Monday, September 3, 2012

Je, Umechoka?



Bwana wetu Yesu alisema wazi: Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate. (Mt. 16:24).
Maisha tunayoishi hayaishi mitihani na majaribu mbalimbali. Mitihani hiyo inaweza kuwa inahusu maeneo ya kiafya, kimahusiano, kiuchumi, kiroho, nk.

Kila mwanadamu katika wakati wowote ule, ni lazima anapambana na uhitaji wa namna moja au zaidi. Mtume Petro anatuambia kwamba tumpinge shetani kila wakati kwa imani thabiti: ... mkijua ya kuwa mateso yale yale yanatimizwa kwa ndugu zenu walioko duniani. (1 Pt 5:9).


Wapo watu wengi sana ambao wamo makanisani lakini wakiwa wamekata tamaa sana. Kuna hali ya kuchoka kiimani kutokana na kule kuona kuwa Bwana anachelewa sana kuwajibu huku siku zinazidi kusonga mbele.

Bwana Yesu aliposema kuwa kumfuata kwetu ni pamoja na kujitwika msalaba, maana yake ni kuwa maisha ya wokovu maana yake si kuwa na ulaini au mteremko tu kwa kila kitu kwa sababu tu eti tumeokoka. Maisha ya wokovu kusema kweli yana gharama yake. Kuna gharama za kudumu katika maombi, japo wakati mwingine mwili unakuwa umechoka kweli; kuna gharama za kudumu katika kuamini – na imani ili iweze kutumika ni lazima upitishwe kwenye hali ambayo hujui nini kinaendelea; kuna gharama za kuikataa dunia na mambo yake, japo katika mambo hayohayo tunaona kana kwamba wana wa ulimwengu wakifanikiwa na kunawiri; kuna gharama za kungoja na kuvumilia hadi wakati wa Bwana, nk., nk.

Kutokana na mapito haya yanayotukabili, wengi wametikiswa katika imani; na wengine wengi wameiacha kabisa imani. Ndiyo maana Bwana alituachia swali kubwa la changamoto kwamba: walakini, atakapokuja Mwana wa Adamu, je! Ataiona imani duniani? (Lk 18:8). 

Je, bado uko ndani ya imani? Je, umechoka kiasi kwamba umeamua kurudi nyuma? Je, shetani amefanikiwa kukuambia kuwa wewe huwezi, hivyo ni bora utafute njia zako mwenyewe? Je, Bwana akirudi leo atakukuta bado umebeba msalaba wako huku ukiendelea mbele?

Ni mambo gani yanawafanya watu kuchoka?

Jambo moja ni hilo ambalo tumelitaja hapo juu, yaani kuona kuwa muda umekuwa mrefu mno tangu mtu aanze kuomba jambo fulani lakini bado hajapata.

Sababu nyingine ni kujilinganisha na watu wengine. Huenda unaangalia watu wengine ambao, kwa mtazamo wako, unawaita kuwa wamefanikiwa. Mafanikio hayo yanaweza kuwa ni nyumba nzuri, magari, mavazi mazuri, watoto wazuri, n.k.

Inawezekana kabisa watu hao wamefikia hatua waliyo nayo kupitia baraka za Bwana. Lakini pia inawezekana kabisa kuwa wamefikia hapo kwa nguvu zingine, maana shetani alimwonyesha Bwana Yesu milki zote za ulimwengu, kisha akamwambia:  Nitakupa wewe enzi hii yote, na fahari yake, kwa kuwa imo mikononi mwangu, nami humpa ye yote kama nipendavyo.  Basi, wewe ukisujudu mbele yangu yote yatakuwa yako. (Lk 4:6-7). Shetani anaweza kuwatajirisha watu, na hivyo ndivyo anavyofanya kila siku kabisa.

Kwa hiyo, huku kujilinganisha ndiko kunakoweza kumfanya mtu aanze kufikiri, “Mbona watu wengine wana maisha mazuri wakati mimi ninahangaika tu? Labda mimi Mungu hanipendi na hana mpango wa kunisaida.”

Ndugu, mimi pia sijui ni lini Mungu atakupa hicho unachokitamani moyoni mwako. Lakini ninajua jambo moja hakika – Mungu ni mwaminifu kwa neno lake! Na tena, kumngoja Bwana hakuna majuto kamwe. Hata Mungu mwenyewe naye anasema:


Maneno yenu yamekuwa magumu juu yangu, asema Bwana. Lakini ninyi mwasema, Tumesema maneno juu yako kwa namna gani?  Mmesema, Kumtumikia Mungu hakuna faida; na, Tumepata faida gani kwa kuyashika maagizo yake, na kwa kwenda kwa huzuni mbele za Bwana wa majeshi? Na sasa twasema ya kwamba wenye kiburi ndio walio heri; naam, watendao uovu ndio wajengwao; naam, wamjaribuo Mungu ndio waponywao.

Ndipo wale waliomcha Bwana waliposemezana wao kwa wao. Naye Bwana akasikiliza, akasikia; na kitabu cha ukumbusho kikaandikwa mbele zake, kwa ajili ya hao waliomcha Bwana, na kulitafakari jina lake. Nao watakuwa wangu, asema Bwana wa majeshi, katika siku ile niifanyayo; naam, watakuwa hazina yangu hasa; nami nitawaachilia, kama vile mtu amwachiliavyo mwanawe mwenyewe amtumikiaye.

Ndipo mtakaporudi, nanyi mtapambanua kati ya wenye haki na waovu, na kati ya yeye amtumikiaye Mungu na yeye asiyemtumikia. (Malaki 3:13-18).

Rafiki, usikate tamaa. Endelea kusimama na Bwana Yesu hadi mwisho. Subirá yako si bure hata kidogo. Hauna jambo hata moja umalotenda kwa ajili ya Bwana ambalo unapoteza – iwe ni kuamini, kuwa na saburi, kutenda kazi yake, kuomba, n.k.

Endelea kusimama! Endelea kusimama! Endelea kusimama!

Tuna maisha ya miaka michache sana sana hapa duniani. Baada ya maisha haya, inafuata milele! Milele maana yake ni hakuna mwisho. Acha Bwana akujibu kwa wakati wake. Lakini, hata kama hatakujibu sawasawa na shauku uliyo nayo, wewe endelea tu kusimama, wala usirudi na kugeuka nyuma!

Imani yako si bure hata kidogo. Kile kinachoonekana kama mafanikio kwa wengine kisiwe kigezo cha wewe kudhani kuwa hiyo ni ishara kwamba Bwana amekuacha. Kama unaendelea kuamini, kwa nini Mungu akuache? Akifanya hivyo, basi hata yeyé atakuwa mwongo na haaminiki. Lakini: Yesu Kristo ni yeye yule, jana na leo na hata milele. (Ebr 13:8).

Alichoahidi hakijabadilika. Usitupe msalaba kwa ajili ya mambo yapitayo! Endelea kusonga mbele hadi uumalize mwendo. Imeandikwa kwamba: Tangu siku za Yohana, ufalme wa Mungu hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu wauteka. (Mathayo 11:12).

Wokovu ni vita! Wokovu ni mapambano! Wokovu si mteremko! Lakini, maisha nje ya Yesu, hasa ndio mzigo wa kulemea sana! Nira ya Bwana Yesu ni laini; lakini bado ni nira.

Usiogope! Usikate tamaa! Hauko peke yako! Bwana aliyeumba mbingu na nchi hayuko tu mbinguni; yuko ndani yako ili kukusaidia. Anachohitaji ni kitu kimoja tu – umwamini! Naye atafanya yote yale ambayo yanaonekana kuwa ni magumu.

Unapoona kuwa unaingiwa na hali ya kukata tamaa, hizo si hisia tu. Wapo mashetani kabisa ambao wanatufuatilia usiku na mchana na kutupandikizia roho za namna hiyo ili kwamba tumwache Bwana na kuangamia kama wao. Usikubali! Yote yawezekana kwake yeye aaminiye. (Mk 9:23).

Iwe ni hapa duniani, au ni kule mbinguni, lakini ni lazima siku inakuja ambapo utajua na kushukuru kwamba imani na subira yako haikuwa bure hata kidogo! Endelea kushikilia imani yako; maana si wewe utendaye bali ni Roho Mtakatifu aliye ndani yako! Usiwaangalie wanadamu, bali mwangalie Bwana na ahadi yake kwako. Unaweza!



No comments:

Post a Comment