tunasikiliza ya
dunia – ambayo kwa sehemu kubwa ni ya adui.
- Hebu tujipime kidogo kwa maswali machache yafuatayo:
- Je, una ugonjwa wa muda mrefu? Je, unawaza zaidi mawazo ya Kristo ya kupona au ya adui ya kutopona?
- Je, haujaolewa? Je, unawaza zaidi kuwa utaolewa au unawaza zaidi kuwa umri unakwenda?
- Je, hauna kazi?
- Je, haujapata mtoto?
- Je, kuna dhambi inayokutesa?
- Je, unakabwa na wachawi kila siku?
- Je, biashara yako haiendi vizuri?
- Je, unafeli masomo darasani?
- Je, una shida gani maishani mwako?
Swali kuu sasa ni je, unawaza zaidi Neno la Kristo juu ya hali yako au neno
la adui? Ni kweli unaweza pia kuwa na maandiko yenye ahadi za Mungu kuhusu hali
yako, lakini je, yako moyoni au yako kichwani tu? Cha moyoni ndicho cha maana. Sasa
hicho ni Neno la Kristo au ni neno la adui?
Neno la Kristo likifika moyoni utajua tu, maana hofu na mashaka yote
yataondoka kwako. Lakini kama hofu na mashaka bado vimo ndani yako, basi ni
wazi kuwa neno la adui ndilo lililoko moyoni; na imani iliyomo ni ya kushindwa.
Tunafikishaje Neno la Kristo moyoni?
- Kusoma Neno la Kristo (Biblia) zaidi na zaidi na zaidi. (Kumbuka, tunazo hofu na mashaka kwa kuwa tunasikia neno la adui zaidi na zaidi na zaidi).
Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia
kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo
utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana (Yoshua 1: 8).
- Kutafakari Neno la Kristo na mambo mema zaidi na zaidi na zaidi.
Hatimaye, ndugu
zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo
ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa
njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakarini hayo. (Wafilipi 4:8).
- Kunena kwa lugha zaidi na zaidi na zaidi.
Yeye anenaye kwa
lugha hujijenga nafsi yake (1Wakor 14:4).
- Kufunga na kuomba ili kutiisha mwili. Kumbuka kwamba hatufungi ili kumshawishi Mungu atufanyie mambo tuyatakayo. Mungu alishafanya kila kitu tayari kwa ajili yetu (Waefeso 1:3).
Tunafunga ili kwamba mioyo yetu iweze kuwa katika mstari
sahihi unaoruhusu kupokea kile amacho tayari tulishapewa na Baba yetu.
Mwanafunzi anapoacha kitanda chake na kwenda kusoma usiku,
hafanyi hivyo ili kumshawishi mwalimu ampe maksi nyingi. Bali anafanya hivyo
ili kuiweka akili kwenye mstari unaoruhusu yeye kupokea maksi nyingi kulingana
na yote ambayo mwalimu tayari
anakuwa amemfundisha.
Kukataa kwa makusudi kila jambo la kidunia ambalo ni kinyume na Neno la
Kristo – iwe ni muziki, sinema, matangazo ya biashara, mazungumzo mabaya, n.k.
Kwa mfano, muziki wa kidunia unavutia sana. Lakini huo ni ujumbe wa mauti. Hauna
uzima ndani yake. Na kati ya vitu vyenye nguvu na uwezo mkubwa wa kwenda moja
kwa moja hadi moyoni ni muziki. Labda mtu atasingizia kwamba anajiburudisha na
kujipatia mafunzo mbalimbali kutoka humo. Huo ni uongo wa kuzimu na udanyanyifu
wa moyo (Yer 17:9).
Shida ya imani, kama tulivyoona, ni kuwa, inazalishwa na neno linaloingia
moyoni – si kwa juhudi za mwanadamu. Pasipo kujua, utajikuta unayo tu hiyo
imani. Kumbe imetokana na neno la adui lililoingia moyoni kupitia bongofleva,
sinema, magazeti ya udaku, n.k.
Hitimisho
Moyo ndiyo sehemu ya muhimu kuliko zote kwa mwanadamu. Ndiyo maana hata
Bwana akasema: Linda sana moyo wako kuliko yote
uyalindayo; maana ndiko zitokako
chemchemi za uzima (Mithali 4:23).
Bidii yetu ni katika kulifikisha Neno la Kristo mioyoni. Kisha Neno hilo
litafanya mengine YOTE yanayosalia. Bwana anaahidi:
Maana kama vile mvua
ishukavyo, na theluji, kutoka mbinguni, wala hairudi huko; bali huinywesha
ardhi, na kuizalisha na kuichipuza,
ikampa mtu apandaye mbegu, na mtu alaye chakula;
ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika
kinywa changu; halitanirudia bure, bali litatimiza
mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma.
Maana mtatoka kwa
furaha, Mtaongozwa kwa amani; Mbele yenu milima na vilima vitatoa nyimbo; Na
miti yote ya kondeni itapiga makofi.
Badala ya michongoma
utamea msunobari, Na badala ya mibigili, mhadesi; Jambo hili litakuwa la kumpatia Bwana jina, Litakuwa ishara ya milele
isiyokatiliwa mbali (Isaya 55:10-13).
Ardhi haifanyi chochote zaidi ya kunywa tu maji ya mvua. Kisha mvua yenyewe
(sio ardhi), inachipusha mimea kwenye ardhi.
Neno la Kristo likiingia kwenye moyo kwa wingi, ahadi zote za Bwana
zitachipuka tu!! Lazima!! Hata kama ibilisi na mashetani wote wangepinga kiasi
gani, lazima Neno la Kristo litashinda tu!! (maana tusisahau kuwa upinzani ni
lazima uko palepale).
Tahadhari
Katika makala yangu mengine huko nyuma niligusia kwamba moyo ndiyo kile
ambacho wanasaikolojia huita ‘sub-conscious mind’. Ukisoma kwenye mtandao au
kwingineko, utakutana na masomo yanayosema: “How to use the power of the sub-conscious
mind to obtain anything you want in life”, yaani “Kutumia nguvu ya akilifiche
kupata chochote ukitakacho maishani mwako.”
Masomo ya namna hii ni hatari sana kwa sababu kimsingi hii ni ibada ya
sanamu (idolatry). Ibada ya sanamu ni kutumainia kitu kingine chochote (au wewe
mwenyewe) badala ya Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo.
Nguvu yetu inatoka kwa Bwana pekee. Anasema wazi: Mtumaini BWANA kwa moyo
wako wote, wala usizitegemee akili zako mwenyewe (Mithali 3:5). Na tena
anasema: ... pasipo mimi ninyi hamuwezi kufanya neno
lolote. (Yohana 15:5).
Watu wanaofundisha masomo haya wanasema,
kimsingi, kuwa sub-conscious mind ina uwezo wa kufanya lolote litokee kama
unavyotaka, maadamu tu uwe na shauku kubwa ya kuyapata na kuamini kabisa kwamba
itayatenda hayo.
Huo ni mtego wa adui utakaosababisha tujitenge
mbali na Mungu wetu na kujitumainia wenyewe.
Hebu basi na tufanye bidii katika kuondoa usikivu
wetu kwa dunia ili Neno la Kristo liweze kukaa kwa wingi muda wote mioyoni
mwetu. Hakika Neno hilo litaichipuza ardhi ya mioyo yetu kulingana na yale
yaliyo shauku za mioyo yetu.
Na imani inakua kadiri tunavyozidisha bidii ya
kusikia!
Sasa, kama ni neno lenyewe ndilo linaloumba
imani; ndilo linalotenda kile alichoahidi Baba yetu wa Mbinguni – ilhali kazi
yetu ni kuliingiza tu ndani yetu kupitia bidii ya kusoma, kutafakari,
kusikiliza, n.k., je, unaona sasa maana ya maneno ya Bwana wetu kwamba: YOTE
YAWEZEKANA KWAKE AAMINIYE (Mk 9:23)?
Sisemi kuwa ni rahisi, bali ninasema kuwa
INAWEZEKANA maana Bwana ndiye anayetenda kazi ndani yetu! Kwa kuwa: Mungu
akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu? (Warumi 8:31).
Bwana Yesu akubariki na kukutia nguvu mpendwa
msomaji na ndugu yangu.
Big Up James
ReplyDeleteAmen Ruta. Sifa kwa Bwana wetu aliye juu ya yote.
ReplyDeleteHuuu!!! yani hapa nimefunguka ufahamu kabisa nimegundua kuwa kumbe Mungu hana shida na sisi bali sisi mioyo yetu ndiyo yenye shida kwa kushindwa kusikia vizuri, mimi nilikuwa namuomba Mungu wa Bwana wangu Yesu Kristo anizidishie imani yaani aiongeze imani yangu, Loh!! kumbe nilikuwa kinyume, huwa natamani sana nione natengeneza miujiza yangu mwenyewe kwa imani lakini nashindwa na ndo maana nikajua imani yangu ni hamna kabisa coz maisha yangu yametawaliwa na kushindwa, kutokuweza na kutokufanikiwa sa najiuliza nifanyeje mimi mara nyingi huwa nasoma sana neno na maombi lakini nimejua kuwa shida ipo moyoni mwangu
ReplyDeletena mtu akianza kuniuliza maneno ninayo mengi sana, hata naweza kufundisha wengine lakini huwa najiuliza nitawezaje ambia wengine kuwa Yesu anaweza na hali bado hajaweza kwangu, lakini nimegundua kuwa kumbe maneno mengi ya Mungu niliyonayo yapo akilini mwangu na si moyoni mwangu,
sasa najiuliza kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yangu ndipo Mungu atanitendea mambo makubwa kumbe kama hiyo nguvu sina ndani yangu siwezi kupata kuipata miujiza yangu,
kwa kweli Mtumishi Mungu akubariki sana tangu sasa nitaanza kuushugulikia moyo wangu mpaka kieleweke.
Mungu azidi kukuinua!!
Shalom mpendwa. Umenichekesha na kunibariki sana hasa nilipofika mwisho wa maneno yako kwamba: "tangu sasa nitaanza kuushugulikia moyo wangu mpaka kieleweke."
DeleteNi kweli kabisa ulichokisema kwamba Mungu hana anachotunyima. Ametubariki kwa baraka ZOTE katika Kristo. Shida ni kuwa sisi hatujakaa mkao wa kuzichukua, Ndiyo maana anasema wazi kuwa: apandacho mtu ndicho atakachovuna. Apandaye haba, atavuna haba.
Andiko hili hutumiwa zaidi kuhusiana na sadaka na matoleo, lakini lina maana zaidi ya hapo. Kadiri tunavyomtafuta Mungu kwa bidii (kwa maombi, kufunga, kusoma neno, n.k.), ndivyo tunavyopanda kwa nguvu na matokeo yake ni kuvuna sana - iwe ni uponyaji, n.k.
Yote haya yanahitaji moyo uliokaa sawa kulingana na neno.
Bwana akubariki na kukutia nguvu.
amina. Mungu awe pamoja nasi.
ReplyDeleteAmina Mtumishi James John Ubarikiwe sana!
ReplyDeleteBarikiwa mtumishi wa bwana.Mungu aendelee kukutumia kwa ajili ya utukufu wake.
ReplyDeleteMungu akubariki sana kwa mafundisho yako mazuri ya kiroho na akujalie ustahimilivu wa kiroho ktk maisha yako duniani.AMINA.
ReplyDeleteMhuuuuuu,ujinga lazima utakimbia tu.
ReplyDeleteBARIKIWA MTUMISHI
ReplyDelete