Saturday, August 17, 2013

Wachawi Wapigwa Kisha Waumbuliwa Waziwazi na Bwana Yesu!



 
[Picha kutoka mtandaoni. Walioumbuliwa si hawa]

Mungu anatenda kazi. Kazi ya kueneza Injili ya Yesu Kristo si kazi nyepesi kwa sababu ushindani wake hautoki kwa wanadamu bali ni kutoka kwenye falme za giza zinazoongozwa na mapindikizi ya mapepo yanayoongoza majeshi kwa majeshi ya pepo wachafu.

Imeandikwa:
Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. (Waefeso 6:12).


Kwa kuwa sisi hatuyaoni haya majeshi, ni rahisi kudhania kuwa upinzani wetu unatoka kwa watu wa dini fulani, au kutoka kwenye tawala za kidunia, lakini ukweli ni kwamba wanadamu wanaopinga Injili ya Mwokozi Yesu wanatumiwa tu na shetani.

Wapo watumishi wa Mungu wengi ambao wanafanya kazi ya kueneza Injili mahali mbalimbali. Hata hivyo, iko huduma moja ambayo ni ya kipekee sana nchini Tanzania. Huduma hii inajulikana kama VHM, au Voice of Hope Ministries. 

Hii ni huduma ambayo inaongozwa na mtumishi wa Mungu,
Mchungaji Peter Mitimingi (tazama picha hapo kulia). Huduma hii ni maalum sana kwa sababu yenyewe imejikita kwenye kupeleka Injili vijijini - si mjini! Maana, mijini kumeshahubiriwa sana, japokuwa huko nako bado Injili inatakiwa kuendelea kuhubiriwa hadi mwisho wa nyakati.

Lakini ukweli ni kwamba, kama mijini ambako kumeshahubiriwa sana Injili bado inahitajika, je, ni vipi basi vijijini ambako ni nadra kuwako mikutano ya Injili?

Unapowasikiliza VHM kwenye kipindi chao siku ya Ijumaa jioni kwenye Redio WAPO FM, ndipo unajua jinsi ambavyo vijijini watu wanateswa sana sana na shetani kupitia maajenti wake, hususani wachawi; na pia unajua jinsi mtumishi huyu na huduma yake walivyojitoa kwelikweli kwa ajili ya kazi ya Mungu kule kulikosahauliwa.

Vijijini watu wanaishi kwenye umaskini mkubwa, magonjwa, umaskini, hofu na mashaka mengi kwa sababu kuna vigagula ambavyo ni kama vimejitangazia serikali zao kule vijijini. Vigagula hawa ndio wanaotoa miongozo ya namna ya kuishi huko – na unajua kuwa mwongozo kutoka kwa ibilisi hauwezi kuwa na uzima bali mauti tu.

VHM wameendelea kupeleka Injili kwenye vijiji mbalimbali, kama vile kule Kilwa, Bagamoyo, Tanga, Dodoma, n.k. Lakini upinzani ni mkubwa sana ingawaje Mungu wa Ibrahimu na Isaka na Yakobo anawapa kushinda kwa kishindo sana kila mahali wanakoenda hawa watumishi wake hawa.

Ili kuonyesha namna Mungu anavyowatumia watumishi hawa na jinsi walivyojitoa kwelikweli, Mungu alimpa neema ya pekee sana mtumishi wake, Mchungaji Mitimingi.

Biblia inasema:
Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru (Luka 10:19).


Katika huduma yao, watumishi hawa wamemkanyaga na wanaendelea kumkanyaga shetani kwelikweli! Wanaharibu zana nyingi za kichawi. Sasa kutokana na kuzidiwa, wachawi wa huko Kilwa ilibidi wampigie simu mchungaji Mitimingi:

  • kwanza ili kuomba msamaha kwa kuifuatilia huduma yao;

  • pili, ili kuahidi kwamba hawataifuatilia tena huduma hiyo;

  • tatu, ili kuahidi kwamba watawaambia wachawi wenzao nao waache kuifuatilia huduma hiyo; na

  • nne ili kuomba warudishiwe ‘ndege’ yao ambayo imeharibiwa vibaya na sasa haiwezi kuruka tena.


Mungu wetu alimpa hekima ya ajabu Mchungaji Mitimingi, ambaye aliweza kuwarekodi wanga hawa bila wao kujua.

Kisha baada ya kuongea na mchungaji, wanga hawa walianza kusutana wao kwa wao. Lakini pia Mungu aliwasahaulisha kuzima simu. Mchungaji aliendelea kuwarekodi wakiwa wanaongea, wasijue kuwa kuna mtu anawasikiliza. Hakika Mungu wetu aliwavua nguo zao na kuwaacha watupu mchana kweupe! 

Watu wengi hujidanganya kwamba uchawi hakuna huku wakijifariji kwa kusema, 'Uchawi ni imani yako tu. Kama ukiuamini, upo; kama hauuamini, basi haupo." Hii si kweli. Uchawi upo.

Tafadhali sikiliza mahojiano na mazungumzo kati ya mchungaji Peter Mitimingi na hao wanga, nawe utamtukuza Mungu na kutiwa nguvu. Bofya HAPA.

Bofya pia HAPA usikie jinsi walivyokuwa wakisutana na kulaumiana wao kwa wao.

Wito maalum
Kazi ya kuepeleka Injili ulimwenguni ni kazi kubwa sana inayohitaji gharama nyingi. Watumishi hawa wamejitoa sana kwenye kazi hii. Lakini wanahitaji kuungwa mkono na kila mtu mwenye kumpenda Mungu. Mchungaji Peter Mitimingi huwa anapokea mchango wowote, hata kama ingekuwa ni shilingi 1,000. Kama watu wengi wakiweza kutuma michango yao kadiri kila mtu anavyojaliwa na Bwana, basi kazi hii muhimu sana ya kupeleka Injili vijijini itaweza kusonga mbele kwa nguvu zaidi na kwa mafanikio zaidi.

Hakika hakuna biashara yenye faida kubwa kama kuwekeza kwenye Ufalme wa Bwana Yesu, na hasa mahali ambako watu wanaokolewa na kuwa wana wa Ufalme wa Mungu!

Kama ungependa kutuma mchango wako wowote, tafadhali wasiliana na huduma hii kupitia namba zao ambazo zimetajwa kwenye website yao iliyo HAPA. Namba hizo ni: +255 22 2775809 na +255 713 18 39 39.

Bwana Yesu akubariki sana kwa moyo wako wa upendo.

No comments:

Post a Comment