Sura ya 5: Kukutana kwangu na Yesu Kristo
Mwezi wa
February 1985, tulikuwa na mkutano wetu wa kawaida baharini. Baada ya hapo
niliamua kusafiri hadi Port Harcourt kwenye Jimbo la Rivers, kumtembelea mke wa
marehemu mjomba wangu. Nilikutana na mtu aliyeitwa Anthony. Alikuwa na karakana
yake kule Nwaja Junction, kwenye barabara ya Trans-Amadi, Port Harcourt, Jimbo
la Rivers. Alituma ujumbe niende kwake na kwa kuwa kwenye kundi letu tuna
sheria kwamba usikatae wito, niliamua kwenda. Nilienda kwake mchana siku ya
Alhamisi. Alianza kwa kusema, “Mungu amenipa ujumbe kwa ajili yako.” Alitoa
Biblia yake na kuanza kuhubiri. Kulikuwa na Wakristo wengine watatu wamekaa (mwanamume
na wanawake wawili). Aliendelea na mahubiri yake kwa muda mrefu na sina uhakika
kama niliyasikia yote. Hatimaye aliniambia nipige magoti kwa ajili ya kuombewa.
Nilitii na nikapiga magoti kimyakimya.
Mara
moja alianza kuomba. Nilisukumwa na Roho wa Mungu na nikaanguka chini. Nikawa nahangaika kuinuka na
nikasimama kama chuma. Niliharibu viti vya chuma ndani ya ile karakana.
Nilitazama nje na kuona watu watatu kutoka kwenye kundi letu la siri; mwanamume
na wasichana wawili. Walikuja kwa maumbo ya kibinadamu na wakaelekea mlango
lakini kutokana na nguvu ya Mungu, hawakuweza kuingia.
Nina uhakika
kuwa alamu kule baharini iliwajulisha kuhusiana na tatizo lililokuwapo; na
kupitia TV, walijua tatizo liko wapi na wakatuma timu ‘isiyo na nguvu’ kuja
kuniokoa. Hii hutokea kila wakati mwanachama wetu anapofikwa na matatizo.
Wakati wale wanaume wawili Wakristo wakinivuta nipige magoti, wale wasichana
waliendelea kuomba na kuyafunga mapepo, lakini hawakuwa wakilenga mapepo yoyote
maalum. Waliniuliza endapo nilikuwa namwamini Yesu Kristo, nikakaa kimya.
Waliniambia niite Jina la Yesu, nikakataa. Waliniuliza jina langu nami nikawaambia.
Walihangaika kwa saa kadhaa kisha wakaniacha niende. Hakuna pepo hata moja
lililotolewa kwangu, kwa hiyo nilitoka kama nilivyokuja.
Tukio la Kanisani
Siku
iliyofuata, Ijumaa, nilialikwa na yuleyule Anthony kwenye mkesha katika Kanisa
la Assemblies of God, Silver Valley, Port Harcourt. Nilikubali mwaliko huu kwa
sababu kwenda makanisani ili kusababisha usingizi na machafuko ilikuwa ni
mojawapo ya majukumu yetu. Ibada ilianza kwa nyimbo. Tuliimba hadi mmoja wa
washirika alipoanzisha wimbo maarufu wa bendi moja ya Kikristo, unaosema kuwa
hakuna nguvu nyingine iliyo juu ya nguvu za Yesu.
Nilianza
kucheka. Nilicheka kwa sababu nilipokuwa kwenye roho na kuwaangalia maisha yao,
robo tatu ya waliokuwa wakiimba wimbo ule walikuwa ni watu wanaoishi kwenye
dhambi. Nilijua hilo kwa sababu ya
dhambi kwenye maisha yao. Walikuwa wako wazi kiasi kwamba wangeweza kudhuriwa vibaya
sana na nguvu hizo. Ni muhimu kwa Wakristo kutii Neno la Mungu na sio kuruhusu
dhambi kubakia kwenye maisha yao. Katika ibada ile, tulikuwapo wanne
kutokea baharini na tulikuwa tukiimba na kupiga makofi pamoja nao. Nataka pia
kusisitiza hapa kwamba, ibada inapoanza, ni muhimu waumini washauriwe kwanza
kukiri na kutubu dhambi zao, ndipo waingie kwenye kipindi cha kumsifu
Mungu. Hii inamfanya ajenti wa
shetani aliyepo humo akose kabisa raha na kimsingi atakimbia ili kuponya maisha
yake.
Katika ibada
hii, tulikuwa na amani kabisa na hata tulianza kufanya mambo yetu. Wengi
walianza kusinzia, nyimbo ziliimbwa kwa udhaifu na mambo yalikuwa hovyohovyo
tu. Anthony alishawaeleza kuhusiana na mimi, hivyo kwenye saa 8:00 usiku
waliniita ili waniombee. Mara tu nilipotoka mbele, walianza kusihi damu ya
Yesu. Niliwasimamisha na kuwaambia, “Kusihi damu ya Yesu si suluhisho. Mimi ni
mwanachama wa kundi la siri. Kama mkikubali kuwa mnaweza kunifungua mimi, basi
nitapiga magoti.” Maneno haya sikuwa nimeyapanga kuyasema. Damu ya Yesu
huwatisha mapepo na inawalinda waamini, lakini haiwafungi mapepo. Mapepo
hufungukika pale tu Mkristo anapotumia mamlaka yake na kutoa amri.
Walikubali
na nikapiga magoti. Wakati huu, dada mmoja akiongozwa na Roho wa Mungu alipaza
sauti na kusema, “Kama unajijua hustahili, usikaribie hapa!” Nina uhakika wengi
hawakumwelewa alichomaanisha. Ni hatari sana kwa Mkristo anayeishi katika
dhambi kukemea mapepo. Wengi waliondoka na wachache wakaja kuniombea.
Walipoanza kusema “kwa Jina la Yesu”, nilisikia kishindo kikubwa ndani yangu na
nikaanguka chini! Mara moja pepo lirukalo ndani yangu lilianza kazi. Nikaanza
kukimbia kwa kifua changu. Mtu yeyote mwenye pepo hili lirukalo huwa ni mwovu
na wa hatari sana. Ndugu wale hawakuona kilichokuwa kikiendelea kwenye
ulimwengu wa roho. Nilikuwa ninakimbia kutokana na nguvu kubwa iliyokuwamo
kwenye chumba kile.
Nguvu mbili
zinazopingana zilianza kupambana na anga likawa limebadilika. Ghafla nilisimama
na nikawa mkali sana, mwenye vurugu sana, n.k. Pepo lilitoka kwangu na kumvaa
kijana mmoja katikati yao na likaanza kupambana nao kujaribu kuniokoa mimi. Ndugu
hawakuhangaika naye, bali walimchukua yeye pamoja na wengine waliokuwa
wakiogopa, na kwenda kuwafungia kwenye chumba kingine cha Kanisa. Mapambano
yaliendelea hadi saa 1:00 asubuhi. Nilikuwa nimechoka sana kimwili na nikawa
kimya. Kwa hiyo, ndugu walinizunguka na kuanza kupiga kelele, “Wataje! Ni akina
nani hao?” n.k. Lakini nilibaki kimya tu.
Baada ya
kungoja kwa muda mrefu na nikawa nimekaa tu kimya, walidanganyika kuwa
nimefunguliwa. Waliomba na tukatawanyika. Nilikuwa dhaifu sana kimwili kiasi
kwamba ilikuwa tabu kutembea ili kutoka nje ya Kanisa. Lakini kuna jambo lilitokea; maana mara tu
nilipotoka nje ya Kanisa na kuvuka barabara, niliingiwa na nguvu nyingi sana
kimwili. Huenda baadhi ya mapepo yaliyokuwa yametoka yalirudi. Nilijawa na
hasira sana na kuamua kulipiza kisasi kwenye Kanisa lile. “Watu hawa walikuwa
wamenitukana,” nilijisemea mwenyewe. Kwa hiyo, kutokana na haya, niliamua kuwa
nitakwenda Lagos kupata nguvu zaidi na wengine walio waovu kama mimi, kisha
tutakuja tena Port Harcourt kulipa kisasi kwa waumini WOTE wa Assembly of God,
Silver Valley.
Njiani kwenda Lagos
Nilipofika
kwenye nyumba ya mke wa mjomba wangu, niliwaambia kuwa naondoka mara moja
kwenda Lagos. Nilikataa kushawishiwa kubakia na nikachukua taksi hadi kituo cha
magari cha Mile 3 ambako nilipanda taksi hadi Onitsha. Lengo langu lilikuwa
kushukia Onitsha na kwenda kumwona rafiki yangu mmoja kisha niendelee hadi Lagos.
Pale Mile 3 tuliondoka na tulipofika Omagwe, kwenye njiapanda ya uwanja wa
ndege wa kimataifa, nilisikia sauti ikiniita kwa jina langu la nyumbani, “NKEM.”
Niligeuka kuona kama kulikuwa na mtu niliyemfahamu kwenye taksi ile, lakini
hakukuwa na yeyote. Sasa, huyo aliyeniita alikuwa ni nani? Ni marehemu mama yangu
tu ndiye alikuwa akiniita kwa jina hilo. Wengine wote, ikiwa ni pamoja na
mapepo kwenye ulimwengu wa roho, walinifahamu kwa jina la Emmanuel.
Wakati
nikiendelea kushangaa, sauti ile iliita tena: “NKEM, utaenda kunisaliti tena?”
Sikuitambua sauti ile lakini iliendelea kuniuliza: “Utaenda kunisaliti tena?”
Ghafla nilipata homa kali sana. Joto
lililotoka kwenye mwili wangu lilikuwa kali sana kiasi kwamba abiria wengine nao
walilihisi. Mmoja wao aliniuliza, “Mr., ulikuwa
mzima kabisa kabla hujaanza safari?” Niliwaambia kuwa nilikuwa mzima kabisa na
kwamba sikuwa hata na maumivu ya kichwa kabla ya kuondoka Port Harcourt.
Tulipofika
Umuakpa kule Owerri, nilizimia ndani ya taksi. Nilichojua baada ya hapo ni
kuwa, wanaume wawili, warefu na wakubwa sana, walikuja kunichukua – mmoja
kushoto kwangu na mwingine kulia; na wala hawakunisemesha hata neno moja.
Walinipitisha kwenye barabara mbaya sana iliyokuwa imejaa chupa na vyuma
ambavyo vilinikata na nikaanza kulia lakini hawa wanaume bado hawakusema hata
neno moja. Tuliendelea hadi tukafika kwenye barabara nzuri kubwa. Ni hapa ndipo
mmoja wao alipoongea na kusema, “Wewe ni mtu unayetakiwa!” na
tukaendelea na safari. Tulifika kwenye jengo kubwa na refu sana ambalo
lilionekana kama ukumbi wa mikutano. Mara tulipopanda hapo, sauti ilisikika
kutokea ndani ikisema, “Mleteni ndani!” Waliniingiza ndani na wakapotea;
nikabakia peke yangu.
Kile nilichokiona
ndani ya jengo hilo, ni vigumu sana kuelezea, lakini nitajaribu kadiri
niwezavyo. Ukumbi ule ulikuwa umepambwa vizuri sana na ulikuwa mkubwa na mrefu
sana kiasi kwamba hungeweza kuona mwisho wake. Mwishoni kulikuwa na madhabahu.
Niliona mwezi na nyota zimezunguka jua. Kisha niliona kiti cha enzi na juu yake
alikaa Mwanamume mzuri sana mwenye mavazi ambayo yaling’aa kama jua. Alisema, “Njoo!”
Lakini kutokana na mng’ao wake, sikuweza kwenda. Kila nilipojaribu kusogeza
mguu, nilianguka.
Niliinuka na
kujaribu tena na kuanguka. Mara mwezi ulitoka kwenye kile kiti cha enzi na kuja
pale nilikokuwa nimekaa na ukaenda kwenye dari juu yangu. Halafu mikono miwili
ilitoka kwenye ule mwezi, ikashika kichwa changu, ikanitikisa na mwili wangu wa
nyama ukavuka kama kuvua nguo. Halafu mimi halisi nikasimama. Ile mikono
ikaukunja ule mwili kama kukunja nguo na kuudondosha kwenye kona. Halafu huo
mwezi ukarudi kwenye kile kiti cha enzi na Yule aliyekaa juu yake akaniambia tena,
“Njoo!”
Utakaso wa kiroho
Nilitembea
hadi hatua fulani kisha Yeye akashuka kutoka kwenye kiti cha enzi na kuja
kwangu; akachomoa miguu yangu, mmoja baada ya mwingine na kumwaga kilichokuwa
ndani yake na kuirudishia tena. Alifanya hivyohivyo kwa mikono yangu na
kuirudishia mahali pake. Kimsingi aliendelea hivyo kwa kila sehemu ambayo yule
malkia wa pwani aliweka nguvu zake.
Nilijiuliza kwa mshangao, “Huyu ni nani na amejuaje mahali ambako vitu
hivi viliwekwa?” Baada ya hapo, alirudi kwenye kiti chake cha enzi na kuniita
nimwendee. Nilipoanza kutembea, vitu vilianza kudondoka kutoka kwenye mwili
wangu – magamba yalidondoka toka machoni mwangu, n.k.’ Lakini kabla sijafika kwenye madhabahu,
viliacha kutoka. “UNAENDA WAPI?” Aliniuliza.
Nikajibu na
kusema, “Naenda Onitsha kumtembelea rafiki yangu.” Akasema, “Ndiyo, lakini
nitakuonyesha kile kilichomo kwenye mawazo yako.” Hadi wakati huu sikuwa
nimejua alikuwa ni nani huyo. Lakini jambo moja lilikuwa la hakika; kwamba
alikuwa na nguvu zaidi ya nguvu zote nilizowahi kukutana nazo! Aliita kwa mkono
mwanamume mmoja kisha akamwambia anionyeshe kile ambacho nilikuwa nimekipanga
kwenye moyo wangu. Mwanamume huyo alinipeleka kwenye chumba na kufungua kitu
kama ubao wa kuandikia. Kimsingi, kama kungekuwa na njia ya kuponyoka pale,
ningetoroka; maana mbele yangu yaliandikwa yote ambayo nilikuwa nimepanga dhidi
ya Wakristo na mipango yangu dhidi ya Kanisa la Assemblies of God, Silver
Valley. Hatimaye yule mwanamume alinirejesha tena kwenye madhabahu na kuondoka.
Yule mtu
alishuka kwenye kiti cha enzi na kunishika mkono na kusema alikuwa anaenda
kunionyesha mambo kadhaa. Tukiwa tunaenda, alisema, “Sitaki uangamie bali
nataka nikuokoe na hii ni nafasi yako ya mwisho. Kama hutatubu na kuja kwangu
na kunitumikia, utakufa. Nitakuonyesha mahali pa waliookolewa na mahali pa
wasio na utii.” Aliposema haya, ndipo nikajua kuwa alikuwa ni Yesu Kristo.
Mafunuo ya Kiungu
Tuliingia kwenye
chumba na akafungua kitu kama pazia. Nikauona ulimwengu wote, watu na mambo
yote yanayoendelea. Niliona Wakristo na wasioamini, wakifanya hili na lile. Tulienda
kwenye chumba kingine. Alifungua kitu kama pazia tena na kile nilichoona
kilikuwa cha kusikitisha sana. Watu walikuwa wamefungwa minyororo! Aliwaita watu
hawa kuwa ni “wanafiki.” Hawa walionekana wenye majonzi sana na akasema,
“Watabakia hivihivi hadi siku ya hukumu.”
Tukaenda kwenye
chumba cha tatu. Akafungua pazia na nikaona watu wengi wakifurahia, wakiwa
wamevaa mavazi meupe. Safari hii nilimwuliza, “Hawa ni akina nani?” Akasema, “Hawa
ni wale waliokombolewa, wanangoja malipo yao.”
Tulienda
kwenye chumba cha nne na nilichokiona hapo ni cha kuogofya sana. Mpendwa msomaji,
ni vigumu sana kuelezea. Ilionekana kama jiji zima linawaka moto. Kuzimu ni halisi na inatisha sana. Kama ulishaaminishwa kuwa Mbingu
na Jehanamu ziko hapahapa duniani na kwamba mwanadamu akifa ndio basi, ni bora
utambue sasa kwamba kuna kuzimu
halisi na kuna mbingu halisi! Si ajabu basi Yesu Kristo alipokuwa duniani
aliwaonya watu juu ya kuzimu. Nasema tena, kuzimu ni halisi! Niliiona na ni
mahali pa kutisha sana! Nikamwuliza, “Hii ni nini?” Akanijibu, “Hapa
paliandaliwa kwa ajili ya shetani na malaika zake na kwa wasio na utii.” Aliwataja
kama ilivyoandikwa kwenye Ufunuo 21:8. “Bali
waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao
waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto
na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili.”
Tuliingia kwenye
chumba cha tano na alipofungua pazia, nilichoona kinaweza tu kuelezwa kwamba ni
UTUKUFU. Ilikuwa kana kwamba ninapaangalia pale kutokea juu ya mlima. Niliona jiji jipya. Jiji hilo lilikuwa kubwa na
zuri sana! Barabara zake ni za dhahabu. Majengo yake hayawezi kulinganishwa na kitu
chochote kwenye dunia hii. Akasema, “Hili ni tumaini la watakatifu. Je,
utakuwa pale?” Mara moja nilijibu, “Ndiyo!” Baada ya hapo tulirudi kwenye
kiti cha enzi na akasema, “Nenda ukashuhudie kile nilichokutendea.”
Akanichukua tena
hadi kwenye chumba kingine na alipofunua pazia, niliona yote ambayo ningeenda
kukutana nayo katika safari yangu ya kwenda Onitsha na Lagos na jinsi ambavyo
mwisho wake ataniokoa na yote hayo. Baada ya hapo akasema, “Usiogope, nenda, nitakuwa na wewe.” Alinisindikiza hadi nje ya
ukumbi ule na akatoweka.
Ndipo niliamka
nikiwa kwenye kitanda kwenye nyumba ya mtu. Nilipaza sauti, hivyo huyo mtu na
mke wake walikimbia kuja toka kwenye chumba chao. Kwanza walichungulia kisha
wakaingia. “Mbona niko hapa?” niliuliza. Ndipo yule mwanamume alipoelezea jinsi
ambavyo nilizimia ndani ya taksi na jinsi ambavyo walinibeba hadi kwenye Kanisa
Katoliki pale Owerri; jinsi walivyomwita daktari, ambaye alikuja akanipima na
kusema mapigo yangu ya moyo yalikuwa kawaida na kwamba wangoje waone kile ambacho
kingetokea. Daktari aliwahakikishia kuwa fahamu zangu zingenirudia. Ndipo huyo
mwanamume alinibeba kwenye gari lake hadi kwenye nyumba yake na alikuwa
akingoja. Akakiri kuwa hakujua kwa nini alimwamini daktari na kwa nini
alichukua jukumu la kunileta kwenye nyumba yake.
Waliniuliza jina
langu na wapi nilikotokea , nikawaeleza, kisha nikakaa kimya, sikuwaleza yale
yaliyonikuta. Nilibaki kimya na familia hii yenye ukarimu kwa siku mbili, kisha
yule mwanamume na mke wake walinichukua kwenye gari lao hadi kwenye kituo cha
magari cha Owerri, ambako nilipanda taksi hadi Onitsha. Yote ambayo Bwana
alinionyesha kuhusiana na safari yangu yalitokea moja baada ya jingine. Asubuhi
iliyofuata, nilichukua taksi nyingine hadi Lagos. Nilitii na kuondoka Lagos
kwenye Port Harcourt asubuhi iliyofuata. Kila mara huwa najiuliza, “Kwa nini
Bwana amwokoe mtu kama mimi? Mtu ambaye ni mwovu na mharibifu; ajenti wa
shetani! Nilipata majibu kwenye maneno haya matatu: Mungu ni pendo. Hakika,
Mungu ni Pendo! (1 Yohana 4:8, 4:16).
ITAENDELEA…..
No comments:
Post a Comment