Yapo mambo mengi sana
ambayo Wakristo tunapishana na kutofautiana katika mitazamo na tafsiri zake
kuhusiana na Maandiko. Jambo mojawapo ni kuhusu unyakuo wa Kanisa. Baadhi ya
watu husema kuwa unyakuo utatokea kabla ya dhiki kuu; na wengine
wanasema kuwa unyakuo utatokea baada ya dhiki kuu.
Lakini tunapoangalia
Biblia tunakutana na mifano ambayo inaweza kutupatia picha ya kile
kitakachotokea.
Mfano wa kwanza unamhusu
Nuhu. Nuhu alikuwa mcha Mungu. Lakini ulimwengu wa wakati wake ulikuwa
umeharibika kwa dhambi na uasi dhidi ya Mungu.
Ndipo Bwana alimwambia
Nuhu: … Na tazama, nitaleta gharika ya maji juu
ya nchi, niharibu kila kitu chenye mwili na pumzi ya uhai, kisiwepo chini ya
mbingu; kila kilichoko duniani kitakufa. Lakini nitafanya agano langu nawe kuwa
thabiti; nawe utaingia katika safina, wewe, na wanao, na mkeo, na wake za
wanao, pamoja nawe. (Mwanzo 6:17-18).
Tunaona hapa kwamba Bwana
alimwondoa kwanza Nuhu na familia yake ndipo akaleta yale mapigo
yaliyokusudiwa. Nuhu alifichwa kwenye safina ambayo aliijenga mwenyewe kwa
maelekezo kutoka kwa Mungu. Alifichwa mahali ambako yale mapigo yalikuwa
hayawezi kufika.
Mfano wa pili tunaukuta
kwa Lutu na familia yake. Uangamivu ulikusudiwa kwa miji ya Sodoma na Gomora
kwa sababu ya kukithiri kwa dhambi na uasi dhidi ya Mungu. Katika Mwanzo 19
tunasoma kuwa Bwana alimwondoa Lutu na familia yake nje ya eneo lile. Baada ya
hapo ndipo moto ulipoachiliwa ili kukomesha uovu katika Sodoma na Gomora.
Imeandikwa: Ikawa walipomtoa nje, mmoja alisema,
Jiponye nafsi yako usitazame nyuma, wala usisimame katika hilo bonde po pote;
ujiponye mlimani, usije ukapotea. (Mwanzo 19:17).
Lutu na wanawe walitenda
kile ambacho Mungu aliwaelekeza nao wakapona. Walijiponya nafsi zao kama
ambavyo Nuhu naye alijenga mwenyewe safina.
Ishara nyingine inayotupa picha ya kile kitakachotokea kabla ya dhiki kuu iko kwenye kitabu cha Ufunuo. Tunasoma Bwana akisema: Kwa
kuwa umelishika neno la subira yangu, mimi nami nitakulinda, utoke katika saa
ya kuharibiwa iliyo tayari kuujilia ulimwengu wote, kuwajaribu wakaao juu ya
nchi. (Ufunuo 3:10). Bwana ana kawaida ya kuwatoa watakatifu wake kwenye mapigo yaliyokusudiwa wenye dhambi.
Hiyo saa ya uimwengu kujaribiwa kwa nini haijaja bado. Sababu mojawapo ni kuwa Muda wa Bwana haujatimia. Lakini sababu ya pili Maandiko yanasema kuwa: Maana ile siri ya kuasi hivi sasa inatenda kazi; lakini yuko azuiaye sasa, hata atakapoondolewa. (2 Wathesalonike 2:7).
Hapa anaongelea roho ya
mpinga Kristo ambayo ndiyo itakayokuwa inatenda kazi yake kubwa katika hicho kipindi cha ulimwengu kujaribiwa, kwamba hata sasa ipo tayari hapa duniani na inatenda kazi. Lakini
haijafunguliwa hadi kiwango chake cha mwisho kwa sababu yuko azuiaye. Huyo atakapoondolewa,
ndipo mafuriko ya ile roho yataachiliwa yamwagike kwenye ulimwengu wote. Anayezuia
ni nani basi? Anayezuia ni Kanisa!
Uko uangamivu mkubwa na dhiki kubwa ambavyo vinaujilia
ulimwengu hivi karibuni. Lakini kila mmoja wetu analo jukumu la kufanya ili
kuweza kupona na kuondolewa kabla huo uangamivu haujaachiliwa; kama ambavyo Nuhu alijenga safina yeye mwenyewe; na kama ambavyo Lutu alijiponya mwenyewe kwa kutembea haraka kwenda kwenye eneo la usalama.
Jukumu hilo ni kumwamini Yesu kama Bwana na Mwokozi wako binafsi na kuishi maisha matakatifu. Maandiko
yanasema:
Kwa
sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni
mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka. (Warumi 10:9).
Yesu ndiye safina yetu ya leo kabla ya gharibu ya mateso ya dhiki kuu. Yesu ndiye Mji wetu wa makimbilio kabla ya moto wa mpinga Kristo haujawaka. Muda
unakwenda mbio sana sana!!
Okoka
leo!!
Hebu
sikiliza Ujumbe wa Mungu juu ya jambo hili kutoka kwa mtumishi wake huyu ili uone
jinsi ambavyo ni muhimu na ni lazima kuokoka duniani sasa.
Hapa
hatuongelei dini; tunaongelea WOKOVU!
Bofya HAPA na usikilize
kwa makini mpendwa wangu katika Kristo
Yesu.
Usidanganywe na maneno ya kejeli ya kutoka kuzimu kwamba: "Mbona tangu tuzaliwe tunaambiwa tu Yesu amekaribia, Yesu amekaribia? Mbona hatumuoni?"
Atakapotokea, itakuwa ni ghafla!
Tujitakase na kuishi katika utakatifu kila wakati.
Kwa nguvu zetu hatuwezi.
Lakini jibu liko kwenye kunyenyekea!
Kumwambia Bwana, "Nisaidie! Niwezeshe! Nishike mkono! Usiniache!"
Wokovu si kwa juhudi zetu BALI ni kwa Neema ya Yesu.
Bwana Yesu akubariki.
Shalom James. Maneno yaliyoko ktk haya yako ya kwanza ktk makala hii inasomeka hivi "..............hakutakuwapo na unyakuo kabla ya dhiki kuu; na wengine wanasema kuwa unyakuo utatokea baada ya dhiki kuu". Nimeshindwa kujua tofauti ya sentensi hizo mbili. Kwamba hakutakuwepo na unyakuo kabla ya dhiki kuu maana yake ni kwamba dhiki kuu itatangulia ndio unyakuo ufuate. Na sentensi kuwa "unyakuo utatokea baada ya dhiki kuu" pia maana yake ni kwamba dhiki kuu itatangulia ndio unyakuo ufuate. Kimsingi hizi ni sentensi zenye maana sawa sawia.
ReplyDeleteNashukuru sana Ruta kwa kunishitua katika hilo. Ni kweli kabisa niliandika sentensi ambazo sikugundua kuwa zilikuwa na maana ileile. Nimeshazirekebisha sasa. Ubarikiwe na Bwana.
ReplyDeleteNimekuwa nikitembelea blog yako kwa muda sasa, nimebarikiwa na kujifunza mengi yaliyo ya baraka Hakika nabarikiwa sana.
ReplyDeleteAmen Goodluck. Ashukuriwe Bwana wetu Yesu.
DeleteHakika ni kweli kabisa ila MUNGU muumba wa mbingu na aridhi atuhurumie rehema zake ziambatane nabkila tunapo tembea
ReplyDelete